KWA NINI WATU WENGI WANAUMIA BAADA YA KUINGIA KWENYE MAHUSIANO?

0
5K

Kumekuwa na takwimu nyingi za wachumba na wanandoa kuumia mara tu au muda mfupi baadaye baada ya kuingia katika mahusiano ya uchumba au ndoa. Zipo sababu nyingi lakini leo naomba niseme au tujifunze hizi chache.

SABABU YA KWANZAKukosa maarifa na ufahamu.

Kuna msemo wa kiingereza unaosema hivi, "Knowledge before marriage" wenye maana ya "Maarifa kwanza kabla ya ndoa". Biblia inasema, Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Maarifa ni ufahamu unaomuwezesha mtu kutekeleza au kuendesha maswala mbalimbali ya muhimu ktk maisha yake. Ni taarifa muhimu zinazompa mtu ujuzi juu ya mambo fulani katika maisha yake unaomuwezesha kuendesha maisha yake katika usahihi. Maarifa ni ujuzi ni ufahamu.

Wachumba wengi na wanandoa wengi wameingia ktk mahusiano bila ya kuwa na maarifa. Wengine wanaingia kwanza ndipo wanaanza kuyatafuta maarifa, hii ni ngumu sana. Huwezi kufaulu ktk jambo lolote bila ya kuwa na maarifa. Kukosa maarifa kunasababisha makosa mengi. Na makosa mengi yanasababisha maumivu. Ukiwa na maarifa juu ya ndoa, hautaingia kwenye mahusiano na mtu yeyote. Maarifa ni mlinzi, anakulinda na mtu mbaya. Maarifa yatakusaidia kufahamu japo kwa sehemu yupi ni mwema kwako. Ukitaka kukosea kosa maarifa, lazima tu utakosea. Si vyema nafsi ya mtu ikakosa maarifa.

Lakini kwa upande mwingine, maarifa ni pamoja na kumsoma mtu kitabia kabla ya kuingia ktk mahusiano ya uchumba. Maarifa ni pamoja na kusoma hisia za mtu unayetaka kuingia naye kwenye mahusiano. Ni pamoja na kuhakiki na kuthibitisha upendo wake kwako. Kosa wanalofanya wengi wanafanya hivi baada ya kuingia kwenye mahusiano ndio maana wanaumia. Usiingie kwenye mahusiano ndipo uanze kusoma na kuchunguza tabia ya mwenzi wako. Chunguza kwanza, ukishaijua na ukawa na uhakika na tabia yake, na kufahamu kuwa unaendana nayo, ndipo fanya maamuzi ya kuingia.

Usiingie kwenye mahusiano ukiwa huna uhakika kama mtu unayeingia naye kwenye mahusiano anakupenda hata kama wewe unampenda. Tafuta kwanza kujua kama kweli anakupenda. Hii itakusaidia kutokuumia hasa pale anapoonyesha tabia ambazo kwako zinatafisirika kama si upendo. Badala ya kuumia utamsaidia, badala ya kudhani anafanya vile kwa sababu hakupendi utasema pengine amejisahau, kwa nini? Kwa sababu unajua na unauhakika anakupenda. Lakini kama umeingia kwenye mahusiano bila kujua hili litakusumbua sana, na kila tendo usilolipenda atakalolifanya litakupa tafsiri ya kwamba, Ni kwa sababu hanipendi ndio maana hajaja kuniona wakati naumwa au hajanipa hongera, au hajanibusu nk.

Maarifa kwanza kabla ya ndoa, au mahusiano ya uchumba. Hii itakusaidia kupunguza makosa na maumivu mengi ktk mahusiano yenu.

Lakini pia, maarifa inamaanisha na kujijua wewe mwenyewe kwanza kabla haujaingia katika mahusiano ya uchumba au ndoa. Usiingie kwenye mahusiano ukiwa hujui kama tabia zako ni nzuri na zinamfaa huyo unayetaka kuolewa naye au kumuoa, itakusumbua wewe na itamsumbua yeye. Usiingie kwenye mahusiano ukiwa hujui kama hizo hisia unazozisikia kweli kumuhusu mtu huyo ni UPENDO au ni tamaa tu. Usiingie bila kujua hili utaumia na utamuumiza mwenzi wako. Ni vizuri ukajijua kwanza ndipo ukaingia katika mahusiano.

Ni kweli, usiingie kwenye mahusiano na mtu ambaye humjui. Hujui tabia zake, lakini hujui moyo wake kuhusiana na wewe mwenyewe. Upendo hukaa moyoni, na tabia pia hukaa moyoni. Mtu anaweza akawa na tabia nzuri zinazokufaa lakini moyo wake ukawa mbali nawe. Pengine kabisa anaweza akawa anakutamani ktk fikra zake, lakini moyoni mwake haumo. Ni vyema ukatafuta kwanza kumjua. Ujue moyo wake kwanza kuhusiana na wewe. Ujue familia yao, mazingira anapotaka. Ukiwa na uhakika chukua hatua.

Kama mtu mwenye tabia nzuri zinazokufaa moyo wake utakuwa mbali nawe, mtakapokuwa pamoja lazima tu, uzuri wake wa tabia utageuka na kuwa ubaya. Utashangaa kwa wengine anakuwa na tabia nzuri lkn kwako ni vikwazo mara kwa mara. Kwa nini, kwa sababu moyo wake haukuelekei wewe, na kwa sababu moyo wake haupo kwako lazima atakuwa mzito kukutendea mambo mema mazuri ambayo pengine kabla ya kuwa naye katika mahusiano alikuwa anakutendea.


SABABU YA PILI: Hawaombi kabla ya kuingia, wanaomba baada ya kuingia katika mahusiano.

Hii ni sababu ya pili. Watu wengi huwa hawaombi kabla ya kuingia katika mahusiano, huanza kuomba baada ya kuingia kwenye mahusiano na hasa pale wanapoona kuna matatizo. Hata hivyo idadi kubwa ya watu wanaoomba kabla ya kuingia katika mahusiano huomba kisha wakatafuta kujibu maombi yao wenyewe. Wanamuomba Mungu lakini hawampi nafasi ya kuwajibu maombi yao na badala yake wanaanza kujijibu wao wenyewe.

Ni majibu ya Mungu tu ambayo hayana kujuta ndani yake, mengine yote nje ya Mungu yana majuto.

Kama unamwamini Mungu basi mkabidhi mahitaji yako yote, kisha fuata kanuni zitakazokuongoza ktk kumpata mwenzi wako. Utawaona wengi na watakuja wengi, itashangaza sana iwapo utaoa au kuolewa na mtu ambaye hajaokoka na ukasimama kumshukuru Mungu eti amejibu maombi yako. Mwache Mungu akujibu maombi yako, usijijibu wewe kisha ndio uombe, wala usiombe kisha ujijibu wewe mwenyewe.

Unaomba nini wakati umeisha chagua majibu yako mwenyewe. Omba ukiwa huna jibu lolote, na usijitafutie majibu yako mwenyewe, lazima tu utaumia utakapoumizwa.

Kikanuni za Biblia ni kwamba, mtu anapaswa kuomba kwa ajili ya jambo fulani mapema mara tu baada ya kufahamu kuwa linamuhusu na atalihitaji hata kama si sasa na hata kama hajui ni lini, tena aombe kwa bidii bila kukoma huku akimpa Mungu nafasi ya kujibu maombi yake. Na hata baada ya maombi yake kujibiwa basi anapaswa kuendelea kuomba. Kwa nini? Kilichopatikana kwa maombi hutunzwa, huifadhiwa na kuboreshwa kwa maombi. Maombi huwa hayakomi eti kwa sababu umepata ulichokuwa unakiomba. Lakini ni muhimu ukakumbuka kuwa, huwezi kumuomba Mungu halafu ukajijibu wewe mwenyewe.
Kwa sababu ya watu wengi kukosea kanuni hii, wamejikuta wakiumia sana na kuumizana sana mara tu baada ya kuingia katika mahusiano ya we ya uchumba au ndoa.

SABABU YA TATU: Msukumo unakuwa si upendo ila ni tamaa.

Tamaa huwa na msukumo wake ktk hisia, tamaa huendesha hisia za mtu na kuzitawala. Tofauti na upendo, wenyewe hauko kabisa kwenye hisia, hauanzi na hisia, unaanza na wazo moyoni, ni Neno linalozungumza moyoni. Huanza kidogo kidogo kisha hukua na kuchukua nafasi katika moyo wa mtu. Baadaye kidogo hufuatiwa na uchaguzi kisha maamuzi ya kumpenda mtu ambaye moyoni ulikuwa umemuwazia. Katika hatua hii hausikii hisia yoyote kabisa ya kimapenzi kumuhusu. Pengine unaweza kuwa unamuona kama dada yako au kaka yako, tofauti na tamaa.

Tamaa haianzi na wazo, inaanza na msisimuko wa kihisia pindi unapomuona binti au kijana fulani na kuvutiwa naye na hasa katika vitu vile unavyovipenda na kuvitamani alivyonavyo muhusika. Au pindi unaposikia maneno matamu ya ubembelezi ya kimapenzi yanayoamsha hisia zako na yanayoufanya moyo wako ujisikie vizuri. Ghafula utaanza kuona moyo unaenda mbio usipomuona huyo mpenzi wako, ukimuona anaongea na mwingine mara unamuhisi vibaya nk.

Biblia inasema, Upendo huamini yote, wewe ukiona humwamini mwenzi wako kila wakati unamtilia mashaka jua humpendi. Na kwa sababu hiyo utaumia tu na pengine utamuumiza. Ukimpenda utamwamini.

Upendo ustiri wingi wa makosa. Wewe ukiona huwezi kusamehe makosa ya mwenzi wako jua hukumpenda tangu mwanzo. Upendo hauhesabu mabaya. Ukiona unahifadhi kumbukumbu ya mabaya ya mwenzi wako jua humpendi. Kama unampenda utamsamehe makosa yake na kumsitiri pale anapokosea.

Upendo huvumilia yote. Kama hawezi kumvumilia mwenzi wako, jua huo si upendo ilikuwa ni tamaa tangu mwanzo. Ukimpenda utamvumilia, utambebea udhaifu wake.

Upendo haukosi kuwa na adabu. Wewe kama unamkosea adabu mwenzi wako kwa sababu tu amefanya jambo usilolipenda, basi ni kwa sababu humpendi. Kama umemtukana na kumsema kwa maneno mabaya na matusi, umemvunjia adabu, hivyo humpendi. Kama unampenda utamstahi na kumuonea adabu mbele za watu na sirini.

Upendo hautafuti mambo yake wenyewe. Ukiona unajiangalia sana wewe mwenyewe hata pale mnapokorofishana na kutofautiana jua kuwa wewe huna upendo. Unajua ukitaka kujua mtu anayekupenda kweli mwangalie pale mnapokuwa mmekorofishana, kama kamba huvutia kwake na hujihesabia haki, na pia akiwa hajali namna unavyojisikia wewe, yeye ni yeye tu, jua hakuna upendo hapo. Lakini kama anakupenda, hata kama yeye hana makosa ataubeba msalaba yeye mwenyewe, na kisha kutafuta njia ya kumuelewesha wakati wa amani na utulivu.

Mambo yote haya ni kinyume na mahusiano yaliyo na msukumo wake ktk tamaa. Tamaa haivumilii, ni ya ubinafsi, inatafuta mambo yake yenyewe, haisamehi, ipo kibiashara zaidi, inadai kupokea na haiko tayari kutoa. Yaani ni shida tupu, haina adabu kabisa, ikitamani imetamani. Huteka na kutawala hisia za mtu na kuziendesha, huanza kwa kiwango kikubwa sana na kwa gharama yoyote mpaka ipate matamanio yake.

Sasa, mahusiano yoyote yenye chanzo chake ktk tamaa, lazima yatasababisha maumivu. Kwa nini? Kwa sababu mahusiano yanahitaji upendo ili kuwa salama na yenye kuleta furaha kwa kila upande. Upendo si tamaa na tamaa si upendo na hivi haviwezi kukaa pamoja, kikiwepo kimoja, kingine hakipo.

SABABU YA NNE: Mtu anaoa au anaolewa kwa sababu ameona wengine wameoa au kuolewa.

Kabla sijaifafanua hoja hii, napenda kwanza nikupe hadithi moja ya Biblia itakayokusaidia kunielewa.

Mara tu baada ya kutoka nchi ya Misri na kuingia nchi ya Kanani, Israeli walitawaliwa na waamuzi ambao waliinuliwa na Mungu. Hawakuwa na mfalme kama mataifa mengine. Lakini baada ya miaka kadhaa kupita, walianza kutamani kuwa na mfalme kama mataifa mengine walivyo na wafalme. Wakamwambia Nabii Samweli awatawazie mfalme ili wawe na mfalme kama mataifa mengine.

Samweli aliwaghadhabikia, na Mungu pia hakufurahishwa na ombi lao hilo. Lakini Mungu alimwambia Samweli awatawazie mfalme kama watakavyo ila yeye Mungu ndiye atakayemchagua.

Swali la kujiuliza ni kwamba, Je, ni kweli Mungu alikusudia wasiwe na mfalme milele? Hapana, Mungu alitaka wawe na mfalme lakini kwa wakati ambao yeye alikuwa amekusudia. Wakati ambao Israeli wanadai mfalme ulikuwa si wakati uliokusudiwa na Mungu, na hivyo Mungu hakuwa amekamilisha maandalizi ya kumwandaa mfalme atakayemtumia kuitawala Israeli.

Unaweza usinielewe, lakini utanielewa tu. Tangu mwanzo Mungu alikusudia kuitawala Israeli kwa kujitwalia wafalme kwa Agano la milele kutoka katika kabila la Yuda, na kutoka ktk kabila hili ajitwalie Masihi, Yesu Kristo atakayewaokoa wanadamu na dhambi zao. Alikusudia aanze na Daudi, lakini wakati Israeli wanataka mfalme Daudi alikuwa bado hajamaliza kuandaliwa kuwa mfalme na ndio sababu Mungu alimpaka mafuta Sauli awe mfalme. Haikupita muda mrefu, Sauli akawa mwiba kwa Israeli na akawa mkaidi kwa Mungu. Mungu akajuta kumpaka mafuta Sauli awe mfalme.

Sasa kama Mungu alikuwa anajuta, je Israeli walikuwa katika hali gani? Sauli hakuwa matakwa ya Mungu, yalikuwa matakwa ya Israeli, Sauli hakuwa kusudi la Mungu, alikuwa ni matamanio ya Israeli na ndio maana Mungu anajuta. Mungu kamwe huwa hajutii matakwa na makusudi yake. Ukiona anajuta jua anajutia matakwa ya wanadamu.

Mungu aliwapa waisraeli mfalme sawasawa na matakwa yao kwa wakati walioutaka wao kwa sababu Israeli walitaka wafanane na mataifa mengine kwa kuwa na mfalme kama mataifa mengine walivyokuwa na wafalme. Lakini baada ya miaka kadhaa walianza kujuta, kuumia, na kuteseka kwa sababu ya maamuzi yao. Hivyo walisubiri Sauli afe kwanza ndipo wawe na mfalme ambaye Mungu aliwachagulia kulingana na kusudi lake.

MUHIMU SANA:
Watu wengi wamekuwa wakiumia mara tu baada ya kuingia kwenye mahusiano kwa sababu waliingia kwa sababu waliona watu wengine wamo kwenye mahusiano. Wengi wamekuwa wakilazimika kuolewa au kuoa baada ya kuwaona watu wengine wanaoa au kuolewa.

Katika kipindi hiki cha watu kuoa au kuolewa, wadada wengi au wakaka wengi ambao hawajaolewa au kuoa huwa na misukumo mikubwa ya kutaka kuwa kama wenzao. Hujiona kana kwamba wameachwa nyuma sana. Huanza kuona kana kwamba wamechelewa. Kwa sababu hiyo huanza kuwa na harakati za kuingia kwenye mahusiano ili waoe au waolewe kama wenzao walivyo. Hii ni hatari sana kwa sababu mtu huamua kuoa au kuolewa na yeyote atakayekuja. Kwa nini? Kwa sababu, ili uolewe au kuoa kwa kusudi la Mungu na kwa chaguo la Mungu unapaswa kusubiri kwanza. Utakapoharakisha utatoka nje ya kusudi la Mungu. Utaoa au kuolewa na mtu ambaye hakukusudiwa na Mungu. Utaumia na utamfanya Mungu ajute. Na kama mmekwisha funga ndoa huwezi kubadili maamuzi yako mpaka huyo afe ndipo uoe au kuolewa na mwingine.

Usioe wala usiolewe kwa sababu wengine wameoa au kuolewa, utajuta. Olewa au oa kwa sababu Mungu amekusudia jambo hilo. Usiharakishe, kuwa na subira mpaka wakati ambao Mungu amekusudia wewe uoe au uolewe.

Usife moyo unapoona wenzako wanaoa au kuolewa, ukiona hivyo wewe jua kuwa kama wakati wao umefika wakati wako unakuja. Hakuna kizuizi; wanaume kuwa wachache si kizuizi, umri wako si kizuizi, umasikini si kizuizi, mazingira uliyonayo si kizuizi. Wewe jitulize, piga moyo konde umngoje Bwana, ana mpango kabambe nawe.

Ubarikiwe sana,

Site içinde arama yapın
Kategoriler
Read More
OTHERS
IS MUHAMMAD THE SPIRIT OF TRUTH?
Today I will answer Muhammadans with biblical proof that Muhammad was not the Spirit of Truth as...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 02:25:52 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
DHIKI KUBWA
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        ...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-12 01:08:15 0 6K
MAHUSIANO KIBIBLIA
NIFANYE NINI ILI KUSHINDA TAMAA ZA MWILI?
Septemba mwaka 2011, Mwanafunzi mmoja wa shule ya Sekondari alinitembelea nyumbani kwangu hapa...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:16:15 0 6K
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Deuteronomy 27
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 06:44:41 0 5K
REVELATION
JIFUNZE UFUNUO SURA YA 4
Shalom! Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo tukiendelea na ile sura ya 4, tulishakwisha...
By GOSPEL PREACHER 2021-10-30 08:59:40 0 5K