USIKUBALI USHAWISHI WA DAKIKA 1 WA SHETANI

BWANA ASIFIWE, unaweza kupakua (download) somo hili kwa kubonyeza hapa. Au unaweza ukaendelea kulisoma hapahapa. Sasa tuanze somo letu rasmi.
Luka 4:5-6 " 5 Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu KWA DAKIKA MOJA. 6 Ibilisi akamwambia, Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo".
Hilo ni moja ya jaribu shetani alilomletea Bwana kule jangwani..
Lakini jiulize ni kwa nini iwe kwa dakika moja?, kwanini amwonyeshe ndani ya muda mfupi kiasi hicho, kwani alikuwa na haraka gani? Chukulia mfano mtu aje na kukwambia nataka kukuonyesha plani ya mji wetu na shughuli zote zinazofanyika ndani yake kwenye CD.. Ni wazi kuwa hawezi kumaliza kukuonyesha kila kitu kwa dakika moja, itachukua dakika nyingi sana kama sio masaa, lakini tunaona hapa kwa ibilisi iliwezekana..
Alifanikiwa kumuonyesha Bwana milki zote za ulimwenguni kwa kitendo cha dakika moja.. Ni kwanini afanye hivyo? Sio kwamba alikuwa hawezi kumwonyesha milki zote kidogo kidogo, huo uwezo alikuwa nao lakini sikuzote ni desturi yake, kutompa nafasi mtu ya kutafakari vizuri kazi zake..
Hakutaka Bwana atafakari nyuma ya milki zile kuna nini? Bali alikuwa anamwonyesha haraka haraka, ule upande mzuri tu wa fahari hizo, ili kusudi kwamba Bwana achukue maamuzi ya haraka haraka ya kumsujudia bila hata kutafakari vema, ili awe amemshinda. Hakumwonyesha Bwana wagonjwa waliolala hoi mahospitalini waliokuwa wanahitaji msaada, hakumwonyesha watu waliofungwa kwa kuonewa, au wanaotumikishwa na nguvu za giza, hakumwonyesha maskini wa roho, wala mayatima ambao wazazi wao waliuawa na huyo huyo shetani, hakumwonyesha uchawi uliokithiri katika hiyo miji n.k .. yeye alimwonyesha tu mali, na fahari.. Lakini hakumweza Bwana kwasababu pale alikutana na Mkuu wa Uzima mwenyewe ambaye anajua vyema kuzipambanua roho!.
Hii ni mbinu ambayo shetani anaitumia hata sasa kuwaangusha wengi katika dhambi.. kwamfano akitaka leo kummaliza mtu na dhambi ya uasherati, mara moja atamletea katika mawazo yake uzuri wa kufanya lile jambo.. Lakini hatamruhusu kutafakari ni nini kipo nyuma yake, na yeye bila kutafakari vyema, moja kwa moja ataingia humo, kuitenda, hajui kuwa nyuma yake kuna hata hatari hata ya kifo hata kupata ukimwi, nyuma yake kuna mimba zisizotarajiwa, nyuma yake kuna kupata aibu, na kibaya Zaidi kuliko vyote ni kuwa nyuma yake kuna laana itokayo kwa Mungu..
Au mwingine shetani anamletea mawazo ya kuwa Tajiri kwa dakika moja, atamwambia njoo utapata utajiri wa haraka, bila kufikiri vema kuwa akienda kule, atakutana na waganga wa kienyeji waliolaaniwa, hajui kuwa nyuma yake kuna kutoa kafara, kuna uchawi, kuna kutumikishwa, na mwisho wake ni kifo, na baada ya hapo ni ziwa la moto.. au anakutana na kazi ya wizi au utapeli, pasipo kutafakari nyuma yake kuna kifo, au kifungo, mtu anaingia huko..... Sasa yeye kwasababu kaonyeshwa pesa tu za haraka haraka ambazo hazihitaji kuzihangaikia sana, anaingia humo na kupotelea humo..
Mwingine, anakutana tu na kazi Fulani ya ghafla, halafu baada ya hapo anashurutishwa akaifanye, lakini yeye badala achukue muda kumwomba Mungu na kuichunguza kazi ile, moja kwa moja atakwenda kuingia nayo mkataba na kuifanya kisa tu imemuahidia mshahara mzuri, hajui kuwa kazi ile ililetwa na shetani, ili kuharibu utaratibu wake aliokuwa nao wa kusali, wa kumtumikia Mungu, na kibaya Zaidi anakuja kugundua kazi yenyewe inafanya shughuli za kipepo kama uuzaji pombe, au bidhaa haramu na mambo mengine ya ajabu.
Mwingine atakuwa anatembea madukani, ghafla anakutana na simu ya mtu imejiegesha mahali ambapo haionekana, na saa hiyo hiyo shetani anaanza kumletea mawazo ya dakika moja ya wizi, kumwonyesha faida za simu ile akienda kuuza atapata laki kadhaa, ndani ya dakika chache baadaye.. kisha atanunua hiki na kile.. Na yeye bila kuruhusu fikra zake kuwaza mbali anakwenda kuiiba, bila kujua nyuma yake, kuna kupigwa na watu, kuna kuchomwa moto, kuna kufungwa, na kibaya Zaidi kuna laana ya Mungu, kwamba hata kama hatakufa pale siku ya mwisho atakwenda motoni..
Mithali 13:11 "Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa".
Mwingine kamwona mwanamke na hapo hapo kamtamani, bila kupata muda mrefu wa kumchunguza tabia zake, yeye wazo la dakika moja tu, anaingia humo, na ndio hapo baadaye anakuja kugundua alikuwa ni mke wa mtu aliyemwacha mume wake, au kahaba tu, na ghafla matatizo ndani ya nyumba yanaanza. Vivyo hivyo na mwanamke naye, shetani atampitishia dakika moja mwanaume mwenye fedha, na yeye bila kujitafakarisha anaingia moja kwa moja, kumbe ndio kaenda kuharibu Maisha yake moja kwa moja.
Na sehemu nyingine nyingi za Maisha ni vivyo hivyo.. Shetani huwa anawaletea watu mawazo ya chap-chap .. Ya dakika moja tu yanayovutia lakini nyuma yake yana miaka mingi ya majuto.
Ndugu, tusiwe majeta wa shetani.. biblia inasema..
1 Yohana 2:15-17 " 15 Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. 16 Maana kila kilichomo duniani, yaani, TAMAA YA MWILI, NA TAMAA YA MACHO, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. 17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele".
Zingatia hilo, ni moja kati ya majaribu makuu 3 ya ibilisi aliyoyaona yanawazomba watu wengi kwake, na ndio maana akamchagulia na Bwana, hivyo hatashindwa kutuletea na sisi (mimi na wewe), hivyo tuwe makini sana na mambo ya huu ulimwenguni.
Mbinu 5 za Kujihami na Kupambana na Majaribu
1. Kesha ukitambua udhaifu wako
Hivi ninajaribiwa kwa lipi? (kumtilia mashaka Mungu, kupoteza hamu na dini, kukosa uaminifu kwa rafiki, kusahau wazazi, kujifurahisha kinyume na maadili?). Tena jiulize, ninahisi kuzidiwa na nguvu ya ushawishi nikiwa wapi? Nikiwa na wenzangu—kwenye party? Au nikiwa mwenyewe faraghani—kwenye internet café? Halafu jichunguze, unashindwa kubakia mwadilifu ukiwa na nani? (na rafiki yako, mwanafunzi mwenzako, mzazi wako?). Mwisho, tafuta kujua unakutwa ukiwa katika hali gani unapoangushwa majaribuni? (Ukiwa una uchovu au msongo au upweke, ukiwa una muda mwingi, wikendi, huna la kufanya?). Usitulia kujihoji mpaka umeridhika umejitambua.
Je! Mtu aweza kukanyaga makaa ya moto, Na nyayo zake zisiungue? (Mith 6:28). Ni ngumu kufikiria madhara ya kishawishika Mjaribu anapokujia na ahadi nyingi. Anakwambia, kula tunda hili nawe utafanana na Mungu. Kunywa kidogo nawe utasahau misongo ya umaskini wako. Achia breki za uaminifu nawe ujimwage katika anasa. Ni hapo baadaye tu, baada ya kuridhia, ndipo unapojiuliza, 'nimefanya nini?' Uzuri wa moto ni pale ukiwa mbali.
Kwa imani Musa alipokuwa mtu mzima, akakataa kuitwa mwana wa binti Farao; akaona ni afadhali kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha katika dhambi kwa kitambo. (Waeb 11:24,25). Dalili ya kuwa mtu mzima ni kujua wewe ni nani na lipi la muhimu katika maisha yako. Musa alipoingia tu utu uzima aljiitambua yeye ni nani. Kwa kujitambua kama mtoto wa Mungu na si wa farao aliweza kuzikimbia anasa za ikulu na kukimbilia mateso pamoja na watu wa Mungu. Upepo wa majaribu hauna nguvu kwa mtu anayejitambua na aliye na vipaumbele anayoyathamini maishani kabla ya vingine.
Ombeni kwamba msiingie majaribuni (Luk 22:40). Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni,....usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. (Mat. 6:9,13). Ombi la kupokea nguvu ya kustahimili majaribu ni ombi ambalo Mungu anatamani kulijibu. Ndiyo maana Yesu alituwekea ombi hiilo mdomoni mwetu akitutaka kila tusalipo tulitaje ili tupokee wokovu. Na Yesu kwa kusema hivyo alijua kuwa, "Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili." (1 Kor 10:13). Na kwa kuwa Mungu anataka kukusaidia katika mapambano yako dhidi ya majaribu, unapaswa uombe. Lakini, omba ipi inayofika masikioni mwa Mungu?
Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. (Yak 5:13; linganisha na Kol 3:16; Efe 5:19). Zaidi ya kuomba kwa imani, unapopatikana na changamoto, changamka katika sifa. Vaa uchangamfu wa Yehoshafati umshinde adui yako (2Nyak 20:20,21). Imba nyimbo za ushindi ukaribisha ushindi. Imba nyimbo za Paulo na Sila uuone wokovu wa Bwana kwa kishindo na tetemeko (Matendo 16:23-29). Kamwe Mungu hatabakia kwenye kiti chake cha enzi ametulia, anawaangalia wanawe pasipo kufanya kitu—wanawe wanaosifia Mungu wao masikioni mwa adui zao. Kamwe, Mungu hatawaangusha watu wake wanaoshikiria imani yao kwake hata kwa kumuimbia. Na kama wataanguka chini, siku ya tatu atawanyanyua toka mavumbini; maana, hawastahili kuwepo hapo chini. Ita ushindi kwa nyimbo za sifa na shukurani, "Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo." (1Kor 15:57)
Mpinge Mbaya wa roho yako kwa kusifia uaminifu na uwezo wa Mungu. Jaribu kufanya hivyo kama ujashuhudia Ibilisi akikugeuzia mgongo na kutimka mbio. Unapolalamikia ugumu wa masomo, wa kuacha pombe au sigara; unapolia kwa ukosefu wa ajira, uonevu wa mfumo; unapolaani unafiki wa waumini au uovu wa wasioamini, unaburudisha masikio ya nani kama sio ya adui wa roho yako? Manunguniko ni mziki mtamu masikioni mwa Nyoka wa zamani, Ibilisi na Shetani. Adui anapata nguvu ya kukuudhi anapoona mashambulizi yake yanafikikia lengo lake. Lengo lake nikukuliza tu. Mwachie Shetani kama nyuma yake. Mnyime Shetani starehe ya kukuona ukiwa na uso uliokunjamana. Vaa tabasamu umuadhibu adui yako anayekughasi na umfurahishe Rafiki anayekutetea.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS