SEHEMU YA 3: MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

0
5KB

Bwana asifiwe!! Unaweza kusoma SEHEMU YA 1, SEHEMU YA 2, SEHEMU YA 4 au SEHEMU YA 5 ya somo hili, au unaweza kuendelea kusoma sehemu hii ya 3 uliyopo.

Cho chote kinachojengwa nje ya msingi kipo nje ya utaratibu wa kawaida, hata kama katika jamii ya watu kinaonekana ni kawaida kukifanya, na kwa sababu hiyo hakina mpangilio sahihi wenye manufaa, hakiko thabiti, imara na kwa hiyo hakiwezi kuaminiwa, kutegemewa wala kutumainiwa, na siyo kielelezo cha maisha tunayopaswa kuishi. Tena, badala ya kujenga hubomoa, badala ya kufurahisha huumiza, na badala ya kuganga hujeruhi.

Ni muhimu sana tukafahamu kuwa, ndoa ni uhusiano unaoanzishwa juu ya misingi ya ki-Mungu kwa sababu Mungu ndiye aliyeianzisha taasisi hii, na tangu mwanzo aliianzisha katika misingi ya Neno lake. Mambo yote yatabadilika na kupita, lakini Neno lake ladumu milele.

MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA.
Tayari tumekwisha angalia misingi miwili katika mfululizo wa somo letu hili, sehemu ya kwanza na ya pili, na sasa katika sehemu hii ya tatu napenda tuangalie msingi mwingine zaidi.

3. Biblia imekataza kuachana/kutalikiana (talaka) mara tu baada ya wawili kuingia kwenye ndoa.
Marko 10:2 - 12; Mathayo 19:3 - 9;

Kama kuna jambo kuhusu uhusiano wa ndoa ambalo Mungu hapendi, a nachukia, ni kuachana. Yeye ni Mungu ashikaye maagano, ni Mungu wa maagano, yeye hudumu kwenye maagano. Yeye ni chanzo cha mahusiano chanya yote ya kimaagano ikiwa ni pamoja na uhusiano wa kiagano wa ndoa. Lakini pia yeye ni shahidi mwaminifu wa milele wa mahusiano haya ya kiagano. Moja ya jambo pekee linalohusiana na mahusiano haya ya kiagano ni kuwa, Mungu alikusudia yawe ni ya kudumu, ya wakati wote, ya milele, ya daima, yasiye ya kuvunjika, ndiyo sababu yana agano kama msingi na kiini cha mahusiano hayo. Kuachana au kutalikiana siyo kusudi la Mungu tangu mwanzo; haikuwa hivyo tangu mwanzo. Na kwa hiyo, Mungu anachukia.

Malaki 2:13-16

[13]Tena mnatenda haya nayo; mnaifunikiza madhabahu ya BWANA kwa machozi, kwa kulia na kwa kuugua, hata asiiangalie tena hiyo dhabihu, wala kuitakabali mikononi mwenu na kuiridhia.

[14]Lakini ninyi mwasema, Ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu BWANA amekuwa shahidi kati ya wewe na mke wa ujana wako, uliyemtenda mambo ya hiana, angawa yeye ni mwenzako, na mke wa agano lako.

[15]Hakuna mtu mmoja aliyetenda hivi, ambaye alikuwa na ufahamu kidogo. Au je! Kuna mtu mmoja atafutaye mzao mwenye kumcha Mungu? Kwa hiyo jihadharini roho zenu; mtu awaye yote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana.

[16]
Maana mimi nakuchukia kuachana, asema BWANA, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema BWANA wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana.



MAMBO YA KUEPUKA ILI KUTUNZA MISINGI YA IMANI KABLA NA BAADA YA KUINGIA KWENYE NDOA.

1. Epuka kuanzisha mahusiano kwa kufuata mihemuko ya kihisia, badala yake anzisha mahusiano kwa kufanya maamuzi ya kudumu na uchaguzi wa kudumu. Uwe na uhakika na unachokifanya ukijua kuwa hakuna kuachana. Msukumo wa maamuzi yako ya kuoa/kuolewa iwe ni upendo katika kweli.

Uhusiano wa ndoa umefananishwa na uhusiano wa Yesu Kristo na kanisa lake. Ni picha ya uhusiano wa Yesu Kristo na mfuasi wake. Ni uhusiano wa kimaamuzi na kiuchaguzi. Na maamuzi mtu anayofanya yanapaswa yawe maamuzi yasiyokuwa na kipengele cha kuangalia nyuma kwa nia ya kugeuka na kuacha kufuata. Ni maamuzi ya msingi sana yanayopelekea kubadilika kwa mtindo wa maisha ya mtu. Ni maamuzi ya kudumu na mtu mmoja maishani kwa gharama yo yote. Sikiliza Yesu Kristo akimwambia mfuasi wake aliyechagua kuwa naye:

Luka 9:61-62

[61]Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.
[62]Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.


Ikiwa umetia nia ya kuoa au kuolewa na kisha kuangalia nyuma (kufikiri kuwa iwapo utakutana na shida yo yote basi unaweza kumwacha) bila shaka wewe haufai kwa ndoa. Kuliko kuoa au kuolewa ukiwa na nia ya kutalikiana, ni bora ukaacha kabisa kwa sababu wewe haupo tayari kulipa gharama za kulitunza agano hili la upendo la ndoa.

2. Epuka kuanzisha mahusiano kwa kufuata (ushawishi wa) hali na mazingira na badala yake, anzisha mahusiano kwa kufuata ukweli na uhalisia.

Yesu mahali pengine akiwaonyesha wafuasi wake uzito wa uhusiano wake na wao ambao ulitegemea sana machaguzi, maamuzi na kujitolea kwao kumfuata Yesu Kristo, anawaambia gharama wanayopaswa kuichukua katika kuhusiana na yeye, anasema,

Luka 9:23-24

[23]Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.
[24]Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.


Mihemuko ya kihisia, hali na mazingira havina nafasi kabisa katika kuanzisha aina hii ya uhusiano. Ni lazima msukumo wa kufanya hivi uwe ni upendo hasa unaoambatana na uchaguzi na uamuzi katika kweli na si nje ya hapo, la sivyo unatengeneza hatari ya kuachana hapo baadae.

3. Epuka kuanzisha mahusiano na mtu usiyemjua ambaye huna uhakika kama utawezana naye katika kipindi chote cha maisha.

Usioe wala usiolewe na mtu usiyemjua tabia yake, haiba yake, na imani yake. Mtu usiyemjua atakuwa ni tatizo kwako si kwa sababu yeye ni tatizo, ila kwa sababu wewe hukumjua, ulimdhania kuwa ni mtu wa namna fulani na kumbe ni mtu mwingine kabisa tofauti na ulivyomdhania.

Hesabu 36:6

[6]BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao.


Ni kweli unampenda naye anakupenda, je unamjua (ni jamaa ya kabila ya baba yako)? Haitoshi tu ninyi kuwa na hisia za upendo kila mmoja kwa mwenzake, mbali na hisia hizo ni vyema mkatangulia kwanza kujuana. Kifungu hiki cha maandiko kinahusu agizo la Bwana kwa binti wa Selofihadi kuwa waolewe na waume wawapendao lakini waolewe na jamaa za baba zao. Hawa jamaa za baba zao ni watu wanaowajua, si jamaa ngeni kwao. Ni watu wanaoishi nao, wanahusiana katika maisha yao ya kila siku kabla ya kuingia kwenye uhusiano wa ndoa. Si wageni kwao. Kabla hawajaingia kwenye mahusiano, walitangulia kujuana kwanza. Kwa hiyo, miongoni mwa jamaa za baba zao (watu wanaowajua) waolewe na waume wawapendao.

Mjue kwanza kabla ya kuanza naye uhusiano wa uchumba hadi ndoa usije ukajikuta utaka kutoka mahali ulipoingia kabla ya kifo kuwatenganisha.

4. Epuka ushawishi wa watu juu ya nani umwoe/uolewe naye au usimwoe/usiolewe naye badala yake kama unaoa/unaolewa iwe ni baada ya wewe mwenyewe kuridhia na kuamua kwa dhati.

Uamuzi wa kuoa au kuolewa ni wa mtu binafsi bila ya kushawishiwa na watu la sivyo hataweza kukabiliana na gharama anayopaswa kulipa. Kwa hiyo, kwa sababu uhusiano wa ndoa ni maisha binafsi ya mtu na mwenzi wake, ni lazima achague na kuamua mwenyewe ili aweze kuwajibika kwa maamuzi na machaguzi yake mwenyewe.

5. Epuka kuwa na moyo mgumu.

Yesu alisema, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, Musa aliruhusu talaka. Kutokuwa tayari kusamehe, kusamehewa na kutaka suluhu ni sababu ya msingi ya kuwepo kwa talaka. Kama hutaki talaka, kuwa tayari kusamehe na kutafuta suluhu.

Mathayo 19:7-8

[7]Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
[8]Akawaambia, Musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi.


6. Epuka kuachana.

Kama kuna kitu unapaswa kukilinda katika uhusiano wako wa ndoa ni ushirika wenu wa karibu, ndoa yenu, baina yako na mwenzi wako. Usiwe mwepesi kuwaza kuachana unapopitia shida, dhiki, masumbufu, na taabu. Ndoa ni uhusiano wa kudumu, na Mungu anachukia kuachana, hivyo epuka kuachana kwa gharama yo yote.

NINI HUTOKEA WANANDOA WANAPOACHANA.

1. Mungu huchukia,
Mungu hapendezwi na kuachana, kwa hiyo wanandoa wanapoachana Mungu huchukia. Kwa nini, kwa sababu agano la ndoa linakuwa limekiukwa, na wahusika wanakuwa wameasi agano lake.

2. Wanandoa huwa wazinifu isipokuwa wamekaa katika hali ya kila mmoja kuwa pekee bila kuoa au kuolewa tena mpaka mmoja wao atakapokufa.

3. Kutoa picha mbaya ya uhusiano wa Kristo na kanisa.

Uhusiano wa ndoa ni picha ya uhusiano wa Kristo na kanisa lake. Wanandoa wanapoachana uharibu picha hii nzuri ajabu ya uhusiano wa Kristo na kanisa lake. Matokeo yake upendo wa Kristo kwa watu wake hushindwa kudhihirika.

4. Husababisha mkanganyiko kwa waamini ndani ya kanisa kuhusiana na ndoa, na hasa tendo hili linapobarikiwa na viongozi ndani ya kanisa na kupelekea mwili wa Kristo kutukanwa.

5. Mara nyingi familia za wawili hawa huingia katika migogoro na chuki.

6. Iwapo wawili hawa wana watoto, husababisha migogoro ya kinafsi kwa watoto hawa na kukosa malezi ya pamoja ya wazazi wao. Watoto hubaki katika hali ya kuchanganyikiwa.

Tutaendelea na sehemu ya nne ya somo hili.

Mungu akubariki sana.

Pesquisar
Categorias
Leia mais
NDOA KIBIBLIA
USIDANGANYIKE, MATUMIZI YA VIDEO ZA NGONO KWA WANANDOA NI DHAMBI
Shalom wapendwa, Leo katika kona yetu hii ya Mahusiano, uchumba na Ndoa napenda tuangalie juu ya...
Por GOSPEL PREACHER 2021-11-06 20:56:12 0 6KB
OTHERS
A’isha: Mke wa Muhammad Mwenye Miaka Tisa
Watu wengi wamesema kuwa Muhammad alifanya tendo la ndoa na mke wake mwenye umri mdogo zaidi,...
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 05:41:42 0 10KB
JOB
Verse by verse explanation of Job 21
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 25 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-04-03 03:51:31 0 5KB
NUMBERS
Verse by verse explanation of Numbers 12
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 26 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-24 14:36:34 0 5KB
BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
7 BIBLICAL PRINCIPLES OF MONEY MANAGEMENT
The 7 Biblical Principles of Money Management that you are about to learn were...
Por BIBLICAL FINANCES 2021-12-29 15:38:36 0 15KB