UFUNUO WA MAISHA YA WOKOVU KWA DHANA YA NJIA NYEMBAMBA NA NJIA PANA

0
5K

Shalom, neema ya Kristo na iwe kwako, ndugu, maadam unaishi uwe na uhakika utakufa na hapo ndipo utakapo yaanza maisha yako ya umilele aidha ndani ya ufalme wa nuru pamoja na Yesu au katika moto wa milele. Ujumbe huu unalenga kukuonyesha maisha ya wokovu kwa dhana ya njia nyembamba na njia pana na kwa jicho la ufalme wa nuru ili ikusaidie kuongeza hofu na nidhamu kwa Mungu katika safari yako.

Maamuzi ya wapi utaishi milele baada ya kifo chako yanafanyika sasa ukiwa hai na sio baada ya kifo. Ndio, maamuzi ya wapi utaishi yanategemea utiifu na nidhamu yako kwenye njia unayopita kutokana na mlango ulioingia ili kuipata njia hiyo. Hivyo, kupitia ujumbe huu nataka nikuonyeshe mambo kadhaa ambayo unahitaji kuyajua na kuyazingatia katika safari yako ya maisha hapa duniani.

KatikaMathayo 7:13-14 imeandikwa ‘Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao WAIONAO ni wachache’. Kutokea kwenye andiko hili yafuatayo ni mambo muhimu kujua:

Mosi ni Uwepo wa milango na njia kwenye ulimwengu wa roho – Katika ulimwengu wa roho kuna milango na njia za kutufikisha kwenye mwisho na umilele wetu. Hii ni milango ambayo inamsaidia yeye aliyeingia kuona na kujua njia ya kuiendea ili kufikia kwenye mwisho uliokusudiwa na mwenye njia. Hivyo suala la kuchagua mlango sahihi wa kuingia ni la muhimu sana na tena suala la kuwa mtiifu kwenye njia unayoiendea bila kutoka ni la muhimu zaidi ili kumaliza salama safari yako.  

Yesu ndiye mlango na njia ya ufalme wa nuru wakati Shetani ndiye mlango na njia ya ufalme wa giza (Yohana 10:7, 14:6).  Malango haya mawili ni halisi kabisa na kila moja linafanya jitihada ya kuhakikisha watu wengi waingia kwa lango lake. Yesu aliye lango la ufalme wa nuru, anakuita uingie kupitia mlango ulio mwembamba. Kinachofanya mlango uwe mwembamba na njia iwe imesonga ni kwa sababu njia hiyo ni njia ya UTIIFU kwenye neno la Mungu wakati kinachofanya njia iwe pana, ni kwa sababu, njia hiyo ni njia ya UASI dhidi ya neno la Mungu.

Kosa kubwa la waamini wengi ni kufikiri ujumbe huu wa ‘ingieni kupitia mlango mwembamba’ ni wa wasiokoka. Hapa Mungu hazungumzi na mataifa pekee bali zaidi watoto wake, naam wale walioingia kwa lango lake, akiwataka wadumu kuwa watiifu kwenye neno lake ili wasiikose mbingu maana imeandikwa ‘Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki’ (Warumi 2:13)

Njia nyembamba ni njia ya kujikana, ni njia ya kutoyapenda maisha yako hata kufa, njia inayotaka ujizuie kuifuatisha namna ya dunia hii bali udumu kutii na kuenenda kwa Roho. Wakati njia pana ni njia ya uhuru wa mtu kutenda vile apendavyo bila kuzingatia sheria za Mungu. Inasikitisha kwamba wengi wameichagua njia hii kwa kuipenda dunia na kuifuatisha namna yake (Mwanzo 3:4, Warumi 1:28).

Pili, kila mtu yupo kwenye mojawapo ya njia hizi – Tambua kwamba njia hizi ni halisi na kwamba kila njia ina watu wanaoipita. Wakati hivi sasa upo hapa duniani. kwenye ulimwengu wa roho pia upo na unapita kwenye mojawapo ya njia hizi. Ili kujua upo kwenye njia ipi, angalia ni sheria ya ufalme upi, unaiishi na kuitekeleza uwapo duniani. Je, ni sheria ya ufalme wa nuru au ufalme wa giza? Je, ni sheria ya Roho wa uzima ulio katika Kristo Yesu au ni Sheria ya dhambi na mauti.

Njia hizi zinaongozwa na sheria zinazosimamiwa na kila ufalme kwenye ulimwengu wa roho. Pale unapotii na kuishi kwa kulifuata neno la Mungu ndipo unakuwa kwenye njia nyembamba iendayo uzimani, pale unapoasi neno la Mungu ina maana umechagua kutii sheria za ufalme wa giza na hivyo unakuwa kwenye njia pana iendayo upotevuni. Mtu anaweza kuwa mshirika mzuri kwa macho ya damu na nyama lakini katika ulimwengu wa roho yupo kwenye njia iendayo upotevuni kwa sababu ya uasi.

Tatu, uamuzi wa kumfuata Yesu una gharama kubwa – Safari ya wokovu nyepesi kama wengi wanavyofikiri maana ni safari inayo wataka wafuasi wa Yesu wajitoe kiuhalisia na wampende Mungu kuliko maisha yao. Hivi ndivyo Yesu na wazee wetu wa imani walivyoishi na Yesu mwenyewe anasema ‘…Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha (Luka 9:23-24).

Shetani kwa kutumia dhiki, shida, adha, njaa, aibu, mabaya nk, amefanikiwa kuwatoa wengi kwenye njia nyembamba na kuwaingiza kwenye njia pana. Ndio, licha ya upinzani huo maandiko yanatusaidia tujue kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi na kwamba tumepewa si tu kumwamini KRISTO, ila na KUTESWA kwa ajili yake na temna imeaandikwa ‘Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu’ (Yohana 16:33).

Sasa, ikiwa tunazo kweli hizi zote, kwa nini tunakuwa wepesi kukata tamaa, kuanguka na kurudi nyuma. Je, sio kwamba sharti na sisi tupitie njia waliyopitia baba zetu kiimani tukikumbuka kwamba Yesu hajatuahidi maisha mepesi tuwapo duniani. Ndio, huwezi kuwa wa Kristo ufalme wa giza ukakupenda, huwezi kuwa na nuru giza likakupenda, huwezi kuwa na kweli, uongo ukakupenda, maadam una nuru, ulimwengu utakuchukia tu, wewe tunza taa yako isizime na vazi lako liwe safi.

Mfano wa Musa na wana wa Israeli:

Katika kitabu cha Hesabu 1:46 tunasoma kwamba wanaume waliotoka Misri ambao waliweza kwenda vitani na umri wao ulizidi miaka 20 walikuwa ni 603,550, lakini walioingia Kanani walikuwa ni wawili tu, yaani Yoshua na Kalebu. Je, takwimu hizi zinatuambia na kutuonyesha nini ukizingatia kwamba wote laki sita waliahidiwa kufika Kanani na walikuwa wanasema na kuamini kwamba watafika.

Hii ni kutujulisha kwamba safari ya wokovu sio rahisi kama wengi wanavyoichukulia na kwamba kiuhalisia wanaoiendea njia pana ni wengi kuliko wanaoiendea njia nyembamba na ndio maana imeandikwa ‘Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani’ (1 Wakorintho 10:6,11).

Hivi unajua kwamba kilichowafanya Musa na Haruni wasiingie Kanani ni UASI pia dhidi ya maagizo ya Mungu kuhusu kutoa maji kwenye mwamba. Ndio, licha ya kwamba maji yalitoka na wana wa Israeli wakafurahi, kwa uasi wao walipata malipo husika maana Bwana aliwambia ‘…Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, HAMTAWAINGIZA kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa’ (Hesabu 20:12).

Wakati wana wa Israel wanasherekea na kuwaona viongozi wao mashujaa huku wakiwapa majina ya kiutukufu, viongozi wao walikuwa wanapokea hukumu kutokana na uasi waliotenda. Hata leo mbele za watu, unaweza ukaonekana uko safi, naam una jina la kuwa hai na ukifa watasema yuko mbinguni, ingawa nafsi yako inakushuhudia upo kwenye njia ipi? Usidanganywe wala kujifariji kwa maneno, sala au matamko ya watu, mbinguni utaingia kwa utii kwenye neno la Mungu na sio vinginevyo.

Je, upo kwenye njia ipi, nyembamba au pana? njia uliyopo inaamua mwisho wako wa umilele. Inaumiza kuona kanisa limejiingiza kwenye uasi usioneneka kwa kuifuatisha namna ya dunia hii, lisijue kwamba kama linataka kuurithi uzima wa milele haliwezi kukwepa kuishi maisha ya njia nyembamba. Ujumbe huu ukusaidie kuifanya imara roho yako ili udumu katika imani hii ya Kristo ukijua kwamba IMETUPASA kuingia katika ufalme wa nuru kwa njia ya dhiki nyingi, naam ndio njia nyembamba, njia ya kujikana, njia ya utiifu.

Kanisa, Yesu aliye mfalme wa nuru anatuonya na kutuagiza tuingie kupitia mlango mwembamba kwani mwisho wake ni mzuri. Tambua kwamba njia unayopita ndiyo inayokufikisha kwenye mwisho uliokusudiwa na MTENGENEZA njia na sio mwisho unaoutaka wewe. Hivyo, kama umeamua kumfuata Yesu, basi tembea kwenye njia yake, njia aliyokuagiza maana kinachoamua wapi unaenda sio kusema umeokoka, bali njia unayopita.

Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu.

Zoeken
Categorieën
Read More
REVELATION
MAJIRA YA KANISA LA SMIRNA
Majira haya ya kanisa la Smirna tutayaona katika {UFUNUO 2:8 -11} ambapo kama...
By GOSPEL PREACHER 2021-09-24 08:49:32 0 6K
EXODUS
Verse by verse explanation of Exodus 33
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-23 05:34:22 0 6K
Religion
HATUA ZA KUINUKA BAADA YA KUANGUKA
Bwana Yesu asifiwe! Huna sababu ya kubakia hapo chini baada ya kuanguka majaribuni. Kwa...
By GOSPEL PREACHER 2021-09-04 07:33:04 1 6K
Injili Ya Yesu Kristo
HABARI ZA MWANA MPOTEVU
(A) MWANA MPOTEVU (MTOTO MDOGO)  LUKA 15;11-24 "Kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-15 22:14:25 0 6K
OTHERS
MUHAMMAD NI MTUME BANDIA
1. Hakutumwa na Mungu2. Alipewa Utume na Mkewe3. Alichezewa na Mashetani tokea utoto wake Leo...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 05:33:15 0 5K