NAMNA MWANAMKE ANAVYOWEZA KUTUMIA NAFASI ZAKE KUBADILISHA MAISHA YA NDOA YAKE

0
8K

Mithali 14: 1 ‘Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’.

Mchungaji mmoja rafiki yangu aliniambia asilimia hamsini mpaka sabini ya changamoto au matatizo anayoshughulika nayo mara kwa mara katika kanisa lake ni ya wanandoa. Kwa lugha nyepesi asilimia 50 – 70 ni matatizo yatokanayo au yanayohusiana na ndoa. Binafsi pia kwa upande wangu kupitia nafasi yangu katika mwili wa Kristo, email za wasomaji ninazopata na pia baadhi ya semina za ndoa ambazo nimefanya kuhusu eneo hili nimegundua kwa hakika ndoa nyingi za wana wa Mungu zina shida na wao hawajajua kwamba vita hii inatoka kwa Shetani, maana anajua ndoa zikitengamaa ni faida kwa ufalme wa Mungu na ni uharibifu kwenye ufalme wake wa giza. Naam anapigana usiku na mchana ili kuhakikisha ndoa hazitengamai kwa kuleta fujo za kila aina.

Kila siku katika ndoa kuna changamoto zinazaliwa mpaka imefika mahala baadhi ya wanandoa wanawaza kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Kwa hakika laiti Biblia ingetoa mwanya kwa wanandoa kuachana basi kuna baadhi ya wanandoa wangehakikisha wanaitumia hiyo nafasi vizuri kwa kuwa ndoa zimegeuka ndoano. Matarajio ambayo kila mmoja alikuwa nayo kwenye ndoa anaona hayatimii. Kinachosumbua watu wengi ni kwamba kabla hawajaonana hawakujua nini kinakuja kupitia ndoa, hawakuweza kuona uhalisia wa maisha ya ndoa utakuwaje? Bali kila mmoja alikuwa na mtazamo/fikra na matarajio yake binafsi juu ya ndoa yake.

Naam zipo sababu nyingi sana zinazopelekea matatizo au changamoto kwa wanandoa. Katika somo hili nitaandika zaidi zile zinazotokana na upinzani kutoka kwa Shetani ili kuathiri kusudi la Mungu. Lengo la ujumbe huu ni kukufundisha wewe mama (Mwanandoa) namna ya kuzitumia ‘nafasi’ ambazo Mungu amekupa Kibiblia ili kuiponya ndoa yako au kubadilisha hali ya sasa ya ndoa yako endapo unaona si ile ambayo Mungu amekusudia.

Kwa nini Mwanamke?

Pengine utaniuliza kwa nini mwanamke ndiye awajibike katika kuponya au kubadilisha maisha ya ndoa yake? Binafsi katika kuisoma Biblia nimegundua kwamba kwa kuzingatia nafasi ambazo mwanamke amepewa kibiblia ni ishara ya kwamba kwa habari ya  ndoa, Mwanamke ana nafasi kubwa ya kuijenga au kuibomoa ndoa yake na hivyo nyumba yake kwa ujumla. Mara kwa mara Mungu ananifundisha masuala ya wanawake, suala la wanawake kuwa kwenye ‘nafasi zao’ husisitizwa sana.

Kwa nini nafasi?

Sijui kama unafahamu maana ya nafasi ambayo Mungu anampa mtu katika ulimwengu wa roho. Hizi ni nafasi ambazo Mungu amekupa wewe mawanamke katika ulimwengu wa roho ili uzitumie kufanikisha kusudi lake kupitia ndoa yako. Nafasi (position) ni eneo ambalo mtu anapaswa kuwepo kwa kuhusianisha na vitu au watu wengine, naam ni wadhifa ambao mtu anakuwa nao kwa kuhusianisha na mtu au watu wengine.

Kwa hiyo hizi ni nafasi ambazo Mungu amempa mwanamke zikihusiana na mwanaume katika kilitumika kusudi la Mungu hapa duniani. Mwanamke anapokuwa amesimama katika nafasi zake ndipo anapoweza kuruhusu mawazo ya Mungu kupitia ndoa yake kutimia naam ndivyo anavyoweza kuzuia mawazo ya Iblisi kupitia ndoa yake yasitimie. Naam nafasi ya mwanamke katika ndoa ndiyo inayoamua uzima au mauti ya ndoa yake, nafasi ndiyo inayopelekea kufanikiwa au kufeli kwa ndoa yake, nafasi ya mwanamke katika ndoa ndio inayoamua nini kingie au kitoke kwenye ndoa.

Katika kusoma kwangu Biblia nimegundua kwamba Mungu amempa nafasi zifuatazo mwanamke;

  • Mwanamke kama ‘msaidizi’ wa mumewe
  • Mwanamke kama ‘mlinzi’ wa mwanaume
  • Mwanamke kama ‘mjenzi’ wa nyumba yake
  • Mwanamke kama ‘mshauri’ wa mumewe
  • Mwanamke kama ‘mleta kibali’ kwa mumewe

Naam kutokana na changamoto zinazoendelea katika ndoa mbalimbali nimelazimika kuanza kuandaa mfululizo huu wa namna mwanamke anavyoweza kusimama kwenye nafasi zake na kuiponya ndoa yake. Jukumu langu kubwa itakuwa ni kufafanua kila nafasi ambayo mwanamke amepewa na namna anavyoweza kuitumia hiyo nafasi kubadilisha ndoa yake ambayo anaona inaangamia.

 

Mwanamke kama Msaidizi

Mwanzo 2:18 ‘BWANA Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye’.  Ukisoma mstari huu katika toleo la GNB Biblia inasema ‘Then the LORD God said, “It is not good for the man to live alone. I will make a suitable companion to help him.” Biblia inatueleza kwamba Adam ndiye aliyetangulia kwanza kudhihirishwa kabla ya Mwanamke. Kabla ya Hawa kuletwa, Mungu alimpa Adam majukumu mengi ambayo alipaswa kuyatekeleza.

Katika kutekeleza majukumu yake Adam aliona kwamba amepungukiwa mwenza wa kufafanana naye na ndani yake akatamani angepata mtu wa kuwa naye karibu kwa kila afanyalo. Ukweli huu tunaupata tukisoma Mwanzo 2:20 kwamba ‘Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. Naam kutokana na upweke wa Adam ndipo Mungu akamfanya Hawa mkewe kama msaidizi. Kitendo cha Mungu kumfanya mwanamke kama msaidizi ni ishara kwamba Mungu alijua kuwa Adam hawezi kuwa na ufanisi mzuri katika kutekeleza majukumu (Kusudi) aliyopewa bila mwenza wa kufanana naye.

 

Maandiko yanasema kwamba ‘Maana mwanaume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanaume. Wala mwanaume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanaume’ (1Wakorinto 11:8-9).  Ile kwamba mwanamke aliumbwa kutoka kwa mwanaume na kwa ajili ya mwanaume ni kuonyesha kwamba wajibu au nafasi mojawapo ya mwanamke ni kuwa msaidizi wa mumewe. Hata hivyo neno msaidizi halipaswi kutafsiriwa vibaya na kuonyesha kwamba mwanamke hana thamani.

Mwanamke ni msaidizi wa mume katika kulitumikia kusudi la Mungu isipokuwa kinacho watofautisha ni utendaji wao tu. Mume hapaswi kumdharau mkewe wala mke kumdharau mumewe kwa kuwa mume si mume bila mke na mke si mke bila mume, wao ni mwili mmoja, kusudi lao ni moja na BWANA wao ni mmoja.   Maandiko yafuatayo yanaonyesha baadhi ya mambo ambayo mwanamke anapokuwa katika nafasi ya Msaidizi anapaswa kuyafanya;

Tito 2:4 inasema ‘Ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’.

1 Timotheo 5: 14 ‘Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, wawe na madaraka ya nyumbani; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu’. Ukisoma pia katika 1 Wakorinto7:4a kwa habari ya tendo la ndoa Biblia inasema ‘Mke hana amri juu ya mwili wake…’ na mstari wa 5a unasema’ Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda…, Naam hii ina maana kama mke ataweka amri kwa habari ya tendo la ndoa kwa mumewe ajue kabisa ameshindwa kumsaidia mumewe na kuna hatari ya kuanguka kwenye zinaa. Naam Mungu anataka akina mama walioko kwenye ndoa wajifunze kuwasaida waume zao wasiingie kwenye zinaa.

Naam hata sasa ni muhimu sana wewe mama ukajua Mungu amewaunganisha ili kufanya nini hapa duniani kwa ajili ya ufalme wake. Changamoto kubwa iliyipo leo ni kwamba wanandoa wengi wameingia kwenye ndoa kwa sababu ni desturi ya wanadamu kuoa na kuolewa. Wengi wameshindwa kuunganisaha suala la kuoa au kuolewa na kumtumikia Mungu kupitia ndoa yao. Mungu anapokuunganisha na mumeo maana yake anakupeleka kwenye wajibu wa kuwa msaidizi kwa mumeo. Naam hakikisha kwamba unafanyika msaada kwa mumeo kwa namna ambayo kile ambacho mnajua kwamba Mungu amewapa kukifanya hapa duniani kinafanikiwa. Zaidi unaweza soma Mithali 31:10-31 ili kuongeza ufahamu zaidi kuhusu nafasi ya mwanamke kama Msaidizi.

Mwanamke kama Mshauri

Katika hali ya kawaida watu wengi hutafsiri mshauri kuwa msiaidizi. Kwa kuzingatia dhana ya nafasi katika ulimwengu wa roho imenilazimu kutenganisha ili kukuonyesha umuhimu wa nafasi ya mwanamke kama Mshauri. Biblia katika Mithali 31:26 inasema ‘Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake’.

Naam andiko hili linatupa kujua kwamba Mke ndiye mshauri mkuu wa mumewe. Siri moja ya mwanamke kuwa mshauri mzuri ni kuwa na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu. Hivyo kama Mke hana hekima itokanayo na neno la Mungu kwa wingi ndani yake, hawezi kuwa mshauri mzuri. Ushauri unategemea nguvu za ufahamu alizonazo Mwanamke, kadri anavyokuwa na ufahamu wa kutosha wa neno ndivyo anavyokuwa kwenye nafasi ya kutoa ushauri bora kwa mumewe.

Biblia katika kitabu cha Mithali 8: 14-16 inasema ‘Shauri ni langu, na maarifa yaliyo sahihi; Mimi ni ufahamu na mimi nina nguvu. Kwa masada wangu wafalme humiliki, Na wakuu wanahukumu haki. Kwa msaada wangu wakuu hutawala, Na waungwana, naam, waamuzi wote wa dunia’. Fahamu kwamba hekima ndani yako mama itakupa maarifa na ufahamu wa kumshauri mumeo ili kufanya maamuzi sahihi katika kila atendalo. Hekima ni sawasawa na   shauri/maarifa/ufahamu/nguvu. Ukiona kiongozi yoyote anatawala/anaongoza watu vizuri ujue washauri wake wanamshauri vizuri au ujue ana wahsauri wazuri. Vivyo hivyo mwanaume anafanya kazi zake vema na kufanikiwa katika yale atendayo ujue nyuma yake kuna mwanamke mwenye nguvu za ufahamu anayemshauri vema.

Naam chanagmoto au matatizo mengi yaliyopo kwenye ndoa leo ni matokeo ya akina mama kukosa hekima itokanayo na neno la Mungu ya kuwashauri waume zao. Wengi wanategemea akili zao, au ushauri wa rafiki zao nk. katika kuangalia ndoa zao na mambo yao yaendaje. Kutegemea ushauri wa watu wengine bila wewe mwenyewe mama kutafuta hekima itokanyo na Mungu kwanza inaweza kukufikisha kupata ushauri wa kipepo kama ilivyomtokea Hawa pale Bustanini. Kumbuka Mshauri ni mtoa taarifa, mtoa pendekezo juu ya nini mume wake aweza fanya au kutofanya.

Mwanamke kama mleta kibali.

Hii ni nafasi ya ajabu sana ambayo Mungu amempa mwanamke. Mwanamke anapokuwa kwenye hii nafasi mambo matatu yanafanyika; 1) Mume anaingia kwenye ngazi ya kushirikishwa siri/mambo/majukumu mengi kutoka kwa BWANA. 2) Kukubalika kwa mume wake katika jamiii/kazi/kanisa nk kunaongezeka 3) Na mwisho maombi ya mume wake yanasikilizwa. Mambo haya yanathibitishwa na Biblia katika  Mithali 18:22 inayosema ‘Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA’, pia   Mithali 31: 23 inayosema ‘Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi’

Zaidi kwa habari ya maombi ya mume kusikilizwa au kutokusikilizwa Biblia katika      1 Petro 3:7 inasema ‘Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe’. Naam hii ni ishara kwamba mke anaweza kusababisha maombi ya mumewe yakasikilizwa au yasisikilzwe. Unaweza ukafikiri hili andiko linawahusu akina baba pekee, lakini ukilitafakari kwa upana utagundua kwamba linawahusu akina mama pia ili wajue kwamba kuwa mke ni nafasi ambayo inaweza kuzuia maombi/baraka/majibu au kukwamisha mafanikio ya waume zao kama hawatukuwa makini katika kuwasaidia waume zao kuishi nao kwa akili.

Si wengi wanaojua kwamba kuna maombi mengi ya familia/waume zao hayajibiwi kwa sababu maombi ya mume ambaye ndiye kichwa hayasikilizwi na Mungu. Na chanzo cha kutokusikilizwa ni kuharibika kwa uhusiano kati ya mume na ‘mleta kibali’ wake yaani mke. Hivyo wewe mama mwenye ufahamu huu jifunze kwenda mbele za Mungu na kuomba toba kwa ajili ya mumeo mara kwa mara. Kwa sababu kuna vitu au maamuzi anayoweza kufanya nay eye akaona yuko sahihi lakini kumbe ni uamuzi ambao unajenga ukuta kati ya maombi yake na Mungu wako.

Hakikisha unasimama vema kwenye hii nafasi ili Mungu alete uponyaji kwa mume wako na maombi yake yaweze kusikilizwa. Naam simama kwenye nafasi yako ili kumjengea mazingira mazuri mumeo ya kuishi na wewe, ndivyo na maombi yake yatakavyosikilizwa, ndivyo atakavyopata kibali mbele za BWANA, naam atakuwa mume bora katika jamii na kufanikiwa katika kila atendalo.

Tamati endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye nafasi hizi haijalishi mume wake ni mgumu kiasi gani, mama akizungumza kwa maana ya maonyo au ushauri lazima mwanaume asikilize au kufuata kile ambacho msaidizi, mlinzi, mleta kibali wake nk anamweleza, na kama akikataa uharibifu ni haki yake. Mungu ameweka sauti ndani ya mwanamke ambayo inaweza kuleta uponyaji kwa mumewe endapo mwanamke atakaa vizuri kwenye hizi nafasi.

Labda nianze kwa kuuliza, je una fahamu kwamba wajibu wa kumlinda mumeo ni wako? Naam Mungu amejiwekea utaratibu mpya kwamba Mwanamke amlinde mwanaume. Je ni ulinzi wa namna gani? Ni ulinzi wa kiroho ndio ambao mwanaume anahitaji kutoka kwa mkewe. Mke anatakiwa kuwa makini ‘sensitive’ katika ulimwengu wa roho kuangalia ni mashambulizi gani Shetani amekusudia kuyaleta kwa mume/ndoa yake. Naam akishajua aweke ulinzi ili mawazo ya Shetani yasitimie kwenye ndoa yake.

Kuwa Mke wa fulani, ni nafasi ya ulinzi katika ulimwengu wa roho ambayo Mungu anaitoa. Kwa hiyo fahamu kwamba unapoingia kwenye ndoa, Mungu anakupa wajibu wa kumlinda mumeo. Biblia katika Yeremia 31:22 inasema ‘Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume. Nafasi ya ulinzi ni nafasi ya pekee sana ambayo Mwanamke amepewa na endapo ataitumia vizuri itamsaidia kweli kweli kuiponya ndoa yake. Hii ni kwa sababu mlinzi ndiye anayeona mambo yanayotaka kuja kwenye ndoa yake akali kwenye ulimwengu wa roho, kabla hayajadhihirika kwenye ulimwengu wa mwili.

 

Ukisoma Mstari huu wa Yeremia 31:22 katika toleo la kiingereza la ESV unasema ‘How long will you waver, O faithless daughter? For the LORD has created a new thing on the earth: a woman encircles a man’ na pia katika toleo la KJV imeandikwa ‘How long wilt thou go about, O thou backsliding daughter? for the LORD hath created a new thing in the earth, A woman shall compass a man’. Maneno ‘Mwanamke atamlinda mumewe’ kwenye ESV imeandikwa ‘a woman encircles a man’ na kwenye KJV imeandikwa ‘A woman shall compass a man’. Maneno haya yana maana ya zingira, zunguka au fanya duara.

Hapa Biblia inajaribu kutueleza jambo la mwanamke ambaye yamkini kutokana na changamoto za ndoa yake/mume wake alijikuta amekuwa mtu wa kuasi/kufanya mabaya. Sasa ili kumsaidia ndipo BWANA akamtuma Yeremia kumweleza ‘acha kutanga tanga, Mungu ameumba jambo jipya nalo ni ‘wewe mwanamke, umepewa wajibu wa kumlinda/kumzingira mwanaume/mumeo’. Naam ulinzi huu ni kwa jinsi ya rohoni. Mwanamke anaweza kumwekea/kumfanyia mume wake ulinzi dhidi ya makahaba, malaya, wenye hila, wala rushwa au chochote ambacho ni chanzo cha uharibifu wa ndoa nk.

Katika nafasi hii ya ulinzi Mke una wajibu wa kujua kwa nini Mungu amekuunganisha na mume uliye naye sasa. Naam lipo kusudi la ufalme wake, hivyo ni jukumu lako   kuhakikisha linatimia katika siku zenu za kuwepo hapa duniani kama wanandoa. Naam msaidie Mume wako kama Mlinzi kwa namna ambayo kusudi la Mungu halitakwama kwenye maisha yenu. Fahamu kazi ya Mlinzi ni kumsaidia Bwana wake kufanikisha majukumu yake. Endapo Mlinzi hatakuwa makini kwenye nafasi yake basi majukumu ya Bwana wake hayatafanikiwa, si kwa sababu ametaka bali ni kwa sababu Mlinzi/Walinzi wake hawakumpa usaidizi wa kutosha kiulinzi.

Ni vizuri ukafahamu kwamba ili Shetani ammalize mumeo, njia kuu kwake ni kupitia kwa mkewe. Angalia leo ndoa ngapi zimeharibika na ukifuatilia chanzo utagundua Mke amechangia kwa sehemu kubwa. Hebu taunaglie mifano kadhaa ndani ya Biblia;

 Ndoa ya Anania na Safira (Matendo ya Mitume 5:1-11).

Ule msitari wa 1-2 maandiko yanasema ‘Lakini Mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali, akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume’.  Ukisoma fungu zima hapo juu utagundua kwamba kutokana na wizi wao wote wawili, walikufa siku moja. Jambo ninalotaka tulione hapa ni ile kusema ‘mkewe naye akijua haya’. Maneno haya yameandikwa ili kuonyesha namna ambavyo Safira hakutumia nafasi yake kuiponya ndoa yake. Kutokana na kutokumshauri mumewe vizuri na kumlinda dhidi ya hatari iliyokuwa mbele yao, wote wawili walikufa. Nani ajuae kwamba pengine Safira angemwonya mumewe, mumewe angemsikiliza. Naam kwa kuwa alinyamaza, na Mungu alinyamaza, mauti ikawajia.

Ndoa Ahabu na Yezebeli (1Wafalme 21:1-23)

Ukisoma andiko hili utaona namna Yezebeli mke wa Ahabu alivyotumia vibaya nafasi zake, kwa kumuua Nabothi ili amrithishe mumewe shamba la Nabothi. Biblia katika mstari wa 9 -10 inasema Yezebeli ‘ Akaandika katika zile nyaraka, akasema, pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki na kumshuhudia, kunena, umemtukana Mungu na mfalme, kisha mchukueni nje mkampige kwa mawe, ili afe’. Watu wa mji walifanya kama Yezebeli alivyoagiza. Naam Yezebeli hakujua huo ndio ulikuwa mwisho wa utawala wao kwa kosa lile, kwani mahali pale ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi ndipo na damu ya Ahabu ilipomwagika wakairamba pia. Naam angekuwa na ufahamu huu, angetumia nafasi zake vizuri kuponya ndoa yake na utawala wao juu ya nchi.

Ndoa ya Abramu na Sarai (Mwanzo 16:1- 6) nk.

Kutokana na Sarai kutokupata mtoto kwa miaka mingi alimshauri Abramu mumewe atembee na mjakazi wake aliyeitwa Hajiri pengine angepata mtoto. Maandiko yanasema Abramu akaingia kwa Hajiri naye akashika mimba. Kitendo cha Hajiri kushika mimba kikamfanya Sarai aonekane duni/asiyefaa mbele za Hajiri. Ndipo Sarai akamwambia mumewe kusema ‘ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. BWANA na ahukumu kati ya mimi na wewe’. Maandiko hayatuelezi endapo Abramu aliwahi kumwambia mkewe kwamba unipe mjakazi wako nimwingie ili kukuzalia mtoto. Lilikuwa ni wazo la Sarai, naam akalitekeleza, bila kujua matokezo ya mawazo yake ni nini. Ukiendelea kusoma Biblia utagundua kwamba jambo hili liliwakosanisha Sarai na Hajiri, si hivyo tu lakini hata ndoa yake iliathirika. Laiti angedumu kwenye ahadi ya Mungu, fedheha aliyoipata isingemtokea.

Ee Mwanamke, Je umeona jinsi wanandoa hawa yaani Safira, Yezebeli na Sarai walivyotumia vibaya nafasi zao? Ni Wake wangapi leo wanafanya mambo yanayofanana na haya kwa kujua au kutokujua? Ndoa ngapi leo zipo kwenye matatizo kwa kuwa Wake wanawadharau waume zao? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa sababu Wake hawawashauri vema waume zao juu ya Zaka na Sadaka? Ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa Wake hawataki kuwapa waume zao haki ya tendo la ndoa? Ndoa ngapi leo zinaharibika kwa sababu Wake wanawaunga mkono waume zao kufanya yaliyo maovu? Naam imefika mahala Wake wanakubali kufanya zinaa kinyume na maumbile na waume zao? Naam ndoa ngapi leo zimeharibika kwa kuwa wanawake hawapo kwenye nafasi zao kama Wasaidizi, Washauri, Waleta kibali na Walinzi, na hivyo Shetani anatumia uzembe wao kuharibu ndoa zao? Naam baadhi ya akina mama wanafanya mambo mabaya kwa lengo la kuwapendeza waume zao, wasijue kadri wanavyotoka nje ya nafasi zao kiroho, ndivyo adui anavyopanda uharibifu kwenye ndoa zao ili kukwamisha kusudi la Mungu kupitia ndoa zao.

Mambo ya muhimu kwa mwanamke kujua kuhusiana na nafsi ya kuwa mlinzi ni a) Mke amepewa/amefanywa  kuwa ‘Mlinzi’ wa ‘Mume’ katika ulimwengu wa roho akali hapa duniani b) Ni wajibu wa Mke kama ‘Mlinzi’ kusimama kwenye nafasi yake ili kuhakikisha kusudi la Mungu linafanikiwa kupitia ndoa yake c) Ili Mungu ampe Mke taarifa kuhusu mumewe na nyumba yake, Mke sharti awe kwenye nafasi yake maana Mungu hua anatoa taarifa kwa walinzi tegemeana na ‘nafasi zao’ d)Mke anapsawa kuitumia ‘taarifa’ anayopewa na Mungu kama ‘fursa’ ya uponyaji wa ndoa yake.

Wake wengi leo wamebaki kuwalaumu waume zao kutokana na mambo wanayoyafanya ili hali wao hawafanyi pia wajibu wao. Je mara ngapi kwa siku unamuombea mumeo kwa kumaanisha? Ni ulinzi kiasi gani umemuwekea mumeo? Je unafafamu kwamba suala la usalama wa mume wako, Mungu ameliweka kwako? Naam usipofanya na Yesu hafanyi? Ukinyamaza na yeye ananyamaza? Unajua kwa nini? Ni kwa sababu Mungu hawezi kuweka ulinzi juu ya mji, kama Mlinzi wa mji hajasema ‘BWANA linda mji huu’ (Isaya 62:6-7). Naam Jenga nidhamu ya kuomba kila siku kwa ajili ya mumeo ili Mungu aachilie ulinzi wake juu ya mumeo kwa kuwa wewe, kama Mlinzi uliyeko kwenye nafasi, umeshauri na umeelekeza kufanya hivyoNaam ni wajibu wako pia kutumia damu ya Yesu kumwekea mumeo ulinzi kwenye kila eneo la misha yake na hivyo kuiponya ndoa yako (Asomaye na afahamu).

 

Biblia katika kitabu cha Mithali 14:1 inasema ‘Kila mwanamke aliye na hekima huijenga nyumba yake: Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’. Tafsiri ya neno nyumba ni familia, naam na familia inajumuisha baba, mama na watoto endapo mmejaliwa. Hata hivyo katika hali ya kawaida watoto watalelewa katika msingi mzuri endapo ndoa husika imetengamaa. Ifahamike kwamba hili andiko si la wanandoa peke yao, bali hata wanawake wasio wanandoa wenye familia kama wajane, walezi nk linawahusu. Kwa kuwa hapa tunazungumzia habari za wanandoa nitalifafanua zaidi kutoka kwenye kona hiyo. Pia neno nyumba limetumika ili kutupatia urahisi wa kuelewa namna nyumba za kawaida zinavyojengwa ili tueguze dhana hiyo kiroho pia. Kwa lugha rahisi ndoa yako ni nyumba, hivyo ubora, uzuri na mvuto wa ndoa yako unategemea namna unavyoijenga daima kwa hekima.

Ni vizuri ukafahamu kwamba suala la ujenzi/maboresho ya ndoa yako ni jukumu la kila siku ya kuishi kwa ndoa yenu mpaka kifo kiwatenganishe. Kila mmoja katika ndoa ni lazima ahakikishe anasimama kwenye nafasi yake na kufanya yale yampasayo ili kuifanya ndoa yake kuwa bora zaidi. Endapo hakutakuwa na jitihada za wanandoa katika kuimarisha ndoa yao, Shetani atatumia fursa hiyo kuivuruga ndoa husika. Kujenga kunakozungumziwa hapa ni kule kuhakikisha ndani ya ndoa kuna mahusiano na mawasiliano mazuri baina yenu ambayo yatafanikisha kutekelezwa kwa kusudi la Mungu.

 

Ukweli wa ajabu na wa pekee

Ni ajabu sana kuona kwamba jukumu la ujenzi wa ndoa/nyumba amepewa mwanamke. Hii haina maana mwanaume hahusiki, hapana, bali ki-nafasi jukumu la ujenzi wa nyumba/ndoa ni la kwako mama. Kumbuka nilikueleza kwamba nafasi hizi tano za Mwanamke katika ndoa zinafanya kazi kwa pamoja na kwa kutegemeana. Katika nafasi hii ya ujenzi unapaswa kuhakikisha unajenga ndoa yako ili kuzuia kila ufa/fursa ambayo Shetani anaweza kutumia kuvuruga ndoa yako. Kumbuka katika hali ya kawaida kujenga ni kuimarisha/kuweka mazingira bora juu ya kile unachokithamini ili kuzuia madhara yanayoweza kutokea. Naam nafasi hii inalenga kukusaidia uwe makini sana na kila kinachoweza kubomoa ndoa yake.

7

Suala la ujenzi wa ndoa ni endelevu kwa sababu siku zote adui anatafuta kubomoa ndoa yako. Ni lazima uwe makini kujua wapi ni mahali palipobomoka ambapo Shetani anapatumia sasa kuharibu ndoa yako au anaweza kutumia baadaye kuharibu ndoa yako, naam ukishajua kwa kutumia hekima, jenga ukuta imara ambao adui hawezi penya. Kama ndoa yako ina nyufa basi ni rahisi adui kupita kwenye hizo nyufa. Kumbuka hata  kama umemaliza kujenga kila kitu kwenye nyumba yako, bado kuna matengenezo ya mara kwa mara yanahitajika ili kuifanya nyumba yako kudumu katika hadhi inayostahili. 

Maeneo ya msingi katika kujenga ndoa yako

  • Utiifu kwa mumeo

Maandiko yanasisitiza sana wanawake kuwatii waume zao (Waefeso 5:22-24,                1 Petro 3:1). Mitume walindika maandiko haya ili kuwaonya wanawake kutokana na mienendo yao mbele za waume zao kitabia na hasa katika suala zima la utiifu. Bahati mbaya baadhi ya akina mama sio watiifu kwa waume zao na tena wengine wana dharau kubwa sana. Naam fahamu kwamba Mke si Mke bila Mume, na Mume si Mume bila Mke. Hata siku moja ndoa yako haiwezi kujengwa kwa kiburi au dharau kwa mumeo bali utakuwa unaumba jambo baya sana ndani ya mume wako.

Najua unaweza ukasema tabia za mume wangu ndiyo zinazifanya kumdharau, kumsema vibaya nk. Suala sio tabia zake, bali ni wewe kutumia hekima katika kukabiliana na tabia zisifofaa za mumeo kwa kuwa kumdharau ni kuendelea kubomoa na si kujenga, naam  ni kuendelea kuleta tatizo na sio kutatua tatizo. Umeshawahi kuwaza juu ya jambo hili kwamba, Mke anaagizwa kumtii mume wake kama vile kumtii Bwana. Imeandikwa katika Waefeso 5:22 ‘Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu’. Je ni kweli ndivyo unavyomtii Mumeo? Naam haijalishi mume wako yukoje usionyeshe dharau, mtiii tu, ni mume wako.

Mtume Petro anawaonya wanawake akisema ‘kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno’ (1Petro 3:1). Sijui kama wewe Msomaji unaona uzito uliopo kwenye mistari hii. Kwa lugha nyepesi utiifu wa mke kwa Mume utawafanya wengine kumwamini Yesu mnayemtumaini. Naam na upande wa pili, kukosa utiifu kwa mumeo kutawazuia wengine kumwamini Yesu, je unajua gharama ya kuwazuia wengine kumjua Kristo kwa sababu ya kukosa utiifu kwa mumeo (asomaye na afahamu siri hizi).

Wanaume kadhaa walioko kwenye ndoa wamekuwa wakiniambia kwenye suala la tabia hawajaona tofauti kati ya wanawake wasiokoka na waliokoka. Na kikubwa wanachosema ni kudharauliwa na wake zao. Hata kama katika hali ya kawaida mumeo anafanya mambo yanayopelekea wengine kumdharau wewe usifanye hivyo yeye ni kichwa chako (Waefeso 5:23).

Fahamu kwamba daharau ni sumu mbaya kwenye ndoa yako yako mama, jizuie kabisa. Naam utiifu ni kila kitu kwa Mwanume, binafsi nimegundua wanachotafuta wanaume kwa wake zao bila kujali elimu zao, uchumi wao nk ni utiifu, naam kumdharau mumeo ni kubomoa nyumba yako ni kumruhusu Shetani kuharibu ndoa yako, ni kumuingiza mume wako fikra za wanawake wengine tofauti na wewe.

  • Kutunza siri za mume wako

Katika kuijenga nyumba yako ni lazima ujifunze kutunza, kuhifadhi na kuficha mapungufu ya mumeo kwa wengine. Naam hiyo ndiyo hekima. Baadhi ya akina mama   bila hata kujali wanaongea na nani, wamekuwa wakieleza mambo ya ndoa yao na siri za waume bila hata kujua athari yake. Naam kufanya hivyoni kubomoa na si kujenga. Unawajibika kmtii na kumtunzia mumeo siri zake licha ya mapungufu aliyo nayo na uzidi kumwomba Mungu kwamba aiponye ndoa yako.

2

Naam na hata kama ni muhimu uwaeleze kwa lengo la kujenga basi ni muhimu kuwe na mipaka ya nani unazungumza naye na nini unawaweleza maana si kila kitu wanapaswa kujua cha wewe na mumeo. Katika kulisistiza jambo hili Paulo anawagiza Tito akimweleza kwamba awatumie Wazee wa kike wenye mwenendo wa utakatifu ‘Ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao, na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’ (Tito 2:3-4).

  •  Matumizi ya kinywa chako

Mara kadhaa nimewasikia wanawake walioolewa wakisema maneno yasiyofaa kwa waume zao. Najua wengine ni kutokana na hasira na wengine kutokana na mfululizo wa matukio yasiyofaa ya mumewe. Nimesikiia wanawake wakiwaaita waume zao wajinga, wapumbavu, na mengine ambayo nisinependa kuandika hapa. Ninachotaka ukijue ni hiki, imeandikwa Mtu atashiba kwa matunda ya kinywa chake.

Tambua kwamba mume wako naye ana nafasi zake kama mwanandoa kwako, na nafasi moja wapo ni kuwa kichwa cha mwanamke. Sasa kila baya unalotamka kwake maana yake unaliumba kwenye kichwa chako mwenyewe na hivyo tarajia mabaya na uharibifu kwenye ndoa yako. Najua utaniambia Patrick kuna mambo yanaudhi sana na hayavumiliki, na mimi nitakujibu ni kweli lakini namna ya kushughulika nayo ni wewe kutumia hekima kama mjenzi na kuiponya ndoa yako na si kumesema vibaya.

Fahamu pia kwamba katika ulimwengu wa roho kuna pepo ambao kazi yao ni kufuatilia maneno/mawazo mabaya ambayo mtu anayanena ili kuyaumba yatimie. Mfano ukiwa na wazo kwamba kwamba Mume wangu si mzuri uwe una uhakika kuna pepo watakuja juu yako na kuhakikisha siku zote wana kufanya umuone mume wako mbaya.

Je hujasoma Zaburi 36: 4 inasemaje ‘Huwaza maovu kitandani pake, hujiweka katika njia mbaya; ubaya hauchukii”. Naam tafsiri yake ni kwamba hali ya sasa ya mtu huyo ni matokeo ya mawazo yake, naam mwanandoa huyu amewaza na kunena mabaya juu ya mume wake, na kwa sababu hiyo ameiingiza ndoa yake kwenye mabaya. Naam ni lazima ujifunze kunena mananeo yenye kuijenga ndoa yako na si kubomoa, ndivyo na nafsi yako, fikra zako zitakapokiri hivyo, naam ndivyo na BWANA Mungu naye atahakikisha hayo yanakujia.

  •  Msamaha (kusameheana)

Ndoa nyingi leo zinashida kwa sababu ya wanandoa kushindwa kusameheana.  Ni kweli kwenye ndoa kuna mambo mengi ambayo katika hali ya kibinadamu yanaweza kukufanya ushindwe kusamehe, nami kama Mwalimu sina budi kukufundisha kile ambacho neno la Mungu limeelekeza. Kumbuka imeandikwa tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote… (Waebrania 12:14). Naam watu wote wa kwanza akiwa na mumeo, hatutegemei uwe na mahusainao mazuri na watu wa nje, wakati mume wako hutaki kumsamehe, utakuwa unajidanganya nafsi yako.

8

Hivyo bila kujali Mumeo amefanya kosa ganii hakuna namna ni lazima ujifunze kusamehe na kusahau. Hii ni kwa sababu kutokusamehe ni kumpa Ibilisi nafasi ya kuendelea kuwavuruga. Si hivyo bali usitegemee kwamba hata maombi yenu nyote wawili yatakuwa yanasikilizwa. Maana kwa kushindwa kwako kusamehe una haribu mahusiano na Mungu (Mathayo 6:14) na kwa mwanaume kwa kushindwa kwake kukaa kwa akili na wewe kama mke, maandiko yanasema maombi yake hayatasikilizwa. Je unategemea nini kitatokea kama hautakuwa tayari kumsamehe.

  •  Kujali mahitaji ya mwenzako (tendo la ndoa)

Paulo Mtume aliwaandikia hivi wanandoa wa Korinto ‘Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanaume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu’ (1Wakorinto 7:1-5).

Kimsingi andiko hili linalenga wanandoa wote wawili, bali kwa kuwa ujumbe huu ni maalum kwa wanawake nitaandika zaidi upande wa mwanamke. Biblia iko wazi kwamba kwa sababu ya zinaa (tendo la ndoa) kila mume awe na mke wake mwenyewe. Moja ya sababu muhimu za wewe kuolewa ni ili kumtosheleza mumeo kwa habari ya tendo la ndoa kama ilivyo na kwako pia.   

Kwa wanandoa wengi haja ya tendo la ndoa inatofautina, hata hivyo mara nyingi uhitaji wa tendo la ndoa kwa Mwanaume uko juu kuliko ilivyo kwa mwanamke. Hata hivyo kila mmoja ana – muhitaji mwenzake ili kutoshelezwa katika hitaji hili muhimu. Baadhi ya wanawake kwa kujua ukweli huu na tofauti hii ya uhitaji wa tendo la ndoa, kwa kutokufikiri athari zake kwa wenzi wao, kwao binafsi na ‘future’ yao huwanyima waume zao haki yao ya tendo la ndoa hasa pale wanapokuwa wametofautiana juu ya jambo fulani. Mbaya zaidi wapo akina mama ambao wakikasirika huwanyima waume zao haki hii ya msingi kwa muda mrefu kwa mfano mwezi mmoja, minne, hata zaidi ya mwaka na wanaishi nyumba moja na wengine wanalala kitanda kimoja.   

Mume wako akijua kwamba unatumia ugomvi/tofauti zenu au hata kwa makusudi kumnyima haki yake ya tendo la ndoa, na jambo hilo likawa endelevu uwe na uhakika taratibu unaanza kuharibu ndoa yako. Maana, Shetani ni mzuri sana wa kutumia nafasi ambazo wana wa Mungu wanampa. Ndani ya mume wako yataingia mawazo mabaya (Ezekieli 38:10) na kumweleza ‘je mbona kuna wanawake wengi, ni suala la kwenda kumaliza haja yako kwa mwanamke yoyote mwingine’. Wazo jingine pia litamwambia kwa nini huyu mwanamke akutese kiasi hiki, kwa nini usiwe na nyumba ndogo nk. Uwe na uhakika endapo mumeo ameokoka, hofu ya Mungu ndani yake ndiyo itakayomzuia kufanya mambo haya lakini ukimuuliza taratibu atakuambia mawazo haya hunijia mara kwa mara unaponinyima haki yangu ya tendo la ndoa.

6

Naam, hata kama hatafanya hayo, uwe na uhakika kwamba tayari kwenye ufahamu wake umeshapanda mbegu mbaya na itaendelea kukua endapo utaendelea na tabia yako ya kumnyima haki yake. Ndiyo, usishangae siku moja kukuta mumeo ametoka nje ya ndoa, usikimbilie kumlaumu Shetani, maana wewe ndiye ulifungua mlango na kumkaribisha. Nakumbuka mwanandoa mmoja (Mwanaume) alisema hizi ndoa za Kikristo zinatutesa sana wanaume, na zinawafanya hawa wanawake wajisahau sana, kwa kuwa wanajua Biblia imetuzia kuoa mke zaidi ya mmoja. Naam ilibidi nitumie muda mwingi kurejesha ufahamu wa huyu ndugu kwenye msingi wa ki-Mungu kwa kuwa nilijua tayari kuna wazo lilishaingia moyoni mwake na nilijua wapi linampeleka.

Nimeandika jambo hili kwa kirefu kwa sababu mara nyingi sehemu kubwa ya kesi za wanandoa inapofika kwenye suala la unyumba, wanawake ndio wanao – wanyima waume zao. Naam nakiri hata wanaume wapo lakini ni mara chache sio kama ilivyo kwa wanawake. Mwanamke sikia, kitendo cha Mungu kukupa huyo mume ni heshima ya pekee sana kwamba ni wa kwako pekee yako. Ukitaka kujua gharama yake waulize wanawake ambao wana ‘share’ mume namna inavyowagharimu kihisia, kifikra na kimaisha. Naam ni lazima ujifunze kujali na kutimiza mahitaji ya mwenzi wako vinginevyo unafungua mlango kwenye ufahamu wa mumeo na kumwambia angalia kule nje kuna wanawake wengine (Asomaye na afahamu).

Ukweli ni kwamba kuna sababu mbalimbali ambazo hupelekea wanawake kwenye ndoa kufanya hivyo, ila ushauri wangu ni kwamba, uamuzi wa namna hii (kumnyima tendo la ndoa mumeo) ni wa kuharibu na si kujenga. Hivyo haijalishi huyo baba kakukosea nini (labda ziwe issue za kiafya), suala la tendo la ndoa kwake ni muhimu sana na ni haki yake, kutokumpa haki yake ni kukaribisha Shetani kwenye ndoa yako. Naam ni vizuri mka-hakikisha kwamba tofauti zenu zote mna – zimaliza kabla hamjaingia kulala, itawasaidia sana.

Kuna maeneo ambayo ningeweza kuandika pia, lakini hayo matano hapo juu ni msingi wa mengine mengi. Kutokana na urefu wa nafasi hii ya Mwanamke kama Mjenzi nimelazimika kuigawanya mara mbili kwa hiyo katika sehemu ya tano nitamalizia kipande kilichobaki ambacho ndani yake nitaonyesha mwanamke anawezaje kupata hekima ya kumsaidia kuafanya haya na nitaweka baadhi ya mifano yenye kusaidia.

 

Hebu tuanze kwa kuangalia mstari wa ajabu sana katika Muhubiri 7: 12 unasema ‘Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi, na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliyonayo’. Hekima ndio nguzo kuu ya ujenzi wa ndoa yako, naam ukiwa nayo ni dhahiri kwamba italeta uponyaji kwenye ndoa yako pia. Mwanamke kama mjenzi anahitaji kuwa na hekima ili kulinda ndoa yake akijua kwamba ki – nafasi yeye ni Mlinzi wa mumewe. Kumbuka kwamba andiko letu la msingi katika sehemu hii ya nne ni Mithali 14:1 unaosema “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa  kwa mikono yake mwenyewe”

Je, utapataje hekima ya kuijenga ndoa yako?

Zifuatazo ni njia ambazo zitakusaidia kupata hekima ya ki – Mungu ili kujenga, kuhifadhi na hivyo kuiponya ndoa yako:

a)    Kwa kuomba

 

Biblia katika Yakobo 1:5 inasema ‘Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa’. Je ni hekima ya namna gani hii? Yakobo anaendelea akifafanua kuwa ‘Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki’ (Yakobo 3:17). Kisha kwenye ule mstari wa 13 anauliza ‘N’nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima’ (Yakobo 3:13).

Photo 2

Je mama umeona jinsi mistari hii inavyozungumzia hekima kwa upekee wake? Ni dhahiri kwamba hekima ya namna hii ikiwa ndani yako kwa vyovyote vile ndoa yako itajengwa kwenye msingi imara, naam unahitaji kuomba kwa Mungu akupe hekima safi ambayo ndani yake itajenga msingi wa amani, upole na kudhihirisha matunda mema. Naam kwa hekima utaonyesha mwenendo wako mzuri katika nyumba yako.

Naam Yesu alisema ‘aombaye hupewa…’ (Matahyo 7:7), omba ukiamini Mungu atakupa hekima hii, si tu kwa ajili ya uponyaji wa ndoa yako, bali kwa ajili ya kusudi lake kupitia ndoa yako pia. Maana kadri ndoa yako inavyokuwa na amani ndivyo na kusudi la Mungu kupitia ndoa yako litakavyofanikiwa.

b)   Kwa kusoma neno la Mungu

Katika Mithali 4:5,7 Biblia inasema ‘Jipatie hekima, jipatie ufahamu; usiusahau; Wala usiyakatae maneno ya kinywa changu. Bora hekima, basi jipatie hekima; Naam kwa mapato yako yote jipatie ufahamu’.

Ni muhimu sana kwako Mwanandoa ukaweka utaratibu wa kujifunza neno la Mungu kila iitwapo leo kwa kuwa ndani ya neno kuna hekima na ufahamu wakukusaidia. Biblia inasema ‘apendaye mafundisho upenda maarifa’ (Mitahli 12:1) tena katika Mithali 19:2a inasema ‘si vema nafsi ya mtu ikakosa maarifa…

Photo 3

Ni vizuri ukafahamu kwamba ‘mlinzi yeyote katika ulimwengu wa roho lazima awe na taarifa za kutosha kuhusu lindo lake na kwa jinsi hiyo hiyo mwanamke kama mlinzi lazima awe na ufahamu wa kutosha wa neno la Mungu ili limuongoze katika kumpa hekima ya kiulinzi wa ndoa/nyumba yake. Naam ni LAZIMA ujijengee mazoea na nidhamu ya wewe binafsi kusoma neno la Mungu kila leo.

c)    Kwa kujifunza kwa waliotangulia

Katika kitabu cha Tito 2:3-5 Biblia inasema ‘ vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe na usingiziaji; wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao na kuwapenda watoto wao na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe’.

Naam ni muhimu sana kujifunza kwa wanawake wenye hekima waliokutangulia na wenye kumjua Mungu vizuri kama Tito anavyoelekeza. Hii ni kwa sababu si tu kwamba utajifunza kutoka kwenye hekima yao bali pia kutokana na uzoefu wao binafsi wa kuwa kwenye ndoa zao. Ni dhahiri kwamba hata wao wamepitia/walipitia kwenye changamoto mbalimbali na kwa msaada wa hekima wakazijenga ndoa zao katika BWANA hata zimekuwa na ushuhuda mzuri na leo tunamshukuru Mungu na kujivunia akina mama ambao licha ya changamoto walizokutana nazo kwanza hawakutoa siri za ndoa zao, pia kwa hekima walijifunza kuvumilia, wakatafuta amani, wakasamehe waume zao na kwa jinsi hiyo jina la BWANA halikutukanwa. Naam watafute hao ujifunze kwao maana hata leo wanapatikana.

d)   Kwa kuokoka

Wanawake wengi sana ambao ni wanandoa, ndoa zao zinashida kwa sababu Yesu si BWANA kwenye ndoa zao. Ili Yesu afanyike BWANA sharti wokovu uingie kwenye nyumba yako, kwa kuamua kuokoka. Najua jambo hili linaweza likaleta shida kwa wewe ambaye umeokoka, ukajiuliza mbona nimeokoka lakini bado ndoa yangu ina shida, naam mosi angalia hizo nafasi nyingine uzifanyie kazi, lakini pili mruhusu Yesu afanyike BWANA (Mtawala, Kiongozi, Mshauri) wa ndoa yako. Endapo utaokoka na kuenenda vema katika kuukulia wokovu uwe na uhakika yeye ni Mponyaji, na uponyaji wake hauna mipaka, naam unaweza kumkaribisha akusaidie kuiponya ndoa yako.

Ukisoma Biblia katika Wakolosai 2:3 biblia inasema ‘ambaye ndani yake yeye (Yesu Kristo) hazina za hekima na maarifa zimesitirika’ Maneno ndani yake yeye ndiyo ninayotaka uyaone kwa upana katika mstari huu. Andiko hili linafanya tujue kwamba ziko hekima za namna mbalimbali kutoka kwa BWANA ambazo tunazihitaji ikiwa ni pamoja na hekima ya kujenga nyumba/ndoa yako. Naam ili hekima ipate nafasi ya kuponya ndoa yako sharti mwenye hekima si tu apate nafasi ndani yako bali afanyike BWANA na mwokozi wa maisha yako kwenye maisha yako. (Ikiwa unataka kuokoka bonyeza link hii https://sanga.wordpress.com/wokovu/ ufuatishe sala ya toba)

Hebu tuangalie mifano kadhaa:

Mfano wa Mke wa Nabali

Ukisoma Biblia katika kitabu cha 1Samweli 25:2-35 utaona habari za mtu aliyeitwa Nabali ambaye alitaka kuleta maafa na msiba mkubwa kwenye nyumba yake kwa kitendo cha kuwatukana Daudi na watu wake, licha ya Daudi kufanya kazi kubwa ya kulinda mifugo ya Nabali ilipokuwa mashambani dhidi ya Wafilisti. Kutokana na dharau ya Nabali, Daudi aliapa kwenda kumuangamiza Nabali pamoja na nyumba yake yote. Maandiko yanasema Mke wa Nabali aitwaye Abigaili alipopata taarifa ya yalitokea alifanya hima kwa hekima kumsihi Daudi amsamehe mumewe kwa upumbavu alioufanya, naam na kwa neno la Abigaili Daudi alisamehe.

Photo 6

Tunajifunza nini?

Abigaili alizijua nafasi zake vema kama mke kwa mumewe na hivyo alizitumia nafasi zake kuiponya ndoa yake. Je, umeshawahi kufikiri kwa nini Mtumishi wa Nabali alienda kumpa taarifa Abigaili ya uovu ambao mumewe amewatenda watumwa wa Daudi? Biblia inasema yule Mtumishi alimweleza hivi Abigali ‘Basi sasa ujue na kufikiri utakavyotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya Bwana wetu (Nabali), na juu ya nyumba yake yote, kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye’ (1Samweli 25:17).

Hii ni kwa sababu Abigaili alikuwa Mlinzi wa Nabali na kwa kuwa alikuwa kwenye nafasi zake, taarifa za msingi juu ya lindo lake zilimtafuta. Naam mwanamke aliyesimama kwenye nafasi zake hakuna jambo litatokea au linalokuja mbeleni litatokea bila yeye kuwa na taarifa, na ndio maana Mungu anataka ujifunze mambo haya.

Baada ya Abigaili kupata taarifa husika, aliandaa chakula na kwenda kwa Daudi kuomba msamaha kwa ajili ya mumewe na  Daudi alijibu hivi … Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli ambaye amekuleta hivi leo kunilaki, na ibarikiwe busara yako, na ubarikiwe wewe, uliyenizuia hivi leo nisimwage damu, wala kujilipiza kisasi kwa mkono wangu mwenyewe (1Samweli 25:32-33).

Je umeliona jambo hili lakini? naomba rudia tena kusoma maneno ya Daudi hapo juu. Naam umeshawahi kujiuliza kwa nini Daudi aanze kumhimidi Mungu kutokana na kitendo cha Abigaili? Kwa lugha rahisi Daudi alikuwa akisema ‘atukuzwe Mungu aliyempa Nabali mke mwenye Busara/hekima kiasi hiki’ (Mithali 19:11), maana kwa busara ya huyu mama nimezuiliwa nisimwage damu’. Naam Daudi hakuishia tu kumbariki Mungu bali alimbariki na Abigaili akasema ‘Na ibarikiwe busara yako naam na ubarikiwe wewe Abigaili’ kwa kuchagua kuwa mwanamke mwenye hekima nk.

Tambua kwamba, kama si Abigaili kusimama kwenye nafasi zake, siku ile si tu Nabali angekufa bali yote yaliyokuwa chini yake yangeharibiwa na kutekwa pia. Pengine Biblia ingeandika matukio yote ya Nabali ungeshuhudia namna ambayo mkewe alitumia hekima yake kuilinda na kuijenga ndoa yake. Ni imani yangu kila mumewe alipotenda kwa uovu, mkewe kwa hekima kama mjenzi alitengeneza ndoa yake kama alivyofanya na kwa Daudi, naam kwa nafasi yake Abigaili alizuia msiba usiingie katika nyumba yake.

Hata leo wapo akina mama wengi sana ambao wanamlilia Mungu aziponye ndoa zao kwa sababu zina shida kubwa. Katika hao wanaomlilia Mungu, si wote wanaojua kwamba Mungu anafanya kazi kwa taratibu na kanuni alizojiwekea. Ni matarajio ya Mungu kuona kila Mwanamke aliyeko kwenye ndoa anasimama kwenye nafasi zake, kutokea kwenye nafasi zake ndipo Mungu atasema na kumuongoza huyo mama juu ya nini cha kufanya ili kuponya ndoa yake na si vinginevyo.

Photo 4

Kumbuka kwamba ‘ni vigumu sana kwa Mungu kukusaidia/kukupigania kama hauko/haujasimama kwenye nafasi zako’. Katika kufanya kazi zake hapa duniani Mungu anaangalia nafasi ambazo amewapa watu kwenye ulimwengu wa roho. Naam wale ambao wapo kwenye nafasi zao ndio ambao Mungu anafanya nao kazi. Hivyo sio suala la kulia tu, bali ni suala la kusimama kwenye nafasi yako kama Mjenzi wa ndoa yako na utaona mabadiliko makubwa sana. Kumbuka pia na adui naye akitaka kuharibu ndoa yako sharti akuondoe kwenye nafasi zako, hii ni kuonyesha kwamba nafasi alizokupa Mungu kwenye ulimwengu wa roho zina thamani kubwa sana.

Mfano wa Stefano

“Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na wale wa kilikia na Asia wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye” (Matendo ya Mitume 6: 9 -10). Naamini umeliona jambo hili wewe mama, jaribu kufikiri watu kutoka kwenye masinagogi matano tofauti walikuwa wakishindana na Stefano kwa habari za Injili aliyowashuhudia. Utamu wa habari hii ni kwamba Stefano alishinda na zaidi ya kushinda kwa sababu mosi, si tu alijazwa Roho Mtakatifu, bali kwa sababu ndani yake kulikuwa na hekima ambayo ilipita fahamu za wapinzani wake wote. Naam hivi ndivyo hekima ilivyofanyika ulinzi kwa Stefano na kwa shauri la BWANA.

Binafsi nalipenda sana andiko hili, maana linadhihirisha uwezo wa hekima katika kutenda, kulinda, kuhifadhi, kuponya nk. Naam si tu Roho Mtakatifu alimsaidia Stefano bali pia hekima aliyokuwa nayo Stefano ilimjengea mazingira mazuri Roho Mtakatifu ya kumshindia Stefano. Hekima hii ndiyo iliyokuwa ndani ya BWANA wetu Yesu Kristo alipokuwa bustanini na wanafunzi wake, wakati wa mateso yake na hata kifo chake. Maana alisema ‘Baba uwasamehe maana hawajui walitendalo’.  Mpenzi msomaji fikiri endapo ungekuwa wewe kwenye mazingira kama ya Stefano au Yesu ungechukua uamuzi gani?

Nimeandika Mfano huu wa Stefano si kwa bahati mbaya bali kwa kusudi kamili. Najua kesi ya Stefano haikuwa ya ndoa, bali upinzani dhidi ya injili ya Kristo. Nilichotaka kukuonyesha ni uwezo wa hekima katika kulinda, kuhifadhi, kusaidia nk wakati mtu anapokutana na changamoto mbalimbali. Hekima ya Mungu ilimsaidia Stefano kutokana na mazingira yake, naam na hata kwako inaweza kukusaidia kuiponya ndoa yako. Naam hekima ni Mlinzi, hekima ni Mjenzi, hekima ni Mponyaji nk, kwa neema ya Mungu, kupitia ujumbe huu nimemtambulisha Hekima kwako mama, MTAFUTE NA KUMTUMIA ATAKUSAIDIA KUIPONYA NDOA YAKO.

 

  • Ndoa ni wito wa mapungufu

Mama mmoja ambaye ndoa yake ilikuwa inasumbua alinitafuta na kuniambia, Mtumishi, changamoto za ndoa yangu ni kubwa kiasi kwamba sasa ni majuto tu, sina raha kabisa hata kidogo, nimekuwa mtu wa kuumizwa na kulia kila siku kwa sababu ya ndoa yangu, naomba msaada wako. Nilimsikiliza kwa kirefu katika yote aliyonieleza kwa upana wake.

Ukweli ni kwamba mpaka leo mama huyu simfahamu hata kwa sura, lakini BWANA alinijulisha kwamba ndani yake kuna huduma kubwa, ambayo Shetani anapamba nayo kupitia mumewe. Nilipojua nafasi ya huyu mama si tu kwa muewe bali kwa mwili wa Kristo kwa ujumla ilibidi kulipa kipaumbele suala lake mpaka Mungu aingile kati. Kwa kifupi nilianza taratibu kumfundisha jambo hili, nikamuonyesha nafasi zake na namna ya kuzitumia, naam naye akaweka kwenye matendo na sasa ndoa yake, BWANA ameiponya, wanaendelea vizuri kifamilia na kihuduma pia.

Jambo ambalo nimejifunza kupitia baadhi ya wanandoa ni kwamba, ndoa ni wito wa mapungufu. Unapoingia kwenye ndoa tegemea kukutana na changamoto kadhaa kutoka mwenza wako na hivyo kuwa tayari kuzikabili na kuvumilia. Kuna mapungufu ambayo yataisha kabisa kadri unavyoendelea kukaa kwenye nafasi zako na pia yapo ambayo hayataondoka kabisa kwa kuwa hayo ndiyo sababu ya wewe kuunganishwa na mwenzi wako, na Mungu aliona katika wanawake wengi wewe ndiye unayeweza kuchukuliana na kumsaidia katika mapungufu yake.

 

Wapo akina mama ambao wanatamani sana waume zao wabadilike tabia zao na zifanane na za kwao kabisa, napenda kukuambia kwamba hilo haliwezekani.  Naam, ile kwamba wewe ni mwanamke na yeye ni mwanaume ni dhahiri kwamba kuna vitu hamuwezi kufanana. Licha ya tofuti za kijinsia, malezi ambayo kila mmoja amepata kwenye famila yake, hitoria zenu, tofauti ya elimu zenu, vipato vyenu, umri wenu n.k. ni dhahiri kwamba mapungufu yatakuwa ni sehemu ya maisha kwenu. Sharti mjifunze kuchukuliana na kusameheana katika madhaifu na mapungufu hayo.

  • Tumia muda mwingi kuomba na si kuongea (Mithali 10:19,17:27, 18:21)

Maneno ni moja ya vyanzo vikubwa vinavyochangia kuharibu ndoa nyingi leo. Biblia katika kitabu cha Mitahli 10:19 inasema ‘Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili’. Wapo baadhi ya akina mama ambao kueleza wengine mambo ya ndoa yao ni kawaida yao. Jambo baya zaidi ni kwamba wanawasema waume zao vibaya hata kwa watu ambao hawakustahili kuelezwa hayo. Kumbuka imeandikwa pia ‘Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi, Na wao waupendao watakula matunda yake’ (Mithali 18:21)

Je unatumia muda kiasi gani kuomba kwa ajili ya mumeo? Na unatumia muda kiasi gani kuzungumza na watu wengine kwa siku? Naam nakushauri jifunze kutumia muda mwingi kuomba kwa ajili ya ndoa yako na kwa hakika BWANA Mungu atakufunulia mambo mengi sana kwa habari ya nyumba yako.

Biblia katika kitabu cha Ayubu 13:5 inasema “Laiti mngenyamaza kabisa, hilo lingekuwa hekima kwenu’. Sikia mwanamke, licha ya matendo, hekima kwa sehemu kubwa inadhihirika kwa njia ya kinywa, naam kunyamaza ni bora kuliko kunena, na hasa unapokuwa na hasira, chunga sana usinene maana hekima

Pesquisar
Categorias
Leia Mais
Injili Ya Yesu Kristo
Alipita katikati yao Akaenda zake!
Luka 4:16-30 “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika...
Por GOSPEL PREACHER 2022-04-01 08:24:42 0 10K
FORM 1
BASIC MATHEMATICS: FORM 1
List of all topics in Basic Mathematics for form 1 class: CLICK HERE TO VIEW. NUMBERS FRACTIONS...
Por PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 12:44:29 0 5K
NUMBERS
Verse by verse explanation of Numbers 13
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-24 14:38:19 0 4K
HOLY BIBLE
THE HOLY BIBLE
Welcome to Proshabo Online Bible Study (POBS). This is the best platform for you to...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-01 08:57:05 0 7K
2 KINGS
Verse by verse explanation of 2 Kings 6
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-03-19 19:33:54 0 5K