SEHEMU YA 1: MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA

0
5Кб

Bwana asifiwe!! Unaweza kusoma SEHEMU YA 2, SEHEMU YA 3, SEHEMU YA 4 au SEHEMU YA 5 ya somo hili, au unaweza kuendelea kusoma sehemu hii ya 1 uliyopo.

Mahusiano ya uchumba hadi ndoa katika Imani (Wokovu) yana misingi yake na mwongozo wake katika Biblia. Biblia imetolea maelezo ya namna ya kuendesha mahusiano hayo baada ya kuchumbiana. Mahusiano haya ambayo yanaunda ndoa ya kikristo ni tofauti na mahusiano yale yanayoanzishwa nje ya Imani (Wokovu).

Ni muhimu sana tukafahamu kuwa, mahusiano ya ndoa ni mahusiano nyeti sana kwa sababu yamefananishwa kwa karibu sana na mahusiano ya Mungu na watu wake (taifa la Israeli) katika Agano la Kale, na katika Agano Jipya mahusiano haya yamefananishwa kwa karibu sana na mahusiano ya Yesu Kristo na Kanisa lake. Hii ndiyo sababu Biblia imetoa misingi ya kuanzisha na kuendesha mahusiano haya katika usafi, utakatifu, uaminifu, utii, unyenyekevu na upendo.

MISINGI YA KIIMANI KATIKA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA.

1. Biblia imekataza uhusiano wa kiagano (kindoa) pamoja na mtu asiye amini. Hii ni kwa sababu ndoa pia ni uhusiano wa kiimani; unahusisha miungu.

2 Wakorintho 6:14-17

[14]Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

[15]Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari?
Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

[16]Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

[17]Kwa hiyo,
Tokeni kati yao,
Mkatengwe nao, asema Bwana,
Msiguse kitu kilicho kichafu,
Nami nitawakaribisha.


Ndoa ni moja ya uhusiano ambao wawili, mwanamke na mwanaume waliokubaliana kuoana hufungiwa nira pamoja. Huku kufungiwa nira pamoja kuna athiri imani walizonazo wahusika. Na kwa sababu swala la imani lina pande mbili; upande wa Mungu wa kweli kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upande wa Shetani kupitia, ndiyo sababu Biblia imekataza kufungiwa nira pamoja na mtu asiyeamini (katika Kristo Yesu Bwana) kwa jinsi isivyo sawasawa. Jambo hili si kwamba litaathiri mahusiano ya wahusika lakini pia mahusiano ya kiroho (KIIMANI) ya wahusika na Mungu.

Ndoa ni kamba ya nyuzi tatu! Sasa hiyo nyuzi ya pili na ya tatu inategemea ni nyuzi ipi; hiyo ndiyo inaamua uimara wa kamba (ndoa). Muhusika wa pili akiwa ni asiyeamini bila shaka na muhusika wa tatu (Mungu) hatajihusisha sana na mahusiano hayo; kwa sababu hiyo kamba hiyo itakatika upesi. Ni muhimu tukafahamu kuwa, kwa sisi tulioamini Mungu anajihusisha na mahusiano ya ndoa ya wahusika wote walioamini.
Muhubiri 4:9 - 12.

Amosi 3:3
Wawili hawawezi kutembea pamoja wasipopatana. Ndoa inahitaji watu wawili waliopatana pamoja hasa katika swala la imani ili waweze kutembea pamoja kwa muda mrefu. Mahusiano ya uchumba hadi ndoa ni mwendo wa mbele katika safari ya maisha ambapo wawili waliokubaliana kuoana au waliooana wanapaswa kutembea pamoja kwa muda mrefu, kwa kipindi chote cha maisha yao, hivyo ili kusudi lifikiwe na safari yao pamoja ya maisha ifanikiwe kwa wao kumaliza pamoja kwa ushindi ni sharti wapatane. Na moja ya jambo wanalopaswa kupatana ni swala la imani yao.

MAMBO YA KUEPUKA ILI KUTUNZA MISINGI YA IMANI KABLA YA KUANZISHA MAHUSIANO YA UCHUMBA HADI NDOA.

1. Epuka kuanzisha mahusiano na mtu asiye amini. Ijue kwanza imani ya mtu kabla ya kuanza naye mahusiano ya uchumba. Malaki 2:10 - 11

Malaki 2:10-11

[10]Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?

[11]Yuda ametenda kwa hiana, na chukizo limetendeka katika Israeli, na katika Yerusalemu; maana Yuda ameunajisi utakatifu wa BWANA aupendao, naye amemwoa binti ya mungu mgeni.


2. Epuka kuanzisha mahusiano kwa kufuata namna, au kawaida au desturi ya dunia hii au ulimwengu huu. Dunia wana mungu wao na sisi tulioamini tuna Mungu wetu kwa hiyo kawaida, namna na desturi zetu zinapingana na zao.

Walawi 18:30

[30]Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.


Walawi 20:23

[23]Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.


Warumi 12:2

[2]Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.


3. Epuka kuanzisha mahusiano bila kumshirikisha Mungu na Roho wake pamoja na mchungaji wako (kiongozi wako wa Imani).
(Wagalatia 6:6; Zaburi 32:8; 2 Nyakati 15:3.)

Mungu anaijua njia yako ya mahusiano; anakujua ni nini unahitaji, na kipi kinakufaa, kwa hiyo ni muhimu sana ukamshirikisha kabla ya kuchukua au kuanza hatua yo yote. Sikiliza na kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu na kumshirikisha mchungaji wako kwa ushauri na maelekezo ili hatua zako ziwe za uhakika na salama.

4. Epuka mazungumzo mabaya yatakayoharibu imani yako.

Mazungumzo mabaya uharibu tabia njema. Kwa kweli hasa katika kizazi hiki ambacho kila mmoja ni mjuzi wa maswala ya ndoa kwa mtazamo wake yeye, kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusiana na mahusiano, na mengi yao ni mazungumzo mabaya. Ukipita vijiweni, katika mitandao ya jamii nk. watu wanazungumzia mahusiano, sasa wewe epuka mazungumzo mabaya yanayopotosha imani yako na kukutoa kwenye misingi ya kiimani ili ubaki salama.

5. Epuka kuwafuata au kuwaiga au kujifunza kutoka kwa watu walioshindwa kuilinda imani yao unapotaka kuanzisha mahusiano.

Siku hizi wapo watu wanaojiita watumishi wa Mungu ambao kutokana na madhaifu na makosa yao wamehalalisha mambo hayo kuwa mafundisho. Wana ujasiri wa kufundisha wakihalalisha mambo yasiyo sahihi kuwa ni sawa tu yakifanywa. Epuka kuwafuata watu wa namna hii watakupoteza.

Hata hivyo, kwa upande mwingine ni muhimu wewe kutojihalalishia makosa ya mtu mwingine aliyotangulia kuyafanya yakawa ni halali na kwako eti kwa sababu wengine (waamini, watumishi na wachungaji) waliorudi nyuma waliyatenda na unaona kana kwamba hakuna shida yo yote. Ilinde imani, ni kati yako wewe na Mungu.

NINI HUTOKEA KIJANA ANAPOANZISHA MAHUSIANO NA KIJANA ASIYEAMINI.

1. Hupelekea vita ya miungu katika ulimwengu wa roho. Jambo hili hupelekea mahusiano ya uchumba hadi ndoa kuwa na mashindano katika ulimwengu wa roho na ndani ya kanisa. Mika 2:10 - 11

2. Hupelekea mashindano ya kiimani katika nafsi za wahusika na ndani ya kanisa (mwili wa Kristo) na hadi kwenye familia za wahusika.

Inapotokea wahusika wenye imani mbili tofauti (zinazopingana) wameanzisha mahusiano hapo ndipo migogoro huanza; muhusika yeye mwenyewe huwa na mgogoro na nafsi yake ndani yake, mgogoro wa yeye na kanisa au dini yake, mgogoro na wazazi wake. Sasa ili kukwepa yote haya na uwe na amani, anzisha mahusiano na mtu mwenye imani moja na wewe (aaminiye imani moja na wewe).

3. Asiye amini huwa mtego na mwiba kwa aaminiye na sababu ya kurudi nyuma.

Kutoka 34:12

[12]Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.


Ndoa ni agano; unapofanya agano na mtu asiyeamini (imani moja na wewe) mtu huyo huwa mtego kwako na ndiyo sababu Biblia imekataza kuoa au kuolewa na watu wasio amini.

4. Mungu anakuwa nje ya muunganiko huo; anajiweka pembeni ili aone mwisho wake. Unakuwa umefarakana na Mungu wako. Mika 2:10 - 12

5. Uwezekano wa kulitumikia kusudi la Mungu katika muunganiko huo unakuwa haupo.

6. Uhakika wa usalama wa ndoa na hali ya kudumu ya ndoa unakuwa haupo. Mahusiano yenu yanakosa uimara na uthabiti.

7. Uaminifu na utakatifu wa ndoa unakuwa haupo.

8. Adui wa mwenzi wako wanakuwa adui zako, roho zinazomtawala zinakutawala na wewe na mungu wake anakuwa mungu wako na kwa sababu hiyo anakuwa na uwezo juu yako.

Поиск
Категории
Больше
1 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 1 Chronicles 8
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 26 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-03-20 04:46:12 0 5Кб
Injili Ya Yesu Kristo
AGIZO LA KUTAWADHANA
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        ...
От GOSPEL PREACHER 2022-01-12 00:56:05 0 9Кб
Injili Ya Yesu Kristo
Je, Mkristo anapaswa kufanya nini kama yeye ameolewa na asiyeamini?
Kuoleka na kafiri inaweza kuwa mojawapo ya changamoto ngumu sana katika maisha ya Mkristo. Ndoa...
От MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 21:09:51 0 5Кб
PSALMS
Verse by verse explanation of Psalm 5
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 42 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-04-04 23:02:55 0 5Кб
2 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 2 Chronicles 34
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 29 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-04-02 02:36:56 0 5Кб