MWANAMUME HAPASWI KUWA MBINAFSI, MCHOYO

0
5K

Bwana Yesu asifiwe, Amani iwe nawe.

Leo napenda tuanze kuangalia mfululizo wa somo hili la, Mwanamume hapaswi kuwa mbinafsi, mchoyo. Katika somo hili tutaangalia mambo mbali mbali au matendo mbali mbali yatokanayo na tabia hizi mbili za ubinafsi na uchoyo afanyayo Mwanamume mwenye tabia hizi dhidi ya mkewe na familia yake. Tofauti na wanawake, wanaume wengi ni wabinafsi na wachoyo, na tabia hii inapokuwa ndani ya Mwanamume lazima mkewe na familia yake kwa ujumla watateseka. Kwa nini? Kwa sababu Mwanamume ndiye MPAJI na MTUNZAJI wa mkewe na familia yake (He is a provider of his wife and of his family as well). Yeye hutimiza mahitaji yote ya mkewe na familia yake. Japokuwa mkewe anaweza kumsaidia lakini msaada wa mkewe hauondoi wala kupunguza jukumu hili la mwanaume hata kidogo. Bado atawajibika kwa mkewe na familia yake ktk kutimiza jukumu lake hili.

Sasa kabla hatujaendelea mbele, ngoja tuangalie ubinafsi ni nini na uchoyo ni nini.

Uchoyo au choyo ni hali ya kuopenda kutoa kitu hata kama aliyenacho hakiitaji wala hakimnufaishi; ni hiyana. Ni tabia ya kutotaka kutoa kitu kumpa mwingine, ni tabia ya unyimifu.

Uchoyo au choyo ni tabia huzaliwa, hukua na hufa. Inapofanywa mara kwa mara huwa mazoea na mazoea hujenga tabia.

Ubinafsi
Hii ni hali au tabia ya kujifikiria na kujipenda wewe mwenyewe. Mtu mwenye tabia hii hafikirii wengine. Hujifikiria yeye tu ktk kila jambo.

Tabia hii huzaliwa, hukua na pia hufa.

Kama ilivyo kawaida ya tabia huzaliwa kwa kuanza kutenda tendo lile lile kwa kujirudia na hatimaye huwa mazoea na mazoea hujenga tabia.

Mwanamume hapaswi kuwa mbinafsi, mchoyo ktk jambo lolote lile kwa sababu tangu mwanzo hakukusudiwa kuwa peke yake. Mwanamume alikusudiwa kuwa na mke, na baada ya kuwa na mke kuwa na watoto; na wote hawa waliwekwa kuwa chini ya uangalizi wake, awatunze, awalinde, na kuwatimizia mahitaji yao yote. Kwa sababu hiyo yeye ni kichwa cha mkewe na ni baba wa watoto wao. Yeye ni kiongozi wa familia, na ni mtunzaji wa familia yake pamoja na mkewe. Kwa hiyo kwa mantiki hii hapaswi kuwa mbinafsi, mchoyo. Anapaswa awe mkarimu, mpaji, atoaye kwa wingi pasipo choyo wala majuto, wala kukemea, wala manung'uniko. Kama Mwanamume bado anajifikiria na kujipenda yeye kuliko wengine, na kama bado ni mchoyo, hawezi kuishi na mwanamke, na hawezi kutunza familia yake kwa ukamilifu na uaminifu wote. Ni vigumu kuishi na Mwanamume wa namna hii.

Kwa kuwa mwanamke asili yake aliumbwa ili kupokea, na baada ya kupokea kuzalisha au kuzidisha ili kulea na kukuza, hawezi kuishi na Mwanamume ambaye hatoi chochote kwa mkewe, mara zote hujifikiria yeye tu. Mwanaume ambaye ni mchoyo wa muda wake na mbinafsi wa muda wake hawezi kutumia muda wake kuonyesha upendo kwa mkewe, na kwa sababu hiyo asitarajie upendo kwa mkewe kwa sababu hakuna chochote ambacho mwanamke amepokea kutoka kwa mumewe. Kama ilivyo ktk eneo la uzazi, mwanamke hupokea mbegu ya mwanamume ambayo ni ndogo sana isiyoweza kuonekana kwa macho, huilisha na kuikuza tumboni kisha huirudisha mikononi mwa mwanamume ikiwa ni mtoto mwenye kilo tatu na zaidi anayeonekana kwa macho, ndivyo ilivyo ktk mambo mengine yote. Ukimpa mwanamke upendo, atakurudishia zaidi ya ule uliyompa. Kila utakachompa kitarudi kwako kikiwa kimezidishwa. Ukimnyima usitarajie chochote kwake.

Mithali 27:18

"Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake,
Naye amuhudumiaye bwana wake, ataheshimiwa."


Katika andiko letu hili, kipengele cha kwanza kinazungumza juu ya mambo matatu, 1.Mtunzaji wa mtini, 2. Mtini, na 3. Matunda ya mtini. Mtunzaji ni mwanamume, Mtini ni mwanamke, na Matunda ni matendo ya mwanamke. Sasa kama hakuna matunzo basi hakuna matunda. Kwa lugha rahisi kabisa, usitarajie chochote kwa mkeo kama humtunzi. Matunzo hupeleka vitu kwa mkeo vinavyopelekea akuzalie matunda, kama hakuna unachompa mkeo usitarajie wala usidai chochote kwake. Hujaweka unataka utoe nini, lazima utakuta akaunti yako inasoma sifuri.

Kama mkulima anavyoutunza mtini, anaupa mbolea, anaumwagilizia maji, anaung'olea majani, anaupulizia dawa ili kuukinga na wadudu waharibifu, anaujengea wigo ili kuuwekea ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu, anaukatia matawi yasiyitakiwa ili wakati wote uvutie na upendeze lakini pia umzalie matunda mengi, ndivyo na mwanamume kwa mkewe anavyopaswa kufanya.

Wanaume wengi leo wameshindwa kuishi na wake zao, na iwapo mwanamke amechagua kumvumilia basi, ana madonda ya tumbo au afya yake imedohofu kwa sababu
wanaume hao hawajautunza mtini halafu wanaulazimisha mtini uwazalie matunda.

Mwanamke, ukiolewa na mwanamume mbinafsi, mchiyo, umekwisha, utaishia kulia, kuugua mpaka basi.... Mwanamume mbinafsi, mchoyo si wa kuolewa naye hata kidogo. Matarajio yako na matamanio yako yatakufa tu. Kwanza unatakiwa kujua kuwa mwanaume mbinafsi, mchoyo hana upendo wowote, na iwapo atakuonyesha upendo wakati anakufuatilia basi ni kama muwindaji amwagae mchele ndani ya mtego wa ndege. Si kwa sababu anayapenda maisha ya ndege na ndege huyo, bali ni kwa sababu anataka amle ndege huyo au ajipatie faida kupitia ndege huyo. Vivyo hivyo na mwanamume mbinafsi, mchoyo, atakumwagia upendo kama chambo ndani ya mtego, akisha kunasa, utaisoma namba.

Katika andiko letu kuna kipengele cha pili ambacho kinasema kwamba, "Naye amuhudumiaye bwana wake ataheshimiwa." Kitu cha kwanza tunachojifunza hapa ni kwamba, huduma ya mwanamke kwa mumewe huja baada ya mwanaume kuutunza mtini na sio kabla ya kuutunza mtini. Mwanaume anayetarajia kuhudumiwa kabla ya matunzo hana akili vizuri. Kama humtunzi mkeo unatarajia akuhudumieje wakati hakuna ulichompa. Unataka upate faida wakati hutaki kuwekeza, weeeeee, acha ujinga huo.

Niseme kidogona wanawake. Kama mumeo anakutunza, unashindwaje kumuhudumia? Huo nao ni ujinga na upumbavu. Kama mumeo anajitoa kwa ajili yako kwa nn usimuhudumie? Heshima ya mwanamke ipo ktk kumuhudumia mumewe.

Mithali 27:18

"Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake,
Naye amuhudumiaye bwana wake ataheshimiwa."


Mtunzaji mtini ni tofauti na mtini na wote Mtunzaji mtini na mtini wanamahita kila mmoja mahitaji yake na kwa kiwango tofauti. Lakini wote wanategemea mtu mmoja ili kukidhi mahitaji yao ya awali. Wote wanamuhitaji Mtunzaji mtini; Mtunzaji mtini anajihitaji ktk kutimiza mahitaji yake, na mtini anamuhitaji Mtunzaji mtini kutimiza au kutimiliziwa mahitaji yake. Na katika hali halisi ya kanuni ya matunzo wote wanahitajiana; wakati Mtunzaji mtini anahitaji matunda ya mtini, mtini unahitaji matunzo ya Mtunzaji mtini. Lakini kitu kigumu ambacho kinahitaji gharama ya upendo kwa upande wa Mtunzaji mtini ni kwamba haanzi kwa kula matunda ya mtini ndipo autunze, bali anaanza kwa kuutunza ndipo ale matunda yake, lakini inategemea sana matunzo anaoupatia mtini, kama hayakidhi mahitaji ya mtini, mtini hauwezi kumzalia matunda hata kama Mtunzaji mtini atakuwa anayahitaji matunda ya mtini. Uhitaji wake ni lazima utanguliwe na matunzo kwa mtini. Kwa lugha rahisi na nyepesi ni kwamba, mahitaji ya mtini yanapotimizwa hupelekea kutimizwa kwa mahitaji ya Mtunzaji mtini.

Kwa hiyo basi, pamoja na mwanamume kuwa na uhitaji, ili kukidhi uhitaji wake kikamilifu ni lazima akidhi kwanza uhitaji wa mkewe na familia yake. Asitarajie kutosherezwa kwa uhitaji wake toka kwa mkewe kabla hajatoshereza uhitaji wa mkewe.

Kwa hiyo, kwa upande wa mwanamke ni muhimu kumtoshereza mumeo iwapo amekutoshereza ktk kila unachohitaji au ktk yale mahitaji muhimu unayoyahitaji yaliyo ktk uwezo wa mikono yake. Mtunzaji mtini huutunza mtini kwa kadri ya uwezo wake. Usitake matunzo kupita uwezo wa mume wako, ni dhambi.

Mwanamume, kwa gharama yoyote, kwa kidogo au kikubwa unachopata, hakikisha unamtunza mkeo. Mwanaume yeyote mwenye upendo na mkewe haachi kumtunza mkewe eti kwa sababu alichopata au anachopata ni kidogo. Atakosa yeye ili mkewe apate, atahakikisha mtini haunyauki, kila siku atahakikisha jani la mtini ni bichi na limesimama halijainama kwa kunyauka.

Sasa tuangalie sifa za mwanamume mbinafsi, mchoyo.

  1. Haoni hitaji la mkewe au familia yake, yeye huona hitaji lake tu. Mwanaume wa aina hii macho yake na nguvu zake ameelekeza ktk uhitaji wake. Chochote atakachopata atatimiza uhitaji wake. Kwa sababu macho yake yanaangalia uhitaji wake hawezi kuona uhitaji wa mkewe hata kama ataonyeshwa. Atamtumia mkewe katika kutimiza uhitaji wake mwenyewe na si wa mkewe. Mwanaume wa jinsi hii ni vigumu sana kuishi naye na kuweka tumaini lako kwake. Atakutumia wewe mwanamke kutoshereza uhitaji wake kwa sababu haoni uhitaji wako. Na haoni uhitaji wako kwa sababu jicho lake halipo kwako lipo kwake mwenyewe. Chezea wewe mwanaume mbinafsi, mchoyo!!
  2. Hana Muda na mkewe au familia yake. Mwanamume mbinafsi, mchoyo atatumia Muda wake kwa ajili ya faida yake mwenyewe na si mkewe wala familia yake. Kila mkewe au watoto wake wanapomuhitaji yeye ana jambo jingine anafanya linalomnyima mkewe na watoto wake Muda wa kuwa naye. Mwanaume huyu huwa na Muda na mkewe yeye anapokuwa anamuhitaji mkewe ila mkewe anapomuhitaji yeye, ooooh yuko bize kweli kweli. Ni shida tupu.
  3. Huficha mapato ya kazi za mikono yake kwa mkewe. Mwanaume anayeona shida kuweka wazi mapato yake kwa mkewe na watoto wake anakwepa jukumu la kuwatunza mkewe na watoto wake kikamilifu, mwanaume huyu ni mbinafsi, mchoyo. Ukimtunza mkeo kikamilifu kulingana na mapato yako atakutunza, vivyo hivyo kwa watoto wako, ukiwatunza, utakula matunda yao. Namba ya siri ya kadi yako ya benki isiwe siri kwa mkeo, na usiifiche kadi yenyewe ili mkeo asiione. Mkeo ajue mapato yako yote na shughuli zako zote zinazokuingizia kipato. Ukiwa tajiri msiri utakufa kimasikini ukiiacha familia yako ktk umasikini na utajiri wako kufaidi wengine kabisa. Weka wazi mapato yako na shughuli zako zinazokuingizia kipato.
  4. Hasikilizi ushauri wa mkewe na hamshirikishi mkewe ktk maamuzi yake au mipango yake. Mwanaume mbinafsi, mchoyo ni vigumu sana kukubali ushauri wa mkewe, haoni haja ya kushauriana na mkewe wala kumshirikisha mipango na maamuzi yake kabla, wakati na baada ya kupanga au kuamua. Atakacho amua basi ndicho hicho hata kama kinamuumiza mkewe na watoto wake, ilimradi kinamnufaisha yeye basi ataona kinafaa kufanya. Naomba ieleweke, mara nyingi tabia hii ya ubinafsi, uchoyo au choyo haianzi kwenye mahusiano ya ndoa tu, huanzia kwenye mahusiano ya uchumba. Kwa hiyo ni vyema kuwa mwangalifu.
  5. Huzungumza kuhusu yeye na hutaka wengine wazungumze kuhusu yeye tu. Mwanaume mbinafsi, mchoyo hujizungumzia yeye tu na hutaka na wengine wamzungumzie yeye. Hujizungumzia yeye mema na wengine huwazungumzia mabaya. Ukikaa naye mazungumzo yake ni mimi mimi mimi.... mpaka mwisho hatasema wewe na iwapo atasema ni wewe kwake.
  6. Huona vigumu kukutambulisha kwa watu. Hii inasababisha aone vigumu kutoka out na wewe, na iwapo itatokea mpo kwenye kusanyiko la watu, akipata nafasi ya kujitambulisha hatakutambulisha, atajitambulisha yeye tu. Na kwa sababu hiyo ili kuepuka hayo yote hatatoka na wewe kwenda popote na hatapenda kutangulizana nawe iwapo itatokea mmetoka wote.


Mungu akubariki.

Zoeken
Categorieën
Read More
NUMBERS
Verse by verse explanation of Numbers 2
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 31 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-24 14:09:28 0 5K
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 2
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 63 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-24 08:46:11 0 5K
DANIEL
DANIELI 2
Kulikuwa na sababu kwanini Mungu aliinyanyua Babeli kuwa taifa lenye nguvu kuliko yote duniani...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-05 23:30:33 0 10K
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Deuteronomy 27
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 06:44:41 0 5K
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 15
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 52 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:13:31 0 5K