UNYETI NA UZITO WA NDOA

Shalom mpendwa,
Leo ktk kona yetu hii nataka tuangalie unyeti na uzito wa ndoa kutokea ktk mahusiano ya Yesu (akiwa Bwana harusi) na kanisa (likiwa ni Bibi harusi). Awali ya yote, napenda nikujuze kuwa, ktk Biblia ndoa imefananishwa na mahusiano ya Yesu na kanisa, na kiini cha mahusiano hayo ni UPENDO usio na sababu, yaani, usiongoja sababu ili umfanyie mwenzi wake mambo mema. Kama uko kwenye ndoa au unatarajia kuoa au kuolewa siku za usoni, somo hili linakuhusu.
Kwa kuanza tuangalie kitabu cha Waefeso 5:22 - 33;
Ktk kifungu cha maandiko haya, Biblia inatuonyesha kuwa, uhusiano wa mume na mke ktk ndoa unafanana na uhusiano wa Kristo na Kanisa na msingi wake ukiwa ni UTII na UPENDO; tena ni Siri kubwa, au fumbo kubwa. Kwa sababu hiyo, yeyote anayetarajia kuingia au aliyemo ktk ndoa ni lazima ajue kuwa ndoa ni Siri kubwa, na ni uhusiano kama alionao Yesu na Kanisa, na kwa sababu hiyo utekelezaji wa majukumu ya kila mmoja ndani ya ndoa una uzito sawa kabisa na utekelezaji wa majukumu ya kila upande ktk mahusiano ya Kristo na Kanisa lake.
Kama vile kanisa linavyomtii Kristo, likaacha kufanya mapenzi yake, na kufanya mapenzi ya Kristo, ndivyo mke anapaswa kumtii mumewe, kiasi cha kuyaacha mapenzi yake na kufanya mapenzi ya mumewe.
Pia, mume ampende mkewe kwa kiwango kile kile cha namna Yesu alivyolipenda kanisa, kiasi cha kuvua utukufu na heshima yake aliyokuwa nayo mbinguni, akajitoa kwa gharama ya maisha yake kwa ajili ya kanisa. Mume naye ampende mkewe, avue heshima na utukufu wake, ayatoe maisha yote bila kubakiza chochote, kwa ajili ya mke wake. Amlishe, na amtunze, na amlinde mkewe kwa gharama yoyote ile hata kama ni gharama ya uhai wake.
Kama vile Kristo alivyo mwokozi wa roho zetu, mume naye ni mwokozi wa mwili wa mke wake. Kwa hiyo anatakiwa agharamikie matunzo yote ya mwili wa mke wake, ahakikishe mke wake anavaa vizuri, anakula vizuri, na analala vizuri ili mwili wake uwe na afya. Na ndio maana wewe mke au unayejiandaa kuwa mke unapaswa umtii mume wako ktk kila jambo ambalo si dhambi kwa Mungu.
Mwanamke, lazima uelewe kuwa mumeo ni kichwa chako kama Kristo alivyo Kichwa cha Kanisa, hivyo lazima umtii, yeye ndiye kiongizi wako. Mwanaume, lazima uelewe kuwa mkeo ni mwili wako kama vile Kanisa lilivyo mwili wa Kristo. Na kwa sababu hiyo unalazimika kuutunza. Hakuna awezaye kuupiga mwili wake, mtunze mkeo kama Kristo anavyolitunza kanisa.
Jamani, kama kuna dhambi itajayowapeleka watu jehanamu, basi, kwa wanaume ni dhambi ya kutowapenda wake zao kama Kristo alivyolipenda Kanisa; na kwa wanawake, ni kutowatii waume zao kama kumtii Kristo. Hapa wengi watanaswa.
Unataka kuoa, Je, uko tayari kumpenda mkeo kama Yesu alivyolipenda kanisa?
Unataka kuelewa, je uko tayari kumtii mumeo kwa kila jambo kama kanisa linavyomtii Kristo?
Mwanaume, upo tayari kuacha heshima na utukufu wako inapofika kwa swala la mkeo? Upo tayari kuacha uanaume wako na kujishusha mpaka chini na kuwa na hali aliyonayo mkeo ili umuokoe mwili wake kama vile Yesu alivyoacha uungu wake na kushuka mpaka chini akawa mwanadamu ili aokoe roho za wanadamu?
Mwanamke, je, upo tayari kuacha mapenzi yako, na matakwa yako na kufanya ya mwanaume kama vile kanisa lilivyoacha mapenzi yake na kufanya ya Kristo? Kama huwezi gharama hizi, hauko tayari kuoa au kuolewa. Jichunguze.
Kwetu sisi tuliomo ktk ndoa, je, mume anafanya hivyo? Je, mke anafanya hivyo? Kama hufanyi unamuumiza mwenzako, na una hatari ya kutokwenda mbinguni. Jichunguze.
Ndoa ni nyeti, na uzito wake ni uzito wa Yesu kwa kanisa lake. Usipokipa umuhimu alichokipa Mungu umuhimu, unatenda dhambi. Iheshimu ndoa, muheshimu mwenzi wako. Timiza wajibu wako kwa upendo usio na sababu. Ndoa huanza na wewe kwa ajili ya mwenzi wako, na si mwenzi wako kwa ajili yako. Usipofuata kanuni, utabomoa badala ya kujenga. Kama unataka ndoa iwe ya amani na mafanikio, fata kanuni hii.
Nakuombea, Mungu akupe kuelewa kanuni hii, akuwezeshe kutekeleza sehemu yako pasipo kusubiri wewe utekelezewe kwanza. Kwa wale wanaojiandaa, kuwa wanandoa, Mungu awape kujua na kutekeleza haya watakapoingia ktk ndoa. Ktk Jina la Yesu, amina.
Maandiko : Wafilipi 2:5 - 9; 1 Petro 3:1, 2, 7 - 9; |
Wafilipi 2:5 - 9;
Ktk maandiko haya tunajifunza kanuni nyingine inayotuonyesha unyeti na uzito wa ndoa. Kanuni hii ni alama kubwa ya upendo wa mwanaume kwa mke wake. Ikumbukwe ndoa imefananishwa na mahusiano ya Yesu na kanisa. Alichofanya Yesu kwa kanisa ndicho mume anapaswa kufanya kwa mkewe.
Tunachojifunza ktk andiko hili ni "Nia ya Kristo kwa kanisa lake" Nia hii ndiyo inapaswa kuwa nia ya mume kwa mkewe. Mwanaume anapaswa kuacha vyote vinavyompa heshima na utukufu na kufanya vile vinavyompa mke wake heshima na utukufu. Heshima na utukufu wa mwanaume uko kwa mkewe. Akitaka heshima na utukufu ni lazima ampe mkewe heshima na utukufu kwa kutimiza uhitaji wa mkewe. Aachilie uhitaji wake, badala yake ashuke chini mpaka kwenye uhitaji wa mkewe na kuutimiliza. Kama vile Yesu alivyofanya, aliacha utukufu wake juu akashuka chini ili atimize uhitaji wa mwanadamu; alifanyika laana ili tubarikiwe, alikataliwa ili tukubaliwe, alifanyika masikini ili tuwe matajiri, aliachilia utukufu na heshima alivyovihitaji zaidi akashuka mpaka chini ili kujibu uhitaji wetu. Vivyo hivyo mwanaume anapaswa kuachilia uhitaji wake na kujibu uhitaji wa mkewe.
Uhitaji wa mwanaume mbele ya uhitaji wa mkewe si kitu, kwa hiyo mwanaume lazima awe na nia ya kuachilia uhitaji wake ili atimize uhitaji wa mkewe. Usiwe mwanaume unajifikiria wewe, ktk kila jambo unalofanya mfikirie kwanza mkeo, tafuta kutimiza uhitaji wake kabla ya kutimiza uhitaji wako. Yesu alihimili mateso msalabani kwa sababu alikuwa anafikiria utukufu atakao upata kupitia utukufu wa kanisa utakaopatikana kwa Yesu kufa msalabani. Utukufu na heshima yako unapata kupitia utukufu wa mkeo unaompatia mkeo kwa wewe kutimiza mahitaji yake. Kwa hiyo, ukitaka ndoa yako idumu na impendeze Mungu, achilia uhitaji wako na ujibu na kutimiliza uhitaji wa mkeo.
1Petro 3:1 - 2;
Mwanamke, kutii kwako kunapelekea wewe kuwa na mwenendo mzuri kwa mumeo. Mwenendo wako mzuri unaotokana na utii wako kwa mumeo kutapeleke mumeo amwamini Yesu Kristo kama hajaamini bado. Kikubwa hapa ninachotaka kusema, ni mwenendo safi kwa mumeo ambao ni zao la utii wa mke kwa mumewe. Kama mwanamke hatakuwa mtii kwa mumewe basi atapoteza mvuto wake kwa mumewe kutokana na kutokuwa na mwenendo safi. Mwanamke atapoteza hata upendo wa mumewe kwake kwa tendo la kutotii. Kutii ni mbegu inayozaa mwenendo safi wa mwanamke mbele ya mumewe. Hivyo anapokosa utii kwa mumewe lazima atapoteza heshima yake kwa mumewe.
Mume anapaswa kuishi na mkewe kwa akili, na kumpa heshima kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima. Kwa nini, kwa sababu kama vile sisi kanisa tusivyoweza kufanya jambo lolote pasipo Yesu kwa sababu kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi kufanya lolote, ndivyo mwanaume anapaswa kufanya kwa mkewe. Aishi naye kwanza kwa akili ktk kumtimizia mahitaji yake yote, ya mwili, kihisia, na kiroho. Kama hawezi kufanya kwa sababu ni mke wake, basi afanye hivyo kwa sababu wao, yeye na mkewe ni warithi pamoja wa neema ya uzima. Iwapo mwanaume atashindwa kufanya hivyo, kuomba kwake kutazuiliwa. Hii ni siri kubwa na Mungu amechagua iwe hivyo.
Kama tunataka tufanikiwe ktk ndoa zetu hatuna budi kufuata kanuni hizi na kumuomba Mungu atufunulie siri hiyo.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS