UMEJIAANDAJE KWA TUKIO LA UNYAKUO? (Sehemu ya 2)

0
5K

Katika sehemu hii ya pili nataka tuweze kuangalia jinsi baadhi ya maandiko yanavyozungumzia tukio hili la unyakuo. Lengo ni kukufanya ujue na uweze kuamini kwamba siku ya unyakuo ipo na inakuja. Kama vile unavyojua kwamba kuna siku kuzaliwa na siku ya kufa, basi amini pia kwamba kuna siku ya unyakuo. Watu wengi sana wanaamini kuna siku ya mwisho wa dunia ambayo Mungu atahukumu wanadamu wote waishio duniani walio hai na wale waliokufa (kwani watafufuliwa pia tayari kwa hukumu hiyo). Naam ni kweli siku hiyo ipo na hukumu hii itafuata mara baada ya ujio wa Yesu mara ya pili ambao utamaliza utawala wa miaka saba ya Mpinga Kristo na kuanza kwa utawala wa miaka elfu moja wa Yesu hapa duniani, kabla ya ile vita ya mwisho ya dunia ambayo Biblia inaiita Gogu na Magogu (Rejea Ufunuo wa Yohana 20:1-15, 2 Wathesalonike 2:1-8).

Hata hivyo si watu wengi pia wanaojua na kuamini kwamba kuna siku ya unyakuo ambayo ni tofauti na ile siku ya mwisho. Watu wengi huwa wanachanganya sana habari hizi za matukio ya mwisho wa dunia na hasa siku ya unyakuo na ile ya mwisho wa dunia. Lengo la kuwepo kwa siku ya mwisho ni Yesu kutoa hukumu dhidi ya watenda dhambi na wenye haki.

Katika hukumu hiyo wenye dhambi watatupwa kwenye ziwa la moto na kiberiti yaani Jehanamu pamoja na Shetani, wenye haki wataurithi uzima wa milele pamoja na Bwana Yesu (Rejea Mathayo 25:31-46Yohana 5:22). Wakati lengo la kuwepo kwa siku ya unyakuo ni Bwana Yesu kuchukua watakatifu na kwenda nao mbinguni, tukio ambalo likishatokea, ndipo utaanza utawala wa miaka saba wa Mpinga Kristo. Hivyo fahamu kwamba, kabla ya siku hiyo ya mwisho kuna siku ya unyakuo ambayo ndiyo itakayoanza. Kwa lugha nyingine tukio la unyakuo litatangulia na kisha baadaye litafuata tukio la hukumu ya siku ya mwisho. 

Hebu tuangalie sasa baadhi ya maandiko yanavyosema juu ya siku hii;

Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 16:15  Yesu mwenyewe anasema “Tazama naja upesi kama mwivi. Heri akeshaye na kuyatunza mavazi yake…” na pia katika Mathayo 24:36-37 anasema “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala mwana, ila baba peke yake. Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adam’.

Paulo naye akiwafundisha wandugu wa Thesalonike anasema ‘Lakini ndugu kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku, wakati wasemapo, kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa’ (1Wathesalonike 5:1-4)

Ndugu zangu siku hii itakuwa ya ajabu sana, ya kutisha na kuogofya kwa wale watakaoachwa, lakini pia ya baraka na furaha kwa wale watakaonyakuliwa. Hii ni kwa sababu tukio hili litakuwa ni la ghafla mno tena bila taarifa kama vile Mwewe awezavyo kunyakua vifaranga vya kuku. Biblia inaweka wazi kwamba hakuna ajuaye siku wala saa na ndio maana Mtume Paulo anajaribu kulifundisha jambo hili kwa mifano kadha wa kadha ikiwa ni pamoja na mwivi ajavyo usiku bila taarifa au utungu umshikavyo mama mjamzito kwa ghafla. Nasikitika kusema watu wengi wataachwa kwani si watu wengi wanaoishi leo kwa namna ambayo Bwana Yesu akija kunyakua kanisa atakwenda nao.

Katika tukio hili la unyakuo maandiko yanaeleza wazi kwamba kwanza kutakuwa na ufufuo wa wenye haki waliolala/kufa katika Bwana, na kisha wataungana na sisi tutakaokuwa hai kunyakuliwa kwa pamoja ili kumlaki Bwana Yesu mawinguni.  

Mtume Paulo katika 1Wathesalonike 4:13-18 anasema hivi ‘Lakini ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twaambieni haya Kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi farijianeni kwa maneno hayo’.

Pia katika tukio hili Bwana Yesu hatakanyaga kwenye ardhi bali atakuwa mawinguni/hewani maana kwa mujibu wa 1 Wathesalonike 4:17 maandiko yanasema ‘Tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani’.

Katika 1 Wakorintho 15:51-53 Paulo anasema ‘Angalieni nawaambia ninyi siri; hatutalaa sote, lakini sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda Italia na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu nasi tutabadilika. Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa

Katika fungu hili la maandiko Mtume Paulo anazidi kufafanua jambo aliloawaambia Wathesalonike juu ya siku hii, kwamba parapanda ya Bwana Italia kuashiria tukio hili la ajabu na ni imani yangu kwamba wale walioishi maisha ya utakatifu ndio watakaosikia sauti ya parapanda hii. Baada ya parapanda hii ndipo nguvu ya Bwana ya ufufuo itakapowafaufua wale waliolala katika Bwana na kisha miili yao hao na wale tutakao kuwa hai siku hizo itabadilishwa na kisha kunyakuliwa tayari kwa kumlaki Bwana hewani. Mambo haya yote yatafanyika kwa muda mfupi sana ambao ambao Paulo ameuita kufumba na kufumbua au dakika moja.

Tukio la unyakuo na Mpinga Kristo

Kama nilivyoandika awali kwamba tukio la unyakuo ndio litakalomfunua mpinga Kristo. Kwa mujibu wa maandiko hata sasa mpinga kristo yupo na anaendelea na kazi zake lakini hajadhihirika kwa kuwa kanisa kupitia Roho Mtakatifu linamzuia ashindwe kufanya kazi yake kwa udhihirisho wake halisi. Lakini punde Bwana Yesu akishanyakua watoto wake ndipo yule asi yaani mpinga Kristo atakapofunuliwa (Rejea 2 Wathesalonike 2:6-8)

Mpinga Kristo huyu kwa mujibu wa maandiko atatawala kwa muda wa miaka saba. Kwa vipindi viwili vya miezi arobaini na miwili (42) au siku elfu moja mia mbili na sitini (1260). Tambua kwamba baada ya tukio la unyakuo ndipo litafuata tukio la dhiki kuu kupitia utawala wa Mpinga Kristo.

Naam lengo langu kama mwandishi kwenye sehemu hii ya pili kukuonyesha uthibitisho wa kimaandiko juu ya uwepo wa siku au tukio la unyakuo. Hata kama hutaki kuamini usipuuzie mambo haya, ila nakushauri endelea kufuatilia mfululizo huu na pia kusoma Biblia, makala, majarida, vitabu  juu ya jambo hili na hasa matukio ya mwisho wa dunia maana Yesu alisema asomaye na afahamu.

Najua kwamba Shetani hapendi watu wafahamu ukweli kuhusu jambo hili, anachotaka ni kuwapumbaza na kuwadanya wasijue kweli, ili siku ile itakapofika waachwe waingie kwenye dhiki kuu ambayo Yesu mwenyewe alisema haijawahi kutokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu, na wala haitakuwapo kamwe (Mathayo 24:21). Usikubali ndugu yangu kutekwa ufahamu wako na fikra za Shetani, akakufanya ukapuuzia mambo haya na kisha ukaingia kwenye dhiki kuu.

Mpenzi msomaji katika sehemu ya tatu ndipo nitakapoanza kuzungumzia namna ya kujiandaa kwa ajili ya unyakuo kadri ninavyosikia na kujifunza kutoka kwa Bwana kupitia neno lakeNaomba sana maombi yako maana vita niliyoipata hata sasa tangu nimeweka nia ya kuanza kuandika ujumbe huu na ule wa vita vya kiroho ni kubwa sana. Ni imani yangu kwamba kwa maombi yako nitaandika mambo haya kwa wakati ili kuuandaa mwili wa Kristo yaani watu wake pamoja nami tayari kwa tukio hili la kubwa.

Tutaendelea na sehemu ya tatu…

Tafuta
Vitengo
Soma Zaidi
Injili Ya Yesu Kristo
VIFUNGO.
Bwana Yesu asifiwe… Kwa ufupi; Neno “vifungo“ni neno la wingi kutoka neno...
Kwa GOSPEL PREACHER 2022-03-30 05:18:35 0 5K
NUMBERS
Verse by verse explanation of Numbers 5
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 32 questions at the...
Kwa THE HOLY BIBLE 2022-01-24 14:15:41 0 5K
Networking
11 marketplace metrics you should be tracking to measure your success
Which marketplace metrics should you really track to know your marketplace is successful? One...
Kwa Business Academy 2022-09-17 04:01:13 0 10K
PSALMS
Verse by verse explanation of Psalm 11
Praise the Lord Jesus Christ, please study this chapter and then answer all 26 questions at the...
Kwa THE HOLY BIBLE 2022-05-20 11:42:38 0 7K
Religion
Sadaka inayomgusa Mungu
Nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza wasomaji wa makala hii, najua kuna faida nyingi za kiroho,...
Kwa GOSPEL PREACHER 2021-08-25 09:39:38 0 8K