MAZINGIRA HATARAISHI YA KUEPUKA KATIKA KUFANYA KAZI NA ROHO MTAKATIFU

0
5K

Roho Mtakatifu, kwa nafsi na nafasi yake ameletwa ili AKAE nasi kama Msaidizi wa kutufundisha na kutongoza katika njia ITUPASAYO kuiendea. Lengo lake ni ili kufanikisha KUSUDI la Mungu chini ya jua kwa kumtumia na KUMSAIDIA  mtu kuishi na kuyatenda yale aliyokusudiwa katika maisha yake. Ndio, mtu anamuhitaji Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu anamuhitaji mtu. Rejea Yohana 14:26 Yohana 16:13, Zaburi 32:8 na 1 Wakorintho 2:10.

Sasa, ili Mwanadamu afanikiwe, anatakiwa kumjua, kushirikiana na kumtumia Roho Mtakatifu wakati ili Roho Mtakatifu afanikiwe anahitaji ushirikiano wa mtu kwa KUTENGENEZEWA MAZINGIRA sahihi ya yeye kufanya kazi. Roho Mtakatifu, daima  anatafuta makazi ili afanye makao yake ndani ya mwanadamu na kumsaidia.

Hivyo ili Roho Mtakatifu afanye makao ndani yako na kufanya kazi zake ipasavyo itategemea MAZINGIRA unayomtengenezea kwa dhana ya MUDA, UTAYARI na UTIIFU. Je, mazingira yanamruhusu KUKAA au kuondoka?, yanamfurahisha au kumhuzunisha, yanamfanya kuwa hai au kuzima? Ndio Roho Mtakatifu anataka apate MAZINGIRA yaliyo sahihi ili afanye kazi kutokea na kupitia kwako.

Yafuatayo ni mazingira hatarishi kuyaepuka ikiwa unataka kuona matokeo ya utendaji wa Roho Mtakatifu kwenye maisha yako:

Moja, Jihadhari USIMHUZUNISHE Roho Mtakatifu – Waefeso 4:30 imeandikwa ‘Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi’. Uasi wetu dhidi ya neno la Mungu, ndio unao mhuzunisha Roho Mtakatifu na hivyo tunaagizwa tusimfanye yeye kuwa na HUZUNI maana athari zake ni mbaya. Je, unaujua mwonekano na mwitikio wa Roho Mtakatifu pale anapohuzunika ukoje?. Je, unajua kwamba yeye pia ana mwili, nafsi, hisia na kwamba ana uwezo wa kufanya maamuzi?

Je, umeshawahi kuhisi au kuwaza akiwa na huzuni anakuwaje? Kumbuka hisia ni mwitikio unaotokana na matokeo ya jambo au mambo fulani. Mtu anapo onyesha hisia zake anatuonyesha mawazo na mtazamo wake juu ya jambo fulani kwa namna lilivyomgusa na kumuathiri. Sasa ikiwa huwa tunajali hisia za wenza wetu, watoto wetu, viongozi wetu hadi tunabadilisha tabia na mwenendo wetu, kwa nini tunashindwa kujali hisia na maelekezo ya Roho Mtakatifu?.

Mbili, Jihadhari USIMZIMISHE Roho Mtakatifu – Katika 1 Wathesalonike 5:19 imeandikwa ‘Msimzimishe Roho’. Kwenye andiko hili kuna tafsiri mbili: Moja, ni kuzuia UNENAJI au MAFUNUO ya Roho Mtakatifu katika Ibada au kusanyiko na pili ni mtu kufanya UASI endelevu licha ya maonyo, jambo ambalo sio tu linamuhuzinisha Roho Mtakatifu bali linaweza kumzimisha na hivyo kumuondoa kabisa kwenye maisha yake (1 Wakorintho 14, Zaburi 78:40 na Mithali 29:1).

Tatu, Jihadhari USIMPINGE Roho Mtakatifu  – Matendo ya Mitume 7:51-52 imeandikwa ‘Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo’. Kumpinga haiishii kwenye kumkataa bali zaidi ni kumzuia asifanye alichokusudia kwa kumtengenezea mazingira ambayo yeye hawezi kufanya kazi ya kuwa Msaidizi wa mwandamu.

Tambua kwamba pale mtu anapozifanya njia zake mwenyewe, anapoatafuta yampendezayo na kusema maneno yake ndivyo anavyompinga Roho Mtakatifu na hivyo kumpa mpaka Roho Matakatifu (Zaburi 78:41). Sasa jihadhari kwa sababu yeye ndiyo mwenye kuijua njia ikupasayo kuiendea na kwamba pasna yeye huwezi kufanikiwa katika safari yako hapa duniani.

Nnne, Jihadhari usimjaribu wala kumwambia UONGO Roho Mtakatifu – Matendo ya Mitume 5:3 imeandikwa ‘Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?’. Roho Mtakatifu anaona na anazijua siri zetu zote, wala hakuna neno au tendo tufanyalo asilojua. Hivyo jihadhari usinene au kufanya mambo ya uongo ukidhani unamficha Mungu.

Kuficha au kuzuia sehemu ya thamani ya mali yao kuiligharimu maisha yao, naam  walisahau imeandikwa USIMJARIBU Bwana Mungu wako. Hebu na tijichunguze katika matoleo, maelekezo na mapatano tunayoyafunga Pamoja naye, je, tumekuwa waaminifu na wakweli katika kuyatekeleza? Je, ni mara ngapi tunafanya tofauti halafu mbele za uwepo wake tunasema na kukirii hadaharani kuwa tumefanya yote sawa na neno la Bwana?

Je, tumeshahu kile kilichompata Sauli baada ya kumjaribu na kumdanganya Bwana kuhusu Ameleki? (1 Samweli 15:20). Je, ni mara ngapi tunamdanganya Bwana katika sadaka na hasa fungu la kumi kwa kutoa pungufu halafu tunasema ni zaka kamili? Je, si yeye aliyesema leteni zaka kamili ghalani mwangu?  Kumbuka yeye haoni tu unachotoa bali anaona na kujua kile kilichoingia katika hesabu yako basi tujihadhari tusimjaribu wala kumwambia uongo Roho Mtakatifu.

Matokeo ya kutojali mazingira au maonyo haya  ni nini?

Isaya 63:10 imeandikwa Lakini wakaasi, wakamhuzunisha Roho yake Mtakatifu; kwa hiyo akawageukia, akawa ADUI, akapigana nao’na Waebrania 3:10-11 imeandikwa Kwa hiyo NALICHUKIZWA na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu; Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, HAWATAINGIA rahani mwangu’.

Hapa tunaambiwa kumbe Roho Mtakatifu anaweza akageuka na kuwa ADUI wa mtu. Ndio, sio kila vita inatoka kwa Shetani, maana unaweza ukafikiri ni Shetani kumbe Roho Mtakatifu, basi jihadhari usimkasirishe wala kumfanyia jeuri. Roho Mtakatifu kwa nafsi na nafasi yake anaweza kufanya maamuzi ikiwa ni pamoja na kuzuia mtu asiingie kwenye ufalme wa Mungu.

Tambua, Roho Mtakatifu anaumizwa sana kutokana na maneno au matendo yetu. Naam, kama vile Yesu alivyomwambia Sauli, ‘mimi ndimi Yesu unayeniudhi’ ndivyo hata leo Roho Mtakatifu anavyougua akisema mbona unaniudhi mimi, unashindwa kunitii, kujali hisia, maelekezo na uongozi wangu? Naam anajiuliza kwa nini wanadamu hawaoni athari za mambo haya wakati neno la Mungu liko wazi kuhusu matokeo ya utiifu na uasi? (Matendo ya Mitume 9:4-5).

Matendo ya Mitume 5:32 imeandikwa ‘Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio’ na Wakolosai 1:29 imeandikwa ‘Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, NIKIJITAHIDI kwa kadiri ya kutenda kazi kwake ATENDAYE kazi ndani yangu kwa nguvu’.

Basi, ndugu, tambua kuwa, utiifu ndio UFUNGUO wa kutunza na kudumisha mahusiano mazuri kati yako na Roho Mtakatifu.Tutambue kuwa, Roho Mtakatifu yu ndani yetu, anatenda kazi kutokea ndani yetu, hivyo na TUJITAHIDI kuhakikisha tunatenda au kufanya kazi kadri atakavyo au aelekezavyo yeye kutokea ndani yetu. Ndio, sisi ni vyombo tu na tupo kwa ajili ya makusudi yake na kwamba bila yeye hatuwezi neno lolote, sharti tumtii na kumpendeza.

Tambua, kiwango cha uhusiano wako na Roho Mtakatifu ndio kinaamua kiwango cha UKARIBU kati yenu kwa dhana ya mawasiliano, mafunuo, maelekezo nk. Mtu anayemfahamu vizuri Roho Mtakatifu atajilinda na kujizuia asimuhuzunishe, kumzimisha, kumpinga, kumfanyia jeuri wala kumwambia uongo, bali atahakikisha anaongeza utiifu wake kwenye maagizo yake. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, ikusaidie kujenga na kudumisha mahusiano mazuri daima na Roho Mtakatifu.

Utukufu na Heshima Vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.

Zoeken
Categorieën
Read More
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 37
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 58 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-21 09:10:49 0 5K
REVELATION
UCHAMBUZI WA KITABU CHA UFUNUO
Maana ya Ufunuo.   Neno Ufunuo kwa kiingereza ni Reveletion au Disclosure au Apokalupsis kwa...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 11:12:11 0 9K
JONAH
YONA 3
Bwana wetu YESU KRISTO ahimidiwe milele na milele. AMEN. Karibu tujifunze Neno la Mungu,...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-20 03:12:44 0 6K
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 10
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 71 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-21 03:18:48 0 5K
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Joshua 10
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 49 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 07:40:06 0 5K