MWANANGU, YULE MAMA HAKUMALIZA VIZURI SAFARI YAKE

0
5KB

Mwanangu yule mama hakumaliza vizuri safari yake!

Hivi ndivyo Mchungaji wangu, alivyoanza kunieleza kwa habari ya kifo cha mama mmoja tuliyekuwa tukisali naye. Nilimfahamu mama huyu kuanzia mwaka 2001 nilipookoka. Kwa ufupi alikuwa ni mama mwenye kumpenda sana Mungu, aliye jali ibada mbalimbali na zaidi Mwana maombi mzuri. Alikuwa ni mama ambaye ni mfano wa kuigwa kwa mambo mengi, na kwa jinsi ya kibinadamu naweza kusema alikuwa, Mshirika mwaminifu. Mama huyu aliwahi pia kuwa mmoja wa viongozi wetu.

Kuanzia mwaka 2001 hadi 2004, nilikuwa nikiabudu pamoja na yule mama. Nilipoanza chuo ndipo nikaondoka na kwenda Mkoa mwingine kimasomo. Mwaka fulani niliporudi likizo, nikaenda kanisani kwenye ibada ya jioni, nilipofika kanisani nikaambiwa ibada ya jioni ile inafanyikia kwa mama huyu kwani amefariki. Moyoni mwangu nilihuzunika kupata taarifa ile, ila nilipata tumaini na kuamini kwamba maadam alikuwa ameokoka na endapo aliendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu wake basi atakuwa yupo na Bwana akifurahi. Ndipo nikaenda kuungana na washirika wenzangu, kwenda kuwafariji familia ile kwa kuondokewa na ndugu yao. 

Kesho yake ndipo nilienda kwa Mchungaji wangu kumsalimu na pia kumpa pole kwa kupatwa na msiba huo. Baada ya kumpa pole kwa kuondokewa na mama huyo, ndipo alipoanza kwa kusema ‘Mwanangu, kwa kweli yule mama hakumaliza vizuri safari yake. Mungu ndiye ajuaye yuko wapi, ila nami pia kama Mchungaji wake, nasikitika kusema hakumaliza vizuri’. Kauli hii ilinishtua sana, nami nikamuuliza kwa nini unasema hivyo Pastor? Ndipo akaniambia yote ambayo yule mama alifanya miezi kadhaa kabla ya kifo chake (samahani kwa sababu maalum sitaweza kuandika yote aliyofanya yule mama).

Baada ya Mchungaji wangu kunielezea maisha yote ya yule mama katika siku zake za mwisho, ndani yangu niliumia sana. Naam niliumia kwa sababu kubwa mbili; Moja ni namna nilivyokuwa namfahamu na kumpenda yule mama kutokana na juhudi na imani yake katika Bwana. Mbili ni ufahamu nilionao kuhusu wapi mtu anakwenda kama hakufa katika Bwana. Maana imeandikwa ‘…Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao’ (Ufunuo 14:13)

Kama mtu hakufa katika Bwana (utakatifu) mahali anapokwenda panaitwa kuzimu.   Kuzimu ni mahali ambapo laiti mwanadamu angejua nini kinaendelea huko, si tu angemwamini Yesu, bali asingeleta mchezo kwenye wokovu na angeishi maisha ya utakatifu kuzidi maelezo. Jambo moja ambalo nina hakika nalo ni hili, endapo mtu atakufa katika dhambi zake, bila kutengeneza njia au mahusiano yake na Mungu akali hai, basi huyo atakuwa amemaliza safari yake vibaya, na kuzimu ndipo mahali ambapo ataenda.

Mpenzi msomaji, najua watu wengi hawapendi kuambiwa ukweli huu, lakini ni vema uujue kabla hujafa, ili ujifunze kuishi maisha ya kumpendeza Mungu wako. Biblia inasema ‘Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu’ (Waebrania 9:27). Je wewe utamalizaje safari yako hapa duniani? Je unajua kwamba kifo chako ndio mwanzo wa maisha mapya ya umilele? Naam maisha hayo ni ama ya mateso milele (kuzimu kisha Jehanamu) au raha milele (mbinguni kisha Jerusalemu mpya).

Wapi mtu atataka kwenda baada ya kufa anapaswa kufanya maamuzi akiwa hai. Naam si tu kuokoka bali kuishi maisha matakatifu, maana wapo wengi ambao waliokoka lakini baada ya kufa kwao wakajikuta kuzimu, na hii ni kwa sababu hawakuwa waaminifu kwa Mungu wao katika kutii amri zake. Kama unafikiri kuwa Mkristo ni tiketi ya kukupeleka mbinguni siku ukifa, badilisha fikra zako mapema, maana, mbinguni hawaendi Wakristo, bali watakatifu, naam wale wayafanayao mapenzi ya Mungu hapa duniani (Mathayo 7:21). Naam ili kuongeza ufahamu wako pia kuhusu wapi mtu huenda baada ya kufa katika dhambi bonyeza link hii http://www.spiritlessons.com/Mary_K_Baxter_A_Divine_Revelation_of_Hell.htm

Kwa maelezo ya Mchungaji wangu yule mama katika siku zake za mwisho alifika mahala pa kwenda kwa waganga wa kienyeji ili kupata msaada. Nami moyoni mwangu nilijiuliza maswali mengi kwamba, kwa nini alienda kwa waganga wa kienyeji kutafuta msaada? Je, ni kweli Mungu wake aliyemwamini siku zote alishindwa kumsaidia? Kwa nini aliruhusu Shetani amdanganye kiasi hiki, kama Hawa alivyodanganywa?      (Mwanzo 3:1-19). Ndipo nikajua kuna mahali yule mama alimpa Ibilisi nafasi (Waefeso 4:27) na Shetani akatumia nafasi hiyo ili kuhakikisha mama yule anamaliza vibaya.

Nilipozidi kutafkari juu ya jambo hili, ndipo nikakumbuka kile ambacho Mtume Paulo aliwaambia Wagalatia akisema ‘Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambaye Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulubiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho mnataka kukamilishwa katika mwili? (Wagalatia 3:1-3).

Ukisoma vizuri sentensi za Paulo ambazo nyingi zipo katika mfumo wa maswali ni ishara kwamba Paulo mwenyewe alikuwa haamini kile ambacho anakiona kinatokea kwa Wagalatia. Kwani alijua walivyoanza vizuri na Bwana, lakini hali yao ya mwisho ilikuwa ni mbaya tena ya mwilini. Kwa sababu hii Paulo akaugua sana rohoni, ndipo ikamlazimu kutumia lugha ngumu (kali) sana ili kuwasaidia. Naam kwa andiko hili tunajua kwamba mtu anaweza akaanza safari yake vizuri na kisha akamaliza vibaya, ndiyo maana Mhubiri 7:8a naye anasema ‘Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake…’

Ni huzuni kubwa sana kwa mtu aliyemjua Mungu halafu akarudi nyuma na kumaliza katika mwili. Mpendwa wangu jifunze kuchunga na kutunza mguu wako katika Bwana ukiwa makini wapi unakanyaga. Ni vema tumruhusu Roho Mtakatifu atuongoze na kutufundisha njia itupasayo kuiendea, huku tukiwa watiifu na waaminifu kwake (Zaburi 32:8). Neno la Bwana na liongoze hatua zetu ndani yake kwa kuwa imeandikwa ‘Neno la Bwana ni taa ya miguu yangu’ (Zaburi 119:105). 

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nawe kukusaidia.

Rechercher
Catégories
Lire la suite
OTHERS
KUMBE ALLAH NDIE MWANZILISHI NA ANAYE TOA MAGONJWA KWA BINADAMU
1. Allah akiri kuwa yeye ndie anaye anzisha magonjwa.2. Allah aliugua Macho.3. Allah hana uwezo...
Par MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 05:47:48 0 5KB
NDOA KIBIBLIA
UKIITWA NA MUNGU KATIKA HUDUMA JIHADHARI USIOE AU KUOLEWA NA MWENZA WA UFALME WA GIZA
Biblia katika Waefeso 4:11-12 inasema ‘Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine...
Par GOSPEL PREACHER 2021-11-19 07:59:25 0 6KB
1 SAMUEL
Verse by verse explanation of 1 Samuel 15
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 36 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-01-26 03:46:33 0 5KB
1 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 1 Chronicles 7
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 32 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-03-20 04:43:04 0 5KB
JOSHUA
Verse by verse explanation of Joshua 6
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
Par THE HOLY BIBLE 2022-01-25 07:24:02 0 5KB