WACHUMBA 7 WATAKAOSHINDWA

0
5K
Kutahadharishwa mabaya ni kutayarishwa kwa mazuri


“Ni yale mambo usiyoyatarajia….ambayo unahitaji kuyaangalia

 

Kabla ya Yote

Dalili zifuatazo kama zinapatikana katika uchumba wako, basi kuendelea kujiandaa na ndoa hiyo ni kujitayarisha kukutana na “majanga” ya jela la maisha. Lakini usiogope; nasema, usi-panic. Zitambue dalili hizi mapema ili ujue namna ya kusonga mbele au kugeuza njia. Dalili zenyewe zinapatikana kwa wachumba wa aina hii ninayoijadili hapa chini.

1. Wapenzi wamekutana muda mfupi tu baada ya kujeruhiwa vibaya moyoni

Baada ya balaa kuwaachia hasara na pengo kubwa moyoni, sasa wanatafuta kuliziba kwa kuoana haraka haraka. Balaa laweza kuwa la kupoteza mzazi wa kutegemewa, mwenzi wa maisha, au mchumba. Kwa kuingilia mahusiano ya mapenzi wanadhani wamepata tiba murwa na kumbe ni paracetamol. Mhathiriwa wa mikasa ya maisha anapaswa kwanza kupokea ushauri wa kiroho na kisaikolojia kabla ya kuwa na hakika yuko tayari kwa ndoa. Ndoa inayokuja na changamoto zake haipaswi ikukute ukiwa umechoka tayari na maisha.

 

2. Wachumba wanaoana ili kuikimbia familia walizotoka 

Wazazi wao hawakuelewana wao kwa wao na wao wenyewe hawakufurahia utoto au ujana wao. Sasa wanakimbia miji yao huku wakibeba picha za machungu waliyoyapitia. Matokeo yake wanaingia katika ndoa mpya wakiwa na uzoefu wa ndoa ya zamani. Mabaya waliyoyakimbia nyumbani ndiyo mabaya watakayoyaendeleza katika mji wao; hata kizazi cha tatu na cha nne. Katisha mzunguko wa laana kwa kuwasamehe wazazi wako na kutafuta mahusiano mazuri nao. Achilia moyoni mwako yaliyopita na chuchumilia yajayo.

 

3. Uzoefu wa nyuma wa familia walikotoka unatofautiana sana

Ndoa ni muunganiko wa  wawili wanaofanana na wasiofanana. Lakini tofauti zikiwa kali mno baina yao mpasuko hutokea mara moja uhalisia wa maisha unapotua mawazoni mwao. Tofauti zilizoonekana kuwavuta zitaanza kuwaachanisha. Tofauti hasa za dini, elimu, kipato, au utaifa zinapaswa zichukuliwe kwa uzito wake; vinginevyo, ndoa inasimama juu ya msingi ulioachana.

4. Wachumba wana mpango wa kuishi karibu mno au mbali sana na familia walikotoka 

Ukaribu sana na wazazi unahatarisha wanandoa kuingiliwa katika ndoa yao. Lakini umbali sana na wanandugu waliokuwa sehemu ya maisha yako unakosesha wanandoa msaada ambao wangeupata unaoweza kuwasaidia katika ndoa yao. Wanandoa ni taifa huru, lakini hakuna taifa huru linaloweza kuwepo pasipo ushirikiano wa mataifa rafiki.

 

5. Wachumba wanaoana wakiwa wachanga kiumri 

Wanapooana wakiwa na umri pungufu ya miaka 20 na/au wangali wanawategemea wazazi au wanandugu kifedha, au kimashauri, ni vigumu ndoa yao kufanikiwa. Ni vigumu kutendea kazi kila ushauri au kumpendeza kila mtu unayemtegemea kifedha. Vile vile katika umri mchanga wanandoa wanakuwa bado katika kipindi cha mabadiliko ya ukuaji. Ni vigumu nyumba kubakia imara kama nguzo za nyumba zinayumbayumba; hisia, shauku, na mitazamo ya wazazi inabadilika badilika kadri umri wao unavyoongezeka.

6. Wanaooana pungufu ya miezi sita ya kufahamiana na baada ya miaka mitatu ya uchumba 

Mwanadamu ni mtu wa ajabu; kusema umeweza kumsoma kwa miezi miwili, au minne ni kujidanganya. Unahitaji muda kumsoma mwenzako mkiwa na wengine na mkiwa wawili peke yenu. Lakini, kutumia muda zaidi kusomana, mpaka miaka mitatu ya uchumba kuna hatari ya kuchokana na kutibuana. Uchumba ni muda wa kufahamiana; lengo likifikiwa uamuzi uchukuliwe.

 

7. Mwanamke anapata uja uzito kabla ya ndoa

Mahusiano ya ngono kabla ya ndoa yanaondoa fursa ya wachumba kufahamiana. Tamaa ikitawala, mazungumzo ya kufahamiana yanakuwa haba na ya juu juu tu. Kila mmoja anafikiria kumtuliza mwenzake kimahaba. Wanadhani upendo unawaunganisha na kumbe ni mhehemuko tu. Msisimuko ukitulia na uhalisia wa maisha unapotua mawazoni ndipo hung’amua kuwa kila mmoja ni mgeni mikononi mwa mwenzake. Mbegu za kutoaminiana zilizopandwa wakati wa ngono haramu  huanza kumea katika kuoneana wivu na kushukiana ("kama amekuwa dhaifu kwangu kwa wengine je"), na mavuno ya mwisho ni ndoa kuyumba au kuvunjika kabisa.

 

Chukua Tahadhari!

Sidhani kama uchumba wenu una dalili nilizoziongelea. Na kama ndiyo, sidhani ni zote tajwa hapo juu. Hata kama unadhani uchumba wako una hali mbaya siamini maji yamewagika. Unaweza kujinusuru kwa kuomba msaada wa Mungu na wa washauri ili usaidiwe. Usifiche ugonjwa; maana, mauti itakuumbua. Tafuta msaada sasa. Ikibidi sitisha mahusiano. Bora uvunje uchumba kuliko baadaye kuvunja ndoa. Siko mbali nawe: nakuombea nikikutakia baraka za Bwana unapochukua maamuzi magumu.
Zoeken
Categorieën
Read More
REVELATION
UFUNUO 21
Bwana YESU KRISTO atukuzwe, Karibu katika mafunzo ya kitabu cha Ufunuo, leo tukiwa katika ile...
By GOSPEL PREACHER 2021-10-30 12:58:19 0 6K
GENESIS
Verse by verse explanation of Genesis 10
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 71 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-21 03:18:48 0 5K
OTHERS
Jesus and Islam
Here are six questions that followers of Islam, and others, often ask about Jesus... This will...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-23 09:45:24 0 5K
Religion
UFAHAMU KUHUSU DHAMBI YA KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU
VIPENGELE VYA SOMO(1). NI MAANA YA KUKUFURU?(2). DHAMBI YA KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU IKOJEE?(3)....
By GOSPEL PREACHER 2021-08-24 12:44:21 4 8K
1 KINGS
Verse by verse explanation of 1 Kings 11
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 51 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-02-05 13:10:21 0 6K