HATUA ZA KUINUKA BAADA YA KUANGUKA

1
6KB

Bwana Yesu asifiwe! Huna sababu ya kubakia hapo chini baada ya kuanguka majaribuni. Kwa hiari yako na uweza wa Bwana unaweza kugeuza kisiki kilichokuangusha kuwa kigogo cha kuvushia kwenye ushindi. Kwa kuzingatia hatua zilizoainishwa kwenye Biblia, mdhambi yeyote anaweza kuinuka kutoka sakafuni mpaka vileleni. Muhimu kati ya zote ninazozifahamu kutoka katika Maandiko, ni hizi hapa:

  1. Kumbuka ulivyoanguka majaribuni.

kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza (Ufu. 2:5)

Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia Bwana tena (Omb. 3:40).

Badala ya kutafuta kunyanyuka haraka haraka, tafuta kuokota masomo ya kuondoka nayo kutoka hapo sakafuni. Aibu itakuharakishe unyanyuke haraka kabla wengi hawajajua. Usikubali. Badala yake tulia ujiulize nimefikaje hapa? Chukua muda kujifunza. Jambo la muhimu sio hadhi yako mbele ya jamii kama usalama wako mbele yako. Usipogundua kisiki kilichokuangusha sasa, unajuaje huko mbele utakiona na kusalimika?

Chukua muda hapo chini kujiuliza maswali kadhaa. Ninawajibika kiasi gani na yaliyonipata? Nilikuwa katika hali gani kabla ya anguko (nimechoka, sina la kufanya)? Nilikuwa na nani na wapi? Nilikuwa na matarajio gani nilipokubali ushawishi. Nimeyapata niliyoyatarajia? Ninahitaji nini hasa maishani? Nimeumia kiasi gani kwa uamizi wangu? Nimewaumiza wengine kiasi gani? Usipochukua muda kuhangaika na maswali haya kutaka kujua kilichokuangusha una hakika ya kusimama ili kuanguka tena hapo hapo.​

 

  1. Tambua kuanguka majaribuni sio mwisho.

Mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena (Mit. 24:16).

Mateso[raah kiebrania, au mabaya, majeraha, fedheha, fadhaa] ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote. (Zab. 34:19)

Mtoto wa Mungu haanguki kama mende, habaki chini akipigapiga miguu juu mpaka atakaponyamaza milele. Mwenye haki akianguka hatanata kama gundi sakafuni bali atanyanyuka. Mungu hachoki kuwanyanyua wanaodondoka dondoka. Mungu kama mzazi yeyote yule anajua wanawe hujifunza kutembea kwa kuanguka. Usimsikiliza adui anayetaka kukumalizia hapo chini akikuambia, 'Mungu hana kazi na mtu asiyejiweza kama wewe'. Mungu aliye mwenye uchungu na wanawe zaidi kuliko mama mzazi kwa mtoto amyonyeshaye hatawasahau wanawe. Kamwe hatatelekeza wanawe wenye nia ya kutenda mema lakini wameishia kutenda mabaya kwa sababu ya udhaifu wa mwili. Hakumwacha Samsoni na Daudi na Sulemani na Petro walipoanguka mara kwa mara na hatakuacha wewe pia. Kwa Mungu hakuna aliyeshindikana, hata maji yaliyomwagika yanazoleka. Kuteleza majaribuni sio kufikwa na mauti.

  1. Jua Mungu ametangulia kukusamehe.

Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo (Luk. 23:34)

Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake (Rum. 5:10)

Kama Yesu aliwaombea msamaha waliomsulubisha msalabani hata kabla hawajamuomba msamaha, si zaidi sana watoto wake wanaoumia na kuugua kwa sababu wamemkasirisha Baba yao wa mbinguni? Tambua Mungu amekwisha kukusamehe kwa sababu Yesu yungali hai mbele ya Baba akuombee (1Yoh 2:12). Kabla hujapata maneno sahii kueleza masikitiko yako Roho wa Mungu amekwisha kukusemea (). Ndiyo maana Bwana ananena kwa kinywa cha nabii Isaya akisema, “na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.” (Isa. 65:24). Mungu hakuonei hasira kwa sababu umepoteza maisha yako dhambini. Na hana uchungu tena nawe.

Yesu amekwisha kunywa kikombe cha ghadhabu ya Mungu dhidi ya dhambi zako ulizotenda na unazotokea kuzitenda mpaka tone la mwisho, kwa nini akuonee ghadhabu? Endapo unaendelea kukiri dhambi zako na kukubali wokovu wake atakosaje kuchukuana nawe katika mambo ya udhaifu? Nani kama siye Mungu mwenye kukufahamu na kukukumbuka kuwa u mavumbi tu? (Zab 103:14). Hakika Mungu hakuhesabii adhabu unapoendelea kumkiri Yesu kama mwokozi anayeweza kukusafisha na udhalimu wako wote.

Pamoja na mabaya uliyotenda, badala ya kukudai adhabu Mungu anakulipa mema. Amekuandikia hundi kwa jina lako inayosomeka "amesamehewa".​

 

  1. Pokea msamaha wa Mungu.

Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Isa. 1:18

Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. Ebr 11:6

Kabla hujanufaika na msamaha uliotolewa, sharti uupokee msamaha huo. Kwanza uupokee kwa kusemezana na Mungu katika toba. Kweli Mungu amekuandikia hundi ya msamaha lakini ni lazima uipeleke hundi hiyo benki ya Golgotha kabla haujavuna baraka zake. Ufikapo hapo dirishani, mwambie Mungu, 'nimekosa.' Hata kama makosa yako yananuka kama damu na kutisha kama rangi nyekundu, ukisikiyasikitikia na kuomba usamehewe, Mungu ni mwaminifu kukusamehe kabisa kabisa (Isa 1:18;1Yoh 1:8,9).

Pili, unapokea msamaha wake kwa kuamini ameipokea toba yako na kukusamehe. Ukiwa na mashaka haiwezekani kumpendeza. Yeyote amwendea Mungu juu ya magoti ni sharti aamini Yeye yuko na kwamba hafichi uso wake wa rehema kwa wale wamtafutao (Ebr 11:6). Usijiadhibu kwa makosa uliyoyaungama. Amini kwa moyo wako umesamehewa ili utembee katika nuru ya wokovu pasipo kivuli cha hatia kikikufuata nyuma yako. Ana "heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake" (Zab 32:1).​

  1. Chukua dhamana kwa madhara uliyosababisha

Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Mat. 23,24

Pamoja na kwamba umepokea msamaha bure kwa makosa uliyotenda, bado unawajibika kwa madhara uliyosababisha. Dhambi ni mkanda wa bomu ambao ukilipuka unakudhuru wewe na waliokuzunguka. Umeumia lakini wameumia pia. Kunyanyuka toka mavumbini pasipokufanyaa kitu kwa wale uliowaangusha ni kujisahau kusikokubalika. Ni dharau kwa Mungu kumkimbia ndugu yako nyumbani unayewiwa naye huku ukikimbiza kupeleka sadaka madhabahuni. Wajibika kumrudishia jirani yako haki uliyompora.

Lakini, unaweza kuuliza ninaanzia wapi sasa? Ni kweli madhara mengine yanaweza kuwa nje ya ufahamu au uwezo wako kushugulika nayo. Lakini kadri iwezekanavyo punguza makali ya athari ya makosa yako kwa uliowadhuru. Unawakumbuka? Waorodheshe. Waombe radhi uliowaumiza; isipokuwa, kama kwa kufanya hivyo utamdhuru muathiriwa zaidi. Warudishie uliyowapokonya yanayowezekana kurejeshwa. Wajibika kwa madhara uliyosababisha na ugundue uhuru na furaha inayopatikana kwa kukiri kama Zakayo alivyoungama (Luk 19:8).​

 

  1. Kubali Mungu akurekebishe

Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu… Maana yale yasiyowezekana kwa sheria, kwa vile ilivyokuwa dhaifu kwa sababu ya mwili, Mungu, kwa kumtuma Mwanawe mwenyewe katika mfano wa mwili ulio wa dhambi, na kwa sababu ya dhambi, aliihukumu dhambi katika mwili. Warumi 7:24,25; 8:3

Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. 1Kor 15:57

Ndiyo ninataka kupona, lakini mbona mazoea yana taabu?! Mbona kuacha mazoea mabaya ni ngumu na kuanza tabia njema ni kazi? Ni kweli. Llakini tambua mabadiliko ni ya muhimu. Chochote kilichoathiriwa na saratani ya dhambi ni sharti king'olewe kabla mgonjwa hajapona. Iwe ni miguu miepesi kukimbilia maovuni, au jicho lisilobanduka kwa visivyoruhusiwa, au iwe mikono inayonasa vibao mashavu, ni lazima itenganishwe na wewe kama unataka usalama. Fahamu hakuna kisichobadilika chini ya mbingu isipokuwa mabadiliko yenyewe. Unaweza kubadilika ukikubali.

Kubali ubadilike kwa faida yako. Ni hasara kuyakataa mabadiliko kuliko kuyakubali. Bora uvikose viungo vyako sasa vinavyokukosesha kuliko kuingia Jehanamu ukiwa navyo. Bila kukubali mabadiliko na maumivu yanayoambatana nayo, huwezi kupona.

Na kama unakubali usaidiwe, unalopaswa kufanya ni jambo moja. Anguka sahii kuonyesha unakubali upasuaji. Hakuna mgonjwa anayejifanyia operesheni. Mtwishe Yeye fadhaa zako na kushindwa kwako. Mwachie Mungu apambane na saratani dhambi inayokumaliza. Mwambie vita ni vyake sio vyako. Tatizo lako ni lake. Shetani akikukumbusha kushindwa kwako badala ya kumjibu mwambie, “Bwana akukemee” (Zek. 3:2). Kisha, tupa mikono hewani na useme pamoja na Paulo, "namshkuru Mungu kwa Yesu Kristo Bwana wetu….Maana yasiyowezekana… [yamewezekana]" (War 7:25;8:3). Na ushindi unabaki kuwa wa Bwana wetu Yesu Kristo.

La sivyo, ukijichukulia mambo usiyoyaweza mikononi mwako utamzuia Bwana Mungu asifanye lolote kukusaidia. Na unapomzuia, Mungu afanye nini zaidi ya kukuangalia kwa huruma huku machozi yakimtoka? Usimtese Mungu bure, kubali arekebishe mazoea yako ya dhambi.​

  1. Kubali mwenzako akusaidie

Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! (Mhu. 4:9-10)

Zaidi ya kukubali Mungu akusaidie, tafuta rafiki salama wa kumshirikisha safari yako ya imani. Ni bora kutembea wawili kuliko mweyewe; ukianguka mwenzio atakuinua (Mhu 4:9-12). Ipo mifano mingi. Daudi alipokuwa akinyanyaswa na mfalme Sauli, rafiki yake Yonathani alimfariji na kumpatia mbinu za kujikwamua kutoka mitego ya Sauli (1Sam 19, 20, 23). Yesu alipojisikia kuugua roho karibu na kufa hakuwaficha marafiki zake; isipokuwa akawaomba wamwombee (Mar 14:33,34). Kama wengine walipokabiliwa na majaribu walihitaji mkono wa rafiki kuminyaminya mabega yaliyochoka, na kutia nguvu mikono iliyokufa ganzi, nawe tafuta mshirika wa pembeni wa kukusaidia katika safari ya imani. Usitembee mwenyewe.

Pata rafiki unayeweza kumueleza mapambano uliyonayo. Mtume Paulo anakuona wewe na mkristo mwenzako kama viungo vinavyotegemeana na anawasisitizia akisema, "uvueni uongo, kila mtu akaseme kweli na jirani yake" (Efe 4:25). Hakuna manufaa ya kuvaa uchangamfu ukiwa na waumini wenzako huku ukibaki mwenyewe mto unalowana kwa machozi. Kwa faida yako na yeye msiache kuungamiana na kuombeana. Mtume Yakobo anasema, “ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa.” (5:16). Ungama uliposhindwa. Peaneni mbinu za kushinda. Shiriki naye furaha ya kushinda. Na kila mmoja adumu kuwajibika kwa mwingine. Hakika nakwambia kweli tupu, Mjaribu hutetemeka anapoona adui zake wameungana kumpinga. Umoja wenu utamfadhaisha.​

Like
Love
2
Rechercher
Catégories
Lire la suite
Injili Ya Yesu Kristo
NINI MAANA YA MTU KUZIKWA NDANI YA KANISA? KATIKA NYUMBA YA IBADA?
Ukisoma katika kitabu cha Mathayo 22:32 inasema mimi ni MUNGU wa Ibrahim, na MUNGU Isaka, na...
Par GOSPEL PREACHER 2021-11-19 05:43:45 0 5KB
HOLY BIBLE
Comforting Bible Verses
Our God cares about us. No matter what is happening, he never leaves us. Scripture tells us God...
Par MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 10:56:09 0 5KB
1 SAMUEL
Verse by verse explanation of 1 Samuel 29
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 24 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-01-26 05:13:18 0 5KB
Injili Ya Yesu Kristo
Mtu ambaye amemwamini Yesu lakini akafa bila kubatizwa je! atenda mbinguni?
JIBU: Inategemea kama hapo kabla alishausikia ukweli au la, kwa mfano kama mtu alishaufahamu...
Par GOSPEL PREACHER 2022-03-29 23:47:51 0 4KB
JOB
Verse by verse explanation of Job 3
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-04-02 13:30:35 0 5KB