TAFADHALI JIHADHARI USIUKUBALI UONGO HUU WA ADUI.

0
307

Bwana Yesu asifiwe mwana wa Mungu, nakusalimu kwa jina la Kristo Yesu, ni matumaini yangu unaendelea vizuri katika kuvipiga vita vya imani, huku imani ukiilinda na hatimaye mwendo uumalize vyema ili kwa pamoja tukamlaki Yesu mawinguni.  Siku moja nikiwa nyumbani, uliingia ujumbe wa Kundi (Group) la whatsapp, ambalo mtumishi mmoja wa Mungu aliiunganisha namba yangu. Lengo la Kundi hili lilikuwa ni kujifunza maneno ya Mungu na kuhubiri injili. Sasa siku hiyo ambayo ilikuwa ni tarehe 02 septemba 2025 mnano saa 2:12 usiku (08:12 PM), kwa masaa ya Afrika Mashariki. Muda huo nilikuwa nimejipumzisha kidogo baada ya majukumu ya siku nzima, na ndipo baada ya dakika chache nikachukua simu yangu ili kuangalia taarifa mbalimbali na ndipo nilipoona notification hiyo ya WhatsApp, na nikaifungua na kuiona hiyo video kisha nikaipakua video hiyo, na nikaiangalia, kisha nikaiangalia tena  na tena (yaani mara 3).

Ni video ambayo ukiiangalia kwa haraka unaweza ukaamini kabisa ni ya ki-Mungu, tena unaweza ukaenda mbali zaidi kwa kuamua kufuata/kutekeleza mafundisho yaliyomo ndani yake, lakini ukweli ni kwamba hii ni video ya kishetani, tena imejaa mafundisho ya kipepo na yanayoweza kukufanya uwe mshirikina kabisa. Nimejaribu kukuandikia katika maandishi kile kilichosemwa kwenye video hiyo. Naomba uyayosome kwanza maneno hayo hapo chini kisha tuendelee kuchambua ukweli na uongo uliomo ndani ya video hii.

NUKUU YA UJUMBE (KADIRI YA NILIVYOMSIKILIZA, MTU HUYO ALISEMA KUWA): “Anza kuamka saa tisa za usiku, na usali hizi sala mbili ambazo nitakwenda kukuonyesha na nikuhakikishie maisha yako yatabadilika kabisa. Sasa chukua Biblia yako na notebook nikuelekeze. Hakikisha ndani ya mwezi mmoja weka alarm, uwe unaamka saa tisa za usiku, na uwe unasali hii sala. Kama unahitaji badiliko kwenye Uchumi, basi utakuwa unasali hivi: Utakuwa unachukua Biblia yako unafungua zaburi ya 51 unaisoma yote halafu unafungua zaburi ya 112 unaisoma yote, unafungua zaburi ya 23 unaisoma yote, unakwenda kumwambia Mungu hivi (ukishamaliza Zaburi zote). “Mungu naomba ukabadilishe uchumi wangu, ukanipe fedha nyingi ili adui asije akanidanganya na hali mbaya nikaacha kukutumikia wewe nikaanza kuitumikia pesa. Nipe fedha nyingi ili katika hizo fedha pia niweze kuifanya kazi yako kwa uzuri.” Sala ya pili: Kama unapitia hali ngumu, unateseka, unahitaji msaada wa ki-Mungu, unasoma zaburi 51 yote, halafu utakuja kusoma zaburi ya 35 mara nne (pande nne za dunia), halafu utakwenda kusoma zaburi ya 69, baada ya hapo utakwenda kumwambia Mungu, naomba unisaidie, unitoe kwenye hii hali. Kama kuna nguvu yoyote ya giza ambayo inakaa ndani yangu, ninaiamuru iniachie, na nikuhakikishie, utakapokuwa unafuata hizi sala mbili ndani ya mwezi maisha yako yatakuwa yamebadilika kabisa. Na wala haiwezekani ukabaki kama ulivyo.”

 

Mpendwa, siku hizi tunaishi kwenye nyakati za mwisho tena sio tu nyakati za mwisho, bali ni muhimu kujua kuwa tunaishi mwishoni kabisa mwa nyakati za mwisho, hivyo siku na saa yoyote ile Yesu Kristo yuaja tena kulichukua kanisa lake, lakini swali ni moja tu, je wewe pia utakuwa miongoni mwa watakaonyakuliwa? Maana imeandikwa katika Ufunuo 19:9 kuwa “Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.” Swali ni je utakuwepo kwenye harusi hii, au utaachwa? Ni heri kukosa vyote vya ulimwengu huu lakini uupate uzima wa milele. Na katika nyakati hizi za mwisho, shetani anajua kuwa muda wake ni mchache mno, hivyo anafanya kazi usiku na mchana tena bila kupumzika, maana anajua ya kuwa muda wake ni mchache sana. Hivyo anafanya kila analoliweza ili kuwapeleka wengi motoni, hasa jamii ya wateule.

Na ili kufanikisha lengo lake hili, basi adui shetani ameachilia roho chafu ya uongo duniani, hasa akiwatumia manabii wa uongo ili kudanganya wengi yamkini hata wateule. Na ndio maana Biblia ikatueleza katika ile 1 Yohana 4:1 inasema kuwa “Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.” Hivyo sisi kama watakatifu (imeandikwa mtakuwa watakatifu kwa kuwa Mungu wetu ni Mtakatifu, 1 Petro 1:16), hatupaswi kuamini tu kila tunachokisikia kinahubiriwa, maana manabii wa uongo nao pia wanatumia Biblia, tena wanakusomea maandiko mengi sana tu, lakini lengo lao ni kukufanya uende motoni, maana baada ya kukusomea maandiko hayo: (a). watakupatia tafsiri ya uongo, (b). watakupa maelekezo ya kishetani ambayo yamechanganywa na ukweli kidogo mno huku uongo ukiwa mwingi. Na utakapotekeleza maelekezo hayo, basi utakuwa umepotea, na utahitaji neema ya MUNGU tu ili kukutoa kwenye upotevu huo.

 

Maana wengi wa hawa (walioelezwa uongo kwa kutumia maandiko), huwa wanaona wanaifuata Biblia, tena Imani yao kwenye huo uongo huwa ni kubwa mno, na mara nyingi hii ndio sababu ya kuibuka kwa madhehebu mengi nyakati hizi. Mfano: Nchini Kenya kuna mtu aliwahi kujiita yeye ni Jehova muumbaji wa mbingu na dunia (tena alikuwa akiishi na wake zake wengi), na mwingine akijiita kuwa yeye ndiye Yesu wa kwenye Biblia. Na hawa wote walifanikiwa kupata waumini wengi mno. Sasa kabla haujakimbilia kusema kuwa waumini hawa hawakuwa na ufahamu, jaribu kwanza kujiuliza, je ni mistari gani kwenye Biblia ambayo walisomewa na hawa watu ili kuthibitisha kuwa wao ndio JEHOVA na YESU?  Fikiria tena, je walipewa tafsiri gani baada ya kusomewa maandiko hayo?  Na hata nchini kwetu Tanzania yupo mwanamke ambaye jina lake maarufu anaitwa Zumaridi, waumini wa mwanamke huyu, wanamwita zumaridi kuwa ni ‘baba’. Ndugu sijakosea, zumaridi ni mwanamke lakini waumini wake hawamwiti ‘mama’, bali wanamwita “baba”. Pia nitarudia tena kukueleza kuwa kabla haujakimbilia kusema kuwa waumini hawa hawakuwa na ufahamu, jaribu kwanza kujiuliza, je ni mistari gani kwenye Biblia ambayo walisomewa na mwanamke huyu ili kuthibitisha kuwa yeye ndio MUNGU BABA?  Fikiria tena, je walipewa tafsiri gani baada ya kusomewa maandiko hayo?

 

Jambo zuri ni kwamba, Biblia inasema katika 2 Wakorintho 2:11, kuwa “Shetani asije akapata kutushinda; maana hatukosi kuzijua fikira zake.” Kwa andiko hili utaona kuwa wanafunzi wa Yesu (wateule), tunapaswa kuzijua fikira (mawazo/mbinu/hila) za adui shetani, na tukifanikiwa katika hili basi kamwe shetani hatatushinda. Pia katika ile Yohana 8:44, Yesu alisema kuwa “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” Na hata katika ile Yohana 10:10, Yesu alisema pia kuwa, “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Hivyo ni wazi Kabisa kwa maandiko haya utaona kuwa Shetani ni baba wa uongo, tena lengo lake haswa ni kuiba, kuchinja na kuharibu, na silaha yake kubwa anayoitumia kufanikisha malengo yake haya silaha ya uongo (hila). Na ili hila iweze kuwa na nguvu zaidi na kuaminika ni lazima ichanganywe na ukweli kidogo. (Hila ni sawa na sumu iliyopakazwa sukari).

 

 

MIFANO MIWILI YA HILA ZA ADUI SHETANI

(A). MFANO WA KWANZA: Ukisoma katika ile Luka 4:1-12 utaona majaribu matatu ambayo shetani alimjaribu Bwana YESU, na katika majaribu yale, unaweza pia ukaona hila fikira (Mawazo ya adui shetani). Na mpaka leo, adui bado anaendelea kutumia mbinu hizihizi kuangusha wengi hasa jamii ya watakatifu.

        i.            Jaribu la 1: TUMBO:  Shetani alimwambia Yesu kuwa abadili jiwe kuwa mkate. Hii ni kwa sababu Shetani anajua chakula ni muhimu kwa binadamu, na binadamu asipokuwa na Mungu basi atakuwa tayari kufanya jambo lolote lile ili mradi tu limpatie chakula, hata kama jambo hilo ni dhambi mbele za Mungu. Mfano jiulize kwa nini watu wengi leo ni wezi, makahaba, au wanafanya kazi zozote zile ambazo ni haramu? Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa sababu ni tumbo yaani wako tayari kufanya hata uovu ili tu wapate uhakika wa chakula. LAKINI YESU ALILISHINDA JARIBU HILI, kwa kukuonyesha wazi kuwa chakula cha kimwili sio muhimu sana kuliko chakula cha kiroho (Neno la Mungu), na hatuishi kwa mkate tu bali kila kinachotoka kwenye kinywa cha Mungu.

      ii.            Jaribu la 2: MALI: Shetani akiona umemshinda kwenye jaribu la chakula, yaani umekataa kufuata maelekezo yake ya kishetani ili yakupatie uhakika wa chakula, basi hapo ndipo atakupokuletea jaribu hili la pili ambalo ni tamaa ya macho (MALI). Atakuahidi kama alivyomwahidi Yesu, kuwa atakupatia mali na ulimwengu wote, kama tu ukikubali  kumsujudia shetani. Hivyo kama unapenda mali sana kuliko kumpenda Mungu, basi inaweza ikawa rahisi kwako kukubali matakwa ya shetani, kama freemasons walivyokubali (ndio, freemasons wamekubali kumsujudia shetani ili wapate mali, na shetani amewapa kweli, ila mali hizo zimejaa mateso na majonzi). LAKINI UKIKATAA na kusema kama alivyosema Yesu kuwa imeandikwa Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Basi hapo ndipo atakapojaribu silaha yake ya mwisho na hatari kuliko zote, nayo ni kukueleza uongo aliuchanganya na ukweli kidogo kutoka kwenye maandiko.

    iii.            Jaribu la 3: KUTUMIA NENO LA MUNGU KWA LENGO LA KUKUANGUSHA DHAMBINI:  Kikawaida ni watakatifu tu ndio ambao wanaoweza kuyashinda majaribu mawili ya mwanzo, wenye dhambi wengi hushindwa kwenye jaribu la kwanza tu. Ni wale tu walioamua kujikana wenyewe na kujitwisha msalaba na kumfuata, ndio wanaoweza kushinda kirahisi, jaribu la kwanza na hata la pili, lakini hili la tatu ni hatari zaidi na wateule wengi huwa linawaangusha. Katika jaribu hili, shetani atatumia maandiko, yaani atakupatia andiko ndani ya Biblia, na kisha atakupata tafsiri au maelekezo ya kufanya kupitia andiko hilo. Shetani atafanya hivi kwa kuwa atakuwa ameona kuwa umemshinda majaribu ya awali kwa NENO (BIBLIA), ndipo na yeye atatumia BIBLIA hiyo hiyo unayoiamini ili kukuangusha. Mfano alimwambia Yesu kuwa Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.UKWELI: Ni kweli hili limeandikwa katika Zaburi 91:11 lakini haikuwa na maana kwamba Yesu ajipeleke mwenyewe kwenye hatari ya kujitakia (bila maelekezo ya ki-Mngu), kisha ategemee ulinzi wa Mungu (huku ni kumjaribu Bwana Mungu wako). UONGO: Ukijipeleka kwenye hatari za namna hii, basi unaweza kufa na ukaenda kuzimu moja kwa moja. Ni sawa na kujaribu kula chakula ambacho unajua kabisa kina sumu, eti tu kwa kuwa imeandikwa tutakula vitu vya kufisha na havitatudhuru (Pointi sio kula chakula hicho, bali pointi ni kula huku ukijua kuwa kina sumu, kama hujui basi Bwana anaweza akakuokoa na wala sumu isikuue, ila kama unajua kuna sumu na umeamua kula hali ukijua, basi utaangamia kwa kukosa maarifa).

 

(B). MFANO WA PILI WA HILA ZA ADUI SHETANI: Katika Mwanzo 3:1-5 alimwambia Eva kuwa akila matunda (ya mti ule) hawatakufa, bali macho yao yatafumbuliwa, na watakuwa kama Mungu, wakijua mema na mabaya. Ukiyachunguza maelezo haya ya shetani, utaona wazi kuwa yamejaa uongo mwingi uliochanganywa na ukweli kidogo, na hii ndio mbinu yake mpaka leo. Sasa ngoja tuangalie kwa kifupi kuhusu ukweli na uongo katika maelezo haya ya shetani. (i). UKWELI: Watafunulia macho yao na watajua mema na mabaya. (ii). UONGO: Hawatakufa bali watakuwa kama Mungu. Ukichunguza kwa makini utagundua kuwa shetani hakumjaribu Eva kwenye Chakula au kwenye Mali. Hii ni kwa sababu (a). Adamu na Eva hawakuwa na shida ya chakula, maana kwenye bustani ya Edeni kulikuwa na chakula kingi ambacho hawawezi kukimaliza. Na hata Eva alivyokula tunda lile, hakula kwa kuwa alikuwa na njaa, la hasha. (b). Adamu na Eva walikuwa ndio watawala wa mali zote za duniani, hivyo shetani hakuwa na mali ya ziada ya kuwapa. NDIO MAANA SHETANI AKAENDA MOJA KWA MOJA KUWAJARIBU KWA KUTUMIA BIBLIA YAO WA WAKATI HUO. Ndio Adamu na Eva walikuwa na Biblia (Neno la Mungu), ila ya kwao haikuandikwa kwa wino wala kwenye karatasi, bali iliandikiwa kwenye mioyo yao. Tena wala haikuwa na maneno mengi mno kama ya kwetu leo, bali yalikuwa machache sana tu. Mfano, kwa uchache tu, mambo yaliyokuwa kwenye Biblia yao ni kama vile: (a). Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha, mkatawale Samaki Wanyama na wadudu, (b). Wanapaswa kuilima bustani na kuitunza. (c). Mwanaume anapaswa kumwacha baba yake na mama yake na kuambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. (d). WANAPASWA KULA MATUNDA YA MITI YOTE, KASORO TU MATUNDA YA MTI WA UJUZI WA MEMA NA MABAYA.

 

 

 

 

 

 

BASI NDIVYO ILIVYO KWENYE VIDEO HIO HAPO JUU, imejaa uongo mwingi wa shetani ambao ameuchanganya kidogo na maandiko ili kupoteza wateule wa Bwana. Na lengo la Makala hii ni kueleza waziwazi hila za adui zilizomo katika video hii, ni maombi yangu kwa Mungu kuwa macho yako yafumbuliwe ili uweze kuelewa. Sasa tuanze kuungalia ujumbe wa video hii hatua kwa hatua:

 

(1). “Anza kuamka saa tisa za usiku:

Hapa mtu huyu anashauri kuwa unapaswa kuamka saa 9 za usiku kisha ufuate maelekezo yake ambayo ni kusoma Zaburi tena kwa mtindo anaotaka yeye kisha kuomba maombi anayotaka yeye. Ukiangalia juu juu huwezi ukaona tatizo, kwa maana  (a). Kusoma Zaburi ni jambo jema, maana hilo ni Neno la Mungu, (b). Kuomba ni jambo jema pia, tena maombi ya usiku yanakubalika kibiblia tena hata Yesu Kristo naye pia alikuwa akiomba usiku kucha. Lakini je, umeweza kuiona hila ya adui shetani hapo?

HILA YA ADUI NI: Unapangiwa muda wa kufanya ibada ya maombi, kuwa ni lazima iwe saa 9 usiku, kana kwamba muda mwingine maombi hayapokelewi au hayapokelewi kwa uzito. Inasemekana kuwa usiku ndio muda ambao ufalme wa giza huwa unafanya kazi mno, tena watu wengi husema kwamba kwa kuwa Yesu Kristo alikufa saa 9 jioni (Marko 15:34-39), hivyo basi saa 9 usiku ndio saa ambayo ufalme wa giza hufanya kazi kwa nguvu mno (sijaona bado uthibitisho wa hili katika maandiko). Lakini hata kama hili ni kweli, je maelekezo haya ya kuamka saa 9 usiku ili kuomba yanapatikana wapi kwenye Biblia? Ninachojua, shetani anafanya kazi muda wote tena kwa nguvu zote, maana anajua muda wake ni mchache mno.

Biblia inahimiza kuwa tunapaswa kuomba bila kukoma, unaweza ukaomba asubuhi, mchana, jioni, usiku, kadri Roho wa Mungu atakavyokujalia. Na sio kwamba ni lazima tuombe muda Fulani, kwamba muda huo ndio muhimu kuliko mwingine, huu ni uongo. Umejaribu kujiuliza malango ya kuzimu yana ajenda gani dhidi ya muda huo unaoambiwa uombe? Na  je, ni nini huwa kinafanyika kuzimu kuhusu maombi yote yanaombwa muda huo hasa kwa kufuata maelekezo ya mawakala wa kuzimu?

Hebu jaribu kujiuliza, kwa nini maelekezo haya yanafanana na maelekezo ya mganga wa kienyeji, ambaye anaweza kumwambia mteja wake, kuwa aamke saa 9 usiku kisha achukue hirizi aliyompa, kisha anuie kwenye hirizi hiyo kisha achimbe shimo dogo nyuma ya nyumba yake na aifukie? Hebu fikiria mwenyewe, kwa nini amwambie lazima iwe saa hiyo anayomwambia na wala sio muda mwingine? Huoni kama muda huo ndio malango ya kuzimu yatakuwa yamejipanga kupokea ibada yake?

KUOMBA SAA 9 USIKU SIO TATIZO, ILA KUOMBA SAA 9 USIKU ETI KWA SABABU NI MAELEKEZO YA WAKALA WA SHETANI, HAPO NDIPO TATIZO LINAPOANZIA. Kwa sababu sio tu kwamba utakuwa unaomba, bali utakuwa umefuata maelekezo ya kipepo. Hata kama shetani akikwambia ufanye jambo jema kiasi gani, haupaswi kufanya, wala haupaswi kumsikiliza.

 

(2). na usali hizi sala mbili ambazo nitakwenda kukuonyesha na nikuhakikishie maisha yako yatabadilika kabisa. Sasa chukua Biblia yako na notebook nikuelekeze: Hakikisha ndani ya mwezi mmoja weka alarm, uwe unaamka saa tisa za usiku, na uwe unasali hii sala.  

Hapa tena ukipaangalia juu juu sio rahisi kuiona hila ya shetani maana unaweza tu ukaona kama vile anataka kukufundisha sala, kama jinsi ambavyo Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuomba katika ile Mathayo 6:9-13. Hivyo unaweza ukawaza kuwa mbona hata mtu huyu naye ni kama anajaribu kukufundisha jinsi ya kuomba. Hapana mpendwa kuna hila ya adui hapa nayo ni hii.

HILA YA ADUI: Ukitazama kwa makini utagundua mtu huyu anakufundisha kuomba maombi ya kukariri, yaani kwa muda wa mwezi mzima wewe uwe unaamka saa 9 usiku, kisha unasoma hizo zaburi alizosema na kuomba sala hizo alizokufundisha. Ndugu huu ni ushetani, ni wapi kwenye maandiko ambapo wanafunzi wa Yesu waliwahi kuomba maombi ya kukariri kama haya? Pia vipi kama Roho wa Mungu akikwambia amka usiku huo na uimbe nyimbo za sifa na kuabudu peke yake (kama walivyofanya Paulo na Sila wakiwa gerezani), je utamsikiliza Roho wa Mungu, au utampuuza Roho na kufuata maelekezo ya mtu huyu anayekwambia uombe mwezi mzima? Ndio, mfano kama Roho anakushuhudia leo imba na mtu huyu anakwambia lazima mwezi huu kila saa 9 usiku uombe tena sala alizokufundisha, wewe utamsikiliza nani?

Pia vipi kama Roho wa Mungu, akikwambia uombee mambo mengine tofauti na hizo sala anazokufundisha, je utatii? Maana ukimtii Roho, utakuwa umeharibu mfumo wa sala anazofundisha. Ukisoma kwenye Matendo 4:19, Biblia inasema, Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe.

Watakatifu wa Mungu hatufanyi maombi ya kukariri, bali tunaomba katika Roho na tunaomba kwa Kadiri Roho anavyotujalia. Mfumo huu wa sala za kukariri unapatikana katika UKATOLIKI na katika UISLAMU. Dini hizi mbili ndizo ambazo zina sala nyingi mno na huwa zinawafundisha wafuasi wake kuzikariri na kuzisema sala hizo kwa kuzirudia rudia, tena zipo mpaka sala ambazo zinapaswa kuzisemwa katika muda fulani tu.

(3). Kama unahitaji badiliko kwenye Uchumi, basi utakuwa unasali hivi: Utakuwa unachukua Biblia yako unafungua zaburi ya 51 unaisoma yote halafu unafungua zaburi ya 112 unaisoma yote, unafungua zaburi ya 23 unaisoma yote, unakwenda kumwambia Mungu hivi (ukishamaliza Zaburi zote). “Mungu naomba ukabadilishe uchumi wangu, ukanipe fedha nyingi ili adui asije akanidanganya na hali mbaya nikaacha kukutumikia wewe nikaanza kuitumikia pesa.  Nipe fedha nyingi ili katika hizo fedha pia niweze kuifanya kazi yako kwa uzuri.”

Hapa pia pana hila nyingi za adui, lakini kwanza tuanze kuuangalia ukweli ambao shetani amejaribu kuuchanganya kwenye uongo wake. UKWELI: Ni ukweli kuwa Mungu anabariki, tena ameahidi baraka tele kwetu tunaomcha yeye (Kumbukumbu 28:1-12). Pia ni kweli fedha ina umuhimu wake kwenye kuwezesha kazi ya Mungu kusonga mbele, maana imeandikwa wataendaje wasipopelekwa (Warumi 10:15)?  Ijapokuwa haya yote ni kweli lakini ngoja tuingie ndani zaidi ili kuiona hila ya adui shetani ilipo:

 

HILA ZA ADUI

i.            Mtu huyu hajaimiza watu kutubu dhambi na kuishi maisha ya utakatifu, bali ameenda moja kwa moja kueleza kuwa unapaswa kusoma hizo zaburi na kuomba hizo sala ili uweze kupata fedha nyingi. Ile Kumbukumbu 28:1 inaeleza wazi kabisa kuwa, tutapokea baraka za Mungu kama tu tutaisikia sauti ya Mungu na kuyashika/kuyafanya yale yote aliyotuamuru, hapo ndipo baraka zitakapotufuata. Pia katika ile Mathayo 6:33, maandiko yako wazi kabisa kuwa tunapaswa kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake, kisha hayo mengine yote tutazidishiwa. Kiufupi mtu huyu hana tofauti na manabii wa uongo ambao wanakupatia maji na mafuta ya upako ukayamimine kwenye biashara yako ili wateja waongezeke upate pesa, bila  kukufundisha kwanza UTAKATIFU. Ukipata yote lakini ukakosa Utakatifu, basi kwako itakuwa ni hasara.

ii.            Pili, ni lazima ujue kuwa kuna utofauti kati ya kupenda pesa na kuhitaji pesa. Anayependa pesa atafanya lolote litakalompa fedha hata kama ni dhambi. Tena maandiko yapo wazi kuwa shina la mabaya yote ni kupenda fedha (1 Timotheo 6:10). Sasa hatari ni hii: INAWEZEKANA KABISA MOYONI MWAKO UKAWA NA TATIZO HILI LA KUPENDA FEDHA, na badala ya kutibu tatizo hili, mtu huyu anakufundisha kutumia maombi haya kama kichaka cha kujifichia. Yaani kwa nje tukuone unaomba fedha nyingi ili uifanye kazi ya Mungu lakini wewe mwenyewe unaelewa kilichomo moyoni mwako.

iii.            Tatu, hebu jiulize, ni nani kwenye Biblia aliyefanya maombi ili apate fedha nyingi? Je, ni Yesu Kristo ambaye ndiye kielelezo chetu, aliwahi kufanya maombi haya? Au wanafunzi wake waliwahi kuomba maombi haya? Je mwanafunzi wa Yesu, alipomueleza Yesu kuwa wanahitaji fedha, Yesu alimpatia fedha au alimpa wazo la kazi (yaani aende kuvua Samaki na kupasua tumbo akute pesa humo) ambalo ndilo likampatia fedha? Sasa hili fundisho la kuomba fedha na utajiri kutoka kwa Mungu limetoka wapi? Ukweli ni huu Mungu huwa hatupatii fedha, bali Mungu huwa anatupatia nguvu ya kupata utajiri (Kumbukumbu 8:18). Ni jukumu lako kuitumia nguvu hii, ndipo upate fedha.

iv.            Je, bado tu huioni hila ya adui shetani, pindi mtu huyu anapokwambia kuwa uombe eti Mungu akupatie fedha nyingi ili shetani asije akakudanganya na hali mbaya ukaacha kumtumikia Mungu na ukaanza kuitumikia fedha? Yaani anataka kukwambia kuwa usipokuwa na fedha basi shetani ndio atakudanganya, na pindi ukiwa na hizo fedha nyingi basi ndio shetani hatakudanganya, je ndivyo anavyotaka kukuaminisha? Shetani ni baba wa uongo, hivi unakumbuka jinsi alivyomweleza Mungu kwa Habari za Ayubu? Alisema Mungu amemzingira pande zote na amembarikia na ndio maana Ayubu anamcha Mungu. Kwa Ayubu haikuwa kweli, maana Ayubu hakumcha Mungu kwa kuwa tu ana fedha, lakini wewe kama ukifuata ushauri wa mtu huyu, basi utakuwa tofauti na Ayubu (yaani wewe utakuwa unamwabudu Mungu na shetani hakudanganyi kwa kuwa una fedha nyigi, MUNGU akuepushie mbali jambo hili). UKWELI ni kwamba shetani atakudanganya kama utampa nafasi, haijalishi una fedha ama la, ndio maana imeandikwa msimpe ibilisi nafasi (Waefeso 4:27).

v.            Yaani hapa zipo hila nyingi mno, maana mtu huyu anaeleza kuwa umwombe Mungu akupe fedha nyingi ili uifanye kazi yake kwa uzuri, je ni kweli bila fedha nyingi haiwezekani kuifanya kazi ya Mungu kwa uzuri? Je, Yohana mbatizaji alikuwa na fedha kiasi gani kwenye hazina yake? Maana alikuwa akikaa jangwani akila nzige na asali. Sasa je hakuweza kuifanya kazi ya Mungu kwa uzuri eti tu kwa kuwa hakuwa na fedha hizo nyingi? NAOMBA NIELEWEKE VIZURI, sipingi umuhimu wa fedha kwenye huduma, maana hata mtume Paulo alitumia fedha nyingi kwenye huduma yake. Bali ninachosema ni hiki: sio lazima wote tuwe na fedha nyingi ili tuifanye kazi ya Mungu kwa uzuri, bali tunapaswa kuenenda kwa kufuata mapenzi ya Mungu. Jiulize swali hili, je wewe Mungu amekuita kama Yohana au kama Paulo? Pia hata Yakobo 4:3 inasema kuwa “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Kumbuka ndugu, unapaswa kuomba mapenzi ya Mungu yatimizwe juu yako, na sio kuomba fedha nyingi. Je ni kweli kuwa ni mapenzi ya Mungu uwe na fedha nyingi kwa sasa?

(4). Sala ya pili: Kama unapitia hali ngumu, unateseka, unahitaji msaada wa ki-Mungu, unasoma zaburi 51 yote, halafu utakuja kusoma zaburi ya 35 mara nne (pande nne za dunia), halafu utakwenda kusoma zaburi ya 69, baada ya hapo utakwenda kumwambia Mungu, naomba unisaidie, unitoe kwenye hii hali. Kama kuna nguvu yoyote ya giza ambayo inakaa ndani yangu, ninaiamuru iniachie, na nikuhakikishie, utakapokuwa unafuata hizi sala mbili ndani ya mwezi maisha yako yatakuwa yamebadilika kabisa. Na wala haiwezekani ukabaki kama ulivyo.”:

Kama kawaida shetani huwa anachanganya ukweli kidogo na uongo mwingi ili kuunda hila yake na kuifanya isiwe rahisi kuigundua. Hata hapa pia ameeleza ukweli kidogo ambao ni huu: Ni kweli Mungu anatusaidia tukimwomba na kututoa kwenye shida na mateso, lakini UTAKATIFU ni muhimu sana.

HILA YA ADUI: Kama nilivyosema awali kuwa ni muhimu sana kufundishwa utakatifu, maana bila utakatifu mateso yatarudi tena. Yesu alisema katika ile Mathayo 12.43-45, kuwa “Pepo mchafu, amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika, asipate. Halafu husema, Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya”.

MWISHO: Nimejitahidi mno kuisikiliza vizuri video hii, lakini sikufanikiwa kuona mahali popote ambapo alimtaja Jehova, ama Yesu, ama Roho Mtakatifu, bali mara zote amekuwa akimtaja Mungu. Huenda ukawa haujui lakini ukweli ni kwamba Mungu sio jina bali Mungu ni cheo. Na ipo miungu mingi na miungu yote hii ina majina (mfano: Allah, Budha, n.k), lakini MUNGU wa kweli ni JEHOVA pekee. Ndio maana ukisema twende tukamwabudu Mungu, kila mtu (Mkristo, Muislam, Mhindu, Mbudha, n.k, atakuelewa unamwambia akamwabudu Mungu wake). Ila ukisema twende tukamwabudu JEHOVA, inajulikana wazi ni Mungu yupi amekusudiwa.

Hata hivyo huenda mtu huyu aliyerekodiwa akiongea kwenye video hii, AKAWA BADO HAJAZIONA HILA hizi za adui shetani, au huenda akawa anajua vizuri anachokifanya (yaani anafanya makusudi, ili ajipatie kipato, maana kwenye video hii anaonekana wazi akivinadi vitabu vyake anavyoviuza Tsh 10,000), hivyo hukumu ya jambo hili, namwachia Bwana Yesu aonaye sirini maana yeye ndiye ajuaye, naye ndiye atakaye mhukumu, wala sio mimi. Yaani Yesu Kristo ndiye ajuaye kuwa mtu huyu hakutaja jina la Yesu, kwa kuwa alisahau, au hakulitaja jina la Yesu ili auze vitabu vyake kwa watu wote na wa dini zote (yaani ambao sio wakristo), Bwana Yesu ndiye ajuaye jambo hili.

Hata hivyo naomba ieleweke wazi kuwa (a). sio kwamba ninamshambulia mtu yeyote, la hasha, bali natamani kweli ya Mungu ifahamike Duniani mwote, pia (b). Wala sio kwamba mimi ni mtakatifu sana kuliko wengine, la hasha; mimi pia ni miongoni mwa wenye dhambi wengi niliyekubali kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yangu, na ninaendelea kujitahidi mno kuvipiga vita vya Imani, hivyo nakuomba sana ndugu uendelee kunikumbuka katika maombi. Lengo la Makala haya kueleza mzigo ambao Roho wa Mungu ameuweka ndani yangu ili ukweli wa Mungu ufahamike vizuri duniani mwote. Amani ya Kristo Yesu iwe Pamoja na roho yako, Mungu akubariki sana mwana wa Mungu, Maran atha.

 

 

Site içinde arama yapın
Kategoriler
Read More
JOB
Verse by verse explanation of Job 1
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 37 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-04-02 13:15:14 0 5K
MASWALI & MAJIBU
Je! Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi?
SWALI : Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu ni ipi? JIBU: Tukisoma; Mathayo 12:25-32 ”...
By GOSPEL PREACHER 2022-06-13 00:19:41 0 6K
OTHERS
MUHAMMAD AKIRI KUWA ALLAH SIO MUNGU WA KWENYE INJIL NA TAURAT BALI NI MUNGU WA KIPAGANI
Je, Wakristo na Waislam, wanaabudu Mungu mmoja?Je, Allah ni Mungu wa Kipagani?Ndugu wasomaji, kwa...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 19:37:36 0 5K
Religion
USIFUATE MAMBO YAKO TU!!
Ipo faida  ya kufuata mambo yako na kutojishughulisha na mambo ya wengine!.. Lakini pia ipo...
By GOSPEL PREACHER 2021-10-09 23:17:01 2 5K
EZRA
Verse by verse explanation of Ezra 9
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 24 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-04-02 06:24:48 0 5K