UNATAKA KUOLEWA NA MTU SAHIHI??

Leo napenda nizungumze na akina dada ambao bado hawajaolewa na wanataka kuolewa.
Mtu sahihi kwako ni mwanaume wa namna gani? Kwanza kabisa ni mwanaume uliyekusudiwa na Mungu awe mume wako, pili ni mwanaume anayekupenda vile ulivyo na kwa sababu hiyo yuko tayari kuwa mume wako na kukuchukulia wewe kama mkewe na kuishi nawe kama mkewe katika hali zote akikupa nafasi ya kwanza kabisa kwa upande wa wanadamu. Na tatu, mwenye tabia njema kwa watu wote bila kujali hali zao, anawajua au hawajui. Na Nne, ni yule unayempenda lakini awe wa aina na asili yako (aliyeokoka kama wewe kama tu umeokoka kweli).
Kwa hiyo, kama unataka kuolewa na mtu sahihi, lazima na wewe msichana uwe mtu sahihi. Huwezi kutaka mtu sahihi wakati wewe mwenyewe sio mtu sahihi. Unataka upate mtu anayekufaa, basi anza wewe kwa kuwafaa watu wengine.
Sasas nataka tujifunze somo hili kupitia kisa cha Ruthu wa kwenye Biblia kwa kuangalia maisha yake ya mahusiano na ndugu zake, jamaa zake, na jamii yote kwa ujumla na mtu aliyemuoa. Ni vyema kujua kuwa, KUNA MAISHA KABLA YA KUOLEWA YANAYOPELEKEA MAISHA YA NDOA SIKU CHACHE KABLA YA KUOLEWA NA BAADA YA KUOLEWA.
Kama unataka kuolewa na mtu sahihi:
Jambo la Kwanza: KUWA NA SUBIRA
Wahenga walisema subira yavuta heri. Ruth baada ya kufiwa na mumewe hakukimbilia kutafuta mume, alisubiri mpaka wakati ulipofika. Si kwamba alikuwa haitaji, alihitaji sana kuolewa, lakini hakutaka kuolewa na yeyote, alitaka kuolewa na mtu sahihi, na kwa sababu hiyo ilimpasa asubiri mpaka mtu huyo atakapopatikana.
Ruthu hakusubiri kuolewa na mwanaume akiwa nyumbani kwa mwanaume anayetaka kumwoa, alisubiri kuolewa akiwa nyumbani kwa mlezi wake ambaye alikuwa mkwe wake. Ijapokuwa huyu mlezi wake alimsisitiza sana aende kutafuta wa kuolewa naye, laini yeye pia alisisitiza kusubiri akiwa nyumbani na si nje ya nyumbani.
Tatizo la wadada wengi hata makanisani hawana subira, kila wanapotambua kuwa wanahitaji kuolewa, macho yao huwa juu juu na mioyo yao hutapatapa huku na huko na humo wakitafuta ni akina nani wanaweza kuwaoa, wakishaona wanaanza kuweka mitego yao ili wawanase. Mwanaume uliyemnasa kwa mtego wako ni ndege asiyefugika, atakapoona mtego mwingine wenye nyama nono kuliko yako au mchele mtamu kuliko wako, atachoropoka na kwenda huko.
Usifanye haraka kwa kumtega bali mvute kwa subira yako. Subira yavuta heri, na Biblia inasema, "Twawahita heri wao waliosubiri" (Yakobo 5:11). Unataka kuvuta heri? Basi wewe subiri, usiwe na papara, usipaparuke, tulia katika kusubiri.
Ruthu alisubiri, na subira yake ilimvuta Boazi. Subira yako itamvuta Boazi wako kwa kukupeleka wewe katika majira sahihi na mahali sahihi ili ukutane na mtu sahihi. Subira ya Ruthu ilimfikisha katika majira sahihi ya kuolewa kwake, na kisha ikampeleka mahali sahihi ambapo alikutana na mtu sahihi atakayemuoa.
Jambo la Pili: MTAMBUE NAOMI WAKO KISHA UAMBATANE NAYE.
Naomi ni mtu aliyefungamanishwa na hatima yako katika eneo fulani. Kwa upande wa Ruthu, naomi alikuwa ni mtu aliyefungamanishwa na hatima ya Ruthu katika upande wa kuolewa.
Mungu hutumia watu kuwabariki watu, na pia hutumia watu kuwakutanisha watu na watu wengine waliobeba hatima zao. Ni muhimu sana ukamwomba Mungu akukutanishe na watu au mtu aliyeunganishwa na hatima yako. Hukutani na watu kwa bahati mbaya, unakutana na watu kwa makusudi, ni muhimu hili ukalijua vyema.
Ruthu alikusudiwa kuwa mmoja wa wanawake ambao Yesu atapitia katika uzao wao, lakini haikuwa rahisi kabisa kwa sababu hakuwa mwisraeli. Lakini Mungu alikusudia kwamba kupitia Naomi afikie kusudi hilo la yeye kuwa moja ya wazazi wa Yesu. Aliolewa na mtoto wa naomi, lakini muda mfupi baada ya kuolewa mumewe alikufa. Kwa sababu alitambua kuwa Naomi amefungamanishwa na hatima yake aliambatana naye mpaka alipoungamanishwa na hatima yake.
Usifanye urafiki na kila mtu, fanya urafiki na watu walioungamanishwa na hatima yako ambao watatumiwa na Mungu kama daraja la kukufikisha wewe kwa yule ambaye Mungu amekusudia.
Kama Mungu huwa anatumia watu kuwabariki watu, na pia shetani hutumia watu kuwalaani watu. Na kama Mungu hutumia watu kuwakutanisha watu na watu waliofungamanishwa na hatima zao, na shetani pia hutumia watu kuwakutanisha watu na watu watakaoharibu hatima zao.
Unapoanzisha urafiki na mtu, ni vyema ukawa na uhakika wa kwamba ana mlengo chanya na hatima yako, ni mjenzi na si muharibifu. Ukiwa na urafiki na watu wabaya wasio sahihi utaishia kuolewa na mtu mbaya asiye sahihi atakayekuharibia maisha yako na kusudi la Mungu maishani mwako.
Jambo la Tatu: FANYA KAZI, ACHA UVIVU.
(Soma Ruthu 2:2 - 7)
Usipojitoa kwa ajili ya watu hakuna atakayejitoa kwa ajili yako. Wewe kama binti unayehitaji kuolewa, ni lazima uinuke na kuanza kufanya kazi, na watu watakapoiona kazi yako, watasema kuhusu habari zako. Biblia inasema, Katika kila kazi mna faida, na moja ya faida ya kazi unayoifanya ni kukukutanisha na watu wengi, miongoni mwao ni watu waliofungamanishwa na hatima yako.
Mdada, usikae tu bila kazi, Ruthu alikutana na Boazi akiwa kazini na si akiwa amelala, au amekaa anachati WhatsApp, au Facebook au amekaa anaangalia luninga. Kazi yoyote halali isiyokuwa dhambi kwa Mungu itakukutanisha na watu sahihi, na inawezakuwa kati ya watu hao yumo na Boazi wako akikupimia tu jinsi unavyofanya kazi.
Pamoja na Boazi kusikia habari za Ruthu, lakini pia aliona bidii aliyonayo katika kazi ile aliyokuwa anafanya. Bidii yako katika kazi itakupa upendeleo mbele ya mume wako mtarajiwa bila hata ya wewe kujua.
Usidharau kazi hata kama ni ya kuokota machupa, kwa sababu kazi ina faida zaidi ya mapato unayopata, faida kubwa ni kukukutanisha na watu wengi na miongoni mwa watu hao wamo waliofungamanishwa na hatima yako. Kwa hiyo jicho lako lisiishie katika pesa unayopata, na wala usiogope au kuona aibu kufanya kazi zinazodharaulika na watu, ili mladi tu kazi ile inakupa fursa ya kukutana na watu, hiyo ni faida kubwa sana na ni fahari kubwa sana, nenda kafanye. Wapumbavu watakudharau lakini wenye hekima watakuheshimu katika kazi hiyo unayoifanya.
Unajua kazi aliyokuwa anafanya Ruthu? Ilikuwa ni kuokota mabaki ya nafaka iliyokuwa ikibaki baada ya wavunaji kuvuna. Kazi hii ilikuwa ni ya kuzunguka mashambani na kuomba uokote. Kupitia kazi hii Ruthu alipata zaidi ya nafaka aliyokuwa anaihitaji, alimpata mume wa hatima yake. Sasa wewe dharau kazi, eti kwa sababu hujapata kazi basi hufanyi kazi, kazi yako ni kulala, kuangalia tamthilia, kuchati na kuperuzi mtandaoni kwa mambo ya kijinga jinga tu, UTAZEEKEA NYUMBANI kama sio kutapeliwa kimapenzi.
Usiangalie hadhi ya kazi, angalia fursa inayopatikana kupitia kazi hiyo, na pia angalia faida inayokupatia kazi hiyo. Katika kufanya kazi hatutafuti hadhi na heshima, tunatafuta faida na pengine fursa tunazoweza kutengeneza kupitia kazi hizo. Faida katika kazi ndiyo imebeba hadhi yako na heshima yako ya kesho machoni pa watu. Kwa hiyo usichague kazi, na usiache kufanya kazi eti kwa sababu umekosa kazi uitakayo.
Jambo la Nne: THAMINI (APPRICIATE) KILE UNACHOFANYIWA HATA KAMA NI KIDOGO:
(Soma Ruthu 2:8 - 10)
Tatizo la wadada wengi, eti kwa sababu wao ni wanawake na wanaonekana kuwa ni warembo, huwa hawaonyeshi kuthamini na kufurahia kwa shukrani kile wanachofanyiwa na wakaka au wanaume. Unajua ni kwa nini? Ni kwa sababu huwa wanaona ni halali yao na wanastahili kufanyiwa hivyo eti kwa sababu wao ni wanawake.
Hakuna unachostahili usichopaswa kukithamini na kuwathamini hao waliokufanyia eti kwa sababu wewe ni mwanamke. Ukifanyiwa jambo onyesha kuthamini na kufurahia kwa maneno, kwa hisia na hata kwa matendo na mwonekano wako, usichukulie kirahisi tu. Haustahili chochote bila kustahilishwa kwa neema na upendeleo, na kama ni hivyo, basi onyesha kuthamini na kufurahia.
Ukisoma Ruthu 2:10 – 13, utamwona Ruthu jinsi alivyoonyesha kuthamini kile alichofanyiwa na Boazi, hakuchukulia kirahisi tu. Tatizo lenu wadada mnapoingia katika mahusiano ya awali na wakaka mnachukulia kirahisi mambo wanayowafanyia na wakati mwingine mnaonyesha lazima ya kutaka kufanyiwa hivyo.
Kaka wa watu ndio tu kaanza kuwa karibu na wewe, basi ishakuwa taabu, kila siku unampa orodha ya mambo ambayo unataka akufanyie na unaonyesha kabisa asipokufanyia utaudhika, na mbaya zaidi hata kama atakufanyia bado huonyeshi kuthamini kile amakufanyia na hasa akifanya chini ya kiwango ulichokitaka wewe ndio kabisaa kama ni chakula utakimwaga chini na kuanza kuropoka vijimaneno. Kwa namna hiyo unategemea kuolewa kweli?
Unataka kuolewa, basi jifunze kuthamini hata vile vidogo vidogo unavyofanyiwa na watu. Ruthu alipothamini kile kidogo alichokuwa akipewa, Boazi alimwongezea zaidi, kutoka katika kile alichokuwa akikiokota mpaka kupewa kile kilichokuwa kimevunwa tayari. Tatizo lenu wadada wetu mnajifanya mnastahili sana kutendewa na wakati huo huo hamuonyeshi kuthamini (appreciate) yale mnayofanyiwa. KAMA SI KUZEEKEA NYUMBANI, BASI UTAFIA NYUMBANI AU MTAANI UKITANGATANGA MARA KWA HUYU MARA KWA YULE.
Ukijua umependelewa kufanyiwa kile ulichofanyiwa utaonyesha kuthamini pamoja na kushukuru. Ukijua kwamba, hustahili chochote ila ni kwa neema na kibali, basi utaonyesha kuthamini hata kile kidogo kisichokidhi uhitaji wako ili mradi tu umepewa. Mdada, ebu kuwa mtu wa kuthamini kila jambo unalotendewa liwe dogo au liwe kubwa, uwe umelilipia au umepewa bure, onyesha kuthamini tu.
Jambo la Tano: KUWA MNYENYEKEVU USIYE NA CHOYO WALA UBINAFSI:
(Soma Ruthu 2:1 - 13)
Sifa moja kubwa ya mtu mnyenyekevu ni yule anayewatanguliza wenzake mbele katika mema yote, na anayekubali kushughulishwa na mambo manyonge. Hawi juu ya wengine akitaka kila mtu awe chini yake.
Wadada wengi wanatabia ya kuwashusha wengine, lakini pia kuwaweka nyuma wengine kwa mambo yote mema, na kuwaweka wengine mbele kwa mambo yote mabaya. Hiki ni kiburi kibaya sana chenye choyo na ubinafsi ndani yake.
Wadada wengi wana kiburi cha kuwadharau wasiokuwa nacho na kuwapapatikie wenye navyo. Mkaka anayeonekana kachoka atadharauliwa na akina dada, na yule anayeonekana kapendeza kimwonekano na mfukoni, wadada watamgombania. Ukiona wadada wanampaparukia kijana mtanashati mwenye nacho jua kabisa wanamdharau kijana yeyote asiyenacho, na tabia hiyo ni dalili ya kiburi kilichomo ndani yao.
Ruthu alianza kwanza kwa kuwaheshimu na kuwanyeyekea watumishi wa Boazi waliokuwa wanafanya kazi shambani, kwa sababu alijua kabisa Mungu anatumia watu na huwainua kutoka mavumbini na kuwaketisha na wakuu. Na alijua kuwa, kila aliye juu alianzia chini na kama alianzia chini anaweza kurudi tena chini, lakini aliye chini anaweza kwenda juu na si chini, kwa sababu hiyo aliwaheshimu wote na kuwanyenyekea.
Ukijua kuwa, hakuna aliye juu ambaye hakutoka chini utajifunza kuwanyenyekea na kuwaheshimu watu wote bila kujali hali zao maadamu tu wako hai na wana siku za kuishi na akili za kufanya kazi.
Alama kubwa ya unyenyekevu ni heshima na adabu unayowatendea na kuwaonyesha watu. Boazi alikuwa pembeni akimwangalia Ruthu ili athibitishe kile alichokisikia kwa watu kumuhusu. Alimwona namna anavyowasikiliza na kuwaheshimu watumishi waliokuwa wakivuna, akajiridhisha na kusema kuwa ni mtu mzuri. Mwisho wao nadhani unaufahamu. Na hata Boazi alipokuja na kumsifia bado Ruthu alianguka china na kusujudu miguuni mwa Boazi. Ungelikuwa wewe ndiye uliyesifiwa, nadhani ungeanza kujibebisha na kumtega Boazi kwa miondoka na mikao ya kimadaha, na tena ungeanza kug’ang’ania hata kula naye kabla ya kuambiwa, na wale watumishi (ambao walikuwa ni wadada kama Ruthu) wangeipata kweli kweli, lakini haikuwa kwa mdada mnyenyekevu Ruthu.
Jambo la Sita: WATENDEE MEMA UNAOISHI NAO
(Soma Ruthu 2:4 - 11)
Kuishi na watu vizuri ni matokeo ya tabia njema na mwenendo mzuri anaokuwa nao mtu mbele za watu hao. Mwenye tabia mbaya hajui kuishi na watu na hawezi kuwatendea mema watu, na kila jema watakalomtendea wao yeye ataliona baya tu kwa sababu yeye mwenyewe ni mtenda mabaya.
Ruthu alimtendea mema Naomi, alijishughulisha kwa ajili yake, alihakikisha Naomi anapata chakula, anajisikia vizuri kwa kumtimizia mahitaji yake yote yaliyokuwa chini ya uwezo wake. Tabia yake mbele za Naomi na majirani wao wote ilikuwa ni njema na kwa sababu hiyo ikamtengenezea nafasi katika mioyo ya watu.
Kabla Ruthu hajafika kwa Boazi, tabia yake na mwenendo wake aliouonyesha kwa Naomi ulikuwa umekwishafika kwa Boazi siku nyingi sana kabla Boazi hajamtia machoni Ruthu. Kabla hujajulikana na watu kwa suru hasa watu walio mbali na wewe, hujulikana kwao kwa tabia yako. Kabla hujafika machoni pake au pao, tabia yako imekwisha kukutangulia na kuwafikia. Wakati wewe unatokea machoni mwao wao wanapokuona wanaanza kukufikiria na kukuzungumzia kwa tabia yako na si kwa sura yako na umbo lako.
Boazi alipomwona Ruthu hakumsifia kwa sura yake bali alimsifia kwa tabia yake, akasema, “Naye Boazi akajibu akamwambia, Nimeelezwa SANA yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo, na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo.” Hizo ni sifa za Boazi kwa Ruthu (Ruthu 2:11).
Boazi anasema kuwa AMEELEZWA SANA JINSI RUTHU ALIVYOMFANYIA MKWEWE NAOMI. Hii inamaana sifa zako ambazo ni tabia yako hukutangulia, na hii inaonekana kwa watu wale unaoishi nao na wanaokuzunguka.
Halafu mambo haya aliyoyafanya Ruthu kwa Naomi ni yale ya kuanzia pale mume wa Ruthu alivyokufa. Hii maana yake nini? Naomi hakuwa na sababu ya kumfanyia Naomi jambo lolote jema kwa kuacha mama na baba yake na nchi yake aliyozaliwa kwa maana sababu iliyokuwa inamfanya afanye hivyo haikuwepo ilikuwa imekwisha kufa. Kwa lugha rahisi, matendo ya Ruthu yalipata nguvu sana kwa sababu hayakuwa na masrahi binafsi ndani yake, bali ni tabia yake na upendo wake. Hiki ni kitu adimu sana kwa wadada wengi, ukiona wanakufuata fuata jua kuna masrahi wanatafuta, lakini sio kwa Ruthu.
Kuwa na tabia njema pasipokuwa na masrahi binafsi unayoyatafuta kunakuweka katika nafsi nzuri ya kuishi na watu kwa muda mrefu katika nyakati zote za raha na shida, taabu na huzuni, amani na furaha bila kubadilika kitabia. Lakini ukifanya mema kwa sababu ya kutafuta masrahi, mara zote utakuwa katika nafasi ya kupoteza kama sio kuangukia pabaya.
Jambo la Saba: KUWA MTII KWA WAKUBWA ZAKO KATIKA YALE WANAYOKUELEKEZA.
(Soma Ruthu 3:1 - 5)
Tatizo tulilonalo katika nyakati hizi, wadada wengi ni wajuaji kuliko wazee wao; wanajua kuliko kile wanachojua wazee wao, na hii sio kweli kwa sababu wao wanajua zaidi njia ya kupotea kana kwamba ni njia ya kufanikiwa na hapo ndipo mtazamo wao na wazee unapoanza kupishana.
Wazee ni watu waliokutangulia, pale wewe ulipo wao walishavuka zamani, wanapaona pale ulipo na wakati huo huo wanapaona pale unapokwenda ambapo wao wapo mbele yake zaidi, kwa hiyo wanajua kwa uzoefu pale ulipo na unapoelekea kuwaelekea wao walipo. Kwa hiyo, kujifanya unajua kuliko wao ni upumbavu na umasikini wa fikra.
Ruthu alitii maelekezo na mafundisho ya Naomi, hakukataa hata pale alipoona haelewi vizuri, na hii ndiyo siri ya kufanikiwa kwake. Alisikia sauti ya mzee aliyemtangulia kisha akaifuata ile sauti, na mwisho wa ile sauti alikutana na mafanikio yake. Tatizo lako wewe mdada unaikataa sauti ya wazee, na unawaficha mambo yako, ndio maana unagonga mwamba na unaona giza mbele yako.
Kuwaona waliokutangulia kana kwamba wamepitwa na wakati ili hali bado wanaishi nyakati hizo hizo unazoishi wewe na walitangulia kuishi kabla yako ni kiburi. Na Biblia inasema, Kabla ya anguko hutangulia kiburi. Sasa wewe jifanye kuwa unajua kuliko Naomi wako, itakula kwako kisha uanze kulialia. Wahenga walisema, Asiyesikia la Mkuu huvunjika guu, na Biblia inasema, Aonywaye mara nyingi akushupaza shingo yake itavunjika na wala hata pata dawa; na siku zote majuto ni mjukuu wa kutokutii kwako maelekezo na mafundisho. Usipotii sasa kesho utakuwa unajuta.
Mtii Naomi wako kwa sababu anajua njia ya kufanikiwa kwako. Upofu wako katika ufahamu wako ndio unaokufanya uone kana kwamba amepitwa na wakati na ajui mambo ya kisasa. Usipomtii Naomi wako katika wakati wako, wakati wako utakuangusha kwa sababu ya kutokujua kwako na kiburi chako, na wakati wako ukipita watakuacha nyumbani au mitaani ukirandaranda.
Naomi wako ananafasi ya kumtambua Boazi wako kama ni Boazi kweli kweli, na anazo mbinu za kukupa ili Boazi asikupite. Sasa wewe jifanye mjuaji, hata kama unamjua huyo Boazi wako bado huna mbinu za kumfanya asikupite, sana sana mbinu zako zitampeperusha. Jishikamanishe na Naomi wako ili akupe mkanda kamili wa kumnasa Boazi wako.
Naomi wako anaweza kuwa ni mchungaji wako, mzazi wako, mlezi wako, au moja ya wazee wa kanisa kanisani kwako nk. Lakini ni yule aliyekutangulia lakini anayemcha Mungu. Kichwa chenye mvi kisichomcha Mungu hakina hekima ya kukusaidia.
Mungu akubariki sana.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS