UFALME WA MUNGU

0
7K
BWANA ASIFIWE, unaweza kupakua (download) somo hili kwa kubonyeza hapa. Au unaweza ukaendelea kulisoma hapahapa. Sasa tuanze somo letu rasmi.
 
Ufalme wa Mungu (au Ufalme wa mbinguni unavyoitwa hasa katika Injili ya Mathayo) ni mojawapo kati ya mada kuu za ujumbe wa Yesu Kristo katika Injili.
 
Neno "ufalme" katika Injili limetafsiriwa kutoka kwenye neno Baseleia ambalo ni neno la lugha ya kigiriki (na kwa Kigiriki huandikwa hivi: βασιλεία, Basileia). Neno hili linapatikana mara 162. Na katika Agano Jipya, maneno Basileia tou Theou (βασιλεία τοῦ θεοῦ), ndiyo yametafsiriwa Kama Ufalme wa Mungu, wakati maneno Basileia tōn Ouranōn, (Βασιλεία τῶν Ουρανῶν), yametafsiriwa Kama Ufalme wa Mbinguni
 
Ufalme wa Mungu unatajwa mara kwa mara katika Injili (mfano, Marko 1:15, 10:15, 15:43, Luka 17:20) na maeneo mengine katika Agano Jipya (mfano, Matendo 28:31; Warumi 14) : 17; 1 Wakorintho 15:50). Ufalme wa Mungu ni sawa na ufalme wa mbinguni. Dhana ya Ufalme wa Mungu inachukua vivuli mbalimbali vya maana katika vifungu tofauti vya Maandiko.

Kwa uwazi, ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu wa milele, Mwenye nguvu juu ya ulimwengu wote. Vifungu vingi vya Maandiko vinaonyesha bila kupinga kuwa Mungu ndiye Mfalme wa viumbe vyote: "Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote" (Zaburi 103: 19). Na, kama Mfalme Nebukadineza alivyosema, "Ufalme wake ni ufalme wa milele" (Danieli 4: 3). Kila mamlaka iliyopo imeanzishwa na Mungu (Warumi 13: 1). Kwa hiyo, kwa maana moja, ufalme wa Mungu unahusisha kila kitu ambacho kilichoko.

UFALME WA MUNGU NI NINI? kwa ufupi, ufalme wa Mungu ni utawala wa kiroho juu ya mioyo na maisha ya wale wanaojitoa kwa hiari kwa mamlaka ya Mungu. Wale wanaopinga mamlaka ya Mungu na kukataa kumtii sio sehemu ya Ufalme wa Mungu; Kwa upande mwingine, wale wanaotambua utawala wa Kristo na kujitolea kwa utawala wa Mungu katika mioyo yao ni sehemu ya ufalme wa Mungu. Kwa maana hii, ufalme wa Mungu ni wa kiroho — Yesu alisema Ufalme wake haukuwa wa ulimwengu huu (Yohana 18:36), na alihubiri kuwa toba ni muhimu katika kuwa sehemu ya ufalme wa Mungu (Mathayo 4:17). Ni Dhahiri kwamba Ufalme wa Mungu unaweza kulinganishwa na nyanja ya wokovu katika Yohana 3: 5-7, ambapo Yesu anasema kuwa lazima mtu aigie katika ufalme wa Mungu ndio azaliwe tena. Ona pia 1 Wakorintho 6: 9.
 
UFALME WA MUNGU UPO WAPI?
Bwana Yesu aliwajibu Wayahudi kwamba, “Baadhi ya Mafarisayo walimuuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Yesu akajibu, “Kuja kwa ufalme wa Mungu si kitu unachoweza kuona. Watu hawatasema, ‘Tazama ufalme wa Mungu uko hapa’ au ‘Ule pale!’ Hapana, Ufalme wa Mungu upo hapa pamoja nanyi.”.[ Luka 17:20-21 TKU].”
 
Kupitia jibu la Yesu kwa Mafarisayo ni kwamba ufalme wa Mungu upo kati yao lakini Mafarisayo hawakuuona bali walizidi kuutizamia mbele, na katika mawazo yao walifikiri ufalme huo ni kuifanya Israeli kuwa taifa kubwa duniani. Na walikuwa na mioyo migumu, na Yesu aliongea nao kwa mifano lakini hawakuelewa. Yesu aliwambia wanafunzi wake kwamba, “Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe. [Luka 8:10].”
 
Hivyo Yesu alikuwa anajiongelea mwenyewe mbele ya Wayahudi kwa mifano kuwa ufalme wa Mungu upo kati yao, ambao yeye ameuleta kati yao na kazi zake zinajionesha machoni pao. Na Wayahudi walimshtumu kuwa anatumia nguvu za giza, akawajibu kwamba, “Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. [Mathayo 12:28].”
 
Hivyo nguvu za Roho Mtakatifu na kazi zake za uponyaji wa maradhi na kutoa mapepo yaliyokuwa yanatesa wanadamu, zilijidhihirisha kwa Yesu, na nguvu hizo zilibainisha kuwa ufalme wa Mungu umekuja na wenye nguvu ndio watauteka. [Mathayo 11:12]. Na hapo Yesu hakumaanisha nguvu za mwili bali nguvu ya nia na Imani; Lakini Wayahudi walidumu kutoamini na kumkataa Yesu, na Bwana Yesu akwaambia Neno gumu sana. “Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake. [Mathayo 21:43].”
 
Hilo taifa lingine, ni taifa la waaminio, wale ambao wana nguvu ya nia na Imani katika Kristo Yesu Mwana wa Mungu. [1 Petro 2:9,10]. Ambao ni wazao halisi wa Ibrahimu kwa njia ya Imani ambao ni Wakristo walio warithi sawasawa na ahadi. [Wagalatia 3:29]. Wayahudi wenye mioyo migumu yenye kutoamini walikatwa katika ufalme na mahali pao ikachukuliwa na wamataifa wenye kuamini, hivyo na wewe uliye katika ufalme usijivune pia usije katwa kama wao. [Warumi 11:20].
 
Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wautangaze ufalme wa Mungu, kuutangaza ufalme wa Mungu ni kumtangaza Yesu kwa nguvu za Roho Mtakatifu na kupooza watu maradhi yao. [Luka 9:2]. Na Mitume waliutangaza ufalme wa Mungu kwa nguvu na kuponywa maradhi kiasi cha Wayahudi na Serikali ya Herode ikatetemeka na Herode akatafuta kumwona Yesu. [aya 7-9]. Na kutangaza ufalme wa Mungu ni kuhubiri Injili. [Luka 9:6]. Ambayo inawapa watu toba na msamaha wa dhambi. [Marko 1:15; Mdo 5:31].
 
Yesu alisema, “Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. [Luka 4:43].” Mitume walimshuhudia pia kwamba. “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. [Matendo ya Mitume 10:38].”
 
Habari njema ya Ufalme maana yake ni INJILI YA UFALME, na Biblia inasema, “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” [Warumi 1:16]. Hivyo Injili inahusika na kila nafsi kuanzia Myahudi na Mmataifa, hakuna injili mbili, ni ile ile habari njema ambayo ilitufanya wawili kuwa umoja kwa kubomoa kiambaza cha kati kinachotutenga. [Waefeso 2:14].” Ni uweza wa Mungu huletao wokovu na uponyaji, na tunaupata uwezo huo ndani yetu kwa njia ya IMANI, maana pasipo Imani haiwezakani kumpendeza Mungu. [Waebrania 11:6].
 
Mitume baada ya Yesu kuondoka walihubiri sana ufalme huu, maandiko yafuatayo yanashuhudia hilo. “Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. [Matendo ya Mitume 8:12].” “Wakiisha kuagana naye siku, wakamjia katika nyumba aliyokaa, watu wengi sana, akawaeleza kwa taratibu na KUUSHUHUDIA UFALME WA MUNGU, akiwaonya MAMBO YAKE YESU, kwa maneno ya sheria ya Musa na ya manabii, tangu asubuhi hata jioni. AKIHUBIRI HABARI ZA UFALME WA MUNGU, NA KUYAFUNDISHA MAMBO YA BWANA YESU KRISTO, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu. [Matendo ya Mitume 28:23,31].
 
Hivyo kuhubiri Ufalme wa Mungu bila mambo yake Yesu ni kuhubiri Injili tupu isiyo okoa, maana hakuna wokovu katika mwingine isipo kuwa Bwana Yesu. [Mdo 4:12]. Maana Yesu ndiye asili yote ya ufalme wa Mungu. Kwahiyo ukihubiri fundisho lolote lisilo kwa jinsi ya Kristo hiyo itakuwa ni Injili nyingine, na mwisho ni kujipatia laana. [Wagalatia 1:8,9].
 
Na Ufalme wa Mungu umegawanyika mara mbili ingawa ni mmoja, ambao ni.
1. Ufalme wa neema
2. Ufalme wa utukufu
 

Ufalme wa Neema.

Ni utawala wa Neema katika mioyo ya waumini kwa njia ya Imani, utawala huu upo duniani ndani ya watu kwa njia ya Imani na ujazo wa Roho.[1 Yohana 3:24,4:13]. Na kiti cha enzi cha Mungu, kiti cha neema kimeondolewa pazia la kutukinga, hivyo wote wanaweza kumwendea Mungu moja kwa moja kwa ujasiri kwa damu ya Yesu mpatanishi ili wapate neema na rehema kwa mahitaji. [Waebrania 4:16]. Ufalme huu unapaswa kutangazwa kwa nguvu zote, kwa sauti kuu, maana ndio Injili ya Milele. [Ufunuo 14:6,7]. Na siri ya kuingia katika ufalme wa Neema ni kumwamini Yesu na kuzaliwa mara ya pili kwa maji na Roho. Yesu anasema, “Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. [Yohana 3:5].
 
Na Ufalme huu watu wanapaswa kuufurahia kuanzia sasa, Mtume anasema, “Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.[ Warumi 14:17].” Haki, Amani na furaha katika Roho Mtakatifu, hayo mambo si ya baadae, yaani ‘ya wakati ujao’ ni mambo tunayopaswa kuwa nayo sasa. Haki tayari tunayo kwa njia ya Imani, Amani tayari tumeshaachiwa, na furaha tunayo tayari kwa njia ya ujazo wa Roho Mtakatifu ndani yetu. [Tazama, Warumi 3:24, Yohana 14:27; Mdo 9:31]. Kama hujisikii kuwa na vitu hivi sasa, jipeleleze na fanya matengenezo.
 

Ufalme wa Utukufu

Huu utawala bado hujafunuliwa, na utakapofunuliwa kwa utukufu waaminio ndio watakao ng’aa kwa utukufu na kubadilishwa kuwa kama Yesu, [1 Yohana 3:2], ila wale walio upuuza ufalme wa Neema, watakuwa na kilio na kusaga meno na maangamizo. Biblia inasema, “Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake, naye atamiliki hata milele na milele. [Ufunuo 11:15]. Ufalme huu utaziondoa falme zote za dunia hii na kuziangamiza kabisa na kusimama waziwazi. Biblia inasema hivi.
 
Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele. “Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii. [Dan 2:44; 7:27].
 
Je waovu watapata nafasi ya pili?
Biblia inasema hakuna kitu kama hicho, wasio mkubali Yesu wote wataangamizwa kwa maangamizo ya milele. “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi;na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu; watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu). [2 Wathesaloniki 1:7-10].”
 
Mungu akubariki sana unapofanya maamuzi ya kumpokea huyu Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, maana wakati huu karibu. Wito ni kuamini Injili. [Marko 1:15].
Search
Categories
Read More
STANDARD 7
STANDARD 7
List of all subjects for the standard 7 class
By PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-09 10:22:31 0 5K
HOLY BIBLE
Responding to the Jehovah’s Witness attacks on the deity of Christ
If Jesus is God, why did he pray to the Father in John 17? Jesus prayed to the Father because as...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-24 06:00:07 0 5K
OTHERS
How to Change WordPress Logo in Login Page?
  Updated on Sep 10, 2020  Posted by Editorial Staff  Website...
By Shabea Disony 2022-09-04 21:37:51 0 8K
OTHERS
USHUHUDA: MWANASHERIA MKUU WA SHERIA ZA KIISLAM WA IRAKI AMPOKEA YESU
KUTOKA: KWENYE GIZA LA UDANGANYIFU WA KIISLAMU HADI: KWENYE NURU YA UTUKUFU WA YESU Ushuhuda wa...
By MAX SHIMBA MINISTRIES 2021-12-22 04:10:49 0 5K
Injili Ya Yesu Kristo
MKRISTO NA UCHUMI: CHRISTOPHER MWAKASEGE
Utangulizi SI MAPENZI YA MUNGU TUWE MASIKINI! (Namna ya mkristo kuishi katika hali ngumu ya...
By GOSPEL PREACHER 2021-11-19 07:19:55 0 12K