UGUMU WA MIOYO NA MAHUSIANO (YA NDOA)

0
5K

Ugumu wa moyo ni sumu ya mahusiano yoyote hususani mahusiano ya uchumba na ndoa. Sababu ya kuwepo kwa hati ya taraka inayompa mume ruhusa ya kumwacha mkewe ni ugumu wa mioyo. Kwa lugha rahisi ni kwamba, kama hakuna ugumu wa mioyo ndani yetu, kusingelikuwepo na kitu kinachoitwa “KUVUNJIKA KWA NDOA” kwa mume kumwacha mkewe.

Leo napenda nizungumzie juu ya jambo hili kwa ufupi lakini kwa kina sana ili kutusaidia katika mahusiano yetu hususani mahusiano ya ndoa.

UGUMU WA MOYO NI NINI?
Kabla hatujaendelea ningelipenda zaidi tujue maana yake UGUMU WA MOYO ni nini kama ilivyozungumziwa katika kitabu cha Mathayo 19:8 wakati Yesu akiwajibu Mafarisayo swali lao la kimtego walilokuwa wamemuuliza.

UGUMU WA MOYO maana yake ni hali ya kutokusamehe anayokuwa nayo mtu ndani yake kutokana na upungufu wa upendo ndani yake. Ni hali ya kutokuwa tayari kabisa kusamehe, ni hali ya kushikilia msimamo wako katika upande wa kinyume wa makosa uliyotendewa pasipo kuupa moyo wako nafasi ya kusamehe kwa kufikiria upande mzuri wa yule aliyekukosea.

Ugumu wa moyo huwa haujalishi udogo au ukubwa wa kosa, una uwezo wa kumwacha mwenzi wako wa ndoa kwa kila sababu ambayo kwako inaonekana kuwa ni kosa. Kwa mtu ambaye ni mgumu wa moyo, anaweza kumwacha mwenzi wake wa ndoa kwa sababu ya dawa ya mswaki tu, na hii inatokea hasa pale upendo wa mtu kwa mwenzi wake unapokuwa umepoa, hutafuta kila sababu ya kumwacha mwenzi wake. Hoja hii ya upendo kupoa tutaiangalia hapo baadaye kidogo.

UGUMU WA MOYO ni hali ya kutokuwa na rehema na huruma kwa mwenzi wako katika yale makosa anayokutenda wewe, iwe kwa lazima au kwa bahati mbaya, iwe kwa kukusudia au kwa kutokukusudia, iwe kwa kujua au kwa kutokujua. Rehema maana yake ni kuzuia ghadhabu yako na hasira yako kinyume cha yule aliyekukosea kwa kuachilia makosa yake. Badala ya ghadhabu unaamua kumwonyesha upendo, badala ya hasira unaamua kumwonyesha huruma zako.

Mahusiano yoyote ambayo ndani yake wahusika wote au mmoja wao anapokosa roho ya kusamehe, rehema na huruma kwa kuachilia makosa anayotendwa au wanaotendeana huwa hayadumu, mwisho wake ni kuacha au kuachwa au kuachana. Rehema, huruma na kusamehe ni kazi ya upendo, na upendo ni mafuta yanayorahinisha moyo wa mtu unapopewa nafsi ndani ya moyo wa mtu huyo.

Hakuna aliye na upendo kweli ambaye hana uwezo wa kusamehe, au kurehemu, au kumuhurumia mtu ambaye amemkosea bila kujali udogo au ukubwa wa kosa na hasa pale mtu huyo anapokuja kwake na kuomba msamaha kwamba asamehewe. Yeyote anayetubu, anayegeuka na kurejea, anayejirudi na kuomba msamaha kweli anastahili kusamehewa kama wewe unavyostahili kusamehewa.

Kushindwa kusamehe ni dalili ya kupungua kwa upendo ndani yako kunakopelekea moyo wako kuwa mgumu. Kutokuwa na huruma kwa mtu yule aliyekukosea na kukuomba msamaha ni dalili ya upendo kupungua ndani yako na kupelekea moyo wako kuwa mgumu.

Biblia inasema katika siku za mwisho kwamba, Kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa, watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema (Rumi 1:28; Mathayo 24:12; 2Timotheo 3:2).

Kupoa kwa upendo ni matokeo ya maasi kuongezeka ndani yako, na kwa sababu ndani yako kutaingia ubinafsi, hutawapenda ndugu akiwemo na mwenzi wako, na badala yake utaanza kujipenda mwenyewe, na kwa sababu utajipenda mwenyewe, basi kwa vyo vyote kinachofuata ni wewe kuvunja agano lako la ndoa, na ukiishafikia hatua hii, huwezi kuupa nafasi moyo wako wa kurehemu, lazima tu utakachokuwa unakiona ni kumwacha huyo mwenzi wako bila kujali namna anavyojisikia, bila kujali kama anakuomba rehema na msamaha na huruma zako.

DALILI AU VIASHILIA VYA MTU MWENYE MOYO MGUMU:

Moja: Huanza kukuhesabia makosa uliyomtendea:
Kila utakapotenda kosa, atakukumbusha na makosa mengine uliyotenda nyuma ambayo tayari ulikwisha yaombea msamaha kwake na kuyamaliza. Lakini kwa nini anayakumbushia? Hii ni kwa sababu hakukusamehe, na kama hakukusamehe makosa hayo, bado hata hilo hatakusamehe kwa sababu tatizo sio makosa uliyomfanyia, tatizo ni moyo wake; upendo wake kwako umeishaanza kupoa. Kuhesabu makosa uliyotendewa na kumkumbusha aliyekukosea, au hata bila ya kumwambia yeye moja kwa moja, ukabaki unayakumbuka moyoni ni dalili kubwa kwamba una moyo mgumu wa kutokusamehe.

Kama wewe usivyo malaika, ndivyo na mchumba wako au mume au mke wako ndivyo asivyo malaika. Kama Mungu ambaye hajawahi kukosea husamehe dhambi na kuzisahau na wala hawahesabihi watu makosa yao, wewe ni nani ambaye ni mwanadamu mwenye uwezekano wa kuwakosea wengine na pengine umewakosea wengi hata usiweze kumsamehe mwenzi wako?

Mbili: Kutokuomba msamaha kwa makosa ambayo amewatenda wengine.
Ukiona mtu asiyeweza kuwaomba watu msamaha wale aliowakosea, jua kabisa moyo wake una shida, na shida yenyewe ni ugumu kama jiwe ndani yake. Mtu ambaye hawezi kuwaomba wengine msamaha, hawezi kuwasamehe wengine waliomkosea. Vitu hivi vinaendana na wala haviachani kwa sababu vyote ni matokeo ya ugumu wa moyo ambao umepelekewa na upendo wa mtu huyo kupoa.

Asiye samehe wengine daima hawezi kuwaomba msamaha watu wengine anapowakosea kwa sababu moyo wake ni mgumu, upendo umepoa na hali ya kujipenda mwenyewe ndiyo imemtawala, ni yeye tu na si wengine.

Kuomba msamaha kwa uliowakosea si udhaifu ni nguvu (strength), na kuwasamehe waliokukosea si udhaifu ni nguvu pia, na vyote vinatokea katika moyo uliojaa upendo, haviwezi kutengana, ni sarafu moja yenye pande mbili. Huwezi kuwasamehe, basi huwezi kuwaomba msamha, huwezi kumsamehe, pia huwezi kumwomba msamaha, na kwa sababu hiyo upendo wako umepoa na ndio maana moyo wako umekuwa mgumu.

WANAUME:
Biblia inatambua kwa sehemu kubwa manaume kumwacha mke wake kuliko mwanamke kumwacha mume wake. Mwenye maamuzi ya mwisho ya kuacha ni mwanaume hata kama mwanamke ndiye ametaka, na ndio maana anayetoa taraka ni mwanaume na si mwanamke.

Kwa sababu wanaume ndio wenye mamlaka ya kuacha, Yesu anawaambia wanaume kuwa, Musa aliruhusu hati ya taraka (kwa wana wa Israeli) kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Akijibu swali la Mafarisayo lililosema kuwa, “Je ni halali mtu kumwacha mke wake kwa kila sababu? Na ilikuaje msa akaruhusu hati ya taraka? Yesu anawaambia kuwa, tangu mwanzo haikuwa hivyo, kama ingelikuwa ni hivyo, basi Mungu angeumba wanawake na wanaume wengi, au angelimuumba Adamu na akina Hawa labda watano hivi ili awaoe wote au huyu akimkorofisha kwa sababu yoyote basi amwache na kumwoa huyu, bali aliyewaumba aliwaumba mtu mke mmoja na mtu mume mmoja basi.

Lakini Yesu anaendela kujibu na kusema, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu (hapa alikuwa anawaambia wanaume wenye mamlaka ya kuacha) Musa aliruhusu hati ya taraka, lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo.

Wanaume wengi ni wagumu wa mioyo kuliko wanawake. Ni wagumu wa kuomba msamaha na ni wagumu wa kutoa msamaha. Uzoefu unaonyesha kuwa, katika ndoa nyingi wanawake wanaishi na waume zao si kwa sababu wanaume hao wanawatendea vizuri wake zao hao bali kwa sababu wanawake hao wameamua kuwa wanawasamehe waume zao na kuomba msamaha kwa makosa ambayo waume zao ndio wameyatenda.

Ni ngumu kukuta mwanaume anamwomba msamaha mwanamke, japokuwa imekuwa kama sifa ya wanaume, lakini hii sio sifa bali ni udhaifu mkubwa sana. Wapo wanaume wachache sana ambao huwaomba wake zao msamaha na kuwasamehe kwa moyo wote pindi wanapowakosea, lakini wengi wa wanaume hawana tabia hii ya kuwaomba wake zao msamaha pindi wanapokosea na kuwasamehe wake zao pindi wanapowakosea. Tena wengi wanaenda mbali hata kufikia hatua ya kuwapiga wake zao. Japokuwa wapo wanawake wanaowapiga waume zao, lakini uzoefu unaonyesha wanaume ndio wanaongoza katika hili.

Mwanaume, usimfanye mke wako aishi na wewe kwa kukuvumilia ili hali anaumia kila saa kila dakika ila kwa sababu hana mamlaka ya kukuacha inambidi tu aendelee kuwa na wewe. Usichukulie kirahisi hali ya moyo wake na kupitia hiyo ukawa unamtesa. Wewe ndiye mwenye makosa lakini unataka yeye ndiye akuombe msamaha, unamtukana na kipigo juu kwa kosa lako mwenyewe eti kisa amekwambia ukweli.

Huwezi kuendesha ndoa kwa kuwa na moyo mgumu, ni kweli ndoa inaweza ikadumu kwa siku chache lakini haiwezi ikadumu kwa siku zote, lazima itavunjika tu. Badilika.

WANAWAKE:
Ni kweli, uzoefu unaonyesha kuwa ninyi ni wepesi wa kusamehe lakini pia kuomba msamaha. Mmekuwa mkisifiwa kwa hali ya mioyo yenu namna ilivyo na uvumilivu wenu, lakini si wote walio na hali hii. Wapo wanawake walioingia katika ndoa kutimiza tama zao wenyewe, inaweza kuwa ni tama ya mali au vinginevy vyote. Wanawake hawa huwa na kiburi sana kwa waume zao, kila siku ni kelele mpaka mwanaume anafikia hatua ya kutopafurahia nyumbani kwake mwenyewe.

Wanawake hawa hawajui kuomba msamaha, na hawajui kuwasamehe waume zao hata pale wanapoomba msamaha, kazi yao ni kelele kwa manane mengi wanayoongea. Mwanamke wa aina hii akianza kuongea hampi kabisa nafasi mume wake ya kuzungumza. Hii sio sawa kabisa, badilika, Mwanamke asifiwi kwa uzuri wake au uwezo wake wa kuongea au umalidadi wake katika kupangilia mavazi yake, mwanamke anasifiwa kwa utii wake kwa mume wake. Na utii wa mke ni matokeo ya moyo wake kuwa raini, kama atakuwa na kiburi, basi ni dalili kwamba ana moyo mgumu.

Ukikosa utii moyo wako ni mgumu kwa sababu utakuwa na kiburi, na mtu mwenye kiburi haonyeki, hakalipiki, hajui kuomba msamaha na wala hajui kusamehe, hafundishiki wala haelekeziki, ameshupaza shingo yake, wala hawezi kunyenyekea kwa mume wake. Kwa hali hii kweli ndoa itabaki au uchumba utabaki, utavunjika tu bila shaka na ndoa itavunjika tu.

HITIMISHO:
Siri ya ndoa nyingi na chumba nyingi kuvunjika ni wahusika kuwa na MIOYO MIGUMU isiyopenda rehema, iliyokosa utii. Uti wa mgongo wa kila ndoa ni upendo ambao kutoka katika huo tabia zote njema huzaliwa. Na upendo wa kweli ni mafuta yanayorainisha mioyo ya wana ndoa husika. Na mioyo raini ni mioyo iliyojawa na upendo ambayo iko tayari kusamehe na kuomba msamaha. Ni vyema wana ndoa au wowote walio katika mahusiano ya uchumba wakajifunza kutokuwa na mioyo migumu ili kudumisha mahusiano yao. Tukipata nafasi nyingine tutajifunza zaidi juu ya jambo hili.

Cerca
Categorie
Leggi tutto
EXODUS
Verse by verse explanation of Exodus 21
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 28 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-22 18:02:53 0 5K
2 KINGS
Verse by verse explanation of 2 Kings 23
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 35 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-03-19 21:10:39 0 5K
2 SAMUEL
Verse by verse explanation of 2 Samuel 17
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-02-05 09:57:31 0 5K
SPIRITUAL EDUCATION
Spirit, Soul, and Body
The Christian doctrine of immortality cannot be understood apart from the right conception of...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 05:38:37 0 5K
Networking
How to grow your marketplace on a budget
Creating a collaborative marketplace is complex. You need suppliers, customers for those...
By Business Academy 2022-09-17 01:57:18 0 5K