SEHEMU YA 5: MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

0
5KB

Bwana asifiwe!! Unaweza kusoma SEHEMU YA 1, SEHEMU YA 2, SEHEMU YA 3, SEHEMU YA 4 ya somo hili, au unaweza kuendelea kusoma sehemu hii ya 5 uliyopo.

Ndoa ya kikristo ni sehemu nyeti kabisa ya ushuhuda wa Injili ya Kristo kwa waaminio na kwa wasio amini. Ni taasisi Mungu anayoitumia kuonyesha upendo wake kwa wanadamu na kujali kwake kwa mume kumpenda mkewe na mke kumtii mumewe. Mume amwone Kristo ndani ya mkewe kupitia matendo ya utii na upendo wa mkewe kwake, na mke amwone Kristo ndani ya mumewe kupitia upendo na upole na unyenyekevu wa mumewe kwake. Lakini pia, kupitia uhusiano na ushirika huu wa wanandoa hawa wawili familia na watu wengine wote wamwone Kristo na upendo wake kwa wanadamu. Hii ndiyo sababu leo nitakuwa nazungumzia ndoa kama kielelezo picha cha uhusiano wa kiagano kati ya Yesu na kanisa kama MISINGI WA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA. Karibu tujifunze.

MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

5. Ndoa baina ya mwanamume na mwanamke ni kielelezo picha cha uhusiano wa kiagano kati ya Yesu Kristo na kanisa lake.
Waefeso 5:22 - 33

Kama nilivyotangulia kusema kuwa, ndoa ni sehemu nyeti ya Injili ya Kristo kwa waaminio na wasioamini. Kwa sababu hiyo inapaswa ifanyike kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake kwa misingi ya ki-Mungu na si vinginevyo, wahusika wakizingatia usafi na utakatifu wa muunganiko huo ili wasije kuharibu kielelezo hicho na kusababisha kazi ya msalaba kudharauliwa.

Katika hili mke anapaswa kumtii mumewe kwa jinsi ile ile anavyomtii kristo kwa sababu mume ni kiongozi (kichwa) cha mkewe kama Kristo alivyo kichwa cha kanisa. Mume pia anapaswa ampende mkewe kwa jinsi ile ile Kristo alivyolipenda Kanisa kiasi cha kujitoa uhai wake kwa ajili yake.

Wajibu huu wa kindoa wa mume kwa mkewe na wa mke kwa mumewe ni wajibu wa lazima kwa kila mtu ambaye yupo kwenye ndoa au anatarajia kuingia kwenye ndoa. Ni wajibu ambao kwa kweli ili utimizwe mume ni lazima ajitolee kikamilifu kwa Mungu kwanza (kutunza na kulinda ushuhuda wa Injili kwa kumfuata daima Kristo) na pili ajitolee kimamilifu kumpenda mkewe kama Kristo alivyolipenda Kanisa (kumstahi, kunyenyekea, kumlinda, kumtunza na kumjali bila masharti). Kwa upande wa mke ni lazima ajitolee kikamilifu kwa Mungu (kutunza na kulinda ushuhuda wa Injili kwa kumfuata daima kristo) na ajitolee kikamilifu kumtii mume wake katika mambo yote kama kumtii Kristo bila ya masharti yo yote. Tendo hili zuri ajabu kwa wote wawili kujitolea kikamilifu kwa Mungu na kila mmoja kwa mwenzi wake ni tendo linalopaswa lifanywe kwa hiari na moyo wa kupenda na kujitolea. Iwapo mtu hayupo tayari kufanya hivyo ni vyema asiingie kwenye ndoa kwa sababu atasababisha shida kubwa kwake yeye na kwa mwenzake.

Unapoingia kwenye ndoa moja ya kazi unayokwenda kufanya ni kumwonyesha Kristo, kutunza ushuhuda wa Injili na kufanya Injili ya Kristo iwe halisi katika maisha ya mwenzi wako, familia yako na jamii ya watu wanaokuzunguka. Ni kumfanya Kristo ajulikane na aonekane kupitia maisha yenu ya ndoa. Kwa hiyo, mahusiano ya namna hii tangu kuanza kwake ni jambo la kuangalia sana na kulitunza sana kwa kuzingatia kanuni za Biblia zinataka nini.

MAMBO YA KUEPUKA ILI KUTUNZA MISINGI YA IMANI KATIKA KUHIFADHI KIELELEZO CHA KRISTO NA KANISA WAKATI WA NA BAADA YA KUANZISHA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA.

1. Epuka kuanzisha mahusiano ya uchumba na ndoa kabla ya kuwa na maarifa na ufunuo wa ndoa ya ki-Mungu na uhusiano wake na Kristo na Kanisa.

Mungu anataka tuwe na maarifa ya mapenzi yake (Warumi 12:2); na tutende mapenzi hayo (Waefeso 6:6). Ametupa Neno lake ili tupate kujua yatupasayo kutenda. Na katika neno lake hilo ametufunulia kila kitu kuhusiana na maisha yetu kwa usalama wetu. Kwa hiyo, tunapaswa tu kukubali na kutii ili kula mema ya yote tunayoyahitaji katika dunia hii (Isaya 1:19). Kufanya mambo bila ufahamu wa ki-Mungu kuhusiana na jambo husika ni kufanya bila kuwa na maarifa ya jambo hilo. Unajua ni nini matokeo yake? Ni kuangamia tu.

Hosea 4:6

[6]Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe... 


Mithali 5:11-13

[11]Nawe ukaziombolea siku zako za mwisho,
Nyama yako na mwili wako utakapoangamia;
[12]Ukasema, Jinsi nilivyochukia maonyo,
Na moyo wangu ukadharau kukemewa;
[13]Wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu,
Wala sikuwategea sikio langu walionifundisha!


Unapokataa mafundisho unakataa maarifa (Mithali 12:1). Kujiepusha na maangamizo sharti upende mafundisho na uyaishi mafundisho hayo ambayo ni neno la Mungu.

Biblia imezungumzia mengi kuhusu ndoa, na yenyewe ndio maarifa sahihi na imebeba ufunuo wa kweli kuhusu ndoa. Usijifunze maarifa mengine nje ya Biblia au yasiyokuwa na msingi wake katika Biblia kuhusu ndoa. Biblia ndio iwe chanzo chako cha maarifa na msingi wa ufunuo wako kuhusu ndoa. Kabla ya kuingia kwenye ndoa elewa kwanza ndoa ni nini, chanzo chake, kusudi la kuwepo kwake, mapenzi ya Mungu kuhusiana na ndoa na kwa nini unaoa au kuolewa. Yote haya utayapata ndani ya Biblia (neno la Mungu).

2. Epuka kuanzisha mahusiano kabla ya kujua wajibu na jukumu la utii la mke kwa mumewe na jukumu la upendo la mume kwa mkewe.

Hii inahusisha utayari wa kupoteza haki zako na uhalali wako wa mambo fulani toka kwa mwenzi wako katika kutekeleza wajibu wako wa kinda. Kabla hujakubali kupoteza usiingie kwenye ndoa - hii ni pamoja na kupoteza umiliki wa mwili wako, nafsi yako, muda wako, heshima yako, na uzuri wako. Ili awe wako ni sharti kwanza wewe uwe wake kabisa kabisa. Kama hutaki kupoteza huwezi kumpata kikamilifu - utampata tu utakapokubali kupoteza.

Kuwa na ndoa nzuri unapaswa kutekeleza wajibu wako bila masharti. Hautekelezi wajibu wako kwa masharti au kupata haki yako kwanza. Unatekeleza wajibu wako bila ya masharti na hata kama ukiwa haujapata haki yako kwa mwenzi wako. Haitoshi tu kujua wajibu wako kwa mwenzi wako, ukijua basi utende. Haitakusaidia sana kujua wajibu wa mwenzi wako kwako na kumlazimisha akutekelezee kama ambavyo haitakusaidia wewe kujua wajibu wako kwa mwenzi wako na usimtendee. Yo yote mtakayo kutendewa watendeeni wengine yayo hayo.

Yohana 13:17

[17]Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.


Katika ndoa kujua ni pamoja na kutenda. Ndoa ni uhusiano wa kumtendea mwenzako matendo mema ya upendo na utii unayotaka kutendewa. Kwa hiyo, kabla ya kuoa au kuolewa jua kwanza wajibu wako wa ndoa kwa mwezi wako na uwe tayari kuutekeleza kwa kujitolea na kikamilifu wakati wote.

3. Epuka kuanzisha mahusiano nje ya imani na mtu asiyeamini vinginevyo wewe mwenyewe uwe umeikana imani.

Hili tumelizungumzia kwa kina katika somo la kwanza. Kusoma somo hili bofya
Sehemu ya Kwanza - MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

4. Epuka ushirika wa kingono kwa matumizi yasiyo ya asili ndani ya ndoa yenu.

Licha ya kuwa kufanya ngono kinyume cha asili ya maumbile kumekatazwa na Biblia pia ni kukiuka uhusiano wa Yesu Kristo na kanisa lake. Na hii ni kuitukana na kuikanyaga chini Injili ya Kristo. Biblia inasema kuwa kanisa ni bibi harusi wa Kristo na Kristo ndiye Bwana harusi wa kanisa. Hii inaonyesha kuwa jinsi na jinsia zimezingatiwa katika mahusiano ya ndoa, lakini pia viungo vya mwili kwa matumizi ya asili. Hoja hii tutaiangalia kwa kila hapo mbeleni katika somo lingine.

5. Epuka ngono kabla ya ndoa.
Hoja hii pia tumeiangalia kwa kina katika somo lililopita. Bofya hapa chini kusoma:
Sehemu ya Pili - MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

NINI KINATOKEA UNAPOANZISHA MAHUSIANO BILA YA KUTUNZA KIELELEZO CHA YESU NA KANISA.

1. Unaharibu ushuhuda wa Kristo Yesu mbele ya waaminio na wasioamini.
Ushuhuda wa Yesu Kristo ni kitu cha kutunza kwa wivu mkubwa. Kuenenda kinyume cha neno lake na kuendesha mahusiano kwa kukiuka kanuni za Biblia ni njia ya kuharibu ushuhuda wa Kristo. Kipaumbele kikuu kwenye mahusiano ya ndoa ya kikristo iwe ni kutunza ushuhuda wa Kristo Yesu.

2. Unakosa baraka za Kristo na Roho wake pamoja na uwepo wao katika ndoa yenu.
Baraka za Kristo na Roho wake zipo katika kanuni ya kutii neno lake. Kama unakiuka neno lake kwa kuishi kama upendavyo wewe, kwa kweli, huwezi kuona baraka hizo. Kuikubali na kutii utakula mema ya nchi, lakini ukikataa utaangamia. Ni hivyo na haiwezi kubadilika. Tumeitwa si tu kuiamini Injili lakini pia kuitii Injili kwa gharama yo yote ili tuzione baraka zitokanazo na Injili hiyo.

3. Kanisa linakuwa halina furaha na wewe, na Mungu pia.
Kama unaishi kinyume cha ushuhuda wa Kristo na kanisa limekuonya lakini hutaki kutii, kanisa haliwezi kukufurahia na kwa hiyo Mungu pia. Unakuwa unaishi maisha ya kumuhuzunisha Roho na kulihuzunisha kanisa.

Mpendwa, kielelezo cha Yesu Kristo na kanisa lake (ndoa) lazima kitunzwe kwa wivu mkubwa kwa sababu kimebeba ujumbe wa Injili kwa watu wote wanaoitazama ndoa. Hiki ni kipawa na zawadi toka kwa Mungu, ni talanta ambayo mwisho wa siku tutaitolea hesabu kwa Mungu mwenyewe. Itunze!

Rechercher
Catégories
Lire la suite
JOB
Verse by verse explanation of Job 23
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 24 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-04-03 03:53:56 0 5KB
1 KINGS
Verse by verse explanation of 1 Kings 10
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-02-05 13:05:59 0 6KB
RUTH
Verse by verse explanation of Ruth 4
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-01-25 11:31:04 0 6KB
Injili Ya Yesu Kristo
ROHO MTAKATIFU
Ndugu msomaji; Je, unamfahamu Roho Mtakatifu? Je, Roho Mtakatifu ni nani kwako?   Katika...
Par MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 19:33:29 0 5KB
PSALMS
Verse by verse explanation of Psalm 5
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 42 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-04-04 23:02:55 0 5KB