ATHARI ZA NGONO NA JINSI YA KUKABILIANA NAZO NA KUSHINDA

0
8χλμ.

Kama kuna jambo ambalo wengi wetu hatulijui au tu hatujalitilia maanani ni athari zitokanazo na kufanya ngono nje ya ndoa. Pamoja na kuwa ngono inaharibu maisha ya wengi na kuwatoa wengi wetu nje ya reli ya kufukuzia ndoto zao hata kupoteza matumaini ya kufanikiwa, bado kwa sehemu kubwa hatujatoa uwanja mpana wa kuangazia jambo hili, si kwa watoto wetu na vijana wetu tu bali hata kwetu pia watu wazima.

Jamii kubwa na hususani Kanisa la Mungu imelinyamazia swala hili isilizungumzie wazi wazi katika kuwafundisha, na kuwaelekeza vijana na watoto wetu athari za jambo hili katika maisha yao. Sawa, unaweza kujiona wewe uko salama, lakini vipi kuhusu mtoto wako, vipi kuhusu mdogo wako, na vipi kuhusu ndugu yako mwingine?

Kila kitu ni kizuri kwa wakati wake, na pia ni salama kinapokuwa mahali pake, kifanyike kwa wakati wake na mahala pake katika utaratibu uliokusudiwa na unaokubalika hasa kwa kufuata sheria na maagizo ya Biblia. Lakini tendo la ndoa limekuwa ni jambo ambalo linafanywa na wengi kabla ya wakati na nje ya mahala pake sahihi pa kufanyia; na kwa sababu hiyo limekuwa na athari nyingi mbaya kwa wengi. Hii ndio sababu imepelekea mimi kama mwalimu wa kizazi changu, mwalimwa wa saa hii, kuvunja ukimwa na kuzungumzia swala hili. Kwa hiyo fuatana nami huenda kuna mtu utamsaidia kwa kutumia maarifa haya; kama wewe huyahitaji kwa ajili ya nafsi yako, unayahitaji kwa ajili ya nafsi ya mwingine.

NGONO NI NINI?
Kabla ya kuendelea, nitapenda sana kutoa maana halisi ya ngono kabla sijazungumzia umuhimu wa kuzungumza jambo hili wazi wazi.

Ngono ni tendo la mwanamke na mwanaume kujamiiana hususani nje ya ndoa; lakini ikiwa katika ndoa linaitwa tendo la ndoa (inaweza isiwe maana rasmi lakini kwa ajili ya kutofautisha tendo hili moja katika mazingira mawali linapofanyika, ndani na nje ya ndoa, naomba ibaki kuwa hivyo). Kwa hiyo, nataka wewe uelewe kwamba, kila nitakapokuwa nazungumza kuhusu ngono, elewa sizungumzii tendo la ndoa ndani ya ndoa bali nazungumzia tendo la mwanamke na mwanaume kukutana kimwili nje ya ndoa.

Kiukweli kabisa, kujamiiana au kukutana kimwili kwa upande wa wanadamu kulikusudiwa kuwe ni baina ya mke na mume katika ndoa na si kwa mwanamke au mwanaume ye yote tu huko nje ya ndoa. Tofauti na wanyama ambao wao hulazimika kufanya tendo hili na ye yote miongoni mwao kwa msukumo wa namna wanavyojisikia mwilini kwa namna walivyoumbwa (kwa kuzingatia tabia za maumbile yao katika kujamiiana), mwanadamu hufanya tendo hili kwa utashi wake akitumia akili na uwezo wake wa kujitawala na kujizuia kihisia na katika misukumo ya asili ya maumbile yake, uwezo ambao wanyama hawana.

Hii ndio maana tendo hili, kwa wanyama sio dhambi kufanya na ye yote hata na mtoto wake au mama au baba yake, nje au ndani ya ndoa kwa sababu wao kwanza hawana ndoa na hawana akili ya kupambanua na kutafsiri mambo; lakini kwa upande wa wanadamu ni dhambi kulifanya nje ya ndoa na nje ya kanuni yake ya asili ya kimaumbile.

Katika Biblia, kwa mara ya kwanza kabisa tendo la ndoa linatambulishwa kwetu kwa Adamu kumjua mkewe Hawa kisha kuzaa mtoto wao wa kwanza Kaini (Mwanzo 4:1). Kwa hiyo tendo la ndoa linatambulishwa kwetu kwa mara ya kwanza kabisa ndani ya ndoa baina ya mke na mume kupitia Adamu na Hawa na si nje ya ndoa. Hii ni hoja ya kuzingatia sana, kwamba tendo la ndoa linatajwa kwa mara ya kwanza kabisa na Biblia likifanywa na mke na mume ndani ya ndoa na si nje ya ndoa.

Kitu cha kushangaza hapa ni lugha aliyoitumia Mungu kusema ushirika huu wa mwili; Biblia inasema, "Adamu akamjua Hawa mkewe..." hii maana yake ni kwamba, tendo la ndoa ni tendo la kujuana kimwili; kila mke na mume wanapokutana kimwili wanafanya tendo la kujuana kimwili. Kwa lugha nyingine ni kwamba, wanaunganikana na kuzidi kuwa mwili mmoja kwa kule kujuana kwa kukutana kimwili, na ndio sababu kunakuwepo na kifungo (bond) cha nafsi baina ya hao wawili kwa sababu nafsi nayo ni sehemu ya mwili na si sehemu roho. Hii nitaifafanua katika masomo yajayo.

Katika lugha ya Kiebrania, neno ambalo kutoka katika hilo limetafsiriwa neno "kumjua" ni "yâda" lenye maana iyo hiyo ya kujua lakini kwa namna ya "kuhakikisha kwa kuona kwa macho." Kwa lugha nyingine kama ni kujua kwa kuona kwa macho basi ni kwa ujuzi wa kimatendo, ujuzi wa kiuzoefu zaidi ya ujuzi wa kinadhalia. Kwa hiyo tendo la ndoa ni ujuzi wa kimatendo, unaokupa nafasi ya kumjua unayekutana naye kimwili hata kuwa na kifungo (bond) cha nafsi.

Kadhalika katika ngono, kwa kuwa nalo ni tendo la kukutana kimwili kati ya mwanamke na mwanaume kama ilivyo katika tendo la ndoa, (tofauti yake hapa linafanyika nje ya ndoa) nayo huwa na matokeo yale yale lakini yanayoathiri maisha ya watendaji kwa namna isiyo nzuri.

Katika Biblia tendo la ndoa nje ya ndoa (ngono) limetanjwa kwa mara ya kwanza pale ambapo Ibrahimu alimwingilia kimwili Hajiri baada ya kushinikizwa na mkewe Sara kwa kusudi la kumzalia Ibrahimu mtoto kwa sababu Sara alikuwa tasa (Mwanzo 16:1 - 3). Inaweza isiwe ni mara ya kwanza kutendwa na Ibrahimu na Hajiri, lakini limetajwa wazi wazi kwa mara ya kwanza katika Biblia kwa Ibrahimu kumwingilia Hajiri.

Neno lililotumika hapa linaloelezea tendo la kukutana kimwili kati ya Ibrahimu na Hajiri ni tofauti na lile lililotumika kwa Adamu na mkewe. Hapa linatumika neno la Kiebrania "" lenye maana ya kumuingilia (go in). Kwa lugha nyingine tendo la ndoa si kujuana tu kimwili lakini pia ni tendo la mwanaume kumuingilia mwanamke kimwili linalosababisha pia, nafsi ya mwanaume iingie ndani ya moyo wa mwanamke na kumshika moyo wake.

Hii ndio sababu huwa ni vigumu sana kwa upande wa mwanamke kumtoa moyoni mwanaume aliyeshiriki naye kimwili (na hasa mwanaume wake wa kwanza). Lakini kwa upande wa mwanaume si kazi sana kumwacha mwanamke aliyekutana naye kimwili kwa sababu yeye kwanza haingiliwi bali ndiye anayemwingilia mwanamke, na pia hufanya tendo hili kwa nia na malengo mengine tofauti kabisa na upendo wake kwa anayefanya naye.

Ni mwanaume ndiye anayemjua mwanamke na ni mwanaume ndiye anayemwingilia mwanamke, na ndio sababu athari za ngono zinamwathiri zaidi mwanamke ukilinganisha na mwanaume ijapokuwa naye anaathiriwa kwa sehemu kubwa na tendo hili. Kungiliwa huku kwa mwanamke kunaacha alama si tu katika mwili lakini pia hasa kabisa katika nafsi ya mwanamke na kwa kiasi fulani katika nafsi ya mwanaume.

Mara nyingi (hususani nje ya ndoa) mwanaume anapomwingilia kimwili mwanamke si kwa sababu anakuwa anampenda, mara nyingi sana huwa ni tamaa ya mwili au malengo mingineyo na ndio sababu kwa upande wa hisia za moyoni haimuathiri sana kama ilivyo kwa mwanamke.

Kwa upande wa mwanamke, anapotoa mwili wake aingiliwe na mwanaume, japo kuwa si mara zote, lakini mara nyingi huwa ni kwa sababu anakuwa amempenda mwanaume huyo mazima, na kama matokeo ya upendo wake kwake anamfunulia mwili wake na kumruhusu amuingilie. Hii ni hatari zaidi kuliko tu ambavyo angeishia kumpenda bila kumpa mwili wake.

Ni wanawake waliokata tamaa, walioumizwa mioyo hata kuathirika kisaklojia ambao hutoa miili yao kwa mwanaume ye yote hata kama hawampendi; na mara nyingi huwa ni kwa sababu za kiuchumi (biashara) na kidogo sana hufanya hivyo kama sehemu ya starehe; hawa huwa hawajali sana kwa sababu ni wagonjwa wa akili au kuna nguvu za giza zinawasukuma kufanya hivyo.

Tukirejea kwenye hoja yetu tukiwa tunamuangazia Ibrahimu na Hajiri, walipokutana kimwili nje ya ndoa (yaani walipofanya ngono) tayari walitengeneza tatizo ambolo limedumu mpaka leo hii kwa upande wa mgogoro kati ya wazao wao.

Migogoro iliyotokana na Ibrahimu kumwingilia Hajiri nje ya ndoa:

Ibrahimu na Mungu:

Kwanza kabisa ni mgogoro kati ya Ibrahimu na Mungu (Ibrahimu alimtenda Mungu dhambi, na baadae tunaona Mungu anamlazimisha akubaliane na Sara mkewe kuhusu kufukuzwa kwa Hajiri na Ishmaeli). Huu ni mgogoro wa mahusiano na ushirika kati ya Mungu na mwanadamu.​


Ibrahimu na Sara mkewe:

Mgogoro wa pili ni kati ya Ibrahimu na Sara mkewe; wanaingia kwenye ugomvi. Huu ni mgogoro wa ndoa; ndoa yao inakuwa mashakani, na kama Mungu asingeingilia kati bila shaka ndoa ingevunjika kama sio kuwa na shida ya kudumu.​


Sara na Hajiri

Mgogoro wa tatu ni kati ya Sara na Hajiri, wanaanza kugombana, mtu na bibi yake; Hapa Sara anatetea ndoa yake na nafasi yake kama mke wa Ibrahimu. Sara awamu ya kwanza anamtesa Hajiri hata kutoroka; awamu ya pili anamshinikiza Ibrahimu amfukuze Hajiri na Ishmaeli mwanaye; hapa Sara anatetea urithi wa mwanae Isaka kama mzaliwa halali katika familia. Hii yote ni kwa sababu ya ngono, tendo la ndoa nje ya ndoa.​


Sara na Ishmaeli

Mgogoro wa nne ni kati ya Sara na Ishmaeli; Sara hataki Ishmaeli arithi pamoja na mwana wa mjakazi, anataka afukuzwe. Sara anatetea nafasi ya mwanae katika swala zima la urithi wa baraka za Agano na mali za familia.​


Hajiri na Isaka

Mgogoro wa tano ni kati ya Hajiri na Isaka; bila shaka Hajiri anamchukia Isaka kwa sababu anaona amekuja kuharibu mambo na kuwa sababu ya mtoto wake kufukuzwa asirithi. Lakini pia Hajiri alimtumia Ishmaeli kumfanya Isaka awe duni.​


Ishmaeli na Isaka

Mgogoro wa sita ni kati ya Ishmaeli na Isaka ambao unadumu mpaka sasa kati ya wazao wao; wazao wao wanaingia katika vita visivyokoma. Ishmaeli anaanza kumfanyia dhihaka Isaka, nadhani alikuwa anaonyesha kuwa Isaka si kitu kabisa, na kwamba yeye ndiye mzaliwa wa kwanza na mrithi (Mwanzo 21:9).​


Ibrahimu na Hajiri

Mgogoro wa Saba ni kati ya Ibrahimu na Hajiri; bila shaka Hajiri hakufurahia kufukuzwa na Ibrahimu na ndio maana alipoishiwa maji jangawani alilia kilio cha kunung'unika, kulaumu na kujiurumia, na ndio sababu Mungu hakusikia maombi yake ila ya mtoto wake.​


Ibrahimu na Ishmaeli

Mgogoro kati ya Ibrahimu na Ishmaeli. Unadhani Ishameli alijisikiaje kufukuzwa na baba yake, na unadhani Ibrahimu alikuwa katika hali gani kumfukuza Ishmaeli?​


Migogoro yote 8 imesababishwa na tendo moja, yaani, ngono; tendo la ndoa nje ya ndoa. Katika Biblia kila mahali ambapo imeandikwa kuhusiana na tendo la ndoa kufanyika nje ya sheria yake, yaani nje ya kusudi lake, ilisababisha matatizo makubwa sana katika maisha ya watu ya wakati huo na ya baadae; na hasa tendo hili liliponyamaziwa bila ya kushughulikiwa linaendelea kuleta athali nyingi zisizo nzuri.

Nadhani hii ndio sababu sheria ya Musa iliagiza watu waliobainika kwa ushahidi wa wazi kuwa wametenda tendo hilo wapigwe mawe hadi kufa.

Ngono ni uzinzi na uasherati na hii inahusikana moja kwa moja na Mungu, yaani ni dhambi kwa Mungu moja kwa moja. Na kama ni dhambi, mshahara wake ni mauti; ndio sababu kuna uharibifu mkubwa ndani yake.

NGONO NA MUUNGANIKO WA NAFSI NA MWILI

Moja ya kitu ambacho watu hawakijui na kama wanakijua basi wanakipuuza ni kwamba, iwe ndani au nje ya ndoa kukutana kimwili, yaani, kujuana kunapelekea wawili hawa, mwanamke na mwanaume waungane na kuwa mwili mmoja, jambo linalopelekea kuungana pia kwa nafsi za watu hao kwa sababu nafsi nayo ni sehemu ya mwili na si sehemu tu ya roho.

Tunapozungumzia nafsi tunazungumzia juu ya akili, nia, hisia, na utashi, na kwa uhalisia kabisa, vitu hivi ni sehemu ya mwili wako na hasa katika mahusiano ya kimwili kwa sababu nafsi yako ndiyo inayohusika zaidi sambamba na mwili wako. Kwa hiyo, tunaposema muunganiko wa mwili tunamaanisha vyote viwili, yaani mwili na nafsi ya muhusika au miili na nafsi za wahusika.

1 Wakorintho 6:16

[16]Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.


Kabla ya kuendelea, kwanza tuangalie misamiati iliyopo katika kifungu hiki cha maandiko matakatifu.

1. Aliyeungwa:

Neno la Kiyunani lililotumika hapa ni "kollaō" lenye maana ya kugundisha pamoja, au funga kwa namna ya kuunganisha pamoja. Kwa lugha nyepesi ni kuwa, mtu anapokutana kimwili na mwanaume au mwanamke, anakuwa ameunganishwa kwa kugundishwa pamoja ili kuwa mwili mmoja pamoja naye. Hapa haihitaji kufungishwa ndoa, bali ni kwa kule kushiriki tu ngono.​


2. Kahaba

Neno la Kiyunani lililotumika hapa ni "pornē" lenye maana iyo hiyo ya kahaba au mwabudu sanamu (idolater). Hii maana yake nafsi ya mtu inahusika kwa kiwango kikubwa sana kwa sababu ya muunganiko wa kiushirika unaokuwepo baina ya wawili hawa wanaokutana kimwili nje ya ndoa kwa sababu tendo la kujamiiana nje ya ndoa linalinganishwa na tendo la mtu kuabudu sanamu, ambapo si roho yake na mwili wake vinavyohusika, bali zaidi sana nafsi yake na mwili wake kwa upande wa ngono..

Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Tuki) ya Oxford, neno kahaba limetafsiriwa kuwa, ni mtu anayefanya mambo ya uasherati agharabu kuwa ni biashara au starehe.​


3. Mwili

Hapa katika vipengele viwili vilivyotaja mwili yametumika maneno mawili tofauti; katika kipengele cha kwanza cha mstari wa 16 neno la Kiyunani lililotumika ni "sōma" lenye maana ya mwili (body as a sound whole) ambalo matumizi yake ni mapata sana, huenda yakahusisha na nafsi ndani yake.

Neno la pili la Kiyunani lililotumika katika kipengele cha pili cha mstari wa 16 ni "sarx" lenye maana ya mwili (flesh) huu wa kawaida kabisa ambao hauhusishi nafsi, ambao katika rejea ya mistari ya Biblia iliyotumika kuelezea muunganiko wa wawili kuwa mwili mmoja limetumika kuelezea muunganiko ulio halali (Mathayo 19:5, 6; Marko 10:8; Waefeso 5:31).

Swali la kujiuliza ni kwamba, kwa nini Roho Mtakatifu ametumia maneno mawili tofauti kuhusiana na mwili katika kuelezea matokeo ya muunganiko unaotokana na kufanya ngono au kukutana kimwili?

Katika kipengele cha kwanza, mtu anapokutana kimwili na kahaba kunatokea muunganiko wa kimwili unaohusisha nafsi ijapokuwa wawili hawa wanaweza wasiishie kuoana na kuwa mwili mmoja (one flesh) kama kipengele cha pili kinavyosema, ambapo watakuwa wanaishi pamoja; wanaweza kushiriki ngono lakini nje ya utaratibu wa wao kuacha wazazi wao na kuambatana hata kuwa mwili mmoja; yaani wanafanya zinaa kwa sababu wanatenda tendo la ndoa nje ya ndoa..

Kwa hiyo, kipengele cha kwanza hakihusishi kufunga ndoa na kuishi pamoja kama mke na mume lakini bado kunakuwepo muunganiko wa nafsi za wawili hawa; hata kama watavunja mahusiano hayo, muunganiko huo utaendelea kuwepo.

Na ikumbukwe kuwa muunganiko huo ni wa kugundishwa pamoja kinafsi na mtu ambaye alifanya ngono na wewe kwa lengo la kustarehe au biashara na si kwa lengo la kukuoa au kuolewa na wewe; na kwa sababu hiyo, alifanya na wewe nje ya ndoa.

Lakini katika kipengele cha pili kuunganishwa kunakozungumziwa ni kuunganishwa kuliko halali ambako kunahusisha kuambatana si tu kinafsi bali kimwili pia ambako kunafuatia baada ya wahusika kufanya maamuzi ya kuoana, kisha kufunga ndoa na kuishi pamoja. Katika hatua hii halali, inayokubalika Kibiblia, muunganiko wa nafsi hauna madhara yo yote katika maisha ya wanandoa ila ni muunganiko ambao ni baraka kwa wote wawili.​


KUUNGANISHWA NA KAHABA.
Kahaba ni mtu anayefanya tendo la ndoa nje ya ndoa kwa lengo la kufanya starehe au biashara. Mtu huyu huja kwako na kuanzisha mahusiano ya kingono si kwa lengo la kukuoa au kuolewa na wewe, hata kama ni kwa lengo la kukuoa, anafanya tendo hilo na wewe nje ya ndoa, yaani kabla ya kuingia katika ndoa, kitu ambacho si sahihi, ni kinyume cha Neno la Mungu. Lakini jambo hatari hapa ni huu muunganiko ambapo mnapofanya hivyo, nafsi zenu zinaunganishwa kama karatasi mbili zilizounganishwa na gundi. Huwa ni ngumu kuachana bila ya kuchanika na wakati mwingine huwa haiwezekani kabisa kuziachanisha. Kama mtu ataziachanisha basi kila karatasi moja itabaki na kipande cha karatasi nyenzake kila moja ikiwa imechanika.

Hii ndio sababu jambo hili limekuwa na madhara mengi sana kwa wahusika; wengine wamepata majeraha ya moyo ya kudumu, wengine wameua na wengine kujiua; wengine wamejikuta wakiingia katika maisha ya kufanya visasi, na wengine kuishia kuwa na chuki dhidi ya wenzi wao wa zamani. Kiufupi nafsi zao zimechanika, mioyo yao imeumia pindi walipokuwa wanajibandua baada ya kugundishwa nafsi zao pamoja na tendo lao la kukutana kimwili nje ya ndoa.

Hebu fikiri sasa, umeingiliwa au kujuana na wanaume wangapi? Nafsi yako imeunganikana na nafsi za wanaume wangapi? Umewaingilia au kuwajua wanawake wangapi? Nafsi yako imeungana na nafsi za wanawake wangapi? Idadi ya watu uliokutana nao kimwili ni idadi ya nafsi za watu ulizounganika nazo, unadhani utakuwa sawa kweli? Unadhani utakuwa salama kweli? Pengine hii ndio sababu huifurahii ndoa yako, na pengine imekuwa vigumu kudumu katika mahusiano na mtu uliyekusudia kudumu naye kwa sababu ya mvutano wa nafsi ambazo wewe umeunganishwa nazo kupitia ukahaba (kufanya ngono kwa sababu ya sitarehe au biashara nje ya ndoa).

Madhara ya kuungana na nafsi za watu ambao hawatakuoa au hautawaoa ni pamoja na;

1. Kutofurahia ndoa yako na mahusiano yako ya kimwili na mke/mume wako kitandani.

Kila unapokuwa kitandani utawakumbuka wapenzi wako wa zamani katika mambo mengi kwa sababu nafsi yako imeungwa nao. Umelala na mke au mume wako lakini watakuja wapenzi wako wa zamani kichwani mwako mmoja mmoja ukiwalinganisha na mume/mke wako katika mambo fulani yanayowahusu ninyi wawili kama mke na mume yale ya unyumba kitandani na yale mengine ya kawaida.

Kwa sababu umekuwa na watu wengi kwenye mahusiano na kushiriki nao ngono kabla au nje ya ndoa, unakuwa katika nafsi yako una uzoefu tofauti tofauti kutoka kwa kila mmoja. Sasa unapoamua maisha ya ndoa, kwa sababu ya muunganiko wa nafsi yako na nafsi za watu wote uliofanyanao tendo hilo, itakusumbua sana kila unapokuwa kitandani na mume/mke wako. Hii ndio sababu wengine wao hulazimika kuanza kuwatafuta wapenzi wao wa zamani ili kushiriki nao ngono kwa sababu watakuwa wanajisikia kutotoshelezwa na wenzi wao wa ndoa. Hii si kweli kwamba hawatoshelezwi, isipokuwa ni ule muunganiko wa nafsi; nafsi za wale watu zinamsonga na kumvuta mtu huyu kinyume cha mume/mke wake.​


2. Kutojitoa kikamilifu kwa mwenzi wako katika ndoa yenu.

Hii ni kwa sababu pengine uliumizwa sana na wapenzi wako wa zamani na kwa sababu nafsi yako imeunganishwa na nafsi zao, kila wakati unakumbuka walichokufanyia na kwa sababu hiyo unahisi kuwa kitajirudia kwa huyo uliyenaye sasa. Matokeo yake unaogopa kujitoa kwake mzima mzima. Kushindwa kujitoa kwake ni jambo ambalo litasababisha matatizo si kwa upande wake tu bali kwa upande wako pia kwa sababu matatizo ya ndoa huwa si ya upande mmoja, ni ya pande mbili mithili ya upanga au kisu chenye makali kuwili kinachokata huku na huku.​


3. Hali ya kutomwamini mwenzi wako wa ndoa.

Hii pia ni kutokana na uliyotendwa, na kwa sababu nafsi za hao watu bado zipo hai ndani ya nafsi yako zikiwa zimegundishwa, basi humwamini mwenzi wako, unakuwa unadhani kuwa yupo anakusaliti na mwingine.​


4. Roho mbalimbali za Shetani zilizokuwa ndani yao zinakuwa ndani yako na kufanya kazi kinyume chako.

Wasichojua wengi, Shetani hupitishia mambo yake mengi na roho chafu nyingi kuwaingia watu kupitia kukutana kimwili na watu wenye roho hizo.

Hii ndio sababu wakati mwingine mganga wa kienyeji kukufanyia tiba italazimika ukutane naye kimwili ili kwa njia hiyo apitishe nguvu za giza kuingia kwako. Katika baadhi ya familia au koo ili kuwarithisha watoto wao roho za kiukoo utakuta mama anaingiliwa na mtoto wake, au baba anamwingilia mtoto wake wa kike.

Katika kufanya kwangu huduma, nilikutana na dada mmoja ambaye alikuja ili nimwombee kwani alikuwa anaumwa sana na mambo yake yalikuwa hayaendi vizuri tena.

Dada huyu aliniambia kuwa, sababu ya yeye kuugua hivyo na mambo yake kuwa mabaya ni kukataa kuingiliwa kimwili na baba yake ambaye huwaingilia kimwili kila mwaka mwanzoni.

Aliniambia kuwa, dada yake wa kwanza ambaye tayari ameolewa huenda kila mwaka na kufanya mapenzi na baba yake kwa sababu za kiimani na anaonekana kufanikiwa katika mambo yake. Lakini Yeye tangu amekataa, baba yake alimwambia kuwa ataugua na mambo yake kuharibika, na ndicho kilikuwa kinatokea.

Wakati nakutana naye alikuwa amedhoofu sana na ilikuwa ni mwaka wa pili hajaenda kwao ili kulala na baba yao. Moja ya sababu iliyosababisha asitishe kwenda ni hali ya kujisikia kulala na kila mwanaume pindi anapolala na baba yake wakati huo anakuwa hajisikii kuolewa kabisa.

Jambo la kushangaza, mambo haya hata mama yao alikuwa anayajua. Na kila wakienda alikuwa anawaachia mume wake na chumba kisha kwenda na kulala chumba kingine. Ilinishangaza sana. Kwa hiyo, tendo hili si la kuchukulia kirahisi kwa sababu lina athari kubwa sana.​


NAMNA YA KUJIONDOA KATIKA MUUNGANIKO HUO WA NAFSI

1. Kama ulikuwa hujaokoka amua wokovu kwa kumpa Yesu maisha yako kwa sababu Mungu ndiye mwenye uwezo wa kutukomboa na nafsi za watu (2 Korintho 5:17)

Katika kifungu hiki cha maandiko, Biblia inasema kuwa, Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita, tazama! yamekuwa mapya; hii maana yake kwa kule wewe kuwa ndani ya Yesu Kristo kwa njia ya kumwamini tayari muunganiko wo wote usio wa ki-Mungu unavunjika, si tu muunganiko wa nguvu za giza, lakini pia na muunganiko wa kinafsi, ya kale yanakuwa yamepita, tazama yanakuwa mapya kwa sababu sasa wewe unakuwa umekuwa kiumbe kipya.​


2. Omba wokovu na ukombozi wa nafsi yako kwa Mungu ukijitenga na nafsi hizo kwa sababu wewe ni kiumbe kipya sasa ndani ya Yesu Kristo na ndani yake unao ukombozi (Zaburi 34:22; 116:24; Wakolosai 1:13-14; Waefeso 1:7; Wagalatia 2:20).

Ukiwa umeokoka kama utakuwa bado unaona vitu hivi vinakufuatilia, basi, amini katika kile Yesu Kristo amefanya kwa ajili yako, kisha ingia kwenye maombi na kuanza kukidai. Maombi yanasababisha wokovu na ukomboazi aliotufanyia Yesu Kristo pale msalabani kwa kufa kwake uwe halisi katika maisha yetu.

Iwapo utaona kuna mapungufu ya kile Biblia inasema Yesu amefanya kwa ajili yako, basi wewe ingia kwenye maombi na uombe kwa Mungu kwa sababu Biblia inasema kuwa, Mtu wa kwenu akipungukiwa hekima, na aombe dua kwa Mungu awapaye wote kwa ukarimu wala yeye hakemei, lakini na aombe kwa imani pasipo shaka (Yakobo 1:5 - 8). Kwa hiyo, unapoona hakuna utimilifu wa yale yanayosemwa na Biblia kuhusu wokovu na ukombozi wako, ingia kwenye maombi na uombe mpaka utakapoona utimilifu huo.​


3. Wasamehe wote waliokuumiza katika eneo la mahusiano hasa ulioshiriki nao ngono;

Ni muhimu sana ukawasamehe wote waliokuudhi na hasa wale waliokutenda wakati unahusiana nao kingono; watoe moyoni mwako kwa sababu msamaha unakutenga na nafsi za watu zilizo kuwa ndani yako; mambo yao na matendo yao yanakuwa hayana nguvu juu yako. Wanakuwa wamekufa nafsini mwako kwa habari ya mabaya waliyokutenda (Wakolosai 3:13).​


4. Ishi maisha mtakatifu, jitenge mbali na zinaa na uikimbie kila uionapo au usikiapo dalili zo zote zinazokusababisha uingie katika zinaa (Rumi 13:13; 1 Korintho 10:8; Waefeso 5:3; Wakolosai 3:5; 1 Thesalonike 4:3).

Maisha matakatifu yanakutenga na uchafu wa zinaa au wa kingono na madhara yake yote. Lakini kama hautaishi maisha matakatifu, kila wakati utajikuta umeingia katika mambo ya ukahaba na kujikuta katika muunganiko wa nafsi yako na nafsi za watu wengine. Utakatifu ni silaha ya kujilinda na dhambi zote ikiwa ni pamoja na zinaa na uasherati.​
NGONO INAHARIBU MISINGI YA NDOA

Katika ujenzi wa nyumba, mnara, au taasisi yo yote ile, msingi ni kitu cha muhimu sana. Iwapo msingi utajengwa vibaya, au msingi ukiharibika mwenye mnara, nyumba au taasisi atafanya nini?

Zaburi 11:3
[3]Kama misingi ikiharibika,
Mwenye haki atafanya nini?

Mahusiano ya uchumba na ndoa misingi yake ni uaminifu na utakatifu kwanza kwa Mungu, na pili kwa mwenzi wako. Hii ndio sababu Mungu ameagiza kuwa ndoa na iheshimiwe na watu wote na malazi (tendo la ndoa) yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumia adhabu wazinzi na washerati (Waebrania 13:4).

Uaminifu na utakatifu ambayo ndiyo misingi ya ndoa inapoharibiwa ndoa pia huharibika na ndio sababu Mungu atawahukumia adhabu wote wanaohusika kuharibu misingi ya ndoa.

Heshima ya ndoa ni utakatifu na uaminifu kwa Mungu na kwa mwenzi wako; ngono, yaani, tendo la ndoa nje ya ndoa ni uchafu unaochafua malazi (tendo la ndoa kitandani) kwa kuleta nafsi za watu wengine kitandani hapo uliowahi kufanya nao ngono au unaofanya nao ngono, na roho nyingine za Shetani zinazokuja kwa njia ya kufanya ngono nje ya ndoa.

Msingi wa mahusiano ya ndoa, ni mume mmoja na mke mmoja, nafsi moja ya mke na nafsi moja ya mume katika ndoa na katika kitanda chao (malazi); mmoja wapo anapofanya tendo la ndoa nje ya ndoa na mwingine au wengine, anachafua malazi kwa sababu ameiharibu misingi ambayo ni uaminifu na utakatifu, na hivyo, Mungu atamuhukumia adhabu.

Kijana ambaye hajaoa na binti ambaye hajaolewa, anapofanya ngono kabla hajaolewa huwa anasababisha mambo mawili;

1. Anaharibu Misingi:
Ndoa ni taasisi ambayo tangu mwanzo mpaka mwisho wake inajengwa juu ya misingi ya utakatifu na uaminifu. Binti au kijana anapofanya ngono maana yake anavunja na kuharibu misingi hii ambayo itapelekea ndoa yake iwe katika hali ya kutotawaliwa na utakatifu na uaminifu.

Utakatifu huu na uaminifu huu ni kwa Mungu na kwa mwezi wako wa ndoa mtarajiwa; haupaswi kuvunjwa wala kuharibiwa. Iwapo itatokea ikaharibiwa, matengenezo yake huwa yana gharama kubwa sana.

Tujifunze kwa Daudi, ilimgharimu kufanya matengenezo ya misingi baada ya kuzini na mke wa Uria, iligharimu hata kifo cha mtoto wake pamoja na kufunga sana! Lakini pia ndio ilipelekea mambo ya uasherati yaambatane na nyumba yake kwa Amnoni kumbaka Tamari (2 Samweli 13), na Absolomu kulala na masuria wa baba yake Daudi hadharani (2 Samweli 16:22) kwa sababu aliiharibu misingi na kwa hiyo ilimchukua muda mrefu kuijenga na kwa gharama ya kupoteza baadhi ya watu wake wa muhimu hata kuhatatisha ufalme wake.

Utakatifu
Utakatifu maana yake ni kutengwa maalumu kwa ajili ya mtu au kazi fulani. Kwa hiyo, kijana au binti katika hili ametengwa kwa ajili ya mume/mke wake wa ndoa, na tendo la ndoa limetengwa maalumu kwa ajili ya wanandoa. Kwa hiyo, kijana au binti mtakatifu anapaswa akutane na tendo la ndoa takatifu ndani ya ndoa takatifu na si nje ya ndoa, hapo ndipo hakutakuwa na kuharibiwa kwa misingi.

Uaminifu
Uaminifu ni hali ya kuaminiwa na kujiaminisha kwa wewe kubaki kuwa mkweli kwa Mungu na kwa mwenzi wako mtarajiwa huku ukiwajibika kwa kila tendo unalofanya na utakalofanya. Uaminifu ni hali ya kubaki katika utakatifu kwa ajili ya Mungu na mwenzi wako wa ndoa mtarajiwa.

Kwa maneno mengine, uaminifu ni uwajibikaji katika kujitunza ili ubaki katika hali uliyonayo tangu mwanzo kwa ajili ya mwenzako huku ukijitenga na wengine wote pamoja na ngono kabla ya ndoa au nje ya ndoa. Biblia katika kitabu cha 1 Wathesalonike 4:3 - 5 inasema;

[3] Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;
[4] kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;
[5] si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu.


Uaminifu na utakatifu ni mambo yanayoenda pamoja, unapovunja uaminifu unakoma kuwa mtakatifu, na unapoharibu utakatifu wako unavunja pia uaminifu wako. Kwa hiyo kila mmoja anapaswa ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima kwa kuendelea kuwa mwaminifu kwanza kwa Mungu na pili kwa mwenzi wake wa ndoa.

Matendo ya ngono na ngono yenyewe nje ya ndoa yamekusudiwa kuharibu misingi ya utakatifu na uaminifu wa mtu katika maisha yake ya ndoa. Kuyaepuka na kuyakimbia ni tendo la kutunza misingi katika ndoa ili mwenye haki awe salama.

Leo hii ndoa zina changamoto za kukosa uaminifu na utakatifu kwa sababu misingi hiyo ilivunjwa tangu mwanzo. Kusalitiana limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa sababu tangu mwanzo misingi iliharibika. Watoto wengi wamekuwa ni kizazi cha zinaa, wanajua mambo ya watu wazima kwa sababu misingi iliharibiwa na wazazi wao, hivyo ile roho ya zinaa imewaingia tangu kuzaliwa kwao; wanatungwa mimba katika hali ya uovu kwa sababu misingi ya utakatifu na uaminifu iliharibiwa.

2. Anachafua malazi
Iwapo wewe kijana au binti utaanza kushiriki ngono kabla ya ndoa, kitu utakachokuwa unakifanya ni kuchafua kitanda chako na mume/mke wako, ni kuchafua unyumba wenu kwanza kwa uasherati na uzinzi utakaokuwa ukiufanya hata kama utafanya na mwanaume/mwanamke huyo huyo atakekuoa au utakayemuoa kwa sababu uasherati na uzinzi ni uchafu na unakaribisha mapepo kitandani kwenu hata kusababisha uharibifu katika ndoa.

Unajua, ugomvi mwingine huwa ni mapepo mliyoyakaribisha kitandani kwenu kwa sababu ya uchafu wa uasherati na uzinzi wenu kabla hamjaona! Unashangaa tu mara tu baada ya kufanya tendo hilo ndipo mnaanza kugombana, hata mnapoingia kwenye ndoa, kila tu mkifika kitandani, au ikifika usiku mnaanza kununiana na kugombana kwa sababu malazi si safi ni machafu.

Jambo la pili, unachafua malazi kwa muunganiko wa nafsi za wanaume/wanawake wote uliofanya nao ngono kabla hujaoa au kuolewa. Kila unapokuwa kitandani unawakumbuka wapenzi wako wa zamani, na ghafula hamu ya kuendelea kufanya tendo hilo kwa muda mrefu inatoweka.

Wengine kwa sababu wamechafua malazi yao kwa kuangalia picha na video za ngono, anakosa raha ya kufanya tendo la ndoa na mwenzi wake na badala yake anafurahia kufanya tendo hilo yeye mwenyewe, au na mwanamke/mwanaume mwenzake, au na kahaba huko nje.

Hii ndio sababu Biblia imeagiza kuwa, unywe maji ya birika lako mwenyewe, na maji ya birika lako yakutoshe wewe mwenyewe, yawe yako, yasitawanyike na kwenda mbali ili kuwe na kufurahiana katika ndoa (Mithali 5:1-23).

Matatizo mengi na changamoto nyingi katika ndoa yanatokea kwa sababu misingi ya uaminifu na utakatifu iliharibika kwa kuharibiwa na watu na malazi pia yalichafuliwa.

Sasa, misingi ikiharibika mwenye haki afanye nini? Arejee kwa Mungu kama Daudi alivyofanya (Zaburi 51) na kutafuta rehema kwa kuwa Mungu ndiye aijengaye Yerusalemu, Mungu ndiye aijengaye ndoa ambayo misingi yake imeharibika (Zaburi 147:2).
MAZINGIRA HATARI YANAYOMTUMBUKIZA MTU KATIKA KUFANYA NGONO

Tunaendelea kuzungumza kuhusu ngono na leo nataka tuangalie mazingira hatari na namna ya kuyaepuka.

Ngono isipokuwa kwa kubakwa tu huwa haitokei kwa ajali; hutokea kwa wahusika wote wawili kukusudia au kukubaliana na aliyekusudia; kwa hiyo ni makusudi kabisa.

Mtume Paulo akiwaandikia Wakorintho kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, kwa lugha nyingine aliyekuwa anasema ni Roho Mtakatifu akitumia kinywa cha Paulo, anaandika:

1 Wakorintho 6:18
[18] Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.

Hii maana yake ni nini? Maana yake zinaa haikemewi, haifungwi, haiteketezwi kwa moto na kwa Jina la Yesu, bali inakimbiwa kwa sababu ni juu ya mwili wako na si roho yako au nje ya mwili wako; hii inahusiana na mwili wako.

Ukiguswa unangonoka, ukitomaswa-tomaswa, ukiona kwa macho, ukiambiwa maneno laini, matamu utajikuta tu unangonoka na wakati mwingine huku umeshika Biblia na unanena kwa lugha. Hapa haimaanishi hauko kiroho, hapana, isipokuwa umekosea kanuni ya jinsi ya kupambana na zinaa.

Kukimbia zinaa ni silaha ya kiroho kabisa ya kushinda zinaa. Yapo mambo manne tu ambayo tumeagizwa tuyashinde kwa kukimbia; ibada ya sanamu, tamaa za ujanani, mafundisho ya uongo na zinaa.

Sasa inashangaza kwamba, watu wanakuwa wa kiroho kumshinda Roho Mtakatifu na Shetani. Roho Mtakatifu ameona kuwa ushindi wa wewe kushinda zinaa ni KUKIMBIA wewe eti unajidai umejaa Roho na nguvu za Mungu utaishinda kwa kukemea. Haiwezekani hata kidogo; hapa kukimbia sio woga ni ujasiri, na sio kushindwa ni kushinda zinaa.

Sasa anaposema tuikimbie zinaa, anamaanisha kwamba, tuyakimbie mazingira yanayopelekea tuingie katika zinaa, na hayo mazingira ni ngome za Shetani.

Kwa sababu tendo hili hufanywa faragha, mazingira yote yanayowapa faragha ninyi wawili peke yenu ni ya kukimbia kabisa. Ninakwambia kitu ninachokijua na ambacho nimekipitia, si mara moja tu bali mara nyingi, kwa hiyo najua ninachokisema.

MAZINGIRA

1. Nyumbani kwa mwanaume/mwanamke.

Mithali 5:8-11
[8]Itenge njia yako mbali naye,
Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.

[9]Usije ukawapa wengine heshima yako,
Na wakorofi miaka yako;

[10]Wageni wasije wakashiba nguvu zako;
Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;

[11]Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho,
Nyama yako na mwili wako utakapoangamia;
Ukianzia mstari wa kwanza utaelewa. Anayezungumziwa hapa ni malaya.

Hata siku moja, hakuna aliyewahi kwenda nyumbani kwa mchumba wake au mpenzi wake wakawa peke yao tu aliyetoka salama bila kuzini. Inawezekana siku ya kwanza ukatoka bila kufanya ngono kwa maana ya kukutana kimwili, lakini ukatoka ukiwa umekulana denda na mchumba wako au kutomasana-tomasana. Na kwa kuwa safari moja huanzisha nyingine, siku nyingine mtamalizia kwa kufanya mapenzi kabisa.

Mbali na uzoefu nilionao, mimi binafsi na kwa watu wa karibu yangu Biblia nayo inaonyesha jambo hili kuwa ni kweli.

Ukisoma 2 Samweli 13, sura nzima utakutana na habari ya Tamari na Amnoni. Amnoni mwanzoni alionekana anampenda Tamari, akafanya namna ili Tamari aje nyumbani kwake baada ya kushauriwa na rafiki yake. Tamari alienda na alipokuwa nyumbani kwa Amnoni, Amoni alitengeneza mazingira ya wao wawili kubaki peke yao chumbani. Kilichotokea wewe mwenyewe unajua.

Yakobo pia alikuwa na binti aliyeitwa Dina. Huyu naye ivyo hivyo alitoka na kwenda kwa binti za mataifa, na huko akakutana na kijana mtanashati mwana wa mfalme, akamwingiza chumbani kwake na kumbaka (Mwanzo 34:1 - 10).

Unakumbuka hadithi ya Daudi kulala na mke wa Uria? Naye aliletwa nyumbani mwa Daudi na Daudi akalala naye. Kama asingekubali kwenda au kuingia chumbani kwa Daudi, Daudi asingeweza kulala naye.

Ukisoma kitabu cha Mithali 7, utakutana na hadithi ya mwanamke kahaba akimshawishi kijana kwenda nyumbani kwake ili washibe upendo.

Hii maana yake ni nini, nyumbani ndipo ilipo ngome ya Shetani ya kuangusha wengi katika zinaa kwa sababu ni sehemu nzuri kwa ajili ya faragha.

Hii hauwezi kukwepa kwa kukemea, hii unakimbia kwa kutokwenda na kama kuna ulazima, usiende peke yako, nenda mkiwa watatu au zaidi na unaweza hata usimwambie kama unaenda na watu kama tayari umeishajua udhaifu wake.

Hii nyumbani sio nzuri kabisa, imewaangusha wengi, imewaingiza wengi matatani. Usiwe wewe.​
2. Nyumba za kulala wageni
Hii ni pamoja na Hoteli, lodge na guest house. Mnasafiri pamoja, au mna mazungumzo, usikubali kuyafanyia kwenye nyumba za kulala wageni, mwisho wa siku utajikuta umeingia dhambini. Kuzikimbia nyumba hizi ni kukimbia zinaa.

Ye yote, awe mwanaume au mwanamke anayetaka mkutane kwenye nyumba za kulala wageni na wakati ninyi mpo wachumba au ni watu wa jinsi mbili tofauti, chunguza sana nia yake; lazima tu atakuwa na mpango kabambe wa kulala na wewe. Na ieleweke kuwa, ukiishaingia mtegoni ni ngumu sana kutoka bila mtego kukunasa, mara nyingi utanaswa tu.

Kama waswahili wanavyosema, heri nusu shari kuliko shari kamili; yaani katika hili, bora mgombane kuliko kuanguka dhambini kwa dhambi ya zinaa. Tena wanasema kuwa, kinga ni bora kuliko tiba; ni muhimu ukajikinga kwa kutoingia kabisa katika nyumba hizi na mtu wa jinsi tofauti na wewe, la sivyo tiba itakuhusu.

Mithali anasema kuwa, Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha, bali mpumbavu huendelea mbele akaumia. Wewe kuingia kwenye nyumba hizi za wageni ni kuyaona mabaya na ukaendelea mbele, bila shaka yo yote utaumia.

Kwani kuna wangapi waliofia kwenye nyumba za kulala wageni mbali tu na kufanya zinaa? Jamani, Shetani yumo humo, usimpe nafasi ya kukumaliza, kimbia kabisa na wala usiangalie nyuma.​

3. Porini, mapangoni au sehemu yo yote isiyokuwa na watu
Wengine huwa ni wajanja, wanakupa mwaliko wa kukupeleka matembezini kisha anakuchukia mpaka huko porini au kwenye mapango, baada ya kukupa chakula kizuri, moyo wako unalainika, kwa vyo vyote vile kile atakachotaka utampa na mtafanyia huko huko hata kama atakuwa ajakupa chakula. Mazingira haya ni ya kukimbia kabisa, si ya kukubali kwenda kichwa kichwa.

Po pote ambapo panawapa faragha ni hatari kwa usalama wako katika jambo hili; kwa hiyo mzingira ya kuwa peke yenu hata kama ni safarini, si salama kabisa, yaepuke haraka.​

4. Usiku peke yenu
Epuka sana kutembea usiku mkiwa peke yenu wawili tu, iwe kwa miguu au kwa gari, au kukaa au kusimamia njiani peke yenu majira ya usiku. Mazingira haya yatapelekea ufanye zinaa kirahisi kabisa.

Binti mmoja alinipigia simu na kuniambia kuwa, nimwombee rehema kwani amejikuta akifanya mapenzi na bosi wake ndani ya gari nje ya nyumba yao. Unajua ilikuwaje? Bosi wake ambaye alikuwa na mke na watoto tayari alimtongoza binti huyu ambaye alikuwa ni mfanyakazi wake. Lakini hata hivyo binti huyu alikataa katakata kwa sababu ameokoka. Bosi alipoona binti ana msimamo mkali, alimwambia basi wawe marafiki wa kawaida, na binti baada ya kusumbuliwa sana akaona isiwe shida, akamkubalia.

Walianza kutoka pamoja mara chache chache kwenda kula chakula cha mchana, lakini kadiri siku zilivyoendelea ilitoka kuwa mara moja moja ikawa ni kila siku. Kutoka kula chakula cha mchana pamoja, bosi akaanza kumpeleka binti nyumbani kwao na kisha yeye kwenda kwake kwa jina la urafiki.

Siku moja wakiwa wamefika nyumbani kwa binti, walikaa ndani ya gari kwa muda mrefu wakifanya mazungumzo, hata jua lilipozama. Katika hali ambayo binti hakuweza kunieleza vizuri, alijikuta tayari wamefanya ngono na wamemaliza wakiwa ndani ya gari; ilitokeaje hajui anachojua ni kwamba wamefanya.

Unaona jisi ilivyo hatari! Kama binti alitaka kukwepa yote haya yasimpate, alitakiwa kuzikimbia ofa za huyu jamaa kwa kuzikataa mwanzo hadi mwisho. Siku zote Shetani ana hila au mbinu nyingi sana za kutuangusha.​

5. Mwanaume au mwanamke anayetaka au anayekuomba ngono
Ukiwa na mchumba au mpenzi ambaye anataka ngono tu, mkimbie usimvumilie, na moja ya kumkimbia ni kumkemea, kumkatalia na kuepuka kuwa naye peke yenu wawili, na ukiona analazimisha sana usisubiri akuache, anza wewe kumwacha mapema. Huku ndiko kukimbia zinaa.

Ni hatari sana kuendelea kuwa kwenye mahusiano na mchumba anayekuomba ngono, na ni hatari zaidi pale unapoamua kuwa naye karibu mkiwa peke yenu, wawili tu. Huwezi kukwepa kuzini au kuanguka kwenye zinaa, dawa ni kukimbia tu.​

6. Mazungumzo mabaya
Moja ya kichocheo cha kufanya ngono ni mazungumzo yahusuyo ngono. Kwepa sana mazungumzo hayo, iwe na mpenzi wako au na rafiki zako, yatakuharibu.

Unakuta mtu anamsifia mpenzi wake matako yake, mapaja yake, kiuno chake, uke wake, maziwa yake kwa sauti ya mahaba au kwa kupitia ujumbe mfupi wa simu, una tegemea nini? Kemea vitu hivi, kataa mambo kama haya na ikiwezekana watupilie mbali watu kama hawa wenye mazungumzo haya.

Usipende sana kusikiliza au kuzungumza mazungumzo yahusuyo ngono iwe na mchumba wako au rafiki zako, yatakupelekea uangukie kwenye zinaa, yakimbie mazungumzo ya namna hii kabisa.​

7. Mitandao ya kijamii, picha na video za ngono
Usiwe mfuasi wa mitandao ya kijamii inayojihusisha na maswala ya ngono, haya yote kupitia makala zao za kingono, picha na video za ngono inakuingiza katika zinaa.

Kwa sababu zinaa ni dhambi unayofanya juu ya mwili wako, si lazima muwe wawili ili kuifanya, wakati mwingine unaifanya ukiwa uko peke yako mwenyewe. Hii ndio moja ya sababu Roho Mtakatifu anatuagiza tuikimbie. Fanya agano na macho yako kuwa usiangalie msichana, mvulana katika hali ya utupu wake.​

Ayubu 31:1
[1]Nilifanya agano na macho yangu;
Basi nawezaje kumwangalia msichana?

Mpendwa kijana, binti, mwanaume, mwanamke, mzazi, zinaa imeharibu kizazi cha leo, si jambo la kuchukulia kirahisi kwa sababu limesababisha vijana wengi na watu wazima pia wawe na ugonjwa wa uraibu wa ngono hata kuathiri maisha yao yote. Kwa hiyo, tuiepuke kwa kuikimbia kabisa.

Mungu akubariki sana
Αναζήτηση
Κατηγορίες
Διαβάζω περισσότερα
OTHERS
MTUME PAULO ANAVYO WANYIMA USINGIZI WAISLAM
Kati ya watu wanaowasumbua sana ndugu zetu Waislamu ni shujaa wa Bwana Yesu, Mtume Paulo. Na hii...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 05:04:40 0 7χλμ.
STANDARD 2
STANDARD 2
List of all subjects for the standard 2 class
από PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 10:19:03 0 5χλμ.
JUDGES
Verse by verse explanation of Judges 14
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-01-25 11:08:10 0 5χλμ.
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 17
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:18:20 0 5χλμ.
OTHERS
Je, Walio-okoka Wanaweza Kwenda Jehanamu?
Kama Paulo anavyoandika, Mungu hutuadhibu “ili isitupase adhabu pamoja na dunia”...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 10:04:22 0 5χλμ.