MTOFAUTISHE NA WENGINE

0
6K

KWELI KUU: Mwenzi wako wa ndoa hafanani na yeyote yule, anafanana na wewe, na wala halingani na yeyote yule; ni tofauti na wengine wote, ni wa pekee kwa ajili yako; kwa ajili ya furaha yako.

Wimbo Ulio Bora 2:3

Kama mpera kati ya miti ya misituni,
Kadhalika mpenzi wangu kati ya vijana,
Nalikuwa kivulini mwake kwa furaha,
Na matunda yake naliyaonja kuwa matamu.

Muktadha Wa Kifungu hiki cha maandiko:
Katika maandiko haya mpenzi anamwimbia mpenzi wake, maneno yake ni matokeo ya upendo wake na jinsi anavyomtazama mpenzi wake. Sasa anamtazama kwa namna ya tofauti sana; si kama anavyowatazama watu wengine, na kwa sababu hiyo hamfananishi na mtu yeyote mwingine, yeye ni wa tofauti kwake, na ni maalumu sana machoni pake na ndani ya moyo wake. Na kwa sababu ya umaalumu na upekee alionao mwenzi wake, basi anamtendea mambo yanayomtofautisha na wengine wote ikiwa ni pamoja na kumwimbia wimbo wa mapenzi. Upekee na umaalumu anaompa mpenzi wake, si kwa maneno tu bali pia kwa matendo unamzalia matunda kwa mpenzi wake, si kwa sababu aliyatarajia tu hayo matunda bali ni kwa sababu ya kanuni ya kupanda na kuvuna. Mpenzi anafurahia matunda yatokanayo na mpenzi wake wa pekee. Kwa sababu hiyo, hapati tabu wala haoni shida kumpenda mpenzi wake kwa namna ya kipekee sana.

Mapenzi ni kupeana upekee ambao hakuna mwingine unayempa upekee na umaalumu huo. Kama mapenzi ni ya kustawi basi lazima yafunikwe na yaambatane na tabia ya kupeana upekee kuliko watu wengine wa nje ya ndoa hiyo. Hii sio kwa watu, mpaka kwa vitu, kazi na shughuli mbalimbali nyingine za maisha. Usiipe simu upekee kuliko mwenzi wako, kazi yako isiwe ya pekee kwako wala biashara yako kuliko mwenzi wako. Upekee ni pamoja na kuacha vyote kwa ajili ya mwenzi wako isipokuwa Mungu tu ambaye ndiye mtawala wa ndoa yenu anayewaweka salama na aliyewaunganisha. Mahusiano ya ndoa ni kupeana upekee na umaalumu kuliko unavyowapa watu wote wengine wa nje na vitu vingine vyote ambavyo vipo kwa ajili ya kuwarahisishia utendaji katika ndoa yenu katika kukabiliana na changamoto mbalimbali ili kutimiza kusudi la Mungu. Sasa endelea na somo.

Somo langu la leo litakuwa linajibu swali la, Kwa nini wanandoa wengi wanatamani wenzi wa ndoa wa wengine wawe wenzi wao wa ndoa? Au Kwa nini wanandoa wengi wanatamani kutoka nje ya ndoa kwa kuwa na wapenzi wengine zaidi ya wenzi wao wa ndoa? Wapo ambao wanatimiza matamanio yao kwa siri, na wengine wazi wazi kwa kuvunja ndoa zao na kuwaacha wenzi wao wa kwanza na kuanzisha mahusiano mapya, na wapo wengine ambao wanaishia kutamani tu lakini wasiweze kutimiza matamanio yao. Pengine ni kwa sababu ya kuogopa kumkosea Mungu kwa kuvuka mipaka ya Neno la Mungu, na wengine labda kwa kuogopa kuvunja heshima zao katika jamii inayowazunguka.

Uzoefu unaonyesha kuwa kati ya taasisi zote hapa duniani, taasisi ya ndoa inaongoza kwa migogoro, changamoto mbalimbali baina ya wahusika wanaofanya taasisi hiyo kuwepo hata kufikia hatua ya taasisi hii ya ndoa kuvunjika. Pamoja na kuwa wengi wanaingia katika ndoa, bado wapo wengi wanaovunja muunganiko wao wa kindoa kwa kuachana kabisa. Na bado wapo wengi wanaovumiliana kwa kuvumilia maumivu yanayosababishwa na wao wenyewe kushindwa kuelewana na kuchukuliana. Hali hii inafanya kuwepo kwa idadi ndogo sana ya ndoa ambazo wanandoa wanafurahia ndoa zao.

Ni lazima tutambue kuwa, ndoa ni taasisi nyeti sana ambayo ndio inaotumika kuzalisha rasilimali watu wanaotumika katika taasisi nyingine zote; iwe ni taasisi za kiserikali, au za binafsi ikiwa ni pamoja na kanisa kwa ujumla wake. Ndoa inapoharibika, familia inaharibika, na familia inapoharibika, kanisa linaharibika, na jamii pia inaharibika, hivi vinapoharibika taifa linaharibika. Hawa wote ninaozungumzia ni watu ambao wanazaliwa na kutengenezwa kuwa wazuri (au kuwa wabaya) na taasisi ya ndoa katika familia. Ndoa ni kitu nyeti sana na ndio maana shetani anatafuta kuharibu ndoa kwa makusudi ya kuharibu kusudi la Mungu kwa wanadamu.

Kila ndoa ipo kwa kusudi maalumu chini ya jua; na kila mwanandoa yupo kwa kusudi maalumu chini ya jua kupitia ndoa yake. Ndoa ikiharibika, basi kusudi limeharibika. Na ndoaa inaharibika kwa wanandoa kuharibika.

Sasa tuangalie sasa somo letu sawa sawa na kichwa chetu cha somo hapo juu. Ndoa nyingi zinaharibika au kuvunjika kwa sababu ya wanandoa wenyewe, na si kwa sababu ya watu wa nje. Hakuna mtu wa nje anayeweza kuvunja ndoa ya wawili wapendanao isipokuwa wao wenyewe. Kama wanandoa watasimama na kujitambua, na kukusudia kutotengana kwa namna yoyote ile katika hali yoyote kwa gharama zote, basi hakuna atakayewatenganisha isipokuwa kifo tu.

Tatizo la ndoa nyingi kuvunjika na kuwepo kwa matendo ya kuvunjiana uaminifu kwa wanandoa, pamoja na migogoro isiyoisha baina yao ni KILA MMOJA KUTOMTOFAUTISHA MWENZI WAKE NA WATU WENGINE.

Jambo la Kwanza:
Mwenzi wako si malaika, kwa hiyo usimfananishe na malaika, mtofautishe na malaika. Mwenzi wako ni mwanadamu kama wewe, na kwa sababu ni mwanadamu na si kama malaika hajui kila kitu, hawezi kila kitu, si mkamilifu hata kidogo, hajakamilika; kwa hiyo anaweza kukosea kwa kujua au kwa kutokujua, anaweza pia hasiweze kufanya yale uyatakayo kwa kiwango na ubora uutakao, kwa sababu ni mwanadamu na hawezi yote. Ni Mungu tu anayejua yote, na ni Yeye tu anayeweza yote, na si mwanadamu; kwa hiyo ni vyema ukamtofautisha na watu wa mbinguni.

Na kwa sababu mwenzi wako wa ndoa si malaika wala si Mungu, ni mwanadamu wa kawaida kabisa, anaweza kughafilika na akatumiwa na shetani kuvuluga ndoa yenu. Kwa sababu hiyo sio hekima sana kudhania kuwa hawezi kukosea hata kidogo, na kwamba hawezi kurudia makosa; anaweza kukosea tena hata mara saba mara sabini kwa siku katika kosa lile lile kwa sababu ni mwanadamu. Kwa sababu anaweza kukosea mara zote nawe unapaswa kumsamehe mara zote; kwa sababu anaweza kushindwa mara zote kufanya yale uyapendayo wewe kwa ubora na kiwango ukitakacho wewe basi unapaswa mara zote kumvumilia na kumwelekeza kwa upole na upendobila kuchoka wala kumwonea hasira.

Kila mtu anaweza kukosea mara zote, na kwa sababu hiyo anapaswa kusamehewa mara zote; wakati mwingine anaweza kukukosea hata bila kujua kama amekukosea, wewe kama mwenzi wake wa ndoa unapaswa kwa upole kabisa kumweleza kosa lake bila kuhoji kwa nini amekosea. Wewe jua tu, kwa sababu sio malaika anaweza kukosea kila sekunde na kila dakika na kila saa siku nzima, lakini cha msingi wewe jua kuwa yeye si malaika kama wewe usivyo malaika.

Petro anamuuliza Yesu kuwa, Jirani yangu anikosee mara ngapi nimsamehe, hata mara saba? Yesu akamjibu kuwa, sio mara saba, hata mara saba mara sabini. Hii inaonyesha kwanza, jirani yako ambaye ni mwanadamua anaweza kukukosea mara nyingi sana kwa siku, pili kusamehe watu si swala la namba ni swala la wakati wote kila unapokosewa, na jirani yako wa kwanza ni mwenzi wako wa ndoa.

Ndoa nyingi zinavunjika pale wanandoa wanapodhani wenzi wao katika ndoa ni malaika hawawezi kukosea kwa sababu wanajua yote na wanaweza yote. Ukiwa na mtazamo huu maana yake umemfananisha mwenzi wako na malaika na Mungu katika utendaji wake na kuenenda kwake, na kwa sababu hiyo atakapoanza kukukosea utanza kutafuta mwingine au kufikiria juu ya mwingine ambaye hawezi kukukosea. Mke au mume wako ni miongoni mwa wanadamu kama wewe ulivyo miongoni mwa wanadamu, ni vyema usimchukulie kama malaika ili uwe na uwezo wa kumsamehe na kumchukulia pale anapokukosea na kushindwa kufanya yale uyatakayo kwa namna utakayo. Ukijua kuwa ni mwanadamu na ya kuwa hawezi yote na hajui yote, utamwelekeza na kumfundisha kwa upole na uvumilivu mwingi huku ukimfurahia vile alivyo. Makosa yake yakuweke karibu na yeye na si yakutenge mabali na yeye, upungufu wake ukuweke karibu na yeye na si ukutenge mbali na yeye. Hivi unajua kwa nini mpo pamoja? Kwa sababu yeye hajakamilika bila wewe na wewe hujakamilika bila yeye, na kwa sababu hajakamilika ndio maana unao uwezo waa kuona mapungufu na makosa yake ili uweze kumkamilisha. Vyovyote alivyo kwako ni kwa sababu wewe ni mtu pekee wa pekee wa kukamilisha mapungufu yake na kurekebisha makosa yake kwa upendo, upole na uvumilivu mwingi hali ukimchukulia vile alivyo.

Muhubiri 4:9, 10:

Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja;
Maana wapata ijara njema kwa kazi yao.
Kwa maana wakiangukammoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua
.​


Makosa ya mmoja katika ndoa ni makosa ya wote, hata kama mmoja amemkosea mwenzake, bado ni makosa ya wote tena ni makosa ya kibinadamu. Kwa hiyo wewe uliyekosewa ndiye uliyeona namna mlivyokosea kwa mwenzako kukosea, na kwa sababu hiyo unapaswa umwinue usimkandamizie chini mahali mlipoanguka. Biblia inasema, Kwa maana WAKIANGUKA, yaani wote, mmoja atamwinua mwenzake. Hii ina maana ya kuwa, maisha ya ndoa sio maisha ya kudidimizana na kukandamizana chini ni maisha ya kuinuana, kila mmoja anamwinua mwenzake kutoka pale walipoanguka wote.

Wanandoa ni mwili mmoja, mmoja akifanya vyema wote wamefanya vyema, na mmoja akikosea wote wamekosea, kwa hiyo mmoja ni lazima amwinue mwenzake kisha waendelee na maisha kama kawaida. Usimkandamizie chini mwenzi wako mahali ambapo mmeanguka, kwa kuwa wewe umeinuka, basi mwinue na mwenzako, usichukulie tu kuwa amefanya makusudi kuanguka; maadamu yeye sio malaika basi, ndio maana ameanguka pamoja nawe na kwa sababu hiyo unapaswa kumwinua.

Ili umfurahie mwenzi wako, ni lazima umtofautishe na malaika katika utendaji kazi wake na mwenendo wake, katika hali ya kujua yote na hali ya kuweza yote anayopaswa kutenda. Ni vizuri ukawa na mtazamo huu, ya kwamba mwenzi wako wa ndoa anaweza kukukosea wewe katika kiwango chochote kile wakati wowote ule bila kujali udogo au ukubwa wa kosa, wakati gani kakukosea katika mazingira yapi. Na ni vizuri ukaelewa kuwa, bila kujali ukubwa wa kosa au makosa aliyokukosea, bila kujali wakati na bila kujali mazingira ya makosa yake kwake unapaswa kumsamehe kabisa kwa upendo, unyenyekevu na upole wote.

Unajua, ukitaka raha ya kukaa chini ya kivuli cha mapenzi ya mwenzi wako na kula matunda yatokanayon na mapenzi yake kwako, mtofautishe na malaika kisha mchukulie kama mwanadamu ambaye ni mwenzi wako wa ndoa aliye karibu na wewe kuliko wengine wote katikati ya wote. Mwandishi wa Wimbo ulio Bora anamtaja mpenzi wake na kusema, "Kama mpera kati ya miti ya misituni, kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana". Hii ni lugha ya kumtofautisha mwenzi wake na kitu kingine chochote na kisha kumweka kwenye viwango vya wanadamu lakini aliye mwanadamu tofauti kwa ule umaalumu anaompatia. Wengine ni vijana kama yeye alivyo kijana, lakini huyu kijana ni kijana aliye mpenzi wake wa pekee, kwa sababu hiyo anapaswa kuchukuliana naye kwa uangalifu mkubwa sana, kwa sababu hawezi kumpata mwingine kama yeye kwa sababu ni wa pekee kama vile mpera ulivyo mmoja tu ndani ya msitu mkubwa wa miti mingine ya mistuni ambako hakujawahi kuwa na makaazi ya watu.

Mpe mwenzi wako upekee, usimlinganishe hata na malaika katika utendaji wake na mwenendo wake mwapo pamoja katika maisha ya kila siku mkipitia changamoto mbalimbali za maisha. Daima usimchukulie mwenzi wako kama malaika, mtofautishe, mchukulie kama alivyo, mchukulie kama Mungu anavyomchukulia, na kisha muhudumie (treat him or her) kama mwenzi wako wa ndoa ambaye ni mwanadamu kama wewe.

Jambo la Pili:
Mwenzi wako hana moyo wa chuma; Usimfananishe mwenzi wako na chuma. Kama mwanadamu anaumia pale unapomkosea bila kujali ukubwa au udogo wa kosa ambalo umemtenda. Kwa sababu unatofautiana kabisa, lililo dogo kwako ni kubwa kwake, na lililo si kitu kwako ni kitu kwake, kwa sababu hiyo ni vyema ukamchukulia kama mwanadamu anayeumia na ukajali hisia zake hata katika mambo yale ambayo wewe unaona ni upuuzi, lakini kwa sababu yamegusa moyo wake, onyesha kujali, usichukulie kirahisi mambo ambayo kwake ni mazito na yanagusa na kusumbua moyo wake. Yeye sio chuma, yeye ana moyo wa nyama na si moyo wa jiwe. Kama Mungu mwenyewe akikosewa anaumia, sembuse yeye mwanadamu kama wewe; mbona wewe ukikosewa unaumia, kwa nini yeye asiumie.

Unajua, wapo watu ambao wanamtazamo wa kwamba kila wakati wao wako sahihi, hawakosei, na hata wanapojua kuwa wamekosea hupotezea makosa yao, na kujichukulia kama wamekosea. Lakini wapo watu ambao wao wenyewe wanajiona kuwa wanastahili kukosea wengine na si kukosewa, kwa hiyo wanaendelea kuwakosea wengine ili mradi tu wapate kile wanachotaka wao; hawa ni watu wenye ubinafsi na moyo mgumu, hawaoni makosa yao ila makosa ya wengine na wao wakati wote wako sahihi. Watu wa aina hii wanapoingia katika ndoa huwachukulia wenzi wao kuwa wana mioyo ya jiwe, hawaumizwi na yale makosa wayatendayo kwa wenzi wao. Hawa ni watu wasiojali hisia za wenzao, wanarahisisha kila jambo na kulipotezea. Ukijaribu kuwaambia kuwa ulivyofanya umenikosea, utasikia wanasema, Na wewe umezidi, jambo dogo kama hili unasanuka kama nini. Ni watu ambao katika fahamu zao wana mtazamo wa kuona wengine hawawezi kuumia kwa yale wanayoyafanya.

Hebu usiwe wewe, usimchukulie mke au mume wako kama gumegume asiyeumizwa na mambo uyafanyayo ambayo hayampendezi, hata kama yanaonekana kwako ni mazuri tu na ni sawa kuyatenda, na kwa sababu hiyo ukalazimisha tu kuyatenda bila kujali hisia za moyo wa mwenzi wako. Wengine huwa hawaongei unapowakosea ila ukiangalia mwitikio wao katika yale unayofanya unaona kabisa wanaumia. Sasa wewe usikuchulie kirahisi eti tu kwa sababu huyo mwenzi wako hajasema. Rudi pale alipo, ingia kwenye viatu vyake, sikia maumivu anayoyasikia, kisha mwinue kwa kumfanya awe vizuri, na kama umemkosea, mwombe msamaha kwa unyenyekevu na upole wote.

Mwenzi wako wa ndoa ni wimbo ulio bora kuliko nyimbo zote, kwa hiyo mchukulie kwa upendo wote, unyenyekevu wote, upole wote na uvumilivu wote; ukimtofautisha na wengine utakula matunda yake ukiwa umeketi chini ya kivuli chake kizuri. Tatizo ni kwa sababu unamchukulia kirahisi tu na kumfananisha na wengine katika matendo yako kwake ndio maana amenyauka, amekauka, hana tena kivuli na wala hana tena matunda. Wewe mtofautishe tu na wengine, utaona matunda yake na kuyala na utaketi chini ya kivuli chake.

Jambo la Tatu:
Mtofautishe mwenzi wako na wewe mwenyewe: Usifikiri watu wote wapo kama wewe, na usifikiri eti kwa kuwa huyo ni mke au mume wako, basi yupo kama wewe. Hapana, mnatofautiana kabisa japokuwa mnafanana kwa maana ya kufaana. Wewe ni tofauti na yeye na yeye ni tofauti na wewe. Ni makosa makubwa sana kumfananisha mwenzi wako na wewe kimtazamo, kihisia, kisilika, kihulka, na kitabia; mnatofautiana. Namna anavyopokea mambo si namna unavyopokea wewe mambo na taarifa mbalimbali, namna anavyochukulia mambo si namna wewe unavyochukulia mambo, namna anavyotazama jambo si namna yeye anavyotazama jambo lile lile. Kwa hiyo kufanya mambo kama uonavyo wewe ukidhani na yeye atakuwa anaona vile vile, au kudhani atakuwa tu anaelewa kama wewe unavyoelewa ni makosa makubwa na lazima mgogoro uzaliwe hapo katikati.

Unajua kuna watu wanashangaza sana, wao huzani watu wote ni kama wao, wana uelewa kama wa kwao, mawazo kama ya kwao, fikira kama za kwa na mitazamo kama ya kwao, na kwa sababu hiyo hata wanapogundua kuna tofauti ya mambo hayo baina yao na wengine huwa hawataki kukubali, huanza kulazimisha watu wafikiri kama wao wanavyofikiri, watazame kama wao wanavyotazama, wawaze kama wao wanavyowaza; hiki ni kitu kisichowezekana kabisa. Huwezi kulazimisha hata mtu mmoja awaze kama wewe unavyowaza au kufikiri kama wewe unavyofikiri wakati mliumbwa tofauti na mkawekewa tofauti ndani yenu kwa kusudi la kuleta uwiano sahihi baina yenu.

Sasa basi, kwa sababu mwenzi wako hafanani na wewe, ni vizuri ukafahamu tofauti iliyopo kati yako na yeye, na katika kila ulifanyalo ulifanye ukizingatia kuwa mwenzi wako sio kama wewe anaweza kuchukulia tofauti hilo ulifanyalo, na kwa hiyo uwe tayari kukubali changamoto hiyo. Usiamue tu kufanya kitu eti kwa sababu wewe hakikupi shida, je na mwenzako hakimpi shida? Sio kwa sababu wewe hakikupi shida basi na mwenzako hakimpe shida, na sio kwa sababu wewe umekikubali na mwenzako moja kwa moja amekikubali, hapana, japokuwa ninyi ni mwili mmoja lakini ni watu wawili tofauti wenye akili kila mmoja na za kwake mwenyewe, wenye uzoefu tofauti wa maisha na malezi tofauti na mmekulia katika mazingira na familia tofauti, kwa hiyo hamuwezi kufanana kabisa na kulingana katika kila kitu.

Sio kwa sababu wewe umeamua kufanya jambo fulani lenye mstakabali na maslai ya familia, basi na mwenzako ameamua; wewe ni wewe na yeye ni yeye; majadiliano ya pamoja ni lazima. Mshirikishe katika kila jambo, heshimu maoni yake hata kama kwako ni pumba lakini kwake amejaribu kutoa kilichobora kabisa. Ametumia akili zake zote kufikiria na kisha kusema, kwa hiyo onyesha heshima katika mawazo yake. Heshimu pia hisia zake hasa katika mambo yale ambayo hayaonekani kugusa hisia zako kama yalivyogusa hisia zake, wewe heshimu tu kisha kwa upendo, msaidie, mweleweshe mpaka aelewe na kama haelewi, mvumilie mpaka atakapoelewa, kufanya vinginevyo ni kuzua ugomvi katikati yenu.

Kwa upande mwingine, si kila kitu mwenzi wako anachokushirikisha mkifanye au msikifanye ni lazima ukielewe kwanza ndipo umkubalie, wakati mwingine kwa sababu ni mtu pekee ambaye umejitoa kumwanini, ni muhimu ukamkubalia hata kama humwelewi. Mpe nafasi, kwa sababu mpo tofauti hata katika uelewa mnatofautiana, pengine wewe ili kuelewa jambo ni mpaka pale utakapoona linafanyika, na kabla halijafanyika hutakuja kuelewa. Sasa ukimkatalia eti kwa sababu hujaelewa na ufahamu wako ni mzito, mtaendelea lini?

Mpe umaalumu mpenzi wako, mpe upekee mpenzi wako; yeye ni wa thamani kuliko kingine chochote chini ya jua, kama utashindwa kumfanya wa pekee na maalumu kwako, kamwe huwezi kumfurahia, na badala yake utamwona kuwa ni kikwazo katika mambo yako. Mwenzi wako anapoonekana kuwa kikwazo katika njia yako, kitu cha pekee cha kufanya ni kumkwepa, sasa hii katika ndoa si kitu kizuri kabisa, ni chanzo cha matatizo mengi katika ndoa.

Niwashauri vijana ambao bado hawajaoa na wale mabinti ambao bado hawajaolewa, kwamba, kama huyo unayetaka kumwoa na huyo unayetaka kuolewa naye huwezi kumtofautisha na malaika, ukamtofautisha na mtu mwenye moyo wa jiwe, na ukamtofautisha na wewe mwenyewe, hairisha mpango wako wa kuoa au kuolewa, ndoa itakushinda; maana unatengeneza tatizo ambalo hapana mtu atakayekuja kulimaliza, hata Mungu mwenyewe hatalimaliza. Tatizo la namna hii haliishi kwa maombi, linaisha kwa wewe mwenyewe kufanya unayopaswa kufanya, ndio maana nimesema hata Mungu mwenyewe hawezi kulimaliza. Biblia imesema wazi kuwa, Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa, haijasema Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maombi. Kama huwezi endelea kuwa 'single' tu, vinginevyo unatafuta matatizo wewe mwenyewe.

Jambo la Nne:
Mtofautishe mwenzi wako na watu wa nyumbani kwenu; Wazazi wako, ndugu zako na rafiki zako: Biblia kwa kuonyesha upekee wa uhusiano wa kindoa baina ya mke na mume, imesema, Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja (Waefeso 5:31; Mwanzo 2:24). Kama mwanaume anaacha, basi na mwanamke anaacha; ili kuambatana na yule ambaye umemwona kuwa ni mtu wa pekee kwako lazima uwaache wengine. Zaburi 45:10, 11; inasema, Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako. Naye mfalme atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie. Hii inaonyesha kuwa swala la kuacha si la upande mmoja sana, lakini inaonekana kwa upande wa wanawake mabinti kuacha watu wa nyumbani kwao huwa ni ngumu sana, na ndio maana mtunga zaburi akimwasa binti ambaye alikuwa ameolewa na mfalme anaweka msisitizo mkubwa katika usia wake kwa binti huyo kumwambia kuwa awasahau kabisa watu wake na nyumba ya baba yake.

Ndoa ni swala la wewe na mwenzi wako katika ndoa hiyo, si swala la wengine nje ya nyinyi wawili. Mke au mume wako ni wa pekee kuliko ndugu zako, na ni maalumu sana kuliko wazazi wako inapofika kwenye swala la ndoa. Inashangaza sana unapowapa wazazi wako umakini kuliko mwenzi wako wa ndoa; wazazi na marafiki na ndugu wanapata huduma bora kuliko mwenzi wako wa ndoa; unasikiliza ushauri wa wazazi wako, ndugu zako na rafiki zako kuhusu maswala mbalimbali ya ndoa yenu unaacha ushauri wa mwenzi wako wa ndoa; unatumia muda mwingi kuwa na rafiki zako kuliko kuwa na mwenzi wako wa ndoa. Swali nakuuliza, Hivi wewe umesahau kweli watu wako na nyumba ya baba yako? Hivi kweli wewe umemwacha baba yako na mama yako na kuambatana na mke wako na kuwa mwili mmoja? Ndoa itakushinda bila shaka!

Ukitaka wewe na mke wako muwe mwili mmoja, waache kwanza wazazi wako na uambatane na mke wako, na wewe mke ukitaka bwana wako autamani uzuri wako tu (kwa maana ya kukupa upekee wa kipekee na umaalumu wa kipekee) wasahau watu wako na nyumba ya baba yako. Ni kwa sababu hujamtofautisha mwenzi wako na wengine na ndio maana hao wengine hawajamtofautisha mwenzi wako na wao wenyewe, wanaona kana kwamba thamani yao na yake mbele zako ni sawa na pengine ya kwao ni kubwa kuliko ya mwenzi wako, sasa ni lini watamweshimu mwenzi wako kama mume au mke wako?

Mtofautishe mwenzi wako kihuduma kwa huduma unazompatia, usimchukulie kama unavyowachukulia wengine ikiwa ni pamoja na ndugu zako na rafiki zako. Yeye ni wa pekee kwako na ndio maana unawaacha wote na kuambatana naye. Hili si swala la wewe au yeye kuondoka nyumbani kwao tu, ni swala na wewe na yeye kuwasahau watu wa nyumbani kwenu inatofika katika swala la ndoa (wewe na yeye). Usiache kumfanyia mwenzi wako jambo analohitaji ikiwa katika uwezo wa mikono yako eti kwa sababu bado hujawafanyia wazazi wako. Sio eti kwa sababu hujawahi kuwafanyia wazazi wako na ndugu zao ndio usimfanyie mwenzi wako. Kama mwenzi wako hana tofauti na wazazi wako basi kulikuwa hakuna haja ya kuoa au kuolewa, ungebaki kwa wazazi wako. Kuwathamini wazazi wako na ndugu zako ni kumtesa mwenzi wako wa ndoa, na hiyo ni dhambi kubwa sana.

Mungu akubariki sana

Pesquisar
Categorias
Leia Mais
SPIRITUAL EDUCATION
NGURUMO SABA
Katika kufunguliwa kwa mihuri saba, kwenye kile kitabu cha ufunuo, tunaona kuwa muhuri wa saba...
Por GOSPEL PREACHER 2021-10-30 11:00:50 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
Yesu alikuwa wapi katika siku tatu toka siku ile ya kufa mpaka kufufuka?
Kama Yesu alivyotabiri, alisalitiwa na mmoja wa wafuasi wake, Yuda Iscariot, na alikamatwa....
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 09:39:59 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
YAFAHAMU MAFUNDISHO YA UONGO
(basi roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani wakiyasikiliza...
Por GOSPEL PREACHER 2021-12-22 01:41:05 0 5K
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 16
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 58 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:15:50 0 5K
OTHERS
How an Atheist Found God
A personal account from an atheist who was convinced no god exists, and what facts led to God....
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 09:43:58 0 6K