ZINGATIA YAFUATAYO ILI KUANZISHA MAHUSIANO SAHIHI YANAYOFIKIA MALENGO

UTANGULIZI
Mahusiano sahihi ni mahusiano ya namna gani?
Mahusiano sahihi ni mahusiano yale ambapo wewe unaingia kwenye mahusiano na mtu unayempenda kweli naye anakupenda kweli na yanayozingatia utimilifu wa makusudi yake ya kuanzishwa.
Mahusiano sahihi ya uchumba hadi ndoa ni yale yanayoanzishwa kwa kusudi la kuoana huku wahusika wakiwa wanapendana kweli, mwanaume akimpenda mwanamke na mwanamke akimpenda mwanaume. Lakini pia ni mahusiano yenye nidhamu ya mahusiano; mahusiano yanayozingatia nidhamu katika kila hatua ya mahusiano. Kwa mfano mahusiano sahihi ya uchumba ni yale yenye nidhamu ya kutofanya mapenzi (tendo la ndoa) kabla ya ndoa.
Haya ni mahusiano ambayo kila upande unamuheshimu mwenzake, kumthamini na kumtanguliza, na haya ni matokeo ya upendo wa kweli na si tamaa za mwili zitokanazo na matamanio yetu katika kuvutiwa na mtu fulani katika vile alivyonavyo ambavyo naweza kufaidika navyo, ikiwa ni pamoja na mapenzi, fedha, mali n.k.
Mahusiano sahihi hayatoki nje ya upendo, msingi wake mkubwa ni upendo usio na unafiki, upendo wa kweli kabisa. Mahusiano yoyote yasiyotokana na upendo kwa kila upande, au yale yanayokuwa na upendo wa upande mmoja si mahusiano sahihi kabisa, na kwa sababu hiyo hayana garantii ya kufikia malengo.
Mahusiano yasiyokuwa na malengo (ya kuoa) yaliyo wazi si mahusiano sahihi; mtu anapoanzisha mahusiano na mtu wakati hana lengo la kumuoa au kuolewa naye maana yake ana lengo lingine na kwa sababu hiyo hawezi kutimiza lengo hasilonalo na badala yake atatimiza lengo alilonalo.
Mahusiano yasiyo sahihi yanatabia zifuatazo; yamegubikwa na udanganyifu, kukosa uaminifu, wivu usio na sababu, upendo wa pande moja, tamaa, usaliti, kutokujaliana, kutokusameheana, ubinafsi na choyo. Mahusiano ambayo mtu anajijali yeye mwenyewe kuliko kumjali mwingine hayo si mahusiano sahihi kabisa. Mahusiano sahihi ni yale ambayo kila mmoja anamjali mwenzake na kumtanguliza yeye kwanzaa katika kila kitu huku akimthamini na kumpa heshima ya kwanza.
HATUA KATIKA MAHUSIANO
Mahusiano ya kweli na yenye tija huwa si matokeo ya dharura, si ajali na wala si jambo ambalo linatokea ghafula tu bila kupangwa na kuandaliwa mazingira. Ni jambo linalotokea hatua kwa hatua mpaka kufikia katika kilele chake.
Bahati mabaya katika dunia ya kizazi cha sasa (leo) mahusiano mengi ni dharura, na ndio maana hayawaachi watu wengi salama. Ajali ni dharura, na huwa hamwachi mtu salama, kuna wachache huponea chupuchupu, laiti kama wangelikuwa wanajua kuna ajali inakwenda kutokea, na wakajiandaa namna ya kuepuka hiyo ajali, basi ajali isingelitokea na kama ingelitokea wasingeliumia au wasingelikufa kwa sababu wamejiandaa kwa kuchukua tahadhari. Lakini kwa sababu ni jambo la ghafula ambalo halikupangwa, wote huumia na wengine kufa.
Mtu ambaye hataki bahati mbaya, hataki ajali, hujiandaa, huweka tahadhari kwa ajili ya usalama wake. Hatua hizi katika mahusiano zinamsaidia mtu kupangilia matakwa yake ya kuwa katika mahusiano kwa kuzingatia ni mtu wa aina gani anapaswa kuwa naye katika mahusiano.
Hatua ya Kwanza: Urafiki (Friendship)
Katika swala la mahusiano ya uchumba hadi ndoa, urafiki ni mahusiano yanayompa mtu nafasi ya kumfahamu na kumjua mtu kwa kumsoma kitabia. Haya ni mahusiano ambayo hufanyika kabla ya mtu kuingia katika mahusiano ya uchumba. Ni mahusiano ya kindugu, si lazima yawe ni ya kirafiki wa karibu sana. Ni katika ile ngazi (level) ya kuishi vizuri na watu wanaokuzunguka, kama ni mdada, unaishi vizuri na wakaka wote wanaokuzunguka, unakuwa karibu nao, iwe ni kazini, iwe ni shuleni, iwe ni nyumbani, iwe ni kanisani au pahala penginepo popote, na vivyo hivyo kwa upande wa mkaka. Huu ndio uhusiano wa kirafiki unaokupa nafasi ya kumsoma kila mtu na kuanza kupambanua ni nani anaweza kukufaa kati ya hao wanaokuzunguka.
Uhusiano huu unakupa nafasi ya kumjua na kumfahamu kila mmoja, na kwa sababu hiyo unakutengenezea uwanja mpana wa kufanya maamuzi yako ya kuingia katika mahusiano. Na katika hatua hii ya mahusiano, ndipo Mungu anaweza kusema nawe kuhusu mume au mke wako atakayekuoa kwa kuweka msukumo ndani yako au kuweka wazo ndani yako. Ni mahusiano yanayokutengenezea mazingira ya kuingia katika mahusiano ya uchumba.
Katika mazingira hayo, utakapokuja kujua ni nani anafaa kuwa mwenzi wako, basi unapandisha kiwango au ngazi ya mahusiano ya kirafiki, kutoka kuwa mahusiano ya kiujumla mpaka kuwa mahusiano ya kirafiki na yule unayewaza kuwa ndiye utakayemuoa au utakayeolewa naye. Unakuwa karibu naye lakini ukiwa bado hujamwambia nia yako (na hasa kwa ninyi wanaume), nia yako inabaki moyoni mpaka pale utakapojiridhisha kuwa yeye ni sahihi kwako na ni kweli umekusudia na si tu mihemuko ya kihisia.
Katika ngazi hii pia, uhusiano wenu unakuwa wa kaka na dada, ni lazima uzingatie mipaka ya kaka na dada, unamuhesabu huyu kuwa ni kaka yako au kuwa ni dada yako.
Urafiki ni nini?
Urafiki ni upendo, kujali, na kushirikiana na kushirikishana (Friendship is love, caring and sharing). Huu ndio urafiki, unawapenda watu, unawajali na unashirikiana nao katika yale wanayokushirikisha na katika yale unayowashirikisha.
Urafiki hauwezi kuwepo pasipo upendo, na upendo unapokuwepo kunakuwa na kujali na kushirikiana. Hii ni ngazi ya kwanza au hatua ya kwanza katika mahusiano. Na moja ya kusudi kubwa au lengo kubwa la hatua hii ni wewe kuweza kumjua mtu ambaye anafaa kuwa mwenzi wako wa ndoa.
Ni muhimu sana ukaelewa kuwa urafiki haunzi pamoja na uchumba, na uchumba unaoanza kabla ya urafiki hauna msingi mzuri kabisa. Huwezi kuanza na mbili bila mojo na huwezi kuanza n azote kwa pamoja katika kuhesabu na katika kuandika, lazima utaanza na moja, na kisha mbili, na mbili haipo bila moja, moja ni msingi na ni alama ya kuanzia (starting point) ya mbili. Kwa hiyo urafiki ni alama ya kuanzia (starting point) ya uchumba. Huwezi kuanza uchumba na mtu usiyemjua, na mtu unayemjua ni rafiki yako, unayehusiana naye kila siku katika mambo mbalimbali.
Hatua Ya Pili: Uchumba
Uchumba ni hatua ya pili katika mahusiano, ni ngazi ya pili ambayo inafuata baada ya kuthibitisha moja, ni nani anafaa kuwa mwenzi wako wa ndoa, na mbili kile unachojisikia moyoni kumuhusu ni kweli, yaani ni kweli unampenda. Ukiisha thibitisha hivyo ndipo sasa unakuwa huru na salama kuingia hatua ya pili au kupanda ngazi ya pili ya uchumba. Kwa lugha nyepesi ni kwamba, huingii kwenye uchumba na mtu usiyemfahamu wala kumjua undani wake, kwa sababu utajikuta unamchumbia au unachumbiwa na mtu asiyejulikana, na watu wasiojulikana sio wema kabisa, wana mitutu ya kuumiminia moyo wako risasi za kutosha tu.
Sasa uchumba ni nini?
Uchumba ni mahusiano kati ya mwanamke na mwanaume yanayompa kila mmoja nafasi ya kutangaza nia yake kwa mwenzake ya kumuoa au kuolewa naye, na yanayowapa nafasi wawili hawa kutangaza nia yao kwa watu wengine kuwa wao wana mpango wa kuoana hivi karibuni.
Haya ni mahusiano ambayo yanakuwa rasmi pale mwanaume anapokuwa kamtolea posa mwanamke anayetaka kumuoa. Mahusiano ya uchumba yanakuwa rasimi au yanaanza rasmi pale ambapo mwanaume anamposa mwanamke anayetaka kumuoa.
Katika Biblia neneno kuposa katika lugha ya Kigiriki iliyotumika kuandika Agano Jipya neno lililotumika ni "mnesteuo" lenye maana ya kuposa (to espouse, betroth), na hii ni kumwomba mwanamke umuoa (to ask her in marriage) na tendo hili huwa linaambatana na kitu unachotoa ambacho ni alama kwa mwanamke husika na kwa wazazi wake kuwa umemuomba kumuoa na umemuahidi kumuoa naye amekubali.
Uchumba ni mahusino yanayowapa nafasi wale walioingia katika mahusiano hayo ya kufanya maandalizi ya pamoja ya kuingia katika mahusiano ya ndoa. Ni mahusiano ambayo wawili hawa wanapaswa kuingia wakiwa na uhakika na nia zao, na kila mmoja akiwa na uhakika kwamba anampenda mwenzake kweli.
Mahusiano haya si maandalizi ya sherehe ya harusi, ni maandalizi ya ndoa. Wawili hawa waliopo kwenye mahusiano ya uchumba, hutumia muda huu kujiandaa kwa ajili ya ndoa yao siku za usoni na si kwa ajili ya harusi yao. Ndoa sio harusi, na harusi haina mchango wowote katika ndoa, haiongezi chochote na wala haipunguzi chochote, kwa hiyo sio lazima ikawepo, na kwa hiyo wachumba hawapaswi kabisa kuipa umuhimu wa juu na kuifanya kipaumbele cha kwanza kuliko ndoa, kufanya hivyo ni kupoteza shabaha na mwelekeo, ni kutoka nje ya kusudi na malengo halisi.
Uchumba sio ndoa, kwa hiyo tendo la ndoa si mahala pake katika uchumba. Na si tendo la ndoa tu, mapenzi (kwa maana ya tendo la ndoa na mambo yote kama vile kutomasana, kubusiana, kunyonyana, kuambiana maneno ya mahaba na kadhalika) si sehemu ya mahusiano ya uchumba. Uchumba ni mahusiano yanayowaandaa tu kuingia katika mahusiano ya ndoa.
Heshima kubwa ya mahusiano ya uchumba hadi ndoa ni uhusiano wa kaka na dada na si zaidi ya hapo. Utamuheshimu mchumba wako kama dada yako na kama kaka yako. Kuvuka mipaka ya kaka na dada ni kuvunjiana uaminifu, lakini pia ni dhambi mbele za Mungu, na hii ina madhara katika ndoa. Siku nyingine nitaeleza hili kwa undani zaidi.
Uhusiano huu wa uchumba unakwenda sambamba na urafiki. Si kwamba urafiki unakoma baada ya kuingia kwenye uchumba, bali ndio unaendelea kwa sababu ndio msingi wa ngazi nyingine zote za mahusiano na alama kubwa katika kila ngazi au hatua ya mahusiano ni urafiki unaozaliwa na upendo wa kweli usio na unafiki. Kwa hiyo upendo ndio kiini cha mahusiano yote, na upendo ni urafiki (Love is friendship) na urafiki ni upendo, kujaliana, na kushirikiana (Friendship is love, caring, and sharing).
Kwa hiyo katika mahusiano ya uchumba kuna upendo, lakini pia kuna urafiki, urafiki hauishii kwenye urafiki, unatelemka chini mpaka kwenye uchumba. Kwa kifupi ni kwamba, haukomi kuwa rafiki yake eti kwa sababu umemchumbia, bali unakua na kuongezeka katika wewe kuwa rafiki yake wa karibu zaidi kwa sababu umemchumbia au amekuchumbia, lakini urafiki huo unakuwa na mipaka ya kimahusiano, na mahusiano hayo ni mahusiano ya kaka na dada na si zaidi ya hapo.
Uchumba ni nafasi ya kujiandaa kwa ajili ya ndoa. Napenda kurudia hoja hii ili iingie barabara katika fikira zako na kupenya ndani kabisa katika moyo wako. Kitchen part, Sendoff na harusi hazina sehemu kabisa katika mahusiano haya kwa sababu hazina mchango wowote katika ndoa yako. Labda utaniambia, “Oooh kwenye kitchen part wanamfunda mwanamke kwa hiyo ina umuhimu” nami nakuuliza, walikuwa wapi siku zote hizo kumfunda? Ng’ombe hanenepi siku ya mnada, kama hawakumfunda kwa miaka yote tangu avunje ungo yatamuingiaje mambo ya mume na mke kwa siku moja yanayotosha kwa kipindi cha miaka yote atakayoishi na mume wake? Haina maana kabisa, na hiyo si sehemu ya uchumba kama wengine wajuavyo.
Niweke msisitizo mkubwa kwamba, "Uchumba sio ajali, wala si huduma ya dharura, hautokei kwa bahati mbaya bila ufahamu wa mtu, ni jambo lililopangwa na kukusudiwa lililopitia katika mchakato mrefu tu wa kutosha katika hatua ya urafiki ambapo wawili hawa kabla hawajaelezana nia zao na pengine kabla hawajajua kama itatokea wao watakuwa pamoja, husomana na kufahamiana na kujuana vyema kupitia mahusiano ya kiudugu na urafiki waliyonayo, na kutokea katika kujuana huko kila mmoja akiwa na uhakika na kile anachokwenda kufanya wanafanya maamuzi na wanakubaliana kuingia katika mahusiano ya uchumba hadi ndoa"
Kuingia katika mahusiano haya ni kusema nimekubali kukuoa au nimekubali kuolewa na wewe na kwa hiyo hakuna kugeuka nyuma kabisa. Yesu akiwa anazungumzia uhusiano wake na mtu anayetaka kumfuata, anasema, "Mtu akichukua jembe lake kwenda shambani kulima, kisha akageuka nyuma, huyo hanifahi". Hii maana yake ni nini, maana yake ni kwamba, kuingia kwenye mahusiano ya kimaisha (yanayochukua siku zako zote za maisha yako) na mtu ni tendo ambalo unapaswa ulifanyie maamuzi ya moja kwa moja ambayo hautakuja kubadilika au kugeuka baada ya kuingia. Na hii ndio sababu ni lazima uwe na uhakika ya kwanba huyo unayeingia nae ndiye, na uhakika huo unaupata kwa sababu unamjua na kumfahamu vyema, vinginevyo utaumia kama sio kuumiza, utaumizwa kama sio kuumiza.
Uchumba si majaribio, huchumbii ili kujaribisha na wala humkubalii aliyekuchumbia ili kujaribisha, hilo ni swala nyeti sana linalohusisha hisia za moyo wa mtu na maisha yake yajayo. Kwa hiyo si jambo la kujaribisha; huwezi kujaribisha kumuua mtu kwa risasi au kwa kumchoma mkuki au kwa kuikata shingo yake na kisu, kufanya hivyo ni kumuua kabisa na kamwe huwezi kurudisha uhai wake. Usijaribishe, kama huna uhakika, nyamaza usimwambie, na wala usimkubalie.
Hatua Ya Tatu: Ndoa
Hii hatua ya tatu ndio hatua ya mwisho na ndio lengo la kuanzishwa kwa mahusiano kati ya mwanamke na mwanaume; wanaanzisha mahusiano ili waoane wawe na ndoa inayowapelekea kuishi pamoja.
Ndoa ni nini?
Moja kati ya neno la Kigiriki lililotumika kuelezea ndoa ni "Suzegnumi" lenye maana ya kuunganishwa (unite) au kufungiwa nira pamoja (to yoke togather) na neno hili hutumika kuelezea uhusiano wa ndoa tu. Na ndilo neno alilolitumia Yesu katika kitabu cha Mathayo 19:6 na Marko 10:9 akielezea ndoa kama uhusiano wa mwanamke na mwanamume wanaoishi pamoja kama mke na mume.
Maelezo ya ufafanuzi (definition) ya neno hili ni, Suzegnumi ni muunganiko (union) ambao katika huo mume na mke wanaishi pamona vizuri kwa ajili ya Bwana kwa ajili ya kusudi la Mungu, kuliko vile ambavyo kila mmoja angeliishi peke yake.
Sasa basi;
Ndoa ni mahusiano yanayowaunganisha wawili (mwanamke na mwanaume) kuwa mwili mmoja na kuweza kuishi pamoja (katika kutimiliza kusudi la Mungu) kwa upendo wakithaminiana, kushirikiana, kujaliana, kuchukuliana, kuombeana, na kufanyiana mambo mema huku wakiwa na wakati mzuri wa kushiriki tendo la ndoa kwa furaha. Ni mahusiano pekee yanayojumuisha mwanaume na mwanamke kushiriki tendo la ndoa na isihesabike dhambi kwao hata kidogo. Na ni mahusianao ambayo tendo la ndoa ni salama kabisa kwa wawili hawa na halina madhara iwapo kila mmoja atakuwa mwaminifu kwa mwenzake kila siku awapo karibu au awapo mbali.
Katika ngazi hii kiwango cha mahusiano ya urafiki hupaswa kuongezeka kwa hali ya juu. Mwenzi wako anapaswa kuwa rafiki anayeambatana nawe kuliko ndugu; urafiki unatoka kuwa wa kawaidia unafikia pahala ambapo ni urafiki usioweza kufananishwa na urafiki wa aina yoyote ule, ni urafiki unaopita mahusiano ya undugu. Unampenda, kumjali, na kushiriki mambo ya mkeo au mumeo kuliko mambo ya wengine wote ikiwa ni pamoja na rafiki zako, ndugu zako, wafanyakazi wenzako, biashara na kazi yako na n.k.
Biblia inasema kuwa katika kitabu cha Mithali 18:24, "Ajifanyiae marafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu".
Huyu ni rafiki wa pekee sana kuliko mtu yeyote na ni urafiki wa kiwango cha juu unaompa mtu huyu nafasi ya kuwa zaidi ya ndugu, anakuwa wa karibu sana na wa pekee sana zaidi ya ndugu, na huyu ni mume au mke wako, na inatokea hivi katika ndoa.
Katika hatua hii ya mahusiano kunakitu kinaitwa "A Law of Separation" (sharia ya kutengana) ambapo mwanaume anawaacha baba na mama yake pamoja na ndugu zake wote ikiwa ni pamoja na marafiki, na mwanamke vivyo hivyo anawaacha watu wa nyumbani ya baba yake pamoja na marafiki kisha wanaambatana hawa wawili wanakuwa mwili mmoja.
[11] Naye mfalme atautamani uzuri wako, maana ndiye bwana wako nawe umsujudie.
Hii ni kuhusu mwanamke au binti kutengana na watu wa nyumbani mwake, lazima awaache, ndio ili aambatane na bwana wake na kumsujudia (kumpenda). Kama hawezi kuacha hawezi kuwa katika ndoa na kama ataingia katika ndoa kabla hajaacha au hajatengana na ndugu zake lazima tu ataleta shida ndani ya ndoa.
Hii ni kwa mwanaume, naye anamwacha baba na mama yake ili aambatane na mkewe. Kwa hiyo kuwa katika ndoa ni uhusiano wa hali ya juu sana ambao unaambatana na kuacha wengine wote kisha kuambatana na yule uliyemchagua. Sasa katika unyeti mkubwa wa uhusiano wa namna hii hauwezi kuwaacha watu wa maana kwako ili kuambatana na mtu ambaye humjui vizuri, au ambaye hakupendi, itakupa shida tu tena si shida ndogo bali shida kubwa ya kukutosha na kukuzidi.
Katika kiwango hiki cha uhusiano, mtu anapaswa kumtofautisha mwenzi wake na watu wengine wote na kummpa upekee wa hali ya juu. Kama utamwona mwenzi wako na kumfananisha na watu wengine wowote katika kila kitu, basi hukupaswa kuoa au kuolewa. Na huwezi kumtofautisha na wengine kama hujawaacha hao wengine na kuambatana naye yeye tu.
Upendo pamoja na urafiki ni kiini cha mahusiano haya pia. Kwa hiyo utakuja kungundua kuwa tangu hatua au ngazi ya kwanza ya mahusiano kumetajwa upendo. Katika urafiki upendo unahusika, katika uchumba upendo unahusika, na katika ndoa upendo unahusika, kwa sababu hiyo "upendo ndicho kiini cha mahusiano katika hatua zote tatu".
UPENDO NA MAHUSIANO
Kwa kuwa upendo upendo umejitokeza katika ngazi au hatua zote za mahusiano, nitapenda kidogo tuangalie mambo kadha wa kadha kuhusu upendo ili tuwe na uelewa katika hili.
Aina Za Upendo
Kuna aina nne za upendo ambazo hujitokeza katika maisha ya mtu katika kuhusiana na watu mbalimbali. Aina hizo ni kama zilivyobainishwa na kuainishwa hapo chini:
Aina Ya Kwanza: Upendo wa Mungu (Agape)
Huu ni upendo wa Mungu, unaotokana na Mungu. Ni upendo wa pekee usiokuwa na sababu, yaanai huhitaji sababu ili kumpenda mtu, unampenda mtu kwa sababu ni mtu aliyeumbwa na Mungu na kwa sababu Mungu ni Upendo na ni amri yake kwamba kila mmoja ampende jirani yake hata kama ni adui yake.
Upendo huu ndio msingi wa upendo wa aina zote. Ndio upendo ambao unakuwezesha kumtendea mema ndugu yako hata kama amekukosea, kumtendea mema rafiki yako hata kama amekukosea, kumtendea mema mpenzi wako, mke wako, mchumba wako hata kama amekukosea, kwa sababu wenyewe hauna sababu.
Huu ndio upendo uliotajwa katika 1 Wakorintho 13 ambao una sifa na tabia zinazotufanya tuishi pamoja kwa amani na upendo hata kama tumetofautiana. Pasipo upendo huu aina nyingine za upendo haziwezi kukusaidia, maana zenyewe hupoa pale tu unapokosewa au kukwaza au kukutana na changamoto yoyote inayokufanya uache kupenda.
Aina ya Pili ya Upendo: Upendo wa kindugu (au upendano wa ndugu)
Huu ni upendo wenye sababu; unampenda mtu kwa sababu mmezaliwa na baba mmoja au mama mmoja au ukoo mmoja, au unampenda kwa sababu mnasali pamoja na kadhalika. Upendo huu ili uwe na maana ni lazima uwe ni umegubikwa na upendo wa KiMungu, kama sivyo upendo huu hupoa na kukoma pale unapokutana na changamoto, na ndio maana utasikia ndugu wamekatana mapanga kwa sababu walikuwa wanagombania shamba na kadhalika.
Aina ya Tatu ya Upendo: Upendo wa Kirafiki
Huu ni ule upendo ambao una sababu; watu wawili au zaidi wanaamua kuanzisha mahusiano ya kirafiki kwa sababu ambazo kila mmoja ameziona kutoka kwa mwenzake na amezipenda, zinaweza kuwa sababu za kimvuto wa kitabia, au silka na hulka, au kazi, au biashara na kadhalika. Pia upendo huu ili udumu ni lazima utawaliwe na upendo wa Kimungu.
Aina ya Tatu ya Upendo: Upendo wa Kimapenzi
Huu ni upendo wenye lengo la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi kati ya mwanaume na mwanamke hususani kupitia ndoa (uhusiano wa kiagano). Upendo huu pia huwa una sababu, unampenda kijana au binti kwa sababu fulani ambayo imekupendeza, inaweza kuwa ni tabia yake, au sura yake, au umbo lake na kadhalika. Katika aina hii ya upendo wawili hupendana kwa sababu ya mvuto wa kimapenzi, kila mmoja humpenda mwingine kimapenzi na kukusudia kuwa naye kama mke au mume wake katika ndoa.
Upendo ili uwe upendo halisi haupaswi kuwa na unafiki ndani yake; unapaswa kuwa ni upendo usio na unafiki kabisa. Na kiuhalisia, chanzo cha upendo usio na unafiki ni upendo wa Mungu, na kwa maana hiyo aina hizi za upendo chanzo chake inatakiwa awe Mungu, uwe ni upendo unaotiririka kutoka katika pendo la Mungu lisilo na unafiki wowote, pendo ambalo ni safi, la kweli lisilokuwa na itilafu yoyote ile (ni takatifu).
Hatua Za Upendo
Kwa mujibu wa utafiti wa kibaiolojia alioufanya mwana-anthropolojia Profesa Hellen Fisher alibaini kuwa kuna hatua tatu ya upendo wa kimapenzi ambao mtu anapitia, na hii ni kutokana na jinsi mwili wake unavyofanya kazi kupitia homoni alizonazo katika mwili wake zinazotawaliwa na ubongo wake na kusafilishwa mwilini mwake.
Katika utafiti wake alisema kuwa mtu anapitia hatua tatu muhimu katika tendo lake la kupenda na katika kila hatua kuna homoni ambazo huhusika kubadilisha hali na hisia anazozisikia katika mwili wake. Aidha hatua hizo ni pamoja na tamaa (lust), mivuto au mvuto (attractions), na mwambato (attachment). Kemikali katika ubongo ndio husimamia onyesho hili la kupenda (falling in love) kutoka hatua moja hadi hatua nyingine ndani ya vipindi tofauti tofauti.
Tamaa (lust)
Katika hatua hii ya tamaa mtu hujisikia kuvutiwa au kuvutika kutokana na mihemko ya vitu vinavyoamsha tamaa yake ya mwili. Hujisikia kama vile anahitaji mtu wa kumtongoza au mtu wa kutongoza ilimradi tu awe karibu na jinsia ambayo ni tofauti na yake ambaye atashirikiana naye siku moja katika tendo la ndoa. Katika hatua hii ni mvuto wa awali wa kimapenzi unaochochewa sana na hamu ya kufanya ngono.
Katika hatua hii, homoni ambazo husababisha mtu ajisikia hivyo, huwa ni za aina mbili, kwa upande wa wanaume huwa ni homoni aina ya ‘testosterone’ na kwa upande wa wanawake huwa ni homoni aina ya ‘estrogen’.
Homoni hizi kwa upande wa wanaume humfanya mwanaume katika nyakati fulani toka vipindi hadi vipindi ajisikie ile hali au hamu au tamaa ya kutaka kukutana kimwili na mwanamke au kuwa karibu na mwanamke ili aweze kukutana naye kimwili. Na kwa upande wa mwanamke pia homoni hizo humfanya vipindi kwa vipindi ajisikie hamu ya kuwa karibu na mwanaume na kutaka kukutana naye kimwili japo kwa wanawake sio sana ukilinganisha na kwa upande wa wanaume.
Katika mazingira haya ndipo unaweza ukamkuta kijana anaamua kuwa anajichua ili ajiridhishwe yeye mwenyewe na mwanamke pia naye akizidiwa na hali hiyo na hana mwanaume wa kukutana naye hujichua ili ajiridhishe yeye mwenyewe. Kumbuka kujichua ni dhambi ya uasherati, kama huwa unafanya acha mara moja.
Muhimu sana: Hali hii ya tamaa inaposhindwa kutawalika bila shaka inakuwa na uchochezi wa kimapepo ndani ya fikira na mwili wa mtu husika. Kama ni ya kawaida, basi inaweza kutawalika, mtu anaweza kuitawala na kujizuia kabisa.
Hii ni tamaa na si upendo, ni hali ya kawaida kabisa kutokea pinti tu mtu anapofikia hatua ya kubale na kuvunja ungo na kuanza kuona anahitaji kuwa karibu na mwanaume au mwanamke. Kuanzisha mahusiano ya kimapenzi kwa misingi ya kitamaa ni hatari sana kwa sababu tamaa huisha kwa kadili inavyotimizwa tofauti na upendo wenyewe. Kwa hiyo hatua hii ya kihisia isitumike kuanzisha mahusiano ya ndoa kwa sababu anachokuwa nakisikia mtu sio upendo ni mihemuko tu ya kihisia inayosababihswa na homoni katika mwili wake.
Kwa hiyo vijana wengi wamejikuta wakianzisha mahusiano kwa misingi ya tamaa na ndio maana kumekuwa na kesi nyingi za wadada kulalamika kuachwa na kuumizwa na wakaka kulalamika kuachwa na kuumizwa. Siku nyingine tutaelezea kwa kina kuhusu kipengele hiki cha tamaa.
Hatua ya Pili: Mivuto (Attractions)
Katika hatua ya pili ni pale ambapo unaanza kumwona mtu anayekuvutia, kwa kaka unamwona dada anayekuvutia katika vitu vile vilivyoshika akili yako, na mdada hivyo hivyo. Hapa ndipo pale unapoanza kumwazia na kutengeneza picha namna utakavyokuwa pamoja naye, namna atakavyokuwa anakujali na kukupenda, namna utakavyokuwa nae kitandani ukivinjali naye na kadhalika.
Katika hauta hii mtu huwa kama ameathiliwa na madawa ya kulevya katika ubongo wake, hawezi kula bila kumwona, hawezi kulala bila kumwona au hata kusikia sauti yake. Akimwona tu kwa mbali anakuja, mapigo ya moyo yanaanza kwenda mbio, mwili unasisimuka, akili inahama, kama alikuwa anasoma basi hawezi tena kusoma, kama alikuwa anapika basi atashindwa hata kupika. Yaani mkaka wa watu amekufa ameoza, na kama ni mdada amezimia na akazimika ile mbayaa, huwezi kumwambia lolote, hata kama utamwambia ubaya wa huyo wa tabia zake ataona unamsingizia tu au unamuonea wivu au humtakii mema, tayari kaishalewa mapenzi.
Katika hatua hii kemikali tatu uhusika katika kusababisha hali hii ambazo ni pamoja na ‘norepinephrine’, ‘dopamine’, na ‘serotonin’.
Dopamine;
Dopamine inayoongezeka mwilini ikiachiliwa na ubongu husababisha msukumo au muhamasisho (motivation), msukumo wa kufukuzia au kutaka kupata kile ambacho umekitamani ili kukidhi haja yako au matamanio yako. Homoni hizo humtengenezea mtu hali ndani ya kuona ana maneno mengi ya kumwambia, humtengenezea shahuku ya kutaka kumwambia yule mtu anayeamini ni maalumu kwake maneno mazuri ikiwa ni pamoja na namna anavyojisikia, kwa mfano Ebitoke kwa Ben Pal, alikuwa katika hatua hii, lakini baada ya kuwa katika mahusiano, badala ya mambo kuwa mazuri, yaliharibika, kwa nini, kwa sababu hakikuwa kitu halisi chenye msingi wa kuutegemea, ni swala la hisia tu zinazotengenezwa na homoni katika mwili kutokana na mambo yale uliyoyapokea katika akili (ubongo) yako kumuhusu mtu ambaye amekuvutia.
Norepinephrine;
Hii ni homoni inayohusika na ongezeko la nguvu katika hali ya msisimko na mapigo ya moyo mtu anayoyasikia pindi anapomwona yule aliyemvutia, pia kupotea kwa hamu ya chakula na usingizi pale unapoona bado hujafanikiwa kumpata yule aliyeubamba sijui ni moyo wako au hisia zako. Homoni hizi zinakufanya uwe tayari kufanya jambo lolote lile ili umpate huyoo aliyekuvutia.
Serotonin;
Hizi ni homoni ambazo humfanya mtu aonekane kana kwamba amepungukiwa na akili inapofika katika swala la yule aliyevutiwa naye.
Hata hivyo, katika hatua hii bado sio upendo, ni mihemuko na misisimko ambayo huja kuisha baada ya kipindi fulani na hasa baada ya kumpata huyo na kukidhi tamaa uliyonayo. Kwa sababu bado hali hii sio upendo na haina maana kuwa ndio unampenda huyo mtu, basi si vyema kuanzisha mahusiano na mtu huyo wakati wa hatua hii ya kihisia ambayo imeitwa ni hatua ya upendo. Ni vyema ukajizui, ukasubiri mpaka kipindi ambacho utakuwa sawa katika hali ya kawaida ambayo unaweza kufanya maamuzi ya kumpenda mtu baada ya kufanya uchaguzi wa kumpenda kutokana na mazingira halisi yaliyokupelekea wewe uone kuwa mtu huyo anafaa kuwa mwenzi wako wa maisha na si swala la mihemko na misisimko ya kihisia tu na tamaa za mwili.
Hatua Ya Tatu: Mwambatano (Attraction)
Hapa ni pale ambapo tamaa na mihemko yote ya kihisia inapokuwa imeisha na hatimaye kugundua kwamba ni kweli si mihemko tu ya kihisia ila unampenda hakika, na hapa mtu huwa na hali ile ya kujitoa kwa ajili ya mwenzi wake katika kumpenda huku akiwa anaangalia sana tabia zake kama msingi wa kuanzisha mahusiano yake na huwa tayari kabisa kumuoa au kuolewa naye.
Katika hatu hii ya upendo, homoni kama vile dopamine hupungua na hatua ya mvuto au mivuto (attractions) hupungua kwa kiwango kikubwa sana, na homoni aina ya ‘hormonesoxytocin’ na ‘vasopressin', huchukua nafasi ambazo uhusiana na hali ya kutaka kuambatana pamoja kama mke na mume, kumjali na kumtunza au kuwajibika kwa ajili ya mwenzi wako. Hapa upendo wa kweli wa kimapenzi huzaliwa.
Katika kumalizia utangulizi wangu katika somo hili nikiweka msingi, naomba ieleweke kuwa hatua mbili za kwanza za upendo huu wa kimapenzi huwa si hatua za kuamini sana kwani shetani pia huzitumia hali hizo kuharibu mioyo ya watu. Unaingia katika mahusiano kwa kigezo cha tamaa yako ya mwili, mihemko na mivuto ya nje, lakini jua hiyo huisha, na itakapoisha kwa mawanamke huyo au mwanaume huyo na yeye kumbe amekupenda kweli na unataka kumwacha, unadhani ataumia kiasi gani?
Ni vizuri kabla hujafanya maamuzi yoyote ujipambanue vyema, usije ukaanzisha mahusiano ukidhani unampenda kumbe ni kazi ya homini mwilini mwako katika kuhitikia tamaa zako za mwili na mihemuko na misisimko uliyoipata baada tu ya kumuona mtu aliyekuvutia, na mwisho wa siku ukajeruhi moyo wa mtu. Kijana lazima uwe na uwezo wa kujizuia, binti lazima uwe na uwezo wa kujizui. Kufanya hivyo unajiweka katika nafasi nzuri na unamweka huyo mwingine katika nafasi nzuri pia.
Hii ndio sababu ni muhimu sana unapokuwa hata na wazo la kuwa kwenye mahusiano na mtu fulani na hasa yule ambaye umemuona kwa mara ya kwanza na fikira za kuingia naye kwenye mahusiano zikakujia, au yule ambaye ulikuwa unamwona kila siku lakini ghafula wazo la kutaka kuwa naye kwenye mahusiano likakujia pengine labda ameanza kuwa mrembo au maridadi tofauti na mwanzo, kabla ya kumtamkia au kumkubalia kuingia naye kwenye mahusiano ukajipa muda kwanza wa kutosha tu ili kupima kama kweli unachokisikia ni kitu halisi, kama kweli wazo lako ni halisi au ni mihemuko, misisimko na tamaa za mwili tu. Vijana tusiwe na haraka ya kuingia kwenye mahusiano, tujitafakari kwanza na kujipima, ndipo tufanye maamuzi ya kuingia au kutokuingia.
MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA KUAZISHA MAHUSIANO SAHIHI YANAYOFIKIA MALENGO.
Sasa baada ya kuangalia mambo ya msingi katika utangulizi wa somo letu yatakayotusaidia kuelewa hoja yetu ya somo letu, sasa tunaanza kuangalia kiini cha somo letu hili.
Yapo mambo ya muhimu sana ambayo wewe kama kijana wa kiume na wa kike ambayo hunapaswa kuyazingatia sana katika kuanzisha mahusiano sahihi yanayofikia malengo. Kama tulivyokwisha kuona hapo awali kwamba, mahusiano ya uchumba hadi ndoa lengo lake ni mwanaume na mwanamke hawa kuoana na kuishi pamoja kama mke na mume. Mambo yafatayo yatawasaidia kuanzisha mahusiano sahihi yanayotimiza lengo.
Jambo La Kwanza: Maarifa ya Ujumla (au katika Ujumla)
Kabla ya jambo lolote unahitaji maarifa kwanza katika jambo lile unalotaka kufanya katika maisha yako. Kwa kuwa mahusiano ni jambo la muhimu sana kwako, unahitaji maarifa ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufaulu kimahusiano.
Maarifa kuhusu Saiklojia ya Mwanaume na ya Mwanamke
Ninaposema maarifa ya ujumla nina maana maarifa kuhusiana na Saiklojia ya mwanaume na Saiklojia ya mwanamke: hawa wawili ni wanadamu walioumbwa tofauti, wanaotofautiana katika mambo mengi sana, lakini tofauti zao hizo ndizo zinazowafanya wafaane na kuwawezesha kuishi pamoja kama kila mmoja atafahamu Saiklojia ya mwenzake.
Kwa hiyo, kama wewe ni mwanaume, unahitaji kuwajua wanawake wakoje kitabia na namna walivyoumbwa na kuwekewa tabia ambazo zinatofautiana na zile za wanaume. Lakini pia licha ya kuwaelewa na kuwafahamu wanawake, unapaswa pia uwafahamu wanaume wameumbwaje na wana tabia gani na wewe ukiwa mmoja wao.
Kwa upande wa mwanamke pia, wewe kama mwanamke licha ya kuwafahamu wanawake wameumbwaje ikiwa ni pamoja na wewe, unapaswa kuifahamu saiklojia ya wanaume ili kujiweka katika nafasi ya kuishi na hao wanaume katika hali ya amani na utulivu.
Maarifa kuhusu ndoa:
Lakini pia kwa upande mwingine si vyema kabisa ukakosa maarifa kuhusiana na ndoa yenyewe. Kuingia kwenye ndoa wakati hujui ndoa ni nini ni makosa na unajiandaa kuwa na mahusiano mabaya. Ndoa si tendo la ndoa na tendo la ndoa si ndoa, ndoa ni zaidi ya tendo la ndoa ni taasisi pana sana inayohitaji maarifa ya kutosha ili kujiweka katika nafasi ya kufaulu kimahusiano.
Kwa hiyo mpendwa unahitaji maarifa sana, na ndio maana mwandishi wa Mithali 19:2 akiwa anaona umuhimu wa maarifa anaandika na kusema, “Tena si vizuri nafsi ya mtu ikose maarifa; naye afanyaye haraka kwa miguu hutenda dhambi”
Kukosa maarifa sahihi kunampelekea mtu kufanya haraka ya kutenda dhambi kwa kuingia katika maamuzi yasiyo sahihi. Kukosa maarifa ni jambo baya sana kwa sababu linakukosesha na linakufanya uumize watu wengine wanao husiana na wewe katika maisha ya kila siku.
Usifanye haraka kuingia katika ndoa bila ya kuwa na maarifa kukuhusu wewe, kumuhusu mtu unayetaka kuingia naye katika mahusiano, na kuhusu mahusiano yenyewe hususani ndoa. Kufanya haraka kuingia pasipo kuwa na maarifa ni kujiweka katika nafasi ya kutenda dhambi, na hii ndio sababu sio vizuri nafsi ya mtu ikose kuwa na maarifa.
Jambo la Pili: _Maombi (Mshirikishe Mungu)
Kwa akili zako huwezi kumtambua mwenzi anayekufaa, unamuhitaji Mungu, badala ya kuzitegemea akili zako mwenyewe, mshirikishe Mungu kwa njia ya maombi. Mithali 16:3, anasema kuwa, “Mkabidhi Bwana kazi zako, na mawazo yako yatathibitika.” Kama unataka mawazo yako yathibitike jifunze kumkabidhi Bwana kazi zako zote.
Katika kitabu cha Luka 6:12 – 13 inasema, “Ikawa siku zile aliondoka akaenda milimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita mitume.”
Yesu alikuwa na aina mbili za watu aliohusiana nao kabla hajachagua mitume kumi na mbili; makutano na wanafunzi wake ambao ndio walikuwa marafiki zake. Lakini wakati huo huo alitaka kuanzisha mahusino na watu 12 ambao atawahita mitume na ambao atafanya nao kazi bega kwa bega, watakaokuwa karibu naye zaidi, atakaoambatana nao kwa kuwa na mahusiano ya karibu zaidi kulinko wengine wote.
Yesu hakuchagua tu wale 12 kwa kuzingatia hisia zake, ijapokuwa walikuwa ni miongozi mwa wanafunzi wake mwenye uhusiano nao wa kirafiki (maana aliwaita rafiki zake) ilimbidi aingie kwenye maombi usiku kucha. Katika maombi hayo Mungu alianza kuweka msukumo ndani yake wa kuwachagua baadhi ya watu miongoni mwa wanafunzi wake atakaowaita mitume ambao wataambatana naye katika kufanya kazi ya Mungu. Maombi yalimfanya awajue watu sahihi ambao wataambatana naye.
Kwa hiyo, unahitaji maombi kumjua mtu sahihi ambaye ni mwambata wako. Kila unapohitaji mwambata unatakiwa kuingia kwenye maombi ili kumjua yule mtu sahihi. Wanafunzi walikuwepo wengi, lakini kwa nini Yesu aliwchagua hao kumi na mbili na si wengine? Na kwa nini alikwenda kuomba? Kwa sababu alihitaji kujua watu sahihi wanaomfaa, ambao ataambatana nao katika maisha yake yote ya hapa duniani katika kutenda kazi ya Mungu na kutimiliza kusudi la Mungu. Hauchagui yeyote tu ilimradi ni mwanaume au mwanamke, wala hauchagui yeyote tu ilimradi ana imani moja na wewe, au ni kabila moja na wewe, au ni miongoni mwa rafiki zako, unachagua kwa sababu unajua ni mtu sahihi kwako na maombi yanakupa kujua na yanakupa uhakika.
Kitu cha msingi ambacho unapaswa ukielewe ni kwamba, pamoja na kuwa Yesu alimwomba Mungu na Mungu akampa akina Petro na akina Yuda wawe waambata wake, hakumpa watu wakamilifu bali alimpa watu sahihi watakaomfaa katika kutimiza kusudi la Mungu.
Maombi hayamfanyi Mungu akupe mkamilifu bali yanamfanya Mungu akupe mtu sahihi. Mtu sahihi si mtu mkamilifu, ni mtu mwenye mapungufu mengi katika maisha yake. Mapungufu yake hayamfanye asiwe mtu sahihi kwako ilo ni jambo la msingi sana kulielewa. Kama unatafuta mtu mkamilifu hapa duniani jua kabisa hautakuja kumpata huyo mtu mkamilifu kabisa. Akina Petro wote na wenzake walikuwa na mapungufu mengi tu lakini Yesu aliwachukulia na kuwapa huduma zote. Kuna wakati aliwaosha miguu yao pamoja na mapungufu yao, aliwafanyia mengi mazuri hata kama alijua kuna wengine watamkana na wengine watamsaliti, aliwapenda upeo na upendo wake ulisitiri wingi wao wa makosa.
Mwombe Mungu, hatakupa mtu mkamilifu, ila atakupa mtu anayekufaa, na katika kuishi kwenu mtaendelea kukamilishana ninyi kwa ninyi kwa sababu Biblia inasema kuwa “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.” Kwa hiyo hauhitaji mtu mkamilifu wa kuishi naye, bali unahitaji mtu anayekufaa wa kuishi naye, na huyo anayekufaa ndiye wa kufanana na wewe na anatoka kwa Mungu na unampata kwa njia ya maombi. Kama vile Mungu alivyompa Yesu kujua moyoni ni akina nani wanamfaa ndivyo atakupa na wewe kujua moyoni ni nani anakufaa kuwa mwenzi wako wa maisha.
Nipende kuweka msisitizo kuwa, Yesu hakuona maono, wala hakuota ndoto, na wala hatuoni sehemu iliyoandikwa kuwa alisikia sauti ikimwambia kuwa awachague hao aliowachagua, hapana. Kilichofanyika akiwa anaomba, ni wazo tu lilikuja ndani yake na uhakika wa wazo hilo kwamba ni halisi; alipata kujua tu moyoni ni akina nani miongoni mwa wanafunzi wake wanafaa kuwa mitume, na uhakika huu aliupata kwenye maombi.
Kwa hiyo, hauombi ili uone maono, uote ndoto, au usikie sauti ikikwambia kuwa fulani ndiye, hapana, unaomba ili upate kujua moyoni na kuwa na uhakika kuwa ni nani anakufaa; wazo tu litakuja katika mazingira ya kawaida kabisa, tena na wakati mwingine ya kulinganisha na kutofautisha mambo katika mazingira unayoyaona kila siku. Ni katika mazingira ya watu wale wale unaoishi nao kila siku, unawafahamu na kuzijua tabia zao na maisha yao ya kila siku, ndipo wazo huja moyoni, na si vinginevyo.
Yesu aliishi na watu hawa kila siku, alijua maisha yao, alijua tabia zao, kupata uhakika moyoni na kujua ni akina nani wa kuambatana naye aliomba, na baada ya maombi aliwachagua, hii maana yake moyoni mwake aliona kabisa fulani na fulani watanifaa.
MAOMBI NA VIGEZO UNAVYOWEZA KUJIWEKEA
Watu wengi huwa na picha za watu wawapendao katika akili zao, hujiwekea vigezo vya watu wawatakao, na wanapomwomba Mungu huweka vigezo ambavyo vitawasaidia kumtambua mtu sahihi wanayemwomba kwa Mungu. Hii ni sawa kabisa wala sio kosa, lakini tatizo tulilonalo sasa kwa watu wengi wanajiwekea zaidi vigezo vya nje ambavyo si vya msingi katika kujenga mahusiano sahihi na yanayomfanya mtu kufikia malengo.
Tujifunze Kwa Isaka na Rebeka
Yule mtumishi wa Ibrahimu alipotumwa kwenda kumtafutia Isaka Mchumba, pamoja naye aliondoka na ngamia 10 hivi kwenda safali ambayo ilikuwa na umbali wa maili 500 hivi. Baada ya siku kadhaa alifika katika nchi aliyoagizwa na Ibrahimu kwamba amchukulie mwanae Isaka mke huko.
Alipofika , aliwakalisha punda wake chini kisha akamwomba Mungu na kusema, “Ee Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi, yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia, basi na huyu awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka, na kwa hayo nitajua kuwa umemfadhili bawana wangu” (Mwanzo 24: 10 – 27)
Hayo ndiyo yalikuwa maombi ya mtumishi wa Ibrahimu ya kumwomba Mungu mke kwa ajili ya Isaka. Vigezo alivyoweka katika maombi yake si vigezo vya nje (yaani vya sura, umbo, tabia, au mwonekano) bali ni vigezo vya ndani vinavyomtambulisha mtu ambavyo ni tabia. Mtu (mume au mke) hatambulikani kwa sura yake bali kwa tabia yake.
Mtumishi aliweka mashariti magumu sana katika maombi yake, si magumu kwa Mungu ila magumu kuyapata kwa mwanamke. Jamaa alikuwa na ngamia 10 na ngamia mmoja kila baada ya dakika 13 hivi anakunywa maji lita 135 ambazo ni sawa na ndoo za maji 7 za lita ishirini. Na kama ngamia hajanywa maji kwa kipindi kirefu hunywa takiribani kuanzia ndoo 20 hivi. Sasa piga hesabu, jamaa ana ngamia 10, je Rebeka alichota ndoo ngapi?
Lakini pia mazingira ya visima vyao hayakuwa rafiki sana, kwani vilikuwa ni visima virefu sana, aidha mtu alipaswa kuchota kwa kutumia kamba, au kutelemka mpaka chini kwa ngazi. Jamaa alikaa pembeni akimwangalia, sio kwamba alikuwa anamsaidia, alikaa pembeni tu akimsoma. Na baada ya kumaliza ndipo alithibitisha kuwa Rebeka ndiye na ndipo alipomwambia.
Baada ya maombi kuna kipindi cha kusubiri, lakini ukiwa mahali sahihi ambapo watu huja, si ukiwa chumbani au mafichoni mahali ambapo watu hawapatikani. Haikuwa kazi rahisi kwa mtumishi wa Ibrahimu kutembea maili 500, na haikuwa rahisi kwa Rebeka kuwanywesha wale ngamia. Tendo lile liloonyesha uzuri na ubora wa tabia yake.
Vipimo havipaswi kuangaliwa au kuwekwa katika mambo ya nje ambayo ni uzuri wa sura, umbo, mali, pesa na kadhalika, bali vigezo au vipimo vinapaswa viwekwe katika mambo ya ndani yanayojenga na kuonyesha tabia ya mtu. Vigezo vya mtumishi huyu wa Ibrahimu vilikuwa vinaidhihirisha tabia ya Rebeka machoni pake, kama angelikuwa ni mwovu asiye na tabia njema asingelichota maji na kuwanywesha ngamia pamoja na mtumishi yule. Kwa hiyo unapojiwekea vigezo zingatia sana jambo hili.
Muhimu sana: Ni muhimu tukajua mazingira ya mtumishi huyu wa Ibrahimu ya kumtafuta mke na kwa nini aliweka vigezo. Mazingira haya yalikuwa kwake ni mageni, na watu pia walikuwa ni wageni, na jambo lake lilikuwa ni la haraka, kwa hiyo hasingeliweza kujua yupi mwenye tabia nzuri na yupi mwenye tabia mbaya na ndio maana aliweka vigezo vigumu sana kutambua hivyo. Hii maana yake ni kwamba, vigezo unavyoviweka ili kumpata mwenzi wa maisha ni muhimu pale unapokwenda kumtafuta mwenzi huyo kwa watu usiowajua, na si vya muhimu kuviweka na kuvitumia kwa watu unaowajua au unaoishi nao, kwa sababu ni lazima tu utakuwa unajua ni nani mwenye tabia njema na ni nani mwenye tabia mbaya.
Katika mazingira ambayo watu unawafahamu na unaishi nao kila siku, jambo kubwa la kufanya, ni wewe kumwomba Mungu kuwa mapenzi yake yatimilike, na akupe kujua moyoni kati ya hao wenye tabia njema ni nani ni mtu sahihi kwako, achana na mambo ya kuweka vigezo wakati watu wenyewe unawajua labda kama unataka kuolewa na mtu wa nje ya jamii unayoishi usiyemjua, sasa na hapo ipo kazi, lazima uwe vizuri kiroho na ujifunze kusubiri katika uvumilivu. Mimi naona kuwa hakuna sababu ya kufanya hivyo wakati wapo watu unaowafahamu kabisa.
Jambo la Tatu: Fanya Maamuzi kabla hujaingia Kwenye mahusiano
Hakuna mahusiano yasiyokuwa na changamoto, na kama nilivyotangulia kusema kuwa, Mungu hakupi mtu mkamilifu ila anakupa mtu wa kufanana nawe atakayekuafaa katika maisha yako yote, mtu sahihi, hii haina maana kuwa amekamilika na kwa sababu hiyo hana mapungufu na hawezi kukosea.
Fanya maamuzi ya kutorudi nyuma na kuvunja agano kabla ya kuingia katika mahusiano;
Kwa hiyo mtu huyu pamoja na kuwa anaweza akakufaa, bado anaweza akawa ana mapungufu mengi tu. Kwa hiyo, wewe unapaswa kufanya maamuzi kabla ya kuingia katika mahusiano, na maamuzi hayo ni wewe kukusudia kumpenda (kwa upendo wa Agape) huyo ambaye utakuwa unatarajia kuwa naye katika mahusiano, pia fanya maamuzi ya kutokurudi nyuma ukiisha ingia katika mahusiano, na kwa sababu hiyo ndio maana unatakiwa uwe na uhakika kuwa unayetaka kumuoa au kuolewa naye ni mtu sahihi kwako.
Makosa yatakuwepo mengi, fanya maamuzi ya kumsamehe hata kabla hajakukosea, msamehe in advance ili atakapokuja kukukosea iwe rahisi wewe kumsamehe. Kwa hiyo, unapaswa kufanya maamuzi ya kuwa katika ndoa na kutimiliza kanuni zote za ndoa na kuwajibika kwazo. Maamuzi ya kulitunza agano la ndoa kwa gharama yoyote, maamuzi ya kutokuvunja uchumba kwa sababu yoyote ile; hii itakusaidia kuwa makini wakati wa kuchagua mwenzi wa maisha.
Pamoja na kuwa ndoa chanzo chake ni rohoni lakini pia ni ya kimwili kabisa, na kwa hiyo inaendeshwa kwa kanuni za pande zote mbili, za kiroho na za kimwili, siku nyingine nitaeleza hili kwa undani. Kanuni hizi ili wewe uweze kuzitekeleza ni lazima ukusudie moyoni, na huwezi ukakusudia kama hujafanya maamuzi thabiti.
Kusudia kujitoa kwa ajili ya mwenzako na kumtanguliza, kusudia kumlinda, kusudia kumthamini, kusudia kumvumilia, kusudia kuchukuliana naye katika udhaifu wake, na kusudia kukabiliana na changamoto za mambo yale yasiyotarajiwa, kwa hiyo utarajie yasiyotarajiwa kwa sababu huyo mwenzi wako yuko zaidi ya vile utakavyokuwa ukimfahamu. Katika kumsoma kote utangundua tu zile tabia za msingi, lakini vile viudhaifu vidogo vidogo utavijua kwa kadili utakavyokuwa unamsogelea ndani ya ndoa. Vitu vidogo huonekana kirahisi kwa kadiri unavyovisogelea na ndivyo ulivyo udhaifu wa mwenzi wako ulio mdogo na wa ndani zaidi ambao kujidhihirisha kwake ni mpaka muwe karibu sana.
Jambo la Nne: Mjue anayekuoa au unayemuoa kwanza kabla hujamwambia
Katika jambo la kwanza tuliangalia maarifa kwa ujumla, na tulijikita katika kuijua saikloajia ya mwanaume na saiklojia ya mwanamke, lakini hapa tunajikita katika kumfahamu moja kwa moja mtu yule ambaye unaolewa naye au unamuoa.
Ukiisha ijua saiklojia ya mwanaume au ya mwanamke kwa ujumla wake, jambo linalofuta ni kumjua yule ambaye unataka kumuoa au kuolewa naye. Usiolewe na mtu usiyemjua hata kama unaijua saiklojia ya wanaume, huko ni kujua kiujumla tu, nenda mbali na hapo, tweka mpaka kilindini, jifunze kumjua yule anayetaka kukuoa au unayetaka kumuoa. Mjue yeye na tabia zake binafsi (hizi ni tabia zaidi ya zile za kiujumla, ni tabia binafsi za mtu), ijue imani yake, jua kule anakotoka kwa maana ya familia yake, ijue kazi yake, kwa ujumla mjue yeye na kila kitu kinachomuhusu yeye.
Usiingie kwenye uchumba na mtu usiyemjua kwani huku ni kuingia kwenye ndoa na mtu usiyemjua, na kwa sababu uchumba haupendezi kuwa ni wa muda mrefu kwa sababu ni maandalizi ya mwisho ya pamoja yanayowaandaa kuingia kwenye ndoa, hupaswi kuingia kwenye mahusiano hayo na usiyemjua vyema. Hakikisha unaingia kwenye uchumba na mtu unayemjua kwa usalama wako mwenyewe.
Inaweza ikawa mtu anayekuchumbia ulikuwa unafahamiana naye kabla, na uliishi naye lakini ikatokea mkaachana labda kwa muda wa mwaka mmoja au zaidi bila mawasiliano kabisa, miaka miwili baadaye au mitatua na kuendelea mnakuja kukutana, na anakutaka uingie naye kwenye mahusiano, hiyo ni hatari sana. Mtu huweza kubadilika kwa siku chache tu akawa mtu mwingine kabisa, kwa hiyo nashauri kwamba, hata kama ulimjua siku za nyuma, anza naye kwanza kwa ngazi ya urafiki, ukijiridhisha ndipo uingie naye kwenye uchumba na hatimaye ndoa. Kataa ndoa au chumba za haraka haraka huwa zina agenda za siri ndani yake, na ukiisha kuingia ni ngumu kutoka.
Jamani ndoa ni agano ambalo halivunjwi na mwanadamu ikiwa ni pamoja na wewe ukiisha ingia katika agano hilo. Ni agano la milele, kwa hiyo usijaribishe na wala usiingie pasipokuwa na maarifa sahihi. Jipambanue, jihakikishe, mpambanue, mwakikishe, kisha ndipo uingie ukiwa huna hofu wala mashaka wala wasiwasi, na uingie ukijua hakuna kugeuka nyuma wala kughairi, ukiisha mtamkia tu, wewe umemaliza maana Mungu anachukia kuachana. Barikiwa sana.
Jambo la tano: Hakikisha kuwa unampenda naye anakupenda
Uhusiano wowote na hasa wa ndoa haujengwi na upendo wa upande mmoja tu, unajengwa na unakuwa na maana iwapo upendo utakuwa wa pande zote. Unaweza ukawa wewe unampenda lakini yeye akawa hakupendi, na inaweza ikawa yeye anakupenda lakini wewe humpendi; kwa hiyo akakubalia kwa sababu anakuonea huruma, au kuna sababu nyingine nje ya upendo zinazomsukuma kufanya hivyo, au ukamkubalia kwa sababu unamuhurumia au kuna sababu nyingine nje ya upendo ambazo zinakufanya uwe naye; hii ni kuhatarisha maisha yako na ya mwenzi wako kwa sababu ndoa itagubikwa na maumivu ya kihisia, migogoro isiyoisha na mambo mengi yasiyokuwa mazuri na mema kwa pande zote mbili.
Usiingie kwenye mahusiano na mtu ambaye hujui kama kweli anakupenda, ni kujiweka hatarini kuwa na mahusiano yasiyo sahihi ambayo yatakupotezea muda na kukuachia jeraha za moyo ambazo itakuwa ngumu kufutika akilini mwako.
Hata kama wewe unampenda kiasi gani, usijiaminishe kuwa kupitia wewe kumwonyesha upendo basi atabadilika na kuanza kukupenda, hapo utakuwa unajidanganya na kwa upande mwingine utakuwa unajiumiza wewe mwenyewe.
Katika swala la mahusiano ya ndoa, hakikisha unampenda anayekupenda kwa sababu msingi wa mahusiano haya ni upendo toka pande mbili zote na si upendo kutoka upande mmoja. Ni muhimu sana ukalijua hili mapema sana.
Mungu akubariki sana.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS