UCHAMBUZI WA KITABU CHA UFUNUO

0
9KB

Maana ya Ufunuo.

 

Neno Ufunuo kwa kiingereza ni Reveletion au Disclosure au Apokalupsis kwa kiyunani Apokalupsis  Maana yake ni Mungu kujiweka wazi, au kujifunua kupitia uumbaji wake, Historia, Dhamiri ya mwanadamu na Maandiko kwa msingi huo linapotumiwa katika maandiko hutumiwa kwa maana mbalimbali tofauti na hakuna maana maalumu, Maneno makuu mawili ya kiyunani hutumika katika Biblia yaani Apokalupsis na Faneroun fanerou'n  ambalo maana yake ni yaliyo juu ya uweza wa kibinadamu, au yaliyo zaidi ya kufunuliwa, ni kupitia maneno haya makuu mawili ndio tunapata maana ya neno Ufunuo ambao kwa maneno ya kufupisha tunaweza kusema ni kuwekwa wazi kwa Maswala ambayo mwanzoni yalikuwa hayajawekwa wazi.

 

Kitheolojia ufunuo unaweza kuzungumziwa katika maana kuu mbili ufunuo wa Mungu wa Ujumla General or Naturral Reveletion na Special Reveletion. Ufunuo wa ujumla wa Mungu ni ushahidi wa kuweko kwa Mungu kwa wanadamu wote waliojuu ya uso wa Inchi kupitia uumbaji, Historia na dhamiri ya mwanadamu. Jambo hili linaweza kuthibitishwa na Maandiko kama Zaburi ya 19;1 Mbingu zahubiri utukufu wa Mungu na anga latangaza kazi ya mikono yake, Matendo 14;8-18,17:16-34, Warumi 1;18-32,2;12-16 na mistari mingine mingi. Dhana hii inakubalika na baadhi ya wakatoliki na waprotestant kwamba ni ya ufunuo wa ujumla ambao unamthibitishia mwanadamu kuwa Mungu yuko bila kuhusisha maswala ya imani bali kwa kujihoji Reasoning, wakati ufunuo maalum ni ule unaotokana na msaada wa Mungu ambao hupatikana kwa imani na uzoefu tu kupitia maneno ya Mungu. Ufunuo huo wa ujumla hauna msaada katika kumuwezesha mwanadamu kuokoka lakini kumfanya asiwe na udhuru kuwa hakuna Mungu.

 

Kwa ujumla ufunuo wa asili au ufunuo wa ujumla umejengwa katika misingi ya jumla ya kuthibitisha tu kuwa Mungu yupo lakini ni ufunuo usiotosheleza kwa habari ya kuleta wokovu lakini angalau unaweza kumsaidia mwanadamu kuwa na ufahamu huo kwa kuanzia, inasemekana kuwa hata wale wanaofikia hatua hii kwa namna Fulani wanajua hayo kupitia imani ingawaje eneo kubwa ni kwa kutumia akili, wakati dhana ya Ufunuo unaotokana na Mungu inajifunua kupitia Historia ya matukio ya kweli ya wokovu na ufunuo utokanao na ujuzi halali wa maandiko.

Baadhi ya wasomi huamii kuwa ufunuo Haufanani wala hauko sawa wakati wote na wanaamini kuwa hata Biblia yenyewe ni Matokeo ya ufunuo na ni nukuu za mafuno kwa watu waliokuwa wakijaribu kumtafuta Mungu na wakajaribu kumuelezea kwa ufahamu wao kupitia kazi za namna alivyojifunua kwa hiyo wao huamini kuwa ufunuo  hutokea wakati Mungu anapojifunua yeye mwenyewe kwa mtu na mtu huyo anapoitikia mwitikio wa Imani katika Kristo kwa hiyo Biblia kwao ni kiongozi tu wa uzoefu huo wa kimafunuo lakini yenyewe sio ufunuo kamili.

 

Maana ya ufunuo kwa Mtazamo wa Kibiblia.

Hatima ya ufunuo wa aina yoyote ile Bado ni makusudi ya Mungu kutuleta kwake ili tupate kumfahamu yeye, Mungu kujifunua kwa mwanadamu hakutegemeani na mfumo au kanuni maalumu au mfumo Fulani wa kimafundisho msingi wa kwanza ni mtu Binafsi kukutana na Mungu na hivyo kibiblia hata kukutana na kumfahamu Mungu wa kweli ni ufunuo hii ni kwa sababu .

  • Mwanadamu kuwa na ujinga wa kutokumfahamu Mungu ni sawa na Ujinga wa kutokujifahamu yeye mwenyewe hivyo kama mtu hamjui Mungu hawezi kujijua yeye mwenyewe.
  • Mwanadamu ana hatia anayotembea nayo inayomuhukumu kuwa amemkosea Mungu na hivyo ufunuo wa kweli katika kristo sio tu unampa maarifa bali unamkamilisha katika utakatifu na rehema na msamaha wa Mungu

Ufunuo wa Kibiblia ni ufunuo wa Mungu na matendo yake ya kweli kihistoria, Mungu alikamilisha mpango wake wa kumuokoa mwanadamu na mpango huo ulikamilishwa katika Yesu Kristo. Kwa msingi huo Hakuna Yesu Kristo wa Imani tu Lakini Pia tunaye Yesu Kristo wa Historia kwa hiyo “hakuna imani katika Kristo kama hakuna Kristo katika Historia”, Kwa hiyo Historia ya Kibiblia ni historia ya kile ambacho Mungu amesema na kutenda Mika 6;5 na Kristo ndiye ukamilifu wa Historia.

Agano la kale ni ufunuo uliokuwa unategemea kuja kwa Yesu Kristo na Agano jipya ni ufunuo unaoakisi na kuthibitisha ukweli wa ujio wa kristo. Kwa msingi huo kufanyika mwili kwa Bwana Yesu ndio ufunuo kamili wa Mungu na ndio kiini cha Injili Warumi 1;3,16, 1Wakoritho 15;1-4, Wagalatia 4;4, Waebrania 1;1,2, Ni wazi kuwa Mungu alijifunua kwa wanadamu kuhusu mpango huo wa wokovu kwa njia nyingi na kwa namna mbalimbali Waebrania 1;1-2 kwa hiyo ingawa ufunuo wa Mungu umekuja katika mwana wake kwa ukamilifu lakini Mungu alijifunua kwa njia mbalimbali kwa hiyo uko ukweli kuwa Mungu amejifunua pia kwa wanadamu kwa njia ya uumbaji, Historia na dhamiri ya mwanadamu yaani ufunuo wa jumla.

 

Ufunuo wa Kibiblia maana yeke ni ufunuo katika neno lake ni mkusanyiko wa matendo ya Mungu aliyoyatenda na kusema akiwasiliana na wanadamu katika njia maalumu na ujumbe wa agano jipya ni tafasiri ya matendo yake ufunuo huo wote wa agano la kale na agano jipya umefungwa katika tukio kuu la Ukombozi wa mwanadamu, Paulo anaonyesha kuwa Hata agano la kale lilikuwa likizungumzia tukio hilo la ukombozi wa mwanadamu 1Koritho 15;3-4 ni wazi kuwa wakati huu alipokuwa akinukuu maneno kama yanenavyo maandiko alikuwa akimaanisha Agano la kale kwamba nalo lilikuwa linaona kwa mbali ukombozi ukikamilisha katika kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu kwa hiyo Historia ya wokovu Kerygma katika agano jipya ni muendelezo wa kazi ya ufunuo ulioanza katika agano la kale hivyo neno la Mungu ni ufunuo wa wokovu kwa maana ya agano la kale na agano jipya.

 

Kwa msingi huo Ufunuo wote wa matukio yaliyopita, yaliyopo na yajayo yanakamilishwa katika tukio moja la Kufufuka kwa Bwana Yesu na hivyo Mungu amajifunua kwa msingi wa maswala yajayo kwa kiwango cha juu katika kristo na kwa mujibu wa Waebrania 1;2 kufanyika Mwili kwa Kristo kunakamilisha maswala ya ufunuo wa tulikotoka tuliko na tuendako ufunuo huo sasa unakuja kwa wanadamu kupitia neno lake yaani Biblia kwa hiyo Biblia sio tu muelekeo wa Ufunuo lakini yenyewe ni Ufunuo kamili

Ili ufunuo uweze kueleweka unapaswa kueleweka kwa kupitia kweli kuu Tatu

  • Mfunuaji ambaye kwa uwazi ni Mungu
  • Njia ya ufunuo ambayo ni maandiko na katika maandiko haya tunaambiwa kuwa Mungu alijifunua kwa Njia mbalimbali ambazo ni maono, Ndoto, usingizi mzito, Urim na thumim, kura, Muonekano wake mwenyewe akijidhihirisha theophanies, kupitia malaika, mazungumzo ya kiungu, historia na matukio na neno la Mungu au Kristo Yesu mwenyewe.
  • Mwisho Mpokeaji yaani mwanadamu ambaye amejiweka katika utayari wa kupokea na kushuhudia

Biblia hata hivyo ni matokeo matukio ya ufunuo wa Mungu ambapo anadhihirisha mpango wake wa ukombozi wa mwanadamu kupitia Yesu Kristo Katika neno Mungu anawasiliana na mwanadamu aliyeanguka ingawa uwazi kabisa wa ufunuo huo huja kwa muitikio wa imani wa kazi zilizofanyika lakini mwitikio huo hauwi wa aina binaamu mwenyewe kwa matakwa yake bali ni kazi kamili ya zawadi na msaada wa Roho Mtakatifu kazi hiyo ya ndani ya moyo wa mwanadamu inayompa uwezo wa kupokea ufunuo huo huitwa illumination au Estimoium kwamba mtu anaweza kukulia katika maandiko na kufunzwa katika maandiko lakini neno la Mungu likawa halijafunuliwa kwake 1Samuel 3;7 kwa hiyo ingawa Mungu alizungumza na Samuel zaidi ya mara tatu lakini halikuwa neno la Mungu kwake ni mpaka mara ya nne ndipo Samuel alipoweza kuelewa na neno la Mungu likawa neno la Mungu kwake, Ni mpaka mtu awe na uwezo wa kusikia na kupokea  kwa moyo ndipo kweli ya Mungu inapokuwa yake 1Thesalonike 2;13.

 

Mamlaka kubwa ya maandiko inatokana na kuvuviwa kwake na hivyo lafaa kwa mafundisho, kwa konya na kusahihisha na kutoa mafunzo ili kuwakamilisha watu wa Mungu 2Timotheo 3;16-17 kwa hiyo Biblia ni ya kimungu au ni ya Mungu kwaasili ingawa Mungu aliwatumia wanadamu kuiandika na waliandika ujumbe kamili kutoka kwa Mungu lakini uelewa kamili wa uvuvio huo lazima upokelewe katika mtazamo sahii wa Ufunuo kwa msingi huo awaye yote anayeisoma Biblia anapaswa kujua kwanza msomaji alikuwa anakusudia nini kwa wasomaji wake wakati huo, kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa mtu anapoisoma Biblia kwanza anapaswa kusikiliza baada ya kuelewa ujumbe uliokuwa ukizungumzwa na ujumbe kwa asili ulihusu nini ndipo unapaswa kujiuliza jinsi ujumbe huo unavyomuhusu kwa wakati alionao lakini hii ni hatua ya pili.

Ufunuo ni lazima utofautishe na maswala mawili Uvuvio (Inspiration) na kuangaziwa (illumination). Ufunuo ni mawasiliano ya taarifa kutoka kwa Mungu kumjia mwanadamu aliye katika hali ya anguko ili ajue kile ambacho Mungu anakisema au anakifanya kwaajili yake, Uvuvio unahusika na swala la Roho wa Mungu kuwatumia wanadamu kuandika kwa mamlaka yale aliyokusudia wanadamu wawe nayo katika neno lake, lakini ingawa maandiko yote yamevuviwa sio maandiko yote ni ufunuo ila tunaweza kuzungumza kwa ujumla wake tu kuwa maandiko ni ufunuo kamili wa Mungu kwaajili ya kuwasaidia wanadamu kumjua na kwaajili ya utukufu wa Mungu.

Kuangaziwa yani illumination ni kazi ya Roho Mtakatifu kumuwezesha msomaji wa neno la Mungu kuwa na uwezo wa kuelewa maandiko akisaidiwa na Roho Mtakatifu 1Koritho 2; 13-14 kwa hiyo katika ufunuo Mungu anafunua kweli zilizokuwa zimejificha lakini katika kuangaziwa iilumination aliyeamini anawezeshwa kuelewa. Kwa hiyo Ufunuo ni Namna alivyowasilisha, Uvuvio ni jinsi alivyowasilisha na kuangaziwa ni kwanini aliwasilisha hii inakuja kwa msaada wa Roho wa Mungu.

 

 

KITABU CHA UFUNUO WA YOHANA

Neno ufunuo kama tulivyogusia awali ni neno linalotokana na lugha ya asili ya Kiyunani Apokavluyi  yaani Apocalypse ambalo maana yake ni Kuweka wazi au kufunua kwa msingi huo kitabu hiki kiliitwa The Apocalypse of John na sawa na neno hilo la Kiswahili Ufuno wa Yohana, hiki ni kitabu cha Mwisho katika mfululizo wa Vitabu vya Agano jipya, ni kitabu cha kipekee sana ukilinganisha na Vitabu vingine kwa ujumla, pekee katika Agano jipya ndio kitabu ambacho kinafanana kwa nguvu na Vitabu vya unabii kama Ezekiel, Daniel na Zekaria na kama ilivyo kwa Vitabu hivyo mwandishi alikuwa na kundi la watu waliokuwa wakizungukwa na mateso na dhiki, Ufunuo ulikuwa ni waraka kwa wakristo wa nyakati za karne ya kwanza, wakati wakristo wakiwa wametengana na dini ya kiyahudi na wakiwa wanatambuliwa kama kundi linalojitegemea kwa Serikali ya Kirumi.kwa hivyo kitabu cha ufunuo ni kitabu cha maswala yaliyokuweko na zaidi sana maswala yajayo it is an escatological book.

 

UFAHAMU KUHUSU KITABU CHA UFUNUO.

 

  1. Ufahamu kuhusu Historia ya kitabu cha ufunuo
  • Historia
  • Jamii
  • Dini
  1. Umoja
  • Mwandishi
  • Tarehe ya uandishi
  • Mahali
  • Makusudi
  • Muda
  • Malengo
  1. Kupitishwa kwenye kanuni
  • Kutambuliwa kwa kitabu cha Ufunuo.
  • Msimamo wa kanisa la Magharibi.
  • Msimamo wa kanisa la Mashariki.
  • Kukubalika kwa ujumla.
  • Jinsi ya kutafasiri litabu cha Ufunuo.
  • Theolojia katika kitabu cha Ufunuo.
  • Mgawanyo kamili.

 

Ufahamu kuhusu Historia ya kitabu cha ufunuo

Historia.

Mazingira ya Kitabu cha ufunuo yanachukua eneo la utawala wa Rumi ya zamani katika jimbo la Asia  ndogo  Asia minor, kulikuwa na uzushi wa kila aina ambao ulikuwa umefunika mazingira hayo pamoja na imani Potofu na Kanisa lilikuwa linapitia changamoto za Udunia na theolojia za kidunia kuingia katika imani, Ibada za sanamu, lakini pia kulikuwa na mafanikio makubwa sana ya kiuchumi, kulikuwa na majengo makubwa ya Miungu, waabudu, na watengenezaji wakubwa wa sanamu, utoaji wa sadaka kwa miungu, pamoja na hayo watawala wakubwa kama Nero (AD 54-68) na Domitian (AD 81-96) walikuwa waefikia kiwango kikubwa cha madai ya kutaka kuabudiwa na hivyo kuharibu aina nyingine za imani, Wakristo walikuwa wakikataa kuabudu wanadamu jambo lilolosukuma kuingia katika mateso na kudhalilishwa kwa hali ya juu kutokana na imani yao.

Jamii.

Msukumo wa dini hizi jamii na aina ya siasa na matukio tofauti tofauti yalisukuma na kuzalisha kanisa la kikristo kuwa na maamuzi magumu, na ili kanisa liendelee kuweko na kujitambua au kutambulika kama kanisa liliamua kuwa na msimamo, Mwandishi wa kitabu cha ufunuo alikuwa ametengwa na jamii kwaajili ya Imani na haishangazi kuona maandiko yake yakifunua uharibifu mkubwa wa utawala wa kirumi, tabia zao mavazi yao na hulka ya ukahaba mavazi yao mekundu na ya rangi ya dhambarau tabia ya mauaji mfano nikamwona mwanamke amelewa kwa damu ya mashahidi wa Yesu Ufunuo 17;6 ingawa maneno ya unabii yanaweza yakahusu nyakati nyingine lakini unapata picha ya mazingira ya wakati ule na kanisa na hali zake.

Dini.

Utengano mkubwa wa Ukristo na Dini ya kiyahudi ulikuwa mpana mara baada ya anguko la Yerusalemu mwaka wa 70 AD. Wakati ule Kanisa na sinagogi la kiyahudi walianza kuwa na muelekeo tofauti Fundisho la kuhesabiwa haki kwa imani nje ya matendo ya sheria lilikuwa ni kama upanga kwa wanasheria wa kiyahudi (Orthodox Judaism) na waamini wa Kikristo na kuharibiwa kwa hekalu mwaka wa 70 kuliharibu kabisa hata uhusiano mwembamba uliokuweko kati ya wayahudi na wakristo na kuharibika kwa uhusiano na kulaumiana na kushitakiana ndiko kulikopelekea kuweko kwa lugha kama Sinagogi la shetani Ufunuo 3;9 na matokeo yalikuwa ni kuachana kabisa kwa dini hizi mbili. Ndani ya kanisa kwenyewe kulikuweko matatizo ambayo yanaakisi katika barua zile kwa makanisa yale saba ya asia ndogo. Upendo ulikuwa umepoa, mmomonyoko wa kimaadili, Mafundisho potofu ambayo yalichochewa na waalimu wa uongo, kuongezeka kwa anasa na starehe na kadhalika Ufunuo ni kitabu ambacho pia kilikuwa kinajaribu kuamsha hisia za kumpenda Bwana na kuwapa maonyo wasomaji na kuwaandaa kwa ajili ya ujio wa Yesu Kristo na Hukumu ya mwisho pia kutia moyo kuwa hatimaye Mungu atakomesha siku moja uovu na huzuni na kiburi cha ulimwengu na amani ya kweli itatawala dunia.

 

Umoja.

 Mwanatheolojia R.H.Charles ambaye ameandika Commentary kubwa inayohisika na maswala ya Ufunuo kwa undani sana anachangia kuwa Mwandishi alikufa alipokuwa amekamilisha kuandika ufunuo 1 - 20;-3 katika kazi yake na shughuli ya umaliziaji iliwekwa katika mfululizo wa kazi zake na mwanafunzi wake mmoja mwenye akili kwa kufuata utaratibu alioubuni kuwa utahitimisha sawia mawazo yeke. Charles anaeleza kuwa Kitabu cha ufunuo kimepangiliwa katika mfumo wa mawazo yanayobebana kwa ufasaha jambo linaloleta umoja mpangilio na mtindo unaoonyesha umoja. Maono yote kwa ujumla yamelenga katika kiti cha enzi cha Mungu kama chanzo cha maono hayo na kwa vyovyote vile inaonekana kabisa kuwa mpangilio wake unatoka katika chanzo kimoja namna mawazo yanavyojegwa na tabia ya usafi wa maono yenyewe unadhihirisha wazi kuwa muandishi alikuwa Patmo utumwani na kuwa ujenzi wa mawazo ya ndani utangulizi wa kila waraka ulioandikwa kwa makanisa yale saba unalenga katika maono yele aliyoyaona mwandishi kuhusu Kristo na namna anavyohitimisha kwa ahadi ni wazi kuwa ahadi izo zilikuwa zinalenga ule mji mtakatifu wa Mungu ambao anahitimisha nao aidha mpangilio wa matukio na hatua za hukumu kutoka moja hata nyingine utaratibu wa kufunguliwa kwa muhuri  na ufafanuzi wae toka sura ya 5-mpaka – ya 20 hata kama kuna muingiliano Fulani haviaharibu umoja wa uandishi huo wa msingi wa uhalisia kuwa kitabu hiki kina umoja na kuwa kimeandikwa na mtu mmoja.

Mwandishi.

Mwandishi najaitambulisha kamaYohana amejiita Mtumwa wa Yesu Kristo ndugu wa wote wenye kuushiriki mateso na ufalme na subira ya Kristo Ufunuo 1; 1, 9 maono anayoyawakilisha kwenye kitabu hiki alionekana kuyapokea akiwa huko Patmo ambako alipelekwa utumwani kwaajili ya Jina la Yesu au imani ya Kikristo alifahamika kwa makanisa mengi ya Asia ndogo na aliwekwa katika daraja la Manabii Ufunuo 22:6, 9, 19, huyu ndiye mwandishi aliyeandika kitabu cha Ufunuo

Simulizi za kijadi zinaeleza kuwa mwandishi ni Yohana mwana wa Zebedayo ambaye pia ni mwandishi wa injili ya Yohana na nyaraka tatu zilizoitwa kwa jina lake Mwanatheolojia

  • Justin Martyr aliyeishi AD 150 alisema hivi Ufunuo umeandikwa na mtu mmoja miongoni mwetu ambaye jina lake aliitwa Yohana mmoja wa mitume wa Yesu Kristo.
  • Irenaeus Askofu wa Lyons alithibitisha kwa nakala nyingi zilizokuwa tayari kama ushuhuda kutoka kwa watu waliomuona Yohana Uso kwa uso
  • Tertulian aliyeishi AD 200 alielezea Ufunuo kama kitabu kilichoandikwa na Yohana na alimtambua Yohana ambaye alikuwa moja wa mitume wa Bwana
  • Origen AD 225 alichangia kuwa mwandishi ni Yohana mpaka karne ya pili na ya tatu Ufunuo wa Yohana kilianza kukubaliwa na makanisa na wasomi kama huko Alexandria
  • Ufafanuzi wenye kuonyesha mlengo mkubwa kabisa wa kuwa Yohana ndiye mwandishi ulitolewa na Dionysius wa Alexandria ambaye alikubaliana na mawazo mengi ya kijadi au masimulizi ya kijadi kwamba Yohana ndiye mwandishi alisema kuwa Ufunuo unajikiri wazi kuwa Yohana ndiye mwandishi wakati injili na nyaraka zake hazifanyi hivyo alisema misamiati na muundo wa Lugha na maarifa una nguvu za kuthibitisha kuwa Yohana ndiye mwandishi ingawa wengine wanahoji kuwa kitabu hiki kiliandikwa kwa mpangilo wa grama nzuri na fasaha za kiyunani jambo linalotia shaka kama Yohana Mwebrania ndiye aliyeandika.
  • Eusebius akifuata nyayo za Dionysius alihoji mamlaka ya kitabu cha ufunuo alichangia kuwa ni kweli kuwa Injili na nyaraka za Yohana hazikuwa na majina lakini zilithibitishwa kuwa zake na wale waliomjua na kuzipokea nyaraka zile  alisema zenyewe zinabeba ushahidi kuwa ni neno la Mungu na zinashuhudia wazi kuwa ziliandikwa na mtu ambaye alimuona Yesu kwa jicho lake Yohana 1;14, 21;24, ni wazi kuwa hata kama ufunuo kinataja jina la Yohana anayedhaniwa siye mwana wa Zebedayo lakini kuna maelezo yaliyo wazi katika Ufunuo 1;2 kuwa aliyeandika alimshuhudia Yesu wazi wazi kwa kumuona. Kwa msingi huo hata kama mtindo wa uandishi unaweza usikubaliane haimaanishi kuwa basi mwandishi wa injili na zile nyaraka siye mwandishi wa Ufunuo.
  • Mabadiliko ya misamiati wa uandishi katika nyaraka na injili tofautia na ufunuo unaweza ukachangiwa na maswala kadhaa kwa nini kuna tofauti kubwa Injili imenukuu habari za Yesu na ni wazi kuwa habari za Bwana Yesu mwana wa Zebedayo aliandika akikumbuka matukio ya siku nyingi wakati Yesu alipoishi duniani tena katika mtazamo wa Kikristo wakati ufunuo kiliandikwa mwandishi akiwa katika hali ya migandamizo Stress tena mwandishi akiwa utumwani au gerezani na kumbuka alichokuwa anakiandika ni maono. Injili iliuwa ikishughulikia mazingira yaliyokuwa sahii ya amani na mwandishi alikuwa akishuhudia wazi yaani iliandikwa katika mazingira ya maisha ya kawaida, Lakini ufunuo umejaa maono, ishara vitu vigeni watu wageni, viumbe vigeni na mazingira ambayo yalizingirwa na uwepo wa kimungu, lakini pamoja na hayo bado kuna kufanana kukubwa kwa matukio ya ufuno na uandishi wa Yohana
  • Alimuita Yesu kwa namna ileile aliyozoea kumuita Neno la Mungu Yohana 1;1 Ufunuo 19;13.
  • Alimuita mwanakondoo Yohana 1;29 Ufunuo 5;6
  • Mchungaji Yohana 10;11 Ufunuo 7;17
  • Anavyomzungumzia shetani ni kwa namna ileile Yohana 8; 44, 27, 14; 30, Ufunuo 2; 10, 12; 9, 20; 2, 7, 10.
  • Kisha msisitizo wa Kifo cha Yesu Kristo Yohana 12;32 na Ufunuo 1; 5, 5; 6

Kufanana huko sio lazima kuwe sawasawa lakini kunathibitisha wazi kuwa tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa maandiko haya ya Ufunuo ni wazi kuwa ni wa Yohana mwana wa Zebedayo. ni wazi uwa kitabu hiki kiliheshimika sana na makanisa ya Asia ndogo ambayo kihistoria walimjua Yohana vema kwa hivyo hakuna shaka kuwa Mwandishi ni Yohana mwana wa Zebedayo aliyekuwa Mtume wa Bwana Yesu. na kuna uwezekano kuwa labda injili ya Yohana iliwekwa sawa kiasi Fulani na msaidizi wake aliyehitimisha mchango wa mwisho katika Yohana 21; 24-25.

Yohana mwana wa Ngurumo Mtume wa upendo

Ni wazi kuwa kulingana na mapokeo na vyanzo vyote vinavyopatikana vinathibitisha wazi kuwa Yohana alikuwa ndiye mtume pekee aliyekufa kifo cha kawaida na bila shaka kuwa huyu ndiye mwandishi wa kitabu cha ufunuo

  • Yohana huyu alikuwa ni ndugu yake na Yakobo wana wa Zebedayo, ingawa wao mara kwa mara wanatajwa pamoja  Yohana anafahamika zaidi kutokana na maandiko yake na yakobo inaeleweka wazi kuwa alikufa mapema sana mongoni mwa mitumeYeye aliitwa na Yesu toka kuwa mvuvi wa kawaida kuwa mvuvi wa watu na pamoja na nduguye waliitwa na Bwana wana wa ngurumo hii inawezekana kutokana na tabia zao za ukali Luka 9;54
  • Yeye  na ndyguye wakati Fulani walikuja na ombi la ajabu kutaka kuketi upande wa kuume na kushoto Marko 10;35-37
  • Mapema katika utumishi wa Yesu Yohana aliwakilisha shitaka la kukemewa kwa mtu aliyekuwa anatoa pepo lakini hafuatani na wao Marko 9;38 ni wazi kuwa Kristo aliwakemea mara kwa mara katika makosa yao hayo yote
  • Kwaajili ya unyenyekevu uliojengeka baadaye ni wazi kuwa ilikuwa mara chache sana kujitaja jina lake katika ijnili yake badala yake alijiita mwanafunzi aliyependwa sana na Yesu Yohana 13; 23, 19, 26, 20; 2, 21; 17, 20. Mwana huyu wa ngurumo alikuwa amekwisha kujifunza kuachana na mambo ya ukuu na kuwa mwana wa upendo aligundua kuwa Upendo sio maneno bali ni matyendo, la muhimu sio cheo bali ni uwepo wa Mungu
  • Aliwaasa watu aliowaita watoto wake kupenda kwa matendo na sio kwa maneno 1Yohana 3;18 alikuwa ameacha kabisa tabia ya kuwa kimbelembele na kutaka kuwa wa kwanza na sasa anakemea hata watu wenye tabia kama ile 3Yohana 9
  • Hata ingawa alikuwa sasa amezeeka sana moto wa injili ulikuwa ukiwaka ndani yake alihesabu mateso ya uzeeni kuwa ushuhuda wa Yesu Ufunuo 1;9 mateso na shida alizozipata huko patmo halikuwa jambo la muhimu kulieleza zaidi ya kile alichoagizwa na Kristo
  • Ni wazi kabisa kuwa kila mmoja ana maswala ya kujifunza kutoka kwa Yohana mabadiliko yake kutoka tabia ya ngurumo mpaka kuwa mtume wa upendo, kutokujihusisha na kusimulia mapito na badala yake kile ambacho Yesu alikuwa amemuagiza, mzigo wa kulitia moyo kanisa kuliko kutaka kutiwa moyo yeye mwenyewe, kuwa katika roho siku ya bwana hata pamoja na kuwa katika mazingira magumu kunaonyesha jinsi alivyotoa kipaumbele kwa maswala ya ibada

 

Tarehe ya uandishi

Kuna hisia kubwa tatu kuhusu tarahe ya uandishi wa kitabu cha ufunuo wa Yohana kulingana na mitazamo tofauti tofauti

  • Epiphanius aliandika mnamo katika karne ya Tatu kuwa Yohana aliandika kitabu chake cha ufunuo mara baada ya kurudi kutoka Patmo wakati wa utawala wa Claudius mwaka 41-54 lakini tarahe hii haikubaliki kwani ni mapema sana makanisa mengi ya asia ndogo yalikuwa hayajaanzishwa wakati huu nah alia ya uhasama kati ya ukristo na serikali ya Rumi pia ilikuwa haijachachamaa, inchi ilikuwa haijaendelea katika ngazi ambayo kibabu kinaonyesha  kwa misingi huo kuna uwezekano kabisa kuwa Epiphanius alikuwa akizungumzia Nerp ambaye pia aliitwa Claudius.
  • Mjadala kuhusu kuandikwa kwa kitabu hiki wakati wa utawala wa Nero umejengeka saa AD 54-68 kutokana na kuweko kwa alama maarufu katika kitabu cha ufunuo yaani 666 kwa kuzijumuisha pamoja namba hizi unapata thamani ya namba za herufi NERON KESAR kwa kiebrania jumla ya namba hizo zilitambuka kumaanisha hilo.Maswala mawili yanaweza kuhusishwa kinyuma na dhana hii, kwamba kuna Herufi nyingi sana ambazo zikijumuishwa zinaweza kuleta idadi kama hiyo na pili kwa jamaii ya Asia ndogo ingekuwa vigumu kwao kuwahusisha na  matumizi ya herufi za Kiibrania
  • Tangazo la kuweko kwa Milima inayomsaidia Mwanamke katika ufunuo 17 imekuwa ikitumiwa pia kumaanisha wakati wa Nero, vile vichwa saba ni milima saba anayoikalia hupo  na mwingine hajaja bado naye atakapokuja imempasa kukaa muda mchache na Yule mnyama aliyekuwako naye hayuko yeye ndiye wa nane naye ni mmoja wa wale saba naye anaenda kwa uharibifu Ufunuo 17;9-11
  • Kama tukio hili linahusishwa na kupeana madaraka kwa watawala wa kirumi wafalemwa kwanza wa Kirumi ni pamoja na Julius Caesar, Caesar Augustus,Tiberius, Caligula na Claudius na kama hao watano wamekwisha kuanguka wasita ni Nero na hapo ndipo kitabu cha Ufuno kilipoandikwa yaani wakati wa utawala wa kaisari Nero.                Tafasiri hii sio uhakikisho  wa ukweli kuwa wafalme hao hawatupi uhakika kuwa kwa sabau hatujui ni yupi anahesabika kama wa kwanza Augustus au la kama ni Augusto basi Nero anahesabika kama mfalme wa tano na kwa kweli Nero hakutawala muda mrefu sana kiasi cha kuwa wa muhimu katika utawala huo na hivyo Vespecian anakuwa wa sita na Tito anakuwa wa saba na Domitian anakuwa wa nane lakini kitabu kinaashiria kuwa ulikuwa wakati wa ukatili mkubwa wa Nero lakini makanisa ya asa yalikuwa hayajafikia kiwango cha mafanikio makubwa wakati wa Nero.
  • Kwa mujibu wa maelezo ya jadi ufunuo ni kitabu kilichoandikwa wakati wa Utawala wa Domitian kwa mujibu wa ushuhuda wa Irenaeus, Clement wa Alexandria pia alikubali swala hilo na ni kweli kuwa katika wakati huo makanisa ya Asia yalifikia kilele kikubwa cha mafanikio na huu ulikuwa wakati wa utawala wa Domitian na huyu alikuwa na madai ya kuabudiwa  kama Dominus et dues akiwa anatajwa kama mnyama aliyekuwa na nguvu kubwa ya kisiasa Ufunuo 13;15 na inakubaliwa kuwa jumla ya namba ya mnyama huyo inamuhusu Domitian yaani 666 ambaye kwa idadi ya herufi za jina lake Domitian yaani A[utokratorKAI[sarDOMET [ianosSEB[astosGER[manikos].kwa kujumlisha idadi ya hesabu ya herufi zake kwa kiyunani unapata jumla ya namba hiyo 666 na kwa kuwa idadi hii inakubalika sambamba na jina la Domitian haliwezi kuthibitishwa inakenda sambamba na kukubalka pia kwa jina la Nero .

 

Mahali

  • Kisiwa cha Patmos mahali ambapo maono yalipokelewa na kuna uwezekano kuwa yalinukuliwa pale au baadaye huko Efeso, Patmos ni kisiwa kilichoko juu ya mwamba katika Bahai ya Aegean (Aegean Sea) katika ukanda wa bahari ya Asia ndogo, lilikuwa ni eneo la koloni la warumi, mahali hapo wafungwa wa kisiasa walipelekwa  wakilazimishwa kufanya kazi ngumu na kuchimba madini, Yohana alisisitiza kuwa alikuwa huko Patmo kwaajil ya neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu Kristo Ufunuo 1;9, aidha mafunuo hayo yaliandikwa hukohuko Patmo au vinginevyo ni wazi kuwa kulikuwa na muda mfupi sana tangu kupokelewa na kuandikwa kwa maono hayo na kwa namna yoyote ile yanaakisi lugha na mazingira ya Kirumi, na jimbo la Asia  ambako kwa wakati huo mwandishi ndiko alikotokea na alikoishi.
  • Patmo kwa kiyunani Pavtmo ni kisiwa klichoko pwani ya Asia ndogo kama maili 35 kusini magharibi mwa kisiwa cha Mileto ni kisiwa chenye miamba na milima na kima ukubwa unaokisiwa kama Maili kumi kwa sita na kina ukavu na baridi kali kwa sifa zake na ni mahali palipotumiwa na Warumi kama eneo la Mateso inaaminika kuwa miaka ya zamani wa Italy walikiitakisiwa hiki Palmosa wakimaanisha kisiwa chenye Mitende kwa hiyo inaaminika kuwa zamani kilikuwa na Miti ambayo ilkatwa na hatimaye kukiacha kisiwa hiki kikiwa kikavu na kuna uwezekano kuwa hakuna maji.
  • Ni katika kisiwa hiki ndio Yohana alipelekwa kuadhibiwa na Mtawala wa wakati huo Domitian na hapo ndipo alipopokea yale maono na kuyaandika Ufunuo 1;9-11
  • Historia ya kisiwa hiki Ilibadilika mnamo miaka ya 1088 wakati mtawa Christodulos alipojenga Ngome ya kitawa ya Mtakatifu Yohana katika eneo ambalo zamani kulikuwa na Hekalu la Artemi na miaka ilivyokwenda watawa waliishi hapo na kujifunza maswala kadhaa na kulima pia kuliwekwa( Library) Maktaba Patmos ilikuwa mahali pa kazi za Wayunani wa Ki Othodox lakini 1453 walitafuta msaada kwa Papa wa rumi kwaajili ya usaidiwa dhidi ya waturuki kwenye Karne ya 16 kikawa chini ya waturuki lakini waliachiwa wajiongoze na kuendesha mambo yao chni ya sultani.Mwaka 1832 kisiwa kiliangukia katika utawala wa waturuki na baada ya 1912 kilirejeshwa kwa Warumi na ilipofika 1947 kilikabidhiwa kwa Wayunani au Ugiriki hata leo.

         

Makusudi

  • Makanisa ambayo viongozi wake wametajwa katika kitabu cha ufunuo yalikuwa yameunganishwa na barabara inayoelekea upande wa Kaskazini kupitia pwani ya Efeso mpaka Pargamo kupitia Smyrna. Kutoka Pargamo kuna njia nyingine inayoelekea kusini zaidi bara na kugusa miji ya Thyatira, Sardis, Philadelphia na Laodikia na kisha njia inarudi nyuma kuelekea Efeso, Kama mjumbe angelipewa Barua au ujumbe angeweza kukamilisha mzunguko huo kwa urahisi, Efeso ndio ulikuwa mji mkubwa mtukufu wa Hekalu kubwa la artemis na Huko Pergamo ndiko kulikokuwa na madhabahu kubwa ya Zeus, Thyatira ulikuwa mji wa kilimo na utengenezaji wa nguo.

Muda

  • Utawala wa Domitian ulianza kwa usumbufu mkubwa, Uharibifu wa Pompeii na Herculaneum na mauaji ya kikatili ya uchunaji ngozi ya Vesuvius mwaka 79AD. Ikifuatiwa na matukio mabaya yaliyoipiga Rumi kwa magonjwa na uasi katika mji mpaka 81AD wakati Domitian akiingia madarakani, Alipoingia madarakani aliamuru kuabudiwa na alijiita kwa Kilatin Dominus et Deus yaani Domitian ni Bwana na Mungu yeye alikuwa mtawala wa kwanza kujilinganisha na Mungu, ingawa wengine walitaka kuabudiwa na walikuwa wakipokea Ibada hata kwa kulazimishwa,  Domitian alijitangaza kuwa Mungu na mama yake Domitia kuwa mungumke fedha yake ilikuwa na alama ya mwezi na mtotoaliyeketi katika njia ya kuzunguka dunia pamoja na sayari kwaajili ya kumkumbuka mwanae aliyefariki akiwa mdogo mwaka 83AD.
  • Heshima yote ambayo alikuwa anastahili kupewa mwokozi Yesu Kristo ilidaiwa kupewa Domitian, Domitian alikuwa muuaji, alimuua mwana wa dada yake Titus Flavius Clemens na alimuua mke wake, Domitilla inasemekana kuwa Clemens alikuwa Mkristo na Domitilla alikuwa akifuata tamaduni za kiyahudi kwa siri, huku yeye aliamini kuwa hakuna Mungu “Atheism” Eusebius anaeleza kuwa Domitian alijistawisha mwenyewe kama mrithi wa Nero kwa ukatili na mwenye kustahili kama Mungu, ni mfalme wa pili kuinua kiwango cha mauaji na mateso kinyume nasi.... Eusebius alikuwa akimnukuu Hegesippus aliyekuwa akishuhudia ushuhuda wa Yohana alipokuwa amerudi Efeso baada ya kuachiliwa wakati wa utawala wa Nero mwaka 96.

 

Malengo

  • Kitabu cha ufunuo kiliandikwa kwa makanisa yaliyokuwa yamefunikwa na tishio la mateso kwa lazima, kulikuwa na tishio la maafisa waliokuwa wakipita huko na huko kutoa vitisho na kwa sababu ya aina ya mapito waliyokuwa wakiyapitia walihitaji kutiwa moyo ili waendelee na kusimama imara katika imani na kuwaonya dhidi ya uadui kutoka nje na ndani, na mafundisho potofu yenye ukengeufu, kwa hiyo pamoja na hali halisi iliyokuweko ndipo sa maswala haya yanajitokeza katika kitabu cha ufunuo.
  • Kanisa linatiwa moyo nakuelekezwa katika kutazamia ujio wa Yesu na kuwa atakuja kuwahukumu maadui na kuliokoa kanisa maswala ambayo yanajitokeza Ufuno 2;5, 16, 25, 3;3,11, 20 na msisitizo wa maneno tazama naja upesi 3;11, 22;7, 12, 20 kwa hiyo maandalizi ya ujio wa Kristo mara ya pili ni msingi wa kitabu cha ufunuo.

 

KUPITISHWA KWENYE KANUNI

  • Utambuzi wa mapema. Kulingana na ushahidi uliokuweko mwanzoni kitabu cha ufunuo hakikukubaliwa na makanisa yote mwanzoni kilikuwa kinafikiriwa kuwa ni swala la mauzauza tu allusions kutoka kwa wachungaji wa Hermas 140AD, lakini haikuendelea kusadikiwa hivyo kwani Kutokana na Mwanahistoria Jerome Melito ya Sardis AD 160-190 aliandika katika michango yake akisimulia kuhusu Justin Martyr AD 135 alihibitisha kuwa kimeandikwa na Yohana mmoja wa wanafunzi wa Bwana Yesu, Irenaeus aliyekuwa Askofu wa Lyons alikubali kuwa kitabu hiki kina asili ya utume na kinakubalika
  • Kanisa la magharibi Kanisa la Alexandria walikuwa wataalamu wa maswala ya kinabii na Clement alikikubali kuwa ni maandiko na wanafunzi wake ama Origen alikikubali ingawa Dionysius wa Alexandria alikataa kuwa sio cha Yohana ingawa alikuwa anajua kuwa kimekubaliwa na makanisa, katika kanuni ya kanisa la Roman iliyopitishwa na Muratorian Fragment AD.170 walikijumuisha kama moja ya Vitabu na mwanatheolojia Hippolytus (190-235) alikinukuu mara nyingi, kanisa la Cathage ambalo lna asili ya Rumi pia walikkubali, Tertullian(190-220) alinukuu sura 18 kati ya 22 zilizokuweko, kanisa la maghari  la karne ya 2 kwa ujumla walikubali kitabu cha  ufunuo, ni sauti mbili tu kama ya marcion aliyekuwa na mipaka yake aliyojiwekea  kwani alikuwa myahudi na Alogi ambaye alipinga kazi za Epiphanius na Irenaeus na hakuunga mkono kazi yoyote au wazo lolote linalohusiana na unabii lakini mpaka karne ya tatu kilikuwa kimekubalika kabisa katika kanuni.
  • Kanisa la mashariki walikuwa kwa namna Fulani kama maadui wakubwa wa Ufunuo hii huenda ilichangiwa na kutiwa shaka na Dionysus Askofu wa Alexandria ambaye alikitilia mashaka, pia Eusebius 260-340 alifuata muongozo huo, yeye hakukiorodhesha kabisa kitabu hiki inawezekana hili pia lilichangiwa na kuweko kwa Ofisi ya Papa na tafasiri yake kuhusu millennium,Ushawishi wa Eusebius ulikuwa na nguvu, naye Cyril wa Yerusalem AD 315- 386 alikataza watu wa kanisa kukisoma kitabu cha ufunuo hadharani au madhabahuni na alikikataza kutumika hata kwa kujitoa binafsi, Baadaye makanisa ya Asia ndogo hayakujumuisha kitabu hiki kwa vile hakikuorodheshwa na mkutano wa Kanuni wa Synod wa Laodekia AD 360 wala katika katiba ya mitume wala katika orodha ya Gregory Nazianzus, Naye thoodore wa Mopsuestia AD 340-428 alikikikataa kitabu cha ufuno akiambatanisha na waraka wa kikatoliki aliongoza kanisa la ki Nestorian pamoja na shule ya Antiokia, Mpaka katika karne ya 4 na 6 ndipo hatimaye kitabu cha ufunuo kilikubalika na kanisa la mashariki, Andrew wa Kaisaria huko Kapadokia aliandika mafafanuzi ya kitabu hicho na Leontius ambaye alikuwa Msomi huko Yerusalem alisema ni kitabu cha mwisho kukubalika na kupita katika kanuni ya Vitabu vya agano jipya.
  • Kukubalika kwa ujumla.

Kukubalika kwa ujumla kwa kitabu cha ufunuo kulitambuliwa rasmi baada ya barua ya Festal wa Athanasuis kunasadikiwa kutoka Alexandria mwaka 367, na mkutano wa Damasine Council wa 382 na mkutano wa Carthage wa 397 na cheti maalumu cha kuvitambua Vitabu na maandiko ya agano jipya kwa wa magharibi, na huko mashaiki msimamo wa kanisa ulitolewa kwa uthabiti mnamo karne ya pili na mamlaka yake kutambuliwa baadaye.

 

 

 

Jinsi ya Kutafasiri Kitabu cha Ufunuo.

 

Ni muhimu kufahamu kuwa kutafasiri kitabu cha ufunuo ni swala Gumu kwa namna Fulani na hakuna tafasiri mbili zinazoweza kukubaliana sawasawa hii ni kwa sababu zinazungumzwa ishara na lugha za mafumbo na kuna wingi wa Maruweruwe Illusions maswala ambayo wakati mwingne ni vigumu kujua hatima yake, Kwa ujumla kuna shule kuu nne za kutafasiri kitabu hiki

 

  1. Preterit: Unabii huu ulitimizwa wakati wa Kanisa la kwanza lilipopitia katika

mateso yaliyoendeshwa na Warumi.  Wengine wanaamini kuwa unabii ulitimizwa mwaka 70 BK wakati Yerusalemu ulipoangamizwa.

  1. 2. Historicit:Nabii hizi zinahusiana na watu na matukio mbalimbali yaliyotokea huko nyuma – km. Napoleon na kuinuka kwa Uislam.
  2. 3. Idealist:Matukio yanaelezea mifano ya kiroho kuhusiana na mapambano kati ya Mungu na shetani uovu na haki.
  3. Futurist: Nabii hizi zinahusiana na matukio halisi yatakayotokea siku zijazo ili kukamilisha mpango wa Mungu. Ni wazi kuwa sisi tunaofuatilia makala haya tunaamini katika mfumo huu wa tafasiri za kitabu cha ufunuo kwani ndivyo tunavyoamini.

MAMBO MUHIMU:

               

Kitabu cha Ufunuo ni cha aina ya Apokrifa, hivyo:-

  • Kinatumia ishara na mifano kutoa ukweli
  • Malaika wanaoelezea matukio
  • Kinaonyesha ushindi wa Mungu juu ya shetani.

 

KANUNI ZA KUTAFSIRI NA MAANA ZAKE:

Kanuni Na. 1 - Acha Maandiko yatafsiri yenyewe – Eze. 12:1-16

Kanuni Na. 2 – Tumia mwonekano wa unabii – mf. Lk. 4:16-21; Isa. 61:1,2

Kanuni Na .3 – Tambua kutumia mara mbili kwa andiko la unabii

Kanuni Na. 4 – Elewa matumizi ya ishara na mifano.

 

Aina za mifano  Mfano                                                 Maana:

                Namba                                 moja                                      Mungu

                                                                Mbili                                     Kuhakikishwa

                                                                Tatu                                       Utatu

                                                                Nne                                       Dunia

                                                                Sita                                        Mwanadamu, uovu

                                                                Saba                                      Utimilifu wa Mungu

                                                                Kumi                                     Kukamilika kwa siasa

                                                                Kumi na mbili                    Mwisho wa kukamilisha

 

Wanyama                           Mwanakondoo                 Yesu

                                                Farasi                                    Uwezo wa Kijeshi

                                                Wanyama                            Mpinga Kristo na nabii wa uongo

                                                Vyura                                    Mapepo wachafu

                                                Silaha                                    Yesu

 

Rangi                                     Nyeupe                                               Utakatifu

                                                Nyekundu                           Damu vitani

                                                Nyeusi                                  Baa la Tauni

                                                Zambarau                            Anasa za Kifalme

                                                Kijani                                    Burudisho

                                                Kijivujivu                             Mauti.

 

Theolojia katika kitabu cha Ufunuo.

Ingawa maswala ya ufunuo hayatiliwi mkazo katika Theolojia ni muhimu kufahamu kuwa kitabu cha Ufunuo kina magfundisho yaliyowazi yenye kukazia kuhusu maswala yajayo au matukio ya mwisho wa dunia Escatology ni wazi kuwa tunaona katika maono haya hatima ya baadaye ya kanisa katika mpango wa Mungu na juu ya maswala yajayo

Kitabu hiki kwanza kinatuonyesha jinsi Mungu alivyo mwenyezi na kuwa ni Bwana juu ya yote ni wazi kuwa kiini cha kitabu hiki ni kiti cha enzi cha Mungu kitabu hiki kinatukumbusha kuwa Mungu ni Mwenyezi ni mkuu kuliko ufalme uwao wote ukiwamo ule wa Rumi, nguvu zake ziko juu kuliko hata taifa lenye kutisha na ndie mwamuzi wa jinsi gani, lina na wakati gani atahukumu na kuwa anajua namna ya kushughulika na wanadamu walio waovu na kila uasi wa aina binadamu yeye ni mwenyezi 4:8; 11:17; 15:3; 16:7, 14; 19:6, 15; 21:22 na ni muumba wa kila kitu 4:11; 14:7 na muhukumu wa wanadamu 20:11-15).

Utatu wa Mungu umegusiwa katika ufunuo 1; 4-5 ambako kuna mazungumzo juu ya yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Roh saba zitokazo katika kiti cha enzi cha Mungu na Yesu kristo ni wazi kabisa kuwa kitheolojia kuna utatu hapa na swala hili linajitokeza katika kitabukizima ingawa si katika namna ambayo inaorodheshwa pamoja kila wakat kwa hiyo kitabu kizima kinamfunuo yeye Kristo Ufunuo 1;1.

Katika kitabu cha Ufunuo kuna somo kuu la Ufahamu kuhusu kristo Christology, kuna Historia ya sifa za Kristo za kipekee Ni samba wa kabila la Yuda Ufunuo 5;5, alikuwa na mitume kumi na wawili 21;14 alisulubiwa huko Yerusalemu 11;8 na alifufuka kutoka kwa wafu 1;5,18, ametukuzwa 3;21 na ana sifa zote zilizoorodheshwa katika sura ya kwanza.

Ana mamlaka dhidi ya Historia 5;6-12 ndio ufunguo muhimu wa kitabu hiki, ni Kondoo aliyechinjwa kwa sadaka 5;6 kama samba wa Yuda ni Mrithi wa kiti cha Enzi cha Daudi 5;5 ni mwana wa Adamu aliyeshinda, atokeaye juu ya mawingu kukamilisha mavuno ya ulimwengu 14;15 Anaitwa Neno la Mungu 19;13 ni mlinzi wa kanisa 1;12-20 na muhukumu wa mwisho wa ulimwengu 11;15 na ndiye Nuru ya mji ule uja 21;23.

Kazi za Roho Mtakatifu zinaorodheshwa ingawa mkazo katika kushughulika na mtu mmoja mmoja haukaziwi sana, anawakilishwa kama Roho saba za Mungu Ufunuo 1;4 ndiye aliyetengeneza mazingira mpokeaji kupokea maono 1:10; 4:2; 17:3; 21:10. Inagwa matumizi ya neno roho yanaonekana kutumia neno Pnuvmati kumaanisha hali ya hisia alizokuwa akizipata muona maonao kuliko kuhusu nafsi lakini Roho yuko pamoja na Bibi harusi wa Yesu kristo na anahusika katika amri ya kuja na kunywa maji ya uzima ufunuo 22;17.

Hali ya mwanadamu mbele za mungu inawekwa wazi, wanadamu wamejitenga na ungu wanamuhofu 6;16, 17 na mawindo wazi ya pepo wachafu 9:4; 13:3, 14; 17:8 na hatimaye watahukumiwa kwa matendo yao Ufunuo 20;12-13, Wokovu unahakikishwa kwa waamini 7;3 mwisho wa walioamini na wasioamini unawekwa wazi kuwa waasi ni katika ziwa la moto 21;8 na waliokombolewa kwenye miwa Mungu 22;14.

Pia kuna theolojia ya hali za kiroho ambazo waamini wanapaswa kuwa nazo na zisizopaswa kuwa ambazo zinaelezwa kwa wingi katika kitabu hiki sura ya 1-3 mwanzoni, mfano uvumilivu wakati wa mateso, upendo kwa Yesu, uaminifu n.k vinakaziwa katika kitabu hiki.

Ulimwengu wa kiroho wa kishetani unawekwa wazi huku shetani na mapepo yakitajwa sawa na sifa zao 9;4-11 ni wazi pia kitabu cha ufunuo knaweka wazi kuwa mgogoro tulionao kati yetu na shetani ni wa kiroho na ni vita  na uwa ulianzia mbinguni na kuja duniani 12;7, hatinma yeke inawekwa wazi kuwa hatimaye atahukumiwa 12;9 na Mungu atashinda na shetani atatupwa katika ziwa la Moto 20;1-3,10. Na kongozi wa kisiasa aliye kiyume na maswala ya Mungu anayetajwa kama mnyama hatimaye ataharibiwa Ufunuo 13.

Swala la malaika nalo limazungumzwa kwa uapana sana katika kitabu cha ufunuo kuliko kitabu kingine chochote katika agano jipya kwa mafano kwa kila kanisa moja kna malaika  na pia wametajwa Karibu katika kila sehemu ya kitabu hikikuwa ni watumishi wa Mungu 5:2; 7:2, 3; 8:2; 10:1; 12:7; 14:6, 8, 9, 17; 15:1; 17:1; 18:1, 21; 19:17; 20:1; 21:9; 22:8 viumbe vyeye uhai Ufunuo 4;6-8 vinafanana na maserafi wa Isaya 6 na ni wazi kuwa vi viumbe maalumu sana  na pia tunawekewa wazi kuwa malaika na mapepo ni viumbe walio katika namna moja ya maumbile ya kiroho wakigawanywa kuwa wema na waovu Ufunuo 12;7

Ni wazi kuwa msingi na makazo wa Kitabu hiki ni mambo yajayo na mafundisho yote yanakubaliana na mpango wa Munu katika historia 2:7, 10, 17, 28; 3:5, 12, 20 eneo jingin

Pesquisar
Categorias
Leia mais
UCHUMBA KIBIBLIA
HASARA ZA KUFANYA TENDO LA NDOA KABLA YA NDOA.
Andiko la Msingi ni Mithali 5:1-20. Mungu ndiye aliyewaumba mtu mume na mtu mke, akawaweka...
Por GOSPEL PREACHER 2021-11-23 07:16:45 0 9KB
FORM 1
BASIC MATHEMATICS: FORM 1
List of all topics in Basic Mathematics for form 1 class: CLICK HERE TO VIEW. NUMBERS FRACTIONS...
Por PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 12:44:29 0 5KB
Networking
KARIBU PROSHABO.COM TUHUBIRI INJILI PAMOJA
KWA MASWALI AU MAONI, BONYEZA HAPA? Bwana Yesu asifiwe!! Karibu sana PROSHABO.COM, kwa pamoja...
Por PROSHABO NETWORK 2021-09-04 09:51:34 3 6KB
Injili Ya Yesu Kristo
UTHIBITISHO WA UTATU WA MUNGU
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        ...
Por GOSPEL PREACHER 2022-01-12 00:36:40 0 5KB
Injili Ya Yesu Kristo
JIHADHARI USIANGUKE TENA ILI USITENGWE NA MUNGU
Na: Patrick & Bernada Sanga Shalom, neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu...
Por GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:36:12 0 5KB