UMEJIAANDAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Sehemu ya 1)

0
5KB

Nakusalimu kwa jina la Yesu!

Ili uweze kuelewa somo hili mpenzi msomaji nakushauri tafuta muda usome vizuri sura ya 24 ya kitabu cha Mathayo.

Mimi nitanukuu mistari michache  kwenye sura hii;

Mathayo 24:36-44 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam.

 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizovyokuwa kabla ya gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa mmoja aachwa, wanawake wawili watakuwa waskisaga; mmoja atwaliwa,mmoja aachwa.

 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamunu neon hili; kama mwenye nyumba angalijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingeliacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyoidhani mwana wa Adam yuaja”.

 Nakumbuka ilikuwa tarehe 27/03/2010, majira ya saa kumi na moja za jioni, nikiwa nimekaa chumbani kwangu, naangalia mkanda kwenye Laptop na nilikuwa na mke wangu. Ghafla nikahama katika ulimwengu huu kimawazo nikaenda kwenye eneo jingine, picha ya siku ya unyakuo ikanijia, na nikaanza kuona kwa sehemu nga kidogo jinsi unyakuo utakavyokuwa, nikaona  nguvu fulani ambayo inamnyanyua mtu na kwenda naye juu.

 Kwa ujumla si rahisi kuandika vizuri jinsi nilivyoona, lakini niliona watu wakianza kunyanyuliwa na dunia ilikuwa kama imepigwa na butwaa!. Baada ya maono haya nikaanza kutafakari na moyoni mwangu nikasikia uzito kwenye moyo kana kwamba Yesu ndiyo anarudi saa ile, ndipo nikasikia sauti kwenye ufahamu wangu ikiuliza umejiandaaje kwa ajili ya unyakuo na umewaandaaje watu wangu kwa ajili ya unyakuo?

 Wakati mambo hayo yanaendelea, mke wangu alikuwa akinisemesha lakini sikumelewa ingawa nilikuwa namsikia kwa mbali, macho yangu yalielekea kwenye mkanda lakini sikuelewa kilichokuwa kinaendelea pia. Baada ya dakika kumi hivi ndipo nikarudi kwenye ufahamu wangu wa kawaida nikaanza kutafakari na nikachukua hatua ya kwenda kuomba kwanza.

 Mara nyingi jambo hili limekuwa likinijia na Bwana ameendelea kunifundisha vitu vingi juu ya suala hili. Kutokana na yale ambayo nimejifunza na ninaendelea kujifunza katika neno lake imenilazimu kuanza kuandika mfululizo wa somo hili mpaka hapo Yesu atapokuja ikiwa atatukuta tukiwa hai au hadi pale nitakapoondoka kwa njia ya kifo. Na nimeamua kufanya hivi kwani swali la pili niliulizwa umewaandaaje watu wangu kwa tukio la unyakuo?. Nitaandelea kuweka mafundisho haya kwenye blog, ili kila mtu anayetaka kuwa tayari kwa unyakuo basi ajifunze na ajue namna ya kujiandaa.     

 Mpenzi msomaji maswali haya mawili kwangu yaliniumiza sana. Unajua wakristo wengi kwa jinsi tulivyo kila mmoja ana amini kwamba Yesu akija leo ataenda mbinguni. Hakuna mtu unaweza ukamsikia anasema siku ya unyakuo nitaachwa. Unajua ni kwa nini?. Wengi si kwa sababu Roho wa Yesu ndivyo anavyowashuhudia kwamba wataenda na Bwana, bali ni kwa sababu Shetani amepanda wazo kwenye fahamu zao kwamba Mungu hawezi kuwaacha hata kama mtu hayatendi mapenzi yake.

 Nisikilize kanisa, maadam niliulizwa nimewaandaaje watu wake, nami nina ujasiri wa kuandika na kukufundisha mambo mengi ambayo najua Shetani asingependa uyasome na kuyasikia. Nami nakuomba anza sasa kufuatilia masomo nitakayokuwa naandika kuhusu unyakuo, lakini pia fuatilia masomo ya watumishi wengine juu ya unyakuo ili uweze kuwa tayari kwa tukio hili la kushangaza na kuogofya.

 Nini anachokifanya Shetani nyakati za sasa?

 Katika kipindi hiki cha dakika za mwisho Shetani anatumia hila na uongo wake kuwapumbaza watu wengi kuhusu unyakuo na habari za Yesu kwa ujumla. Anachokifanya shetani ni kuhakikisha anazuia kwa kila hali watu wasisikie habari za Yesu na hasa kuhusu matukio ya mwisho wa dunia. Na hii ni kwa sababu anajua chanzo cha imani katika Kristo ni kusikia habari za Kristo Yesu.

 Na kwa wale waliokwisha kusikia ana hakikisha hawaliweki kwenye matendo lile neno. Si hivyo tu bali, anajitahidi kuwafanya watu wasiamini kweli ya neno la Mungu. Anapofusha amri/sheria nyingi za Mungu kwenye fahamu za watu. Ananyanyua watumishi wa ufalme wa giza na kuwapa uwezo mkubwa na hao watumishi anawaagiza kutofundisha kweli yote ya neno la Mungu (kumbuka yeye hujigeuza na kujifanya malaika wa nuru). Si hivyo tu bali hata wale watumishi wa ufalme wa nuru anawapumbaza na kuwalaghai kwa hila na kuteka fahamu zao kwa njia nyingi ili wasiwafundishe wanafunzi/washirika wao kweli yote ya neno la Mungu. Shetani anawafanya watu kuwa ‘busy’ na kazi na pia mambo yasiyo ya msingi /yasiyofaa hata kama ni halali.

 Sikia kanisa, si tu kusema kwamba  umeokoka ndiyo tiketi ya kwenda mbinguni. Warumi 2:13 inasema “kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki”.

 Ndugu yangu maadam umeamua kumwamni Yesu, sharti uwe tayari kufuata sheria zinazoongoza ufalme/utawala wake, na sio tu kusema mimi ni mwanachama wa Yesu. Je, unakumbuka jinsi shetani alivyotumia hila kuwadanganya Adam na Eva pale bustanini (Mwanzo 3:1-7). Naam hata leo ndivyo anavyofanya, na kwa njia hiyo atawafanya wengi kuachwa na Bwana siku ile itakapofika.

 Je, unajua kwa nini anafanya hivyo?

 Lengo ni kuwapumbaza watu wasiwe macho kiroho/wasikeshe wakidumu kuzitenda amri za Bwana, wala kutafakari neno lake wasije wakafunguka macho yao na kugundua hila zake. Yesu alisema kama ilivyokuwa siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa katika kizazi hiki.

 Je kwa Nuhu ilikuwaje?

 Watu walikuwa wakiendelea na shughuri zao za kila siku kama kawaida, wakioa, wakiolewa, wakilima, kufanya biashara nk. Unisikilize ndugu hakutakuwa na matangazo kwenye vyombo vya habari kwamba watu jiandaaeni Bwana Yesu atakuja siku au mwezi fulani kulichukua Kanisa Lake. Itakuwa ni kitendo cha ghafla na bila wengi kutarajia. Ni katika saa usiyoidhani wewe ndipo Bwana atakapokuja.

 Kwa hiyo Shetani anawapumbaza watu wawe ‘busy’ na mambo mengi ili ile siku Bwana atakapokuja waachwe. Nasema usikubali, maadam umeokoka wewe si mtu wa giza, haipasi siku ile ikukute kama vile mlevi. Huu ndio wakati wa wewe kujiandaa na kuwaandaa wengine.

 Sikia ee, Kanisa, kurudi kwa Yesu kumekaribia sana. Mara nyingi kwenye ufahamu wangu wazo la unyakuo huwa linanijia na nina amini kwanza ni kwa ajili yangu kujiandaa, lakini kila likinijia huwa nafikiri na watu wengine ambao bado hawajaokoa, lakini pia na wale ambao wameokoka lakini maisha yao hayapo sawasawa na mapenzi ya Mungu tunawasaidiaje?.

 Ndugu zangu siku hiyo haisemeki, itakuwa ni siku ya aibu, huzuni isiyo na kipimo, majuto yasiyosemeka. Ni heri kama usingelizaliwa mpenzi msomaji, kuliko kuokoka halafu ukaachwa kwenye ile siku. Huruma ya Yesu itafikia mahali itakoma. Yesu anatuvumilia sana, na laiti ungelijua namna anavyokulinda usife na sababu kubwa ikiwa ni kukupa nafasi ya kutengeneza maisha yako, usingefikia mahali pa kujisifu, kuhukumu wengine, kudharau na kuishi maisha ya kienyeji kiasi hicho.

Ngoja nimalizie kwa sentensi hii, siku moja nikiwa natembea kwenda kanisani Bwana aliniambia “watu wengi ninawapigania na kuwalinda wasikutwe na mauti, maana najua wakifa kwa kuwa hawako tayari hawawezi kuja kwangu, inaniuma sana hao watu wanapotafsiri vibaya ulinzi wangu kwao, wao wanafikiri ni kwa sababu wana haki ya kuishi tokana na elimu, fedha, madaraka yao, kumbe sivyo. Na mbaya zaidi licha ya kuwatengenezea watu hao fursa nyingi za kutubu/kutengeneza njia zao, wao hawakubali kutii/kubadilika. Sina namna ya kumsaidia mtu ambaye hayuko tayari kunitii”.

 Mpendwa wangu uvumilivu wa Mungu kwako na kwangu kwanza ni ili tutengeneze njia zetu, ukiendelea kufanya shingo ngumu, huruma yake itafika mahali na kukoma. Watu wengi ambao wako kuzimu hivi sasa, ujue sehemu kubwa walipuuzia nafasi/fursa ambazo Mungu aliwapa za wao kutengeneza njia zao.

Tutaendelea na sehemu ya pili...

Pesquisar
Categorias
Leia mais
Injili Ya Yesu Kristo
UNAJIFUNZA NINI KUPITIA HUDUMA YA ANANIA NA BARNABA KWA PAULO?
Nakusalimu katika jina la Bwana, mpenzi msomaji.   Katika nyanja hii, leo nimeona ni vema...
Por GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:24:28 0 4KB
SPIRITUAL EDUCATION
What will happen to those who die without hearing anything of Christ Jesus?
The Holy Bible makes it conspicuous and crystal clear that while there are might be people in the...
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 06:15:50 0 5KB
MAHUSIANO KIBIBLIA
Biblia inasema nini juu ya kushirikiana katika ngono kabla kuoana?
Pamoja na matendo mengine ya uchafu, kufanya kitendo cha mapenzi kabla kuoana kumekatazwa katika...
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 04:08:31 0 7KB
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 16
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 58 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:15:50 0 5KB
JOB
Verse by verse explanation of Job 6
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-04-03 03:12:54 0 4KB