NDOA NA ROHO YA SIKU ZA MWISHO

0
5K

Siku Za Mwisho:
Siku za Mwisho ni siku zilizotajwa katika Biblia kuwa ni siku zote baada ya Yesu kupaa kwenda mbinguni ambazo zinatangulia kabla ya siku ya mwisho ambayo ni siku ya kuja kwake Yesu Kristo kwa kusudi la kulichukua kanisa lake na hatimaye kuwahukumu wanadamu wote, ulimwengu wote, Shetani na malaika zake.

Tunaposoma Biblia, inaonyesha wazi kwamba, siku za mwisho zilianza tangu kipindi cha Kanisa la Kwanza mara tu baada ya Yesu kuondoka duniani sawasawa na alivyotabiri nabii Yoeli akitabiri juu ya ujio wa Roho Mtakatifu kwa wote watakaomwamini Yesu Kristo. Hivyo, tangu kipindi cha Agano Jipya kianze ndipo na siku za mwisho zilianza kuhesabika kuwa ni siku za mwisho. Kwa sababu Roho Mtakatifu alitabiriwa kumwagwa kwetu sisi katika siku za mwisho, kumwagwa kwake kwetu sisi tunaomwamini Yesu Kristo ni ishara ya kwamba siku za mwisho tayari zipo, zimeanza kuhesabiwa katika majira ya karenda ya Biblia; hivyo hadi sasa tunaishi katika siku za mwisho.

Matendo 2:16 - 17

Lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.​


Roho Ya Siku Za Mwisho:
Roho ya siku za mwisho ni roho ya Shetani itendayo kazi katika nyakati za siku za mwisho iliyoachiliwa na Ibilisi kwa kusudi la kusababisha uharibifu wa kimaadili katika ngazi ya ndoa, familia, na kanisa lakini pia kwa kusudi la kupotosha na kuwadanganya wengi dhidi ya Kristo. Hii ni roho ya Mpinga Kristo ambayo inatenda kazi katika siku za mwisho ili kuharibu kanisa ikianza na kuharibu mtu mmoja mmoja, ndoa, na familia. Lengo kubwa la roho hii ni watu wasimwone Mungu, watu wawe waovu mbele za Mungu lakini pia wao kwa wao; na roho hii inafanya kazi kwa kasi sana.

Roho ya siku za mwisho (roho ya Mpinga Kristo) katika utendaji wake hutenda kazi kwa kuachilia tabia zilizo kinyume na tabia za Mungu ndani ya nafsi za watu na kupitia tabia hizo kusababisha uharibifu katika ndoa, familia, na katika Kanisa la Kristo iwapo hazitashughulikiwa ipasavyo. Na kwa kuwa roho hii hufanya kazi zake kwa udanganyifu kwa kuachilia roho zidanganyazo, wakati mwingine ni ngumu sana mtu kujitambua mpaka amemruhusu Roho Mtakatifu na Neno la Kristo lifanye kazi ndani yake, vinginevyo atajiona yuko sawa tu.

Isivyo bahati, roho hii ya siku za mwisho imeachiliwa sana na Ibilisi ili kusababisha uharibifu (hasa wa kimaadili katika kuhusiana) katika taasisi mbili za muhimu sana ambazo ni ndoa na kanisa. Hizi ni taasisi nyeti sana katika kuzalisha watu wanaomfaa Mungu na kuifaa jamii ya watu duniani hapa. Kama ndoa itazalisha watu waovu na kanisa likashindwa kuzalisha watu wema, dunia haitakuwa na watu wenye maadili na wema wanaomcha Mungu na wanaowafaa watu wengine.

Sasa katika somo letu hili, kwa sababu ya unyeti wa jambo hili (kwa maana roho hii hupelekea uharibifu mkubwa na mwisho wake watu huiacha Imani), kwa pamoja, napenda tujifunze juu ya utendaji kazi wa roho hii ya siku za mwisho lakini hasa tutajikita katika upande wa ndoa na wakati mwingine tutagusa kanisa kwa sababu taasisi hizi mbili zinakwenda pamoja, zinaingiliana na zinategemeana sana.

Kabla hatujaendelea sana na somo letu, katika huu utangulizi, naomba kwanza usome maandiko yafuatayo;

2 Timotheo 3:1-7

[1]Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

[2]Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

[4]wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;

[5]wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

[6]Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi;

[7]wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.

[8] Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kwelini watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.

[9] Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri.


Haya maandiko ndio yamebeba somo letu lote. Nitaomba wewe uyasome tena na tena tunapoendelea na somo letu.

Dondoo zitokanazo na kifungu chetu cha msingi cha maandiko:

Ufahamu Juu Ya Nyakati Za Hatari Zitakazokuwepo Katika Siku Za Mwisho;
Biblia inaanza kwa kutuambia kuwa, "Lakini ufahamu neno hili," hii maana yake ni kwamba, uwezo wa sisi kukabiliana na nyakati za hatari zinazokuwepo katika siku za mwisho unaanza kwanza na sisi kufahamu kwamba; (1). Tunaishi katika siku za mwisho, (2). Katika siku hizi za mwisho kuna nyakati za hatari, na (3). Uwepo wa siku za hatari unasababishwa na roho itendayo kazi ndani ya watu katika siku hizi za mwisho.

Katika mambo yote, ufahamu wa jambo ni jambo la muhimu sana na ni jambo la kwanza kabla ya mtu kuanza kufanya jambo lolote. Usilolijua ni usiku wa giza, na kweli usiyoijua au usiyoifahamu haiwezi kukuweka huru (Yohana 8:32). Kutojua au kutofahamu neno hili, yaani, ya kuwa, siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari, ni hatari sana kwetu kwa sababu tutaumia, tutaharibikiwa kimaisha, na tutaangamizwa kabisa. Lakini tukiwa na ufahamu juu roho hii na namna inavyotenda kazi hatutakosa kuzijua fikira au hila za Ibilisi maishani mwetu.

Mwandishi wa kitabu cha Timotheo anatoa wito wa sisi sote kila mmoja kwa nafsi yake ya kwamba, afahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Kwa nini? Kwa sababu ambazo amezitaja hapo chini katika kifungu cha maandiko tuliyoyasoma. Na sababu hizo zote zina msukumo nyuma yake wa roho ya siku za mwisho itendayo kazi ndani ya watu kwa werevu sana ili kusababisha uharibifu na upotevu.

Kwa kuwa pona yetu ni kufahamu neno hili kwa kina na kuweza kupambanua roho hii kwa kujua hila na fikira zake, yaani, mbinu na njia zake katika utendaji wa kazi zake, basi, kama wanandoa na wale tunaotarajia kuingia kwenye ndoa, nimeona vema tujifunze ili tujipatie ufahamu.

Mithali 4:5-9

[5]Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau;
Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu.

[6]Usimwache, naye atakuhifadhi;
Umpende, naye atakulinda.

[7]Bora hekima, basi jipatie hekima;
Naam, kwa mapato yako yote jipatie ufahamu.

[8]Umtukuze, naye atakukuza;
Atakupatia heshima, ukimkumbatia.

[9]Atakupa neema kuwa kilemba kichwani;
Na kukukirimia taji ya uzuri.

Ufahamu unakuja kwa kujifunza; na unapopata ufahamu na kuukumbatia, yaani, kuufanyia kazi, ufahamu huo unakupatia neema itakayokuwezesha kushinda yote.

Ufahamu huu tunaokwenda kuupata, unakupatia neema ya kushinda roho ya siku za mwisho katika eneo la ndoa zetu na familia zetu. Kwa hiyo uwe makini katika kujifunza ili usiipoteze neema hii.

Ufahamu juu ya namna roho ya siku za mwisho inavyotenda kazi;
Biblia inatutaka pia tufahamu namna ambavyo roho hii ya siku za mwisho inavyofanya kazi katikati yetu. Jambo la kwanza kabisa, ni kwamba, roho hii inafanya kazi kupitia watu walio miongoni mwetu, pengine ni wana ndoa wenza, au wanafamilia wenzetu, au wapendwa wenzetu kanisani, au wafanyakazi wenzetu huko maofisini. Si watu wanaotokea mbali, bali ni watu tunaoishi nao; roho hii huwaingia inapopata nafasi na kuanza kutumikisha dhidi yetu. Lakini pia kwa kuwa wewe pia ni miongoni mwa watu, upo hatarini kutumiwa na roho hiyo dhidi ya mtu mwingine. Hii ndio sababu Biblia inatufundisha kwamba, tusimpe Ibilisi nafasi (Waefeso 4:27).

Jambo la pili hapa ambalo Biblia inataka tulifahamu ili kwamba tuweze kukabiliana na roho hii ya siku za mwisho hata tuweze kuishinda ni tabia ambazo roho hii inazitumia kuharibu ndoa, familia, kanisa, na mahusiano mengine ya watu kwa kuzipanda ndani ya watu ambao wamempa Ibilisi nafasi ya kufanya hivyo. Tabia hizo zimetajwa katika kifungu chetu cha maandiko zikihusianishwa na watu hao ambao kiukweli wanapokubali kutumiwa na roho hii huzifanya nyakazi kuwa ni nyakati za hatari katika siku hizi za mwisho.

Ni muhimu tukafahamu kwamba, nyakati zinakuwa ni nyakati za hatari kwa sababu watu wametoka kuwa watu wazuri na badala yake kwa sababu ya kuingiwa na roho hii ya siku za mwisho wanakuwa hatari kwetu kwa namna wanavyotumiwa na Shetani, vinginevyo nyakati zetu ni nzuri na salama. Katika mstari wa pili katika kifungu chetu cha maandiko, Biblia inasema, "Maana watu watakuwa...." kinachowafanya wao kuwa watu wa hatari ni roho ya Shetani itendayo kazi ndani yao.

Ufahamu juu ya watu wanaotumika na roho ya siku za mwisho;
Biblia pia inataka tufahamu juu ya watu waliokubali kutumiwa na kutumika na roho hizo za siku za mwisho. Jambo la kwanza, ni watu wanaopingana na kweli ya Mungu, yaani Neno la Kristo; daima wapo kinyume na Neno la Mungu. Jambo la pili, ni watu walioharibika hakili zao kwa hiyo hata kujitambua hawajitambui kabisa, wao wanajiona wako sawa na wako sahihi kabisa. Jambo la tatu, ni watu waliokataliwa kwa mambo ya imani, hawana sehemu katika wokovu na faida zake maadamu tu wanatumika na roho ya siku za mwisho.

Jambo la nne kuhusu watu hawa ni watu ambao hawataendelea sana, wataangamizwa, hawatadumu katika hayo wayafanyayo. Kwa lugha nyingine anaposema kwamba, hawataendelea sana, anamaanisha kuwa hawatafanikiwa katika maisha yao, watakuwa duni; lakini pia hawatafanikiwa katika hila zao na mipango yao mibaya ya kuharibu kwa sababu watajulikana na watu, na somo hili ni mkakati wa kukuwezesha wewe kuwafahamu watu wa jinsi hii na kuweza kujihadhari nao mapema ili roho waliyonayo isije ikakujeruhi au ukaambikizwa na kuwa kama wao.

Baada ya utangulizi huu wa somo letu wenye lengo la kuweka msingi wa somo letu na kukupa ufahamu wa kuelewa uzito wa hiki tunachojifunza, katika sehemu ya pili tutanza kuangalia tabia moja baada ya nyingine inayosababishwa na roho hii ya siku za mwisho na namna inavyoharibu ndoa zetu na familia zetu iwapo itamshika mmoja miongoni mwetu.

Watu Wenye Kujipenda Wenyewe (Choyo na ubinafsi)

2 Timotheo 3:2

[2] Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,


Siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari kwa sababu watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe na si wenye kumpenda Mungu na kuwapenda wengine; hii tunaita ni choyo na ubinafsi. Kinachofanya siku za mwisho kuweko na nyakati za hatari ni watu kuwa wenye kujipenda wenyewe; hii maana yake ni watu ndio wanafanya kuwepo kwa nyakati za hatari. Kwa lugha rahisi ni kwamba, watu wenye kujipenda wenyewe ndio hatari na si nyakati kwa sababu kama watu wasingekuwa wenye kujipenda wenyewe nyakati za hatari zisingetajwa kwa sababu zisingekuwepo.

Kwa nini watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe? Kwa sababu watashikwa na roho ya siku za mwisho ambayo ndiyo itakayowafanya wawe wenye kujipenda wenyewe. Neno "watakuwa" linaaonyesha kuwa, mwanzoni watu hawakuwa hivyo, au kiasili kabisa watu hawako hivyo, isipokuwa kuna kitu kinawafanya wawe hivyo na kitu hicho ni roho ya siku za mwisho, ikiisha waingia na kuwashika, inawafanya wawe ni watu wenye kujipenda wenyewe.

Watu wenye kujipenda wenyewe ni hatari sana katika mahusiano ya uchumba na ndoa kwa sababu ni wenye choyo na wabinafsi, wanatafuta faida yao wenyewe, hawajali mambo ya wengine wala kujishughulisha nayo. Wanatumia watu wengine kujipatia faida wao wenyewe, ni walaghai na wadanganyifu, hawathamini wala kujali watu wengine, wanathamini ulichonacho wanachokihitaji na si wewe na ndio maana wakiisha kipata au kukikosa watakuacha na kisha kwenda zao bila kujali maumivu yako unayoyasikia kwa ajili yao.

Katika ndoa mke/mume ambaye ana tabia hizi, huyu bila shaka anakuwa ameshikwa na roho ya siku za mwisho; anajipenda yeye mwenyewe na kwa sababu hiyo inapofikia kwenye swala la wewe kumuhitaji yeye au kuhitaji msaada wake anakuwa yupo bize na mambo yake; haonyeshi kuthamini juhudi zako kwa ajili yake, haonyeshi kukujali, ilimradi umeishampa anachokitaka, yeye anakuwa hana haja na wewe tena.

Haoni umuhimu wa yeye kujitoa kwa ajili yako; wakati unaumwa yeye atajifanya kama vile haoni hata kama utamwambia, lakini akiwa anaumwa yeye atataka hata kazi nyingine usifanye uwe unamwangalia yeye; utamjali yeye akiwa mgonjwa lakini wewe ukiwa mgonjwa hata kukuangalia au kukujulia hali hatakujulia kabisa.

Mwanaume/mwanamke mwenye kujipenda mwenyewe utampa zawadi, utamfanyia wema au jambo zuri na bado hata kukushukuru asikushukuru na badala yake akaanza kubeza na kudharau hicho ulichomfanyia. Mtu wa namna hii katika mahusiano atataka vitu au jambo kutoka kwako kwa nguvu hata kama itamaanisha kukuumiza au hata kukutoa uhai wako ili akipate. Atakupiga, atakufanyia matendo ya kishujaa ikiwa ni pamoja na kukunyima tendo la ndoa, fedha ya matumizi n.k.

Mtu huyu vitu vyote vizuri na mambo yote mazuri atajifanyia yeye tu, na kukukumbuka wewe katika mabaya. Yupo tayari kukudanganya ili akuibie, au ajipatie kile anachokihitaji kwa sababu hafikirii kuhusu wewe ila yeye tu. Hana huruma na wewe wala mapenzi na wewe, atakuibia, atakutapeli hata kama wewe ni mume/mke wake au mchumba wake. Mwisho wa mambo yote haya ni kuumiza moyo wa mtu, kuharibika na kuvunjika kwa mahusiano ya ndoa au uchumba.

Nirudie tena kusema kuwa, nyakati zinafanywa kuwa nzuri au hatari na watu, watu wakiwa hatari nyakati nazo zinakuwa hatari, wakiwa wazuri nyakati zinakuwa nzuri. Ni hatari kwako na kwa maisha yako kuishi na mtu anayejipenda mwenyewe kwa sababu atakuweka kwenye nyakati za hatari; kila wakati utajikuta uko hatarini. Kwa hiyo ni vyema sana kujihadhari na watu wenye kujipenda wenyewe, ambao wao wakikosea unajikuta wewe mwenyewe ndio unawaomba tena msamaha wao hata kushituka hawashituki na badala yake wanakuona wewe ndio mkosaji.

Mtu anayejipenda mwenyewe ameshikwa na roho ya siku za mwisho ambayo ni roho ya uharibifu na inafanya kazi zaidi ndani ya ndoa, familia na kanisa ili kuharibu na kuvuruga mahusiano ya watu na ushirika walionao. Kama hutatambua roho hii, bila shaka utakuwa ni muhanga na muathirika wa roho hii, kama sio kutokea ndani yako basi itatokea ndani ya mwenzi wako katika ndoa, uchumba, familia au ndani ya kanisa.

Wanandoa hawapaswi kuwa wenye kujipenda wenyewe, wabinafsi na wenye choyo kwa sababu Biblia imetuagiza mambo mawili kuhusu upendo; kumpenda Mungu kwa moyo wote na pili kumpenda jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako.

Kujipenda mwenyewe ni mkakati na mbingu janja za Shetani ili kutuharibia uhusiano wetu na Mungu lakini pia na watu walio karibu nasi, ndani ya familia, katika ndoa na kanisani.

Huwezi kusema unampenda Mungu wakati humpendi jirani yako. Kama unampenda Mungu, utampenda kwanza mume/mke, mchumba au jirani yako.

Watu wenye kupenda fedha

2 Timotheo 3:2

[2] Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,


Mapenzi ya fedha yanapozidi utu wa mtu na thamani ya fedha unapozidi thamani ya nafsi ya mtu hata kufikia hatua mtu anaamua kutoa uhai wa mtu kwa sababu ya fedha bila shaka hapo kuna tatizo.

Miezi kadhaa iliyopita (mwaka 2018) katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ilivuma habari ya mchungaji mmoja aliyemuua mke wake aliyekuwa mhadhili wa chuo kikuu UDOM kwa kumkatakata na kitu chenye ncha kali hadi kufa. Hakufanya hivyo kwa sababu ya wivu wa mapenzi, hapana, alifanya hivyo kwa sababu alikuwa akimtaka ampe fedha; mwanamke alipokataa, ndipo alipoamua kumuua.

Mwanaume huyu alipenda fedha kuliko mke wake, na haikuwa bure, kwa wakati huo alishikwa na kutawaliwa na roho ya siku za mwisho ambayo inamfanya mtu apende fedha kuliko kuwapenda watu na kumpenda Mungu. Mwanamke huyu alijikuta yupo katika nyakati za hatari kwa sababu ya mumewe alipenda fedha kuliko kumpenda yeye. Na kwa kuwa hakujihadhari aliuawa kwa kukatwa katwa visu.

Unapoishi na mtu anayependa fedha kuliko kumpenda Mungu na kukupenda wewe, bila shaka uko hatarini katika nyakati za hatari, na unahitaji ufahamu ili kujinasua hapo. Kudhani kwamba upo salama ni hatari sana zaidi ya hatari inayokukabili.

Mtu mwenye kupenda fedha, ataficha kipato chake, atatumia muda mwingi kutafuta fedha bila ya kuwa na muda na wewe wa kutosha, hatatumia fedha yake kwa ajili yako lakini atataka atumie fedha yako kwa ajili yake, na ukimnyima ataitaka kwa nguvu hata kukubebea kisu atakubebea ili aipate tu.

Mtu wa namna hii inapofikia mnazungumzia fedha yake anakasirika na hali ya hewa inachafuka. Mtu huyu kila ukigusia fedha zake tu amani ndani ya nyumba inatoweka, ugomvi unaanza. Ukitaka muwe na amani, usigusie fedha yake.

1 Timotheo 6:10

[10] Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.


Kupenda fedha (love of money) ni shina la mabaya yote; kuna usaliti wa mapenzi humo, kuna ukatili na mauaji, kuna unyanyasaji, kuna uonezi n.k. Kwa sababu ya kupenda fedha wengi wamefarakana na imani na kujichoma kwa maumivu mengi.

Kwa upande wa wanandoa, fedha yako si yako mwenyewe, ni yenu wote na kwa sababu hiyo haipaswi kuwepo na siri yo yote au kufichwa kwa namna yo yote ile; fedha yote toka pande mbili iwekwe mezani na muipangie mipango kwa pamoja. Inapotokea mmoja wenu hataki fedha yake iguswe hiyo ni dalili ya kuwa, hakupendi wewe anapenda fedha yake na fedha yako au anapenda fedha kuliko wewe, na kwa hiyo siku moja ama atakuacha kwa sababu ya fedha, au atakuua, atakuumiza au kukuaibisha kwa sababu ya fedha.

Ni muhimu sasa ukawa na tahadhali mapema, ukaanza kupambana na roho hiyo ya siku za mwisho iliyomo ndani ya mume/mke wako au mchumba wako. Jamani, haya mambo si madogo, ndiyo yanayoua na kuumiza watu kila siku, na ndio matatizo yanayoondoa amani ndani ya ndoa nyingi. Unahitaji ufahamu kutambua utendaji wa roho ya siku za mwisho ili kukwepa nyakati za hatari kwa kuomba kinyume cha roho hiyo na kuikemea na inapobidi kukimbia kwa muda ili kukwepa hatari, fanya hivyo kuokoa roho yako.

Asikudanganye mtu, uhai wako ni wa muhimu sana, usiache mtu auondoe kwa jina la mapenzi eti unavumilia! Uwe na ufahamu wa kujua nyakati za hatari na kuziepuka inapofikia uhai wako upo hatarini. Kupenda fedha kumeua wengi, kumesababisha ulemavu wa maisha, kumefarakanisha ndugu na wanandoa; lakini kama tutafahamu kuwa hii ni roho ya siku za mwisho na kisha tukachukua hatua, bila shaka tutashinda.

Kwenu nyinyi ambao hamjaolewa au kuoa, usiolewe na wala kuoa mtu anayependa fedha, ni mtego, ni mwiba! Mara nyingi hawa huwa hawabadiliki mpaka mwisho. Utawajuaje? Utawajua kupitia namna walivyo ndani ya familia zao, ndani ya kanisa, na ndani ya jamii wanayoishi kwa sababu namna walivyo kwa watu wengine ndivyo watakavyokuwa kwako, namna walivyo kwa familia zao na namna walivyo kwa kanisa ndivyo watakavyokuwa kwako; ni ngumu sana kuwa tofauti kwako na namna walivyo kwa watu wengine.

Kumbuka kuwa kila nyuma ya tabia fulani moja wapo kuna roho inayopelekea tabia hiyo iwe ndani ya mtu na pia idhihirike, inaweza ikawa ni Roho ya Mungu, roho ya Shetani au roho ya mtu. Kwa hiyo tunapoona uwepo wa tabia katika maisha yetu ni muhimu tukachunguza zaidi roho iliyo nyuma ya tabia hizo. Na iwapo ni tabia mbaya, badala ya kupambanua na mtu basi tupambane na roho iliyoko nyuma ya tabia hiyo ambayo roho hiyo inakuwa imo ndani ya mtu huyo huku tukijihadhari nafsi zetu tusije tukadhurika kiroho, kinafsi na kimwili.

Mahusiano ni tabia, yanajengwa na kuimarishwa na tabia zetu, yawe ni mahusiano ya ndoa, uchumba, familia, kijamii, kikazi, kiroho nk. Mara nyingi tabia za wanaohusiana zinapoharibika mahusiano huharibika pia, kwa sababu yanaathiriwa kwa sehemu kubwa na tabia zetu ambazo kwa sehemu kubwa zinaathiriwa na roho itendayo au zitendazo kazi ndani yetu.

Katika mfululizo wa somo letu hili tumekuwa tukiangalia ndoa na roho ya siku za mwisho ambayo roho hii ikiisha kuwaingia watu kitu cha kwanza inachofanya ni kuharibu uhusiano wetu na wale tunaohusiana nao kwa kuharibu tabia zetu. Roho hii huharibu uhusiano wetu si na watu tu (wake/waume zetu, watoto wetu, wazazi wetu, rafiki zetu, jamaa zetu, jirani zetu wapendwa wetu, waumini wenzetu nk.) lakini pia zinaharibu uhusiano wetu na Mungu. Ni muhimu tukafahamu kuwa, ndoa ya kikristo ni mahusiano yanayohusisha nafsi tatu; Mungu katika utatu wake, mume na mke. Tabia ya mmoja wapo kati ya mke na mume inapoharibika, mahusiano pande zote tatu huharibika. Hii ndiyo sababu kuna umuhimu wa kujifunza somo hili. Basi sasa napenda tuendelee.


Watu Wasio na Shukrani

2 Timotheo 3:2
[2] Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,


Unaweza ukaona shukrani ni jambo dogo kabisa, lakini asikwambie mtu, shukrani inamfanya mtu anayeshukuriwa ajisikie vizuri na ya kwamba amethaminiwa katika kile alichokitenda. Shukrani ni njia ya pekee sana na inayogusa hisia za mtu inayoonyesha kujali, kuthamini, kuheshimu na kufagilia kile mtu alichotendewa. Lakini pia ni ishara ya unyenyekevu inayotoa tafsiri ya kuwa, hukustahiri kutendewa lakini umetendewa hivyo basi unaonyesha kunyenyekea zaidi katika kupokea.

Shukrani inawakilishwa na neno 'asante' ambalo husemwa likiwa limeambatana na hisia na hali anayokuwa nayo mtu inayoonyesha kuwa anaheshimu na anapokea kwa unyenyekevu wote kile alichotendewa.

Kuna msemo mmoja unaosema kuwa, "Asante ilimaliza machungwa ya Padri" unaotokana na hadithi ya watoto waliokuwa wakipita katika njia iliyokuwa karibu na nyumba ya padri huyo.

Katika nyumba ya padri huyo kulikuwa na mchungwa wenye machungwa mengi. Watoto walimuomba padri machungwa, na padri akawapa. Watoto hawa baada ya kupewa walisema asante, ndipo padri akawapa tena, nao wakamwambia asante. Waliendelea na mchezo huu mpaka machungwa yalipoisha mtini.

Kilichomfanya padri atoe tena na tena kwa furaha ni shukrani alizopewa na wale watoto wakiwa na hisia za furaha usoni mwao. Wakati wote shukrani humpa mtu nafasi ya kuona kile alichomtendea mtu mwingine ni chema, kimethaminiwa na kimepokelewa kwa heshima. Hii inampa mtendaji msukumo na nguvu ya kutenda tena na tena.

Lakini pia shukrani inaimarisha mahusiano baina ya mtu na mtu katika kutendeana mambo mema. Unapomshukuru mtu kwa tendo jema alilokutendea bila kujali ni dogo au ni kubwa mahusiano baina yenu yanaimarika kwa sababu nafsi zenu zinakuwa katika hali ya kufurahiana; huyu anafurahia shukrani alizopewa kwa tendo alilofanya, na huyu anafurahia jema alilotendewa. Kwa hiyo kila mmoja anajisikia kuthaminiwa kutokana na kile kila mmoja amefanya kwa mwenzake.

Biblia inatuambia kuwa, siku za mwisho kutakuwa na watu wasiokuwa na shukrani; hii maana yake ni kuwa, watu wanaochukulia kirahisi yale wanayofanyiwa, wanaoona kuwa si kitu saaana hata washukuru, hata uwafanyie kitu gani, kiwe kidogo au kiwe kikubwa hawatakushukuru hata kidogo; hawataonyesha moyo wa shukrani. Watu wa namna hii wanajiona kuwa wanastahili kufanyiwa mema, ni halali yao na hivyo hawana haja ya kushukuru, kuonyesha shukrani (gratitude) zao. Watu wa aina hii huvunja moyo sana na wakati mwingine huumiza kwa sababu wanaonyesha kutokujali kabisa wema na juhudi za wema za mwingine kwao.

Katika mahusiano moja ya kitu kinachoumiza ni kumfanyia mtu mambo mema alafu akachukulia kirahisi tu asitoe shukrani yo yote! Inaumiza na inavunja moyo na nguvu ya kuendelea kumtendea mtu jambo.

Watu wasio na shukrani ni watu wanaoumiza sana - hawaonyeshi kujali matendo yako, kazi zako na juhudi zako kwao. Hawathamini wala kuheshimu kile unachowafanyia na kwa sababu hiyo hata wewe watakuchukulia kirahisi sana.

Mtu asiye na shukrani ni hatari sana kwa sababu licha ya juhudi zako na bidii yako kwa ajili yake ataona hujafanya cho chote na kwa hiyo hatakushukuru na badala yake atakuonyesha kuwa hakuna ulichofanya cha maana.

Wanandoa wakikosa kuwa na shukrani kila mmoja kwa mwenzake au mmoja wao hupelekea kuwepo kwa maumivu ya ndani kwa ndani yasiyokoma lakini pia ugomvi wa mara kwa mara. Shukrani ni tendo linaloonyesha kutambua juhudi za mwingine kwa ajili yako, na wema wake kwako. Ni tendo linaloonyesha kuthamini matendo mema ya mwingine anayoyafanya kwako.

Kama nilivyotangulia kusema kutokuwa na shukrani kunavunja moyo mtu wa kukutendea mema, ndivyo ilivyo katika ndoa. Wanandoa wanapokosa kuwa na shukrani hukoma kutendeana mema, na badala yake huanza kukomeshana.

Biblia inatuagiza kuwa tuwe watu wa shukrani katika mambo madogo madogo na yale makubwa.

Wakolosai 3:15
[15]Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.


Wanandoa wanapaswa kuwa watu wa shukrani kila mmoja kwa mwenzake, lakini wanapokosa shukrani ni dalili ya kushikwa na roho ya siku za mwisho.

Jinsi ya kupambana na roho ya siku za mwisho ni wanandoa kuwa watu wa shukrani. Mnapokosa kuwa watu wa shukrani mnafungua mlango wa kushikwa na roho ya siku za mwisho.

Usione kuwa huna sababu ya kumshukuru mwenzi wako kwa kila tendo analokutendea, kwani hata yeye kukubali kuwa na wewe ni jambo la kumshukuru kwa kuwa haukustahili na hakuna cho chote unachostahili hata usimshukuru anapokustahilisha.

Ieleweke kuwa, kila mwenzi wako wa ndoa anapokutendea jambo jema maana yake huwa amekustahilisha kile kitu ambacho hukustahili; kwa hiyo mshukuru, usichukulie kirahisi.

Maisha ya ndoa ni maisha ya shukrani kwa wanandoa kila mmoja kwa mwenzake; hata mnaposhiriki tendo la ndoa, na mkamaliza, mshukuru mke/mume wako, mwambie asante na umpe busu la shukrani. Usiwe mchoyo wa shukrani, kwani haukustahili kupewa, alikuwa na sababu ya kukunyima, ila mke/mume wako amekustahilisha.

Mke amekupikia chakula, mshukuru, haukustahili kupikiwa chakula ila mke amekustahilisha! Mume wako akikuletea chakula cha kupika kwa ajili yako na familia, mshukuru kwa sababu haukustahili ila yeye amekustahilisha.

Hakuna tendo jema ambalo huna sababu ya kumshukuru mwenzi wako kila anapokutendea kwa sababu haukustahili ila amekustahilisha, hivyo mshukuru.

Watu wasio na shukrani ni wajuaji, wasaliti, wachoyo, wabinafsi na wasio na huruma. Usiwe wewe.

Watu wasiotaka kufanya suluhu

2 Timotheo 3:3
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,


Ni ngumu sana kuishi pamoja bila ya kukwaruzana, kupishana au kutofautiana na wakati mwingine kugombana kabisa pale watu wanaposhindwa kumaliza tofauti zao mapema.

Mungu akiwa anajua kabisa kuwa sisi wanadamu tu dhaifu, akatuumbia mioyo yenye uwezo wa kusamehe na kuachilia na hasa pale mtu mmoja kati ya waliokosana anapoamua kutafuta suluhu na mwenzake.

Katika maisha ya mke na mume, swala la kutofautiana au kupishana au kukwaruzana ni la kawaida maadamu tu wanaisha pamoja na wana mahusiano ya karibu. Na kwa sababu hiyo wanatakiwa wawe ni watu wenye kutaka kufanya suluhu; watu ambao wako tayari wakati wote kufanya suluhu kwa sababu wanajua kupishana, kukwaruzana au kugombana ni jambo ambalo linaweza kutokea.

Hata hivyo, Biblia inatutahadharisha kwa kinywa cha Mtume Paulo akimwandikia Timotheo kwamba, Siku za mwisho kutakuweko na watu wasiotaka kabisa kufanya suluhu; yaani mkipishana hata kama utataka mtengeneze, yeye hatataka kabisa; na badala yake ndio atakuwa anayakuza mambo. Watu wa namna hii huzua mambo baada ya mambo, visa baada ya visa ilimradi tu kusiwepo na suluhu.

Mtu asiyetaka suluhu ni mtu anayekuza mambo kila unapotaka kufanya naye suluhu, ni mtu anayevuruga mikakati au hatua zinazofanywa na watu wengine ili kufanya suluhu naye au na mtu mwingine.

Mtu wa namna hii huwa na visingizio vingi, na visababu vingi anavyovitumia ili asifanye suluhu. Ili kukuza tatizo na kulifanya liwe kubwa anaweza hata akatunga uongo na kumsingizia mwenzake ambaye wametofautiana au kupishana naye na wakati mwingine kugombana kabisa.

Mtu asiyetaka suluhu katika dalili zake za kwanza, ukimkosea atasema weee hata kama utamuomba msamaha, yeye ataendelea kukusema, na mara kwa mara atataja kosa ulilomkosea wakati uliopita, atatumia hilo kama fimbo ya kukuchapia na sababu ya kukunyima haki zako za kindoa ikiwa ni pamoja na tendo la ndoa.

Ukweli ni kwamba, tabia hii inachochewa na roho ya siku za mwisho ili kuharibu mahusiano ya kifamilia, kindoa na ya kiushirika ndani ya kanisa. Ni roho ambayo inafanya kazi ili kuwafarakanisha watu wawe na mashindano ya wao kwa wao ili mwisho wa siku wasimwone Mungu maishani mwao na waishi maisha ya uchungu dhidi ya wengine.

Ndoa ni maisha ambayo wawili hawa ambao ndio wanandoa watapishana tu, watakwaruzana tu, na watatofautiana tu kwa sababu wanaishi pamoja na wapo karibu sana; kung'ang'ania vijitofauti hivyo bila kutaka kuviachia au kivimaliza kwa kushikilia madhaifu au makosa ya mwenzako na kuyaona ni mabaya kiasi cha kwamba hafai kabisa ni dalili ya kuwa unatawaliwa na roho ya siku za mwisho ambayo ni roho za familia (familiar spirits) inayoharibu mahusiano na ushirika wa ndoa, familia na kanisa au jamii ya watu wanaoishi pamoja katika ushirika.

Ni rahisi sana kudhani ya kuwa, labda ukianzisha mahusiano na mtu mwingine yatakwenda vizuri kuliko kuendelea na huyo; hii ni mbinu ya hizo roho, hupanda mawazo kama hayo ili kukutumainisha uongo kwa kukutoa nje ya mstari (sidetrack you secretly) bila ya wewe kujua; lakini ukweli ni kwamba, hata kwa huyo mwingine utapishana naye na utakuwa mgumu kufanya suluhu.

Namna ya kupambana na roho hii ni kuomba Mungu akuumbie nia ya Kristo, akuumbie moyo wa nyama na si wa jiwe.

Lakini pia ni muhimu ukajizoesha kuomba msamaha hata kama ni wewe umekosewa, na ukajifunza kusamehe kabla ya kukosewa (forgive in advance) na kuachilia makosa kabla hujaombwa msamaha.

Jambo lingine ni vizuri ukajizoesha kusikiliza ushauri wa watu wanaokushauri kutafuta suluhu. Usisikilize daima ushauri wa watu wasiopenda kufanya suluhu, hawa watakupa ushauri ambao utakufanya uwe mzito kutafuta suluhu na mwenzi wako.

Ni muhimu ukachunguza nia ya ndani ya washauri wako; kwa nje wanaweza kuonekana wanakutakia mema lakini ndani katika nia zao wanakuchimbia shimo baya sana ili udumbukie mazima.

Kuwa na msimamo wa kutotaka kufanya suluhu kiasi cha kukataa ushauri wa pengine walezi, wazazi wako au viongozi wako wa dini (wazazi wako wa kiroho) ni dalili ya kuwa roho ya siku za mwisho imepofusha macho yako ya ndani; una macho lakini huoni na una masikio lakini husikii. Hapa ili usaidike ni lazima urudi na kutubu kwa Mungu ili akuondolee moyo wa jiwe ndani yako.

Watu Wasiojizuia

2 Timotheo 3:3
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,


Kujizuia ni moja ya nidhamu muhimu sana katika maisha ambayo kila mtu anayetaka kufanikiwa katika maisha hususani katika mahusiano anapaswa kuwa nayo. Ni tabia na nidhamu inayomwezesha mtu kutawala nafsi yake katika kutotenda mambo ambayo yanaweza kuleta hatari au madhara hasi katika maisha ya mtu.

Biblia inatutahadharisha kuwa katika siku hizi za mwisho kutakuwepo na nyakati hatari kwa sababu kutakuwepo na watu wasiojizuia.

Watu wasiojizuia ni watu waliokosa kiasi; hawana uwezo wa kujitawala wala kujizuia, watu wa namna hii ni wabaya sana katika kila eneo la maisha yao na ya wengine na hasa katika mahusiano kwa sababu ni watu hatari.

Watu wa namna hii ni wale ambao wana matumizi mabaya ya fedha kwa sababu hawawezi kujizuia au kujitawala katika matumizi yasiyo ya lazima. Hii huleta migogoro katika mahusiano.

Watu wa namna hii ni wale ambao hawawezi kuzuia wala kutawala hasira zao; wakikasirika hudhihirisha hasira yao yote kwa maneno makali ya kuumiza au kwa matendo mabaya dhidi ya watu waliowakasirikia.

Mithali 29:11
[11]Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote;
Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.


Watu wasioweza kujizuia mtakosana kidogo tu na yeye ataenda kulala nje ya nyumba au ataanza mahusiano na mtu mwingine. Watu wa namna hii watatembea na wanaume/wanawake wengi wakati wapo kwenye ndoa na wewe na watamsingizia Shetani. Hawawezi kutulia na mtu mmoja, hawazuii wala kutawala tamaa zao za mwili. Watu hawa watakuumiza kila siku.

Watu wasiojizuia wala kujitawala watakuomba tendo la ndoa kabla hamjafunga ndoa mngali wachumba; na kwa sababu wana roho ya siku za mwisho, nikuhakikishie kuwa, hawakuombi wewe tu ngono, na hata kama ukiwapa, sio kwamba wataridhika na kutulia na wewe, wakati wapo na wewe watakuwa na watu wengine wanaofanya nao ngono, kwa sababu hawawezi kujizuia wala kujitawala.

Kutaka tendo la ndoa kabla ya ndoa ni dalili kubwa inayoonyesha kuwa anayeomba tendo hilo hana uwezo wa kujizuia wala kujitawala, na yule anayekubali au anayetoa tendo la ndoa pia anakuwa naye hana uwezo wa kujizuia au kujitawala.

Tatizo la usaliti katika ndoa (uzinzi) ni matokeo ya wanandoa mmoja au wote wawili kukosa uaminifu na uwezo wa kujizuia. Vijana kufanya ngono kabla ya ndoa ni kukosa kujizuia matamanio yao. Kwa sababu ya kutokujizuia tumekuwa na kizazi cha zinaa; watu wanaingiliana kinyume cha maumbile, watu wa jinsi moja wanawakiana tamaa wao kwa wao, matumizi ya picha na video za ngono yameongezeka, wasiooa wala kuolewa wanashiriki ngono kama vile wako katika ndoa. Yaani mambo hayatendeki katika utaratibu wake mzuri wa kimaadili na watu wanaona ni sawa tu.

Mtu ambaye hana uwezo wa kujizuia ni mtu ambaye atakuacha kwa sababu ya changamoto za kimaisha. Hawezi kujizuia kukuacha, hawezi kujizuia kukutelekeza, hawezi kujizuia kukukasirikia au kukuchukia kwa sababu ameshikwa na roho ya siku za mwisho.

Ukiona mwanaume hafikirii hali ya mke wake ambaye anaumwa au anajisikia vibaya na badala yake anataka tendo la ndoa, jua kabisa huyu mwanaume ameshikwa na roho ya siku za mwisho; kwanza anajipenda mwenyewe, pili hawezi kujizuia; huyu anaweza hata kumbaka mkewe.

Ukiona mwanaume anatoka nje ya ndoa kwa sababu mkewe ni mja mzito na yupo mapumzikoni (bed rest) kwa sababu mimba iko hatarini kutoka au vinginevyo jua kuwa mwanaume huyu hawezi kujizuia, ameshikwa na roho ya siku za mwisho.

Mungu alipotuumba ndani yetu alitupa uwezo wa kujizuia na kujitawala; uwezo huu unapokosekana ndani yetu na hasa kwa wale tuliookoka ni hakika kwamba kuna roho ya namna nyingine inayofanya kazi ndani yetu ikitusukuma (influences) tufanye mambo bila ya kujizuia au kujitawala, na roho hiyo ni roho ya siku za mwisho.

Mwanamke asiyejizuia atatoka nje ya ndoa yake kwa kisingizio cha mume wake hamridhishi katika tendo la ndoa au mume wake naye anatoka nje ya ndoa; vivyo hivyo na kwa upande wa mwanaume.

Mwanamke asiyeweza kujizuia atatoka nje ya ndoa kwa sababu mumewe ameshindwa kumtimizia mahitaji yake kama anavyotaka.

Mtu ambaye hawezi kujizuia hawezi kuweka akiba ya fedha, kila akipatacho atakitumia mpaka kitaisha. Ni roho ya siku za mwisho. Ishughulikie.

Unaweza kupambana na roho hii kwa kuomba na kufunga, kujizoesha kujizuia kwa kujijengea nidhamu ya maisha kwa kujiwekea mipaka ambayo hutaivuka katika kila eneo la maisha yako. Lakini pia tumia muda mwingi kuwa na mawazo chanya kwa kutafakari zaidi matokeo mema ya muda mrefu utakayoyapata kwa kujizuia kwako kuliko raha ya muda mfupi itakayokuletea madhara au hasara ya muda mrefu.

Kujizuia kunaitunza nafsi yako na hatari lakini pia kunawahifadhi wengine unaohusiana nao na hatari inayoweza kutokea kupitia tendo lako moja ulilolifanya kwa kushindwa kujizuia. Kwa mfano, mtu mlevi (kupindukia) ni hatari kwa nafsi yake, kwa mke wake, kwa watoto wake na kwa wengine karibu yake kwa sababu ameshindwa kujizuia. Katika hali ya akili yake kutawaliwa na pombe au kilevi anaweza kusababisha madhara makubwa kwa nafsi yake au kwa familia yake na watu walio karibu yake. Mpaka anakunywa kiasi hicho ni kwa sababu ameshindwa kujizuia kutokunywa.

Watu wasingiziaji

2 Timotheo 3:3
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,


Katika Biblia ya Kiingereza (KJV) watu hawa wameitwa, "false accuser" watu wanaosingizia kwa uongo ili tu watimize matakwa yao au wakwepe majukumu yao au wafiche makosa yao au katika mkakati wa kuwakandamiza wengine.

Katika mahusiano kumekuwa na visingizio vingi vya uongo; wanandoa wengi wamejificha au wameficha dhambi zao dhidi ya wenzi wao katika visingizio.

Wasingiziaji ni watu ambao huwa na malengo yao mabaya katika kusingizia kwao. Anaweza akakuzulia jambo la uongo tu kumbe kuna kitu anataka akifanye kupitia wewe kuonekana kuwa una makosa.

Mtu aliyeshikwa na roho ya siku za mwisho, akitaka kuvunja mahusiano ya uchumba, au kukuacha au kuvunja ndoa kwa sababu tu anataka kuwa na mtu mwingine, atakusingizia mambo ambayo haukuwahi hata kuyasikia licha tu ya kuyafanya.

Mtu wa namna hii atakusingizia wewe au kuwasingizia wengine au kumsingizia Shetani ili kuficha dhambi na makosa yake yeye ionekane kuwa hajafanya au ni ajali tu na kumbe alikusudia.

Watu hawa ni waongo sana; hutunga uongo na kujificha katika huo. Atafanya kitu alafu atamsingizia mtu Mwingine. Mtu wa namna hii anaweza kuchukua fedha zake mwenyewe na kuziweka kwenye mkoba wako alafu akakusingizia wewe ndio umeiba na akakufukuza kwa sababu hiyo na kuwaambia watu amekufukuza wewe au kukuacha wewe kwa sababu wewe ni mwizi.

Ogopa sana msingiziaji; anaweza kukufunga, kukuacha, kukukosanisha na watu kwa visingizio vya uongo. Kuingia kwenye mahusiano na mtu wa namna hii ni kujichimbia shimo wewe mwenyewe.

Kama utaangalia kwa ukaribu sana, mambo haya yanahusiana na mahusiano ya mtu na mtu na mtu na Mungu, lakini kwa sehemu kubwa ni mahusiano ya mtu na mtu.

Kwa hiyo roho ya siku za mwisho ni kwa ajili ya kuharibu mahusiano ya mtu na mtu na mtu na Mungu. Ni muhimu tukawa makini sana na utendaji wa roho hizi za siku za mwisho ili tuweze kuziepuka maishani mwetu.

Tunamuhitaji Mungu, lakini pia tunahitaji kuwa ni watu wenye hekima, wapole kama hua na wajanja kama nyoka katikati ya ulimwengu huu ambao ndani yake roho ya mpinga Kristo na roho ya siku za mwisho inafanya kazi kwa kasi zaidi.

Jinsi ya kupambanua na tabia hii ya usingiziaji ni wewe kukata shauri la kuwa mkweli nafsi mwako, kwako mwenyewe na kwa wengine, na kumwombea Mungu akupe neema itakayokuwezesha kuishinda roho hii ya siku za mwisho. Lakini jambo jingine ni wewe kujaa Roho Mtakatifu na Neno la Mungu ndani yako ambalo ni kweli na ni taa na mwanga wa njia yako.

Watu wasiopenda mema

2 Timotheo 3:3
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,


Katika tafsiri ya Biblia ya King James Version (KJV) ya Kiingereza, neno "wasiopenda mema" limetafsiriwa kuwa "despiser of those that are good" yaani watu wadharau mambo yaliyo mema. Watu wasiopenda mema ni watu wanaodharau mambo yale yaliyo mema na ya kupendeza maishani.

Biblia inatuambia kuwa, siku za mwisho ambazo ndizo siku hizi tunazoishi sasa, watu watakuwa wasiopenda mema kwa maana ya watu wanaodharau mema yanayofanywa na wengine na yale ambayo wao wanapaswa kuwafanyia wengine.

Kudharau maana yake ni kuona kitu si cha maana kabisa hata kama ni cha maana kwa wengine; ni kushushia au kuondolea thamani kitu, jambo, tendo au mtu na kuona si kitu, wala si wa maana kabisa na kwa hiyo wewe huna ulazima wa kuthamini tena.

Katika siku hizi tunazoishi usishangae sana kukutana na watu wa aina hii, ambao yale mambo mema unayoyathamini wewe, wao wanayadharau kabisa na kuyabedha.

Katika ndoa, kila mwanandoa huwa ana mambo mema anayopenda kutendewa na kumtendea mwenzake. Kwa mfano utakuta mwanamke anapenda maua na vijizawadi vidogo vidogo; anapenda kupewa na mume wake na anapenda kumpa mume wake lakini utashangaa mumewe anadharau mapenzi mema ya mke wake tena wazi wazi, huu ni mfano mdogo tu.

Mwenzi wako anapenda busu, anapenda muwe na muda wa mazungumzo lakini wewe hupendi kufanya hivyo, tena unaonyesha kudharau mambo hayo kwa maneno ya kejeri, bila shaka utamuumiza mwenzi wako.

Mwenzako anapenda mahaba na huba wewe unasema hayo ni mapenzi ya kwenye tamthilia au sinema na kwa hiyo hutaki kufanya mambo hayo ya ovyo. Sasa mimi nikuulize, kuna ubaya gani? Mbona hilo ni jambo jema?

Mwenzako amejipinda kwa kadiri ya uwezo wake amekununulia labda nguo au kiatu au cho chote kile, lakini anapokupatia unaonyesha kubedha zawadi aliyokupatia.

Wewe ni mtu wa aina gani? Unamnyima mwenzako raha; unadharau kumpa pole, unadharau kumwambia asante, unadharau kumpongeza eti unaona havina ulazima kwa sababu ni maneno tu. Huko ni kutopenda mema.

Usiwe mtu ambaye unajisikia vibaya kumtendea mema mwenzi wako; kufanya hivyo ni kuvuruga amani ya ndoa au mahusiano yenu kwa sababu utakuwa umechafua hali ya furaha ya moyo wa mwenzi wako.

Biblia inatuagiza kuwa, kama kuna mema yo yote, basi tutumie muda mwingi kuyatafakari hayo. Tunapotumia muda mwingi kutafakari mema mawazoni mwetu tunajijengea ndani ya mioyo yetu hali ya kuyathamini mambo hayo na kuyapenda, na kwa sababu hiyo tunajiweka katika nafasi nzuri ya kuyatenda kwa wengine na kuyathamini tunapotendewa na wengine.

Wafilipi 4:8
[8]Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.


Watu Wakali

2 Timotheo 3:3
[3]wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

Watu wakali ni watu ambao wakati wote wana hasira na ghadhabu, hawana upole ndani yao, hudai malipizi kwa kila tendo baya wanalotendewa na hucharuka wanapoguswa kidogo bila kujali kama ni kwa wema au kwa ubaya.

Siku za mwisho pia kutakuwa na watu wakali; watu ambao kila wakati wao ni wakali tu ambao ukiwagusa kidogo tu, balaa utakayokutana nayo hujapata kukutana nayo.

Watu wakali ni wale ambao unapika chakula na unazidisha chumvi kidogo tu lakini unatukanwa na kuambiwa maneno mazito ya kukuumiza moyo au unapigwa mpaka unashindwa kusimama.

Watu wakali ni wale ambao kwa isivyo bahati umevunja wanja wake alafu anakushushia matusi kede kede kana kwamba umeua mtu kwa makusudi.

Watu wakali ni wale ambao wakati wote wamekasirika, ukiwauliza jambo au kuwaongelesha jibu watakolokujibu utatamani kwamba usingelizaliwa ili usisikie neno hilo alilokujibu.

Watu wakali ni wale ambao ukiwakosea adhabu watakayokupa inazidi kosa ulilolitenda, ni watu wanaokuadhibu kwa kila kosa unalowatenda; si wapole na hawajui kusamehe kabisa.

Watu wakali ni wale ambao wakichukizwa au wakikasirika kwa sababu ya jambo fulani, wanaanza kuvunja vunja vitu, kujipiga piga ukutani n.k. kwa hasira.

Watu wa namna hii kwa mabinti au vijana ambao hawajaoa au kuolewa wanapaswa kuwaepuka. Watu ambao wakigombana au kukasirika huwezi kuwaamua kwa sababu ni wakali; watu hawa ni hatari kwa maisha yako.

Na kwa wewe ambaye umeoa au kuolewa, watu wa namna hii ni wa kuishi nao kwa tahadhari kubwa sana, na unapohisi hatari yo yote inayohatarisha uhai wako, kimbia, jiepushe naye.

Namna ya kupambana na roho hii ni muhimu sana ukachagua kuwa mpole, mtu mwenye kuachilia makosa na mwenye kutohesabu makosa uliyotendwa. Uwe ni mtu ambaye unajizoesha kumfurahia mwenzi wako hata wakati anapokuwa amekosea na pia uombe kwa Mungu akuumbie moyo wa upole na kukuepusha na roho ya siku za mwisho. Tafuta kujaa pendo la Mungu ndani yako na uchague kuufuata upendo zaidi kuliko hisia zako. Mambo yote uyatende kwa (katika) upendo.

Site içinde arama yapın
Kategoriler
Read More
JOSHUA
Verse by verse explanation of Joshua 12
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 25 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 08:07:08 0 5K
EXODUS
Book of Exodus Explained
Exodus relates the story of freedom for God’s people from slavery and the beginning of...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-21 12:25:44 0 7K
JOB
Verse by verse explanation of Job 38
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 31 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-04-03 04:20:58 0 5K
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 2
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 43 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-01 10:35:25 0 5K
1 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 1 Chronicles 26
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 27 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-03-20 05:20:12 0 6K