UMEHESABU GHARAMA?

0
6χλμ.

Mahusiano ya uchumba hadi ndoa yanajengwa. Na kama yanajengwa, basi yana gharama na yanachukua muda, si jambo la mara moja au ghafula. Kuna gharama za ujenzi wa msingi, kuna gharama za kuinua, kuna gharama za kuendeleza, na kuna gharama za matengenezo (repairs).

Kwa kifupi, mahusiano ya uchumba hadi ndoa ni gharama. Pasipo kulipa gharama hakuna mahusiano, iwe ni uchumba na hasa ndoa. Kushindwa kulipa gharama ni kushindwa ndoa, kwa wale ambao wako kwenye uchumba ni kushindwa uchumba.

Kwa sababu mahusiano ni gharama, ni muhimu sana mtu kabla ya kuingia katika mahusiano na mtu ampendaye akaa chini na KUHESABU GHARAMA YOTE, na akiisha maliza, jambo la Pili ajipime kama ANAO UWEZO WA KULIPA GHARAMA HIZO, na tatu ajipime kama YUPO TAYARI KULIPA GHARAMA HIZO kwa ajili ya mtu huyo anayetaka kuingia naye kwenye mahusiano, la sivyo ataishia njiani.

Luka 14:28-30

[28]Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

[29]Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

[30]wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.


Kuanzisha mahusiano ukashindwa kumalizia, maana yake wewe hukuwa na nguvu za kumaliza. Na kama hukuwa na nguvu za kumaliza, ulianzisha ya nini? Bila shaka huo ni upumbavu. Unaanzisha mahusiano wakati huna ubavu wa kufika mwisho, wewe ni mpumbavu aliyejikinai na kumkinai yule anayeanzisha mahusiano naye.

Unajua kabisa kuwa wewe huna pumzi ya kumaliza mbio, lakini unang'ang'ania kuingia kwenye mashindano, unalipa na kiingilio, unajaza na fomu, na unajitangaza hadharani wakati unajua huwezi kufika mwisho, kama sio upumbavu ni nini? Acha kusumbua na kuwataabisha watu wewe!!

Huyo unayetaka kumuona au kuolewa naye ni jamaa mmoja ambaye hajakamilika, ana mapungufu mengi sana, na mojawapo anaweza kudanganywa na akadanganyika. Hawa pamoja na kuwa aliongea na Mungu kila siku, lakini alidanganywa na akadanganyika, naye alipodanganyika akamdanganya mumewe Adamu naye akadanganyika. Pamoja na hayo yote Adamu hakumuacha mkewe. Unajua ni kwa nini? Kwa sababu alikuwa na nguvu za kumaliza na kwa sababu hiyo alikuwa na uwezo wa kulipa gharama.

Tatizo si mchumba wako kuwa ni mbaya, hapana kabisa! Tatizo ni wewe mwenyewe, ukishindwa kuhesabu gharama kabla na kwa sababu hiyo hukujua kama kuna gharama za kulipa na hata unapokuja kujua unakuwa hauko tayari kuzilipa kwa sababu hukujipanga kuzilipa gharama hizo.

Popote palipo na gharama sharti ilipwe ili kufanikisha jambo. Kukwepa gharama ni njia ya kushindwa kufanikisha jambo. Mahusiano ni gharama, hivyo usiingie kabla hujahesabu gharama, la sivyo UTAISHIA NJIANI.

Moja ya gharama kubwa kabisa ni kumpenda mke wako, Na mke ni kumtii mume wako. Gharama ya pili ni kunyenyenyekeana, na gharama ya tatu ni kuheshimiana, na gharama ya nne ni kufurahiana nyakati zote, na gharama ya tano ni kukubaliana (to appreciate each other), Na gharama ya sita ni kusameheana bila kujali ukubwa au udogo wa makosa, na bila kujali aina ya makosa, na gharama ya saba ni kuchukuliana udhaifu kila mmoja auchukue udhaifu wa mwenzake.

Gharama ya nane ni kila mmoja amtangulize mwenziwe, gharama ya tisa kila mmoja amvumilie mwenzake, na gharama ya kumi ni kila mmoja atafakari mazuri ya mwenzake na si mabaya.

Hizo ni baadhi ya gharama, kama huwezi kuzilipa basi wewe huna nguvu ya kufika mwisho, utamwacha tu. Na hata kama utaoa au kuolewa na mwingine, kama huwezi kulipa gharama, huwezi kufika mwisho, utaishia njiani.

Kuvunjika kwa mahusiano mengi huwa si mpango wa Mungu bali huwa ni kushindwa kulipa gharama ya mahusiano yao kwa wahusika wenyewe. Kwa kuwa hawakuhesabu gharama, walijali raha wanayoiona mbele yao wasijue kuwa kuna gharama, hawakujipanga kulipa gharama mpaka mwisho.

Ulishawahi kusikia KIAPO CHA NDOA? Maneno yake yote ni AHADI YA KULIPA GHARAMA ambayo kiuhalisia mtu hupaswa kuapa kiapo hicho mwanzoni kabisa akiwa na ufahamu kamili wa anachosema. Bahati mbaya wengi wao huwa hatuelewi maneno ya kiapo hicho na ndio maana ni rahisi sana kuvunja kiapo hicho kwa kutotimiza maneno tuliyoyaahidi ndani ya kiapo hicho.

Moja ya gharama ambayo unapaswa kulipa ni uaminifu kwa mwenzi wako kwa wewe kuwa mwaminifu kwa kiapo chako kwake. Kwa kuwa huwa hatujakaa chini na kutafakari kiapo hiki, huwa tunajitamkia tu tukiwa hatujui tunafanya nini na ndio maana ni rahisi kuvunja kiapo.

Ndoa ni gharama na inaanza na uchumba. Kama unajua kuwa utaishia njiani USIMSUMBUE BINTI WA WATU au USIMKUBALIE KIJANA WA WATU. Kabla hujamkubalia hata kama una njaa ya kuolewa au kabla hujamwambia hata kama una njaa ya kuoa, KETI CHINI KWANZA KISHA UHESABU GHARAMA, UJUE KAMA UNA UWEZO WA KUZILIPA NA UWE TAYARI KUZILIPA NDIPO UFANYE MAAMUZI.

MUNGU ANACHUKIA KUACHANA. Kwa lugha rahisi ni kwamba, ukiisha ingia kwenye mahusiano ya ndoa hakuna sababu ya kuachana, bora usiingie kuliko kuingia halafu ukaachana na mwenzako.

Tujifunze kwa Yesu Kristo, alihesabu gharama ya wokovu wetu, akaona kuwa ni kifo cha msalabani, kisha akaona kuwa anao uwezo wa kuilipa gharama hiyo, na akawa tayari kuilipa gharama hiyo. Na ndio maana akakubali kufanyika mwanadamu wakati yeye ni Mungu, kufanyika mtumwa wakati yeye ni Mfalme wa wafalme, kufanyika dhambi wakati yeye haijui dhambi kwa kusudi moja tu, la kutukomboa sisi wanadamu wenye dhambi. Kama asingelihesabu gharama, asingeliweza kufika mwisho. Pengine angeliishia katika bustani ya getisemani, au jangwani alipojaribiwa na Ibilisi. Upendo wake kwetu na utii wake kwa Mungu, unyenyekevu wake, upole wake ni vitu vilivyomfanya afike mpaka mwisho na hasiishie njiani bila kumaliza.

Sio kwa sababu yeye ni Mungu ndio maana aliweza, ni kwa sababu yeye alikuwa na upendo lakini pia alikuwa mtii naam, hata mauti ya msalaba. Na wakati akilipa gharama ya kifo, yeye hakuwa tena Mungu, alikuwa mwanadamu Yesu Kristo, alisikia maumivu, alisikia kukataliwa, aliona kuachwa na Mungu kwa sababu ya dhambi zetu, lakini bado aliwasamehe wote waliomtesa na kumkataa ili makusudi akamilishe kazi ya ukombozi kwa njia ya msalaba.

Alivumilia, alistahimili, alinyenyekea, alituchukulia mizigo yetu na udhaifu wetu, alitusamehe dhambi na makosa yetu, alitutakasa kwa damu yake mwenyewe, ijapokuwa tulikuwa hatusitahili, lakini kwa mauti yake alitusitahilisha mbele za Mungu, ijapokuwa tulikuwa wachafu lakini alituosha na kututakasa kwa damu yake, unajua ni kwa nini? Kwa sababu alitupenda upeo na akakubali kulipa gharama yote. Unajua ni kwa nini? Kwa sababu alikuwa mtii na mnyenyekevu kwa Mungu kiasi kwamba akakubali kulipa gharama yote.

Kama unampenda utakubali kulipa gharama zote, na kama unamtii utakubali kulipa gharama zote. Kama hauko tayari kulipa gharama, wewe humpendi na wala humtii, na kwa sababu hiyo hakuna haja ya wewe kuingia kwenye mahusiano ambayo unajua kabisa huwezi kulipa gharama au unao uwezo lakini hauko tayari kulipa gharama. Nimalize kwa kusema tena, Mahusiano ni gharama unayopaswa kulipa kila siku wakati wowote ule unapopaswa kufanya hivyo.Kama hauko tayari kulipa, basi usiingie.

Mungu akubariki sana.

Αναζήτηση
Κατηγορίες
Διαβάζω περισσότερα
OTHERS
Do you think Kadhi’s courts should be part of the new Tanzanian Constitution?
The current debate is about whether or not these “Kadhi” courts should be entrenched...
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 20:32:21 0 5χλμ.
SPIRITUAL EDUCATION
What does the Bible say about sex before marriage?
There is no Hebrew or Greek word used in the Bible that precisely refers to sex before marriage....
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 10:27:04 0 5χλμ.
REVELATION
UCHAMBUZI WA KITABU CHA UFUNUO
Maana ya Ufunuo.   Neno Ufunuo kwa kiingereza ni Reveletion au Disclosure au Apokalupsis kwa...
από GOSPEL PREACHER 2021-11-23 11:12:11 0 9χλμ.
OTHERS
Yesu Kristo hajaumbwa bali alikuwepo tangu milele yote
Ni kweli kabisa kwamba Yesu alikuwepo tangu milele yote kabla ya kuumbwa kitu cho chote kile....
από MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 08:58:24 0 5χλμ.
MAHUSIANO KIBIBLIA
MWANAMKE NA NGUVU YA USHAWISHI (UBEMBELEZI)
Mwanamke aliumbwa na nguvu ya ushawishi ndani yake kwa kusudi la kuweza kutimiliza jukumu lake...
από GOSPEL PREACHER 2021-11-07 23:52:21 0 7χλμ.