MAJIRA YA KANISA LA EFESO

2
6Кб

(1) MLENGWA WA KANISA

{UFUNUO 2:1}
"Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika;.......... ".

- Mlengwa hapa Ni KWA MALAIKA WA KANISA LILILOKO EFESO
- Tunapoangalia juu kipengele hichi tutakuwa tunaangalia mambo kadhaa ambayo yapo ndani ya mlengwa huyu na ya muhimu kuyaelewa tunalikuwa tunaendelea

1) MAELEKEZO KWA KIONGOZI MKUU WA KANISA

Tunaona kwamba Yesu kristo anapozungumza na Kanisa anakuwa anazungumza na MALAIKA WA KANISA ambaye ndiye anawajibika, ndiye anayetoa hesabu juu ya kanisa. Kristo Yesu hazungumzi tu na mtu yeyote katika kanisa lakini mawasiliano yake yapo kwa malaika wa Kanisa

▶Neno MALAIKA -ANGELLOS(KIYUNANI) ANGEL(KIINGEREZA) MJUMBE/MCHUNGAJI WA KANISA(KISWAHILI) {MALAKI 2:7}

Mchungaji au Kiongozi mkuu wa kanisa lililoko mahali fulani ndiye malaika wa Kanisa hilo. Mahali hapa tunajifunza kitu kimoja kwamba Yesu kristo hawasilikani na mtu yeyote katika kanisa kuacha Malaika

Tunapokuta wapo watu wengine wapo ndani ya kanisa lililoko mahali fulani ambao wapo wanajifanya wanajua, wanajifanya kwamba wao wamepokea kutoka kwa Bwana kuhusiana na kanisa na kusema yule kiongozi husika(Mchungaji wa kanisa) haelewi ila mimi Bwana amenifunulia juu ya hili au lile na lile kuhusiana na kanisa hili au anadai ameonyeshwa ndoto au maono, Huyu ujue moja kwa moja ni Mwongo, kama ni chochote ambacho Mungu anataka kuwasiliana na kanisa, Mungu atawasiliana na Malaika

Wakati wote Yesu Kristo akitaka kuleta ufunuo /kalipio au pongezi au chochote kile katika kanisa, wakati wote atayaleta yote hayo kwa MALAIKA WA KANISA la mahali hapo, kwa kiongozi mkuu wa mahali hapo sio mtu yeyote


Kiongozi wa Kanisa au Mchungaji mkuu wa kanisa ndiye ataleta hesabu juu ya kanisa alilopewa kulichunga, ndiye ambaye ni mjumbe wake Bwana


Ndio maana utaweza kuona kwa mfano kwa mfano wakati ule wa Musa katika Sura ya 12 ya HESABU, Tunaona malaika wa Kanisa lililoko Jangwani alikuwa ni Musa ingawa walikuwepo viongozi waliokuwa chini yake lakini Malaika wa kanisa hilo alikuwepo mmoja tu, MUSA. Na ndio utaona hata alipotokea huyu NABII MIRIAM Ambaye alikuwa mmoja wa viongozi alipoanza kusema
{HESABU 12:2}
“Wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao. ”

Lakini utaona mistari ya mbeleni Mungu anajaribu kuwaeleza tofauti kati ya Malaika wake wa Kanisa yaani Musa na Viongozi wengine ndani ya kanisa kwa kusema yafuatayo


{HESABU 12:6-8}
“Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?

Kwahiyo hapa tujifunze Neno moja kuwa maelekezo yoyote Kuhusiana na Kanisa yatakuwa yanatolewa na malaika wa kanisa husika. Na pale kutakapokuwa kuna matatizo yanayojitokeza, kalipio lolote au chochote kile kitalengwa kwa malaika wa kanisa maana ndiye anapaswa kuwaelekeza watu katika njia ambayo tunapaswa kuelekezwa

Ndio maana maandiko yanatuelekeza kwamba tuwasaidie Malaika huyu aweze kufanya kazi hiyo aliyopewa na Mungu pasipo kuugua au mzigo wa kuelemea hasa pale tunapokuwa chini ya Mtumishi anayefundisha kweli yote ya utakatifu na kutuelekeza katika kufanya mapenzi ya Mungu
{WAEBRANIA 13:17}
“Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi. ”

Tusikubali kumsapoti mtu yeyote katikati yetu ndani ya kanisa anayejifanya anajua zaidi wakati wao sio Malaika wa kanisa wala tusimsikilize kwani kwa kutofanya hivyo tunakuwa tunaenda mbali na Mungu na Mungu siku zote hawezi kuwa upande weny bali atakuwa upande wa MALAIKA WAKE (LUKA 13:6-9)

BMAZINGIRA NA MWANZO WA KANISA LA EFESO

EFESO - Efeso ulkuwa ni mji mkubwa nyakati hizi za kanisa la kwanza na mji huu ulikuwa katika Asia ndogo(Uturuki). Ulikuwa ni Mji mkubwa wa kibiashara hivyo kulikuwa na pilikapilika nyingi sana. Lakini la kukumbuka zaidi kuhusu mji huu wa efeso kwamba hapa ndipo kulikuwa na hekalu kubwa la mungu wa Kike aitwaye DIANA au ARTEMI (MATENDO 19:23-41)

Hapa katika Efeso ndio Paulo mtume alifanya kazi kubwa sana hapa na alikaa kwa miaka mingi akilifundisha kanisa ambapo alihubiri na kuvunja vunja ngome nyingi sana hapa kutokana na ushawishi wa mahubiri yake.


Hapa ndipo kulikuwepo na wengi hapo mwanzo na huyu ARTEMI/DIANA Ilikuwa ni ngome kubwa sana ya shetani na kiti cha Enzi cha shetani hapa Efeso ingawa pia kulikuwepo na waganga na wachawi wengi ambao walitumia mambo ya kiganga kwenye kazi zao


Kutokana na Neno alilolihubiri Paulo lilipelekea watu wengi waliona uganga hauna kitu na ngome zote zilizotokana na kiti hichi cha enzi cha efeso zilikuwa zimebomolewa na watu wakachoma mambo yao ya uganga na Neno la Mungu kupitia mtume Paulo likashinda kwa nguvu hapa Efeso hivyo maelfu elfu walimjia Bwana Yesu {MATENDO 19:13-20}

Kila tutakayoyasikia katika mlengwa wa kanisa tutaelewa kanisa lile lilikuwaje, mazingira yalikuwaje na hayo ndiyo yatatupa kuelewa vizuri juu ya ujumbe wa Yesu kuhusu kanisa husika

{MATENDO 19:18-20}
Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu. Ghasia katika Efeso

Hala utaona watu wengi walimgeukia Yesu na kuchoma vitu vyao vya kuganga ambayo thamani yake inatajwa kuwa ni FEDHA 50, 00 kwa mwaka 1952 ambapo fedha yetu Tz ilikuwa karibu sawa na dola
▶ Neno FEDHA linamaana ARGULION lenye thamani sawa na SENTI 64 ZA MAREKANI. Hivyo Fedha 50, 000 zilizokusanywa hapo ni sawa na USD 32, 000 ambayo ni sawa Tsh Millioni 26

Hivyo utaweza kuona ni Fedha kiasi chote hicho karibu mil 26 ndio ilikuwa thamani ya vitu vya kiganga vilivyoletwa kwa wakati mmoja kuchomwa moto, ndipo utaelewa mji huo ulikuwa umefunikwa na giza na mambo ya ushirikina kiasi gani. Lakini baada ya mahubiri ya Paulo mtume ndipo kulipotokea uhamsho mkubwa sana kwenye kanisa la Efeso na ndipo kanisa lilipoanza na wale wote waliokuwa wanachonga sanamu za ARTEMI wakaanza kuonekana hawana kazi na kuwa imekufa maana wale waliokuwa wanunuzi walikuwa wamempokea Yesu

Kwahiyo kanisa hili Baada ya Paulo mtume kuhubiri na watu kuokolewa kwa namna hiyo, alikuwepo hapa kulichunga kanisa hili hivyo walipata neema ya ya kuwa na mafundisho ya ngazi ya juu sana yaliyokuwa yanalifanya kanisa kuwa nuruni sana

Hivyo kanisa lilikuwa na Upendo mwingi sana kwa Yesu walizishika sana amri za Mungu kwa kwa hofu sana. Kumpenda Yesu ni Kuzishika Amri zake

{YOHANA 14:23-24}
"Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka".

C/ MAFUNDISHO NA WAALIMU WA KANISA LA EFESO

Hivyo kanisa hili kutokana na kuanza kwake kwa Mahubiri ya Mtume Paulo lilipelekea waefeso kuwa na mafundisho ya Usafi na utakatifu wa hali ya Juu
▶ WALIFUNDISHWA KUTOKUENENDA KAMA MATAIFA WAENDENDAVYO {WAEFESO 4:17}
Walifundishwa jinsi wanavyotakiwa kuwa tofauti na mataifa katika mwenendo wao katika usemi, matendo na mavazi
▶ KUVAA UTU UPYA KATIKA HAKI NA UTAKATIFU WA KWELI{WAEFESO 4:24
▶KUTOMPA IBILISI NAFASI
▶UTUMISHI WA KUJITOLEA KWA BWANA
▶ KUJILINDA KATIKA VINYWA VYAO NA MATUSI, MANENO MAOVU, YA HASIRA N. K
▶ UASHERATI WALA UCHAFU WOWOTE USITAJWE KABISA KWAO (WAEFESO5:3)
▶ VITA VYA KIROHO KWA MAOMBI, NENO NA IMANI(WAEFESO 6:11-17)

Kwa ujumla Kanisa hili la Efeso lilianza kwa mafundisho ya Usafi na utakatifu wa hali ya juu kwa utumishi, ushuhudiaji, Maombi na kujitoa kwa hiyari zao wakijua wanamtumikia Mungu si Mwanadamu, Walikuwa wanaukomboa wakati, Hakuna uasherati unaotajwa

✍ Hivyo baada ya Paulo kuwa anasafiri kwenda safari za Injili Kukingana na na Historia inaonyesha alikuja Mtumishi wa Mungu APOLO Ambaye aliendeleza yake mafundisho ya mtume Paulo na Baadae tena wakaja wakina TIMOTHEO na MTUME YOHANA

Hivyo utaona Kanisa hili lilipata Neema Kubwa sana ya kuwa na wahubiri na waalimu wa ngazi za juu nyakati zao ambaye ni PAULO MTUME, APOLO, TIMOTHEO na MTUME YOHANA Hivyo ndio lilipelekea kanisa kuwa moto jina la Yesu lilitukuzwa sana Efeso nzima na miji ya kando kando yake. Huu ndio ulikuwa Mwanzo wa kanisa la Efeso

Lakini hali hiyo ya umoto ulianza kupoa hatua kwa hatua kadifi miaka kadhaa ilivyokuwa inazidi kwenda mpaka Upendo wao wa kwansa ukawa umekufa kabisa, haupo tena wale waliokuwa na kitu zamani wakageuka na kuanza kufundisha mafundisho potofu kinyume na kweli waliyojifunza na wengine ndio wale wa kwanza kwanza kabisa waliokuwa katika kanisa la kwanza, lakini wao ndio waliokuwa miongoni mwa walioanza kuwapotosha watu wengine, na mmoja wao ndio huyu NIKOLAO

D/ MAFUNDISHO NA MATENDO YA WANIKOLAI

{UFUNUO 2:6}

"Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia".


Haya tunayoyasoma kwamba ni matendo au mafundisho ya wanikolai ni yapi❓
WANIKOLAI - Ni wale waliofuata mafundisho ya huyu aliyeitwa NIKOLAO ambaye tunaona anatajwa katika MATENDO 6:5 Kwamba alikuwa ni Kiongozi wa mwanzo mwanzo wa kanisa la kwanza waliochaguliwa pamoja na kina Stephano na Filipo kuwa Mashemasi, alijulikana kama NIKOLAO MWONGOFU WA ANTIOKIO

Huyu NIKOLAO aliyekuwa na kitu sana hapo mwanzo, alikuwa amejawa imani na Roho mtakatifu na alikuwa moto sana, lakini miaka ilipopita alikuja kurudi nyuma sana kulingana na historia ya kanisa la kwanza na akaanza kufundisha mafundisho ambayo yapo kinyume kabisa na Neno la Mungu na hata akajaribu kuwavuta baadhi ya watu katika makanisa mengine pia ili wamwelekee yeye na hata wakawepo watu wengiine waliofuata mafundisho yake ndio hawa wanaoitwa WANIKOLAI


Mafundisho aliyokuwa anafundisha NIKOLAO yalikuwa ni mafundisho yaliyo kinyume na Neno kabisa lakini ndiyo tunayaona mpaka leo katika sehemu nyingine yakifundishwa mpaka sasa katika dunia tuliyo nayo

Mafundisho ya NIKOLAO yalikuwa yanatokana na Philosofia za kiyunani zilizokuwa zinafundishwa na watu wanaitwa kibiblia kuwa ni WATU WENYE UJUZI MATENDO 17:18, Sasa philosofia hizo za kiyunani ndio zilikuja kuingizwa ndani ya kanisa la kwanza kupitia Mtu huyu Nikolao ambaye alikuwa tayari amesharudi nyuma

NIKOLAO alifundisha kwamba Mtu anapookolewa, anakuwa amesafishwa kwa damu ya Yesu, Roho yake inaendelelea kuwa safi wakati wote na haihusiani na mwili unafanya nini nje mwili wake au katika mwili wake

NIKOLAO aliweza kusema kuwa kama mtu anakunywa pombe, Kinachokunywa pombe ni mwili tu sio roho (Ni kama mafundisho ya NABII TITO wa Tanzania anavyohubiri juu ya pombe bila hofu ), Pia kama mtu anavuta sigara au kutumia madawa ya kulevywa kinachokula ni mwili tu sio roho kwahiyo roho haidhuriki, Kama mtu anafanya uasherati au uzinzi, Roho yake haifanyi uasherati lakini ni mwili tu ndio unafanya uasherati /uzinzi roho haidhuriki inabaki kuwa safi tu na mtu huyu anaenda mbinguni bila kujali mwilini anafanya nini?

Hivyo alikuwa akifundisha kwamba mtu anaweza kufanya chochote katika mwili lakini roho yake ikaendelea kuwa safi bila matatizo yoyote. Kwa ujumla wake ni kama alikuwa anafundisha Mafundisho MUNGU HAANGALII MAMBO YA MWILINI BALI YA ROHONI


MUNGU HAANGALII MAMBO YA MWILINI BALI YA ROHO

Kimsingi huyu Nikolao alikuwa anafundisha mafundisho ya namna hiyo ambyo kimsingi ni mara nyingi mambo au vitu vya namna hii vinavutia sana watu katika mwili, kwani mtu akijua anaweza kufanya lolote au chochote lakini anaenda mbinguni, kitu hicho au mahubiri hayo yanavutia sana watu hata leo. Hivyo ndivyo nikolao akawa amevuta watu wamemfuata

Lakini kwa kuwa hapa Efeso washirika wengi walikuwa wamefundishwa kwa undani sana juu ya mafundisho mengi ya usafi kama yale ya Uasherati usitajwe kabisa kwao na yake ya kuuvua utu wa kale yaliwasaidia sana kujiepusha na mafundisho ya hawa wanikolai na ndio maana hapa katika UFUNUO 2:6 inaonyesha walikuwa wanayachukia mafundisho ya wananikolao
Kaka zangu na dada zangu lazima tujihadhari na mafundisho ya namna hii ya watu wasemao TUNAWEZA KUFANYA HIKI NA HIKI KATIKA MWILI ILIMRADI TU ROHO YENYEWE IKO SAFI, HAKUNA TATIZO. Mafundisho ya namna hiyo ni mafundisho ya wananikolai ambayo BWANA YESU ANYACHUKIA maana yeye ndiye Aliyesema SAFISHA KWANZA NDANI YA KIKOMBE ILI NJE YAKE IWE SAFI(MATHAYO 23:26) akiwa na maana kwamba Utakatifu ni mwili na Roho kama alivyofundisha Paulo si Roho pekee yake {2WAKORINTO 7:1 }

Hivyo hata leo tukimsikia mtu au Mchungaji yeyote anafundisha kuwa eti Mungu haangalii mambo ya mwili bali ya Roho, Huyo ni Muongo wa kumkimbia haraka anatuletea mafundisho ya wanikolai. Biblia inataja Matendo ya mwili ni dhahihiri katika

{WAGALATIA 5:19-21}
"Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Tunda la Roho"

Hapa tunajifunza kuwa inataja Uasherati, ulevi, Ugomvi kuwa ni matendo ya mwili. Je tuyafanye kwa sababu Mambo ya mwili Mungu hayaangalii❓ Je unavyolewa inalewa Roho au mwili? Je unavyopigana ngumi ni Roho ndiyo inarusha ngumi ❓ Unavyofanya uasherati je ni Roho ndio inafanya uasherati❓. Hivyo mafundisho yoyote ya kwamba eti Mungu haangalii mambo ya mwilini bali ya Rohoni hayo ni mafundisho ya kuzimu na ni Mafundisho ya Nikolao‼

Mafundisho kama haya yatakuwepo hata leo katika makanisa mbalimbali tuliyokuwepo nayo nyakati hizi ambayo watu hawatataka kuambiwa juu ya vitu vya nje ya miili yao wanavyofanya, watavaa wanavyojisikia na hawatapenda kuambiwa juu ya mavazi yao na mambo fulani ya kidunia wanayifanya kwa madai kwamba Mungu haangalii mambo ya mwilini

Sasa hili ndilo kanisa la Efeso ambalo lilianza vizuri lakini ilipokuwa inafika katikakati ya mwaka 32 mpaka 100 kama tutakavyoona baade tutaona ule upendo wa kwanza na moto wa kwanza waliokuwa nao mwanzoni ukaanza kuondoka kwasababu wale wahubiri na waalimu walikuwa hawapo tena, wameshakufa hivyo utakatifu uliokuwapo mwanzoni ukawa haupo tena, utendaji kazi ya Bwana, Ushuhudiaji na ufuatiliaji uliokuwepo ukawa haupo tena, Moto wa Kanisa hili ukaanza kufufia watu wakawa wameuacha upendo wa kwanza. Hili ndio Yesu Kristo alikuwa anazungumza juu ya mlengwa wa kanisa la Efeso

(2) WASIFU WA YESU KRISTO

{UFUNUO 2:1}
"Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu".

Hapa Yesu Kristo anajitambulisha Kwamba amezishika Nyota 7 mkono wa Kuume wake na tena anatembea katikati ya vile vinara 7 vya dhahabu

- YEYE ASHIKAYE NYOTA 7 MKONO WA KUUME

NYOTA 7 Wachungaji au Malaika wa kanisa

Hapa Yesu Kristo anatokea kama Kiongozi mkuu wa kanisa, na kwamba Malaika wa Kanisa 7 wako chini ya maongozi yake. Ndio maana Yesu anaitwa MCHUNGAJI MKUU WA KONDOO {WAEBRANIA 13:20, 1PETRO 5:2-4}

MKONO WA KUUME Inazungumzia Msaidizi wa karibu

Maaanake Kama Mchungaji akiboronga au akikosea basi Kristo Yesu atampa Kalipio kwa malaika au Nyota hizo au Wachungaji wanaofanya kazi kwa niaba yake kama wasaidizi wa karibu nae


Kwahiyo kanisa lililo hai ni pale ambapo maelekezo yote yatatoka kwa Yesu kristo ambaye ni Neno la Mungu kupitia Malaika wake

YEYE AENDAYE KATIKATI YA VINARA 7 VYA DHAHABU

VINARA 7 VYA DHAHABU Ni Makanisa yake 7 ya Asia ndogo


Yesu anayezungumzwa kutembea katikati ya vile vinara 7 vya dhahabu maanake Yesu ndiye alikuwa anatembea katikati ya makanisa yale 7 na Yesu ndiye anaona chochote kile kinachoendelea katika kanisa moja mpaka lingine. Na ikiwa Yesu atatembea katikati ya kanisa fulani lazima watu watafanya mapenzi ya Mungu na kumuona Mungu kwa ajabu. Lakini ukiona kuna makanisa ambayo Yesu hatembei katikati yao ni kwasababu wameruhusu machukizo fulani au hawapo tayari kuongozwa na Neno la Kristo

{2 WAKORINTHO 6:14-18}
“Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema Bwana Mwenyezi. ”

Yesu Kristo hawezi kutembea katikati ya makanisa ambayo yanaruhusu mambo yafuatayo :-
▶ Yanayoruhusu Nuru na giza kuwepo sehemu moja, Mahali ambapo matendo ya giza na dhambi haikemewi‼
▶ Yanayoruhusu urafiki kati ya mambo ya kidunia na mambo ya kanisa
▶ Yanayoruhusu Masanamu ndani ya kanisa na kuyaita ni watakatifu au wanayaheshimu tu‼


Hivyo Kanisa ambalo linampendeza Mungu ni kanisa ambalo wachungaji wote wataelekezwa na Yesu, wanamfuata Yesu kama Kielelezo, wanaongozwa na Neno la Mungu, Wanamruhusu Yesu kutembea katikati ya kanisa, Neno kwao ndio linakuwa Central part( Msingi wa kanisa), wapo tayari kufanya chochote ambacho Neno linasema sio katiba yao inavyosema

Leo tuna makanisa mengi ambayo katiba ndio Central part(Msingi wa kanisa), katiba ni kitu kinachotungwa na wanadamu kina makosa chungu mzima, lakini Biblia ni Neno lisilokuwa na makosa ambalo tumepewa tayari. Hivyo kama Neno hili litakuwa mwongozo kwa kanisa maanake Yesu sasa anakuwa amelishika Katika mkono wake wa kuume.

 

(3) SIFA NJEMA ZA KANISA
{ UFUNUO 2: 2-3, 6}

Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka. Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.
-WENYE KUWAJARIBU WAJIITAO MITUME
-WALIYACHUKIA MATENDO YA WANIKOLAI
-HAWAKUCHULIANA NA WATU WABAYA
-WENYE SUBIRA NA UVUMILIVU KATIKA TABU


Tunaona Yesu anwasifia kuwa waliweza kuwajaribu wao wajiitao mitume na kuwaona ni waongo, mmojawapo ndio yule tuliyemuona anaitwa NIKOLAO ambaye alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kwanza kabisa katika kanisa la kwanza ukiacha wale mitume, ndiye aliyekuwa pamoja na kina Stephano na Filipo. Lakini hatimaye Nikolao alikengeuka na kujiita Mtume na ndivyo ilivyo hata sasa, kwani hakuna jipya chini ya jua kwani yaliyokuwako ndiyo yaliyiko hata sasa
{MHUBIRI 1:9}
"Yaliyokuwako ndiyo yatakayokuwako; na yaliyotendeka ndiyo yatakayotendeka; wala jambo jipya hakuna chini ya jua. "

Vivyo hivyo hata sasa tusishangae kusikia kwamba kuna viongozi fulani ambao ni wa mwanzo mwanzo katika kanisa ambao nao wamekengeuka, hawako kwenye kweli ile ya kwanza, Hili si Ajabu ‼Hili ndio lililotokea kwa Nikolao


Lakini hapa waefeso wanapongezwa kwa jinsi ambavyo waliweza kuwajaribu hao wajiitao mitume na kuwagundua ni waongo Kwani waliweza kuwapima na kuyapima maneno yao na matendo yao kama yanaendana na kweli bila kujali wao waliokuwa ni viongozi wa ngazi gani❓

Vivyo hivyo hata sisi hatupaswi tu kusikiliza maneno ya hawa wanaojiita kuwa walikuwa eti ni viongozi wa mwanzo mwanzo kanisani na wapo karibu na mchungaji na ndio walianzisha kanisa (Wapuuzi hao‼Mwanzilishi wa kanisa ni Yesu sio wao WAEBRANIA 12:2) kwani hata Nikolao alijisifia kuwa yeye alikuwa karibu na mitume lakini waefeso hawakujali hilo waliyapima maneno yake na mafundisho yake wakaona hayaendani na kweli wakamuona ni Mtume wa uongo hivyo wakamtupilia mbali wala hawakuwa tayari kuchukulia na watu wabaya wanaoleta fitina kati kati yetu kinyume na kweli {WARUMI 16:17}

Wakati wote tusichukuliwe na watu wanaojifanya wameokoka kabla yetu, au ni viongozi wa mwanzo mwanzo(Hata shetani ni kiongozi wa mwanzo mwanzo) lakini inatupasa kuwajaribu kwanza tuone Je wanayofanya au wanayozungumza yanaendana na kweli ya Neno la Mungu?❓ Inawezekana kweli alikuwa mzuri pale mwanzo lakini sasa amekwisha kengeuka kama Nikolao. Hatumfuati mtu tu kwasababu eti ni mshirika wa Zamani. Na hii ndio sababu waefeso walisifiwa kuwa hawakuweza kuchuliana na watu wabaya

Vile vile Yesu aliweza kuwasifia watu wa Efeso kwa jinsi walivyokuwa wanapita katika maziyo na magumu tabu na shida nyingi lakini bado hawakuweza Kumuacha yeye kwani walikuwa na Subira na uvumilivu kwa namna ya ajabu


(4) KALIPIO


{UFUNUO 2:4}
"Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza. "


KALIPIO kwa Kanisa hili lilikuwa ni UMEUACHA UPENDO WA KWANZA
▶Moto ule wa kwanza uliokuwepo kwako haupo tena
▶Jinsi ulivyokuwa unafanya kazi ya Bwana kwa bidii na ushuhidiaji na ufuatiliaji, sivyo ulivyo sasa
▶Jinsi ulivyokuwa umesimama kukaa kwenye usafi na utakatifu wote, Sivyo ulivyo sasa
✍ Nimeyaangalia matendo yako nimeona kuna mapungufu kuwa umeuacha Upendo wa kwanza, Sasa hivi umepoa, Wokovu kwako umekuwa ni kama dini tu, unaingia kanisa kwa mazoea tu, Lile neno langu halikufanywi tena kulia kama mwanzo, neno halikufanyi kujuta, upige kelele na kutubu kama mwanzo, hulitendei tena kazi Neno langu kama mwanoz bali unasikiliza kama hadithi tu,  UMEUACHA UPENDO WA KWANZA. Hilo ndio lilikuwa KEMEO AU KALIPIO kwa Kanisa la Efeso

Hivyo hivyo Kalipio hili Yesu Kristo analitoa hata kwetu pale ambapo tunakuwa tumeuacha upendo wa kwanza, tu tunakuwa tumekalipiwa. Mungu anatutaka tuendelee kuthibitika katika upendo wetu wa kwanza bila namna yoyote ya kuyumba bali tutende kazi ya Mungu kama Mwanzo na Kuishi maisha ya Usafi na utakatifu kama mwanzo na kuzidi { WAEBRANIA 3:14}

Hapa napo tunajifunza kitu kingine cha Muhimu tena Kwamba Yesu anaanza kutoa sifa njema za kanisa ndipo anafuata na Kalipio. Vivyo hivyo kama ni viongozi wa kanisa au ni wachungaji hatunabudi kulizingatia hili, Kabla ya kuanza kutoa Makalipip kwa mtu au kanisa hatunabudi kutanguliza kwanza sifa njema ndipo tunaleta makalipio mwishoni


Tunapoinua Mema juu ya mtu alafu tukaleta makalipio juu ya mtu, ni rahisi makalipio hayo kuingia na kupenya na huu ndio utaratibu mzuri unaleta matokeo mazuri

(5) MAELEKEZO KUHUSU JINSI YA KUFANYA

{ UFUNUO 2:5}
"Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu".

KINARA KUONDOLEWA MAHALI PAKE USIPOTUBU Inazumgumzia Kutupwa nje na kuondoa mahali pake, Kukuondoa kwenye ufalme wake, kuondolea uwepo na utukufu wake kwako, Kuondolewa kwa vile vitu vyote ndani yako vilivyokuwa vinakufanya ujione umeokoka na unaenda mbinguni hivyo atakuonyesha jinsi alivyo mbali na wewe kabisa

Kwahiyo hayo ndiyo ambayo Yesu anayasema na kuyamaanisha kwamba USIPOTUBU kuwa Sitajali Mema yote uliyofanya Mwanzo, Sitajali jinsi ukivyokuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya kama nukolao! Kama umeacha upendo wa kwanza basi nitakuwa siwezi kukaa na wewe mbingu wala sitaweza kutembea na wewe tena na kujidhihirisha kwako

Hii hali kuna watu wanaweza wakawa wanajiuliza mbona siku hizi simuoni Mungu kama mwanzo akijidhihirisha kanisani au kwangu binafsi kama mwanzo, Mbona sina furaha ya wokovu kama ile ya mwanzo? Hii ni kwasababu Umeuacha upendo wakwanza hivyo amekiondoa kinara mahali pake, ameondoa utukufu wote uliokuwa nao. Ukiona hali hiyo kwako anguka mbele zake anza kutubu usije ukakataliwa mbele za Mungu na Mema yako yote uliyotenda yasikumbukwe ‼

(6) AHADI

{UFUNUO 2:7}
"Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu".

BUSTANI YA MUNGU - PARADISO Bustani iliyojaa raha. Hata sasa Mbinguni kuna Bustani ya Mungu yenye Mti wa uzima wenye matunda aina 12 (UFUNUO 22:2)

Sasa hapa Yesu anaahidi kwa Yeyote ashindaye na Kutubu kwa kuurudia Upendo wake wa kwanza na kuishi kwa usafi na Utakatifu kuwa sio tu atakuwa kwenye hiyo Bustani ya Mungu ya raha bali ATAKULA MATUNDA YA MTI HUO WA UZIMA. Kumbuka adamu na Hawa walizuiwa kula matunda haya ya mti wa uzima kwasababu alitaka wale watakao kuwa wameshinda ya dunia ndio waje kuyala matunda hayo


Mara nyingi mtu anapookoka pale mwanzoni mwanzoni anakuwa analipenda sana Neno, akisikia Neno tu linamvunja vunja upesi, analichukua neno kama lilivyo na kulifanyia kazi mara moja kwa hofu na kutetemeka lakini kadiri miaka inavyokwenda, wale watu wazamani waliokaa muda mrefu katika wokovu wana nafasi kubwa ya kwenda motoni zaidi kuliko wale watoto wachanga wakilisikia neno wanalitendea kazi mara moja, lakini wale wazamani wanafikia mahali wanalizoe Neno, kile walichokuwa wanakifanya mwanzo wanakiweka pembeni.

(7) UNABII KUHUSIANA NA MAJIRA YA KANISA

Katika Unabii hata haya majina ya makanisa yalikuwa na maana kubwa juu ya yale yatakayotokea kwenye majira ya kanisa hilo. Kwamfano Ebu tuangalie Maana na Neno Efeso katika lugha za asili maana yake

EFESO inamaana KUYAACHA MEMA YAONDOKE /KUPUMZIKA

Sasa kanisa hili katika unabii lilianza kuwa na moto wa ajabu kuanzia mwaka 33 lakini kadiri wale waalimu wa mwanzo walipoanza kuwa wametoweka au kufa, ule moto wa kwanza ukaondoka na kufa kabisa ikafika mahali likawa baridi mwishoni mwaka 100

Katika historia ya kanisa la kwanza inaonyesha, Mtu kama Petro aliuwawa mwaka 68 B. K na kipindi hichi hichi ndicho alichouwawa Paulo mtume, Lakini ipofika mwishoni mwaka mwaka 100, kanisa likaanza kuwa kama dini kabisa, watu wanaenda kanisani lakini ule moto haupo tena, hawaongozwi tena na Neno Kama mwanzo, uwepo wa Mungu ulikuwa umeondoka si yu kwa kanisa la Efeso bali ulimwengu wote wa nyakati hizo

Ina maaan ule moto aliouacha Yesu Kristo na mitume ulikwenda kufifia ukafifia hadi kufikia mwaka 100, ukawa hakuna tena kanisa lolote katika ulimwengu, yote yalikuwayameuacha UPENDO WA KWANZA NA KUYAACHA MAMBO YOTE MEMA YAONDOKE. Hivyo ndivyo unabii ulivyotimizwa katika majira haya ya kanisa la Efeso

Like
Love
2
Поиск
Категории
Больше
DANIEL
DANIELI 9
Jina la Bwana wetu na mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe; Katika sura hii tunaona...
От GOSPEL PREACHER 2021-11-08 01:31:39 0 9Кб
JOSHUA
Verse by verse explanation of Joshua 4
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 32 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-01-25 07:19:15 0 5Кб
2 CHRONICLES
Verse by verse explanation of 2 Chronicles 13
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 30 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-04-02 01:23:16 0 5Кб
FORM 1
BOOK-KEEPING: FORM 1
List of all topics in Book-Keeping for form 1 class: CLICK HERE TO DOWNLOAD. INTRODUCTION TO...
От PROSHABO ONLINE SCHOOLS 2021-10-30 04:47:42 0 5Кб
PSALMS
Verse by verse explanation of Psalm 14
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 19 questions at the...
От THE HOLY BIBLE 2022-05-20 11:56:20 0 7Кб