UNA HOFU YA KUTOKUOLEWA, AU KUACHIKA? SOMA HII ITAKUSAIDIA

0
6K

Kama wewe ni mwanamke na bado hujaolewa, na sasa kitu kama hofu ndani yako ya kutokuolewa kimeingia, somo hili linakuhusu sana tu. Lakini pia labda una hofu ya kupoteza mchumba wako, au mume wako, somo hili pia linakuhusu.

Leo japo nitazungumza kwa kirefu kidogo lakini kwa kina nataka nizungumzie tatizo linalowakumba wanawake wengi wa sasa katika mahusiano yao, HOFU YA KUTOKUOLEWA, KUACHIKA AU KUPOTEZA MCHUMBA (AU MUME). Naomba usome mpaka mwisho, ITAKUSAIDIA

Uzoefu unaonyesha wazi kuwa, wadada wengi wana hofu ya kutokuolewa na hasa inapofika wakati ambao wao wanadhani wako tayari kuolewa lakini hakuna maendeleo yoyote zaidi ya mahusiano kuvunjika au kutokuwa katika mahusiano kabisa, au kuwa katika mahusiano na watu ambao sio sahihi wanaowaumiza mara kwa mara. Au kufuatwa na wanaume wasio sahihi kabisa, kwa mfano mdada kufuatwa na wanaume ambao wameisha oa, au mdada aliyeokoka kufuatwa na wanaume ambao hawajaokoka, au mdada kufuatwa na wanaume wazee wasio wa makamo yake na kuonyesha nia ya kumuoa kabisa.

Wewe kama dada unayejitambua, na umeokoka na unamcha Mungu, na unajua kuwa uliumbwa kwa kusudi hupaswi kuwa na hofu kabisa ya kutokuolewa, kwa sababu kila unachokipitia ni hatua kuelekea kwenye hatima yako.

Bora kuolewa ukiwa mzee kuliko kuolewa ukiwa kijana na mtu asiye sahihi akakutesa maisha yako yote. Bora raha kamili ya muda mfupi kuliko mateso na uchungu wa muda mrefu. Na bora kubaki ukiwa hujaolewa lakini ndani ya kusudi la Mungu kuliko kuolewa lakini nje ya kusudi la Mungu. Kwa hiyo hupaswi kuwa na hofu kabisa kwa sababu nina uhakika UTAOLEWA NA UTADUMU KATIKA NDOA YAKO UKIWA MWINGI WA FURAHA IWAPO UTASIMAMA KATIKA KWELI NA KATIKA KUSUDI

KWA NINI HUPASWI KUWA NA HOFU ISIPOKUWA UHAKIKA?

MOJAMAKUSUDI YA MUNGU KATIKA UUMBAJI WAKE

Mathayo 19:4, inasema,
“Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba Yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,”

Hili ni sehemu ya jibu la Yesu baada ya kuulizwa swali na Mafarisayo kama ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu. Ili kujibu swali hili Yesu Kristo aliwarudisha Mafarisayo hawa katika maandiko kwa kuwaambia “HAMKUSOMA KWAMBA” kwa lugha nyingine ni kusema kwamba, “IMEANDIKWA”.

Lakini pia katika maandiko hayo aliwachukua na kuwarudisha mwanzo katika uumbaji wa Mungu na kuwaambia kuwa, “Yeye ALIYEWAUMBA mwanzo ALIWAUMBA MTU MUME NA MTU MKE, na hapa ndipo penye hoja yangu ya kwanza ya msingi itakayokujenga wewe mwenye hofu ya kutokuolewa au kumpoteza mchumba wako, na hata kwa wewe uliyeko kwenye ndoa mwenye hofu ya kuachika.

ALIYEWAUMBA MWANZO ALIWAUMBA MTU MUME NA MTU MKE
Katika mawazo ya Mungu alipokuwa anawaza kukuumba wewe na kwa njia ya mama na baba yako uzaliwe, hakuwa anawaza juu yako peke yako, kama wewe mwanamke alipokuwa anakuwaza, aliwaza na juu ya mume wako, na aliporuhusu uzaliwe katika majira haya pamoja nawe aliruhusu mume wako pia azaliwe katika majira haya. Kwa hiyo, haukutokea duniani ukiwa “single” bila mume, ulipozaliwa na mume wako alizaliwa, ulitokea duniani ukiwa na mume wako. Wewe hukuwa unajua, lakini Mungu aliyewaumba anajua hilo, kwa sababu alipowaumba aliwaumba mtu mume na mtu mke.

Huna haja ya kuwa na hofu ya kutokuolewa, hata kama unaona umechelewa kuolewa tambua kuwa, Mungu alikuumba wewe pamoja na mumeo, na ya kwamba alichokiumba kwa ajili yako hawezi kukichukua na kumpa mtu mwingine, maana Mungu wetu HANA KIGEUGEU hata ageuke na kubadilikabadilika.

Kama unaona umechelewa, hiyo ni hali ya kibinadamu tu yenye msukumo wake katika mazingira ya kibinadamu. Lakini ukweli ni kwamba Mungu huwa HACHELEWI wala HAKAWII kutimiliza Neno lake na ahadi zake. Yeye ni Mungu asiyefungwa na majira na nyakati, ambaye hujibu mambo kwa majira na nyakati zake sawasawa na kusudi lake. Hauna haja ya kuogopa wala kuwa na shaka yoyote ukijua hili.

Kwa wewe ambaye umeolewa na unayo hofu ya kuachika, Yesu alisema kuwa, “Kwa sababu hiyo, (ya Mungu kuwaumba mtu mume na mtu mke tangu mwanzo), mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”

Kitu ambacho unapaswa ukielewe ni kwamba, Mume wako baada ya kukuoa wewe amekusudiwa kuwaacha baba yake na mama yake na si kukuacha wewe, anawaacha wao ili aambatane na wewe, na si kukuacha wewe ili aambatane na wao. Akiisha kukuoa wewe, amekuwa mwili mmoja na wewe, na kwa sababu hiyo hapaswi kukuacha kwa namna yoyote ila anapaswa kuwaacha wengine wote kwa ajili yako. Ukilijua hili hofu ya kuachika haitakuwepo kabisa hata kama utakuwa unaona dalili za kuachika, utatumia Neno hili kumwomba Mungu kufunga mlango wa kuachika kwako.

Biblia inasema kwamba, tumepewa funguo, tutakalolifunga duniani na mbinguni litakuwa limefungwa, na tutakalolifungua duniani, na mbinguni litakuwa limefunguliwa. Kuliko kukaa na hofu yako, tumia mamlaka yako kufunga usichokitaka na kufungua unachokitaka kwa kusimama katika Neno la Mungu na makusudi yake tangu mwanzo. Wewe haukuolewa ili uachike, uliolewa ili udumu katika ndoa, basi.

Binti, haukuumbwa peke yako, uliumbwa pamoja naye wa kukuoa, kwa hiyo haukuumbwa ili ukae katika hali ya kuwa peke yako, uliumbwa ili uolewe na uishi na mumeo pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisa. Kwa hiyo hakuna haja ya kuogoma.

MBILIUHAKIKA WA KUPEWA MATAKWA YAKO
Biblia inasema kuwa, “Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; Na wenye haki watapewa matakwa yao” Hofu ni kwa wale wasio wenye haki kwa sababu wao matakwa yao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo. Lakini kwa mwenye haki yeye hapaswi kuogopa kwa sababu ATAPEWA MATAKWA YAKE.

Wewe kama ni mwenye haki wa Mungu, basi unao uhakika wa kupewa matakwa yako, hata kama yatachelewa kiasi gani, laiki uhakika upo. Kitu ambacho unapaswa uwe nacho ukiishakuwa na uhakika wa kupewa matakwa yako ni SUBIRA na TUMAINI.

Ayubu anasema, “Kwani yapo matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena, Wala machipukizi yake hayatakoma” (Ayubu 14:7). Hata kama utachumbiwa na mchumba wako akakuacha, bado tumaini lipo, kuachwa sio mwisho, inaweza kuwa umekatwa ili uchipue upya katika uzuri wa ajabu uliokusudiwa. Kwa hiyo, usiwe na hofu ya kutokuolewa kabisa eti kwa sababu umeachwa na mchumba wako.

Ayubu anaendelea kusema, “Ijapokuwa miziz yake huchakaa mchangani, Na shina lake kufa udongoni, Lakini kwa harufu ya maji utachipuka, Na kutoa matawi kama mche.” (Ayubu 14:8 – 9). Hata kama unajiona unaelekea kuzeeka umri unasonga, kwa harufu ya maji (ambaye ni Roho Mtakatifu) atayarejesha majira ya usichana wako, kwa kuwa kwake hakuna lisilowezekana, na Anasema katika Zaburi 103:4, kwamba Mungu anao uwezo wa kuurejesha ujana wako kama tai. Kwa hiyo huna haja ya kuwa na hofu ya kutokuolewa eti kwa sababu umri unasonga.

Miaka yako isikutishe, kadiri umri unavyosonga ndivyo majira yako yanavyokaribia ya kuolewa kwako. Badala ya kuhuzunika na kukata tamaa mshukuru Mungu na umsifu kwa kuwa alikuumba mwanamke, na ya kwamba huyajibu matakwa yako yote.

HOFU NI MLANGO WA KUPITISHIA USIYOYATAKA YAKUJILIE NA KUKUPATA

Ayubu anasema, “Maana jambo hilo nilichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia” (Ayubu 3:25). Hofu ni mlango wa kupitishia yale yote usiyoyataka yatokee katika maisha yako. Unaloliogopa (lile usilolitaka), maadamu unaliogopa litakujilia na litakupata bila shaka. Na hofu ni matokeo ya kutokuwa na imani. Hofu ni kazi (is a function) ya kusitasita, na mwenye haki anayesitasita Mungu hana furaha naye, maana ni kama wimbi la bahari lipeperushwalo na upepo likipelekwa huku na huku. Lakini mwenye haki wa Mungu ataishi kwa imani yake, na si kwa kusitasita.

Kwa kuwa wewe unajua kuwa, Mwenye haki atapewa matakwa yake, na ya kwamba kusudi la Mungu (la kuwaumba mtu mume na mtu mke) ndilo litakalosimama, hauna haja ya kuwa na hofu kabisa hata kidogo. Kwa sababu utakapoanza kuogopa, ukiogopacho kitakujilia na kukupata, na ndio maana Mungu katika kitabu cha Isaya alitukataza kuhofu kwa hofu yao.

Anasema, "Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, Msiseme, Ni fitina, katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni fitina; MSIHOFU KWA HOFU YAO, WALA MSIOGOPE.” (Isaya 8:11, 12).

Ni kweli watu wa dunia hii wana hofu ya kutokuolewa na sababu wanazo, wana hofu ya kuachika, na sababu wanazo, lakini wewe haikuhusu kabisa, maadamu umerejea kwa Bwana Mungu wako na kwenda katika njia zake Biblia inasema kwamba, “..Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini” (Isaya 30:15)

Kwa kurudi na kustarehe (relax): Kila unapoona hali ya kutaka kuwa na hofu, rudi katika ahadi na Neno la Mungu, kisha katika hilo starehe (relax). Tatizo la wengi haturudi kwa Bwana na kustarehe kwa Mungu wetu katika ahadi zake, ndio maana hofu zao zinakuwa hofu zetu na kwa sababu hiyo yanatupata tusiyoyataka yaliyowapata wao waogopao.

Nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini: Unataka nguvu ya kuendelea mbele katika kusubiri majira ya Bwana ya kujiliwa kwako? Jibu kama ni ndio, basi acha papara, utulize moyo wako kisha utumaini. Aliyewaumba mtu mume na mtu mke ndiye tumaini lako, utulize moyo wako kwake, na umtumaini yeye naye atafanya. Nguvu zako zipo katika KUTULIA NA KUTUMAINI.

Moja ya sifa kubwa ya mtu aliye na hofu ni kwamba, Hana utulivu wowote, utamwona anahangaika mara huku mara kule, anashika hiki mara kile, anakanyaga hapa mara pale, anapepesa macho yake huku mara kule, hana utulivu kabisa. Lakini pia hana tumaini lolote, mashaka yamejaa moyoni mwake. Ndivyo walivyo mabinti wa leo, hawana nguvu ya kusubiri malangoni pa Mungu kwa sababu hawana utulivu na kutumaini; wanadhani kila kijana anayekuja mbele ya macho yao ndiye, na mwisho wao wanaumizwa na kubaki na mejeraha mioyoni mwao.

Mtulivu na mwenye tumaini huwa ni ngumu kudanganyika, lakini pia huwa hakati tamaa na wala hawewesuki, ni kama mlima Sayuni usiotikisika, hatikiswi anakaa milele. Hata ukija na njonjo zako, yeye ni imara wala hutoweza kumtikisa. Ila ukikutana na binti aliyejaa hofu ya kutokuolewa, mara moja tu utambeba, usiwe wewe miongoni mwao waogopao kutokuolewa au kuachika au kupoteza wachumba au waume zao.

Căutare
Categorii
Citeste mai mult
OTHERS
JEHANNAM NI NYUMBA YA MILELE YA WAISLAM
JEHANAMU IPO NA INASUBIRI WATENDA DHAMBI Huko motoni Jehanum kukoje? Mwanangu, kunatisha,...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 22:29:42 0 5K
REVELATION
UFUNUO 16
Jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe…Karibu katika mwendelezo wa kitabu cha Ufunuo,...
By GOSPEL PREACHER 2021-10-30 11:58:27 0 6K
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 15
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 52 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:13:31 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
ENYI WANAWAKE MSINILILIE MIMI
Kwa nini Yesu aliwaambia akinamama jililieni nafsi zenu na watoto wenu ?Luka 23:27-28 “Na...
By GOSPEL PREACHER 2021-12-16 12:14:49 0 5K
GENESIS
THE BOOK OF GENESIS
  TY GENESIS 1 Verse by verse explanation of Genesis 1 Questions on Genesis 1 GENESIS 2...
By GOSPEL PREACHER 2021-08-26 05:35:22 0 5K