AINA 8 ZA WANAWAKE WASIODUMU KWENYE MAHUSIANO

0
10K

Hakuna mtu anayependa kuachika au kuvunja mahusiano. Iwe mwanaume au mwanamke kitengo cha kuvunjika kwa mahusiano huleta majeraha ya moyo ambayo yasipotibiwa vema yanaweza kudumu mpaka kifo au kuathiri kabisa mfumo wa maisha ya mhusika. Bila shaka utakubaliana nami kwamba wapo watu walioamua kujiua kwa sababu ya mahusiano, wapo walioapa kwamba hawawezi kupenda tena, wapo walioamua kuwa walevi na makahaba kwa sababu ya kuachwa hasa na mtu ambaye alikuwa ‘wa moyo’ na wa kuaminika, lakini mbaya zaidi ni pale watu wanapofikia hatua ya kudharau uwepo wa Mungu eti kwa sababu aliyemfanyia ‘ufigisu’ ni mtu anayesemekana kuwa mtumishi mzuri wa Mungu. Sina wa kumtetea katika hili, ninachojua ni kwamba lolote linaweza kutokea, jambo la msingi ni kuchukua tahadhari.

Hatari kubwa ni pale mwanamke anapoachika mara kwa mara kiasi ya kufikia hatua ya kuwa sugu moyoni na kukosa tumaini kabisa, kujiona hafai, kuwa mtu wa kujihami, na kupoteza thamani ya upendo hata kwa watu wanaostahili upendo wake. Hatua hiyo ni mbaya sana kwa mwanaume atakayemuoa mwanamke wa aina hiyo kwa sababu ni mwanamke ambaye haoni umuhimu wa kupalilia mahusiano yake akiamini hakuna jambo zuri anaweza kumfanyia mwanaume akaridhika na kudumu naye (Hata kwenye ndoa). Ni kosa kubwa kukosewa na mwanaume mmoja, wawili au watatu ukaamua kuwaadhibu wanaume wote unaokutana nao. Maandiko matakatifu yanasema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa (Taz. Hosea 4:6). Ashukuriwe Mungu aliyenipa maarifa ambayo kwa sehemu naenda kushirikiana nawe.

Sababu za kuachika ni nyingi. Lakini leo sitazungumza kuhusu sababu hizo bali nitalenga aina za wanawake (kitabia) ambao wako kwenye hatari kubwa ya kuachika wanapoingia kwenye mahusiano ya uchumba au ndoa, au kwa lugha nyepesi ni wanawake ambao hawawezi kudumu kwenye mahusiano kiasi cha kufikia malengo. Mwanamke yeyote anaweza kuachwa katika hatua yoyote ile, yaani katika urafiki, uchumba au ndoa kutokana na uzito wa sababu kwa mwanaume. Hii haina maana kwamba Mungu anaruhusu talaka. Na kwa kweli kuvunjika kwa mahusiano si jambo jema hata kidogo. Tabia hizi nitakazokuonesha hapa zinarekebishika, iwapo tu mhusika akaamua kwa dhati kuziacha na pia akaomba mwenza wake amsaidie.

Nimeamua kuleta somo hili kwa sababu wanaume wengi wanawaacha wapenzi wao kwa sababu kadhaa, lakini ukichunguza kwa undani sababu hizo ni chambo tu bali ukweli hasa ni tabia za mwanamke ambazo mwisho wa siku mwanaume anagundua hawezi kuzimudu kwenye maisha yake, au atazimudu pasipo kufurahia maisha yake ya mahusiano. Mbaya zaidi ni kwamba wanaume wengi hutumia muda mfupi zaidi kumchunguza mwanamke kabla ya mahusiano. Wanapendelea kumsoma mtu akiwa naye ndani ya mahusiano. Kwa hiyo ewe mwanamke, usishangae kuachwa na kuanza kulalamika na kusema “Kwani mbona nilikuwa hivi tangu zamani”, hilo unajua wewe! Mwanaume wako amelijua baada ya kuwa nawe na hawezi kuvumilia. Unaweza kuwa na upendo wa dhati sawa, lakini usipojua baadhi ya mambo ambayo wanaume hawayapendi utaachika na pamoja na upendo wako. Naamini kwa kusoma makala hii utatoka hatua moja kwenda nyingine kiufahamu. Zifuatazo ni aina 8 za wanawake (kitabia) ambao wako kwenye hatari (risk) kubwa ya kuachika au ya kutodumu katika mahusiano:



1. Wanawake wenye tabia ya mamlaka.
Kwa bahati mbaya sana mfumo wa maisha kwa sasa unaruhusu wanawake kuwa viongozi na watawala sehemu nyingi. Hali hii inapoingia kwenye mahusiano huvunja nguvu za kisaikolojia na kimtazamo za mwanaume polepole. Tabia inapochanua ndipo mwanaume anatengeneza hali ya kujihami/kutetea uanaume wake na nafasi yake kama kiongozi wa familia. Atakapoona maji yanafika shingoni, si ajabu akaamua kuvunja mahusiano bila kusema sababu halisi ya maamuzi yake. Kwa asili, wanaume wamepewa na Mungu nafasi ya kuongoza na mamlaka(kichwa) bila kujali uwezo wao kiakili, kifedha au cheo. Mwanamke mwenye nia njema na mahusiano yake anapaswa kutambua nafasi yake na ya mwanaume wake kabla mambo hayajaharibika. Ni jambo la fedheha kumkuta mke anamtukana, anamsema vibaya au anamdharau mume wake, anamkaripia, na kumshurutisha mwenza wake. Mwanamke mkali (aggressive) anapoteza mvuto haraka kwa mwanaume. Mwanamke anapaswa kumstahi mumewe hata kama anajua ni mpumbavu (1 Samweli 25:23-25)


2. Wanawake wenye kiburi.
Hili ni tatizo kubwa sana kwa wanawake wengi wa kizazi cha sasa. Wanapenda kujiamulia mambo yao wenyewe, hawapendi ushauri, hawapendi kukosolewa. Wengi wao wanapokosolewa wanahisi kuonewa au kukandamizwa. Dhana hizi zimezaa kiburi. Kiburi ni kinyume cha kutotii, na katika hili maandiko yako wazi kabisa kwamba mwanamke imempasa kumtii mumewe. Hebu chukua mfano mdogo; katika uchumba kila jambo ambalo mwanaume anataka ulifanye wewe unakataa, tena unatoa sababu hazina kichwa wala miguu, na muda mwingine unapokuwa na sababu za msingi unatumia lugha ya jeuri, ni nani anakudanganya kwamba kuna mwanaume aliye tayari kuishi na mwanamke mwenye kiburi? Wengine uzuri wao umekuwa sababu ya kiburi ndio maana si jambo la ajabu kumuona mwanamke mwenye kila aina ya uzuri lakini hadumu kwenye mahusiano (Tazama Esta 1:13-20) Ukiona mwanamume anakuvumilia (hasa kwenye uhusiano ambao haujafikia ndoa) kuna mojawapo kati ya haya; Aidha anaamini utabadilika au hana mpango na wewe kwa hiyo haoni umuhimu wa kukukosoa. Hakuna haja ya kupeleka gari service wakati huna mpango wa kulitumia.

 

3. Wanawake wenye tabia au mwonekano wa kiume.
Nimewahi kukutana na wanawake wamevaa kama wanaume, wanaongea kama wanaume, wamenyoa kama wanaume, wanatembea kama wanaume nakadhalika. Kwa bahati mbaya wengine huenda mbali zaidi na kutafuta wapenzi wa kike ili wafanye nao usagaji. Hao sio walengwa wangu kwa leo. Hebu tutafakari kwa pamoja; kwa nini Mungu alituumba wanaume na wanawake? Mwanamke anapokuwa na tabia au mwonekano wa kiume, sio kwamba atakosa mwanaume, hapana, wanaume wengi wanaamini wanaweza kumbadilisha mwanamke kufikia kwenye viwango stahiki kulingana na njozi zao. Ukweli ni kwamba wanaume hawapendi mwanamke-mwanaume. Ladies! Wake up! We don’t marry men, we want women! Mwanaume mwenye malengo na wewe anataka kama mwanamke uwe na mwonekano wa kike, uongee kama mwanamke, uvae kama mwanamke, utembee kama mwanamke nakadhalika. Unaweza kushangaa sana unapoona mwanamke anakimbilia daladala kama vile mwanaume, mwanamke anabishana barabarani bila staha, na mengine mengi, kwa kweli haipendezi. Ukimpata mwanaume anayependa aina hiyo ya wanawake , akiamka usingizini utajuta. Mwanamke anapendeza akiwa mwanamke, na si vinginevyo hakuna nyongeza juu ya hilo. Au labda nikuulize dadangu, Je ungependa kuwa na mwanaume mwenye mwonekano au tabia za kike?

4. Wanawake wabishi
Hii ni aina nyingine ya wanawake. Wanaume wana majina mengi yanayoashiria tabia ya mwanamke mbishi. Utasikia mwanamke pasua kichwa, yaani mgumu kumueleza jambo akakubali. Wengi wao hufikiri kwamba wana akili kama au zaidi ya wenza wao. Wengi wao hujiona bora zaidi aidha kwa sababu ya elimu, pesa au historia za maisha yao. Wengine ni hulka tu iliyojengeka kutokana na mazingira waliyoishi au watu wanaoshinda nao muda mwingi. Tofauti ya ubishi na kiburi ni kubwa japokuwa kuna uhusiano mkubwa pia. Mwanaume anapenda akisema jambo likubalike, endapo utalipinga unahitaji kutumia hekima ili asijisikie vibaya, na wakati mwingine ni vizuri kukubali tu hata kama mwanaume ametoa ushauri wa kijinga, hii itaboresha mahusiano yako. Unaweza kuepusha hatari ya matokeo ya maamuzi ya mumeo halafu ukashindwa kuepesha hatari ya kuvunjika kwa ndoa yako. Usiwe mwepesi wa kusema, usiwe mwepesi wa kukasirika/kununa, usiwe mwepesi wa kubisha. Kitu cha ajabu juu ya tabia ya ubishi ni kwamba ukiiendekeza unafikia hatua ya kubisha hata jambo la maana au jambo la kweli. Mwanaume anapenda kuwa na mwanamke msikivu, mtiifu na mshauri mzuri mwenye hekima.

5. Wanawake wasiojali.
Kundi hili pia limezaliwa kipindi cha kizazi kipya. Ni wanawake wasiojali habari za mpenzi wake. Katika ndoa wanawake wa jinsi hii husababisha malezi mabaya ya watoto kwa sababu hukosa tabia ya kusisitiza alichosema baba kwa watoto. Katika mahusiano ya kawaida mwanaume anatamani aone uwepo wa mwanamke katika mambo yake. Sasa ni jambo la kufikirisha kidogo pale unampata mwanamke hajui mchumba wake anajishughulisha na nini, ana ndoto gani, ana mipango gani, kwa nini yuko pale alipo, ana kipato gani, anapenda nini nakadhalika. Si ajabu kuona watu wako kwenye mahusiano lakini kila mtu ana mambo yake kimya kimya. Kwa wanaume wanaweza wasitake kujua kwa undani shughuli nyingi za mwanamke kwa dhana kwamba anataka kukutunza kwa hiyo unachopata ni kwa ajili yake(dhana hii kwa mtazamo wangu ni dhaifu), lakini mwanaume anapoona hujawahi kumpa mawazo juu ya kazi zake, afya yake, familia yake, marafiki zake (yaani chochote anachofanya kwako wewe ni sawa) ataanza kuingiwa na wasiwasi endapo utakuwa msaada wake au mzigo, kumbuka jambo hili; mwanaume anapoanzisha mahusiano anatafuta msaidizi sio mzigo, unaposhindwa kuwa msaada wake lazima atafanya maamuzi mapya.

 

6. Wanawake wasioendana na ndoto.

Mwanaume yeyote anatamani ndoto yake itimie. Kwa bahati mbaya sana ni wanaume wachache wanaoweza kuwaza kwamba hata wanawake nao wana ndoto wanazotamani kuzitimiza. Binafsi naamini watu wenye ndoto mbili lazima watapishana tu, kwa hiyo huwa nashauri watu wa namna hiyo wakae chini na kutengeneza ndoto moja ili washirikiane kwa pamoja kuitimiza. Inapotokea mwanamke hakubaliani na ndoto za mwanaume au anakubaliana lakini hana mchango wowote kwenye ndoto ile halafu kwa bahati mbaya mwanaume akamuona mwanamke mwingine ambaye yuko tayari kuona ndoto yake inatimia, basi shimo la uharibifu huongezeka kina chake kwa kasi kubwa. Mungu alimuumba mwanaume mwenye ndoto (vision), akamfanyia msaidizi wa kufanana/kuendana naye. Ni wakati wako mwanamke kuamka na kujifunza kuhusu mwanaume, nini anataka kwenye maisha yake, kaa chini muulize halafu tafakari ni hatua gani utachukua kumsaidia badala ya kupeleka hoja za kutaka ufanyiwe mambo kibao kwenye maisha yako.​


7. Wanawake watetezi wa usawa (Feminists)

Mada hii imeleta mgongano wa mawazo na mtawanyiko wa mitazamo kati ya wanaume na wanawake walio wengi. Binafsi sipati shida sana kuelewa kwamba kuna wanawake wenye uwezo mkubwa kuliko wanaume. Sipati shida pia kuelewa kwamba wapo wanawake wanaotamani kuwa juu ya wanaume, achilia mbali suala la usawa ambalo kwa sasa linapiganiwa kila sehemu. Swali la kujiuliza ni kwamba wanawake hawa wanaodai usawa wanataka usawa kwenye mambo yapi hasa? Kwa mfano, mwanamke ni binadamu kama alivyo mwanaume, ana mahitaji muhimu kama ya mwanaume, wakati mwingine zaidi; wanaponyimwa haki zao za msingi naamini wanakuwa sahihi kudai haki hizo, lakini endapo watadai kwa hekima. Linapokuja suala la nafasi ambazo Mungu ametoa kwa mwanaume na mwanamke usawa sio ajenda muhimu kwa sababu kila mtu ana nafasi yake kwa ajili ya kumfaa mwingine na kwa makusudi ya Mungu. Tatizo ni pale wanaume wanapowadharau wanawake na nafasi zao, hapo ndipo wanawake hutamani kushika nafasi za wanaume ili kuepukana na dharau hizo. Lakini kwa kuwa kufanya hivyo sio jambo la asili, (mwanamke kuwa sawa au kuwa juu ya mwanaume) mahusiano mengi yamejikuta kwenye migogoro isiyokwisha. Jiulize tu kwa nini ndoa za zamani zilidumu zaidi ya hizi za leo? Utagundua kuwa wanawake walikuwa na heshima, walikuwa watii, na walifanya yawapasayo kufanya kwenye nafasi zao badala ya kupambana na waume zao. Ukielewa nafasi yako kama mwanamke, huwezi kuachika.
 
8. Wanawake wenye tabia ya Kulalamika.

Mwanaume yeyote angependa kuwa na mwanamke anayeridhika, anayetia moyo, anayetambua juhudi za mwanaume wake na mwanamke ambaye anavumilia wakati wa shida. Kwa kweli kuna wanawake hata kama ‘utawapeleka mwezini’ hawawezi kuridhika, wao hulalamika tu, wamejawa na mtazamo mbovu (wrong attitude), jambo dogo tu ataalamika siku nzima, akiudhiwa anaweza kununa na kukatisha mawasiliano siku nzima, siku mbili, tatu hata wiki zima. Mara nyingi wanawake wa jinsi hii wana tabia mbili zinazosababisha haya, ya kwanza si wepesi wa kusamehe nay a pili ni tabia ya kujilinganisha na wengine. Kwa hiyo mwanaume pasipo kujua analinganishwa na wanaume wengine siku zote ataonekana hafanyi ipasavyo. Lawama zinapokuwa sehemu ya maisha ya mahusiano yenu, mwanaume taratibu anapoteza ladha ya mapenzi na kuamua kuvunja uhusiano.​


Hitimisho

Binafsi siamini usemi kwamba tabia ni kama ngozi, naamini hakuna tabia isiyobadilika. Hatua ya kwanza kubadili tabia yako ni kumsihi aliyekuumba ahusike ndipo nia ya dhati na juhudi vifuate. Maisha ya mahusiano yanahitaji maelewano, mapatano na mawasiliano bora ndio nguzo kuu ya mahusiano bora. Naamini kwa mwanzo huu unaweza kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza mahusiano yako, kukaza nati zilizolegea na kuweka spea mpya. Mungu akitupa nafasi tutaangalia na upande wa wanaume. Naamini ningeweza kuandika mengi lakini kwa sasa hebu tushirikiane haya machache hadi wakati mwingine tena. Hongera kwa kufauatana nami na Mungu akubariki sana, nakupenda!!!!​
Cerca
Categorie
Leggi tutto
SPIRITUAL EDUCATION
THE SPIRIT OF TRUTH
John 14:16-17 is written “And I will ask the Father, and He will give you another...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 07:33:12 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
NAMNA YA KUMTUMIA ROHO MTAKATIFU KAMA MSAIDIZI KUPITIA KAZI ZAKE
Yohana 14:16-18 … Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:56:52 0 5K
UCHUMBA KIBIBLIA
MAMBO YA KUFANYA/KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA UCHUMBA
Mpenzi msomaji tunakusalimu kwa jina la Yesu! Baada ya kuwa tumepata maombi ya vijana wengi...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-23 07:25:47 0 6K
OTHERS
YESU HAKUWA MUISLAM
USHAIDI WA KIBIBLIA NA KORAN Waumini wa dini ya Kiislam wamekuwa na tabia ya kuseka kuwa, eti,...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 08:09:35 0 5K
JOSHUA
Verse by verse explanation of Joshua 19
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 08:25:49 0 5K