MAKANISA SABA.

0
5K

Shalom,

Kwa ufupi;

Kwenye kitabu cha Ufunuo sura ya 2 &3,tunasoma kuhusu makanisa yale saba. Kuna mambo mengi na kushangaza kuhusu haya makanisa saba,hata hivyo ninajaribu tu kutafakari kwa ufupi kati ya mengi yanayoweza kupatikanika kwenye haya makanisa. Nilipata neema ya kutembelea kwenye haya makanisa,ambapo kwa sasa hakuna kilichobakia isipokuwa ni magofu. Lakini kanisa la Smirna limeendelezwa,na lipo hai hata sasa. Tukiwa tumepitia mbali,tulioneshwa na tour guide wetu “ tazama,lile ndio kanisa la Smirna…” Makanisa haya yapo katika Asia ndogo (Uturuki)

Hivyo,Lengo mama la ujumbe wa leo ni kupitia kwa haraka katika haya makanisa saba yaliyopo katika kitabu cha ufunuo. Ujumbe wa kila kanisa ni mpana sana,na kwa sababu hiyo ninajaribu kuchungulia tu kimtazamo kuhusu makanisa saba bila kutulia kiundani katika kila kanisa.

Yohana mtume anajitambulisha kuwa ni yeye aliyesikia na kuyaona maono hayo na kuyaandika;” Nami Yohana ndimi niliyeyasikia na kuyaona mambo hayo…. “Ufunuo 22:8 Pia hata mwanzoni mwa kitabu hiki cha ufunuo tunaona akianza kijitambulisha kwamba ni yeye Yohana ndie aliyekuwa katika kisiwa cha Patmo kwa ajili ya Neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu ( Ufunuo 1:9)

Lakini kile alichokiandika hakikutoka kwake Yohana bali kimetoka kwa Bwana Yesu; “ Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi. ” Ufunuo 22:16. Yapo mambo muhimu ambayo yameandikiwa kwa kila kanisa. Mambo hayo huitwa “ujumbe wa ujumla”,ujumbe huo ni;

01.Kwa malaika wa..

“ Kwa malaika wa..” ni ujumbe unaoanza kwa kila kanisa. Neno malaika maana yake ni mjumbe wa Bwana. Hivyo,katika kila kanisa lilikuwa na mjumbe wa Bwana. Mtu ambaye amepewa dhamana ya kulichunga kanisa hilo,aliitwa “malaika”. Kwa leo yule mchungaji kiongozi wa kanisa lako,yeye anapaswa awe malaika na ndiye haswa aliyelengwa. Hivyo makanisa haya saba,yalikuwa na viongozi wa juu wa kuchunga na kuongoza kanisa,waliitwa malaika.

02.Uweza wa Yesu Kristo.

Ikwa kanisa ni mwili wa Kristo,basi Yesu hana budi kuwa jiwe kuu la pembeni,yaani ni Yeye ndiye msingi wa kanisa lake. ( Katika Ufunuo 2:1b,8b,12b,18b,
Ufunuo 3:1b,7b,14b.) Yesu anatambulisha uweza na nguvu pamoja na malmaka aliyonayo juu ya kanisa lake.

03.Maonyo – Makanisa yote yamepewa maonyo makali pasipo kuhurumiwa,kwa sababu maonyo ni moja ya njia ambayo Mungu hutumia kutuweka katika mstari unaostahili. Mahali popote penye neno la Bwana,huwezi kukosa kuyaona “maonyo” kwa sababu kanisa haliwezi kuwa kanisa la Bwana kama litakosa maono (2 Timotheo 3:16)

04.Yeye aliyo na sikio,asikie.-Ujumbe huu ni muhimu sana kwa kila kanisa,kwa kulitaka kanisa lazima liwe jepesi ya kusikia na kutendea kazi kile kinachosikiwa ( Yakobo 1:19). Kanisa lisiposikia kile Bwana atakacho,litaiacha njia ya haki,hivyo kusikia kunahusisha na utendaji.

 

01. Kanisa la Pergamo.

57 Kanisa la Pergamo linavyoonekana kwa sasa.

Neno “Pergamo”  limetokana na neno liitwalo“ mwinuko ‘‘. Kanisa la Pergamo lipo juu ya mlima mlefu ambapo kwa sasa kama mtu atahitaji kwenda huko juu,basi hana budi kutumia ” cable car”– Cable car ni lifti ya umeme mfano wa gari linalosafili upande mmoja wa mlima hadi upande wa pili wa mlima.

  • Historia fupi;

Kumbuka ; Pergamo ulikuwa mji upo ndani ya Asia ndogo. Kanisa la Pergamo lilikuwa takribani kilomita 100 kaskazini mwa Smirna na kilomita 25 kutoka pwani. Umbali huu wa kutoka katika kanisa la Pergamo hadi kanisa la Smirna ni sawa na umbali wa kutoka Dar es salaam hadi Chalinze,kwa wakazi wa Dar. Hivyo utagundua kwamba,kulikuwa na umbali mkubwa sana kati ya kanisa hadi kanisa,
Mji huu ulikuwa ndio makao makuu ya mamlaka ya kirumi. Na ndipo mahali ambapo ibada za Kaisari zilikuwa zikifanyika.Alikadhalika,palikuwa na hekalu la mungu zeu akiabudiwa, (Matendo 14:13)
Ndio maana pale tusomapo barua hii,utakuta biblia ikisema;”Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani;... ” Ufunuo 2:13

Hivyo,ile namna ya kumuabudu mungu mwingine ilikuwa ni chukizo sana kwa Mungu wetu,Yesu alipafananisha mahali hapo na kiti cha enzi cha shetani.
Pergamo ulikuwa maharufu sana kwa kuwa na maktaba kubwa ya vitabu.Kupitia maktaba hii,watu wa Pergamo walianza kujitengenezea vitabu vyao wao wenyewe kwa kuandika katika ngozi za wanyama. Nyenzo hii ya kuandika maandishi katika ngozi ya wanyama wakaliita kwa jina la “perchment” yaani gombo.Kanisa hili,linakadiliwa kudumu ndani ya miaka 225 hivi,yaani kutoka mwaka wa 313 B.K hadi mwaka wa 538 B.K.

  • Nini kifanyike kwa Kanisa la Pergamo?

Baada ya ujumbe mkubwa,Bwana analitaka kanisa litubu kama njia ya kutafuta suluhu/uhusiano na Mungu (Mwanzo 2:16). Kunapo na uovu wa namna yoyote,njia ni moja tu ni kutubu,na ukisoma kwa umakini utagundua kwamba kama hawatatubu basi kuna maangamivu makubwa ambayo watayapata. Ni watu wa ajabu tunaowaona kwenye kanisa hili,kwa maana wanashika sana jina la Bwana lakini bado wameketi kwenye uovu! Toba inastahili ichukue mkondo wake.

02. Kanisa la Sardi ( Ufunuo 3:1-6)

Camera360_2014_10_1_100631_jpg Kanisa la Sardi linavyoonekana kwa sasa.
  • Historia fupi;

Sardi ulikuwa ni mji wa zamani. Sardi ilikuwa karibu kilomita hamsini kusini mwa Thiatira.Hivyo Sardi ukashamiri sana kwa biashara maana hata barabara muhimu tano zilikutana hapo,ambazo zilifanya  kuwepo kwa biashara iliyo hai na kuupa mji umaarufu.Eneo lililozunguka mji lilikuwa na nafasi nzuri ya kufuga kondoo,kwa hiyo Sardi ilikuwa kituo cha biashara ya manyoya na nguo.Inasemekana hapo baadaye miaka ya 333 KK ,mfalme Alexandra mkuu akaja na huku,akakaa hapo.

  • Ujumbe kwa kanisa la Sardi.

Matendo ya Sardi yalionekana kana kwamba ni mema,na ya kuvutia lakini kumbe hakukua na uhai wa kiroho,Bwana alimjua Sardi kwamba alikuwa na jina lililo hai lakini amekufa. Hii ni kuonesha kwamba Sardi hakuwa sawa kiroho. Hata hivyo Bwana anamtaka Sardi awe mtu wa macho,(akeshe) na kutubu ili asije akaangamia.

 

03. Kanisa la Filadelfia.

 

20141001_124638 Nikiwa na baadhi ya watumishi,hapa kwa nyuma inaonekana moja ya nguzo ya kanisa la Filadelfia. Mimi ni wa tatu kutoka kushoto waliosimama.
  • Historia fupi;

Filadelfia unaojulikana kwa jina la “Alasehir” maana ndio jina la mji huu,ulianzishwa na Attalos II ( 159-138 BCE).Filadelfia ukawa ni mmoja wa mji wa Kirumi na utawala wa Byzantine. Filadelfia ilikuwa yapata kilomita arobaini kusini mashariki mwa Sardi katika barabara kuu iliyounganishwa na miji mingine kama Smirna na Pergamo. Umuhimu wa mji huu ulikuwa ni mdogo kuliko miji ile sita.
Asili ya umuhimu wa mji huu ni kuwepo kwa mashamba ya zabibu yaliyostawi katika uwanda wa Volkano.Hivyo basi,watu wa mahali hapa wakajikuta wanamuabudu mungu “dionisio(dionysus)” mungu huyu alikuwa ni mungu wa divai.Watafiti wa mambo ya kale wanasema kuwa neno “Philadelphia ” lilitokana na neno upendo.Filadelfia ilikuwa na ibada nyingi sana,lakini sio kubwa kama ile ya artemi huko efeso.

Palikuwa na desturi ya kuandika jina la raia mashuhuri katika nguzo za mahekalu haya.Hata hivyo,katika barua hii ya Filadelfia,hakukua na maonyo makali sana,ingawa kanisa la Filadelfia linaonekana halikuwa na nguvu sana.Hivi sasa eneo la kanisa hili limebanwa sana,yaani padogo kuliko maeneo ya makanisa yote sita,tena pembeni mita chache mno kuna msikiti.Hakuna kinachoendelea mahali hapa zaidi sana imebakia kumbukumbu.

Watafiti wanasema kuwa,katika karne ya 17,kanisa hili lilikumbwa na tetemeko na likajengwa tena na Tiberius ambaye alipewa jina la pili akaitwa Neo-Caesarea.Katika mwaka wa 1391 mji ukatekwa na waturuki.

  • Ujumbe wa kanisa;

Kanisa lina nguvu kidogo kwa kuwa limetunza Jina la Bwana. Hii ni sifa nzuri kidogo kwa kanisa kuwa na nguvu,lakini changamoto ya nguvu hii ipo kidogo,inaonesha kuna mambo ambayo kanisa lingejitahidi basi nguvu yake ingeongezeka zaidi.Kanisa hili limekabidhiwa jukumu kubwa la kuwaongoza watu wa dunia na wale wa shetanai,hata hivyo wote watainama mbele zake kwa kuwa Bwana amelipenda. Hata hivyo limepewa onyo la kushika sana kile kilichokuwepo kwa kanisa.

 

04. Kanisa la Laodikia ( Ufunuo 3:14-22)

Camera360_2014_10_1_112833_jpg Kanisa la Laodikia.
  • Historia fupi;

Laodikia ilikuwa kama kilomita sabini kusini mashariki mwa Filadelfia.Inasemekana mji uligunduliwa na mfalme Antiochus II Theos(261-246 BCE).Mfalme huyu akauita jina la mji huu Laodoce jina la mke wake.Mji huu ulikuwa ni tajiri.Mji huu ulikuwa maarufu kwa ustawi wake na ulikuwa na shule maarufu ya utabibu.Mahali hapa palisifika na kuwa na manyoya mazuri,lakini pia kulikuwa na dawa ya macho.

  • Ujumbe mfupi;

Matendo ya Laodikia yalikuwa ni ya kushangaza kwa maana alikuwa si baridi wala si moto. Hii ni sawa na kusema Laodikia alikuwa ni vuguvugu. Kitu ambacho kilikuwa kibaya kwa Bwana,maana yeye hachukui vugu vugu bali hutapika. Kwa kuwa Laodikia alikuwa tajiri,utajiri wake ulikuwa ukimwangamiza kwa maana alidhani kuwa tajiri ni kujitoshereza na kumbe ndio kupotea ikiwa utajiri wake hakuunganisha kwa Bwana. Hata hivyo bado neema ya Bwana i juu yake,maana Bwana anabisha mlangoni,anapaswa kumfungulia ili atengeneze upya na Bwana.

 

05. Kanisa la Efeso ( Ufunuo 2:1-7)

Camera360_2014_10_2_031134_jpg Efeso hiyo.
  • Historia fupi;

Efeso ulikuwa ni mji mkubwa na tajiri sana katika ulimwengu wa zamani . Kulikuwa na bandari juu ya Asia ndogo,hivyo Efeso ulikuwa ni makao ya biashara na usafiri.Hapa ndipo palipokuwa na hekalu kubwa la Artemi pia Artemi alijulikana kama Diana. Artemi alikuwa mungu wa uzazi,hivyo aliabudiwa sana. Mji ukawa maarufu hata kwa biashara,(Matendo 19:23-24) & Matendo 19:34. Pana eneo la michozo la kizamani. Palikuwa na miungu mingi iliyokuwa ikiabudiwa.mfano palikuwa na mungu wa uzazi Diana au Artemi. mungu huyu alikuwa na matiti mengi. Paulo alifika mahali hapa na kuhudumu takribani muda wa miaka miwili.

  • Ujumbe kwa ufupi;

Efeso alikuwa na uwezo wa kuzichunguza roho za watumishi wanaojiita mitume,hata kuwatambua vyema. Na kwa sababu hiyo,hakuweza kuchukuliana nao. Efeso alikuwa na subira,Lakini hata hivyo kuna mahali Efeso alijisahau na kuanguka,Bwana anamkumbusha ajihoji ni wapi alipoanguka akatubu mapema. Kulikuwa na mambo mema ya kwanza,na hayo Efeso hana budi kuyarudia kuyafanya la sivyo,Bwana atamwondolea sifa zake zote.

06. Kanisa la Smirna (Ufunuo 2:8-11)

  • Historia fupi;

Hili ndilo kanisa la pekee lililobaki hai mpaka leo. Smirna sasa ni Izmir,ulikuwa ni kilomita hamsini kaskazini mwa Efeso.Lakini pia Smirna ulijulikana kwa ibada za kipagani,ingawa barua ya kanisa hili imewaja na faraja.
Hivi sasa,watu waendao kujifunza habari za mkanisa,hupitia kufanya ibada mahali hapa.

  • Ujumbe mfupi;

Bwana anamtia moyo Smirna kwa mambo yatakayompata kwa maana hana budi kuyapata. Lakini hayo yote yatakapotukia Smirna anapaswa awe mwaminifu hata kufa. Kwa sababu kuna taji ya uzima kutoka kwa Bwana atakayoipata. Ujumbe huu unaonesha hali ya mateso ambayo Smirna hana budi kupitia,kama ilivyo kwako ambapo huna budi kupitia lakini usiogope,wewe uwe mwaminifu tu hata kufa.

07. Kanisa la Thiatira.

Ilikuwa mji wa kibiashara kwa miaka ya zamani. Biashara hasa ya rangi ya zambarau.

Ujumbe mfupi;

Kanisa lilimkumbatia Yezebeli,mwanamke ambaye alikuwa akijiita ni nabii lakini nabii mwenye kuwapoteza watumishi wa Bwana. Hii ni hatari kama nini,kanisa limemshikilia na kumpenda Yezebeli mwenye kuua watumishi wa Bwana. Hata hivyo kwa pendo la Bwana amempa Yezebeli muda ili atubu,lakini asipotubu Bwana atawaangamiza wote pamoja na wale wanzinzi wenzake. Ukiangalia kwa ukaribu ujumbe huu unalihusu sana kanisa la leo,kwa sababu wakina Yezebeli wapo wengi makanisani ambao kazi yao ni kuangusha watumishi wamwache Bwana na wageukie uzinzi.

Căutare
Categorii
Citeste mai mult
SPIRITUAL EDUCATION
INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA* .
INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA* .
By Martin Laizer 2023-10-17 20:10:29 7 6K
Injili Ya Yesu Kristo
HAZINA ILIYOSITIRIKA NA MFANYABIASHARA
Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Mkuu Zachary Kakobe      ...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-12 01:43:14 0 5K
JONAH
YONA 1
Yona alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli wakati wa utawala wa Yeroboamu Mfalme wa Israeli,...
By GOSPEL PREACHER 2022-01-20 03:02:57 0 8K
DEUTERONOMY
Verse by verse explanation of Deuteronomy 32
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 62 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-01-25 07:05:04 0 5K
2 SAMUEL
Verse by verse explanation of 2 Samuel 22
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 27 questions at the...
By THE HOLY BIBLE 2022-02-05 10:08:34 0 5K