KIPI KINAHITAJI MAANDALIZI SANA KATI YA NDOA NA HARUSI?

0
5Кб

Shalom mpendwa wangu katika Kristo Yesu, Leo katika kona yetu hii ya mahusiano ya uchumba na ndoa, nataka tuangalie kuhusu maandalizi katika mambo mawili, yaani ndoa na harusi. Nataka tuangalie katika mambo haya mawili, ni kipi kinahitaji maandalizi zaidi. Na kwa sababu hiyo, tutakuwa tunaangalia umuhimu wa kimoja zaidi ya kingine.

Imekuwa ni kawaida sana siku hizi za leo baada ya watu wawili, mwanaume na mwanamke kukubaliana kuoana kutumia Muda wao mwingi kujiandaa na kufikiri zaidi juu ya siku moja na usiku mmoja, siku ya harusi na usiku wao wa kwanza kukutana kimwili. Kwa hiyo, kwa upande wa mwanaume atatumia nguvu nyingi ya akili na ya kiuchumi kuhakikisha siku hiyo moja inafanikiwa. Mwanamke naye vivyo hivyo, atatumia nguvu nyingi kiakili na kiuchumi katika kuhakikisha siku yake ya sendoff na harusi vinakwenda vizuri. Kwa upande mwingine wakati wanajiandaa kwa mambo hayo, wanajiandaa pia kwa ajili ya fungate ambalo litachukua kuanzia siku tatu hadi saba. Watatumia nguvu nyingi kiuchumi na kiakili kufanikisha jambo hili. Wataumiza vichwa vyao, kwa kufanya hiki na kile ili kuhakikisha wanafanikisha mambo haya.


Kikubwa zaidi, wakati wanafanya yote haya, watakuwa pia wanafikiria fahari ya shughuli nzima, Watatumia Muda na nguvu nyingi kuandaa shughuli yao nzima ikiwa inajumuisha sherehe ya sendoff, harusi, na fungate vinakuwa vya fahari. Sisemi kabisa mambo haya si ya muhimu, na wala sisemi kwamba si mazuri, na kwa sababu hiyo sisemi yasifanyike.

Hapana, mambo haya ni ya muhimu lakini umuhimu wake si zaidi ya jinsi ndoa ilivyo ya muhimu. Na kama ndoa ni ya muhimu kuliko sendoff, harusi, na fungate, na tena haiishi kwa siku moja au saba, bali hudumu kwa kipindi chote cha maisha yenu, basi, inahitaji maandalizi zaidi kuliko sendoff, harusi, na fungate. Cha kushangaza sasa, kwa kipindi chote cha mahusiano ya uchumba, na hasa pale siku ya kufunga ndoa inapokuwa imekaribia, wahusika huwekeza zaidi, muda wao, akili zao, fedha zao, nguvu zao katika kufanikisha mambo haya na kumtengeneza mazingira mazuri ya mambo haya kuliko ndoa yao. Hili ni tatizo kubwa. Kumbuka kuna maisha baada ya sendoff, harusi, na fungate, na maisha hayo ni ndoa yenu.

Kwa hiyo, badala ya kutumia Muda mwingi, nguvu nyingi, fedha nyingi, na akili nyingi kuandaa sendoff, harusi, na fungate, tumia kuandaa ndoa yenu. Unapokutana na mwenzako, badala ya kutumia Muda mwingi kuongelea harusi yenu, tumieni muda mwingi zaidi kuongelea ndoa yenu kuliko harusi na fungate yenu. Wekeni misingi ya ndoa yenu, pangeni mipango ya ndoa yenu na namna ya kuitimiza, kubalianeni juu ya mambo yatakayodumisha ndoa yenu kiuchumi na kimahusiano. Kila mkutanapo fanyeni hivyo. Mkitumia Muda mwingi kuandaa harusi na fungate yenu, mara baada ya hivyo kuisha hamtajua nini cha kufanya kwa pamoja, na nini cha kufanya kila mmoja kwa sehemu yake ili kuendelea mbele, kwa nini, kwa sababu hamkujiandaa kwa ajili ya ndoa mbali mlijiandaa kwa ajili ya sendoff, harusi, na fungate, kwa hiyo vyote vimeisha, mnaanza kuangaliana.

Unajua, inashangaza sana, mtu anatumia gharama nyingi za kiuchumi kuandaa harusi na fungate, wakati hajajiandaa kabisa juu ya maisha yake baada ya harusi. Anajiandaa kula na kunywa wakati wa harusi, wakati hajaandaa chakula cha kula baada ya harusi na kuendelea. Anaandaa mahali pazuri pa kulala, tena pa kifahari wakati wa fungate, wakati hajaandaa vizuri mahali pa kulala mara tu baada ya fungate na kuendelea. Huu ni ujinga kabisa, tena ujinga uliokithili. Unakula vyuku wakati wa harusi wakati huna chakula cha kumlisha huyo mkeo baada ya harusi. Unalala kwenye kitanda cha 8 x 8, hotelini kwenye chumba cha kiyoyozi, wakati kwako huna hata feni, neti huna, kitanda chenyewe godoro limechoka, shuka moja, chumbani hapaeleweki kama ni chumbani au stoo. Yaani ni vulugu mechi tu. Kwa namna hii, harusi ya kifahari wakati umepanga chumba kimoja tena uswahilini, huna chakula, ni ya nini? Bora mara kumi ukafunga ndoa inayoambatana na sherehe ndogo ya kawaida kabisa, na fedha utakazokuwa umepata, itumie kwa mambo mengine katika kuimarisha ndoa yako. Bora mara 100 ukafanyia fungate nyumbani kwako kuliko kufanyia fungate hotelini wakati huna chakula, na hapo hapo mahali pa kulala hapako vizuri, ukazitumia pesa hizo za fungate kurekebisha mambo mengine ya nyumbani mwako.

Mambo mengine haya, yaani sendoff, harusi, na fungate, yana maana pale tu kwa upande wa maisha ya ndoa yanapokuwa yameandaliwa vizuri. Usiandae sendoff, harusi, au fungate wakati hujaandaa ndoa yako. Lazima itasumbua tu.

Hata hivyo, usifanye jambo kwa kuiga. Eti kwa sababu harusi ya fulani ilikuwa vile, nataka yangu iwe kama yake. Je, unajua namna alivyojiandaa? Usifanye, jambo kwa mashindano. Eti harusi ya jamaa yangu ilikuwa vile, basi yangu ni lazima iwe zaidi ya vile? Umejiandaa? Kwanza kwa nn uzungumzie harusi badala ya ndoa. Bila shaka uelewa wako ni mdogo. Tumia Muda wako kuandaa ndoa yako;

  1. Omba
  2. Soma Biblia
  3. Soma vitabu vitakavyokuongezea maarifa ya ndoa.
  4. Hudhuria mafundisho yanayokuandaa kuwa mume/mke au mzazi bora.
  5. Andaa mazingira ya ndani mwako vizuri, hakikisha kila kinachohitajika kuendesha maisha yenu kipo tayari. Kama unauwezo wa kujenga nyumba, jenga, hakikisha chumba cha kulala kiko vizuri, jikoni pako vizuri, sebuleni pako vizuri.

Kumbuka, uzuri wa harusi si ubora wa ndoa yenu, na fahari ya harusi si fahari ya ndoa yenu, na utukufu wa ndoa yenu hauletwi na utukufu wa harusi yenu, na wala harusi haina sehemu katika ndoa yenu, na kwa sababu hiyo, maandalizi ya harusi si maandalizi ya ndoa. Hivyo, kama hujajiandaa na unaona wakati wa wewe kuoa au kuolewa umewadia, ni bora kufanya ibada ya ndoa, mkafunga ndoa kisha mnaendelea na maisha yenu ya ndoa. Harusi si ya lazima kihivyo japokuwa inapendeza ikifanyika. Na hasa ikifanyika pasipo kujikamua saaana.

Поиск
Категории
Больше
EXODUS
Verse by verse explanation of Exodus 15
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 67 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-01-22 17:49:38 0 5Кб
Injili Ya Yesu Kristo
MOTO WA KIGENI
Walawi 10:1-2 “Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake,...
От GOSPEL PREACHER 2023-06-25 01:00:10 2 8Кб
Injili Ya Yesu Kristo
YAFAHAMU MAFUNDISHO YA UONGO
(basi roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani wakiyasikiliza...
От GOSPEL PREACHER 2021-12-22 01:41:05 0 5Кб
Injili Ya Yesu Kristo
JINSI WACHAWI WANAVYOCHUKUA NYOTA YAKO
UTANGULIZI: Huu ni mwendelezo wa somo la Nyota na Maisha mtu aliyonayo. Mathayo 2:1; Kama...
От MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 21:13:14 0 6Кб
Injili Ya Yesu Kristo
NITAMTAMBUAJE MKE AMBAYE MUNGU AMENIANDALIA?
SwaliBwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu.Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa ajili yenu...
От GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:20:18 0 4Кб