MAMBO SITA MUHIMU KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA NA NDOA

0
6χλμ.

KWELI KUU: Ndoa nzuri ni matokeo ya kuoa au kuolewa na mtu sahihi pasipo kuacha kufuata kanuni za mahusiano hususani kanuni za ndoa kabla na baada ya kuoa au kuolewa.

Yohana 10:27 - 30

[27] Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.[28] Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakaowapokonya mkononi mwangu. [29] Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. [30] Mimi na Baba tu umoja.


UTANGULIZI:
Mahusiano ya mke na mume kwa maana ya ndoa yamefananishwa kabisa na mahusiano ya Yesu na kanisa lake kwa maana ya Mchungaji (Bwana arusi) na Kondoo ambao ni Kanisa (Bibi arusi). Kama Yesu alivyolipenda Kanisa na kujitoa kwa ajili yake, ndivyo na mume anapaswa kumpenda mkewe na kujitoa kwa ajili yake. Na kama kanisa linavyomtii Kristo, ndivyo mke anavyopaswa kumtii mume wake (Waefeso 5:21 - 33; Mathayo 9:15; 25:1 - 15; Ufunuo 19:7, 9). Kwa sababu hiyo, kwa sehemu mahusiano ya Yesu na Kanisa lake yanatufundisha kanuni za mahusiano ya ndoa kati ya mke na mume. Leo nataka tutumie mahusiano ya Yesu na Kanisa lake katika kanuni ya Mchungaji na Kondoo kujifunza mambo muhimu sana katika ndoa ambayo yatatusaidia kuboresha na kuimarisha ndoa zetu iwapo tutayapokea na kuyatenda. Biblia inasema hivi, "Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda(Yohana 13:17); hii ina maana kwamba, unachokijua wewe katika ufahamu wako kina matokeo katika maisha yako na ya mwingine pale tu unapokiweka katika matendo katika usahihi wake, na si vinginevyo.

MAHUSIANO NA UMILIKI KATIKA MAHUSIANO:
Katika maandiko yetu ya somo hapo juu, ule mstari wa 27, umeanza kwa kusema, Kondoo wangu; hapa kuna nomino yaani jina ambalo ni 'Kondoo', lakini pia kuna kiwakilishi kimilikishi nafsi ya kwanza ambacho ni "Wangu" kiwakilishi kimilikishi hiki nafsi ya kwanza kinamwakilisha Yesu Kristo. Ukisomoa Mstari wa 11 wa sura ya 10 ya kitabu hiki cha Yohana, Yesu anajitaja kuwa Yeye ndiye mchungaji mwema, kwa hiyo hapa anaposema, "Kondoo wangu" anatambulisha uhusiano wake wa karibu sana na Kondoo wake; Yeye ndiye mmiliki wa Kondoo hao kwa sababu alijitoa kwa ajili yao akawanunua kwa damu yake iliyomwagika pale msalabani.

Hapa tunaona kuwa kuna mahusiano kati ya Yesu na Kondoo; na katika mahusiano haya kuna umiliki wa kila upande kwa mwenzake. Kama Yesu amesema "Kondoo wangu" maana yake ni kwamba na hawa Kondoo watasema, "Mchungaji wetu" licha ya kuwa ni Mchungaji aliyewanunua kwa damu yake, lakini hata hawa Kondoo walimkubali na kumwanini kuwa Yeye ndiye Mchungaji mwema kwa ajili yao. Ijapokuwa si Kondoo waliomchagua Mchungaji, bali ni Mchungaji aliyewachagua Kondoo, bado kukubali kwao, kutii kwao na imani yao kwake imemfanya mchungaji huyu awe Mchungaji wao; na kuanzia hapa Mahusiano ya karibu baina ya pande mbili zote yanaanza.

Popote mahusiano yanapoanzishwa na pande mbili ambapo upande mmoja unakuwa mtoaji, na upande wa pili unakuwa mpokeaji, na upokeaji huo unaambatana na mwitikio wa kurudisha kile alichopokea kwenda kwa mtoaji, swala la umiliki ufuata mara tu baada ya mahusiano kuanzishwa. Mchungaji anakuwa wa Kondoo, na Kondoo wanakuwa wa Mchungaji; mume anakuwa wa mke na mke anakuwa wa mume, ni wawili na si zaidi ya hapo kila mmoja akimilikiwa na mwingine ambaye kwake amejitoa kuwa wake.

Mahusiano ya ndoa ambayo hayazingatii uaminifu kwa yeye anayekumiliki hayawezi kuwa imara, lazima tu yataambatana na usaliti unaosababishwa na kuvuka mipaka ya ndoa ambayo kwayo unamilikiwa na yule aliyekuoa au uliyeolewa naye. Sasa, kutokea hapa ndipo nataka tuangalie MAMBO SITA (6) MUHIMU KATIKA MAHUSIANO YA NDOA NA UCHUMBA. Katika sehemu hii ya kwanza nitakutajia tu mambo hayo, na katika sehemu ya pili nitayabainisha na kuyaainisha hatua kwa hatua, kwa kina na kwa mapana ili unielewe zaidi.

Yohana 10:27 - 30

[27] Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.[28] Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakaowapokonya mkononi mwangu. [29] Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. [30] Mimi na Baba tu umoja.

Jambo la KwanzaNami nawajua, Nao wanajua mimi (Kabla ya Yote Mjue Kwanza): Hii ni sababu ya kuanzisha mahusiano. Kwa sababu Yesu alitujua alianzisha mahusiano na sisi, na sisi tulipomjua tukaingia katika mahusiano na yeye. Yohana 10:14, Yesu anasema, "Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi" Usianzishe mahusiano ya ndoa na mtu usiyemjua; na usiendelee kukaa katika uchumba na mtu usiyemjua. Yesu daima huwa haanzishi mahusiano na ushirika na mtu asiyemjua, shariti umjue kwanza ndipo aanzishe mahusiano na wewe. Maarifa juu ya mtu unayetaka kuingia naye katika mahusiano ya ndoa ni moja ya jambo la msingi sana katika mahusiano hayo, na iwapo halitazingatiwa, basi kuna hatari ya kuwa na mahusiano mabovu na mabaya kama sio kwa mahusiano hayo kuvunjia kabisa.

Usianzishe mahusiano na mtu eti kwa sababu tu unampenda naye anakupenda au umevutiwa naye, pamoja na kuwa unampenda naye anakupenda, je, unamjua? Kama humjua basi, jipe nafasi ya kumjua kwanza kabla haujamchumbia au kumuoa, au kabla hajakuchumbia au kuolewa naye.

Kwa nini ni lazima Umjue unayetaka kumwoa, au kuolewa naye?
Mosi, ni kwa sababu sio wote wanaokuja kwako ni wachungaji, wengine ni wevii na wangang'anyi. Yohana 10:1, Yesu anasema, "Amin amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi." Sifa moja kubwa ya mwivi na mnyang'anyi ni kwamba, Yeye huwa haingii kwa kupitia mlangoni, hupitia kwingineko anakojua yeye; na huwa hajionyeshe mara moja, mwanzoni huja kama mchungaji, huku akiwa ameficha makucha yake, ili kuhakikisha anakunyang'anya na kukuibia maisha yako mazuri uliyokusudiwa.

Yesu ndiye mlango wa kandoo; hii ina maana kuwa, yeyote ambaya anakuja kwako ni lazima awe ni mtu ambaye kweli ameokoka na anamwamini Yesu Kristo, sio tu yule anayesali katika makanisa ya wokovu (maana wapo wengi wanaosali lakini wakiwa hawajaokoka kabisa), bali yule ambaye ameokoka kweli kweli. Lakini pia ina maana ya kuanzisha mahusiano kwa kufuata msingi wa Neno la Mungu bila kuvuka mipaka ya Neno hilo maana Yesu ni Neno aliyefanyika mwili, Yeye ni mlango wa Kondoo (Yohana 10:9)

Wakati mwivi na mnyang'anyi ana sifa ya kuingilia penginepo, mchungaji ana sifa ya kuingilia mlangoni, katika mlango wa kondoo (Yohana 10:1, 2). Hata hivyo kwa kufanya haraka huwezi kumjua kondoo ni yupi na mwivi na mnyang'anyi ni yupi mpaka unawajua vizuri; na swala la kumjua mtu ni swala la muda lakini pia linalohusisha viongozi wenu wa kiroho kanisani. Washirikishe kabla hujafanya maamuzi. Tatizo la vijana na mabinti wengi, bado wanaenda kwa kubahatisha lakini hawataki kuwashirikisha viongozi wao wa kiroho, wanakuja kuwashirikisha wakiwa wamekwisha maliza kila kitu, na katika hatua hii hakuna anayeweza kukushauri vinginevyo zaidi ya makubaliano yenu wawili kwa yeye kuwatakia heri. Lakini matatizo yanapoanza kutokea katika ndoa, wanakimbilia kwa viongozi wao wa dini ili wawasaidie kutatua matatizo yao, hii ni shida kweli kweli.

Mchungaji atakuchunga, atautoa uhai wake kwa ajili yako, atakupa malisho tele yatakayokushibisha, atakata kiu yako kwa maji atakayokunywesha, na atakulinda. Sio mwivi na mnyang'anyi, yeye atakuibia kila kilichochema kwako na kukunyang'anya kila ulichonacho kizuri; atakuondolea furaha yako, amani yako, upendo wako, atakibia vipawa vyako, huduma yako, karama yako na kadhalika. Hujawahi jiuliza kuwa, kwa nini watu wanapoolewa au kuoa wanapunguza bidii yao katika huduma walizokuwa nazo kama sio kuacha kabisa? Unaanza kuona mtu haji tena kwenye maombi, ibadani ndio usiseme, kama alikuwa mwanakwaya na kwaya anaacha kabisa, kama alikuwa anashuhudia mtaani, anaacha kabisa, kila kitu kimeibiwa, ameishanyng'anywa alivyokuwa navyo, kwa sababu ameolewa au ameoa mwivi na mnyang'anyi.

Pili, kwa sababu wengine ni mbwa mwitu waliojivika ngozi ya kondoo. Mbwa mwitu atakurarua tu, ukishamuoa, atavua ngozi yake na kubaki kuwa mbwa mwitu, kwa sababu huwezi kubadilisha asili ya mbwa mwitu kwa kumvika ngozi ya kondoo. Kwa hiyo, ni muhimu sana, tena sana kumjua yule unayetaka kuolewa naye au yule unayetaka kumuoa. Upendo tu hautoshi, namna alivyokuvutia si kitu, swali kubwa, je, unamjua? Angalia usije ukaelekeza upendo wako kwa mwivi na mnyang'anyi au mbwa mwitu, utakuwa umepoteza.

Mwizi ni mwizi tu, hata kama utampenda kwa namna gani, atakuibia tu. Kuna ndugu yangu mmoja, mtoto wake wa kiume ni mwizi, mara ya kwanza alidhani anaiba kwa sababu anakuwa na mahitaji na hana pesa, kumbe ni tabia yake. Alijaribu kuwa anampa pesa pengine ataacha wizi, alijaribu kumwonyesha upendo wa hali ya juu kuliko wengine, lakini kila alipokuwa akiondoka nyumbani mtoto wake alivunja mlango wake na kuiba japokuwa alimwachia pesa. Chochote alichowekeza kwa mtoto huyu kilimsababishia maumivu zaidi yeye mwenyewe. Ndivyo ilivyo kwa mwivi na mnyang'anyi.

Mbwa mwitu hapendeki hata kidogo, utampa nyama, kweli ataila, lakini atakapoimaliza atakula wewe mwenyewe. Mbwa mwitu afugiki, ipo siku tu atajifanya kakusahau kisha atakurarua na kukumaliza kabisa. Sasa wewe leta mchezo tu, kwa kusema kwamba, "Hata kama hajaokoka, hata kama simjui ilimradi tunapenda tu, tutaishi pamoja kwa maana upendo haushindwi na jambo lolote" Tema mate chini, kisha waulize waliokutangulia watakupasha habari.

Hebu waza tu, ufungiwe nira na mbwa mwitu, atakumaliza tu. Waza ufungiwe nira pamoja na mwivi na mnyang'anyi, atakukatakata mapanga akuibie tu. Unajua mwizi huwa anaiba kwa siri, na mnyanganyi huwa naiba wazi wazi bila kificho akitumia silaha. Sasa mkeo au mumeo ni vyote, ni mwizi na mnyang'anyi pata picha hiyo; anaiba kwa siri pasipo wewe kujua, siku utakayokuja kugutuka, huna chochote. Lakini kwa kuwa pia ni mnyang'anyi, pale inapobidi atumie nguvu, atatumia nguvu, na hapo ndipo utakodoa macho yako ukisema, sikujua; lakini sasa umejua... na kama hukujua, kwa nini hukusubiri mpaka ukajua ndipo ufanye maamuzi? Majuto ni mjukuu, walisema waswahili.

JAMBO LA PILI: Waisikia Sauti Yangu: Jambo hili la Pili ni matokeo ya mahusiano yaliyoanzishwa yakiwa yamezingatia Jambo la Kwanza ambalo ni Kigezo au Sababu (reason) ya kuanzisha mahusiano ya uchumba hadi ndoa.

Kusikia sauti ya mtu ambaye umeingia naye katika mahusiano ya ndoa ni matokeo ya wewe kumjua mtu huyo vizuri; kujua hakika ya kwamba unafanana naye, ni mtu mwema, mcha Mungu, mwenye Imani moja na wewe katika Kristo Yesu Bwana, na anakupenda kweli, na kwa sababu hiyo haitakuwa vigumu kuisikia sauti yake.

Maneno ya mtu ni mawazo ya moyo wa mtu yaliyozungumzwa, na ndio maana kinywa husema yale yaujazayo moyo. Sauti ya mtu imebeba maneno ya mtu huyo, na maneno ya mtu huyo yamebeba mawazo ya mtu huyo, na mawazo ya mtu huyo yamebeba makusudi na nia ya mtu huyo juu yako. Kwa kuwa unamjua, basi utaisikiliza sauti yake, na kwa kadiri unavyoisikia sauti yake, utayajua mawazo yake juu yako, na kwa kadiri unavyoyajua mawazo yake, utaijua nia yake juu yako; na kwa sababu hiyo, utaendelea kumjua zaidi, na kwa kadiri utakavyomjua zaidi, utaendelea kuijua sauti yake zaidi; na kwa sababu hiyo hutababishwa na sauti zingine za wasiokuwa mchungaji wako.

Yohana 10:3

Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kwa majina yao... Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.


Tatizo lililopo katika mahusiano ya watu wengi, yawe ni ya ndoa na hasa yale ya uchumba, ni kila mmoja kutomjua mwenzake, na kwa sababu hiyo hakuna kuaminiana; na hapo ndipo huja sauti za wageni, na huyu kondoo huanza kubabaishwa na sauti hizo, unakuta mahusiano ya watu wawili yanakuwa ya watu watatu au wanne au zaidi. Ukimjua, utaisikia sauti yake, ukiisikia sauti yake, hautazisikia sauti za wageni kwa sababu huzijui, wewe unajua sauti moja tu, ya huyo umpendaye, na unampenda kwa sababu unamjua.

Huyo mwenzi wako ili aendelee kukujua, anahitaji kusikia sauti yako; kama haisikii sauti yako basi ataanza kuwa na mashaka na wewe kwa sababu hapati muda wa kutosha na wewe wa kusikia sauti yako. Na kwa sababu hasikii sauti yako masikioni mwako, anaanza kuwa mgeni na sauti yako; ikitogea akatokea mgeni ambaye anajifananisha sauti na wewe akazungumza naye, atamsikia yeye kuliko wewe, na hapo ndipo shida huanza, utakuta anaanza kutoka nje ya ndoa kwa sababu kuna sauti anaisikia huko nje inayomwonyesha kile wewe usichomwonyesha.

Huyo mwenzi wako ili aendelee kusema na wewe, ni lazima na wewe umpe nafasi ya kuisikia sauti yake. Kama hautamsikiliza, kwanza hautamjua, pili utaanza kumpa mashaka ya kwamba pengine wewe sio kondoo wake au mchungaji wake, na kwa sababu hiyo kuanza kuangalia penginepo. Sauti yako ni ya muhimu sana kwake, na suti yake ni ya muhimu sana kwako; msikilize, sema naye, sema naye, msikilize anaposema nawe.

Changamoto kubwa tuliyonayo sasa hivi katika kizazi hiki cha 'smartphon' na mitandao, ni vidole vinaongea zaidi kuliko mdomo pindi wawili wanapokuwa pamoja. Na mbaya zaidi, kila mmoja kakaa kwenye kona yake akizungumza si na mwenzake bali na rafiki zake au akiangalia jambo fulani mtandaoni. Kila mmoja wakati huu katika fikira zake hawazi kuhusu mwenzake, anawaza kuhusu simu na hao walioko mtandaona, wakijakushituka muda umesonga sana na kila mmoja amechoka, na iliyobaki ni kulala bila kuzungumza. Kwa hiyo kwa siku kadhaa, hakuna mtu anayeisikia sauti ya mwenzake katika mazungumzo ya karibu ya wawili hao kama wanandoa, kidogo kidogo mioyo yao inakuwa mbali kila mmoja na mwenzake ijapokuwa miili yao ipo karibu; na kwa sababu hiyo mahusiano yao ya mke na mume yanabaki kuwa ni MAZOEA tu. Akipatikana wa nje ambaye atamtendea mmoja wao zaidi ya mazoea, shida itaingia ndani ya ndoa. Sauti ya mwenzi wako ni ya muhimu sana katika kuhakikisha mnakuwa salama.

JAMBO LA TATU: Nao wanifuata ninapowatangulia: Huu ni mwitikio (A response) katika mahusiano.
Mahusiano yoyote yale lazima yawe na mwitikio; kwa kuwa kondoo wanamjua, nao wanaisikia sauti yake, kutokea katika suti ile wanaoisikia wanamwitikia mchungaji kwa kumfuata anapokuwa ametangulia mbele yao. Ndivyo ilivyo katika mahusiano; mume ni kiongozi na mke ni mfuasi wa uongozi wa mumewe; kama kiongozi lazima atoe sauti yake kwa mfuasi wake kwa sababu anamjua; na mke kama mfuasi ni lazima afuate sauti ya kiongozi kwa sababu anamjua. Kufuata ni matokeo ya mambo yote mawili; kumjua, na pili kuisikia sauti yake.

Yohana 10:4, 5;

Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.​


Tatizo tulilonalo katika hoja hii ni waume wengi kutowatangulia wake zao, na wake nao kutaka kuwatangulia waume zao; hili ni tatizo, haiendi hivyo kabisa.

Kondoo hawamfuati mchungaji eti tu kwa sababu amewatangulia, hapana, wanamfuata kwa sababu tu, (pamoja na kuwatangulia ambalo nalo ni jambo la muhimu) wanaijua sauti yake, na kwa sababu wanaijua sauti yake wanaisikia, na kwa sababu wanaisikia sauti yake, anapowatangulia wanamfuata kwa kuifuata sauti yake. Kumfuata mumeo ni kutii sauti yake; kama unamjua utaijua na sauti yake, na kama unaijua sauti yake basi utaifuata kwa kutii. Mume, kama unamjua mkeo, utamtangulia, na kama utamtangulia utafumbua kinywa chako kumsikilizisha sauti yako ili aifuate.

Mume, katika kila jambo katika mahusiano yako na mkeo, kuna sauti yako ambayo mkeo anapaswa kuisikia ili aifuate, lakini hawezi kuisikia kama huna kawaida ya kusema naye wakati mwingine wote kwa sababu itakuwa ni vigumu kuitambua kwa kuwa itakuwa ni kama sauti ngeni kwake. Jizoeze kusema na mkeo, zungumza naye wakati wote ili aijue zaidi sauti yako. Usisubiri wakati wa tatizo au changamoto fulani ndipo uanze kuzungumza na mkeo, zungumza naye awapo nawe, na awapo mbali nawe, sema naye.

Mume, ni sauti yako ndiyo itakayomfanya mkeo aendelee kukufuata wewe asisikie sauti ya wengine. Kwa lugha nyingine, sauti yako itamlinda mkeo na wageni. Kama unataka usimpoteze mkeo, basi zungumza naye, sema naye, kuwa na muda mwingi wa kusema naye; aijue sauti yako unapokuwa unaomba, ajue sauti yako unapokuwa unafundisha, aijue sauti yako unapokuwa unashukuru, aijue sauti yako unapokuwa unafariji na kutia moyo, aijue sauti yako unapokuwa unampongeza, aijue sauti yako unapokuwa unampa pole, aijue sauti yako unapokuwa unamwomba msamaha, na aijue sauti yako kwenye simu unapomwambia nimekumisi, nakupenda na kadhalika, na ndipo ataijua sauti yako unapokuwa unamkemea, kumuonya na kumkalipia. Sasa wewe pengine kote huko haijui sauti yako, halafu unataka aijue wakati unamkemea, kumuonya na kumkalipia!!! ajabu sana.

Mke, wajibu na kazi yako ni wewe kuijua sauti ya mumeo na kuifuata. Tatizo la wanawake wengi wanazijua sauti zao wenyewe kuliko sauti za waume zao, na wanajua sauti za mashoga zao na rafiki zao kuliko sauti za waume wao. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu muda mwingi wanapokuwa na waume zao wao ndio wanaoongea sana bila kuwapa waume zao nafasi ya wao kuonge, na kwa sababu hiyo wanataka hoja zao ndio ziwe mwongozo na si za waume zao. Lakini wanajua sauti za marafiki zao kwa sababu wanatumia muda mwingi kuongea na hao marafikia zao. Unakuta hata kwa siku zile mume yupo nyumbani, mke anamwacha mumewe ndani anakwenda kijiweni au saluni kupiga sogo na marafiki zake, hii ni hatari sana, haujengi ila unabomoa.

JAMBO LA NNEYatoe maisha yako kwa ajili yake: Katika hoja hii tutaangalia vipengele viwili ambavyo vinajitegemea lakini vinajenga hoja hii. Kabla ya kuangalia hoja hii, napenda ufahamu kuwa, Jambo la Tatu ambalo ni mwitikio wa mahusiano linawahusu wote, mume na mke; mume kama kiongozi anayetangulia, na mke kama mfuasi anayetangulia. Yote haya yanasababishwa na sababu fulani nyuma yake, na sababu hiyo ni Jambo la Nne.

Yohana 10:28

"Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mikono yangu"


Kipengele cha KwanzaMpe Maisha yako. (Nami nawapa uzima wa milele) Kama mke ameamua kumfuata mume wake ni kwa sababu mwanamke huyu amempa mumewe maisha yake; maisha yake yote ameyaachilia kwa mwanamume huyu kwa sababu anamwamini na amejitoa kwake. Ijapokuwa hajui usalama wake mbele ya safari, lakini amechagua kumwamini mumewe na kuamini kuwa katika mikono yake atakuwa salama. Unajua kwa nini? Kwa sababu anamjua, anaijua sauti yake na ndio maana anaisikia, na sasa anamfuata huku akiwa na uhakika wa usalama wa maisha yake.

Sasa, kwa sababu mwanamke huyu ameyatoa maisha yake kwa mumewe, sasa mume pamoja na kuwa ametangulia, ni lazima ayadhabihu maisha yake kwa ajili ya uzima wa mkewe. Uzima (usalama wa maisha) wa mke unagharimu maisha yote ya mwanaume hata kama mwanaume itamaanisha kufa kwa ajili ya mkewe.

Yohana 10:11 inasema,

"Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa mwitu anakuja na kukimbia; na mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wla mambo ya kondoo si kitu kwake"


Kama Yesu alivyo Mchungaji mwema wa kondoo wake, ndivyo mume anapaswa kuwa mume mwema kwa mke wake. Na kwa kuwa ni mwema, basi yuko tayari kuyatoa maisha yake kwa ajili ya mkewe, kama sivyo, basi ni mume wa mshahara; yaani ambaye amekuoa si kwa sababu anakupenda, bali kwa sababu kuna kitu anataka kufaidika yeye na maisha yake kupitia wewe, huyo ni mume wa mshahara kama alivyo mchungaji wa mshahara.

Kama ilivyo kwa mchungaji wa mshahara kwamba, mambo ya kondoo si kitu kwake, basi ndivyo ilivyo kwa mume wa mshahara (anayetafuta faida yake yeye mwenyewe), mambo ya mkewe si kitu kwake kwa sababu kilichomsukuma kuwa na huyu mwanamke si upendo bali ni kitu au vitu fulani vinavyompatia faida yeye. Kwa sababu hiyo, hawezi kujali kabisa usalama wa mkewe; wanaume wa namna hii ndio wale ambao wao wakiwa na shida watataka msaada wa haraka toka kwa wake wao, lakini wake wao wakiwa na shida, wao wanapotezea, na wanakuwa bize na mambo yao. Hii siyo sawa, TOA MAISHA YAKO KWA AJILI YAKE.

Maisha yako ni pamoja na muda wako ambao unaambatana na uwepo wako; toa muda wako kwa ajili ya mke wako, jitoe wewe mwenyewe kwa ajili ya mke wako kwa kuwa naye kila anapokuhitaji na hata wakati ambapo haonyeshi sana kukuhitaji, wewe kuwa naye tu. Maisha yako ni pamoja na mali ulizonazo; toa mali yako kwa ajili ya mke wako, mwache hazitumie kama wewe unavyozitumia, usimbanie, usimwekee mipaka inayomnyima haki ya kutumia mali ulizonazo au mlizonazo, mpe uhuru kwa sababu ni zake pia. Kumbuka maisha yako ni maisha yake na ndio maana tatizo lako ni tatizo lake, furaha yako ni furaha yake.

Maisha yako pia ni pamoja na pesa yako; kuwa muwazi kwake kuhusu mapato yako, ajue unapata kiasi gani cha fedha, lakini pia mpe uhuru na uwezekano (access) wa kutumia pesa hizo bila masimango wala kificho chochote lakini kwa kuzingatia utaratibu mliojiwekea au mtakaojiwekea wa kuhusu mapato na matumizi ya fedha. Fedha yako usiifiche machoni pa mke wako, wala yeye fedha yake asiifiche machoni pako.

Mume, kama mke ni mali yako, yaani ni wa kwako wewe, basi utautoa uhai wako kwa ajili yake, wakati wowote ule, mahali popote pale na katika mazingira yoyote yale; ni bora wewe uumie, yeye abaki salama.

Kipengele Cha PiliUsimpoteze; (wala hawatapotea kamwe); Kama maisha yake hayatakuwa ya muhimu kwako na hayatakuwa kipaumbele kwako, basi utampoteza mkeo (au mumeo). Upendo ndio kiini na msingi wa mahusiano yote; na upendo sio hisia, upendo ni uchaguzi wa kumfanyia matendo mema yule ambaye umechagua kumpenda; hisia ni swala linalojengwa na matendo yako mema kwa muhusika. Kwa hiyo, kama unampenda mke wako, utamlinda kwa wivu mkubwa, kama unampenda mume wako utamlinda kwa wivu mkubwa.

Kama wewe hutaonyesha kumjali, kumthamini, kujitoa kwa ajili yake, kwa kumpenda bila mashariti, basi, moyo wake utaanza kuelekea kwingine; taratibu ataanza kuvunjika moyo, kukukatia tamaa, na kuondoa moyo wake kwako. Ikiishakuwa hivi, ni rahisi kwa yeye kuhamishia moyo wake au upendo wake kwa mtu au kitu kingine. Wakati unakuja kushituka, tayari mwenzako amekwishakupotelea kwingine. Tatizo si yeye, tatizo ni wewe, umempoteza, hukumlinda kwa kumpenda, kumjali, kumthamini na kujitoa kwa ajili yake.

Kama unataka wewe usilipoteze pendo la mke wako au mume wako kwa ajili yako, mpende, mthamini, na ujitoe kwa ajili yake wakati wote. Si kila anapoonekana kukuhitaji wewe unatoa visingizio tu, mara hili mara lile. Yatoe maisha yako kwa ajili yake, na uutoe uhai wako kwa ajili yake kwa maana hakuna upendo pasipo kujitoa kwa ajili ya umpendaye; dhabihu inahusika wakati wote ukitaka awe wako wakati wote. Lakini ukitaka awe wa mwingie, wewe acha tu kujitoa kwa ajili yake, usionyeshe kumjali wala kumthamini, mchukulie poa tu, mchukulie kirahisi rahisi tu kama vile humjui na kama vile si wako.

Kipengele cha TatuAsiwepo wa Kumpokonya toka kwako (wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mikono yangu); Waonyeshe watu wanaokuzunguka ya kuwa unampenda mke wako kwa gharama ya maisha yako yote. Waonyeshe kuwa hauko tayari kumpoteza, na ya kuwa hakuna awezaye kumwondoa kwako. Na hii unaionyesha vipi? unaionyesha kupitia kile unachomfanyia mkeo mbele ya watu wanaokuzunguka. Upendo ni nuru, na nuru si kitu cha kuficha; mwosheshe mke wako au mume wako kuwa unampenda kuliko wote wanaokuzunguka na wanaomzunguka yeye; waonyeshe wengine kuwa mkeo au mumeo ni wewe na wewe ni yeye. Usifiche upendo wako juu yake kwa wengine, waonyeshe kuwa unampenda na umuonyeshe kuwa unampenda mbele ya hao watu.

Mlinde mkeo au mumeo kwa wivu mkubwa kama Mungu anavyowalinda watu wake kwa wivu mkubwa. Usiruhusu mazoea kati ya mke wako au mume wako na watu wengine. Yeyote ambaye anataka kumwiba au kumpokonya mumeo au mkeo kutoka kwako, huanza kwa kumzoea; hujenga urafiki unaopelekea mazoea yanayovuka mipaka na hatimaye hutimiliza kusudi lake pale tu anapouteka moyo wa mumeo au mkeo.

Mpendwa, mlinde mumeo au mkeo kwa maombi, shetani na wajumbe wake wasimpokonye kwako. Asiwepo mtu atakayetumia uchawi kumpokonya kwako. Mlinde, walevi wasimpokonye na kumfanya kuwa mlevi kama wao, mlinde kwa maombi moyo wake usipokonywe na chochote kitakachoushika moyo wake, iwe ni biashara, kazi, au kingine chochote.

Mpendwa, lakini pia umlinde mkeo au mumeo kwa kutimiliza wajibu wako kwake; mpende kuliko vingine vyote hapa chini ya jua; mfanyie mema, onyesha kuwa unamthamini na kumjali; mtofautishe na wengine, mfanye ajisikie kuwa ni malkia au mfalme kwa upekee na umaalumu unaompatia. Kama hautampatia upekee na umaalumu, akipatikana ambaye atamfanya kuwa wapekee na maalumu, lazima atampokonya toka mikononi mwako.

Vipengele vyote hivi vinawezekana iwapo tu wewe utakuwa umejitoa kwake kwa kutoa maisha yako yote kwa ajili yake bila kubakiza chochote. Lakini kama hautajitoa kwake, lazima tu utapokonywa, utampoteza tu kwa yeye moyo wake kuelekea kwingine.

JAMBO LA TANOBaba yangu amenipa hao: Ni nani amekupa mwenzi wako huyo kuwa mke au mume wako? Ni vyema kabla haujaoa au kuolewa na mtu huyo umpendaye, licha ya kuwa unamjua, basi ni vyema kabisa ujue ni nani amekupa mtu huyo kuwa mume au mke wako. Kwa wewe ambaye umeokoka kila kitu chako hutoka kwa Mungu, wewe hupewa na Mungu. Mali na urithi mtu hupewa na baba yake, lakini mke mwema au mume mwema mtu hupewa na Mungu. Kama Mungu anatoa mume au mke Shetani naye hutoa mume au mke; Mungu hutoa kilicho chema ili kutupa amani katika maisha yetu na katika mwisho wetu, Shetani hutoa kilicho kiovu ili kuharibu maisha yetu na hatima zetu mwishoni. Kwa hiyo ni vizuri wewe kuwa makini sana juu ya jambo hili. Tafuta kujua kuwa, huyo unayempenda na unataka kumuoa au kuolewa naye, je, ametoka kwa Mungu!! Kwa hiyo, katika hoja hii ya kujua kama ametoka kwa Mungu inakwenda sambamba na hoja ya kumjua muhusika mwenyewe, na ndio maana nikasema kuwa mambo haya yanakwenda pamoja.

Katika Yohana 10:29; Yesu anasema,

"Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwa Baba yangu.​


Yesu akiwa ni Mchungaji wa kondoo, pamoja na kuwajua hao kondoo, na kwa sababu anawajua, anajua kabisa ni Mungu ndiye aliyempa hao kondoo, na kwa sababu ni Mungu ndiye aliyempa, wametoka mikononi mwa Mungu na wapo mikononi mwa Mungu, na kwa sababu hiyo hakuna mtu awezaye kuwapokonya kutoka kwa Mungu. Kwa nini? Licha kuwa hao kondoo ni wa Yesu, lakini pia ni wa Mungu na Yesu mwenyewe ni wa Mungu, na hao kondoo wamekuwa wa Yesu kwa sababu Mungu amempa Yesu. Kwa hiyo kilicho cha Yesu ni cha Mungu kwa sababu kimetoka mikononi mwa Mungu.

Kwa upande wa wanandoa, Kama huyo unayemuoa au anayekuoa ametoka kwa Mungu, haishii tu kuwa wako, bado anabaki kuwa wa Mungu pamoja na kuwa ni wako na kwa sababu hiyo Mungu anawajibika kwa ajili yake. Kama vile wewe unavyomlinda asiwepo atakayempokonya kutoka mikononi mwako, ndivyo Mungu anavyomlinda ili asiwepo mtu yeyote atakayeweza kumpokonya toka mikononi mwake. Kwa hiyo haiishii tu kwako, wewe kumlinda, inaanza na Mungu kwanza ndipo wewe.

Bwana asipoulinda mji wao wakeshao wakilinda wanakesha bure. Mungu akilinda kulinda kwako ndiko kunakuwa na manufaa; na Mungu analinda kile kilicho cha kwake. Ukioa mke au ukiolewa na mume ambaye hatoki kwa Mungu, ambaye Mungu hajakupa, huyo hayumo kabisa mikononi mwa Mungu na kwa sababu hiyo Mungu hajishughulishi naye. Ni kile tu kisichoweza kupokonywa mikononi mwa Mungu ambacho Mungu amekupa ndicho hakitaweza kupokonywa mikononi mwako, kwa sababu unapokilinda Mungu naye anakilinda; hata wakati umelala, hauoni, Mungu yeye anaona na nakilinda.

Wewe kulinda kile Mungu asichokilinda ni kukesha bure na kufanya kazi bure. Mungu analinda kile kilicho chake. Kilicho chake kikiwa mikononi mwako, hata kama hujamwambia akilinde, japokuwa ni muhimu kukiombea ulinzi, Yeye atakilinda tu, na kwa sababu hiyo kazi yako ya kukilinda itakuwa nyepesi.

Kama unataka asiwepo mtu atakayewapokonya mikononi mwako, na uwe na ujasiri wa kusema na kuamini hivyo, basi huyo mwenzi wako hakikisha anatoka mikononi mwa Mungu. Usimchukue ambaye Mungu hajakupa na wewe kutaka kumweka mikononi mwa Mungu. Tatizo la watu wengi leo wanachukua kutoka huko kwingine halafu wanawaleta wawaweke mikononi mwa Mungu. Wewe huna uwezo wa kumweka yeyote mikononi mwa Mungu kwa sababu huna hata uwezo wa kumwondolea dhambi zake. Bora kuchukua kutoka mikononi mwa Mungu yule anayekupa, kuliko kuhangaika na wale wasiokuwa mikononi mwake tena asiokupa.

Yesu alikuwa na ujasiri kabisa wa kusema kuwa hakuna mtu atakayewapokonya mikononi mwake kwa sababu alijua ni Mungu ndiye aliyempa, na kwa sababu ni Mungu ndiye aliyempa basi hao aliompa wapo mikononi mwa Mungu, na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwa Mungu. Mungu akishahesabu kuwa kitu fulani ni cha kwako, hawezi akakichukua na kumpa mtu mwingine hata iweje, na wala hakuna awezaye kukichukua toka kwako na kujimilikisha yeye. Kwa nini? Kwa sababu alichokupa Mungu ni chako wewe lakini pia ni cha Mungu, kipo mikononi mwako lakini pia kipo mikononi mwa Mungu. Wewe na kile alichokupa wote mpo mikononi mwa Mungu na ndio sababu hakuna awezaye kukupokonya wala kukipokonya hicho ulichopewa.

Ili mahusiano yenu yawe na amani daima, hakikisha kuwa mwenzi wako anatoka kwa Mungu, maadamu wewe unatoka kwa Mungu. Hakikisha kuwa Baba yenu ni mmoja yaani Mungu; maana yake hii ni kuwa muwe na asili moja, na asili hiyo ni Mungu; mkiwa na asili moja, ndipo wote mtakuwa washirika wa tabia ya uungu. Na kuanzia hapo ndipo linafuata jambo la Sita.

JAMBO LA SITAMimi na Baba tu umoja (Yohana 10:30): Kuwa umoja na Mungu, endeleza ushirika wako na Mungu. Ukijua kuwa ni Mungu ndiye amekupa mke huo au mume huyo, basi utaendelea kuwa na ushirika naye kwa kufanya mambo yanayowafanya wewe na Yeye kuwa na umoja, kuwa mmoja.

Hapa ndipo wengi wamekosea, kabla hawajaoa au kuolewa, walikuwa wanamwomba sana Mungu, watii wa Neno, wanatafuta kujua mapenzi ya Mungu, waaminifu katika zaka na dhabihu na matoleo mengine; kwa ufupi walikuwa na bidii katika mambo ya Mungu yanayowafanya wao kudumu katika kuwa na ushirika na Mungu. Lakini wanapooa au kuolewa wanapunguza kama sio kuacha kabisa kuwa na ushirika na Mungu. Bidii yao inapungua kama sio kuisha; hakuna tena maombi, hakuna tena kusoma Neno, hakuna tena kwenda ibadani, hakuna tena kushuhudia na mambo mengi kama hayo. Na hii sio tu katika swala la kuoa na kuolewa, ni katika maswala yote yanayohitaji majibu toka kwa Mungu. Mara nyingi mtu kabla hajapata anachohitaji kwa Mungu, huwa mwaminifu sana na mwenye bidii kwa Mungu, lakini mara tu baada ya Mungu kumjibu na kumpatia, basi, hugeukia upande mwindine.

Yesu anasema, Mimi na Baba tu umoja; kwa sababu anajua kuwa ni Mungu ndiye aliyempa hao, basi ni Mungu ndiye atakayeendelea kuwahifadhi na kuwalinda waendelee kuwa wake, na kwa sababu hiyo inampasa kudumisha ushirika wake na Mungu. Ni kweli Yeye na Baba wana mahusiano ya Baba na Mwana, lakini pia ili usalama uwepo kwake na kwa kondoo wake ni lazima awe na ushirika na Baba yake.

Kuyalinda mahusiano yako ya ndoa unahitaji kuwa na ushirika na Mungu aliyekupa huyo mwenzi wako wa maisha. Siku ushirika wako na Mungu ukikoma, basi ndoa yako itayumba, na mambo mabaya yataanza kukwandama wewe na mwenzi wako.

Pamoja na wewe kuwa na ushirika na Mungu, pia ni vyema ukawa na ushirika na mke au mume wako. Mahusiano yenu ili yadumu yanahitaji ushirika baina yenu wenyewe ambao msingi wake ni ushirika wa kila mmoja wenu kwa sehemu yake na Mungu. Kila mmoja wenu akiwa na ushirika mzuri na Mungu, basi mtakuwa na ushirika mzuri ninyi kwa ninyi.

Wakati mwingine wanandoa wengi hawana ushirika wao kwa wao kwa sababu wanandoa hao kila mmoja binafsi hana ushirika mzuri na Mungu. Kila nilipopunguza kuwa na ushirika na Mungu, ushirika wangu na mke wangu ulianza kuyumba na tatizo nilikuwa mimi. Ilikuwa ni swala la muda tu; nikipunguza au kuacha kabisa kusoma Neno, kutafakari, kuomba na kufanya mambo mengine, nilianza kujikuta baada ya muda fulani nashindwa kukaa na mke wangu na kuwa na ushirika naye.

Kipimo cha ushirika ni muda unaotumia na huyo uliyenaye kwenye mahusiano. Kama huna muda naye, basi huna ushirika naye. Pamoja na kuwa Mungu ni Baba yako na wewe ni mtoto wake, kama huna muda naye, basi huna ushirika naye, na kama huna ushirika naye basi, huna muda naye. Kila nilipokosa kuwa na muda na Mungu, muda wa kuwa na mke wangu ulikosekana, na hata pale ulipopatikana katika kuwa pamoja kilitokea kitu hapo katikati kinachotufanya tusielewane na kisha kukwazana. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu sikuwa najua nini cha kufanya ninapokuwa na mke wangu, na hata ninapojua sikuwa na nguvu na uwezo wa kukifanya kitu hicho kwa sababu mwenye kunipa uwezo na nguvu, na mwenye kunifundisha nini cha kufanya nilikuwa sina ushirika naye.

Kusema samahani ni kitu kigumu sana kwangu nje ya Mungu, kumpongeza mke wangu au kumshukuru au kumwambia pole, ni kitu kigumu sana na hakuwa tabia yangu niliyoizoea. Vitu hivi tangu utoto wangu vilitokea mbali sana, havikuwa karibu, ili niviseme ilibidi mtu anilazimishe tena kwa viboko au kwa makaripio. Lakini tangu nimekuwa na ushirika na Mungu nafurahia zaidi ninapovifanya hivyo na hasa kwa mke wangu. Lakini kila ninapopunguza kuwa na ushirika na Mungu, ushirika wangu na mke wangu unakuwa wa shida sana na inanibidi nitumie nguvu nyingi kufanya mambo haya kwa mke wangu na hata kwa watu wengine. Ilinichukua muda kutambua hili. Ilikuwa kila ninapogombana na mke wangu ninapoanza kutafakari njia zangu, nakuja kungundua kuwa nina muda nimeacha kuwa na ushirika na Mungu. Ilipotokea hivi mara nyingi, ndipo nilipogundua kuwa tatizo si mke wangu wala kingine chochote, tatizo ni mimi sina ushirika na Mungu.

Chochote ulichopewa na Mungu kama matokeo ya kuwa na ushirika naye kinaendelezwa na kinadumishwa kwa wewe kuendelea na kudumu katika kuwa na ushirika na Mungu. Yesu anatuonyesha njia nzuri ya kuishi maisha yanayomtukuza Mungu na yanayotupa sisi amani na furaha; basi kama ni hivyo, na tuzifuate njia anazotuonyesha.

Na hapa ndipo tumefikia sehemu ya mwisho wa somo hili. Mungu akubariki sana, na akupe dhawabu ya uvumilivu wako katika kujifunza somo hili refu kidogo. Amina.

Love
1
Αναζήτηση
Κατηγορίες
Διαβάζω περισσότερα
SPIRITUAL EDUCATION
The Son, Jesus Christ, is God
The Deity of Jesus Christ from the Scriptures Characteristic God Jesus Christ Who is omnipotent...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 18:30:54 0 5χλμ.
Injili Ya Yesu Kristo
UTHIBITISHO 10 KUWA YESU NI MUNGU
“Wahubiri wa injili” wa Kiislamu huwa wanapinga kuwa Yesu ni Mungu na unapowakatalia...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 03:09:17 0 6χλμ.
Injili Ya Yesu Kristo
JE, UNAWEZA KUOKOKA BILA YA KUPITIA YESU?
Je naweza kuingia mbinguni bila kumkubali Yesu kama Bwana na Mwokozi wangu? Jibu: Hapana, huwezi...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 21:01:24 0 4χλμ.
NUMBERS
Verse by verse explanation of Numbers 10
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 39 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-01-24 14:32:28 0 5χλμ.
OTHERS
MUHAMMAD AKIRI KUWA ALLAH SIO MUNGU WA KWENYE INJIL NA TAURAT BALI NI MUNGU WA KIPAGANI
Je, Wakristo na Waislam, wanaabudu Mungu mmoja?Je, Allah ni Mungu wa Kipagani?Ndugu wasomaji, kwa...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 19:37:36 0 5χλμ.