MWANAUME: KAA NA MKE WAKO KWA AKILI

0
6كيلو بايت

KWELI KUU: Mwanaume mwenye akili akishindwa kukaa na mke wake ni kwa sababu amekosa akili.

1Petro 3:7

Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa heshima, kama chombo kisicho na nguvu; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.


UTANGULIZI:
Ndoa ni taasisi ambayo Mungu mwenyewe aliianzisha kwa kusudi la kuwa na familia bora zinazomwabudu yeye siku zote mbele za uwepo wake. Ndoa ikiharibika ni vigumu sana wana ndoa kuwa na mahusiano mazuri na Mungu, lakini pia na watu na hivyo kuwa katika nafasi ngumu ya kufurahia maisha yao. Ukweli ni kwamba ndoa haina tatizo lolote, na wala haina ubaya wowote, kama kuna tatizo au ubaya basi upo kwa wanandoa wenyewe na si katika ndoa. Ndoa ni njema, na wanandoa wakitaka kuifurahia ndoa yao ni lazima kabisa wao wenyewe wajue namna ya kuondoa matatizo au ubaya uliopo katikati yao wote wawili. Ndoa haiwezi kuwa mbaya kwa wao kuwa wabaya, na ndio maana kuna wengine wanafurahia ndoa zao wakati wengine hawafurahii kabisa ndoa zao. Hii ni kutokana na kuwa, si ndoa iliyo na ubaya au tatizo bali ni wanandoa ndio wenye tatizo, anaweza kuwa mmoja au wote wawili. Wakati wao wanatofautiana, wanagombana, wanapigana, na kuchukiana kwa sababu ya matatizo yao au ubaya ulipo kati yao, ndoa yao ipo inawasubiri wamalize tofauti zao ili waweze kuishi kwa furaha ndani ya ndoa yao hiyo ambayo ni baraka kwao, kwa Mungu, na kwa watu wanaowazunguka.

Kwa sababu hiyo, wanandoa wawili (mke na mume) wakitaka kufurahia ndoa yao ni lazima wajifunze wkufurahiana wao wenyewe, kuchukuliana, kukabiliana na changamoto zinazowakabili kwa (au katika hali ya) upendo, kupendana, kunyenyekeana, kusameheana, kuthaminiana, kuvumiliana, kuaminiana, kushirikiana pamoja na kuombeana. Wao wote kwa pamoja ni lazima wajifunze kukabiliana na changamoto zinazowakabili bila kulaumiana, kunung'unikiana wala kushindana katika jambo lolote. Ni lazima wajifunze kukubaliana katika yale mambo ambayo wanatofautiana, kumuhusisha Mungu katika kila jambo la maisha yao na yawengine. Pia kila mtu asiwe na lengo tofauti na ndoa yao, kila mmoja ndoto yake iwe ni ndoa yake nzuri anayoifurahia kwa kumfurahisha kwa upendo mwenzi wake wa ndoa. Mambo yote haya yanahitaji wote wawili kila mmoja ajitoe (commitment) na kuchiachilia (submission) si kwa mwenzi wake tu lakini kwanza kwa ndoa yao. Kila mmoja apanie kuifurahia ndoa yake kwa kutekeleza wajibu wake na majukumu yake anayopaswa kutekeleza kwa mwenzi wake ndani ya ndoa. Licha ya wanandoa kupendana wao kwa wao, pia wanandoa waipende ndoa yao kwanza, na wote wawili wajitolee kuitunza na kuihifadhi ndoa yao kwa gharama zozote zile isije ikavunjika kwa sababu yoyote ile.

Katika somo langu leo, napenda nijikite kwa upande wa mume hususani katika swala la kuishi na mke wake kwa akili. Katika somo hili tutaangalia nini maana ya mume kukaa na mke wake kwa akili, namna ya kukaa na mke wake kwa akili, na mambo yanayoweza kupelekea mume asikae na mke wake kwa akili. Labda nikwambie kuwa, mume mwenye akili akikosa akili hawezi kuishi na mke wake kabisa. Kwa nini? Kwa sababu hana hakili zinazomuwezesha yeye kuishi na mkewe. Akili hizo ni zipi? Fuatana nami katika somo hili mpaka mwisho.

MUME KAA NA MKE WAKO KWA AKILI:
Ni nini maana ya akili zilizotajwa katika kitabu cha 1Petro 3:7?

Ukiangalia tafsiri ya Kiingereza ya King James Version utaona neno lililotumika kutaja akili ni neno Knowledge lenye maana ya maarifa kwa lugha ya Kiswahili. Kwa sabubu hiyo, akili zinazotajwa hapa si akili zile za kuzaliwa, au akili zile za shule ya msingi, kitato au chuo, hizi ni akili nyingine kabisa. Akili zako za kuzaliwa tu bila akili ambayo ni maarifa haziwezi kukusaidia kuishi na mkeo, unahitaji maarifa kuishi na mkeo.

Ukisoma katika kitabu cha Mithali 19:2, anasema, Tena si vyema nafsi ya mtu ikose maarifa; Naye afanyaye haraka kwa miguu yake hutenda dhambi. Kama unavyohitaji maarifa kuendesha ndege, kuendesha gari ndivyo unavyohitaji maarifa kukaa na mke wako. Kama unavyohitaji maarifa kuwa mwana taaluma bora, ndivyo unavyohitaji maarifa kuwa mume bora anayekaa na mke wake bila tatizo lolote. Ukikosa maarifa utafanya mambo kwa haraka, na ukifanya mambo kwa haraka (bila kufikiri, yaani bila kuwa na akili za kurejea zinazokuongoza njia bora ya kufanya majakumu yako na kutekeleza wajibu wako kwa mkeo) lazima tu utakosea au kutenda dhambi, kwa sababu afanyaye haraka kwa miguu yake kwa sababu ya kukosa maarifahuishia kutenda dhambi au kufanya makosa.

Akili ya mwanaume ya kukaa na mkewe ni maarifa aliyonayo kuhusiana na yeye mwenyewe, kuhusiana na mke wake, kuhusiana na ndoa, na kuhusiana na Mungu na Neno lake.

MAARIFA KUHUSIANA NA YEYE MWENYEWE:
Mwanaume yeyote kama hajitambui ndoa itamshinda. Ili awe na uwezo wa kuishi na wengine, mwanaume anapaswa ajielewe jinsi alivyo; udhaifu wake, uwezo wake, tabia yake, hulka na silika zake. Asipojifahamu itakuwa ni ngumu sana kuishi na wengine kwa sababu haitakuwa rahisi kugundua makosa yake pale anapowakosea wengine, lakini pia si hivyo tu, bali hataweza kujitawala pale anapokuwa na wengine na hasa mkewe. Kwa mfano, mwanaume mwenye hasira na anajielewa kuwa ana hasira, na anaelewa nini anapaswa afanye wakati anapokuwa ana hasisa, hawezi kufanya chochote wakati anapokuwa ana hasira. Tofauti na mwanaume ambaye hajui kama yeye ana hasira na haelewi nini cha kufanya anapokuwa amekasirika, huyu atafanya mambo kwa msukumo wa hasira yake. Na mara zote maamuzi, uchaguzi na matendo au maneno yanayosemwa wakati wa hasira huwa si mazuri na maranyingi huwa ni ya kuumiza.

Waswahili husema, Hasira hasara, na Biblia imesema, Mtu wa hasirahuchochea ugomvi (Mithali 15:18), tena inasema, Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa (Mithali 16:32), tena anaendelea kusema, Busara ya mtu huiahirisha hasira yake, Naye ni fahari yake kusamehe makosa (Mithali 19:11), tena anasema, Mpumbavu hudhihirisha hasirayake yote, Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza (Mithali 29:11). Kwa hiyo kama mtu atajifahamu, itakuwa rahisi kushughulikia mapungu yako, na kuimarisha mambo mazuri.

Wakati nikiwa bado sijajifahamu ilikuwa vigumu sana kuishi na watu, mara nyingi nilijikuta natofautiana na watu, na marazote hizo niliona kama watu hao ndio wenye makosa. Siku moja mtu mmoja wa karibu nami akaniambia kuwa "Haiwezekani kila mtu akawana na shida na wewe, hapa kuna tatizo, wewe ndio mwenye shida na sio watu wanaohusiana nawe. Kaa chini tafakari njia zako, kisha jirekebishe, kwa nini iwe wewe tu kila siku?" Maneno haya yaliniingia sana, ndipo nilipoanza kujisoma (to study myself), kujichunguza na kujitafakari. Kwa kadiri nilivyokuwa natofautiana na kugombana na watu ndivyo nilivyojiangalia zaidi mimi kuliko kuwaangalia watu, na hapo ndipo nilipojifahamu. Baada ya kujifahamu, tatizo lilibaki katika kuyarekebisha mapungufu yangu niliyokuwa nayaona. Haikuwa rahisi kabisa kushughulikia makosa na mapungufu yangu, na haikuwa kazi ya mara moja, ilikuwa ni kazi ya kila wakati kila siku.

Mchungaji mmoja ambaye ni mzazi wangu wa kiroho, siku moja aliniambia, akasema, "Ni lazima uwe kama Yakobo, alipogundua tabia yake ya udanganyifu na namna ilivyowaumiza watu wengine na namna ilivyomuumiza yeye kwa kulipa malipo ya kile alichowafanyia wengine kwa yeye kufanyiwa icho hicho, alipigana na Mungu, akamwambia juu ya maisha yake ya tabia ziumizazo na matendo yaumizao wengine na yeye mwenyewe, akamwambia Mungu, Sikuachi usiponibariki. Mungu akabadili jina la Yakobo kutoka Yakobo na kuwa Israeli." Mchungaji akaendelea na kuniambia, "Mpaka Mungu amekuvunja nawe ukavunjika, tabia yako mbaya haiwezi kukuacha, mpaka Mungu amekubariki kwa kukupa sifa (jina) njema huwezi kuwa mtu mpya." Hapo ndipo nilipoanza kukabana mashati na kupigana mieleka na Mungu nikimuonyesha kila tabia isiyokuwa njema na kumuomba anibadilishe. Hii yote ilitokea nilipojifahamu mimi mwenyewe. Na hapa ndipo nilianza kupania kuwa mtu mzuri, na taratibu maisha yangu yalianza kubadilika, sikuwa tena mtu wa kugombana na watu.

Nilipokuja kuoa, nilitumia kanuni hii hii kuhusiana na mke wangu katika maisha yetu wawili ya kila siku. Halikuwa jambo rahisi, kwani hapa napo nilianza kuona madhaifu niliyonayo ambyao hapo awali sikuyaona kwa kutumia kanuni zile zile nilizotumia hapo awali kujua madhaifu yangu nilipokuwa nahusiana na wengine. Baada ya kujua nilishikana tena mashati na kupigana mieleka na Mungu ili anisaidie. Sijaacha mpaka leo naendelea. Maarifa huwa hayakomi maadamu mtu anaishi. Maadamu kila siku naishi, nahitaji akili za kuishi na mke wangu ili kukabiliana na changamoto mpya za kila siku.

Wanaume wengi wanashindwa kuishi na wake zao kwa sababu wao wenyewe hawajielewe, hawajifahamu, na wale wanaojielewa kwa sehemu hawako tayari kushughulikia mapungufu yao na kuimarisha mambo mazuri waliyo nayo. Mara nyingi hii ni kwa sababu ya ubinafsi na kiburi walichonacho wanaume wengi.

MAARIFA KUHUSIANA NA MKE WAKE:
Huwezi kuishi na mtu ambaye kwako ni fumbo, huelewi kitu chochote kuhusiana na yeye. Ukweli wanawake wana mambo mengi sana, ni watu ambao mwanaume anahitaji maarifa mengi kuwahusu ili kuishi nao. Mwanaume anapaswa aelewe vizuri kuhusiana na namna wanawake wameumbwa, tabia zao, silika na hulka zao kwa ujumla wake. Na akishaoa ni lazima ajifunze kumuelewa mke wake kila siku, tabia zake, mapenzi yake, vitu asivyopenda, hulka na silika zake. Iwapo mwanaume atamfahamu mkewe vyema, ataishi naye kutokana na anavyomfahamu bila tatizo lolote. Mwanamke yule yule ambaye watu wengine wanashindwa kuishi naye, yeye ataweza kuishi naye kwa sababu anamfahamu vyema na amkusudia kuishi naye kwa jinsi alivyo.

Ukijua kuwa mke wako ni muongeaji kupitiliza, si kwa sababu anapenda bali ni tabia yake, utajua namna ya kuishi naye na kumfurahia alivyo. Lakini kama humjui, utajua kuongea kwake huko anafanya makusudi na hivyo kukasirishwa naye.

Wakati namuoa mke wangu, bado kuna mambo mengi nilikuwa sijui kumuhusu. Mwaka wa kwanza wa ndoa yetu kwangu ulikuwa mgumu sana, na hii ni kwa sababu nilikuwa simjui mke wangu vyema kuhusiana na silika na hulka zake kwa undani zaidi ambazo hapo mwanzo kabla hatujaoana zilikuwa hazijajidhihirisha sana. Nilianza kujifunza kumfahamu na kumchukulia. Mara tu baada ya kugundua silika na hulka ambazo siwezi kuzibadilisha ambazo kwa uhalisia wake si dhambi kwa Mungu lakini mimi zilinipa shida, nilianza kujifunza kuzikubali kwa sababu nilikuwa nimekwisha mkubali yeye. Katika hatua hii, sikuwa tayari kurudi nyuma, hata kama ningetaka kurudi nyuma, bado nisingeliweza kabisa. Kwa kadiri nilivyokaa naye ndivyo nilivyozidi kumjua, kabla sijamjua mara kwa mara tulitofautiana hata katika vitu vidogo. Kuna wakati ilipita siku hatuongei vizuri, na wakati mwingine siku mbili hadi tatu. Wakati mwingine kwa sababu nilikuwa simjui upande fulani nilishindwa hata kuelewa ni kitu gani anataka kwa wakati huo. Hii ilinisumbua sana, lakini zaidi ilimtesa yeye, mimi kutokujua yeye anataka nini ilimtesa sana.

Mara chache mke wangu alijaribu kunielewesha ni nini anataka, mimi sikuona uzito wa anachotaka kwa sababu sikuwa namjua vizuri na sikuwa nawajua wanawake vizuri katika hicho alichokuwa anataka. Kwa sababu hiyo sikuwa naona kama kuna ulazima wa kutekeleza kile alichokuwa anataka kwangu kwa wakati. Hii ilimuumiza sana, na kila alipoumia, mimi niliumia zaidi. Namshukuru Mungu taratibu, nilianza kujitia nia katika kujifunza kumjua mke wangu, mwaka baada ya mwaka, mahusiano yetu katika ndoa yalianza kubadililika, mpaka sasa tunaishi vizuri kabisa. Sisemi kuwa nimemjua tayari kwa ukamilifu, bado naendelea kujifunza kumjua. Maarifa hayakomi, hukoma pale mtu anapokufa.

ukitaka kuishi na mke wako vizuri, kaa naye kwa akili; jitahidi kuwa na maarifa kumuhusu yeye, kila siku jifunze kumuelewa mke wako, na uishi naye kwa kadiri ya unavyomuelewa na unavyojielewa wewe.

Kumbuka kuwa ndoa ni taasisi inayotegemea sana uwajibikaji wa wanandoa kila mmoja kwa mwenzake bila kujali kama umetendewa au haujatendewa. Kila mmoja katika ndoa akitaka aifurahie ndoa yake na mwenzi wake katika ndoa ni lazima afanye uchaguzi wa kutimiliza wajibu wake bila kujali kama mwenzake ametimiza wajibu wake kwake au la. Ndoa haijajenga msingi wake katika kufanyiwa, kupokea, au kutendewa; haya yote ni matokeo baada ya wewe kumfanyia, kutoa au kumpa na kumtendea mwenzi wako wa ndoa. Msingi wa ndoa ni kutoa, kumtendea na kumfanyia mwenzi wako yote unayopaswa kumpa, kumfanyia, na kumtendea ili awe na furaha. Hujaoa ili utendewe, ufanyiwe, au upewe, umeoa ili umtendee, umfanyie, na umpe. Vivyo hivyo kwa wewe mwanamke, haujaolewa ili ufanyiwe, utendewe, na upewe, umeolewa ili umfanyie, umtendee na umpe.

Ndoa ipo katika msinga wa, "Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu (pamoja na mke au mume wako), nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii." (Mathayo 7:12). Kwa hiyo, Kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo kwanza (Luka 6:31). Hii ina maana kuwa, kila unapokuwa na uhitaji wa kutendewa kitu au jambo fulani, badala ya kudai wewe kutendewa, anza kwanza wewe kumtendea mwenzi wako. Tendo lako kwa mwenzi wako ni mbegu itakayokuletea mavuno ya matendo mengi kutoka kwa mwenzi wako.

Biblia katika kitabu cha Mithali 27:18 inasema, Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake, Naye amuhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Katika mstari huu mwandishi anazungumzia swala la ndoa; mke akiwa anawakilishwa na mtini, na mume akiwa anawakilishwa na bwana. Mwanaume akitaka matunda ya mtini ni lazima autunze mtini. Mume akitaka kutendewa mema ayatakayo na mkewe ni muhimu yeye akaanza kumtendea mema hayo kwa sababu matunzo si maneno, matunzo ni matendo. Mke naye, akitaka heshima kutoka kwa mumewe ni lazima amuhudumiaye mumewe, na huduma si maneno tu, huduma ni matendo. Heshima nayo si hali fulani tu ya kudhanika au kuonyesha, heshima nayo ni matendo yanayoinua, yanayotunza na kuthamini utu wa mtu na kumfanya aonekane na kujisikia vizuri.

Mtini unatoa matunda yafaayo kwa matumizi ya chakula. Kwa mwanamke kama mtini matunda yake ni matendo yake mema kwa mumewe. Kuweka mkazo, heshima inayozungumzwa hapa ambayo mke ataipata hapa kwa mumewe ni matendo yanayomtukuza, yanayomuinua, yanayomuhifadhi, yanayomtunza, yanayomstahi na yanayomthamini mwanamke na utu wake. Hii ndio heshima anayopaswa mwanamke apewe kwa kumuhudumia bwana wake au mume wake. Hii inahitaji maarifa ambayo ni akili ya mume ya kukaa na mkewe. Siku moja nikipata nafasi nitanzungumzia hoja hii kwa mapana na marefu katika somo linaloitwa, HESHIMA YA MUME KWA MKEWE (MUME AMPE HESHIMA MKEWE). Katika somo hili nitatoa ufafanuzi wa kina wa heshima ni kitu gani, na mke hupewa heshima kwa jinsi gani.

Katika somo letu lililopita tuliangalia maarifa katika mambo mawili anayopaswa kuwa nayo mume ili aweze kukaa na mkewe. Tuliona maarifa kumuhusu yeye, na maarifa kumuhusu mwanamke hususani mkewe. Leo nataka twende mbele kidogo baada ya kupata utangulizi huu mfupi ambao ni sehemu ya maarifa yatakayokusaidia kuboresha ndoa yako. Endelea kufuatana nami.

MAARIFA JUU YA NDOA
Ni vigumu sana kuishi ndani ya jambo usilolijua. Pia ni vigumu kuendesha taasisi usiyokuwa na maarifa nayo, itakufa tu. Inachosha sana kutumia kitu kigumu usichokijua na chenye mkanganyiko, lazima tu kitakushinda, kwa sababu kinazidi uwezo wako wa akili na uelewa, badala ya kukitawala, kitakutawala, badala ya kukiendesha, kitakuendesha.

Mwanaume asiyejua ndoa ni nini na namna gani inafanya kazi yeye akiwa muhusika na mwajibikaji namba moja, ndoa itamshinda. Sio kwamba tu mwanamke atamshinda, bali ndoa yenyewe itamshinda. Hii ina maana hata kama ataoa mwanamke mwingine, kwa kuwa ndoa imemshinda, mwanamke huyo pia atamshinda. Ndoa itamshinda mwanaume, kila mwanamke atamshinda hata kama ataoa wanawake mia moja, wote watamshinda tu, kwa sababu ameshindwa ndoa.

Maarifa sahihi kuhusu ndoa anayokuwanayo mwanaume katika ufahamu wake, yatamsaidia kupunguza matatizo mengi ya ndoa, sio tu kupunguza, yatamsaidia pia kukwepa matatizo ya ndoa, kwa sababu atayaona matatizo hayo yakiwa mbali na kuyakwepa pengine kwa kuyatatua kabla hayajawafikia yeye na mkewe. Mithali 22:3 inasema, Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Mwenye busara ni mtu mwenye maarifa, kwa lugha zaidi maarifa yanamsaidia mtu kuona mabaya yakiwa mbali, na kujificha au kuyatatua. Mwanaume, unahitaji akili kukaa na mke wako. Kukosa maarifa sahihi kuhusu ndoa ni kushindwa ndoa hata kabla haujaingia katika ndoa. Kuna msemo wa kiingereza unaosema, Knowledge before marriage, wenye maana ya maarifa kwanza kabla ya ndoa.

Mithali 10:14

[14]Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.


Kama unataka matokeo mazuri katika ndoa yako, tafuta akili, tafuta maarifa. Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa, wanatafuta maarifa mapema na wanayahifadhi ili yatakapohitajika warejee na kuyatumia. Kama unavyohitaji maarifa kuwa na uwezo wa kuendesha taaluma yako, kipawa chako, biashara yako, unahitaji maarifa kuendesha ndoa yako. Tafuta maarifa, usiishi na mkeo kwa kupapasa. Soma vitabu vya ndoa, hudhuria washa mbalimbali za ndoa, nenda kwenye makongamano ya wanandoa, jifunze upate maarifa.

MAARIFA JUU YA NENO LA MUNGU:
Ukiwa hauna ufahamu wa nini Biblia inasema kuhusiana na ndoa, wewe kama mume kwa mkeo, na mkeo kwako, na Mungu kwenu ninyi na kwa ndoa yenu, hautaweza kukaa na mke wako kabisa. Neno la Mungu ndio akili yetu na hekima yetu inayotufanya tutende kwa ubora wa hali ya juu na viwango vya tofauti sana ukilinganisha na viwango vya dunia hii. Hii ni akili ambayo tunapaswa kuwa nayo ndani yetu na kuirejea kila wakati.

Kumbukumbu la Torati 4:5-6

[5]Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.
[6]Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.


Maarifa ya Neno la Mungu ndio akili ya hali ya juu ambayo ndani yake ina maarifa yote ikiwa ni pamoja na maarifa juu ya mambo ambayo tumekwisha kuyaangalia. Akili ya Neno la Mungu ni akili yetu ambayo tunapaswa kurejea kila wakati na kila saa kwa sababu ndio hekima yetu na ndio maisha yetu ikiwa ni pamoja na maisha ya ndoa.

Kila kitu anachopaswa mwanaume amfanyie mkewe kipo ndani ya Neno la Mungu, jinsi mwanaume anavyopaswa kukaa na mke wake kimo ndani ya Neno la Mungu. Hata vile mwanaume anapaswa kuwa kwa mkewe imo ndani ya Neno la Mungu. Majukumu na wajibu wake kama mume yote haya yako ndani ya Neno la Mungu. Hata namna ya kuishi, yaani stadi za maisha ya kuhusiana, maisha ya kukaa pamoja yote haya yako ndani ya Biblia. Hii ndio akili yetu na hekima yetu. Kwa hiyo Biblia inaposema kuwa mume aishi na mke wake kwa akili inasema kuwa mume aishi na mke wake akiongozwa na Neno la Mungu. Maarifa ya Neno la Mungu ndio maarifa ya ngazi ya juu kabisa, ndiyo yanayotupa maarifa ya ndoa ilianzaje, mfumo wake, Kusudi lake, mwanzilishi wake, na uzuri wake. Kutoka katika maarifa haya tunapata kujua kwa nini mwanaume aliumbwa na kwa nini mwanamke aliumbwa. Mwanaume aliumbwaje, na mwanamke aliumbwaje. Kiukweli kila kitu tunakifahamu kupitia Neno la Mungu.

Ieleweke kuwa, maarifa yanatupa akili zinazotufanya tuendeshe maisha yetu kwa wepesi na kukwepa makosa (errors) yanayoweza kutokea kwa sababu ya kukosa maarifa, na pia yanatuwezesha kujua vikwazo vinavyotukabiri na kuvivuka, kujua changamoto na kuzitatua haraka kabla ya kuleta matatizo.

MAMBO YANAYOSABABISHA MUME ASIKAE NA MKE WAKE KWA AKILI:

  1. Kudharau mafundisho: Uzoefu unaonyesha kwamba wengi wanaoudhuria kwenye mafundisho ya ndoa, iwe ni kwenye semina, washa au makongamano mbalimbali ni wanawake, wanaume wanakuwa wapi? Tangu nimeanza kuudhuria mafundisho mbalimbali ya ndoa mara nyingi nimekuwa nikiwaona wanawake wanakuja peke yao bila waume zao. Imekuwa ikinishangaza sana kuona mpaka kwenye semina za ndoa ambapo kila mwanamke hupaswa kuja na mumewe na kila mwanaume hupaswa kuja na mkewe, wanawake huwa wengi kuliko wanaume. Hata ukifuatilia wengi wanaosoma makala au vitabu vinavyohusu ndoa ni wanawake. Sijui wanaume wana shida gani. Mara nyingi wanaume utakuta wanasoma makala zinazohusiana na tendo la ndoa tu, sijui kama maisha ya ndoa ni kuhusu tendo la ndoa, yote ni tendo la ndoa tu. Mwanaume akiona kitabu au makala yenye kichwa cha habari kinachohusu jinsi ya kuongeza nguvu za kiume, au jinsi ya kumpagawisha mwanamke kitandani ndipo utaona anajipinda na kuanza kusoma. Mambo mengine kuhusiana na ndoa hawezi kusoma kabisa, anaona kama ni upuuzi tu.
  2. Kushindwa kutumia maarifa aliyonayo kwa kuogopa kuonekana dhaifu. Maarifa yasiyotumiwa hayawezi kumsaidia mtu. Wapo wanaume ambao kweli wana maarifa sahihi, lakini wanaona haya kuyatumia au wanakuwa wazito kutekeleza yale wanayoyajua. Wanaume wa namna hii hawawezi kukaa na wake zao kwa akili, na katika ndoa zao huwa kuna migogoro isiyoisha kwa sababu hawana utayari wa kutumia kile wanachokijua kinachoweza kuwasaidia. Mara nyingi hii ni kutokana na ubinafsi na kiburi walichonacho wanaume. Ubinafsi na hasa kiburi ni kikwazo kinachosimama kati ya maarifa aliyonayo mtu na uwezo wake wa kutenda au kutekeleza maarifa hayo ili kuweka uzito wa kutekeleza na kuweka hali ya kutoona ulazima wa kutenda au kutekeleza. Kiburi kinaleta dharau kila kinapokuwepo na hivyo huondoa ulazima, umuhimu na thamani ya kitu kwa muhusika. Kinapokuwepo, mtu huona yupo juu ya kila mtu na kila kitu, mtu humshusha kila mtu chini na kuanza kuwaona wengine hawafai kabisa. Hali hii ikiwa ndani ya mwanaume inafunga akili yake isifanye kazi sawasawa, na wakati mwingine huwa kama mnyama.
  3. Maarifa yasiyo sahihi kuhusu ndoa aliyonayo mwanaume. Kuwa na maarifa yasiyo sahihi ni kikwazo cha mwanaume kukaa na mke wake kwa akili. Mara zote atafanya jambo lisilo sahihi kwa wakati usio sahihi kwa mke wake. Hali hii inaweza kusababisha manung'uniko na maumivu kwa mke wake. Ni lazima mwanaume awe na maarifa sahihi kuhusiana na ndoa, mkewe, na yeye mwenyewe.
  4. Kuwa nje ya uwepo wa Mungu. Kuna mambo ambayo mtu hawezi kuyafanya isipokuwa kwa msaada wa Mungu. Ndoa ni ya kimwili na pia ni ya kiroho, na mwanzilishi ni Mungu. Kwa hiyo anayeijua ndoa kuliko mwingine yeyote ni Mungu, na mwenye uwezo wa kuihifadhi salama ni Mungu. Hata hivyo yapo matatizo tunayoweza kutatua kwa kufuata kanuni za kawaida kabisa za mwilini, lakini kuna mengine hatuwezi bila Mungu. Sina maana kwamba kuna mambo tutafanya bila Mungu, la, ukweli ni kwamba tunamuhitaji Mungu katika mambo yote yawe madogo au makubwa. Ninachosema hapa ni matatizo ambayo chanzo chake ni rohoni; Kwa mfano mkeo ana pepo kiburi na kisirani, au ana pepo la uzinzi, au ana pepo la ugomvi, hapa hauitaji kutumia kanuni za kawaida, unahitaji maombi. Na maombi yako yatafanya kazi iwapo upo uweponi mwa Mungu, ushirika wako binafsi na Mungu upo vizuri kabisa (you're connected). Tofauti na hapo hautaweza kuishi na mkeo. Lakini matatizo ya namna hii uhitaji maelekezo ya papo kwa papo kutoka kwa Mungu ili kuyatatua. Mungu atatumia moyo wako kukuelekeza, kukutia nguvu na ujasiri wa kukabiliana nayo bila jambo kuharibika kabisa. Lakini hii inawezekana tu iwapo ushirika wako na Mungu upo vizuri.


Mume, unaweza kabisa kukaa na mke wako kwa furaha iwapo utachagua na kuamua kufanya hivyo. Mungu akubariki sana.

البحث
الأقسام
إقرأ المزيد
Religion
Jinsi Shetani Anavyopofusha Fikra za Watu: Maandiko ya Biblia Yanayofafanua
Katika Biblia, Shetani anaelezewa kama roho mbaya ambaye anaweza kushawishi, kudanganya, na...
بواسطة GOSPEL PREACHER 2025-09-28 05:02:20 0 138
Injili Ya Yesu Kristo
INJILI niliisikia ila NILISHUPAZA SHINGO YANGU!!!!.
(Ushuhuda wa dada Penina)."""""'"""""""""""""""""""'''''''''''''''''''"Siku moja nikiwa na...
بواسطة GOSPEL PREACHER 2022-02-21 22:18:50 0 5كيلو بايت
NDOA KIBIBLIA
MWANAUME: SIO MKE WAKO NI WEWE
Mchungaji wangu Emmanuel Nhyama Manwele ambaye ni mwalimu wangu wa kwanza wa ndoa na maswala...
بواسطة GOSPEL PREACHER 2021-11-08 00:15:02 0 6كيلو بايت
OTHERS
JE MTU ALIYEOKOKA ANAWEZA AKAVAMIWA NA ROHO ZA GIZA ?
1. Je, anaweza kuwa chini ya vifungo, wakati Yesu alimaliza yote Msalabani? Ndugu mpendwa...
بواسطة MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 03:25:14 0 5كيلو بايت
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 40
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 21 questions at the...
بواسطة THE HOLY BIBLE 2022-01-21 09:21:25 0 6كيلو بايت