HATUA TATU MUHIMU KABLA YA KUFUNGA PINGU ZA MAISHA

0
5K

Mojawapo ya swali gumu kuhusiana na mahusiano ni pale vijana wanapouliza wakae kwenye uchumba kwa muda gani? Wapo watumishi ambao wanashauri kipindi cha miezi sita, wengine mwaka mmoja au miwili lakini wengi wao hawana majibu ya moja kwa moja au yanayoeleweka. Atukuzwe Mungu kwa sababu leo ndio siku ambayo kiu yako itakatika kwa kupata jibu sahihi.

Mara nyingi uchumba unaodumu kwa muda mfupi husababisha majaribio ya mara kwa mara ya talaka baada ya ndoa. Hiyo ni kwa sababu uchumba wa muda mfupi hautoi muda mzuri wa kufahamiana, kukomaa kifikra na kihisia, na kujenga msingi imara wa maamuzi ya kuingia kwenye ndoa. Kwa ujumla, maamuzi yao ya kuoana yanakuwa yametokana na mvuto au hisia za kimapenzi au uhitaji mkubwa wa kuwa na ndoa bila kutafakari na kujua uhalisia wa maisha ya baadaye. Kwa upande mwingine uchumba wa muda mrefu husababisha kuchoka na kupoteza radha ya uchumba. Vijana wengi wanajikuta wakishiriki tenda la ndoa wakati huu kwa sababu ya kuzoeana na kukaribisha fikra za kuwa wao ni mke na mume. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema, Uchumba unaodumu kwa muda mrefu unapoteza maana ya uchumba. Na tunaposema kuchoka sio kupoteza upendo ila mtu anapokuwa kwenye hatua moja kwa muda mrefu hali ya kuchoshwa na hatua hiyo hutokea. Japokuwa kila uchumba unatofautiana na mwingine, tunashauri vijana waingie kwenye ndoa baada ya kupitia hatua tatu muhimu za uchumba. Hatua hizo ndio zinatoa jibu la kwamba vijana wanatakiwa kukaa kwenye uchumba kwa muda gani.

 

HATUA YA KWANZA: KIPINDI CHA HISIA

Hatua ya kwanza ya uchumba ni ile ambayo wachumba wanatumia hisia zaidi kuliko fikra. Kila mmoja anavutiwa na mwonekano kila kitu cha mwenzie. Kipindi hiki wachumba huonekana wakiwasiliana mara kwa mara, wakisikilizana na kuoneshana hisia za upendo wazi wazi. Ni mara chache sana kwa wachumba kubishana au kukosoana kwenye hatua hii, hata linapokuwepo la kuwakwaza hujilazimisha kulirahisisha ili waendelee kuimarisha mapenzi yao. Wachumba hufurahia sana wanapoonana na kushinda pamoja, kila mmoja anaonekana mpya kwa mwenzie. Ni kipindi ambacho wazazi na walezi wa kiimani huwa wanakosa nguvu ya kuwazuia. Hatua hii huwashawishi vijana kiasi cha kuamini kweli kila mmoja alizaliwa kwa ajili ya mwenzie.

HATUA YA PILI: KIPINDI CHA KUWEKA MSINGI

Baada ya kipindi cha hisia, kila mmoja anaanza kumchunguza mwenzie kuona kama ataweza kukidhi hatua ya ndoa. Hiki ni kipindi muhimu sana kwa wachumba kufahamiana. Ni kipindi ambacho inashauriwa mtu kuwa halisi zaidi ili kusaidiana katika kufahamiana. Katika hatua hii wachumba huanza kuulizana maswali ya msingi na kukosoana. Kwa kutoelewa wengine wanapokosolewa wanaanza kuhisi wanaonewa au hawapendwi. Ukosoaji huambatana na dhamira ya kuweka msingi mzuri wa mahusiano lakini mara nyingi ukosoaji uliopitiliza huwa na lengo la kuvunja uchumba baada ya kuchokana au kwa sababu nyinginezo. Hiki ni kipindi ambacho wachumba wanachunguzana tabia, mapendeleo, vitu wanavyothamini, mitazamo yao, namna bora ya kuwasiliana, nakadhalika. Katika hatua hii tofauti zenu zinakuwa wazi na kuwasaidia kufanya maamuzi ya kuvunja mahusiano au kukubaliana na kusonga mbele. Yafuatayo ni mambo muhimu zaidi ya kuyafahamu katika kipindi hiki ili muweze kwenda pamoja (Amosi 3:3 Je! Watu wawili waweza kutembea pamoja, wasipokuwa wamepatana?)


1. Ndoto zenu.
Kila mmoja wenu ana ndoto katika maisha. Anatamani awe mtu wa aina fulani au afanikiwe kwa kiwango fulani. Ndoa ni muunganiko wa watu wawili. Ikiwa mnatofautana kabisa ndoto zenu ni vizuri kuweka sawa katika kipindi hiki ili kuunda ule umoja halisi katika ndoa. Kujua ndoto za mwenzio kunakupa nafasi ya kujitathmini na kuona endapo uko tayari kuishi na mtu mwenye ndoto hizo, kwamba utaweza kumsaidia na kufurahia maisha yenu ya baadaye au la. Hii ni changamoto kwa vijana ambao wanataka kuoa lakini hawana maono, matokeo yake ni kwamba mke ataonekana hafai kwa sababu hakujua tangu awali kwamba ataishi na mume wa aina gani ili ajiandae kiufahamu na kwa kumuomba Mungu. Ndoto ni mwelekeo wa maisha yenu, pasipo maono hakuna ndoa salama (Mithali 29:18a).


2. Namna mnavyowasiliana.

Mawasiliano ni msingi wa mafanikio katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Katika mahusiano mawasiliano nayapa uzito wa kipekee kwa sababu bila mawasiliano bora hakuna ndoa bora. Kwa uzito wa suala hili nitalileta kama mada kamili, lakini kwa hapa nakupa mwongozo wa vitu vya kutathmini ili kujua kama mawasiliano yako na mchumba wako yanatoa picha ya ndoa bora.

  • Mchumba wako anakusikiliza kwa makini unapoongea au anaendelea na mambo yake?
  • Mnaongea vipi ikiwa mmoja au wote mmekasirika?
  • Je uko huru kumshirikisha mchumba wako mawazo yako ya ndani zaidi?
  • Je, umefikia hatua ya kuelewa akiwasiliana na wewe kwa vitendo? Kwa mfano akiwa na tatizo unaweza kumgundua hata asiposema?
  • Mnatumia muda gani kupatana baada ya kukosana?
  • Mnakabiliana vipi pale mnapotofautiana mawazo (Ugomvi, kununa, matusi, kukaa chini na kuzungumza)?
  • Mnatumia mtindo upi kumaliza mgogoro (Kubishana hadi ushinde, Kupotezea, Kuondoka, au Kupata suluhu ya pamoja) ?

3. Matarajio yenu.
Tofauti na ndoto zenu, kila mtu anatarajia mambo kadhaa baada ya ndoa. Matarajio mara nyingi yanahusisha vitu vidogo vidogo, tabia, mapendeleo (interests) pamoja mtindo wa maisha yenu. Wanandoa wengi wamejikuta kwenye kwenye huzuni na masikitiko yasiyokwisha kwa sababu hawakuweka wazi matarajio yao na mtindo wa maisha ambao wangependa kuishi baada ya ndoa. Matarajio yaliyofichwa ni chanzo cha migogoro ya ndani (internal conflict) kwa watu wengi katika mahusiano. Si kwa sababu ya uhalisia wa matarajio hayo bali kwa sababu ya kutofahamishana mapema kuhusu matarajio yao. Ni vizuri matarajio yako yawe halisi, yanayoweza kupatikana na yenye mantiki. Lakini muhimu zaidi ni kwa mwenzio kujua nini unatarajia kutoka kwake. Swali ni je mmepata muda wa kushirikishana na kupatana namna ya kutimiziana matarajio yenu wewe na mchumba wako?


Angalizo muhimu: Hakuna mtu anaweza kumbadilisha mtu mwingine, ni Mungu pekee mwenye uwezo huo. Dhana ya kwamba utambadilisha mtu si dhana sahihi, endapo unampenda mtu lakini mnatofautiana sana lakini ungependa kuishi na mtu huyo, unapaswa kujipa muda wa kutosha na kumuomba kwa Mungu ambaye ndiye awezaye kubadilisha mioyo. Hii ndio sababu tunasema uhusiano wako na Mungu ni muhimu katika kila hatua ya maisha yako.

 

HATUA YA TATU: UAMUZI WA KUFUNGA NDOA

Hatua ya mwisho ni kutangaza nia ya kufunga ndoa. Maana yake uchumba umeimarika, wote wawili mmefikia makubaliano na mmejitoa kwa ajili ya ndoa. Nitoe angalizo mapema kwa wanaume, kuamua kuoa ni kuamua kuingia kwenye majukumu, lakini sio majukumu yako peke yako tu bali ya mke wako na watoto wenu wa baadaye. Mwanaume kama mwanzilishi nambari moja wa familia anapaswa kujitosheleza kihisia, kifikra na kiroho ili anapomwalika mke kuingia kwenye ulimwengu wake basi awe ni chachu ya kukuza ndoa. Mwanaume anapaswa kuwa na fikra za kumlea, kumtunza, kumuwezesha, kumuimarisha na kumpenda mke wake kiasi cha kuwa tayari kufa kwa ajili yake (Efeso 5:25). Mwanaume anayeoa ili akalelewe au akanufaike na maisha mazuri aliyonayo mwanamke huyo bado hajakomaa. Na mwanamke anayeolewa anapaswa kuelewa kwamba anaenda kuwa msaidizi ili kufikia ndoto yao (kwa sababu wanakuwa kitu kimoja). Hii ndio sababu katika mafundisho yangu nawaasa vijana kwamba kila kijana anapofikia utu uzima anapaswa kutengeneza dira ya maisha yake ya baadaye yaani kazi atakayofanya, mahali atakapoishi, aina ya mke au mume atakayeishi naye, namna atakavyolea watoto wake nakadhalika. Mara nyingi vijana wanavunja mahusiano kabla ya kufikia hatua hii ya tatu sio kwa sababu hawakupata watu sahihi bali ni kwa sababu ya kukosa dira ya maisha kiasi cha kuona kila mtu hafai kwenye maisha yao. Ukiwa na dira ya maisha yako ya baadaye huwezi kuvunja mahusiano hovyo ovyo kwa sababu utakuwa makini kuchagua mtu sahihi.

Hiki ni kipindi cha kuanza kutekeleza mipango ya ndoa. Kipindi hiki kinachangamoto zake. Tofauti kadhaa zitajitokeza wakati wa mipango ya ndoa, ni vema mkachukulia kuwa ni jambo la kawaida na kusaidiana katika hali na mali. Msipozikabili vyema changamoto mnaweza kufikiri kwamba mnahitaji miaka kadhaa zaidi ya uchumba. Kwa kweli kipindi hiki mnaweza kukatishwa tamaa na mtu ambaye mlitegemea angewaunga mkono, lakini Mungu mwaminifu mkiwa imara katika Bwana atawavusha kwa ushindi. Ni kipindi cha mawazo, kila mtu anawaza mambo yatakuwaje, ni vizuri kila mmoja akawa tayari kuachilia baadhi ya misimamo na mitazamo yake ili kufikia muafaka katika kila mpango. Usiwe mwamuzi wa mwisho kwa kila jambo, ongeza utayari wa kumsikiliza mwenzio, mpe nafasi ya kujieleza.


Kwa kuwa mnaingia hatua ambayo itathibitishwa kwa maandishi mbele ya mashahidi, nachelea kusema kwamba ni hatua ambayo haihitaji mzaha hata kidogo. Kwa kuwa katika hatua ya pili ulifanya tathmini yako binafsi na kumtathmini mwenzio na kujiridhisha kwamba mnaweza kuoana, sasa ni wakati wa kufanya tathmini ya pamoja kwa ajili ya kukubaliana mambo kadhaa muhimu yahosuyo maisha baada ya kufunga ndoa. Mjadala huu ni kwa wale ambao tayari wamekubaliana kwamba wataoana. Wachumba wakae chini wajadili, endapo watakosa majibu sahihi au watashindwa kuelewaa juu ya jambo wanalojadili ni vizuri wakawaona viongozi wao wa kanisa, mshauri nasaha au wazazi. Lakini wachumba wanapaswa kujijengea utaratibu wa kumaliza mijadala yao pasipo kuhusisha mtu wa tatu ili hata baada ya ndoa waweze kuelewana na kutatua migogoro kwa urahisi. Hao wengine wanaweza kuhusishwa pale ambapo kwa kweli kuna ulazima wa kufanya hivyo. Kama nilivyosema hapo juu, hatua hii inataka subira, upole na kutangulizana. Sumu kubwa ya hatua hii ni ubinafsi. Ukitaka kujitanguliza wewe katika kila jambo mtaingia kwenye ndoa mkiwa na furaha ya kuigiza. Sasa basi wakati mnaendelea kupanga siku ya kufunga ndoa na kufikiria sehemu nzuri ya kwenda fungate (honeymooon), tafakarini kwa pamoja mambo yafuatayo:

 

1. MAJUKUMU

  • Nani atakuwa kichwa cha familia yenu? Kuwa kichwa maana yake nini?
  • Katika familia yenu, majukumu ya mwanamke yatakuwa yepi na ya mwanaume yatakuwa yepi?
  • Kwa mtazamo wako ni nani atakuwa na jukumu la kulisha familia? Na mwingine atafanya jukumu gani?
  • Ni nani atahusika na kazi za nyumbani? Na mwingine atashirikiana naye vipi?


2. FEDHA

  • Ni nani atawajibika kwa masuala ya fedha katika familia?
  • Utakapotaka kununua kitu muhimu/kikubwa utawasiliana na mwenzio?
  • Ulilelewa katika familia tajiri au familia maskini?
    Je hiyo itakuathiri kwa upande wa matumizi kwenye ndoa?
  • Andika makadirio ya matumizi yenu kwa
    mwezi, anza na mahitaji muhimu kwanza.

 

3. MASHEMEJI, MAWIFI NA WAKWE

  • Je uhusiano na familia zenu ni muhimu?
  • Nani anawajibika kuendeleza uhusiano na familia za pande zote mbili?
  • Je mtatumia baadhi ya likizo kuimarisha undugu na uhusiano na ndugu
    zenu? Kivipi?
  • Wazazi wenu wakizeeka nani atawajibika kuwahudumia?
    Mtapendelea zaidi mtindo upi wa kuwahudumia?
  • Wazazi wenu wakiwa chanzo cha migogoro mtafanyeje?
  • Mtaunda utaratibu gani ili kila mmoja aisonekane kupendelea ndugu
    zake?

 

4. IMANI NA MALEZI (2 Wakorintho 6:14)

  • Mtaabudu wapi baada ya ndoa, na kiimani mtawalea watoto kwa mtindo gani?
    Watakuwa huru kuabudu au watafuata imani yenu? Kwa nini?
  • Mkubaliane aina ya malezi kwa familia yenu.
  • Kama mnatofautiana imani, ni vema mkapata ushauri kwa viongozi wenu wa kiimani kabla ya kuoana.


5. MTAKABILIANA VIPI YATAKAPOTOKEA MSIYOYATARAJIA

  • Unapogundua hamuwezi kuwa na watoto
  • Mwenza wako atakapougua sana kwa muda mrefu.
  • Kukosa kazi
  • Mtakapolazimika kuhamia kwenye makazi duni (kutokana na kushuka kwa kipato au kuhamishiwa kazi kijijini sana)
  • Hali ngumu ya maisha.
  • Kufariki kwa mtoto
  • Utakapogundua mwenzio si mwaminifu kwako (infidelity).

Maswali hayo yanapaswa kujibiwa ukiwa peke yako kwanza ndipo mnaweza kukutana na mchumba wako na kulinganisha majibu yenu. Ili kufikia mafanikio ya maandalizi haya mnahitaji mtaalamu wa mahusiano au mtu ambaye amedumu kwenye ndoa kwa miaka mingi, kwa hiyo usisite kutafuta ushauri juu ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo. Usikae kwenye uchumba wa siri, mnapokuwa kwenye mahusiano hakikisha mnakuwa na mlezi mtu mzima (mzee wa kanisa, kiongozi mwenye hekima, au mwanandoa mcha Mungu ambaye ndoa yake ni mfano wa kuigwa).

Tunapohitimisha mada hii, nitoe angalizo kwamba usiingie kwenye ndoa kwa sababu unataka kujikwamua kifedha, unataka kuponya majeraha ya moyo, kufuata mkumbo, umechanganywa na uzuri wake (Mithali 6:25), umechoka maisha ya nyumbani au unataka kufanya maonesho na kumkomoa mtu fulani. Ewe kijana wa kiume, unaoa mke ambaye ni msaidizi wako, sio mtumwa wako. Msaidizi anafanya kazi pamoja na wewe, jifunze kumshirikisha mke wako kwa kila jambo, huna sababu ya kufanya mambo sirini. Barikiwa sana!

Buscar
Categorías
Read More
Injili Ya Yesu Kristo
BIBLIA INAWEZA KUAMINIWA NA KUTEGEMEWA
Kimsingi mwanadamu anaweza kumfikiria Mungu kwa njia kuu mbili: Njia ya kwanza ni ile ya...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 04:11:59 0 5K
REVELATION
UFUNUO 5
Shalom! Karibu katika mwendelezo mfupi wa uchambuzi wa kitabu cha ufunuo, kwa neema za Mungu...
By GOSPEL PREACHER 2021-10-30 09:41:30 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
NAMNA SHETANI ANAVYOTUMIA ROHO YA USAHULIFU KUHARIBU MAISHA YA WAAMINI
  Shalom, katika waraka huu wa Desemba 2016 nimeona ni vema kukumbusha juu ya jambo hili...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:31:32 0 5K
NDOA KIBIBLIA
NDOA YA MKE MMOJA NA MUME MMOJA NI AGIZO NA NI SHERIA YA MUNGU
UTANGULIZI:Kumekuwepo na mkanganyiko mkubwa katika swala la ndoa kati ya ndoa ya mke...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-08 00:04:02 0 7K
MASWALI & MAJIBU
Je! Mtu Aliyeokoka Anaruhusiwa Kumiliki Lodge Ambayo Ina Bar Ndani Yake?
Swali linaendelea….na kutoa fungu la kumi kwa kupitia hiyo?,kwa mfano mimi nina rafiki...
By GOSPEL PREACHER 2022-06-13 09:17:15 0 6K