MAJIRA YA KANISA LA LAODIKIA

0
7χλμ.

(1) MLENGWA WA KANISA

Mlengwa hapa ni kanisa lililoko Laodikia


Laodikia ulikuwa ni mji ambao ulikuwa maili zipatazo 40 kaskazini mwa mji wa Efeso. Kama jinsi tulivyokuwa tukijifunza kuwa miji yote hii ilikuwa katika Asia ndogo ambayo kwa sasa katika ramani ya sasa ni katika maeneo yanayokuwa karibu na Uturuki


Mji wa laodikia ulikuwa ni mji uliojaa utajiri mwingi sana. Katika Miji ya Asia ndogo, Laodikia ulikuwa ni mi uliokuwa umejaa utajiri wa kila namna. Ilikuwa ni Eneo au mji ambao wafanyabiashara wakubwa wazito, matajiri sana walikuwa eneo hili. Maduka mengi yaliyokuwa yanauza dhahabu yalikuwepo hapa. Watu walikuwa wanachukua dhahabu sehemu mbalimbali na kuja kuziuza hapa. Kwahiyo watu hapa hawakuwa mafukara, wengi wao walikuwa matajiri wa kifedha na mali, walikuwa wanaishi katika majumba ya kifahari wakiwa na vitu vya kisasa kwa Nyakati zao ukilinganisha na wale waliokuwa wanaishi sehemu nyinginezo na sehemu nyingine a dunia za Nyakati hizo


Kwasababu kulikuwa ni mahali pa watu matajiri hapa Laodikia, watu walichukuliwa na anasa za kila namna. Kwahiyo kulikuwa ni eneo la kila namna ya anasa ambayo ungeweza kuitaja, kulikuwa na maholi ya dansi, walikuwa wakilewa pombe na kucheza dansi na anasa za kila namna zikifanyikia hapa. Na watu wengi waliokuwa wametoka sehemu nyingi mbalimbali wakiwa wameleta dhahabu na madini mbalimbali kuja kuyauza hapa, na vifaa mbalimbali kama ilivyo katika miji yetu mingine. Sasa baada ya kuwa wamepata fedha baada ya mauzo yao walizitumia katika anasa za namna nyingi mbalimbali ambazo zilikuwa zimezagaa kila kona kila mahali


Si hilo tu, Hapa Laodikia kulikuwa na shule ya uganga (Medical School) ambayo ilikuwa maarufu sana katika dunia ya Nyakati hizo. Na moja kati ya kazi za shule ya uganga iliyokuwepo katika Laodikia iliyofanya shule hiyo kusifika sehemu nyingi mbalimbali ilikuwa ni UVUMBUZI WA DAWA YA MACHO. Dawa ya macho ambazo zinakuwa kama za mafuta mafuta ambazo watu wanapokuwa wanaumwa macho ambayo yanaleta shida za namna mbalimbali kunakuwa na dawa za kupaka ambazo zinakuwa za mafuta mafuta, zinazokuwa kwenye chupa Fulani alafu mtu udondoshewa dawa hiyo ktk macho alafu yale macho yaliyokuwa yanauma yanakuwa hayasumbui tena kama mwanzo.


Sasa dawa hii ya macho ilivumbuliwa hapa na kutengenezwa hapa Laodikia kutokana na kazi zilizokuwa zinafanyika katika shule hiyo yya uganga iliyokuwepo hapa laodikia Nyakati hizo


Kwahiyo tutaweza kuelewa vizuri huko mbele ya somo letu, baadae Yesu kristo katka UFUNUO 3:17 inazungumzia watu hawa walikuwa matajiri sana na hawakuwa na haja ya kitu kwa Nyakati zao na tena tutaweza kuelewa vizuri huko baadae kwanini anazungunmzia “ NAKUPA SHAURI UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO”, Hapa kulikuwa ni mahali ambapo kulikuwa na dhahabu nyingi ikiuzwa na kununuliwa. NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA- Kulikuwa na mavazi ya kila namna kwasababu ni matajiri walikuwa wanabadilisha nguo mara chungu mzima katika kuonyesha ufahari wao


Na anasema “NA DAWA YA MACHO YA KUIPAKA MACHO YAKO UPATE KUONA”, hapa tunaweza kuelewa kwanini Yesu kristo anazungumzia dawa ya macho kwamba waweze kukunua dawa ya macho kwa Yesu ili wapate kuona. Ni kutokana na dawa ya macho ambayo ilikuwa inatengenezwa hapa Laodikia kutokana na uvumbuzi uliofanywa na shule ya kiganga iliyokuwepo hapa Laodikia


Sasa kutokana na utajiri uliokuwepo katika mji wa Laodikia, watu wengi walipuuza mambo ya Mungu,Hawakuona maana ya kujishughulisha na mambo ya Mungu lakini mawazo yao yote yalikuwa kutafuta fahari ya dunia. Na kulikuwa na kejeli za kila namna kutoka kwa hao matajiri na hawa wasomi ambao walikuwepo kutokana na shule mbalimbali kuwepo hapa laodikia pamoja na shule hii ya uganga ambayo tumeshajifunza habari zake.


Wasomi walikejeli mambo ya Mungu, Mambo yaliyohusu biblia waliyakejeli na kuyaona kwamba ni hadithi tu ambazo zimetungwa na wanadamu kuataka kuwafanya watu wasizame katika anasa za dunia,Na wakakejeli kwamba hayo ni ya watu ambao ni maskini ambao hawana fedha, ambao hawajasoma, hawana nafasi katika maisha, kwahiyo wakaona hayo mambo yanaweza kusikilizwa sehemu nyingine katika dunia ambazo ni maskini wasiokuwa na kitu lakini watu wa hapa Laodikia wakasema hawana kazi na mambo ya Mungu. Kwahiyo wakaendelea katika anasa zao, wakawa ni WATU NI WENYE KUPENDA DANSI kupindukia, wakawa ni watu wenye kupenda kila namna ya anasa na mambo tu ya kidunia


Kanisa la laodikia sasa, kutokana na mazingira yaliyolizunguka, kanisa hilo nalo likawa na watu waliosemekana wameokoka lakini ni jina tu kwamba wameokolewa lakini wao nao wamechukuliwa na mambo tu ya dunia yaliyokuwa yameishika Laodikia. Kwahiyo wakawepo watu katika kanisa la laodikia waliosema wameokoka lakini wamekuwa wakijihusisha na kucheza dansi kama watu wa dunia.


Wakawepo watu waliokuwa katika kanisa la laodikia ambao WALIKUWA HATA WAZITO KUHUDHURIA IBADA kwasababu ya kuchukuliwa na anasa na mambo mengi ya kidunia katika mji wa laodikia, Masumbufu ya dunia,masumbufu ya maisha yaliwashika kipekee sana sana watu wa kanisa la laodikia kiasi cha kwamba kwao kujifunza neno ilikuwa ni mzigo kwao mpaka katika kushurutishwa sana ndipo kuweza kuja kanisani na hata walipokuja kanisani viwango vyao vya usafi na utakatifu vilikuwa ni vya chini sana maana ilikuwa vigumu sana kuwatofautisha watu wa kanisa la laodikia na watu wa duniani.


Na kwasababu hiyo hawakuwa na sifa zozote za kuwatambulisha kama watu waliomuaini Yesu kwasababu maisha yao ayalikuwa hayana tofauti kwa kiasi kikubwa na watu wa dunia waliokuwa wamewazunguka


Kwahiyo kwa ujumla wake ni kwamba watu walijiita wameokolewa kama tu jina ila ule moto wa wokovu ulikuwa haupo kabisa katika kanisa la laodikia lakini yale mambo ya kidunia yalikuwa yameingizwa kanisani, na kanisa lilikuwa na watu wachache wenye uwezo na walikuwa hawako tayari kuongozwa na neno hasa pale neno linapokuwa linawapa msisitizo wa kufanya mambo ambayo yatawagharimu kuacha hiki au kile ambacho wamekizoea katika desturi zao za anasa na za ulimwengu


Kwahiyo walichagua neno la kulifanya maana walipenda yale maneno ambayo hayawabughudhi, walipenda yale maneno ambayo hayawagharimu, walipenda yale maneno ambayo hayawafanyi kuacha hiki au kile ambacho ni sehemu ya anasa walizozizoea. Hiyo ndio ilikua hali ya kanisa la laodikia Nyakati za mtume Yonana na ndio yalikua mazingira ya mji wa laodikia ambayo yatatusaidia kujua juu ya onyo/kalipio la Bwana Yesu juu ya kanisa hili la laodikia na kuhusiana na mambo ya unabii kuhusiana na majira haya tuliyo nayo kuhusiana na laodikia.


(2) WASIFU WA YESU KRISTO


UFUNUO 3:14

“Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo YEYE ALIYE AMINA, SHAHIDI ALIYE MWAMINIFU NA WA KWELI, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU. ”


YEYE ALIYE AMINA


Anajitambulisha hapa Yesu kristo kama AMINA. Neno AMINA lina maana nyingi mbalimbali. Tunapolitumia mwisho wa sala linamaanisha “NA IWE HIVYO”. Lakini linapotumika mwanzoni, na mara nyingi limekuwa likitumika “AMINI AMINI NAKWAMBIA” 2WAKORINTHO 1:20 inatumika NDIYO NA AMINI. Sasa Neno hilo linamaanisha “HAKIKA” au “KWELI ILIYO HAKIKISHWA”. Yesu kristo ni Hakika, ni kweli iliyohakikishwa, ni kweli iliyothibitisha


Sasa hapa anapojitambulisha kama yeye ni AMINA anamaanisha Yeye ni kweli iliyohakikishwa. Na watu hawa kama ambavyo tumetangulia kuzungumza katika watu wa laodikia, waliona maneno ya Bwana Yesu na maneno ya Mungu kwa ujumla ya biblia kwamba ni maneno kama ya hadithi tu zilizotungwa ili kuwafanya watu waache anasa. Ndio maana Yesu kristo anajitambulisha kama AMINA yaani Kweli iliyohakikishwa


Anazungumza na watu wa laodikia ambao walikuwa hawaamini maneno ya Mungu walikuwa wanayaona kama hadithi,hawakuyatilia uzito kutokana na utajiri wao na wengine kutokana na usomi wao. Na hivyo anakuja kwao kwa wasifu wa yeye aliye amina, Yeye aliye kweli iliyohakikishwa


YEYE ALIYE SHAHIDI MWAMINIFU NA WA KWELI


Yesu vile vile alijitambulisha katika kanisa la laodikia kama shahidi aliye mwaminifu na wa Kweli. Yesu kristo alipokuwa duniani alikuwa shahidi mwaminifu na alijaribiwa sawa saw aba sisi katika mambo yote lakini hakutenda dhambi kwahiyo akawa shahidi.


Kwamba inawezekana kuishi maisha yanayompendeza Mungu na kuwa mbali na dunia, kwahiyo sio hadithi, sio kwamba ni viwango viliwekwa ambavyo haviwezekani kutimilizwa lakini ni viwango ambavyo vinawezekana kabisa kutimizwa hapa duniani na Yesu kristo alikuwa shahidi mwaminifu na wa kweli na alivyotimiza viwango hivyo alijaribiwa sawa sawa na sisi katika mambo yote lakini hakutenda dhambi


Kwahiyo anakuja kwa watu wa laodikia ambao sio tu waliona mafundisho ya biblia kama hadithi lakini waliona mambo hayo ni yasiyowezekana kutimizwa, waliona kwamba ni viwango vya usafi na utakatifu isivyowezekana kutimizwa. Ndio maana anakuja kwao kama Aliye shahidi mwaminifu na wa kweli


YEYE ALIYE MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU


Yesu tena hapa anajitambulisha kama Mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

Watu hawa kutokana na usomi ulioanza kuwepo na utajiri wao, hapa laodikia walianza kuhoji mambo yanayohusiana na uumbaji wa Mungu na wakaanza kuondoa imani yao kwa Mungu kutokana na uwezo wao wa kifedha na usomi uliokuwepo hapa na hawa watu waliokuwa wanaanza kuvumbua dawa waliokuwa katika shule za kiganga wakawa wako msatari wa mbele kuhoji juu ya uumbaji wa Mungu


Kwahiyo ndio maana Hapa Yesu akajitambulisha kuwa MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU kwamba hapo mwanzo kulikuwapo Neno na huyo Neno ndio Mungu,ndiye muumbaji mwenyewe, ndiye mwanzo wa uumbaji wote. Kwahiyo Yesu hapa anajitambulisha kama MUUMBAJI, anajitambulisha kama mwenye vitu vyote wanavyojivunia walaodikia kuwa hivyo vyote vimeumbwa na Mungu mwenyewe, fedha na dhahabu zote wanazojiunia vyote ni mali ya Mungu


Kwahiyo Yesu anakuja hapa kama MUUMBA yeye ambaye vitu yote ni mali yake, kwahiyo pale wanapofikiri kuwa wao ni matajiri, kwamba pale wanapofikiri wana kitu hawana kitu mbele za yeye aliye mwanzo wa kuumba kote. Pale wanapofikiri wao ni wasomi hawana kitu wanachokijua lakini ni sehemu Ndogo tu ya yale waliyofunuliwa na huyo mwenye maarifa yote ambaye aliumba vyote vikapata kuwako. Kwahiyo anajitambulisha kwa kanisa la laodikia kwa jinsi hii kama tutakavyoweza kuona jinsi hayo anavyohusika kipekee katika kizazi hiki tulicho nacho tutakapokuwa tumesogea mbele kuangaia kuhusiana na unabii unaohusiana na laodikia katika majira haya tuliyo nayo


(3) SIFA NJEMA ZA KANISA


Katika makanisa yote 6 tuliokuwa tumekwisha kujifunza habari zake kila kanisa lilikuwa na sifa njema ambazo Yesu alizitaja juu ya kanisa husika. Utaona EFESO linatajwa hapa UFUNUO 2:2 inataja sifa njema ya kanisa ndipo utaona anakuja kuzungumzia juu ya kalipio, ndio iliyokuwa hata kwa makanisa haya mengine. Katika SMIRNA anasea naijua diki yako na umaskini wako lakini u tajiri, anaeleza hapa kuwa hawa walionekana ni maskini kwa nje lakini walikuwa ni matajiri sana katika mambo ya rohoni. Na kwa PERGAMO anasema katika UFUNUO 2:13 bado anataja sifa njema za kanisa ndipo anamaizia LAKINI NINAYO NENO JUU YAKO. Kwa THIATRA anasema Katika UFUNUO2:19 kwa kutaja sifa njema ndipo anamalizia kalipio


Kwa SARDI anasema anajua matendo yake ya kuwa ana jina la kuwa hai kumbe amekufa lakini UFUNUO 3:4 inasema Una majina machache ambayo hawajayatia mavazi yao uchafu, utaona pamoja na SARDI iliyokuwa na matatizo makubwa lakini bado kulikuwa na majina machache ambayo hapa anayasifu kuwa yalifanya vizuri. Kwa FILADEFIA hapo sasa ndipo waraka wote unazungumzia juu ya sifa jinsi waliyokuwa wamelishika neno lake kwa namna isiyo ya kawaida na anaeleza jinsi aliyowapenda kipekee


Lakini kitu tunachokiona hapa tofauti na makanisa haya mengine, ni kuwa kanisa la laodikia pekee yake, YESU hatoi sifa njema za kanisa kwa kanisa hilo la laodikia. Kwahiyo hakuna sifa njema zozote kwa kanisa la aodikia ila utaona moja kwa moja katka mstari ule UFUNUO 3:15 na kuendelea anaanza kuleta makalipio tu moja kwa moja wala hazungumzi chochote juu ya sifa njema za kanisa


Kwahiyo laodikia hakukuwa na kitu chochote cha kupongezwa kwa kanisa la Laodikia wala sifa yeyote njema iliyotajwa. Tuliweza kuona kwa kanisa la Filadefia na Smirna hakukuwa na kalipio lakini sasa hapa Laodikia hakukuwa na sifa njema zozote ziizo tajwa kwamba ni njema kuhusiana na kanisa la laodikia, lakini ilikuwa ni kalipio tu. Maanake kanisa hili lilimuudhi kipekee sana Bwana Yesu maanake halikuwa na jema lolote kwake, lilikuwa ni vuguvugu lisilofaa kabisa mbele yake.

 

(4) KALIPIO

{UFUNUO 3:15-17}

“Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi
au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa
changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa
wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. ”


  • YESU ANACHUKIA WATU AMBAO NI VUGUVUGU


Kanisa la laodikia kwa msingi huo analitaja kwamba ni VUGUVUGU, si baridi wala si moto. Watu ambao wanatajwa ni baridi ni watu ambao hawajaokoka kabisa na wale walio moto ni wale ambao kweli ni wanafunzi wa Yesu wanaoishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu ambaye ni moto ulao hivyo nao watoto wa Mungu wanakuwa ni moto


Sasa hawa Vuguvugu kwa Mungu hawapo wala kwa shetani wanajifanya vile vile hawako kwahiyo wamechanganya tu mambo yote, wanachukua kwa shetani na kwa Mungu kidogo, watu hawa sasa ni Vuguvugu. Kwahiyo Yesu kristo hapa anasema VUGUVUGU ATAWATAPIKA WATOKE KATIKA KINYWA CHAKE


Sasa Yesu kristo anachukia kabisa mtu ambaye ni vuguvugu, ni afadhali mtu awe ni baridi awe hajaokoka kabisa kuliko mtu ambaye anadai kwamba ameokolewa wakati duniani yupo hana tofauti na watu wa dunia na katika viwango vya kristo hayupo, anachanganya tu masomo, mtu wa namna hiyo asidhani ya kuwa atamuona Mungu


  • YESU ANAWACHUKIA WATU WANAJIONA NI MATAJIRI WA DUNIA HII, WASOMI NA ANAWAITA MNYONGE, NA MWENYE MASHAKA, NA MASKINI, NA KIPOFU, NA UCHI.


Yesu kristo anachukia kabisa mtu ambaye wanajiona ni matajiri kutokana na utajiri wa dunia hii, wanaojiona ni wasomi kutokana na maarifa tu kidogo waliyopewa na Mungu mwenyewe na wanafikiri kutokana na hayo hawana haja ya Mungu, Yesu kristo anawaita hao kuwa ni MASKINI.


Wanafikiri kuwa ni matajiri kumbe ni maskini kwasababu vyote walivyo navyo hawatakwenda navyo popote, Utajiri walionao hawata kwenda nao popote watakapozikwa wataishia kwenye numba hiyo Ndogo, KABURI na sana sana watakwenda na nguo hiyo moja tu watalazwa katika sanduku hilo, basi na hakuna chochote cha ziada. Utajiri wao wanaojivunia utakuwa umewasaidia nini?


Kwahiyo hao wanaofikiri kwamba ni matajiri hawana haja ya Mungu ni WANYONGE, WENYE MASHAKA NA MASKINI WAKUBWA. Kutokana na jinsi wanavyovaa sana kifahari na kutokana na jinsi wanavyojipamba sana, Mungu anawaona wako UCHI hawana mavazi yeyote kwasababu mbele za Mungu mtu ambaye anafanya dhambi yupo uchi(dhambi inatufanya tuwe uchi). Adamu na hawa baada ya kuwa walipofanya dhambi baada ya kuwa wamekula matunda waliyokatazwa kuyala tayari walijiona wakiwa UCHI.


Dhambi inatufanya tuwe VIPOFU mbele za Mungu, kwasababu Neno la Mungu linasema YOHANA 9:39-41 “Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao
wanaoona wawe vipofu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, JE! SISI NASI TU VIPOFU? YESU AKAWAAMBIA, KAMA MNGEKUWA VIPOFU, MSINGEKUWA NA DHAMBI; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa. “ Yesu aliwaaambia watu hao ni Vipofu kwa hakika


Mtu yeyote mwenye dhambi ni kipofu, kipofu anaweza kunywa maji machafu au chakula kichafu kwasababu haoni uchafu wake, anaweza kupata mbali na barabara halisi na akatumbukia shimoni ndivyo alivyo mwenye dhambi haoni kinachofuata hivyo kwake kilicho kibovu kilicho kibaya kinaweza kuonekana safi, anaweza kunywa pombe akaona ni kitu kizuri, yote ni kwasababu ni kipofu haoni, anaweza akavuta sigara akafikiri ni anasa kumbe anaona ni anasa kwasababu ni kipofu haoni,a naweza kucheza dansi akaona ni kitu cha kufurahisha kumbe ni kwasababu ni kipofu haoni.


Uasherati na uzinzi kwake anaweza kuuita uroda kwasababu ni kipofu hajui kuwa ni kitu kitakachomuangamiza milele na milele, Upofu wake ndio unamfanya aiite dhambi ya uasherati ni uroda na Upofu wa mtu huyu ndio unaoweza kumfanya Kuuita wizi kuwa ni utapeli anafikiri ni kit utu Fulani cha ujanja ujanja na anajaribu kuuwekea rangi wizi ili uonekane si wizi lakini wizi ni wizi tu ingawa shetani amekuwa anajaribu kubadilisha majina kwa kuupaka paka rangi. Ataita wizi kusogeza, ataita wizi ni utapeli ataita wizi majina mbalimbali ili kupunguza nguvu yake, ila wizi unabadki bado kuwa wizi ila kwasababu wao ni vipofu wataweza kuona wizi ni kusogeza au utapeli. Wataweza kuona Rushwa ni takrima, ni vipofu wana dhambi ndani mwao. Dhambi inawafanya watu hawa kuwa vipofu hawawezi kuiona dhambi kama dhambi na kuiona jinsi inavyochukiza


Yesu kristo sasa anasema juu ya watu hawa kwamba ni vipofu na uchi. Na ni muhimu kila mmoja wetu kufahamu waziwazi kwamba tukiwa kweli tumemaanisha kuwa wakristo basi hatuna budi kweli kufuata nyayo za Yesu kinyume chake ni afadhali kabisa tuwe wapagani kwasababu uvuguvugu hauwezi kabisa kutusaidia kumuona Mungu maana unatupotezea tu muda wetu kwasababu Vuguvugu watatapikwa kabisa katika kinywa chake hawana nafasi, kinyonge hakitaingia katika mji ule. Haiwezekani watu wengine wawe wameingia kwa kukatwa vichwa, wakaingia kwa kuchomwa moto kama tulivoona wengi wao wakati tulipokuwa tunaangalia majira ya smirna hivyo haiwezekani sisi tuingie kwa urahisi rahisi tu kwa kukwepa gharama tukifanya mambo yote ya dunia alafu tukaingia katika mbingu hiyo hiyo, Hapana maana Kinyonge hakitaingia kabisa UFUNUO 21:27


Vuguvugu hawataingia kabisa katika mji ule wa mbinguni wala kinyonge, kama tumeamua kuokolewa hatuna budi kukubali gharama zote na kufuata yale yote yanayotupasa kufanya lakini tukiwa tunatafuta maandiko yanayotufariji kwa maandiko ambayo hayatubughudhi kama ilivyokuwa Nyakati za kanisa la laodikia tutakuwa tunajisumbua bure kuja kanisani ni afadhali tuwe duniani kabisa na kumaliza nguvu zetu huko. Kama tumechagua kula nguruwe basi tule nguruwe aliyenona


(5) MAELEZO KUHUSU JINSI YA KUFANYA


{UFUNUO 3:18-20}

“Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi
meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako,
upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu. Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. ”


  • UNUNUE KWANGU DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO, UPATE KUWA TAJIRI, NA MAVAZI
    MEUPE UPATE KUVAA


Kwakuwa unasema MIMI NI TAJIRI umejitajirisha wala sina haja ya kitu wakati hujui wewe ni mnyonge, mwenye mashaka maskini na uchi, sasa Bwana Yesu anatoa ushauri na haya ndio maelekezo ya kufanya anaeleza kama ni Vuguvugu basi tununue kwake dhahabu iliyosafishwa kwa Moto tupate kuwa tajiri. Utajiri halisi unapatikana kwa Bwana Yesu na ndio anasema tuutafute huo


Tunapokuwa ni watakatifu tunakuwa ni Matajiri, Lazaro ingawa alionekana maskini hapa duniani ukilinganisha na Yule Tajiri katika LUKA 16 lakini hatimaye wote walikufa. Lakini alivyokufa Tajiri Yule alikwenda katika moto katika mateso mazito na ule Lazaro akawa ndio tajiri milele akitembea mbinguni kwenye barabara zenye dhahabu safi inayong’aa kama kioo


Na tukiwa watakatifu sasa tutakuwa warithi pamoa na kristo, tutakuwa warithi pamoaj na utajiri wake wote Mungu na hautakuwa utajiri wa muda mfupi ila utakuwa ni utajiri wa milele na milele


Pia anasema TUTAFUTE MAVAZI YA KUVAA KWAKE ILI APATE KUFICHA UCHI WETU. Mungu mwenyewe ndiye aliyetafuta mavazi ya ngozi na kuwavika adamu na hawa katika ile bustani ili kusitiri uchi wao ingawa walijaribu kuivika mavazi ya majani lakini bado hayakuwasaidia kuficha uchi wao. Mavazi ya kuvicha uchi wetu yanatoka kwa Mungu mwenyewe na lazima Damu ihusike katika kutupa mavazi hayo, damu ya Yesu kristo iliyomwagika msalabani ikitusafisha dhambi zetu ndipo tunaweza kupata mavazi meupe, mavazi safi, mavazi ya utakatifu ambayo hayo yanaficha uchi wetu tunaonekana wa thamani mbele za Mungu


  • UNUNUE KWANGU DAWA YA MACHO YA KUJIPAKA MACHO YAKO, UPATE KUONA


Dawa halisi ya kujipaka macho ambayo tunapaswa kuitafuta sio ile dawa ile dawa iliyokuwa inapatikana Laodikia iliyokuwa imevumbuliwa na wale wataalam katika shule ya uganga ya laodikia lakini ni dawa ya macho itokayo kwa Yesu kristo ambayo itaondoa upofu wetu hata tupate kuiona dhambi kama dhambi, tupate kuyaelewa mambo a rohoni, tupate kufunuliwa macho tupate kuona mambo ya rohoni, tunafikiri tunajua kumbe hatujui


Na Yesu kristo akamwambia petro wewe usingeweza kuniita mwana wa Mungu aliye hai isipokuwa tu umefunuliwa na Baba, Damu na nyama havikukufunulia hili ila baba yangu wa mbinguni. Kama tunataka kuyaona mambo yaliyofichika katika mambo ya rohoni hatunabudi kuwa na macho ya rohoni kwasababu mambo ya rohoni yanatambulikana tu kwa jinsi ya rohoni lakini kwa namna tu ya kutumia akili hatuwezi kuyaelewa mambo ya rohoni. Ndio maana mtu ambaye anafikiri ni msomi sana atakuwa ni mjinga sana katika mambo ya rohoni kwasababu ya rohoni yanatambulikana kwa jinsi ya rohoni si kwa jinsi ya akili


Kwa akili hatuwezi kumfahamu Mungu, sisi katika akili tunapofikiri kwamba ni wasomi sana na akili zetu zinapolinganishwa na akili za Mungu ni sawasawa na akili ya kitoto kichanga, kidogo zikilinganishwa na akili za mzazi wake. Kitoto kidogo kitakuwa kinamuuliza mzazi anapokuwa amerudi kujifungua na kusema “mama huyu mtoto umemnunua wapi?” maana kwa akili yake ya kitoto anafikiria huyu mtoto ananunuliwa mahali kama madoli yanavyonunuliwa mahali Fulani basi anadhani ndivyo mtoto anavyoweza kununuliwa.


Kwahiyo mzazi utapoteza mda wako kuzungumza na Yule mtoto ili umueleze huyu mtoto mwingine amepatikana wapi?Utapoteza muda wako sana kwasababu upeo wake ni mdogo sana, hawezi kuelewa hata ungemueleza. Na ndivyo Mungu alivyo tukilinganishwa nae, akili zetu ni za kitoto kiasi hicho. Akili hizo unazoona wewe kuwa una PHD mbele za Mungu wewe ni mtoto kwa kiasi hicho. Akili zako na upeo wako ni mdogo sana kiasi cha kwamba huwezi kufahamu mambo ya Mungu na ndio maana hata unapopiga makelele na kujifana mjuaji Mungu ananyamaza kimya tu, akwambie nini? Utaelewa nini? Wewe ni kama kitoto kichanga! Kwako ni sawa sawa na hako katoto kanachowaza mawazoni mtoto ananunuliwa tu mahali Fulani. Akili yako ya PHD ni fupi sana ni Ndogo sana,upeo wako ni mdogo huwezi kujua mambo ya Mungu, Kwahiyo ni vizuri kutulia kimya na kumsikia Mungu anapotuambia tufanye


Na anasema hapa Kwamba tukisafishwa macho yetu kwa dawa ya macho, ambayo inapatikana kwa kristo mwenyewe, macho yetu yatafumbuka. Hatuielewi biblia kwasababu macho yetu hayajafunguka wala hatuelewi juu moto ndio maana kuna watu wengine wanaweza kupiga kelele na kusema “Moto mimi unanitisha nini? Kama ni moto wacha niende motoni”. Mtu huyu hajui moto ni nini? Ndio maana unaweza kupiga kelele na kusema niacheni niende motoni kwasababu macho yako hayajafunguka kujua moto ni nini?,Macho yako hayajafunguka hata kujua mbinguni ni nini? Omba dawa ya Macho kwa Yesu akupe kujua mbinguni ni nini?


Ukijua mbinguni nini utaangaika lakini watu wengine utawakuta wanalalamika kuona mtu anaenda kanisani mara kwa mara wanataka iwe ni jumapili tu ila wanashangaa mtu anayeangaika kwenda kanisani hata kwenye ibada za katikati ya wiki, Mtu huyo analalamika ni kwasababu macho yake hayajafunguka ndio maana huwezi kujua kwanini anaenda kanisani mara kwa mara na hujui kuna faida gani ya kuja kanisani wakati wote!Macho yako hayaoni, omba dawa ya macho maana dawa ya macho ikipitishwa kwako utaweza kuona kwanini watu wanakuja kanisani hata kwenye ibada za katikati ya wiki siku za kuichambua biblia


Na unaweza kupiga kelele eti “unaona mnadanganywa kuwa eti Mungu anaweza kutuunguza kwenye moto, ebu waza kweli wewe mzazi unaweza kweli kumchukua mtoto wako ukamuingiza kwenye moto, kweli? Kama huwezi basi Mungu hawezi kutuchoma na kutuunguza kwenye moto”. Ni kweli unasema hivyo kwa majigambo kwasababu wewe ni kipofu una macho ya kuona, ungefunguliwa macho na dawa hii ya macho ingepakwa kwenye macho yako ungejua hasira za Mungu kwamba aliweza kuteketeza sodoma na gomora wote hata na vitoto vichanga vilivyokuwemo!Ungefunguliwa macho ungeweza kujua ni LUTU na mkewe ndio walioweza kutolewa huko katika sodoma na gomora ndio ungejua Mungu anapokasirika, hasira zake zinatisha kiasi gani? Ndio maana maandiko yanasema sehemu nyingine kuwa INATISHA KIASI GANI KUANGUKA MIKONONI MWA MUNGU ALIYE HAI!


Ungejua kwamba wakati wa Nuhu kwamba dunia yote iliangamizwa wakabaki watu 8 tu, usingesema unayosema. Ungejua hasira za MUNGU zinapowaka hawezi kuangalia maana anaweza kufutilia mbali kizazi chote akaanza upya kuumba kwasababu kwake wanadamu ni kama madongo tu ambayo yeye kama mfinyanzi anaweza kuyaharibu madongo hayo aliyoyaumba akaanza kuyafinyanga tena upya. Ungemjua MUNGU jinsi alivyo ungeutimiza wokovu kwa kuogopa na kutetemeka


  • WOTE NIWAPENDAO MIMI NAWAKEMEA, NA KUWARUDI; BASI UWE NA BIDII, UKATUBU


Yesu Anasema WOTE NIWAPENDAO MIMI NINAWAKEMEA NA KUWARUDI. Kaka zangu na dada zangu wako watu wengine wasioelewa ambao wanachukia kukemewa, wakikemewa tayari wanakuja juu “oooh basi kama ni hivi afadhali nihame kanisa” hawataki kukaa mahali wanapokemewa na kurudiwa. Utawasikia wanasema “Yaani Inakuwaje mchungaji huyu atukemee namna hii kama watoto wadogo wakati sisi ni watu wazima tuna akili zetu tuna usomi wetu?inakuwaje tukemewe namna hii?”. Biblia inasema YEYE ACHUKIAYE KUKEMEWA ATAKUFA


Na lazima tufurahie kukemewa na kurudiwa WAEBRANIA 12:5-13 tunajifunza hapa katika mistari hii kwamba tunatakiwa tusiyadharau marudia ya Bwana, tusizimie mioyo yetu ikikemewa naye, anasema yeye ambaye Bwana anampenda humrudi na tena umpiga kila mwana anayemkubali na ni mwana Yupi asiyerudiwa na babaye? Na maandiko yanaendelea kusema Kama hatutaki kukemewa/Kurudiwa basi sisi ni wana wa haramu si wana wa halali.


Lakini kama kweli sisi ni wana wa halali wa Mungu tutafurahia kukemewa kwasababu kwa kukemewa, kwa kurudiwa, kwa kupigwa hata akufikishe mahali maana tunaweza kupitishwa katika adhabu kuwa Fulani na Fulani kuanzia sasa hivi hutakiwi kuwepo katika kanisa hapa na unatengwa katika kanisa kwamba awaye yeyote asikusalimu, Tufurahie adhabu hata kama hizo maana adhabu hizo zina lengo la kutufanya tuushiriki utakatifu wa Mungu na pale ambapo tunafurahi tu kuweepo mahali ambapo hakuna adhabu, hakuna kukemewa, hakuna kurudiwa kama ilivyokuwa ilivyo katika kanisa la laodikia basi tujue tunakwenda pabaya, tuna kwenda kutapikwa kabisa na Bwana Yesu maana anasema WALE ANAOWAPENDA HUWARUDI, tunachotakiwa kufanya tunaposikia tunakemewa kwa neno lake tunatakiwa kuwa na BIDII NA KUTUBU MARA MOJA NA KUACHA YALE TULIYOKUWA TUNAYAFANYA


  • TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI, NABISHA; MTU AKIISIKIA SAUTI YANGU, NA KUUFUNGUA MLANGO, NITAINGIA KWAKE


Yesu anaendelea kusema TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI, NABISHA; MTU AKIISIKIA SAUTI YANGU, NA KUUFUNGUA MLANGO, NITAINGIA KWAKE, NAMI NITAKULA PAMOJA NAYE, NA YEYE PAMOJA NAMI. Hivyo anasema tukiwa tayari kutubu anaingia na tunakula pamoja nae na kuwa pamoja nae milele na milelekule mbinguni pale alipo na sisi ndipo tutakapokuwapo


Hivyo maonyo haya Yesu hakuyatoa kwa kanisa tu la laodikia bali hata kwako ambaye unajifahamu uko vuguvugu, unaishi maisha ya unafki, unajiita umeokoka lakini bado unapenda dunia. Yesu anazungumza na wewe ambaye hujaokoka ambaye unatumia akili kufikiri kuwa Wokovu ni kuchanganyikiwa hivyo anasimama hapa mbele yako kupitia Somo kama hili na yote uliyojifunza ANABISHA HODI! Je utafungua mlango wa Moyo wako ili aingie na ili akupe hiyo dawa ya macho uweze kuiona dhambi kama dhambi na kupewa mavazi meupe ili uufiche uchi wako kwa kuishi maisha ya utakatifu katika ulimwengu huu wa sasa?. Yesu anataka ukupatie uwezo wa kushinda dhambi na kushinda hali ya uvuguvugu uliyo nayo ili apate kukaa na wewe pamoja nae milele na milele mbinguni



Basi ikiwa hujaokoka wasiliana name nikuombee au unaweza kutafuta kanisa lolote linalohubiri wokovu au mtu yeyote aliyeokoka akuombee upewe uwezo wa kushinda dhambi na upokee Yesu. Hata kama umeguswa na unahitaji kubadilika kutoka katika hali yako ya uvuguvugu uliyo nayo basi pia unaweza kufanya hivyo hivyo kwa kuwasilaiana name kwa ajili ya ushauri na maombi au kutafuta msaada kwa mchungaji wako au kiongozi yeyote wa kanisa lako la kiroho upate msaada zaidi na maombi. MUNGU AKUBARIKI KWA KUFUATILIA.

 

(6) AHADI


♨{UFUNUO 3:21} “Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. ”


NITAMPA KUKETI PAMOJA NAMI KATIKA KITI CHANGU CHA ENZI


Yesu kristo anatuambia tukiweza kuwa katika hali ya kuwa moto katika mazingira ya uvuguvugu ambayo yatakuwa yametanda katika majira yetu ya Laodikia ambayo tutayangalia muda si mrefu katika unabii basi tutaketi katika kiti chake cha enzi kama yeye nae alivyopewa kuketi katika kiti cha enzi cha baba yake baada ya kuwa ameishi maisha ya usafi na utakatifu bila dhambi hapa duniani katika mazingira ambayo yalikuwa yamejaa kila namna ya dhambi na ukengeufu


Tutatawala pamoja nae katika utawala wa miaka 1000 wa kristo duniani, tutaketi katika kiti chake cha enzi, sisi nasi tutakuwa wafalme ambao tutatawala pamoja na Bwana Yesu. Na hilo litadhihirika kwa wale watakaokuwa moto na si vuguvugu



(7) UNABII KUHUSIANA NA MAJIRA YA KANISA


KIPINDI NA MAANA YA LAODIKIA


Kama tulivyotangulia kuona uko mwanzo majina yote ya makanisa 7, kila jina lina maana yake,na maana ya jina hilo katika lugha ya asili linakuwa lina maana inayohusiana na yale yanayotokea katika unabii husika. Tumeona huko nyuma jinsi ambavyo Efeso maanake Kupumzika, kuyaachia mema yaondoke. Sardi maanake wale wanaotoroka na majira ya sardi katika unabii yakawa ni majira ya mwaka 1517- 1750 wakati Martin Luther alipotoroka na kuacha kanisa katoliki na wengi wakatoroka wakaacha kanisa katoliki baada ya kuona lipo mbali na imani, lipo mbali na Neno wala hawafanyi yale yaliyoelekezwa na Neno


Sasa Neno LAODIKIA katika lugha ya asili maanake HAKI ZA WASHIRIKA WA KANISA KUFANYA LOLOTE WANALOLITAKA. Maanake lolote wanalotaka kulifanya wasibughudhiwe na mtu wala hawataki mchungaji asiwakemee wala asiwaambie lolote ila lile wanalotaka kulifanya ndio hilo hilo walifanye wala wasiingiliwe na mtu, hiyo ndio maana ya Laodikia


Sasa katika unabii, majira ya Laodikia ndio majira ambayo tunayo sasa. Majira haya yalianza mwaka 1905. Kuanzia mwaka 1750-1905 yalikuwa ni majira ya Filadefia ambavyo kama tulivyoweza kuona kuwa watu waliweza kurudi tena katika usafi na kukaa katika Neno kwa bidii yote. Na sasa kuanzia Mwaka 1905 mpa ka majira ya kunyakuliwa kwa kanisa ndio majira ya Laodikia katika unabii, kwahiyo inamaana kipindi hichi tulichopo ni majira ya kanisa Vuguvugu


Majira ya Laodikia yalianza kwa vyuo vya Theologia mwaka 1905 kuanza kukosoa yale yaliyopo katika biblia na kuanza kuyadhihaki na kuyakejeli. Na haya yalianzia ujerumani, kwani nchi ya ujerumani ni nchi ambayo yenye anasa sana, ni nchi yenye walevi wa kupindukia na ina penda pombe kupindukia kiasi cha kwamba watu wenginie ujerumanii wengi sana wameona ni shida hii mambo ya kununua chupa za bia kuwa inawapotezea muda. Kwahiyo wapo watu wengine ujerumani wao wana mabomba ambayo wanafungulia tu pombe kwenye nyumba zao kwa namna ile ile unavyofungulia maji, alafu wanalipa bili kwa mwezi. Ni nchi ambayo ni wanywaji wa pombe kupindukia


Kwa namna hiyo, sio tu wanajivunia utajiri na ufahari wao, ujerumani wanalinga na kujiona kana kwamba wao ndio bora sana katika mambo ya maendeleo kuliko hata wengine huko ulaya na wanadharau sana hata hizi, nchi nyingine za ulaya. Hivyo wanajionea fahari sana kwamba mtu kuwa mjerumani ni kitu cha kujionea fahari sana kuliko kuwa mwingine katika nchi nyingine zinazowazunguka



CHIMBUKO LA UVUGUVUGU KATIKA MAJIRA YA LAODIKIA


Sasa ujerumani hapa, kuanzia mwaka 1905 ndipo kulipoanza kutokea matatizo ya watu kukosoa mambo ya biblia na kuona kama ni hadithi tu ambazo zinalenga kuwafanya watu wasikae katika anasa au furaha ya maisha, na mambo hayo yalianzia huko ujerumani mwaka huo 1905


Na kile cha mambo haya ilikuwa ni kwamba mtu mmoja ambaye anajulikana kama THOMAS ALTYZER, ambaye alikuwa ni mwalimu wa theologia katika chuo kimoja cha theologia huko ujerumani. Na ndio maana kuna tofauti kubwa kati ya mtu kusema nimefuzu kusoma Theologia na mtu kuwa mwalimu wa biblia. Huyu Thomas baadae kidogo katika miaka iliyofuta baada 1905 alianza kufundisha na kusema Mungu amekufa na akasema kwasababu Mungu amekufa hivyo kanisa linatakiwa lijengwe na wanadamu vile ambavyo wanaona linafaa, kwahiyo Mungu hashughuliki na kanisa lake tena, hivyo akasema kuwa hata ukimuomba Mungu hajibu wala hasikii wala hashughuliki na sisi bali alikuwa anazungumza na waisrael tu ila siku hizi hazungumzi na mtu yeyote kwahiyo Mungu amekufa wala hayupo


Kwahiyo akasema kanisa linafaa kujengwa na wanadamu kama ambavyo wanaona linafaa, na kufikia mwaka 1920, hali ikawa mbaya sana. Huko marekani! Kule nyuma wakati wa majira ya filadefia kule marekani walianza na Mungu kwa hofu isiyokuwa ya kawaida. Taifa la marekani hata Baraka zilizopo sasa hivi bado zimetokana na kile kipindi cha majira ya filadefia. Wakati wa majira ya filadefia kule marekani, kama jinsi ambavyo tuliweza kuona majira hayo yalikuwa kuanzia mwaka 1750-1905.


Hivyo kulikuwa na hofu ya Mungu kule marekani kwa namna isiyokuwa ya kawaida. Hofu ile ilipelekea Fedha ya marekani, yaani hii DOLLAR kuweza kuwa na maneno hayo, IN GOD WE TRUST (KATIKA MUNGU TUNAAMINI). Na hayo yote ilitokana na wimbi la kukaa katika neno katika majira hayo kule marekani. Majira yale, viongozi wengi, marais wa marekani walikuwa wameokolewa na marais hawa walikuwa na hofu ya Mungu isiyokuwa ya kawaida, na yalianzishwa mambo mengi sana ambayo yalileta hofu ya Mungu katika kila eneo la maisha


Kwa mfano iliwekwa sheria kwamba katika shule zote za marekani anapokuwa anakwenda shuleni, mwanzoni kabisa darasa la kwanza anapokuwa anaingia shuleni, marekani baada tu ya kumsalimu mwalimu ilikuwa wote wanaanza kusema amri 10 za Mungu kwa kichwa. Na hali hii imeendelea majira yote ya filadefia na mambo mengi sana ya kiMungu yalikuwepo Nyakati hizo. Ilikuwa masomo ya biblia yanafundishwa, biblia zinakuwepo katika mashule na ilikuwa hata katika vikao vingi vya mashauri vya miji mbalimbali, vikao vilikuwa vinafunguliwa kwa maandiko n. k. Hivyo hofu ya Mungu ikawa imetanda marekani na ndio maana marekani imetumika katika kipindi hicho kuwa chimbuko la kipekee sana sana la kueneza ukristo duniani kote.


Lakini kutokana na wimbi lililoanza mwaka 1905 kule ujerumani ambalo lilipigiliwa msumari na huyu Thomas altyzer. Sasa mwaka 1920 mambo yakaanza kuwa mabaya sana. Katika kanisa moja kule marekani alikuwepo mchungaji mmoja wa kanisa moja ambaye alifika siku moja kanisani, akasema akizungumza na kanisa kuwa, Vitabu 5 vya Musa yaani kuanzia MWANZO mpaka KUMBUKUMBU LA TORATI, akasema vitabu hivi ni vitabu vya historia ya Israel ambayo imeandikwa kwa mifano na hadithi za kubuni na akazifananisha kama ambavyo tunazijua hizi hadithi za watoto.


Akasema hivyo vitabu vyote vimeandikwa ni kama vitabu vya hadithi sio vya ukweli, kwamba eti bahari ya shamu iligawanywa kwa fimbo, hicho sio kitu cha kweli na hakiwezekani, haiwezekani maji yakapatikani kwa fimbo kupiga mwamba tu alafu watu wakanywa maji mamilioni, haiwezekani eti kwale wakaletwa kwa upepo alafu wakaanguka katika kambi za Israel. Akaanza kukosoa kila kitu akasema hizo ni hadithi tu ambazo zimetungwa kama hadithi zinazohadithiwa watoto za paka na sungura ambazo hazina ukweli


Kwahiyo akasema vitabu hivyo 5 anasema amevichunguza akaona ni hadithi tu si za ukweli hivyo tunatakiwa tuzipuuze, maana alikuwa mtaalam wa theologia. Kwahiyo katika kanisa hilo siku hiyo walichana karatasi zote hivyo vitano tangu Mwanzo mpaka Kumbukumbu la torati wakaviondoa katika bibilia. N a jumapili ijayo iliyofuata, mtu huyu huyu akaja tena akasema kipindi chote hicho katika wiki alikuwa anatafakari juu ya vitabu vya unabii kama Isaya, Yoel, Yona, Ezekiel, Yeremia n. k.


Akasema amechunguza ameona ni vitabu vya watu ambavyo wameota ndoto za ajabu ajabu ambazo hatahazieleweki, na ndizo wakawa wanazieleza alafu zikaandikwa na akasema ndio maana ni vigumu kuelewa vitabu hivi vya unabii vinasema nini. Ni vigumu kuelewa DANIEL, EZEKIEL maana maneno yake hayaeleweki kwasababu ni ndoto za ajabu ajabu. na kanisa lote wakasema aaha kumbe ndio maana hatuelewi, akasema ndio hivyo vitabu vyote vya unabii wakavichana katika biblia zao wakaviondoa


Na jumapili inayofuata, akaja tena huyo mchungaji akasema vitabu hivyo vya injili vya MATHAYO, MARKO, LUKA NA YOHANA hivi ni vitabu vya wanafunzi wa Yesu ambavyo kutokana na walivyodanganywa na Yesu waliweza kubuni dini mpya ambaye kiongozi wao alikuwa ni kiongozi wa dini huyu Yesu na kwa lengo kuweza kuwafanya watu waweze kuishi maisha duni (anti-social) ambayo hayana raha wala furaha bali maisha ya ajabu ajabu. Na hao washirika nao wakasema aaha ndio maana tukijaribu kutaka kuishi haya maisha ambayo anataka Yesu tuishi inakuwa ni maisha ya ajabu ajabu tu. Mfano mtu akiipenda dunia, kumpenda Mungu hakumo ndani yake wakaona maisha hayo hawawezi kuyaishi. Basi wakavichukua tena hivyo vitabu vyote vya injili navyo wakavichana chana na kuvichoma moto


Tena akaja jumapili iliyofuata akawaambia kwamba nyaraka zote hizi za zilizoandikwa za mitume mbalimbali kama kina Petro au Paulo, basi nyaraka hizi ziliandikwa tu kwa makanisa yale ya Nyakati hizo. Yaani alisema Waraka kwa wakorintho ulikuwa kwa wakorintho sio sisi, waraka kwa waefeso huko kwa waefeso, sisi ni wamarekani sio waefeso, na waraka kwa wagalatia ilikuwa wagalatia maana alikuwa anataka kushughulika nao wale sio sisi, hivyo alidai Nyaraka zote zilikuwa ni za watu wa Nyakati hizo sio sisi. Basi watu nao wakaamini wakasema aaha kumbe zilikuwa hazihusiki na sisi basi wakayachukua nayo yote wakayachana.


Ina maana biblia nzima ikabaki tea Ufunuo wa Yohana, ila bado baadae akaja akasema Ufunuo wa Yohana huo ilikuwa ameandika wakati amechanganyikiwa, kwahiyo akawa anaandika vitu vya ajabu ajabu, hivyo akadai hicho kitabu cha ufunuo hakina kazi kwetu, hivyo na kitabu hicho nacho wakakiondoa na kubaki na ganda tu la biblia, hivyo washirika wote wakaondoka maana walion wanapoteza muda kwa kitu ambacho hakina maana kwasababu waliona biblia yote haina kazi yeyote na kanisa likabaki tupo na mchungaji nae akaenda zake



KUSAMBAA KWA NADHARIA ZA KUPINGA JUU YA UUMBAJI WA MUNGU


Kitu hicho kikaanza kusambaa na kundelea kusambaa, miaka ile ya 1920 na kitu kuwa na hali ya ajabu sana ambayo inaanza kupenya katika kanisa, na iliendelea kwa namna nyingi mbalimbali na kufikia hapa tulipofikia, hali ni mbaya zaidi, maana wakati huo kulikuwa na mambo mbalimbali ambayo yalikuwa yamevuma mwanzoni mwanzoni mafundisho Fulani ya nadharia ya uumbaji.



Vitu kama Darwin’s theory, mambo ya EVOLUTION, mambo haya ya sayansi kwamba hakukuwa na uumbaji wa Mungu a mbingu na nchi na vitu vyote vilivyomo lakini wanadamu wakaanza hizo nadharia za kisayansi zikaanza katika miaka ya mwanzo ya mwaka 1920 na kwamba mwanadamu alitokana na nyani ambaye alipitia hatua mbalimbali hatimaye nyani akapoteza mkia ndio akawa mwanadamu na kuwepo vitu vya ajabu hivi vya kisayansi ambavyo vinavuma kuhusiana na mwanadamu alivyopata kuwapo vikaaaminika kwa Nguvu sana sana


Kwa mfano hiyo nadharia inayoitwa DARWIN’S THEORY ya mwana sayansi mmoja aliyeitwa Darwin ilivuma sana Nyakati hizo. kwahiyo ikapenya sana makanisani na kila mmoja akiwa na watu wake wakawa na mashaka sana juu ya uumbaji wa Mungu.


Kwahiyo kukaanza kuwa na wakristo ambao ni wakristo kwasababu wamezaliwa wakristo kwasababu ya baba zao ambao waliishi katika majira yale ya filadefia lakini sasa hawamuamini MUNGU na wanaishi tu maisha wanayojua wenyewe


Na utajiri umekuwa wa ngazi za juu sana marekani katika kipindi hiki na taifa limeendelea kuwa tajiri. Ulaya kumeendelea kuwa na utajiri katika nchi mbalimbali. Kwahiyo kwasababu ya utajiri ambao umetanda sasa Ulaya na marekani watu wakawa na usomi mwingi sana ambao umetanda kama Nyakati za laodikia tulivyoona, ndipo watu wakaanza kuona Mungu kwetu ni wa nini?, na hivyo kila kitu sasa kikawa kinaelezwa kwa sayansi kwa sayansi kwa sayansi na ni nadharia nadharia tu za kisayansi kwasababu ya wanasayansi hao ambao walikuwa wanatajwa. Kwahiyo hali ikawa mbaya sana na kufikia hapa tulipofikia unaweza kusema tuna hali nzuri sana AFRIKA kuliko sehemu nyingi za marekani na ulaya


MAKANISA KUGEUZWA KUWA KUMBI ZA MADANGURO NA DANSI


✍Kule sehemu nyingi za ulaya hivi tunapojifunza, ilikuwa Nyakati zile za filadefia kulikuwa na makanisa mengi mengi kila kona kila mahali yaliyochipuka kama uyoga na yakaengwa makanisa ya kila namna na kila design kila kona kila mahali ulaya yote, lakini hivi ninavyoelezea sasa, Makanisa mengi Ulaya magharibi yamefanywa kuwa ma holi ya dansi. Makanisa mengi mpaka hivi tunavyozungumza hayana watu, yanauzwa na kununuliwa kuwa klabu za usiku. Na makanisa mengi sana huko yamefanywa kuwa madanguro


✍Ukifika maeneo mengi katika ulaya magharibi kama Ufaransa, ujerumani kwenyewe, kama uingereza au sehemu mbalimbali za Scandinavia utaona jingo bado limebaki vile vile na kwa mbali utafikiri ni kanisa, na kama umetoka huku kwetu afrika na kwenda kule utadhani ndio umepata sehemu ya kusali lakini ukifika karibu tu utaona bao moja kubwa limeandikwa kuwa ni NIGHT CLUB Fulani. Na humo ndani ni uchafu wa kila namna tangu asubuhi mpaka usiku


✍Majengo mengi ya makanisa yamegeuzwa kuwa madanguro. Na watu wengi wanaosali kule ulaya ni wazee sana. Wazee wengi wa kule utakuta wana miaka 80 au 90 ndio wanaosali na kuwakuta huko kanisani. Ukimkuta kijana wengi watashangaa maana mtu mwenye miaka kumi na kitu aua shirini na kitu au miaka thelathini kwamba yupo kanisani ataonekana ni mtu wa tofauti sana na ndio sehemu nyingi ulaya zipo hivyo na wanaishi maisha ya ajabu ajabu sana na wakiishi mpaka uzeeni wanasema kwasababu wamefika uzeeni na kwasababu hawana hakika sana juu ya haya mambo ya Mungu, sasa basi kama kweli Mungu Yupo basi katika uzee huu kwasababu hatuwezi kucheza dansi basi kama mwanzo hatuwezi kufanya mambo ya ujana ebu twende kanisani ili ikitokea ikiwa kweli Mungu yupo basi atatupokea!! Ndio wanavyosema


✍Hali ya kule ulaya, dada zangu na kaka zangu inatisha sana ulaya kiasi cha kwamba utatamani kulia. Namkumbuka mhubiri mmoja hapa nchini kwetu katika safari zake alivyokwenda ulaya alihubiri injili moja nzito sana akibonda sana mambo yao lakini ile alivyotelemka pale, kulikuwa na mmishenari mmoja alimfuata na kuwambia huu ni wakati wenu waafrika kutuletea injili huku ulaya maana hili bara sasa ndio limekuwa eneola umishenari hivyo akasema kweli huu ndio wakati tunahitaji injili kutoka afrika kwasababu kweli tumekufa


MAKANISA KIROHO KURUHUSU MATUMIZI YA SIGARA HATA KWENYE VYUO VYA BIBLIA


Ninavyokueleza sasa hivi makanisa mengi sasa hivi kule marekani kuliko unavyoweza kufikiria, watu wengi kama wanatoka mahali kama Tanzania kama hajakomaa vizuri kwenye imani alafu akaenda kule, sio vizuri sana kama hajakomaa vizuri katika imani kwenda sehemu kama marekani au ulaya ukasoma kule, inahitaji neema ya Mungu sana kuendelea katika wokovu, maana wengi wanaokwenda kule na wokovu huwa wanauacha wokovu wenyewe


✍Makanisa haya ninayosema ni makanisa ya kiroho haya ninayosema habari zake, wanasema wameokoka lakini wanaenda kanisani wakiwa wanavuta sigara na wanasema hizi sigara baridi hizi hazina tofauti na Big G wanasema “This a just mail sigarate” yaani ni sigara baridi kama SM. Kwahiyo ni vigumu sana kufundisha juu ya sigara katika makanisa mengi marekani.


Nakumbuka kuna mhubiri moja anasema alivyokwenda kuhubiri katika mji mmoja ulioitwa bangnium, alikutana na mzee mmoja wa kanisa la Assemblies of God ambaye alikwishakuwepo hapa mjini,Tanzania ila alikuwepo kule katika chuo kimoja cha biblia cha Assemblies of God ila alipofika akaonana na huyo mzee. Kumbuka Assemblies of God walipokuwa wameanza walikuwa ni moto otelea mbali, kwasababu ule moto uliotokana na Filadefia ndio ambao uliingia mwanzo mwanzo wakati majira haya ya Laodikia yalipokuwa yanaanza, ule moto ulikuwa unazidi kuzimika kuzimika na kuzimika ndipo lilipoibuka Kanisa la ASSEMBLIES OF GOD(AG) kwenye mwaka 1924 ndipo kanisa hili lilikuja kwa moto mkubwa sana na wakaanza kwenda na kupenya sehemu nyingi mbalimbali duniani kufanya kazi za umishenari mpaka likawa limezagaa kwa ghafla


✍Kwahiyo ikaonekana Nyakati hizo moto ulikuwepo katika kanisa hilo AG, ila sasa huyu mzee ndio alikuwa kwenye chuo hicho sasa Yule mhubiri akamuuliza huyu mzee umeona marekani wanafundisha nini?. Sasa ndio huyu mzee akawambia INAHITAJI MSAADA WA MUNGU KWELI KUSOMA HATA KWENYE VYUO HIVI kwasababu kama kweli hujakomaa ukija huku basi tayari utaharibiwa kabisa.


Lakini akaulizwa tena kuhusu maisha ya hawa walimu na jinsi wanavyoishi na wanafundisha nini?. Yule mzee akajibu akasema “ Huku matumizi ya sigara ni kitu cha kawaida, waalimu wanaofundisha kwenye chuo wanavuta sigara akiwa anafundisha” Na ukiuliza kuvuta sigara kuna matatizo gani watakushangaa bali watakujua wewe ni mtu wa mbali yaani mgeni. Na ndivyo kweli ilivyo kule marekani




NYAKATI AMBAZO WATU WANAKATAA KUMUAMINI MUNGU BALI WANAJIAMINI WENYEWE


Marekani hata ulaya yote inatisha sana sana nyakati hizi, Nyakati za Laodikia ni Nyakati ambapo kanisa ni Vuguvugu kuliko unavyoweza kuweza, Duniani kunatisha na Ndani ya kanisa napo kunatisha. Sehemu nyingi ulaya ni sehemu ambazo kama unapita hivi ukiwa ndani ya tax, ukijaribu kumshuhudia labda dereva wa tax, alafu msikilize maneno anayoweza kukujibu.


Kuna siku moja kuna mmhubiri mmoja alikuwa katika mtaa mmoja kule Copenhagen, dernmark anatembea akawa pastor mmoja akamwambia huyu mhubiri aliyetokea Tz, akamwambia huku ilivyo ni kwamba hakuna mtu anayemuamini Mungu, watu wanajiamini wenyewe, kwahiyo ukimueleza mtu “Do you believing Jesus?” atakwambia “ am believing in myself” yaani unamuuliza unamuamini Yesu, yeye anakujibu anakwambia anajiamini mwenyewe kwanini nimuamini mtu mwingine, ninajiamini mwenyewe. Na kweli hata walipopanda kwenye tax alijaribu kumuuliza Dereva tax ikiwa kama anamuamini Yesu ila Yule dereva alimjibu “kwanini nimuamini mtu ambaye ameishi zamani hizo wakati dunia hata haijaendelea, kwanini nimuamini huyo? Najiamini mwenyewe”


Hayo ndio maisha ya watu waliopo Nyakati hizi maana hali inatisha kuliko tunavyoweza kufikiria. Hata sasa hivi huwa nawashangaa sana watu hapa Tanzania wanaopapatika na wazungu wanakuwa wanatoka sijui ulaya au marekani na wakishamuona mzungu wanawaza labda ana kitu cha ajabu sana cha kiroho, na sisi tunajidharau sana na kuwaona wa hawa ndio watu wa rohoni. Wengi wenye ulimbukeni huo hawaijui ulaya ikoje au marekani kukoje, inavyotisha?

Like
1
Αναζήτηση
Κατηγορίες
Διαβάζω περισσότερα
JOB
Verse by verse explanation of Job 8
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 24 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-04-03 03:15:06 0 4χλμ.
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Deuteronomy 3
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 33 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-01-24 19:18:47 0 5χλμ.
1 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 1 Chronicles 24
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 23 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-03-20 05:16:40 0 6χλμ.
MAHUSIANO KIBIBLIA
MWANAMKE NA NGUVU YA USHAWISHI (UBEMBELEZI)
Mwanamke aliumbwa na nguvu ya ushawishi ndani yake kwa kusudi la kuweza kutimiliza jukumu lake...
από GOSPEL PREACHER 2021-11-07 23:52:21 0 7χλμ.
PSALMS
Verse by verse explanation of Psalm 15
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 19 questions at the...
από THE HOLY BIBLE 2022-05-20 11:57:31 0 7χλμ.