KWA NINI WAAMINI WENGI WANATESWA NA VIFUNGO VYA UOVU?

0
5K

Waamini wengi wana changamoto kuhusu suala zima la uponyaji na kufunguliwa katika vifungo mbalimbali kama vile magonjwa, mapepo, ndoto mbaya, ndoto za mapenzi, kutozaa, kutoolewa, kutoajiriwa, kutengana, umaskini, kuonewa, kufeli nk. Wengi wamekuwa wakijiuliza ikiwa  nimeokoka kwa nini naendelea kuonewa na kuwa mtumwa wa mapepo kiasi hiki? Wengine kwa kutoona uponyaji wa Mungu juu yao wamefikiri Mungu ameshindwa kuwasaidia na hivyo kutafuta uponyaji nje ya Mungu. 

Ndio, watu wengi wameshindwa kujua kwa nini wanaendelea kuteswa na vifungo vya uovu ikizingatiwa wana jitihada nzuri  katika kuhudhuria ibada, utoaji, maombi, kusoma neno la Mungu, kusaidia wengine nk. Ujumbe huu unakuja ili kukuonyesha sababu zinazopelekea watoto wa Mungu waendelee kuteseka licha ya kuwa wameokoka.

Shetani ni baba wa uongo na ni mwerevu sana katika utendaji wake. Kupitia na kwa kutumia dhambi ameendelea kuwashikilia wengi katika vifungo vya uovu na mateso mbalimbali juu ya miili yao licha kwamba wameokoka. Shetani anafahamu vema nafasi na matokeo ya dhambi kwa watoto wa Mungu na hivyo kazi yake kubwa ni kuwatengenezea mazingira ya wao kuasi . Ndio, kumfanya mwanadamu atende dhambi ndio kipaumbele chake.

Katika ulimwengu wa roho, dhambi ni MLANGO wa uharibifu ambao Shetani huutumia ili kuharibu maisha ya mwanandamu. Naam, ili Shetani aingie ni lazima kwanza atengeneze njia kwa mtu husika. Pale mtu anapotii wazo la ufalme wa giza na kutenda dhambi, anakuwa amefungua mlango ambao Shetani atautumia kuharibu mahusiano ya mtu huyo na Mungu wake na hivyo kuruhusu laana na mabaya.

Sasa zifuatazo ni baadhi ya sababu ambazo hupelekea wanadamu kuendelea kuteseka katika vifungo mbalimbali vya uovu pamoja na kukiri kuwa wameokoka:

  • Kuficha dhambi – Katika Mithali 28:13 imeandikwa ‘Afichaye dhambi zake HATAFANIKIWA; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema’. Je unaweza kumuombea mtu anayeficha dhambi akapokea baraka au uponyaji, wakati ameficha dhambi na dhambi ni uasi?. Ikiwa Mungu amesema afichaye dhambi zake hatafanikiwa, kwa nini unategemea ufunguliwe au kupokea uponyaji bila kutengeneza kwanza na Mungu wako? Je, dhambi yako haikushuhudii ndani yako na kwamba ukitenda vema utapata kibali?
  • Kurudisha mabaya badala ya mema – Mithali 17:13 imeandikwa ‘Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya HAYATAONDOKA nyumbani mwake’. Katika Isaya 48:22 imeandikwa ‘Hapana amani kwa WABAYA, asema Bwana’ Je, unawezaje kutarajia mafanikio, baraka au uponyaji katika mazingira ya kweli hizi? Sharti tujifunze kusamehe, tuchukuliane, tudumishe pendo la Kristo na tudumu katika kuomba na kutenda mema. Ndio, kwa njia hii tutafungua mlango wa mema au baraka kutujia, vinginevyo mabaya yatakuwa sehemu yetu.
  • Uasi didi ya sheria za Mungu (1 Yohana 3:4-8)  – Kuasi ni kukiuka au kuvunja sheria zilizowekwa na Mungu. Naam kuasi ni kutozitambua sheria wala yeye aliyeziweka na hivyo kuonyesha dharau kwa yeye aliye mtakatifu. Mtu anapoasi anakuwa amechagua kuwa mali ya Shetani na kukataa utawala wa Mungu na hivyo kumhuzunisha na kumsairisha sana Mungu.

Kutokana na Isaya 59:1-2 dhambi inamtenga Mungu na watu, naam inamzuia Mungu kuwaponya, kuwasikiliza na kuwaponya watu wake. Ndio, dhambi inazuia sauti na mafunuo ya Mungu juu ya mwandamu. Sasa katika mazingira kama haya, utategemea mwanadamu aone uponyaji au kufunguliwa katika vifungo vyake vya uovu?  Kumbuka imeandikwa ‘Kwa sababu hiyo hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu’ (Isaya 59:9).

Dhambi inakata na kuharibu mahusiano na mawasiliano kati ya mtu na Mungu. Ndio, uasi kwenye sheria za Mungu unatengeneza mpenyo, mlango na njia  ya laana kupita na kumpata mtu. Daima dhambi huleta gadhabu ya Mungu, maana kwa kuasi mtu anakuwa amemkataa, hamtambui na amemdharau Mungu (Wakolosai 3:5-6, Kumbukumbu la Torati 28:15-16).

Hebu tone mifano kadhaa:

Mfano wa kwanza: Watu waliokataliwa na Mungu kwa sababu ya uasi – Katika Yeremia 7:16 imeandikwa ‘Basi, wewe USIWAOMBEE watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala USINISIHI kwa ajili yao; kwa maana SITAKUSIKILIZA’ na pia Yeremia15:1 imeandikwa ‘Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; WATUPE, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao’.

Hii ni kutufundisha kwamba, Mungu anaweza kumkataa mtu au watu kutokana na uasi wao. Wapo baadhi ambao kuna mapigo au laana zimeachiliwa juu yao aidha kwa muda au milele na ndio maana hawapokei uponyaji wala kufunguliwa. Je, unawezaje kumbariki yule ambaye BWANA amemkataa? Hivi ndivyo BWANA alimvyojibu Samweli akisema utamlilia Sauli hata lini ikiwa mimi nimemkataa? Kumbuka imeandikwa ‘Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea?’… (1 Samweli 2:25a).

Mfano wa pili: Laana juu ya nyumba ya Kuhani Eli (1 Samweli, sura ya 2 hadi 4). Ukisoma fungu hilo utaona uasi wa watoto wawili wa kuhani Eli, Hofni na Finehasi sambamba na matokeo ya uasi wao. Kufuatia uasi wao, watoto wote wawili walikufa  siku moja, Mungu alifuta rasmi ukuhani kwa nyumba ya Eli, naam aliweka ukomo wa umri wa wao kuishi kwamba hapatakuwa na mzee kwao na mwisho waliosalia kwenye jamaa yao walikuwa vibarua na omba omba.

Kupitia mifano hii hebu  jiulize, unatarajiaje kufunguliwa au kuona watu wakiponywa ikiwa Mungu ameshasema mimi nimewakataa, hata ukiomba sitakusikiliza?  Mwenyewe amesema hakutakuwa na mzee kwao, unawezaje kuwaombea waishi miaka mingi? Naam, ikiwa yeye amewaondolea ukuhani, wewe unawezaje kuwatia mafuta? Hapa ni tuhakikishe tunajizuia kufanya uasi ili Mungu asifikie hatua ya kutoa matamko mazito kiasi hiki juu yetu, uzao wetu na hata taifa letu.

Uasi ndio sababu kuu kwa nini watoto wa Mungu wanateseka na bado wapo kwenye vifungo licha ya kuokoka. Naam kwa vinywa vyao wanakiri wokovu lakini mioyo yao iko mbali na Mungu. Ndio, kwa macho na mizani ya kibinadamu ni watakatifu, lakini kwa mioyo yao ni wachafu na ndio maana mabaya hayaondoki kwao, naam wana majina ya kuwa hai, lakini wamekufa. Ndugu zangu, kupitia ujumbe huu, Yesu anatuita tutengeneze njia zetu na maisha yetu kungali mchana.

Ndio, uasi kwenye neno la Mungu ndio mlango mkuu wa uharibifu na mabaya yote kwenye maisha yetu, naam dhambi inatoa uhalali wa vifungo vya uovu kushikila na kutesa watu. Laiti macho yetu yangefunguka tukaona mwitikio wa Mungu kwetu pale tunapotenda dhambi TUNGEACHA mara moja. Basi ndugu zangu na tujizuie  kufanya uasi dhidi ya sheria zake huku tukidumu kuwa watu wa toba na kutengeneza njia zetu kila iitwapo leo, tukijua yeye aliyetuita ni mtakatifu.

Utukufu na Heshima vina wewe Yesu, Wastahili BWANA.

Buscar
Categorías
Read More
Injili Ya Yesu Kristo
MAANA YA KANISA
Kwanza kabisa neno Kanisa linamaanisha "mkusanyiko wa waamini" kama ule wa Waisraeli chini ya...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 21:00:38 0 5K
FORM 1
CHINESE: FORM 1
List of all topics in Chinese : for form 1 class: COMMING SOON GREETING AND SELF INTRODUCTION...
By PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-30 05:01:18 0 5K
JOSHUA
Verse by verse explanation of Joshua 13
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 08:09:48 0 5K
OTHERS
UONGO WA AYA ZA QURAN KUHUSU UKRISTO KUTOA DHABIHU YA WANYAMA
"Dhabihu" hufafanuliwa kama sadaka ya kitu cha thamani kwa ajili ya kusudi au sababu. Kufanya...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 02:03:08 0 4K
Injili Ya Yesu Kristo
Yesu alikuwa wapi katika siku tatu toka siku ile ya kufa mpaka kufufuka?
Kama Yesu alivyotabiri, alisalitiwa na mmoja wa wafuasi wake, Yuda Iscariot, na alikamatwa....
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 09:39:59 0 5K