MKRISTO NA UCHUMI: CHRISTOPHER MWAKASEGE

0
12Кб

Utangulizi

SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASIKINI!

(Namna ya mkristo kuishi katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu)

            Kati ya mambo yaliyotabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho ni dhiki katika mataifa, pamoja na hali ngumu ya uchumi. Soma mwenyewe katika Luka 21:25-26 na Ufunuo wa Yohana 6:5-6.

          Pia, tunasoma kutoka katika biblia ya kuwa biashara na uweza wa kuuza na kununua utafuata mfumo fulani uliojaa dhuluma, ambao utatawaliwa na kundi fulani ulimwenguni. Watu hawatauza wala kununua bila ya kupatana na watu wa kundi hilo, na hasa kiongozi wao. Na asomaye na afahamu. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura yote ya 13.

          Si hivyo tu, bali biblia inaeleza wazi kabisa kuwa katika siku hizi za mwisho kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na uasherati na pia kati ya biashara na uasherati. Soma kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura za 17 na 18. Lakini pia unaweza kuwa na utajiri na ukafanya biashara bila kujihusisha na uasherati na mambo mengine yaliyo kinyume na maadili ya Mungu.

              Tutawezaje kupona katika hali ya namna hii tusimkosee Mungu wetu aliyetuita katika utakatifu ndani ya Mwana wake mpendwa Yesu Kristo? Kwa nini wakristo wengi wanaishi katika hali ngumu kiuchumi kama vile kuna mtu aliyewawekea vikwazo vya uchumi wasifanikiwe?

          Watu wengi wanapenda kuishi maisha matakatifu na wengi pia wanapenda kuokoka na kudumu ndani ya kristo, lakini swali linalowasumbua ni wafanyeje katika hali ngumu hii ya uchumi wapate chakula, malazi na mavazi kihalali bila kumkosea Mungu?

          Ni watu wachache wanaofahamu uwezo wa mawazo katika kuongoza maneno na matendo yao ya kila siku. Ni budi ufahamu ya kuwa maneno yako na matendo yako ni matokeo ya jinsi unavyowaza. Kwa maneno mengine naweza kusema ya kuwa maisha ya mtu yanategemea mtazamo wa mawazo yake.

              Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba jinsi ulivyo ni matokeo ya jinsi unavyowaza; kwa kuwa unayowaza ndiyo unayoyasema na kuyafanya.

          Watu wengi wamekuwa wakifikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyewapangia kuwa maskini. Na hata wakristo wengine kudiriki hata kuuona umaskini kama sehemu ya utakatifu na unyenyekevu.

          Lakini Biblia haisemi hivyo, wala haifundishi mawazo hayo. Ni lengo langu kukueleza katika ujumbe huu ya kwamba SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI.

           Nataka ufahamu pia ya kuwa nitakapokuwa natumia neno wakristo katika ujumbe huu, ujue namaanisha wakristo wale wanaomkiri Yesu Kristo ya kuwa Bwana na Mwokozi wao; ambao pia humwabudu Mungu katika Roho na Kweli.

          Ni maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo kuwa atakuwezesha kusoma na kuelewa somo hili, ili wote tulio wakristo tusimame katika haki zetu zote zilizopatikana pale msalabani. Nia hasa ni kukupa mafundisho ya msingi ya kukusaidia uweze kuishi hata katika hali ngumu ya uchumi bila kumkosea Mungu.

Mafundisho ninayotarajia kukufundisha yatakuwa na mfululizo wa masomo kama yafuatayo:

  • Kwa nini si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?
  • Mafundisho manne yasiyo sahihi unayopaswa kuyatambua
  • Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?
  • Utajiri wake Kristo usiopimika
  • Uchumi wa ufalme wa mbinguni
  • Tofauti ya zaka na dhabihu
  • Ukitoa tegemea kupokea
  • Sadaka na wokovu
  • Natoa lakini sipokei – nifanyeje?
  • Ufanyeje katika hali ngumu ya uchumi?

    Haya ni mafundisho ambayo nitayaweka kwa namna ambayo yatakupa changamoto ya kuyasoma zaidi wewe binafsi na kuyaweka katika matendo. Kwa hiyo usitegemee kupata majibu ya maswali yote uliyonayo juu ya mambo niliyoorodhesha hapa juu, bali tegemea mwongozo wa changamoto itakayokusaidia katika kujifunza zaidi juu ya utajiri  na mkristo.

 

KWA NINI SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI?

              Napenda kuanza kukuambia ya kuwa si mapenzi ya Mungu uwe maskini. Kwa sababu tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu huu, Mungu hakupanga kuwa watu wake aliowaumba wawe maskini; bila kujali rangi, kabila, wala taifa.

                Nafahamu ya kuwa katika Mathayo 5:3, Yesu Kristo alisema; “Heri walio maskini wa roho; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Watu wengi wanapousoma mstari huu, wanadhani Yesu Kristo alisema “Heri walio maskini wa mahitaji ya MWILI; maana ufalme wa mbinguni ni wao.” Lakini Kristo hakusema hivyo.

              Mtu maskini maana yake ni mtu mhitaji. Yesu Kristo aliposema “Heri walio maskini wa roho …….” Alikuwa ana maana ya kusema ‘Heri walio wahitaji wa mambo ya rohoni; maana ufalme wa mbinguni ni wao. Ndiyo maana aliongeza kusema, “Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa" (Mathayo 5:6).

          Mtu aliye maskini wa mambo ya mwili ni yule aliye mhitaji wa mambo ya mwili. Na mambo ya mwilini ninayoyasema ni mavazi, chakula na mahali pa kulala. Yesu Kristo hakusema heri wale walio na mahitaji ya chakula, mavazi, afya na malazi.

          Ninaposema mahitaji ya mwili usije ukachanganya na matendo ya mwili yaliyoandikwa katika Wagalatia 5:19-21 ambayo ni uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda na ulevi. Mimi siyazungumzii hayo ninaposema juu ya mahitaji ya mwili. Mahitaji ya mwili ninayoyasema ni mavazi, chakula, nyumba na matibabu.

          Kwa hiyo si sawa kabisa kwa mtu kuhalalisha umaskini wa mwili, yaani ukosefu wa chakula, mavazi, matibabu na nyumba, kwa kutumia maneno ya Bwana Yesu Kristo yaliyo katika Mathayo 5:3:

Nataka kurudia tena; si mapenzi ya Mungu mtu awe maskini.

          Unaweza ukaniuliza na kusema, “Bwana Mwakasege kama si mapenzi ya Mungu mtu awe maskini, mbona basi kuna matajiri na maskini, je! Mungu hakuwaumba wote?

          Ni kweli kwani hata imeandikwa katika Mithali 22:2, kuwa “Tajiri na maskini hukutana pamoja; Bwana ndiye aliyewaumba wote”. Lakini fahamu ya kuwa ingawa matajiri na maskini waliopo wote waliumbwa na Mungu; tangu mwanzo wa uumbaji Mungu hakuyaweka matabaka haya mawili.

          Hapo mwanzo Mungu alipomuumba mtu, hakuweka ndani yake utajiri na umaskini pamoja. Wala hakuumba watu wengine wawe matajiri na wengine wawe maskini.

              Tunafahamu ya kuwa mtu aliumbwa kwa mfano wa Mungu na kwa sura ya Mungu. Na naamini ya kuwa utakubaliana nami nikisema Mungu wetu si maskini kwa hiyo hatukuumbwa kwa mfano wa kimaskini wala sura ya kimaskini.

          Kwa nini nasema na kusisitiza ya kuwa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini?

            Ninazo sababu nne ambazo ningependa kukushirikisha:

  • Mungu ndiye atupaye nguvu za kupata utajiri

“ Bali utamkumbuka Bwana , Mungu wako, maana ndiye akupaye NGUVU ZA KUPATA UTAJIRI; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo” (Kumb. 8:18).

          Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini kwa kuwa yeye mwenyewe ndiye atupaye nguvu ili tupate utajiri! Kama basi Mungu anatupa nguvu za kupata utajiri, ina maana ni wazi kwamba Mungu hapendi tuwe maskini wa mambo ya mwilini.

         Lakini fahamu ya kuwa si matajiri wote waliopo duniani wameupata utajiri kutokana na nguvu walizopewa na Mungu. Wengi wamepata utajiri kwa njia ya dhuluma. Na ndiyo maana sehemu nyingi katika Biblia matajiri wa jinsi hiyo wamekemewa. Soma Amosi 5:11, 12. Kwa sababu hii Mungu hayuko upande wa matajiri hawa. Hii pia haimaanishi kuwa Mungu yuko upande wa KILA  maskini aliopo duniani. La hasha! Mungu yuko upande wa yule ayafanyaye mapenzi yake awe tajiri au maskini (Mathayo 7:21)

        Watu wengi wametajirika kwa njia ya rushwa na kutokusimamia haki pamoja na uchoyo. Na hii si sawa hata mbele za Mungu. Ni dhambi zilizo wazi kabisa. Na wote wafanyayo hayo wanahitaji kutubu!

        Ngoja nikueleze jambo muhimu: Mungu anapokupa nguvu za kupata utajiri, anakupa akiwa na lengo na kusudi muhimu.

          Ni lengo gani hilo?

          Imeandikwa, “………. Ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo”

       Na Yesu Kristo alisema, “ ……. Kikombe hiki ni AGANO JIPYA KATIKA DAMU YANGU, inayomwagika  kwa ajili yenu” (Luka 22:20).

          Mungu akikupa nguvu za kupata utajiri ni kwa ajili ya kulifanya imara agano lake katika damu ya Yesu Kristo. Na hii ina maana utajiri utakaokuwa nao kutoka kwa Mungu ni kwa kueneza injili! Ni kwa ajili ya kueneza habari njema ya ukombozi kutokana na dhambi, mauti, magonjwa na umaskini. Habari njema hii inatakiwa kuenezwa kwa maneno na kwa matendo.

        Kwa kuwa tu kuna matajiri wasio wa haki basi haimaanishi kuwa matajiri wa haki hawapo. Ni budi tuweze kutofautisha utajiri ulio wa haki na utajiri usio wa haki.

  • Mungu ndiye atufundishaye kupata faida

Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu si Mungu wa hasara bali Mungu wa faida. Imeandikwa hivi;

  “ Bwana, Mkombozi wako, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi;Mimi ni Bwana, Mungu wako,   nikufundishaye  ili upate faida, nikuongozaye katika njia  ikupasayo kuifuata” (Isaya 48:17).

           Ndiyo maana kila mtu ndani yake ameumbiwa kupenda kufundishwa ili apate faida katika mambo anayoyafanya. Mungu akikufundisha kupata faida; njia utakayotumia kupata faida itakuwa njia ya haki. Na faida hiyo haitakuwa kwa ajili yako mwenyewe, bali utawashirikisha na wengine pia faida hiyo .

          Watu wengine kwa kutokuwa wavumilivu, na kutokujali mafundisho ya Mungu; wameamua kujipatia faida kwa kuwadhulumu, kuwakandamiza na kuwanyonya wengine. Na inasikitisha jinsi wanavyomshirikisha Mungu katika faida najisi namna hiyo waposema ya kuwa ni Mungu aliyewasaidia ‘kudhulumu na kunyonya’. Ni wazi ya kuwa Mungu hakuwasaidia kupata faida kwa njia ya udhalimu.

        Si mapenzi ya Mungu tuwe maskini, ndiyo maana anatufundisha ili tupate faida ya halali. Kwa ajili hiyo imeandikwa; “Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji” (Waefeso 4:28).

        Je! Si jambo la kushukuru hili, la kuwa na Mungu ambaye hapendi tupate hasara?

       Kama Mungu asingekuwa anapenda tufanikiwe katika mahitaji yetu ya mwili, basi ingeandikwa wazi katika Biblia. Lakini badala yake naona maneno kama yafuatavyo; “Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo YOTE na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo” (3Yohana 1:2).

       Kwa maneno mengine anatuombea ya kuwa kwa kadri roho inavyofanikiwa basi tufanikiwe vivyo hivyo katika mahitaji ya mwili – yaani tuwe na chakula, mavazi, n.k.

  • Vitu vyote vyema ni mali ya Bwana, na vyote vya Bwana ni vyetu ndani ya Kristo

              Katika Zaburi 24:1 imeandikwa;“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana; Dunia na wote wakaao ndani yake”

            Na pia ukisoma katika Hagai 2:8 unaona imeandikwa hivi “Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi”

          Ngoja nikuulize swali; Je! unadhani vitu vyote hivi Bwana amemwekea nani? Unadhani alimwekea shetani na watu wanyonyaji wachache?

La hasha!
        Mungu aliviweka vitu hvi vyote na mali hii yote kwa ajili ya watu wake wote, ili itumike katika usawa. Kwa nini? Kwa kuwa Mungu hapendi watu wake wawe maskini. Ndiyo maana mtu alipoumbwa aliwekwa awe wakili wa mali yote ya Mungu hapa duniani.

        Utajiri uliomo duniani umetawaliwa na watu wachache na nchi chache siku hizi kwa sababu ya dhambi za uchoyo, ubinafsi, uonevu,unyonyaji, unyang’anyi na dhuluma zilizoingia ndani ya mwanadamu.
         
Na hii imefanya watu wengine kufikiri ya kuwa Mungu ndiye aliyegawa matabaka haya mawili, ambavyo si kweli. Na si vizuri kumsingizia Mungu katika jambo ambalo mwanadamu mwenyewe amejiletea uharibufu.

  • Yesu Kristo alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri

              “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi   alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” (2 Wakorintho 8:9).          

            Je! unafahamu kwa nini Yesu Kristo aliamua kuwa maskini? Ni “…….. ili kwamba ninyi mpate kuwa MATAJIRI kwa umaskini wake”.

           Najua kuna wengine watashangaa kuusoma mstari huu; lakini ndivyo ilivyo.

          Nimewahi kusikia mkristo mmoja akisema: “ Mimi ni maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.

          Na mwingine alisema; “ Napenda kuwa maskini kwa kuwa Yesu Kristo alikuwa maskini”.

         Nadhani kuwa kuna wakristo wengi ambao wana mawazo kama haya. Ni kweli kwamba Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini. Lakini hakuwa maskini ili sisi tuwe maskini; bali alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri! Kama alikuwa maskini ili sisi tuwe maskini kama wengine wanavyodhani, basi kazi hiyo haina faida kwetu. Lakini Yesu Kristo asifiwe kwa kuwa alikuwa maskini ili sisi tuwe MATAJIRI.

        Na ndiyo maana alisema katika Luka 4:18a ya kuwa; “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri MASKINI habari njema.”

        Je! kuna habari njema kwa maskini zaidi ya kumwondoa katika umaskini wake?

       Injili ni habari njema. Na injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu kwa kila aaminiye (Warumi 1:16). Kuokoka si kuenda tu mbinguni; bali kuokoka maana yake ni uokolewe usiende motoni bali uende mbinguni ukifa, PAMOJA na kuokolewa kutoka kwenye  matatizo ukiwa hapa duniani ambayo ni pamoja na umaskini.

       Petro aliposema “Bwana niokoe” alipokuwa anazama katika maji unafikiri alikuwa anataka wakati huo aokoke aende mbinguni? La hasha! Yeye Petro alitaka aokoke ASIZAME KATIKA MAJI. Na Yesu akasikia kilio chake akamwokoa. Hivi leo kuna watu wengi mijini na vijijini wanalia Yesu awaokoe kutokana na njaa, kukosa mavazi, magonjwa, maonezi, nakadhalika. Kanisa kama mwili wa Kristo linatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia watu hao, kwa kuwa kazi hii ni sehemu ya utume wake.

       Wakristo wengine utawasikia wakisema; hapa duniani hawahitaji kitu bali thawabu yao wataipata mbinguni. Lakini matamshi ya namna hii yanaeleza ukweli nusu na usiokamilika. Kuwa mkristo kuna thawabu duniani na kuna thawabu mbinguni.

       Kama hakuna thawabu yoyote tunayoipata tukiwa hapa duniani kwa kumfuata Yesu Kristo; basi ukristo wetu hauna maana na hauna msaada wowote kwa mwanadamu. Ukristo usiotatua matatizo ya mwanadamu ya kila siku, ni ukristo usio na uhai.

        Mtume Petro naye aliwahi kusumbuliwa sana na jambo hili, hata ikabidi amuulize Bwana Yesu.

        “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata, TUTAPATA NINI BASI?” (Mathayo 19:27)

          “Yesu akasema, Amini, nawaambiaeni, hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa MARA MIA SASA WAKATI HUU, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:29,30).

          Majibu haya ya Bwana Yesu, yanazidi kutudhihirishia ya kwamba si mapenzi ya Mungu tuwe maskini. Yesu Kristo ameeleza wazi kabisa ya kuwa atakayemwamini na kufuata maagizo hayo atapata MARA MIA SASA WAKATI HUU akiwa bado duniani. Na kati ya vitu atakavyopewa ni pamoja na nyumba na mashamba!

          Ni kweli Bwana Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani alikuwa maskini, lakini baada ya kufufuka alirudishiwa utajiri wake. Ndiyo maana Mtume Paulo anazungumzia juu ya “….. utajiri wake Kristo usiopimika”. (Waefeso 3:8). Na katika Wafilipi 4:19 tunasoma hivi; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”.

          Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na magonjwa yetu , na kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5; Mathayo 8:16,17; 1Petro 2:24). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na kuombea wagonjwa na kutoa huduma za afya kwa wagonjwa.

        Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alichukua dhambi zetu na akafanyika dhambi kwa ajili yetu, “ Ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2Wakorintho 5:21). Na kwa kujua hili kanisa linahubiri habari za ondoleo la dhambi kwa yeyote atakayemwamini Kristo.

        Kumbuka ya kuwa; Yesu Kristo alikuwa maskini, ingawa alikuwa tajiri, ili kwa umaskini wake sisi tupate kuwa matajiri (2 Wakorintho 8:9). Na kwa kujua hili kanisa linajihusisha na miradi mbalimbali ya kimaendeleo ili mtu aondokane na umaskini.

MAMBO MANNE UNAYOPASWA KUYAJUA

            Kuna mafundisho ambayo si sahihi yaliyowafanya wakristo wengi hasa wale waliookoka kutokujua cha kuamini juu ya uhusiano wa ukristo wao na utajiri. Na tuangalie maeneo manne yafuatayo ambayo wakati mwingine yamezaa mafundisho yasiyo sahihi:

1. TAJIRI NA UFALME WA MUNGU:

            Nadhani utakuwa umewahi kusikia watu wakisema; “Matajiri hawataurithi ufalme wa Mungu” Na wanasema ndivyo Bwana Yesu alivyosema baada ya tajiri aliyetaka uzima wa milele kukataa kuuza mali yake.

            Hata mimi mwanzoni ilikuwa karibu sana nikubaliane na usemi huu. Lakini baada ya kuyachunguza maandiko niliona ya kuwa Yesu Kristo hakusema hivyo bali anasingiziwa tu.

            Yesu Kristo alisema hivi;“Kwa shida gani wenye mali WATAUINGIA ufalme wa Mungu” (Luka 18:24)

Kwa mstari huu tunajua ya kuwa Yesu Kristo hakusema ya kuwa wenye mali hawatauingia ufalme wa Mungu; bali alisema “kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!”

            Na akaendelea kusema, “ Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” (Luka 18:25). Na wale waliosikia wakashtuka na kushangaa, kwa maana waliona itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuokoka, na naona walifikia mawazo kama waliyonayo wengi siku hizi ya kuwa tajiri hawezi kuingia katika ufalme wa Mungu. Ndiyo maana wakauliza “Ni nani basi awezaye kuokoka?” (Luka 18:26).

Yesu Kristo akawajibu akasema;“Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu” (Luka 18:26).

Kwa maneno mengine alikuwa anasema tajiri anaweza KUWEZESHWA NA MUNGU kuingia katika ufalme wa Mungu akiiamini injili inayookoa. Hata hivyo maskini naye anaokolewa kwa neema ya Mungu.

Na kwa kuamini kuwa tajiri hawezi kuurithi ufalme wa Mungu, wakristo wengi kwa kudhamiria kabisa wameamua kuwa maskini ili wasije wakaukosa ufalme wa Mungu. Lakini hii si sawa na ni kukwepa wajibu wetu tulionao kama mawakili wa mali zote za Mungu.

            Na ni vizuri ufahamu ya kuwa umaskini wa kukosa chakula, mavazi na nyumba ya kukaa siyo tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Na wala umaskini siyo utakatifu – ingawa kuna maskini walio watakatifu! Na pia utajiri siyo utakatifu ingawa kuna matajiri walio watakatifu.

            Kuna Mkristo mmoja wa dhehebu fulani alikuwa akinieleza hali iliyowasonga katika dhehebu lao; alisema;

“Katika kanisa letu Mchungaji akionekana amevaa vizuri,   wakristo wake wanasema amepoa kiroho. Kwao mtu wa kiroho  ni mtu aliye maskini, asiyevaa nguo nzuri wala viatu vizuri.”

Niliposikia maneno hayo nilisikitika sana, na nikakumbuka maneno ya Mungu aliyosema kwa kutumia kinywa cha nabii Hosea, yasemayo, “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa ….” (Hosea 4:6) na pia Yesu Kristo  aliwahi kusema ya kuwa watu wanapotea kwa kuwa hawajui maandiko wala uwezo wa Mungu.

Kwa hiyo fungua moyo wako uisikie kweli ambayo ndiyo neno la Mungu. Na utaifahamu kweli na hiyo kweli itakuweka huru (Yohana 8:32)

2. MUNGU NA MALI

            Kuna uhusiano gani kati ya Mungu na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya Mkristo na Mali? Kuna uhusiano gani kati ya wokovu na mali?
Je, ni dhambi kwa mkristo kuwa na mali nyingi? Hebu na tuangalie maneno ya Yesu Kristo juu ya Mungu na Mali.

            “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili, Kwa maana  atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu  na Mali” (Mathayo 6:24)

Neno la kiingereza lililotafsiriwa na kuandikwa ‘mali’ ni ‘mammon’ Na neno hili ‘mommon’ ni jina la roho ya ibilisi inayotawala mali. Kwa maneno mengine naweza kusema kuwa ‘mammon’ ni jina la pepo.

            Kwa hiyo, neno ‘mali’ lilivyotumika hapa linamaanisha ‘pepo linaloitwa Mali’ Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Hakuna  mtu awezaye kutumikia MABWANA wawili ….” Yesu Kristo asingeliita mali kuwa ni mojawapo ya MABWANA kama hakuwa anasema juu ya roho inayoitwa mali. Roho hii ya shetani iitwayo Mali imewafanya watu wengi, hata wakristo waache kumtumikia Mungu aliye hai, na badala yake waitumikie roho inayowasukuma na kuwatamanisha juu ya mali, ili waitumie kwa uchoyo na ubinafsi.
            Wakristo wengine wanadhani wanaweza kumtumikia Mungu na vile vile wamtumikie Mali. Yesu Kristo alisema; “HAKUNA mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana ATAMCHUKIA HUYU, NA KUMPENDA HUYU: AMA ATASHIKAMANA NA HUYU, NA KUMDHARAU HUYU. Hamwezi kumtumikia Mungu na Mali.”

Kwa kusema hivi hakuwa anamaanisha kuwa na vitu vinavyoitwa mali ni vibaya. Kitu anachosema ni kibaya ni KUITUMIKIA MALI! Biblia inasema katika Zaburi 24:1 kuwa, “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana; Dunia na wate wakaao ndani yake.”

Mtu hakuumbwa ili kuitumikia mali. Mtu aliumbwa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na amtumikie Yeye peke yake. Mali ya dunia iliwekwa kwa ajili ya kumtumikia mtu, na siyo mtu kuitumikia mali! Mtu aliwekwa juu ya mali yote na aliagizwa kuitawala (Mwanzo 1:28 – 30).

Kuwa na mali siyo vibaya, wala siyo dhambi. Mali inakuwa kikwazo katika maisha ya ukristo inapoanza kumfanya mtu amsahau Mungu na mapenzi yake. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema; “Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu” (Luka 18:24) siyo kwamba hawezi kuuingia ufalme wa Mungu, bali kwa shida wenye mali watauingia ufalme wa Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba wakimtanguliza na kumtumikia Mungu, mali haitakuwa kwazo katika maisha yao ya ukristo.

Sasa tuishije katika ushauri wa namna hii?

            “Kwa sababu hiyo  nawaambieni, msisumbukie maisha   yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? NI YUPI KWENU AMBAYE AKIJISUMBUA AWEZA KUJIONGEZA KIMO CHAKE HATA MKONO MMOJA? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini  maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti; nami nawaambia ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, JE! HATAZIDI SANA KUWAVIKA NINYI, ENYI WA IMANI HABA? Msisumbuke basi, mkisema, Tule nini? au Tunywe nini? au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote” (Mathayo 6:25 – 32)

            Kuna wakristo wengine wameyaelewa vibaya maneno haya ya Bwana Yesu Kristo hata kufikia kutokufanya kazi kwa kisingizio cha kwamba Yesu Kristo alisema tusiyasumbukie maisha. Kwao kufanya kazi ina maana kusumbukia maisha. Lakini napenda kukuambia ya kuwa Yesu Kristo hakuwa ana maana ya kutuambia tusifanye kazi aliposema tusiyasumbukie maisha.

Nadhani unaamini ya kuwa ni Roho wa Kristo aliyemwongoza Mtume Paulo kuwaandikia Wathesalonike juu ya mashauri mbali mbali ya kikristo. Katika 1Wathesalonike 3:10b anasema, “Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.” Ni muhimu kufanya kazi. Kufanya kazi siyo kusumbuka na maisha. Kusumbuka na maisha siyo kufanya kazi.

Jambo ambalo Bwana Yesu Kristo alitaka tufahamu wakati alipokuwa akisema tusisumbukie maisha, ni kwamba katika kila jambo tumshirikishe Mungu na kumtanguliza Yeye. Wakristo wengine wanadhani wanaweza kula, kunywa na kuvaa bila msaada wa Mungu. Yesu Kristo alisema katika Yohana 15:5b kuwa; “…… maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya NENO LO LOTE” (Hili ni pamoja na kula, kunywa na kuvaa) Ndiyo maana katika Wafilipi 4:13 imeandikwa kuwa “Nayaweza mambo yote katika YEYE anitiaye nguvu” Yesu Kristo ndiye atutuaye nguvu.

Yesu Kristo alitoa mwongozo mzuri sana wa jinsi ya kuishi hapa ulimwenguni aliposema;

“Bali utafuteni KWANZA ufalme wake, na haki yake; na hayo  yote  mtazidishiwa” (Mathayo 6:33)

Ukiyaangalia maisha ya watu wengi waliookoka utadhani Yesu Kristo alisema, “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote MTAONDOLEWA.” Inahuzunisha kuona ya kuwa watu wengi wakiokoka maisha yao yanageuka kuwa duni, wanashindwa kula vizuri, wala kuvaa vizuri.

            Ngoja nirudie kusema kuwa SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASKINI. SI MAPENZI YA MUNGU TUKOSE CHAKULA WALA MAVAZI. Ni Mungu yupi ambaye atawapenda ndege akawavika na kuwalisha, na akawaacha watoto wake aliowaumba kwa mfano wake wakose chakula na mavazi?

            Mungu wetu tunayemwabudu na kumtumikia katika Kristo Yesu, anapenda tuishi maisha mazuri, tule, tunywe na kuvaa vizuri. Tunachotakiwa kufanya ni kuutafuta KWANZA ufalme wake, na haki yake, na hayo yote (chakula na mavazi) TUTAZIDISHIWA na siyo TUTAONDOLEWA.

    Ukiona mtu anasema ameokoka na halafu anajikuta anakosa chakula na mavazi huku anafanya kazi, basi ujue anafanya kazi na kukusanya vitu hivyo pasipo Bwana; kwa kuwa asiyekusanya pamoja na Bwana hutapanya.

3. FEDHA NA KUPENDA FEDHA

            Nimewahi kumsikia mhubiri mmoja akisema; “Fedha ni shina la maovu, kwa hiyo wakristo wajihadhari nazo.” Na wakristo wengi wamekuwa wakisikika wakisema hivyo, kwa hiyo wanaogopa kuwa na fedha za kutosha.

Lakini ninaposikia watu wakisema hivi, huwa najiuliza wanaupata wapi usemi huu? Biblia haisemi; “Fedha ni shina la maovu.”

Badala yake Biblia inasema hivi;“ Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha;ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”(1Timotheo 6:10)

Kupenda fedha ni kuwa na tamaa ya fedha; ni kuzitamani fedha. Na kupenda fedha huku ndiko shina moja la mabaya ya kila namna.

Kuwa na fedha nyingi au kidogo siyo dhambi, kwa kuwa fedha ni mali ya Mungu (Hagai 2:8) Lakini kupenda fedha nyingi au kidogo ni shina moja la maovu.

Tamaa ya fedha ndiyo inayoleta wizi, ujambazi, mauaji, dhuluma, kutokutosheka, uchoyo, wivu, uasherati; nakadhalika. Lakini unaweza kuwa na fedha bila ya kufungwa na roho ya kupenda fedha.

Je! Unafahamu ni kwa nini shetani hapendi wakristo safi wawe na fedha? Maana ni kazi ya shetani kuwapiga vita wakristo wanaotaka kujipatia fedha kwa njia ya halali. Akishindwa kuwazuia kupata fedha; atahakikisha zile fedha walizonazo wanazimaliza haraka hata kwa matumizi ambayo hawakupanga.

Je! Unafahamu ni kwa nini?

Kwa sababu anafahamu mkristo safi akiwa na fedha za kutosha, atazitumia hizo kumpiga nazo vita kwa kuihubiri injili! Na shetani anafahamu kuwa Yesu alisema mwisho hautakuja mpaka injili ihubiriwe katika mataifa yote. Kwa hiyo anajua akiweza kuwakosesha wakristo fedha za kutosha ili injili ihubiriwe, yeye anapata muda wa kupumua na kupumzika.

Wengi wameshindwa kujenga makanisa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Watumishi wa kanisa wanalipwa mishahara kidogo, kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Mikutano ya injili na semina za neno la Mungu hazifanyiki mara kwa mara kwa kukosa fedha. Wainjilisti wanatafuta fedha za kununulia vipaza sauti wanakosa. Na matokeo yake ni kazi ya Mungu kupoa.

Je! Unadhani ni nani ambaye anaweza kutoa fedha yake ili ikahubiri injili kama siyo wakristo wenyewe? Na wakristo watatoaje fedha kama hawana fedha? Na watakuwaje na fedha, kama wanadhani kuwa na fedha nyingi ni dhambi?

Na shetani ameutumia mwanya huu kuzitumia fedha ambazo wanazo watu wasiopenda haki kueneza dhambi na uovu. Je, ni haki kwa nchi nyingine kutumia ma-billioni ya fedha kutengeza silaha ambazo baadaye wanaziharibu tena, huku mamillioni ya watu wanakufa kwa njaa na maafa mengine?

        Kwa hiyo usikubali unaposikia mtu akisema kuwa na fedha ni vibaya; lakini uwe mtu wa kutokupenda fedha. Kwa kuwa ukizitamani fedha utajikuta unaanza kuzitafuta hata kwa njia ambazo ni kinyume cha maadili yetu ya Kikristo; na pia kinyume cha utu wa mwanadamu.

4. MASKINI NA TAJIRI

            Nafahamu ya kuwa si mpango wa Mungu kwa mtu aliye tajiri kumtawala maskini kwa sababu ya umaskini wake. Na pia nafahamu si mpango wa Mungu kwa nchi zilizo tajiri kuzitawala nchi maskini kwa sababu ya umaskini wake.

    Lakini ni vizuri tufahamu uhusiano uliopo kati ya matabaka haya mawili:-

    Biblia inasema;“Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake  akopeshaye.” (Mithali 22:7)

Maneno haya ni kweli kabisa, na mtu ye yote ambaye ni msomaji wa historia na magazeti, anafahamu majadiliano ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini duniani.

Ukoloni mbaya uliopo sasa hivi kati ya nchi na nchi, ni ukoloni wa kiuchumi. Katika ukoloni huu wa kiuchumi nchi tajiri zinatumia utajiri wake katika kuzikandamiza nchi maskini. Na kwa njia hii mamillioni ya watu wamo katika hali mbaya sana kimaisha.

Na njia kuu ambayo nchi hizi tajiri zinatumia kuzitawala nchi maskini ni kwa njia ya kuzipa mikopo. Na nchi maskini zote zimejikuta zimeingia katika utummwa mbaya kwa sababu ya mikopo ambayo haijajulikana kama inaweza kulipwa yote.

Inakisiwa ya kuwa jumla ya madeni yote ya nchi zinazoendelea ni mabilioni ya dola za Kimarekani na yanazidi kuongezeka.

Ni kweli kabisa kwamba utajiri huu wa nchi hizo si wote uliopatikana kwa njia ya halali. Na wafuatiliaji wa mambo ya uchumi duniani, wanafahamu jinsi nchi hizi zilizoendelea zinavyobuni mbinu mbalimbali kuzinyonya nchi zinazoendelea.

Ingawa si mapenzi ya Mungu tuwe maskini, lakini pia si mapenzi ya Mungu tuwe matajiri ili kuwatawala wengine kwa sababu ya umaskini wao. Ole ni kwa matajiri wanaoutumia utajiri wao kuonea na kuwafanya wenzao kuwa watumwa.

Mungu anapotupa nguvu za kupata utajiri ndani ya Kristo ni kwa kusudi muhimu la kuimarisha agano lake la kumhudumia mtu mzima – kiroho na kimwili.

          Ni kweli maskini ana shida, maana hata biblia inasema maneno yake hayasikilizwi (Mhubiri 9:16). Na hii imejionyesha wazi sana katika maoni na malalamiko ya nchi maskini ambayo yanapuuzwa na kutosikilizwa na nchi tajiri.

          Lakini hali hii si kwa nchi tu, bali hata katikati yetu humu humu makanisani. Sehemu nyingi kuna wakristo ambao ni matajiri, na mara kwa mara huwa wanatumia utajiri wao katika kuwatawala viongozi wa kanisa; na hata wakati mwingine kudiriki hata kutaka kubadilisha maamuzi ya vikao vya kanisa.

          Na kwa upande mwingine viongozi wa sharika wanajikuta wameingiwa na hofu na kushindwa kuwakemea matajiri hao wakati wanapokwenda kinyume na maadili ya kikristo. Kama siyo ukoloni wa namna yake ulioingia katika kanisa ni nini basi?

          Naamini ya kuwa wachungaji na viongozi, wengi wao wangekuwa na hali nzuri kiuchumi, baadhi ya matajiri wanaotaka kutawala viongozi wengine wangeshindwa katika mbinu zao. Au wewe unasemaje?

          Shetani amekuwa akijitahidi sana kuwakandamiza wakristo wasiwe matajiri kwa kutumia njia mbali mbali kwa kutegemea mazingira yalivyo. Mahali pengine ametumia mifumo na vyombo vya fedha kama mabenki; pengine ametumia serikali, pengine ametumia mafundisho mabaya kwa wakristo, nakadhalika.

Na shabaha yake ya kufanya hivyo ni:-

(a)               Maneno ya wakristo yasisikilizwe wanapohubiri, kwa kuwa imeaandikwa; “….Walakini hekima ya maskini hudharauliwa wala maneno yake hayasikilizwi” (Mhubiri 9:19b). Kwa lugha nyingine maana yake “hayatiliwi maanani.”

(b)               Wakristo waendelee kuwa watumwa ingawa wanadai ya kuwa wamewekwa huru. Kumbuka imeandikwa hivi; “Tajiri humtawala maskini. Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye” (Mithali 22;7)

        Na maneno haya ni kweli kabisa. Hebu nieleze ni nani atakayesikiliza na kuyaamini maneno ya mchungaji au mwinjilisti au mtumishi yoyote wa Mungu anayesema mtegemee Yesu katika kila kitu wakati yeye mwenyewe ana nguo yenye viraka! Jambo la kwanza ambalo msikilizaji atajiuliza ni kwamba kama huyu Yesu ameshindwa kumpa mtumishi wake nguo nzuri, atawezaje kunisaidia mimi mkristo wa kawaida?

     Kwa hiyo lazima tuwe waangalifu ili tunayosema yawe sawa na tunavyoishi. Na tuishi sawa sawa na ahadi za Mungu tunazozisimamia.

     Siku moja nilimsikia mchungaji mmoja mwanafunzi wa chuo kimoja cha biblia akisema hivi; “Kuna mtu mmoja alikuja kutufundisha kuwa sisi kama wachungaji tusisikitike tunapoona hatuna nguo nzuri, wala chakula kizuri, wala sabuni nzuri za kuogea kwa sababu IKO SIKU MOJA VITU HIVI TUTAVITAWALA NA BWANA MBINGUNI”.

     Mara moja nikamkatisha na nikasema; “ Hayo mafundisho si sawa. Unadhani Mungu aliweka hivi vitu duniani (chakula, mavazi, sabuni) kwa ajili ya shetani na watu wake? Unadhani mbinguni tukifika tutahitaji tena chakula, mavazi na sabuni? Hivi vitu Mungu aliviweka kwa ajili yetu tuvitumie wakati huu.”

NANI ANAUPENDA WOKOVU WA KIMASIKINI?

            “Nani anaupenda wokovu wa Ukristo wa kimaskini?” Ukiona mtu amefika hali ya kujiuliza swali la jinsi hii, ujue ana hali ngumu sana kiuchumi.

            Hili swali nilijikuta najiuliza mwenyewe baada ya kuwa na hali ngumu sana kimaisha baada kuokoka. Kuna wakati fulani baada ya kuokoka mimi na mke wangu tulijikuta tumefika mahali pa kukosa hata dawa ya mswaki, nguo, viatu, na chakula kizuri. Licha ya shida hizi zote bado zilifuata zingine baada ya ndugu zetu wawili tuliokuwa tunawalipia masomo yao kufukuzwa na kurudi nyumbani kwa kukosa ada. Na waliambiwa wasirudi shuleni bila nusu ya ada!

            Unadhani tulikuwa na furaha tena? Ingawa tulikuwa tunasema tumeokoka, na mtu akituambia ‘Bwana asifiwe’ tuliitika ‘Amina’ ndani ya mioyo yetu tulikuwa na vita vikali na maswali mengi.

            Ni vigumu kuieleza hali hiyo tuliyoipitia ilivyokuwa ngumu kwa maneno. Lakini utaelewa mtu mwenye familia anavyojisikia anapoona anakosa hata fedha za kuwanunulia mke na watoto wake chakula licha ya mavazi. Wakati huo tulikuwa na mtoto mmoja.

            Hali ilivyozidi kuwa ngumu, ndivyo nilivyozidi kusongwa na mawazo. Ilifika wakati ambapo nilikuwa naona aibu hata kukaa sebuleni, maana niliogopa hata kuwaangalia wale vijana waliofukuzwa shule, nikijua kuwa wataniangalia kwa macho ya huruma ili niwape ada warudi shule. Lakini si kwamba nilikuwa siwahurumii, bali sikuwa na fedha za kuwapa.

            Ningeanzaje kuwaambia kuwa sina fedha, wakati wanajua nafanya kazi, na pia waliona nilikuwa na fedha nyingi kabla sijaokoka? Jambo hili lilinifanya niwaze sana. Inakuwaje kabla sijaokoka nilikuwa na fedha nyingi na baada ya kuokoka najikuta nimefilisika? Ingawa ni kweli kwamba kabla ya kuokoka fedha zingine nilizipata kwa njia zilizo kinyume cha ukristo lakini nilikuwa nazo. Na baada ya kuokoka ilibidi niziache njia hizo – na matokeo yake nilijikuta nimefilisika.

            Lakini nilikuwa nimesoma katika Hagai 2:8 kuwa fedha na dhahabu ni mali ya Mungu. Na pia nilijua kuwa vyote vya Mungu ni vyangu nikiwa ndani ya Kristo. Kwa hiyo ilikuwa vigumu kuelewa kwa nini Mungu aseme fedha ni mali yake, halafu mimi niliye mtoto wake nisiwe nazo.

            Ningewezaje kusema wokovu ni mzuri wakati baada ya kuokoka nimejikuta sina fedha za kutosha kununua chakula, nguo, dawa ya mswaki na hata kukosa ada za watoto! Je ndivyo Mungu anavyotaka tuwe baada ya kuokoka?

            Wakati huo ndipo nilipoelewa kwa nini wana wa Israeli waliyakumbuka masufuria ya nyama ya Misri, ingawa walikula nyama hizo wakiwa utumwani. Ni rahisi sana mtu aliyeokoka kurudia njia au maisha mabaya ya kutafuta fedha kwa njia zilizo kinyume cha ukristo anapokuta anabanwa na matatizo ya kiuchumi maishani mwake. Na hata wakati mwingine unakesha katika maombi ili kumlilia Mungu akupe chakula na mavazi unaona kama vile hasikii.

            Nilipokuwa nasumbuliwa na hali hii ndipo nilipojikuta najiuliza mwenyewe; “ Nani anaupenda wokovu wa kimaskini?” Nilijikuta siupendi kabisa. Ni wokovu gani huu ambao haunisaidii hata kutunza familia yangu?

            Siku moja nilimuuliza mke wangu; nikasema; “Je! wewe unaupenda wokovu wa kimaskini?”

            Akajibu; “Hapa, siupendi!”

            Nikasema; “Naona tuna mawazo yanayofanana. Kwa hiyo naona ni muhimu tumuulize Mungu katika maombi kwa nini tulipokuwa kwa shetani tulikuwa na fedha za kutosha, lakini baada ya kuokoka na kuja kwake tunajikuta hatuna fedha hata za kununulia vitu muhimu?”

            Baada ya kukubaliana hayo, mimi na mke wangu tulianza kumwomba Mungu kwa mfululizo wa siku tatu juu ya jambo moja hilo hilo. Namshukuru Mungu kwa kunipa mke ambaye aliweza kusimama pamoja nami katika maombi juu ya jambo hili. Sijui ningekuwa na hali gani kama angelalamika. Namshukuru Mungu mke wangu hakulalamika bali ALIOMBA PAMOJA NAMI.

            Mungu alitujibu maombi na akaanza kutufundisha mambo mengi ambayo mengine nawashirikisha katika ujumbe huu.

            Tulijua hakika kuwa hayakuwa MAPENZI YA MUNGU tuwe na hali ngumu ya kimaisha namna hiyo – kukosa fedha za kutosha kununulia nguo, chakula na vitu vingine muhimu. Na baada ya kuyaweka katika matendo yale tuliyoambiwa na Bwana yaliyo katika neno lake, hali yetu ilibadilika. Na matatizo tuliyokuwa nayo wakati ule yakaisha. Tukaanza kuona furaha tena katika maisha haya ya wokovu.

            Ni vizuri kujua kuwa Mungu wetu hapendi tuwe maskini. Wala hapendi wokovu wa kimaskini! Ndiyo maana alimtuma Mwana wake wa Pekee, Yesu Kristo kutukomboa.

            Kwa kukumbusha tu, Yesu Kristo aliyafanya yafuatayo kwa kufa na kufufuka kwake:

            "Yesu Kristo alifanyika dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tuhesabiwe haki bure ndani yake ya kusimama tena mbele ya Mungu" 
(2Wakorintho 5:21)

            "Yesu Kristo aliuchukua udhaifu wetu, ili katika mambo yote tuzitegemee nguvu zake" (Mathayo 8:17; Wafilipi 4:13)
            Yesu Kristo aliyachukua magonjwa yetu, ili tusitawaliwe na magonjwa tena na kwa kupigwa kwake tumepona (Isaya 53:4,5; Mathayo 8:17; 1 Petro 2:24)
Yesu Kristo aliyachukua masikitiko na huzuni zetu, ili tukae katika amani yake ipitayo fahamu zote (Isaya 53:34; Wafilipi 4:6,7)
            Yesu Kristo alikuwa maskini kwa ajili yetu ingawa alikuwa tajiri, ili sisi tupate kuwa matajiri katika Yeye (2 Wakorintho 8:9)

Ndiyo maana matunga Zaburi 23 aliandika hivi:

“Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU.Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake …. Hakika WEMA
NA FADHILI zitanifuata siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele”.

            Ni rahisi sana kusema. “Bwana ndiye mchungaji wangu, SITAPUNGUKIWA NA KITU, lakini je! Ni kweli hujapungukiwa na kitu? Je! Zaburi hii ni ya kweli, au ni maneno mazuri tu ya kutungia nyimbo?

            Lakini napenda kukutia moyo kuwa maneno haya ni ya kweli, ukikaa ndani ya Kristo hutapungukiwa na kitu. Ndiyo maana Mungu alimwambia Yoshua ya kuwa atii maagizo yake yote na kuyafanya HATAMPUNGUKIA WALA KUMUACHA (Yoshua 1:5)

            Kwa kuwa maneno haya ni ya kweli, mbona basi wakristo wengi WAMEPUNGUKIWA NA VITU? Tatizo haliko kwa Mungu, bali kwetu sisi. Na tuwe watendaji wa neno na tutaona mafanikio.


WAJIBU WA WAKRISTO:
            Ni wajibu wa wakristo (a) kusaidiana sisi wenyewe kiuchumi; na (b) Kuwasaidia kiuchumi watu wengine wasio wakristo. Kuna wakati fulani mtu mmoja alikuja kwangu kuomba ushauri.

            Nikamuuliza. “Una tatizo gani linalokukabili?”

            Akasema; “ Baada ya kuokoka ilibidi niache njia fulani fulani ambazo zilikuwa zinanisaidia kupata fedha kwa kuwa zilikuwa ni kinyume cha maadili ya kikristo. Lakini sasa naona napata shida, sina fedha za chakula, wala sijui kodi ya nyumba mwezi huu nitapata wapi. Licha ya hayo, wale niliowakopa fedha kufanyia biashara hizo nilizoziacha wananidai fedha zao. Hata naogopa kukutana nao. Hebu nisaidie mawazo, najua nimeokoka kweli, lakini NITAISHIJE KATIKA HALI HII?”

            Unadhani swali lilikuwa jepesi kujibu? Si swala la kumwambia tuombe halafu umwache aende zake! Yeye anachotaka baada ya kuomba aone msaada unamjia. La sivyo maombi hayo yanakosa maana kwake.

            Swali hili “Nitaishije katika hali hii?” Linawasumbua walio wakristo wengi siku hizi. Na umefika wakati wa kulijibu.

            Ngoja nikuulize swali jingine. Unadhani mwanamke ambaye anafanya uasherati ili kupata fedha za kuwalishia watoto wake hajui kuwa uasherati ni dhambi? Nina uhakika anajua kwa kuwa kuna mwingine hata kama anafanya hayo hakosi kila jumapili kanisani, na wakati mwingine hutoa sadaka kwa fedha hiyo hiyo. Unadhani hajui kuwa uasherati ni dhambi? Unadhani hamwelewi mchungaji anaposema acheni dhambi? Unadhani haogopi magonjwa ya zinaa? Unadhani anapenda kufanya hivyo? Nina hakika walio wengi hawapendi kufanya hivyo. Lakini jambo linalomsumbua, akiacha uasherati atapata wapi fedha za kuwatunza watoto wake? Nina uhakika akijibiwa swali hili ni rahisi kuacha tabia hiyo chafu.

            Wasichana wengi mashuleni wamejikuta wamebeba mimba na kuharibu usichana wao kwa kudanganywa na fedha wanazozihitaji kwa ajili ya kununulia mafuta ya kupaka, nguo, na kutengeneza mitindo ya nywele.

            Vijana wengi wa kiume wamejikuta wamejiingiza katika biashara haramu kwa sababu ya kutaka utajiri wa haraka haraka.

            Kwa sababu ya kutokujua la kufanya wakristo wengi wamepoteza ushuhuda wao kwa sababu ya matatizo ya kiuchumi.

            Wakristo wenzetu walifanyaje? Tusome kitabu cha Matendo ya Mitume 4:32,34,35.

            “Na jamii ya watu waliamini (Wakristo) walikuwa na MOYO MMOJA NA ROHO MOJA; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na VITU VYOTE SHIRIKA. WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa; wakaiweka miguuni pa mitume, kila mtu akagawiwa KWA KADRI YA ALIVYOHITAJI”

            Utaona katika habari hii ya kuwa kwa sababu ya Ukarimu na kutokuwa na ubinafsi wakristo hao waliweza kupambana na tatizo la umaskini katikati yao. Ndiyo maana ikandikwa kuwa; “WALA HAPAKUWA NA MTU MMOJA MIONGONI MWAO MWENYE MAHITAJI”. Jina la Bwana libarikiwe!

            Matokeo ya usharika namna hii ni haya; “Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote” (Matendo ya Mitume 4:33)

            Je! Siku hizi hakuna wakristo wenye mahitaji kati yetu? Na tunafanya nini ili kuwasaidia? Je! Kuwaombea tu kunatosha? Je! Unashangaa kwa nini ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu hautangazwi kwa nguvu na wakristo? Nadhani wakristo wengi wanatumia muda wao mwingi sana kujitafutia mahitaji yao kiasi ambacho muda unaobaki hautoshi kufanya kazi ya kushuhudia.

            Wenzetu walisaidiana, na sisi tusaidiane. Wazazi mara nyingi huwa wanawasaidia vijana wao waliowaoza kuanza maisha mapya. Na fahamu kuwa wokovu ni maisha mapya. Tunawajibika sana kuwasaidia wale wanaookoka kiroho na kimwili kuanza maisha mapya ndani ya Kristo. Kwa kukosa msaada wa kiuchumi, wengi wamepoa na kurudi nyuma.

            Niliwahi kushirikishwa ushuhuda mmoja ambao naamini utakusaidia kukuelewesha jambo hili ninalokuambia.

   

Поиск
Категории
Больше
DARASA LA 7
DARASA LA 7
Orodha ya masomo yote ya darasa la 7
От PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 10:17:36 0 5Кб
ESTHER
Verse by verse explanation of Esther 2
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-04-02 12:47:34 0 6Кб
FORM 1
BIOLOGY: FORM 1
List of all topics in Biology for form 1 class: CLICK HERE TO DOWNLOAD. INTRODUCTION TO BIOLOGY...
От PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-30 04:39:58 0 5Кб
1 SAMUEL
Verse by verse explanation of 1 Samuel 23
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-01-26 04:15:25 0 5Кб
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Deuteronomy 11
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 31 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-01-25 06:01:25 0 5Кб