KARIBU SANA KATIKA MDAHALO WETU:
UTANGULIZI: Biblia inatufundisha kuwa Mungu ni mwema (Zaburi 106:1) tena huwa anatuwazia mawazo mema na ya amani tena ni mawazo ya kutupatia tumaini siku zetu za mwisho(Yeremia 29:11). Ndio maana lengo lake hasa la uumbaji lilikuwa ni kutengeneza koloni lingine la mbinguni (Dunia), na katika koloni hili amuweke mwanadamu awe kiongozi (Gavana) wa koloni hili. Ukisoma mwanzo 1:1-31) utaona kuwa Mungu aliandaa mazingira bora sana ili huyu mwanadamu aishi maisha mazuri na ya furaha tena ya kifalme (akiwa mtawala). Mwanzo 5:1-2 na Mwanzo 1:27, inaonyesha wazi kuwa hapo Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke katika siku moja (i.e. tukio hili lilifanyika katika ulimwengu wa roho), tena akawabariki na akawaita jina lao Adamu, ndio sijakosea ndugu, Mungu aliwaita wote Adamu. Hivyo mbele za Mungu roho ya mwanaume na ya mwanamke zina thamani sawa, maana wote hawa ni jina lao ni Adamu.
Lakini ukisoma katika Mwanzo 2:7 utaona kuwa, aliyetangulizwa katika ulimwengu huu wa mwili alikuwa ni mwanamume, ambapo Mungu alichukua udongo akaufinyanga na kumtengeneza mwanaume huyu kisha akampulizia pumzi ya uhai puani mwake, na mwanaume yule akawa nafsi hai. Baadaye Mungu akampa maagizo mwanaume huyu kuwa anaweza kula matunda yote ya miti katika bustani ya Edeni kasoro tu matunda ya mti ujuzi wa mema na mabaya asiyale, kwa maana siku atakayokula atakufa (Mwanzo 2:16). Pia tunaona katika Mwanzo 2:18-25, kuwa baadaye tunaona Adamu alikuwa mpweke sana kiasi kwamba Mungu akaona kuwa sio vema mwanaume yule aendelee kubaki peke yake, hivyo Mungu akampatia Adamu usingizi na akautoa ubavu mmoja wa Adamu akamtengeneza mwanamke na akamleta kwa Adamu. Adamu alifurahi sana kumpata mwanamke huyu na upweke wake ukaisha.
Mwisho katika Mwanzo 3:1-24, tunaona Nyoka akimdanga mwanamke (Hawa), naye akamuasi Mungu kwa kuamua kuyala matunda yale waliyokatazwa na Mungu kuwa wasiyale, tena akachukua baadhi ya matunda yale akampelekea mumewe (Adamu) naye akayala. Baadaye Mungu alipowaweka kwenye baraza ili wajibu mashtaka yao, hakuna hata mmoja aliyekubali kosa wala kutubu, bali wote wawili walikana makosa yao huku wakitupa lawama kwa wengine (i.e. Mfano Adamu alitupa lawama zake kwa mkewe, huku Hawa akitupa lawama zake kwa Nyoka). Mungu alichukia sana, na ndipo akawapa wale wazazi wetu (Adamu na Hawa). adhabu nyingi zifuatazo:
- Wote watakufa
- Uadui kati ya mwanadamu na Nyoka
- Mwanaume atakula kwa jasho
- Mwanamke atazaa kwa uchungu
- Mwanamke atatawaliwa na mumewe
Baadae Mungu akawafukuza Adamu na Hawa watoke bustanini Edeni, na akaweka malaika wawili ili kuilinda bustani ya Edeni. Huu ndio ukawa mwanzo wa mwanadamu kuishi maisha magumu, mabaya, yaliyojaa dhiki, laana, magonjwa na matatizo ya kila namna, yaani matatizo yale yanayoonekana na hata matatizo yale yasiyoonekana.
SWALI: Kwa ugumu huu wa maisha, nani alaumiwe zaidi kati ya Adamu na Hawa?
MASHARTI
- Huu ni mdahalo (Debate), hivyo ni lazima uchague upande mmoja wa kuutetea, aidha upande unaosema kuwa Adamu ndiye anayepaswa kulaumiwa zaidi (TIMU EVA) au upande unaosema kuwa Hawa/Eva ndiye anayepaswa kulaumiwa zaidi (TIMU ADAMU). Na kila utakapochangia ni lazima uanze kutukumbusha Timu yako.
- Sio lazima uwe mwanaume ndio uwe timu Adamu, unaweza ukawa mwanamke na ukawa timu Adamu. Pia sio lazima uwe mwanamke ndio uwe timu Hawa, unaweza ukawa mwanaume na ukawa timu Hawa.
KARIBU SANA TUANZE MJADALA WETU.