KARIBU SANA KATIKA MDAHALO WETU:
UTANGULIZI: Katika kitabu cha Mithali 18:22, Biblia inasema kuwa, “Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa Bwana. Hivyo mke ni kitu chema kutoka kwa MUNGU”. Lakini pia ukisoma Biblia kwa kina utaona kuwa hata Ruthu naye alipopata mume bora na tajiri aliyeitwa Boazi ndipo historia ya maisha yake ikawa nzuri, maana alitoka kuwa masikini akawa tajiri, tena mpaka akapata nafasi ya kuingia katika ukoo wa Yesu Kristo (Ruth 4:9-22 na Mathayo 1:1-17). HIVYO NI WAZI KUWA BIBLIA INARUHUSU KUOA NA KUOLEWA.
Pamoja na hayo, katika kitabu cha 1 Wakorintho 7:7-8 tunaona mtume Paulo, kwa uongozi wa Roho Mtakatifu akisema kuwa, “7 ila nipendalo ni kwamba watu wote wawe kama mimi nilivyo; walakini kila mtu ana karama yake mwenyewe itokayo kwa Mungu, huyu hivi, na huyu hivi. 8Lakini nawaambia wale wasiooa bado, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo”. HIVYO PIA NI WAZI KUWA BIBLIA INARUHUSU PIA KUTOKUOA AU KUTOKUOLEWA.
MADA YETU NI HII:
Ingawa ni kweli kuwa inawezekana kabisa kumtumikia Mungu ukiwa kwenye ndoa au hata ukiwa hauna ndoa, lakini je, kwa mtazamo wako unaona kuwa wapi ni rahisi zaidi na penye uhuru wa kumtumikia Mungu kwa nguvu zote ili uweze kupata taji ing’aayo mbinguni, je, ni ukiwa kwenye ndoa (yaani ukiwa umeoa au umeolewa) ama ukiwa hauna ndoa (yaani ukiwa hujaoa au kuolewa)?
ANGALIZO:
(1). Huu ni mdahalo (Debate), hivyo ni lazima uchague upande mmoja wa kuutetea, aidha upande wa ndoa (TIMU SULEMANI) au upande wa kutokuwa na ndoa (TIMU PAULO). Na kila utakapochangia ni lazima uanze kutukumbusha Timu yako.
- Ukiwa Timu Sulemani: utakuwa unatetea kuwa, ukiwa ndani ya ndoa (yaani ukiwa umeoa au kuolewa), ndio rahisi zaidi kumtumikia Mungu tena kwa uhuru kiasi cha kupata taji ing’aayo.
- Ukiwa Timu Paulo: utakuwa unatetea kuwa, ukiwa hauna ndoa (yaani ukiwa haujaoa au kuolewa), ndio rahisi zaidi kumtumikia Mungu tena kwa uhuru kiasi cha kupata taji ing’aayo.
(2). Haijalishi hali yako ya sasa ya ndoa, upo huru kuchagua upande wowote ule upendao, kwa mfano:
- Sio lazima uwe ndani ya ndoa ndio uwe Timu Sulemani, unaweza ukawa bado haujaoa au hujaolewa lakini ukaamua kutetea Timu Sulemani.
- Pia sio lazima uwe hauna ndoa ndio uwe Timu Paulo, unaweza ukawa umeoa au umeolewa lakini ukaamua kutetea Timu Paulo.
(3). Mjadala huu ni kwa ajili ya kupanua tu uelewa wa neno la MUNGU.
- Hivyo hata ukiwa Timu Sulemani haimaanishi kuwa unalo wazo la kuja kuingia katika ndoa hapo baadae, hii ni hiari ya mtu kadri Roho wa Bwana anavyomjalia.
- Pia hata ukiwa timu Paulo haimaanishi kuwa unalo wazo la kutokuingia katika ndoa, hii ni hiari ya mtu kadri Roho wa Bwana anavyomjalia.
KARIBU SANA TUANZE MJADALA WETU.