SEHEMU YA 2: MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

0
5KB

Bwana asifiwe!! Unaweza kusoma SEHEMU YA 1, SEHEMU YA 3, SEHEMU YA 4 au SEHEMU YA 5 ya somo hili, au unaweza kuendelea kusoma sehemu hii ya 2 uliyopo.

Mahusiano ya uchumba hadi ndoa katika Imani, yaani wokovu ni mahusiano yanayojengwa katika misingi ya kiimani ambayo imeonyeshwa waziwazi katika Biblia takatifu ambayo ni Neno la Mungu lililohakikishwa. Ili yaweze kumpendeza Mungu, kuwa thabiti, na kutimiza kusudi lake la ki-Mungu ni lazima yaanzishwe au yajengwe kwa kuzingatia msingi wa Neno la Mungu. Ni mfano wa mtu aliyejenga vizuri nyumba yake juu ya mwamba, upepo, tufani, na tetemeko vinapokuja nyumba hiyo husimama imara.

Tayari katika sehemu ya kwanza tuliangalia msingi wa kwanza wa kiimani katika mahusiano ya uchumba hadi ndoa. Leo nataka tujifunze zaidi kwa kwenda mbele zaidi.

MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA.

2. Biblia imekataza ngono kabla ya ndoa na nje ya ndoa, kwa kuwa tendo hilo ni tendo la kiagano, na ni mahususi na takatifu kwa wanandoa; linapofanyika nje ya ndoa au kabla ya ndoa tendo hilo huwa dhambi kwa Mungu.

Waebrania 13:4

[4]Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.


Mungu aliumba ngono (tendo la ndoa). Tendo hili lenye kuleta kujisikia na msisimko wa namna yake ni maalumu sana na takatifu kwa wanandoa. Biblia inasema kuwa, Mungu alikifanya kila kitu kizuri kwa wakati wake. Hii maana yake ni kuwa, kila kitu huwa kinafaa kwa matumizi yasiyo na madhara ndani ya wakati wake mahali pake na si nje ya wakati wake au mahali pake. Ngono ni tendo zuri ndani ya ndoa baina ya mke na mume; huo ndio wakati wake na mahali pake, nje ya hapo si tendo zuri, ni dhambi ya uzinzi na uasherati (zinaa) na kwa hiyo huleta mauti.

MAMBO YA KUEPUKA ILI KUTUNZA MISINGI YA IMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA.

Kijana mwamini anapaswa aepukane na mambo yafuatayo ili asimkosee Mungu kwa kufanya ngono kabla ya ndoa na kutunza misingi ya kiimani katika kipindi chote cha mahusiano ya uchumba hadi ndoa:

1. Epuka mahusiano yanayohusisha kushikana shikana kimahaba. Yatosha mahusiano yenu kuwa na heshima na nidhamu ya kaka na dada mpaka pale mtakapooana.

Wimbo Ulio Bora 2:5-7

[5]Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera,
Kwa maana nimezimia kwa mapenzi.
[6]Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,
Nao wa kuume unanikumbatia!

[7]Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,
Kwa paa na kwa ayala wa porini,
Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,
Hata yatakapoona vema yenyewe..


Ngono ni mwako wa tamaa mwilini unaodai kutoshelezwa pindi unapoamshwa na kuchochewa. Tamaa hii inatabia moja na moto katika mafiga. Moto huzimika unapokosa kuni na mchochezi, kadhalika ngono tamaa zake huzimika zinapokosa mchochezi. Kushikana-shikana na kukumbatiana kimahaba huchochea mapenzi (matamanio ya kingono, hanjamu au ashiki za kingono). Vijana ambao wapo katika mahusiano ya uchumba ili kutunza na kulinda imani yao, ni muhimu sana na lazima wakaepuka aina hii ya mwenendo katika mahusiano yao hayo; wasishikane-shikane na kukumbatiana kimahaba.

2. Epuka mazingira ya faragha yanayowatenga ninyi wawili peke yenu na watu wengine kama vile nyumbani kwa mwanamke au kwa mwanaume, au sehemu nyingine yo yote.

Wimbo Ulio Bora 3:3-5

[3]Walinzi wazungukao mjini waliniona;
Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu?
[4]Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea,
Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu;
Nikamshika, nisimwache tena,
Hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu,
Chumbani mwake aliyenizaa.

[5]Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu,
Kwa paa na kwa ayala wa porini,
Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha,
Hata yatakapoona vema yenyewe.


Mithali 5:3,8

[3]Maana midomo ya malaya hudondoza asali,
Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
[8]Itenge njia yako mbali naye,
Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.


Faragha baina ya mwanaume na mwanamke wawili peke yao ni kichocheo kingine cha hanjamu (matamanio ya kimapenzi/ngono). Mazingira haya ni hatari sana kwa wachumba kwa sababu huwa na mvuto wa kimapenzi katika fikira za wahusika unaoamsha hanjamu au ashiki au matamanio ya kingono. Wawili (mwanaume na mwanamke) wanapokuwa faragha peke yao fikira zao huvutwa na kuelekea kwenye ngono. Kwa hiyo ili kulinda imani yao ni muhimu sana wakaepuka faragha zinazowabakiza wawili peke yao na kuwapa uhuru wa kufanya mambo ya kimahaba na ngono.

3. Epuka matumizi ya maneno ya kimahaba kwa mwenzi wako.

Mithali 7:13,21

[13]Basi akamshika, akambusu,
Akamwambia kwa uso usio na haya,
[21]Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi,
Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.


Maneno huamsha hisia yanapozungumzwa na pia hutengeneza picha ya tendo katika fikira za mtu yanapozungumzwa na kusikiwa. Maneno ya kimahaba huwa na ushawishi wa kimapenzi, huamsha hisia na matamanio ya kingono yanapozungumzwa hasa na wapenzi (wachumba).

Wachumba wanapokuwa wakihusiana ili kulinda imani yao ni muhimu sana wakaepuka maneno ya kimahaba yanayochochea ngono. Katika kuhusiana kwao ni muhimu sana wakafanya uchaguzi wa maneno wanayoambiana kila mmoja akielezea hisia zake juu ya mwenzake, jinsi anavyomsifia mwenzake nk. Wahusika wanapaswa waweke akiba ya maneno, kuwe na mipaka ya mazungumzo na maneno wanayoambiana ili wasijikute katika jaribu la uasherati. Lugha yao wakati wa uchumba izingatie heshima ya kaka na dada kulinda imani yao au wokovu wao.

4. Epuka kusoma makala au machapisho ya kingono (maudhui ya ponografia).

Makala au machapisho ya ngono huamsha hisia na matamanio ya kimapenzi. Machapisho haya hutengeneza picha na kuzikuza katika fikira za muhusika na mwisho wa siku wazo la kutekeleza matamanio hayo huumbika ndani ya fikira hizo, kisha mtu hutoa nia au huazimu kufanya hivyo akitawaliwa na wazo hilo lenye msukumo wa tamaa nyuma yake. Katika hatua hii ni rahisi sana kufanya ngono nje/kabla ya ndoa.

5. Epuka kuangalia picha na video za ngono.

Kama ilivyo kwa makala na machapisho yaliyobeba maudhui ya ngono, ndivyo ilivyo kwa picha na video za ngono, huchochea mapenzi. Ni lazima zikaepukwa ili kulinda imani.

6. Epuka mazungumzo ya ngono.

Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema; epuka mazungumzo na rafiki zako yanayozungumzia ngono. Tabia ya mazungumzo huharibu fikira na nafsi ya mtu taratibu kwa kadiri anavyozungumza na huchochea matendo yatokanayo na mazungumzo husika. Ni muhimu ukajiepusha na mazungumzo yatakayochochea ngono.

Mambo yote haya yanachochea na kuhamsha mapenzi au hanjamu (hamu na shahuku za kingono (matamanio). Kwa hiyo ni vyema yakaepukwa na kukimbiwa.

1 Wakorintho 6:18

[18]Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.


Mazingira haya yote yanayochochea zinaa ni ya kukimbiwa. Moto pasipo mchochezi huzimika kadhalika ngono au zinaa pasipo mazingira chochezi huzimika.

Mithali 26:20

[20]Moto hufa kwa kukosa kuni;
Na bila mchongezi fitina hukoma.


NINI HUTOKEA KIJANA ANAPOFANYA NGONO KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA, NJE AU KABLA YA NDOA.

1. Muunganiko wa kinafsi; ngono ni tendo linalowaunganisha wahusika nafsi zao hata kuwa kitu (mwili) mmoja. Sehemu ya huyu inabaki kwa huyu na sehemu ya yuhu inabaki kwa huyu.

1 Wakorintho 6:15-17

[15]Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!
[16]Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.
[17]Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.


Madhara ya muunganiko huu wa kizinaa (ngono nje/kabla ya ndoa) ni kuwa unachafua malazi. Kitanda cha wanandoa kinakuwa na nafsi zaidi ya mbili kwa kuwa nafsi ya mke au mume inakuwa imeungwa na wote aliofanya nao uasherati. Kwa hiyo, nafsi za hao wote zinajidhihirisha kitandani katika fikira na mawazo ya muhusika awapo na mume au mke wake. Hii huchafua malazi ambayo kwa kweli yanapaswa yawe safi kwa wanandoa.

2. Linachafua malazi (kitanda cha ndoa). Kwa sababu ya muunganiko wa kinafsi, malazi (wakati wa tendo la ndoa) baada ya kuoa au kuolewa huwa machafu kwa uasherati na uzinzi kwa kuwepo kwa nafsi za wapenzi wa kingono wa zamani. Hii nineifafanua zaidi katika hoja ya kwanza hapo juu.

3. Linaondoa heshima ya kijana na miaka yake ya kuishi.

Mithali 5:3,8-9

[3]Maana midomo ya malaya hudondoza asali,
Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
[8]Itenge njia yako mbali naye,
Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
[9]Usije ukawapa wengine heshima yako,
Na wakorofi miaka yako;


4. Linaondoa au kutawanya nguvu za kijana (hususani mwanaume).

Mithali 5:3,8,10

[3]Maana midomo ya malaya hudondoza asali,
Na kinywa chake ni laini kuliko mafuta;
[8]Itenge njia yako mbali naye,
Wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.
[10]Wageni wasije wakashiba nguvu zako;
Kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni;


Fahari ya kijana ni nguvu zake. Mithali 20:29.

5. Linapelekea mauti ya kiroho (kabla ya mauti ya kimwili).

Mauti ya kiroho ni pale dhambi ya zinaa inapokutenga wewe na Mungu na kuuficha uso wa Mungu usione. Dhambi yo yote inamtenga mtu na Mungu, hii inatajwa na Biblia kuwa ni mauti (ya kiroho).

6. Linatukanisha mwili wa Kristo kwa sababu limebeba ushuhuda mbaya kinyume cha imani.

Kwa kuwa tendo hili si maadili ya kikristo na pia ni kinyume cha maadili ya jamii zetu nyingi tu, vijana waliookoka wanapojihusisha na mwenendo wa namna hii (ngono kabla au nje ya ndoa) hupelekea wasioamini walitukane kanisa yaani mwili wa Kristo na wokovu kwa ujumla.

7. Linapelekea hukumu na adhabu kutoka kwa Mungu.

Waebrania 13:4

[4]Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.

Mungu akubariki sana. Tutaendelea na sehemu ya tatu.

Love
1
Pesquisar
Categorias
Leia mais
LEVITICUS
Verse by verse explanation of Leviticus 19
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 95 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-24 10:22:54 0 6KB
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 8
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
Por THE HOLY BIBLE 2022-01-21 03:07:14 0 5KB
Injili Ya Yesu Kristo
JIHADHARI USIANGUKE TENA ILI USITENGWE NA MUNGU
Na: Patrick & Bernada Sanga Shalom, neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu...
Por GOSPEL PREACHER 2021-11-23 12:36:12 0 5KB
OTHERS
ALLAH ANASEMA KATIKA KORAN KUWA WAISLAM WOTE WATAINGIA JEHANNAM
Jamani huu ni Msiba katika taifa la Islam kwa kushindwa kusoma aya hii ambayo ipo wazi (Quran...
Por MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 08:48:28 0 7KB
CHEKECHEA
CHEKECHEA 2
Orodha ya masomo ya chekechea  kwa darasa la wakubwa
Por PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 10:08:03 0 5KB