MWANAMKE NA NGUVU YA USHAWISHI (UBEMBELEZI)

0
7K

Mwanamke aliumbwa na nguvu ya ushawishi ndani yake kwa kusudi la kuweza kutimiliza jukumu lake katika familia la Kujenga na Kulinda nyumba yake. Lakini kwa bahati mbaya, nguvu hii ya ushawishi ambayo hufanya kazi yake kupitia uwezo wa ubembelezi alionao mwanamke, mara nyingi imekuwa ikitumika vibaya. Mwanamke mwenye hekima hujenga nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe akitumia hazina ya uwezo aliowekewa ndani yake, na mojawapo ni nguvu ya ushawishi na ubembelezi alionao ndani yake.

Ushawishi hufanya kazi mkono kwa mkono na ubembelezi. Huwezi kutenganisha ushawishi na ubembelezi, ni vitu vinavyoenda pamoja bila kuachana kabisa.

Lengo la somo hili ni kuwasaidia wanawake wote wajue na kuwa na ufahamu kwamba, ndani yao Mungu amewekeza nguvu ya ushawishi (na ubembelezi) kwa kusudi la kujenga na kulinda ndoa na familia zao, na si kwa kusudi la kubomoa. Baadhi ya wanawake hawajui kama wana nguvu hii ndani yao, na baadhi yao wanajua, na katika hao wanaojua baadhi hawajui namna ya kuitumia na wakati gani waitumie, na baadhi yao wanajua namna ya kuitumia na wengine wanaitumia vibaya kwa sababu ya makusudi mabaya mioyoni mwao, na wengine wanaitumia vizuri.

Katika mfululizo wa somo hili tutapata fursa au nafasi ya kujifunza mambo mengi yatakayomsaidia mwanamke yeyote kuitumia nguvu hii na uwezo huu wa ushawishi na ubembelelezi ambao Mungu ameweka ndani yake ili ulete matokeo yaliyokusudiwa. Tutaangalia mifano halisi katika Biblia ya wanawake waliotumia nguvu na uwezo huu vizuri na kuleta matokeo mazuri, na mifano ya wanawake waliotumia nguvu na uwezo huu ulioko ndani yao vibaya na kuleta matokeo mabaya.

Kabla ya kuendelea mbele, katika utangulizi huu ningelipenda sana ufahamu jambo la muhimu sana tunapoendelea kujifunza siri hii.

Kila kitu alichokiumba Mungu ni chema, na vyote vilivyo ndani yake ni vyema, viliumbwa kwa kusudi la kutimiza kusudi jema la Mungu. Lakini tangu wanadamu walipomkataa Mungu katika fahamu na akili zao, waligundua magunduzi mengi yanayowaharibia njia zao mbele za Mungu. Tangia hapo, kila kitu chema kikawa kinaharibika katika matumizi; wanadamu wakawa wanatumia vitu vyema kutimiza makusudi yao mabaya kinyume cha Mungu.

Hakuna kitu kibaya alichokiumba Mungu, kila alichokiumba aliona kuwa ni chema, ila kwa sababu ya dhambi wanadamu walianza kutumia vibaya vyema walivonavyo. Ni muhimu ukaelewa kuwa, matumizi mabaya ya chema ulichonacho yanaleta matokeo mabaya. Hii haimaanishi kuwa kile chema ulichonacho kimegeuka na kuwa kitu kibaya isipokuwa wewe mwenyewe ndio umegeuka na kuwa na nia mbaya na kwa sababu hiyo ukatumia vibaya kitu chema ulichonacho ndani yako.

Ni muhimu sisi sote tukajua kuwa, si kwa sababu kitu alichonacho mtu ambacho Mungu aliweka ndani yake ni kibaya na ndio maana kimeleta matokeo mabaya, hapana, kitu ni chema ila matumizi mabaya ya kitu chema ndiyo yanayoleta matokeo mabaya. Tatizo si kitu, tatizo liko kwa mtumiaji wa hicho chema kilichomo ndani yake. Chochote ambacho Mungu ameweka ndani yako ni kitu chema sana, na kipo kwa ajili ya kukurahisishia wewe kutimiza kusudi la Mungu maishani mwako, kwa hiyo havina ubaya kabisa.

Ushawishi na ubembelezi wa mwanamke hauna ubaya kabisa, ni vitu vyema ambavyo Mungu aliviweka ndani ya mwanamke ili aweze kutimiza makusudi yake aliyokusudiwa na majukumu yake ya Kujenga na kulinda nyumba yake pamoja na kulea. Matumizi mabaya ya hazina hizi ni matokeo ya tamaa mbaya na ubinafsi wanaokuwanao wanawake wengi.

Usipotumia hazina uliyonayo ndani yako ya ushawishi na ubembelezi vizuri, badala ya kujenga na kulinda nyumba yako utabomoa nyumba yako kwa mikono yako mwenyewe na utampa adui nafasi ya kuingia na kuharibu kila kitu chema.

nataka tuangalie juu ya MATUMIZI MAZURI YA NGUVU YA USHAWISHI NA UBEMBELEZI NDANI NA NJE YA FAMILIA YANAYOLETA MATOKEO MAZURI KATIKA NDOA NA FAMILIA na si tu katika familia na pia katika jamii nzima. Katika somo letu leo, nataka tutumie uwezo aliopewa mwanamke katika kujifunza matumizi mazuri na nguvu ya ushawishi na ubembelezi alionao mwanamke.

Tutapata nafasi ya kuangalia mambo mbalimbali ambayo kwayo mwanamke anaweza kuyatumia vizuri kushawishi na kubembeleza kwa nia ya kujenga na kulinda ndoa yake, familia yake, na jamii yake kwa ujumla, lakini hasa nitajikita kwa upande wa ndoa yake.

JAMBO LA KWANZA: Maneno na Sauti: Uwezo wa kuzungumza:

Mithali 7:21
Kwa maneno yake mengi na ulaini (wa sauti yake) akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.

Kuna nguvu ya ushawishi katika maneno ya mwanamke, na katika midomo yake kuna uwezo wa ubembelezi ambao mwanaume hawezi kuponyoka iwapo mwanamke atatumia uwezo huu kwa ulaini wa maneno yake mazuri yanayotokana na sauti laini na nyororo inayobembeleza moyo wa mwanaume.

Mara zote ushawishi na ubembelezi ni lazima uambatane na ulaini wa maneno na sauti ili ukamilike na kufanikiwa. Kama hapatakuwa na ulaini wa maneno na sauti basi, hapo hakuna ubembelezi wala ushawishi. Lengo la ushawishi na ubembelezi si kupata vitu vya mwanaume ila ni kuupata moyo wa mwanaume, si kwa kusudi la kuutawala bali kwa kusudi la kujenga kwa wewe kuonyesha upendo wako kwake na utii wako kwake.

Nasikitika kusema kwamba, wanawake wengi wamepoteza waume zao kwa sababu wametumia vibaya vinywa vyao.

Moyo wa mwanaume ni dhaifu sana kwa mwanamke na hasa mwenye ushawishi na ubembelezi unaoambatana na ulaini wa maneno na sauti. Lakini moyo huo ni mwoga sana kwa mwanamke mwenye ukali wa maneno na sauti ngumu. Kama ulikuwa hujui, leo ujue sasa, moyo wa mwanaume unahitaji ubembelezi na ushawishi kwa mwanamke kuwa laini katika maneno yake na sauti yake ili upate kulainika.

Siku zote moyo wa mwanaume huwa ni mgumu sana kukubali hoja zinazokinzana na hoja zake na hasa hoja za mwanamke, lakini kwa ushawishi na ubembelezi mwingi wenye ulaini wa maneno na sauti, moyo wa mwanaume huwa hauna ujanja kabisa. Biblia inasema, Jawabu la upole utuliza hasira, si zaidi wakati wa amani, maneno matamu hufichua siri zilizositirika zilizomo moyoni mwa mwanaume.

Mwanaume shujaa wa vita, mwenye nguvu hurainishwa na ubembelezi na ushawishi wa mwanamke mwenye maneno na sauti laini. Mkumbuke Samsoni, pamoja na kuwa hodari mwenye nguvu nyingi, lakini kwa ulaini wa maneno na sauti ya Delila alisalimu amri, moyo wake ulilainika mpaka akaitoa siri ya nguvu zake ambayo hakuitoa kwa mtu mwingine yeyote isipokuwa kwa Delila (Soma Waamuzi 16).

Moyo wa mwanaume unaposikia maneno matamu, laini yanayoambatana na sauti laini huwa unanywea na kutulia na kisha kuanza kusikiliza. Mwanaume anaweza kukwepa kama Samsoni lakini mwisho wa siku ataisalimu amri tu. Na kwa sababu hiyo, wewe mkewe ukikosa ushawishi na ubembelezi, mumeo atautafuta kwa mwanamke mwingine hata kama atakuwa ni kahaba.

Jeshi la Wafilisti pamoja na kuwa na nguvu nyingi na uwezo mkubwa, walimshindwa Samsoni, lakini kwa sababu walikuwa wanajua nguvu ya ushawishi na ubembelezi iliyomo ndani ya mwanamke walilazimika kumtumia mwanamke. Wafilisti walimtumia mwanamke katika nyakati mbili tofauti kupata siri kutoka kwa Samsoni. Mara ya kwanza walimtumia mwanamke ambaye alikuwa ni mke wa Samsoni kutegua kitendawili cha Samsoni. Kwa ubembelezi na ushawishi wa maneno laini na matamu yaliyoambatana na kilio Samsoni alijikuta anatoa siri (Soma Waamuzi 14).

Walipotaka pia kujua siri ya nguvu za Samsoni, walimtumia mwanamke Delila ambaye alikuwa ni mke wa Samsoni. Mwanamke kupitia ushawishi na ubembelezi wake ana uwezo mkubwa wa kuufanya moyo wa mwanaume ufunguke, na uwe wazi mbele zake. Mwanamke yeyote anayetumia kinywa chake vizuri, hakuna siri ya mumewe iliyofichika kwake kwa sababu moyo wa mumewe u wazi wakati wote. Mwanaume yeyote hawezi kumficha mwanamke mwenye ubembelezi na ushawishi siri yoyote, hata kama atamficha ni kwa muda mfupi, hawezi kudumu katika kumficha, atuufunua moyo wake. Tutakapoendelea kujifunza somo hili utaelewa vizuri. Lakini kumbuka hazina hii ndani ya mwanamke ni kwa ajili ya KULINDA NA KUJENGA NYUMBA YAKE NA SI VINGINEVYO.

Tumia kinywa chako kutamka maneno matamu, na tumia sauti yako kuuteka moyo wa mumeo na kuusogeza karibu na moyo wako badala ya kutumia kinywa chako kumsogeza mumeo mbali nawe.

JAMBO LA PILI: Chakula: Uwezo wa kupika chakula kitamu akipendacho mumewe.

Mwanamke amepewa uwezo wa kupeka chakula kitamu akipendacho mumewe. Ndani ya chakula kitamu akipendacho mume kilichopikwa na mkewe kuna nguvu ya ushawishi na ubembelezi. Mwanaume ni dhaifu sana anapokula chakula kitamu akipendacho kilichopikwa na mkewe kwa namna maalumu sana na kupewa au kuandaliwa kwa namna ya kipekee sana.

Mke, unapoandaa chakula kile akipendacho mumeo kwa namna maalumu sana na kukitenga katika mazingira ya pekee sana huku na wewe ukiwa umejiandaa kwa kuvalia mavazi yanayokupa muonekano wa pekee sana kwa mumeo wenye mvuto, meza ikiwa na maua na mishumaa pamoja na marashi ayapendayo mumeo, kisha ukamkaribisha kwa namna ya upole na ubembelezi na ulaini wa maneno na sauti yako, utauyeyusha moyo wake kabisa.

Chakula pamoja na ulaini wa maneno na sauti yako, pamoja na uwepo wako wenye mwonekano wa kuvutia na kupendeza, utamshawishi mumeo sana sana.

Sauti yako laini na nyororo itapendeza masikioni mwake, maneno yako matamu, na yaliyo laini yatapendeza moyoni mwake, chakula chako kitamu kile akipendacho kitapendeza kinyani mwake, harufu nzuri ya manukato yako uliyojipulizia itapendeza puani mwake, na muonekano wako mzuri wa mavazi mwilini mwako na uso wako wa kuvutia utapendeza machoni mwake; kwa hali hii unafikiri atachomokea wapi?

Zungumza naye vizuri kwa ubembeleze wa maneno matamu na sauti laini, mpikie chakula kizuri kile akipendacho, vaa vizuri nguo zinazoleta ushawishi machoni pake zitakazomfanya macho yake yasibanduke kwako, jipulizie manukato mazuri yatakayomfanya kila wakati pua zake zichezecheze kwa kuvuta hewa, harufu itakayomfanya kila wakati atake kuwa karibu nawe pembeni yake; usikae kihasara-hasara tu. Uwe ni mwanamke mwenye ushawishi wa kujenga ndoa yako na si wa kubomoa ndoa yako. Nia yako iwe njema na usiwe na ubinafsi.

Tatizo la wanawake wengi wamechukulia kirahisi maswala ya ndoa zao, mazoea yamepata nafasi, wanafanya mambo kwa mazoea, na wanaishi na waume zao kwa mazoea. Na kwa sababu hiyo makahaba wamejua udhaifu wao na udhaifu wa waume zao, wanawaiba kwa ushawishi wa maneno na chakula chao wanachowapikia. Sasa wewe jiweke kihasara hasara, uwe mkali na mkorofi kwa mumeo na umwachie binti wa kazi au watoto wako wampikie chakula kila siku, akibaki kwako njoo kwangu mimi nikupongeze, ila akiondoka basi jipongeze badala ya kukaa na kulia-lia.

Esta alitumia nguvu ya chakula kumshawishi mumewe kinyume cha rafiki yake kipenzi ambaye alikuwa ni Adui wa Esta na familia yake au watu wake. Naamani alikuwa ni rafiki wa mfalme lakini ni adui wa Esta na Israeli yote, na mwenye mamlaka na nguvu ya kumwangamiza Naamani alikuwa ni mfalme ambaye ni mume wa Esta.

Haikuwa kazi rahisi kugeuza makusudi ya mfalme, lakini kwa sababu Esta alijua siri ya nguvu ya chakula, mwonekano wake na maneno yake laini, matamu ya kupendeza, alitumia vizuri nguvu ya chakula na maneno yako kukabiliana na adui yake kwa kumshawishi mfalme. Moyo wa mfalme uliyeyuka mbele ya chakula na mbele ya maneno ya Esta yaliyokuwa na ushawishi mkubwa na ubembelezi mwingi wenye tija. (Soma Kitabu cha Esta).

JAMBO LA MUHIMU SANA.
Unajua, huwezi kufanya mambo haya kama huna nia ya dhati, utii na upendo wa kweli kwa mumeo. Kama unamtii na kumpenda ushawishi wako utakuwa na maana na utazaa matunda. Ushawishi unafanya kazi pale tu palipo na utii wa kweli na kujitoa kikamilifu kwa mumeo. Kama huna utii kwa mumeo na kujitoa kwake ushawishi wako utakuwa kama matusi mbele zake. Kabla ya ushawishi na ubembelezi hutangulia kwanza utii wa kweli. Pasipo hutii ushawishi wako na ubembelezi wako hauwezi kukuzalia matunda mema zaidi ya kukataliwa na kupingwa. Mtii mumeo, mshawishi na kumbembeleza kama unataka kujenga ndoa yako.

Căutare
Categorii
Citeste mai mult
EXODUS
Verse by verse explanation of Exodus 7
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 62 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-21 14:23:46 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
UNAFAHAMU NINI KUHUSU HERODE?
Picha kutoka Google.   Kwa ufupi… Bwana Yesu asifiwe… Hivi unafahamu ni nini...
By GOSPEL PREACHER 2022-03-30 05:12:08 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
AGIZO LA KUTAWADHANA
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        ...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-12 00:56:05 0 9K
Food
MAPISHI MBALIMBALI
BIRIANI VITU VINAVYOHITAJIKA:- Mafuta ya kula Nyama kilo 1 Vitunguu maji kilo 1 Viazi mviringo...
By tabitha Prosper 2023-02-08 12:50:05 2 6K
Injili Ya Yesu Kristo
KWA NINI WIVU NI DHAMBI
Kwa nini wivu au husuda ni dhambi? (Wagalatia 5: 19-21.) Wakati wivu unapoibuka na unauacha uishi...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-19 07:35:34 0 5K