BIBLIA NA MATULIZO YA MAPENZI

Kumekuwepo na kesi nyingi za wanandoa; kuvunjika kwa ndoa ni jambo la kawaida sana, watu waliokuwa wanapendana sana kupita maelezo leo wanachukuana kupita 'kupita maelezo' si jambo la ajabu kuliona kwa wanandoa. Swali kubwa la kujiuliza, ni, Je, ndoa ilikusudiwa kuwa chanzo cha wanandoa kuchukiana na hatimaye kuachana? Je, ni kweli ndoa ilikusudiwa kuwa tanuru ya mateso kwa wanandoa? Je, ni kweli katika ndoa hakuna kupishana kwa namna yoyote ile? Jibu la maswali haya ni HAPANA!!!
Mafarisayo walimuuliza Yesu baada ya Yesu kuwajibu swali lao lililokuwa linahusu mume kumuacha mkewe kwa kila sababu, "Ilikuwaje basi Musa aliwaruhusu waandike hati ya taraka kama kuacha haikuwa kusudi la Mungu tangu mwanzo? Kwa nini hati ya taraka?“ Jibu la Yesu la swali hili lilikuwa hili, “Ni kwa sababu ya UGUMU WA MIOYO YENU“ Hii inamaanisha nini!!! Haina maana zaidi ya KUTOKUWA TAYARI KUSAMEHE, yaani kuachilia makosa uliyotendwa ndio maana Musa aliruhusu hati ya taraka.
Kwa sababu hiyo hati ya taraka ni mpango wa wanadamu kutatua migogoro ya wanandoa waliokoseana makosa yaliyopelekea maumivu ya mioyo yao, maumivu ya hisia zao ambayo kibinadamu ni magumu kusamehe na kuendelea kuwa pamoja. Na mara zote mpango wa mwanadamu haumletei Mungu utukufu, na kiuhalisia hautatui tatizo, bali ni njia ya kumpeleka muhusika kwenye matatizo zaidi.
KUSAMEHE ni mpango wa Mungu wa kutatua matatizo ya wanandoa yaliyoumiza mioyo yao na hisia zao za ndani kabisa unaotoa nafasi ya kupenda tena kwa furaha na amani. Makosa hayo ni pamoja na yale ambayo kibinadamu ni ngumu kusamehe wala kuchukuliana nayo. Licha ya uzito wa makosa hayo, msamaha ambao msukumo wake ni UPENDO wa Mungu hutoa nafasi ya kuachilia ili kupenda tena kana kwamba hakujawahi kutokea jambo lolote baya kwa wanandoa husika. Hati ya taraka haitoi nafasi ya kupenda tena ila chuki kwa wahusika na kwa sababu hiyo hakuponyi bali kunaongeza ugonjwa. Hati ya taraka haiachilii, haitoi nafasi mpya na inaweka jeraha katika mioyo ya wahusika, na inaumiza wahusika wa tatu kama vile watoto, marafiki, wazazi na ndugu wa wanandoa husika lakini hasa watoto wao. Kama Mungu alivyo na ndivyo sisi tunapaswa kuwa. Yeye hutusamehe makosa yetu yote bila kujali ukubwa na uzito wa makosa tuliyomkosea, moyo wake si mgumu hata asitusamehe, bali utusamehe ili mrudi tu tumemuomba msaada. Anao uwezo wa kutusamehe hivi kwa sababu alishatusamehe tangu mwanzo. Kwa hiyo na sisi tunapaswa tuwe hivyo kwa wenzi wetu wa ndoa. Msamehe mkeo kabla hata hujamuoa wala hujamjua ili uwe na uwezo wa kumsamehe kila anapokukosea bila kujali ukubwa makosa na bila kujali wingi wa makosa yake. Siku unapomuoa au kuolewa naye mwambie nimekusamehe kwa makosa yote utakayonitenda na kunitendea. Ukimsamehe utamtuliza moyo wake kwa mapenzi yako ndani ya moyo wako.
Wanandoa waliotofautiana katika mambo fulani, hadi kufikia hatua ya kugombana na kupigana (kwa sababu kutofautiana sio kugombana wala kupigana) ni kwa sababu wamekosea kanuni fulani fulani za ndoa na namna ya kuhusiana. Kanuni hizo ni pamoja na Upendo (huu hutoka bila kujali namna unavyopokea: unajali kutoa kuliko kupokea), unyenyekevu, uvumilivu, upole (kutokuwa mwepesi wa hasira na mwepesi wa kutoa hukumu), kusamehe, shukrani, staha, kuchukuliana, nk.
Leo hii nataka nizungumzie kanuni moja tu ambayo haipo katika orodha hapo juu. Kanuni hii ni ya muhimu sana, na inafanya kazi ndani ya kanuni zote nilizotaja hapo juu na nyingine ambazo sikuzitaja. Kanuni hii ni 'MATULIZO YA MAPENZI' hii ni kanuni muhimu sana kwa wanandoa katika kuhusiana kwao na hasa pale wanapoonekana kutofautiana katika mambo fulani fulani. Katika kanuni hii kuna maneno mawili, Matulizo na Mapenzi.
Matulizo ni matendo yanayopelekea utulivu mahali pasipo na utulivu au panapoelekea kukosekana kwa utulivu iwapo yatatendwa.
Mapenzi ni hali ya ndani ya huba, mahaba, nyonda anayokuwa nayo mtu juu ya kitu fulani au mtu fulani inayomsukuma mtu huyo kumtendea mwenzi wake matendo mema yanayoakisi na kutafsiri hali yake ya ndani ya huba, mahaba, nyonda aliyonayo kwa mwenzi wake.
Katika kitabu cha Wafilipi 2:1-2, Paulo anasema, "Basi ikiwako faraja yoyote katika Kristo, yakiwako MATULIZO YOYOTE YA MAPENZI..... Ijalizeni furaha yangu, ili muwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja."
Matulizo yoyote ya mapenzi maana yake ni matulizo yenye msingi wake katika mapenzi. Matendo unayotenda kwa mwenzako ili kurejesha au kudumisha utulivu yake na msukumo wake katika mapenzi uliyonayo kwa mwenzi wako. Hii inamaanisha kuwa hali yako ya ndani ya mapenzi kwa mwenzi wako inatakiwa isipotee wakati wote, unatakiwa uidumishe kwa sababu ni muhimu sana katika kudumisha UTULIVU WA NDOA YENU. Hali hii ambayo msingi wake na shina lake ni UPENDO usio na sababu ikipotea tu, ni rahisi sana utulivu wa ndoa yenu kupotea.
Tunapozungumzia UTULIVU tunazungumzia swala la mambo yote kuwa shwari, kutawala kwa amani na furaha katika ndoa. Matulizo ya mapenzi yanampa kila mtu furaha katika ndoa na hasa yanapopewa nafasi na kufanywa wakati wa matatizo.
Wakati wa matatizo ni wakati ambapo moyo wa mtu unakuwa haujatulia, mashaka, hofu, na wasiwasi vinakuwa vimeushika moyo wa mtu, hakuna tena utulivu wa moyo. Na moyo wa mwanandoa mmoja ukikosa utulivu, kuna hatari ya ndoa kukosa utulivu iwapo hatua madhubuti za kurejesha utulivu wa moyo hazitachukuliwa. Moyo uliokosa utulivu unahitaji utulivu kuwa katika hali yake ya kawaida.
Mume/mke mwenzi wako anapokuwa katika hali ya matatizo mtulize kwa mapenzi hata kama tatizo alilonalo amesababisha yeye mwenyewe, usimlaumu, mtulize kwa huba, mahaba na nyonda. Moyo ulioumia tiba yake ni mapenzi. Ni muhimu tukajua kuwa injini ya ndoa ni mioyo ya wanandoa, mioyo ikiharibika ndoa uharibika kabisa. Ndoa iliyoharibika au inayoelekea kuharibika hutibiwa kwa mioyo ya wanandoa husika kutibiwa. Utulivu wa ndoa unategemea sana utulivu wa mioyo ya wanandoa husika.
Mke/mume una wajibu wakutuliza moyo wa mwenzi wako kwa mapenzi na si vinginevyo. Muonyeshe mwenzi wako huba, Mpe mahaba, mfanyie nyonda. Usimuache katika hali ya moyo wake kuwa na mashaka, hofu, huzuni, wasiwasi, ukadhani hali hii itaondoka yenyewe. Mtulize mumeo/mkeo kwa mapenzi.
Biblia inasema, heri kuwa wawili kuliko kuwa mmoja, kwa sababu mmoja akianguka mwingine atamuinua na mmoja akiwa na baridi mwingine atamtia mwenzake joto. Hii inamaana pia na Matulizo Ya Mapenzi.
Wanandoa wengi wanapopishana katika kauli au mambo fulani huwa hawatafuti kutuliza kwa mapenzi zaidi ya kushindana. Kila mmoja anadhani atamtuliza mwenzake kwa kumshinda. Kwa hiyo kila mmoja atajitahidi kushindana na mwenzake ili amshinde, na kwa sababu hakuna anayekubali kushindwa, kushindana kwao kutawaletea majivuno yaani kiburi kila mmoja dhidi ya mwenzake. Katika hatua hii, hapa hakuna tena ndoa.
Ili kufanya kanuni hii ya Matulizo ya Mapenzi, mmoja au wote wawili hawana budi kushuka na kunyenyekea. Ni lazima wakubali kushindwa. Mapenzi hayaonyeshwi katika kiburi na mashindano, mapenzi yanaonyeshwa na kutolewa katika unyenyekevu na kukubali kushindwa. Mapenzi ni utumishi, na mwenye kiburi hawezi kumtumikia mwenzi wake. Mtu anayetaka kuwa juu tu kila siku, yeye anataka kushinda hawezi kuonyesha mapenzi. Mapenzi hayapatikani juu kwa wewe kujikweza, mapenzi yanapatikana chini kwa wewe kujishusha. Kujishusha na kukubali kushindwa ni moja ya njia ya kuonyesha mapenzi yako kwa mwenzi wako. Palipo na mapenzi kuna Matulizo ya mapenzi. Matulizo ya mapenzi yanategemea sana moyo wako. Ni vyema ukaulinda moyo wako usipoteze mapenzi yake kwa mwenzi wako katika hali zote nyakati zote itakusaidia sana.
Wanaume wengi wanadhani kuwa kwa wao kuwa jeuri kwa wake zao, kwa kuwapiga na kuwafanyia mambo ya kibabe kutawatuliza. Ni kweli kunaweza kuwatuliza kwa nje lakini ndani ni fukuto la moto wa volkano itakayolipuka na kuonekana nje baada ya muda fulani hivi. Usitumie ubabe kumtuliza mkeo, tumia mahaba kumtuliza mkeo kwa sababu si swala la mwili ni swala la moyo.
Wanawake wengi wanadhani kwa wingi wa maneno yao makali na matusi, na vitendo vibaya vya kujilipiza visasi kwa waume zao wanadhani watawatuliza waume zao. Wanaweza kuwa wamenyamaza lakini siku wakiamua kuitikia matendo hayo, ni shida!!!! Mwanaume hatulizwi kwa wingi wa maneno na jeuri zako zilizojaa visasi, mwanaume anatulizwa kwa mapenzi.
Usitumie nguvu zako za mwili kumtuliza mkeo, tumia mahaba kumtuliza mkeo ili furaha yako ijazwe. Usitumie wingi wa maneno yako na uwezo wako wa kulipiza kisasi kwa matendo ya kinyume kumtuliza mumeo, tumia mapenzi kumtuliza mumeo ili furaha yako ijazwe. Furaha ya mwenzi wako itazidisha furaha yako. Kwa hiyo usianze kwanza kutafuta furaha yako, tafuta kwanza furaha ya mwenzi wako, ukiipata umeipata na yako.
Nimalizie kwa kusema, mtulize mwenzi wako kwa mapenzi na si vinginevyo huku mkinyenyekeana, mkivumiliana, mkichukuliana, mkipendana, mkisameheana pasipo kulaumiana, kunung'unikiana, wala kushindana katika jambo lolote ili mpate kuwa watu wenye nia moja, mapenzi mamoja, roho moja huku mkinia mamoja. Hukumuoa wala hukuolewa naye ili umuumize moyo wake kwa visa na mikasa, umemuoa au umeolewa naye ili umtulize moyo wake kwa mapenzi. Acha Matulizo ya mapenzi ambayo ni faraja, mahaba, huba, nyonda, zawadi, pongezi, Shukrani, pole nk. yawe ni kipaumbele chako katika ndoa yenu au mahusiano yenu.
Mungu akubariki sana.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS