HATARI ZA KUWA NA MAHUSIANO YASIYO SAHIHI

0
8كيلو بايت

UTANGULIZI
Mahusiano yasiyo sahihi ni mahusiano ya namna gani? Haya ni mahusiano kwanza kabisa ambayo mtu unaoa au unaolewa na mtu ambaye kusudi lake au nia yake ya kukuoa si sahihi. Pengine labda anakuoa au anakubali kuolewa na wewe sana sana kwa ajili ya kutimiza matamanio au matakwa yake.

Pili ni mahusiano ambayo aliyekuchumbia au uliyemchumbia ni mtu ambaye hana lengo la kuolewa na wewe au kukuoa wewe. Pengine kuna kitu anafukuzia kwako na akiisha kukipata basi atavunja mahusiano hayo.

Tatu, ni mahusiano ambayo wewe umeingia ndani kwenye uchumba au ndoa nje ya mpango wa Mungu na kanuni za Biblia.

Kuna mtu mmoja alisema, “Ajali si ile tu ya kuanguka au kugongwa na gari au pikipiki, hata kuoa au kuolewa na mtu asiye sahihi ni ajali.” Hii inaweza kuwa kweli kwa upande mmoja na hasa kwa mtu ambaye hana maarifa juu ya ndoa, lakini kwa mtu ambaye ana maarifa kuhusiana na ndoa, kwake sio ajali, ni makusudi yake aliyoyafanyia maamuzi na uchaguzi kwa hiyari yake mwenyewe. Pengine naweza kusema ni ajari ya kujitakia wewe mwenyewe kwa mapenzi yako.

UMUHIMU WA KUMJUA UNAYETAKA KUMUOA AU KUOLEWA NAYE
Si vyema kabisa mtu kuingia katika mahusiano na mtu asiye mjua. Ni muhimu ukamjua mtu unayetaka kuolewa naye au unayetaka kumuoa, ukajua yeye ni nani na kwa nini anataka kukuoa

Ili uwe salama kataika mahusiano yako ni muhimu ukaoa au kuolewa na mtu unayemjua na anayejulikana na watu unaowaamini na ameshuhudiwa kuwa ni mtu mwema. Lakini pia ukamwomba Mungu akuongoze moyo wako kukutana na mtu sahihi. Na hii ndio sababu enzi zile za wazazi wetu walisisitiza sana watoto wao kuoa au kuolewa katika familia ambazo walikuwa wanazijua na zimethibitika kuwa ni nzuri kimaadili. Mbali na familia waliangalia muhusika anayetaka kuoa au kuolewa kama ni mtu safi mwenye nidhamu na maadili katika jamii husika.

Aidha waliangalia namna alivyoishi na jamii yote, walihakikisha kuwa ni mtu mwenye mapenzi mema, nia njema, na mwenye adabu kwa watu wote. Hawakukubali mtoto wao kuoa au kuolewa na watu au mtu wasio mjua, au mtu anayetoka katika familia wasiyoijua. Hii ni kanuni (principle) na kanuni huwa hazibadiliki ijapokuwa mfumo wa maisha unaweza kubadilika kutoka nyakati hadi nyakati ukiathiriwa na maendeleo ya kiteknologia, kanuni za maisha hubaki pale pale.

MIFANO KUTOKA KATIKA BIBLIA

ISAKA
Tukianza na Isaka mtoto wa Ibrahimu, alipofikia umri wa kuoa, baba yake aliagiza aolewe na watu wanao wafahamu. Alimtuma mfanyakazi wake kwenda mpaka kule alikotokea Ibrahimu na kumtwalia Isaka mume kutoka kwa watu wa jamaa yake ambao wanawajua. Isaka alimuoa Rebeka mtoto wa jamaa ambayo ni ndugu zao na walikuwa wanawajua.

YAKOBO
Baba yake na mama yake wanamwagiza aende kwa mjomba wake akajitwalie mke huko asioe binti wa Kaanani kwa sababu hawawajui kabisa. Yakobo anakubali na kwenda mpaka kwa Labani, na kule anajitwalia wake ambao kupitia hao taifa la Israeli linazaliwa.

Kuingia katika mahusiano yasiyo sahihi ni kuingia katika mahusiano na mtu asiye sahihi, ambaye nia yake si ndoa ila ni kingine kinachokidhi matakwa na matamanio yake. Na kwa sababu ndoa ni kitu nyeti sana, wazee wetu walipofika katika swala la vijana wao kuoa na mabinti zao kuolewa waliongeza umakini mkubwa sana kwa sababu ni swala la kufa au kupona. Ukipatia umepona, ukikosea hicho ni kifo.

HATARI YA KUWA KATIKA MAHUSIANO YASIYO SAHIHI

Tulianza kwa kuangalia utangulizi, sasa ni mwendelezo wa somo katika kiini chenyewe cha somo letu hili. Karibu tuendelee na Mungu akubariki sana.

HATARI YA KWANZA: Kupoteza au kupotezewa muda wako

Unapoingia katika mahusiano na mtu asiyekuwa sahihi, hatari ya kwanza ni wewe kupotezewa muda wako. Katika kupotezewa muda wako kuna kucheleweshwa; unaweza kujikuta unachelewa kuoa au unachelewa kuolewa kwa sababu mtu yule aliyekuchumbia au uliyemchumbia atakuwa na wewe kwenye mahusiano kwa muda fulani halafu mwisho wa siku atakwambia hataki kukuoa au hataki kuolewa na wewe na kukuacha wakati tayari umeshatumia muda murefu kuwa katika mahusiano hayo ukiwa na matarajio ya kuolewa.

Biblia inasema, Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huinama, jambo hili linapotokea, kwa vyovyote vile litakuumiza moyo wako na kukukatisha tama. Usiolewe na mtu anayezima matarajio yako kama kuzima mshumaa wakati wa giza. Usioe wala Usiolewe na mtu ambaye hana malengo na wewe, atauzima mshumaa wako ukiwa karibu kuishilizia.

Kadili siku zinavyozidi kwenda ndivyo muda wako wa kuishi unavyozidi kupungua, ni mithili ya mshumaa unaowaka wakati wa usiku, kwa kadiri unavyowaka ndivyo unavyopungua, kwa hivyo, usikubali mtu kukupotezea muda wako na kisha akakuacha ukiwa na maumivu. Kuwa na tahadhari ni nani unamchumbia na ni nani anakuchumbia, Hakikisha Unamjua na unaijua nia yake

HATARI YA PILI: Kufunga fursa au mlango wa mahusiano yako sahihi na mtu sahihi

Wakati uko katika mahusiano kitu utakachojaribu wewe kukifanya ni kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako. Na kwa sababu hiyo, wote wengine wanaokuja kwako utawakataa, na kama ni mwanaume hutaenda kuchumbia mtu mwingine, kwa kipindi chote utakuwa umejifunga kwa mtu mmoja. Hii itakuzuia kuingia kwenye mahusiano mapya, hata kama atakuja mtu sahihi wa kukuoa wewe hutajua kwa sababu umejifungia nira na jamaa mmoja unayemwamini lakini yeye hana nia njema na wewe kabisa ila kutimiza matakwa na matamanio yake.

Kwa upande mwingine, na hasa pale mahusiano yanapokuwa yamefahamika kwa watu, yawe rasimi au si rasimi kwa maana ya kwamba labda mmevikana pete ya uchumba au bado lakini watu wanajua kuwa mpo kwenye mahusiano, yule mwingine mwenye nia njema na wewe hata kama atakuwa na msukumo wa kutaka kukuoa au kuolewa nawe hataweza kuja na kukuambia kwa sababu anajua upo kwenye mahusiano. Kwa sababu hiyo utakuwa umepoteza fursa hiyo ya kuwa na mtu sahihi katika maisha yako.

HATARI YA TATU: Kuumizwa kihisia

Hii inatokea wakati mnaendelea na mahusiano yenu na baada ya kuachwa au kuachana. Kwa sababu aliyekuchumbia au aliyekuoa hakuwa na nia njema na wewe, kitu atakachokuwa anajali ni nafsi yake tu, kama yeye anafurahi basi hawezi kujali furaha yako kabisa; atafanya mambo yanayompa faida yeye hata kama kwa upande mwingine yanakuumiza wewe. Na itakapofika wakati ambao anaona ni wakati wa kukuacha wewe, basi, atakuacha bila hata kujali unajisikiaje.

Katika kipindi chote hiki utakuwa unaumia kihisia, na mtu ambaye anakuumiza ni yule ambaye ulitegemea ndiye awe furaha yako katika maisha yako, sasa amegeuka na kuwa mwiba, kwa nini? Kwa sababu tangu mwanza hakuwa na nia ya kuwa na wewe kwa ajili yako na yake, bali alikuwa anatafuta kujifaidisha kupitia wewe.

Ijapokuwa upendo si hisia, lakini unajumuhisha hisia katika kupokea kwake na kutenda kwake. Upendo ni uchaguzi na maamuzi yanayoambatana na hisia wakati wa kutenda kwake na kupokea kwake. Upendo unatoka moyoni, na hisia pia za upendo hutoka moyoni. Unapoumizwa kihisia maana yake ni moyo wako unaumizwa. Na moyo wako ukiumia ni hisia zako zote zimeumizwa, na si hisia zako tu, lakini pia mpaka namna unavyojisikia kunaathirika; japokuwa utakuwa unasikia njaa, lakini hutasikia hamu ya kula, ijapokuwa utakuwa unataka kulala, lakini hutasikia usingizi kabisa. Wakati mwingine hutasikia kufanya kitu chochote wala kuwa na mtu yeyote bali kuwa peke yako tu.

Hisia zako zikiumizwa, machozi hayaepukiki; utakuwa ni mtu wa kulia na mtu wa uchungu na hasira moyoni mwako. Msongo wa mawazo katika fahamu zako, kila kitu kinakuwa kichungu maishani mwako kwa wakati huo japokuwa inaweza isiwe kweli kabisa, ila kwa sababu umeumizwa kihisia ndivyo uonavyo kwa wakati huo, maumivu na uchungu unakuwa umekupofusha. Na hapa kwa wengine ndio hufikia maamuzi ya kujiua kwa sababu wanaona hakuna uwezekano wa kuishi tena. Siku nyingine nitafundisha Faida na Hasara Za Kuumizwa jambo hili nitalielezea kwa undani.


HATARI YA NNE:

Kuathirika Kisaikolojia

Mtu aliyeumizwa sana katika kile kitu ambacho aliweka moyo wake wote, iwapo atakosa msaada wa karibu sana kutoka kwa watu wengine, itapelekea yeye kuathirika kisaikolojia kama tu ataendelea kuwa katika maumivu hayo.

Dariri za mtu aliyeathirika kisaikolojia ni pamoja na yeye kutowaamini wanaume wote au wanawake wote na kuwaona kuwa ni watu wabaya, kutokutaka tena kuoa au kuolewa na mtu yeyote kisa eti ameumizwa, kuamini kuwa hakuna ndoa isiyokuwa na matatizo na mateso na uchungu, kila ndoa ni mbaya tu watu wanaishi kwa ugumu, anakuwa na hali ya kuchanganyikiwa, kutokujiamini anapokuwa mbele za watu, kuona duniani si mahali salama pa kuishi ni bora afe, nk.

Mtu akifikia hatua hiyo, maana yake ni mgonjwa wa kisaikolojia na anahitaji msaada wa haraka na wa karibu, kwa sababu mtu wa namna hii hata kuomba hawezi, kuwaza vizuri hawezi, kufanya mambo vizuri hawezi, hawezi tena kuhusiana na watu vizuri kwa sababu atakuwa mtu wa uchungu na hasira ndani yake, na hasira na uchungu wake anaweza kumalizia kwa watu wengine ambao hawana shida na yeye kabisa.

HATARI YA TANO:

Kuacha imani (yaani wokovu)

Hii inaweza ikatokea katika mazingira mawili: Moja, wewe kuwa katika mahusiano na mtu ambaye hajaokoka kunaweza kupelekea wewe kurudi nyuma na kuuacha wokovu kabisa. Na ndio maana mtume Paulo anaandika na kusema, Msifungiwe nira na wasioamini kwa jinsi isiyo sawasawa kwa maana hakuna mapatano, hakuna ulinganifu, hakuna urafiki, kati ya mtu aliyeokoka na asiye okoka kwa jinsi isiyo sawasawa.

Katika upande wa pili, kama aliyekuacha na kukuumiza ni miongoni mwa watu waliookoka, unaweza ukaona hata wokovu wenyewe hauna maana kisa aliyekuacha naye ameokoka, ukaamua kurudi nyuma na kuacha wokovu.

Mahusiano yasiyo sahihi ni hatari sana ten asana kwa hatima ya maisha yako na kwa afya ya maisha yako ya kiroho mbali na haya ya kawaida, ni vyema ukawa makini.

HATARI YA SITA:

Kukosa raha katika ndoa yako yote na hata uchumba wako

Hii ni kwa sababu ya maugomvi ya mara kwa mara yasiyokuwa na sababu za msingi. Kwa kuwa hauko na mtu sahihi, mara kwa mara mtajikuta mnapishana, na hamuelewani, kila saa mnazozana, kitendo ambacho kila siku kitakuwa kinapelekea ugomvi. Maugomvi ya mara kwa mara yanaondoa raha ya moyoni, maisha yako yanakuwa ya taabu na udhuni kwa sababu ulitarajia amani lakini sasa ni ugomvi na maumivu, ulichokitarajia unakuwa umekikosa.

MAMBO YA KUFANYA ILI KUEPUKA KUINGIA KATIKA MAHUSIANO YASIYO SAHIHI

Moja: Kusudia moyoni mwako kusubiri malangoni mwa Bwana

Biblia inasema, “Ana heri mtu yule anisikilizaye, Akisubiri siku zote malangoni pangu, akingoja penye vizingiti vya milango yangu.” Mithali 8:34 Ni muhimu tukaelewa kuwa, mke mwema mtu hupewa na Bwana, na kadhalika mume mwema mtu hupewa na Bwana. Ni vyema ukatulia katika maombi na katika neno la Mungu ukimsihi Mungu aziongoze hatua zako kwa kukuongoza moyo wako kumjua mtu sahihi anayekufaa.

Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana.” Zaburi 37:23 iwapo utamtegemea Mungu na si akili zako katika jambo hilo Mungu atauongoza moyo wako kwa mtu sahihi kwa sababu hatua za mtu zaimarishwa na Yeye. Jambo kubwa ni wewe tu kusubiri malangoni pake.

Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Mithali 23:4 Katika jambo hili la mahusiano ili usikosehe, unapaswa umtegemee na kumtumainia Mungu bila kuzitegemea akili zako mwenyewe, lakini uzitumia akili zako jinsi ipasavyo. Usichague mwenye wa maisha kwa kuzitegemea akili zako, mtegemee Mungu, lakini wakati unamtegemea Mungu, tumia akili zako kupambanua jema na baya kwa kila anayekuja kwako au unayemuona huku amani ya Kristo ipitayo akili zote ikiamua moyoni mwako.

Mbili: Epuka kuoa au kuolewa na mtu usiye mjua au asiye shuhudiwa mema na watu.

Si kila anayekuja na kukuambia anataka kukuoa anaweza kuwa mume wako, na si kila unayemwona unafaa kumuoa akawa mke wako. Zingatia mambo mawili haya, Unamjua? Mbili, Anashuhudiwa mema? Kama unamjua na anashuhudiwa mema kilichobaki ni amani ya moyo wako, kama moyo wako una amani ya kumuoa au kuolewa naye basi endelea.

Tatu: Epuka kuoa au kuolewa kwa shinikizo au ushawishi wa ndugu na marafiki

Kama utakubali kuoa au kuolewa ni kwa sababu wewe mwenyewe umeridhia moyoni mwako kumuoa au kuolewa na mtu huyo, na si kufata shinikizo au ushawishi.

Nne: Usiuachie moyo wako mapema kumpenda mtu uliyeingia naye katika mahusiano ya uchumba

Hii ni kwa ajili ya tahadhali, pengine ameificha tabia yake, au pengine amekuja na kubadilika ghafla na kukataa kuwa na wewe kwa sababu watu hughafirika kabisa. Unapoingia kwenye mahusiano weka na kakipengele kadogo kakuona wasiwasi katakachokusaidia kuwa mwangalifu. Usijiachie sana, wewe ni uchumba, na ndio kwanza ni mwezi mmoja, tayari umeisha mimina moyo wako na kujimimina na wewe mwenyewe kwa mtu huyo, ikitokea akaghafirika kisha akakuacha si ndio itakuwa majanga?

Tano: Epuka watu wanaotaka tendo la ndoa kabla ya ndoa

Ukiona tu anakutaka kingono huyo hakupendi, na ukiona kama ni mwanamke anakushawishi kupitia mwili wake ili kuingia kwenye mahusiano naye, huyo ana kitu anakitafuta na si ndoa, mwepuke kabisa.

Sita: Epuka kuinga katika mahusiano na mtu katika mazingira yasiyo rasimi

Ni vizuri kama anayetaka kukuoa ana kusudi hilo akakufuata sehemu salama kwako, asikueleze nia yako katika mazingira hatarishi na yasiyo rasimi. Mtu amekutana na wewe njiani halafu anakwambia anataka kukuoa. Kama ana nia ya kufanya hivyo, basi aidha aje nyumbani kwenu au aweke mihadi na wewe ya kukutana na wewe sehemu salama ukiwa na watu unaowaamini.

Na pia mnapokubaliana kuoana ni muhimu mkawajuza watu mnaowaamini kwa ajili ya usalama wa mahusiano yenu. Anaweza kuwa ni mchungaji, au kiongozi yeyote wa kanisa mnaye mwamini, na pia anaweza kuwa rafiki au ndugu wa karibu mnayemuheshimu na mwaminifu katika kuweka siri.

Saba: Epuka kuingia kwenye mahusiano mapya kuganga moyo wako au hisia zako zilizoumizwa

Kama ulikuwa kwenye mahusiano kabla, na bahati mbaya ukatendwa nawe ukaumia sana, epuka kuingia kwenye mahusiano mapya ukiwa ukiwa bado una maumivu ya mapenzi. Hali hiyo itakufanya usijue ni wakati gani kwako ni sahihi kuanzisha mahusiano mapya, na ni mtu yupi kwako ni sahihi kuanzisha mahusiano mapya naye.

NITAMJUAJE MTU ASIYE SAHIHI KABLA SIJAINGIA KWENYE MAHUSIANO NAYE?:

Swali hili nimekuwa nikiulizwa na watu wengi sana, ukweli ni kwamba, ni rahisi sana kumjua mtu asiye sahihi kabla ya kuingia naye katika mahusiano, lakini ni ngumu sana pia kumjua, inategemea na wewe umesimama wapi. Kama ni mcha Mungu na unamtumainia Mungu wako kwa kila jambo na huzitegemei akili zako, jambo hili ni rahisi sana, na kama unazitegemea akili zako, sikufichi, huwezi kumtambua kabisa.

Hata hivyo, nitakueleza vitu ambavyo vinaweza kukusaidia kumtambua mtu ambaye si sahihi kwako.

Moja1: Mjue kwanza yeye ni nani, na anatokea wapi, na anaishi vipi na watu wanaomzunguka, na je, alishawahi kuwa kwenye mahusiano? Kama ndio, ni kwa nini mahusiano hayo yalivunjika?

Enzi za wazee wetu walizingatia sana jambo hili, hawakuruhusu mabinti wao au vijana wao kuingia kwenye mahusiano na mtu wasiyemjua, na wasiyeijua familia yao. Walihakikisha wanamjua kwanza na kujua familia yao. Hawakuishia hapo, walifuatilia pia historia na mazingira ya familia yao, pia walitaka kujua tabia ya muhusika na anaishi vipi na watu. Vitu hivi vina maana sana.

Mbili 2: Tumia amani ya moyo wako kufanya maamuzi:

Moyo wako unajua kwa sehemu kubwa, na una uwezo wa kuhisi hatari hata kabla haijatokea. Wengi wetu katika mahusiano, tunapotaka kuanzisha mahusiano huwa hatusikilizi moyo unasema nini. Moyo kama una amani, basi huyo mtu anaweza kuwa sahihi, lakini moyo kama una mashaka na kukosa amani, bila shaka mtu huyo anaweza kuwa ni bomu, mchunguze kwa kina.

Tatu 3: Kwa wadada, mtu ambaye anakuja kwako moja kwa moja au baadaye kidogo baada ya kumkubalia na kukutaka kimapenzi, muanze kufanya naye tendo la ndoa, huyo si sahihi kwako. Na kwa wanaume vivyo hivyo, mdada anayekulazimisha au anayekutega ili ufanye naye ngono, huyo si sahihi, anatumia ngono kupata anachokitaka kwako.

Nne 4: Mtu ambaye si mkweli kwako, asiyejari hisia zako, na asiyesikiliza hoja zako na kuzipa nafasi ya kwanza.

Kutambua hili inahitaji muda kidogo, na ndio maana mimi nashauri, kabla hujamkubalia, ni vyema kwa tahadhari kubwa sana mkawa marafiki wa kawaida ili kumpa kila mmoja nafasi ya kumjua mwingine. Mkisha ridhika basi ndipo mkubaliane kuingia kwenye mahusiano ya uchumba.

Tano 5: Mtu asiyemcha Mungu, anayeishi bira utaratibu.

Ukiona mtu tu anayekuchumbia au unayemchumbia hamchi Mungu, basi, tambua kuwa huyo hutomweza, na yeye kwa sababu hana hofu ya Mungu, kukuacha wewe si jambo kubwa sana, ni kufumba na kufumbua.

Sita 6: Unayepishana naye kitabia:

Ukiona tabia zako na zake zinapishana, kila wakati yeye anaona makosa kwako, na wewe unaona makosa kwake, na kwa sababu hiyo mnakwaruzana hata kwa sababu ya silka na hulka zenu, jua kabisa huwezi kufika naye mbali, mapema kabla hamjaingia kwenye uchumba wakati mko kwenye urafiki wa awali, kimbia huyo si sahihi kwako.

Tatizo la mahusiano mengi ya siku hizi yanatokea kwa ajali; Umemwona mtu madhabahuni anaimba, tayari umeisha mpenda, unamfuata na kumchumbia anakufuata na kukuchumbia na wewe unamkubali, umekutana na mtu harusini, tayari unamchumbia, anakuchumbia na wewe unamkubali, umekutana na mtu safarini, mmekaa siti moja, masaa manne ya kusafiri kwenu mnazoeana kiasi cha kuchumbiana, hiyo si ni ajali jamani!!?

Wewe mtu huwa unamwona-mwona tu hapo mtaani, humjui, anamchumbia au anakuchumbia na wewe unamkubali, swala ni kwamba, unamjua? Wewe mtu humjui, kisa umemwona siku mbili anacharaza maombi kanisani na ananena kwa lugha ile mbaya, unamchumbia au anakuchumbia na wewe una mkubali, je unamjua?

Ndoa ni swala la moyo wako uliobeba hisia zako zote, na ni swala la maisha, hutakiwi kuingia katika mahusiano kwa ajali, it shouldn’t be an accident, it should be a planned and processed matter that secures and protects your heart and its emmotions so that you may be not hurt. Ukileta mzaa, utachezewa kweli na wewe utachezeka kweli mpka utabaki huna matumaini tena.

Ni maombi yangu kwamba, uwe na mahusiano yenye mafanikio maishani mwako, Mungu akukutanishe na mtu sahihi atakayekupa raha maishani mwako na si maumivu. Ukastawi na kuongezeka katika eneo la mahusiano ukiwa mwenye amani tele na furaha daima. Ukamfurahie mke/mume wa ujana wako tangu ujana wako mpaka uzee wako. Kujuta kukafichwe na macho yake Mungu Baba aliyemtoa Yesu Kristo afe kwa ajili yako ili uwe na amani siku zote. Mahusiano yako yakadumu katika wingi wa amani na heri na fanaka. Katika Jina la Yesu Kristo Bwana, ninatangaza haya,

Amina.

Mwisho

البحث
الأقسام
إقرأ المزيد
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 38
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 39 questions at the...
بواسطة THE HOLY BIBLE 2022-01-21 09:13:18 0 5كيلو بايت
OTHERS
UISLAMU NI UPAGANI ULIOBORESHWA
Waisalmu wamekuwa ni watu wa kujivuna kujingamba kuwa wao ndiyo wenye Dini ya kweli, Ibada ya...
بواسطة MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-25 11:28:19 0 5كيلو بايت
PRE-UNIT
PRE-UNIT 1
List of all of subjects for pre-unit 1 students
بواسطة PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 10:08:46 0 5كيلو بايت
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 4
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 84 questions at the...
بواسطة THE HOLY BIBLE 2022-01-24 08:55:38 0 5كيلو بايت
MAHUSIANO KIBIBLIA
SEHEMU YA 5: MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA
Bwana asifiwe!! Unaweza kusoma SEHEMU YA 1, SEHEMU YA 2, SEHEMU YA 3, SEHEMU YA 4 ya somo hili,...
بواسطة GOSPEL PREACHER 2021-11-06 11:49:18 0 5كيلو بايت