CHANZO CHA MATATIZO KATIKA NDOA

USIMWEKE MBALI NAWE
Maisha ya mume na mke ni maisha yasiyokuwa na nafasi katikati inayowaweka wawili hawa kila mmoja awe mbali na mwenzake. Kama ilivyo andikiwa, "Wawili hawa si wawili tena bali ni mwili mmoja" na mwili ni mjumuiko wa viungo vilivyounganikana ambavyo havijaachana, kila kimoja kimeshikana na chenzake.
Umbali wo wote katikati ya wanandoa huwa ni tatizo; ni Upungufu wa Kinga katika ndoa unaopelekea magonjwa na hatari zinazohatarisha uhai na usalama wa ndoa.
Kama ilivyo kwa mwili mmoja, unapokitenganisha kiungo (au kichwa) na mwili wake, hii maana yake unaua mtu, ndivyo ilivyo katika ndoa; unapomtenganisha mume na mke wake au mke na mume wake, unaua ndoa.
Mke na mume ni mwili mmoja, mmoja kujitenga au kumtenga mwenzake kwa namna yo yote ile ni kuua ndoa.
Kutengana na, au kumtenga mwenzi wako wa ndoa kunaanza na wewe kumweka mbali nawe, au yeye kukuweka mbali na yeye , na kuacha nafasi katikati yenu inayowafanya kila mmoja awe mbali na mwenzake. Na hapa joto la ndoa hushuka hata kupotea, kwa sababu joto la ndoa huwa juu iwapo wawili hawa katika ndoa wanagusana na kutiana joto.
Katika taasisi ya ndoa, jambo baya kuliko yote ni kutengana au kuachana kwa sababu tendo hili linaua ndoa, na ndio maana Mungu anachukia kuachana. Na mtu akifa joto mwilini hupungua hatimaye kuisha, kadhalika na katika ndoa, kwa sababu kinachowatia joto wanandoa ni ule u-moja (oneness) wao wanapokuwa karibu wakigusana bila kuachana.
Leo nataka kidogo nizungumzie mambo ambayo kupitia hayo unaweza ukawa unamweka mwenzi wako mbali na wewe na hivyo kuiweka ndoa yenu hatarini kufa.
1. SIMU :
Katika ulimwengu huu wa smartphone watu wengi wamekuwa bize na simu zao.
Ukipanda kwenye gari, ukiwa ofisini, au kwenye mkusanyiko wa watu wakiwa wametulia, utakuta wengi wenye simu janja wana simu zao mkononi, na hata ukiwaongelesha hawasikii, wamekata mawasiliano na watu wanaowazunguka na kuunganisha mawasiliano na watu waliomo kwenye simu zao ambao kiuhalisia wako mbali nao, hata shida ikitokea hapo hawawezi kuwasaidia.
Kila mahali, mtu yuko bize na watu waliomo ndani ya simu na si watu walio karibu naye! Ijapokuwa watu wanaomzunguka wanaonekana kuwa karibu naye, lakini ukweli ni kwamba yeye yuko mbali nao na badala yake yupo karibu na simu yake. Simu yake imemweka mbali na watu hao.
Ndani ya ndoa, simu pia imekuwa ni tatizo, mtu anaongea na simu yake lakini haongei na mke/mume wake, hawezi kusahau nywila ya simu yake lakini siku ya kuzaliwa, namba ya kiatu, namba ya simu ya mke/mume wake amesahau.
Atalala karibu kabisa na simu yake na akiamka kitu cha kwanza kuchukua na kuangalia ni simu na si mke/mume wake; yeye atalala naye mbali na akiamka anaweza kuondoka hata bila kumsalimia.
Simu ikiita atafanya haraka kupokea na akiwa mbali atakimbia mbio za hatari, lakini mume/mke wake akimwita, hata kusikia anaweza asisikie kabisa kwa sababu masikio yote yameelekea kwenye simu.
Jumbe za Instagram, Facebook, Twitter na WhatsApp atafanya haraka kujibu lakini mume/mke wake anapomwongelesha hata kumwangalia hamwangalii, yupo bize tu na simu.
Kwa namna hii huyu mtu amemweka mbali na yeye mke/mume wake, na badala yake yupo karibu sana na simu! Simu imewafanya wasiwe karibu, kuwe na nafasi au umbali katikati yao; si ajabu wanandoa hawa ukawakuta wanagombana na kuzozana na chanzo cha mizozo yao ikawa ni simu.
Asikudanganye mtu, kitu cho chote unachokipa nafasi na muda wako kuliko mume/mke wako kinakuweka mbali na mke/mume wako na hii huzaa wivu wa kimapenzi hata kusababisha migogoro kwa sababu mmoja hapati utoshelevu kutoka kwa mwenzi wake. Na hii inakuondolea hamu na shahuku ya kuwa karibu na mke/mume wako na ukaona ni sawa tu wala usishituke.
Matumizi ya simu yawe na mipaka, yasiingilie muda wa wanandoa, tena ikiwezekana simu zizimwe au ziwekwe kwenye silent mode ili mpate faragha nzuri ya kuwa pamoja na kushibishana upendo.
Simu isiibe moyo wako, isiibe muda wako na mke/mume wako, hakikisha moyo wako na muda wako kwa ajili ya mke/mume wako vinabaki kwa ajili yake.
2. KAZI :
Hii ni moja ya kitu kinachowaweka wanandoa mbali na hasa kunapokosekana mipaka.
Kazi inapoletwa mpaka nyumbani na ikawa ndio kawaida, na mtu huyu akawa bize na kazi yake kuliko mke/mume wake, lazima tu mmoja hapa ataanza kuionea wivu kazi; na ikumbukwe kuwa wivu ni hasira.
Utashangaa mtu tu anakukasirikia, na kufanya visa visivyoisha, kumbe kazi yako imechukua nafasi yake kwako, imemweka yeye mbali na wewe hata asiweze kufurahia uwepo wako maishani mwake.
Mwenzako hasikii kabisa uwepo wako ijapokuwa upo kwa sababu wewe upo bize na kazi; makaratasi ya kazini unayaleta mpaka nyumbani; kila wakati upo bize na kipakatalishi (laptop), kila anapokuhitaji wewe upo bize! Lazima aumie na hapo ndipo matatizo ya ndoa huanza.
3. HUDUMA NA UTUMISHI WAKO KWA MUNGU:
Hapa nitazungumzia shughuli zote za kiroho ikiwa ni pamoja na maombi, kusoma Biblia, ibada, na huduma zote ambazo mtu anaweza kuwa nazo kanisani.
Mambo haya yanaweza kusababisha mke/mume wako awe mbali na wewe na pale anapodai haki yake aanze kuonekana kama kikwazo, na tena kwa sababu ya ujinga wako utaanza kumkemea na kusema ameingiliwa na mapepo kumbe tatizo ni wewe.
Ni lazima uenende kwa utaratibu, kwa kuhakikisha kila kitu kinakuwa mahali pake; ndoa iwe ndoa na huduma iwe huduma, na kila kitu kubaki mahali pake kwa wakati wake.
Ukiwa nyumbani wewe ni mume, wewe ni mke na si mchungaji, mwinjiristi, nabii, mwalimu au mtume; wewe nyumbani kwako si mwimbaji, mwombaji, shemasi, mzee wa kanisa n.k. wewe ni mume kwa mke wako, wewe ni mke kwa mume wako. Huko kujifanya wakati wote unamtafuta Mungu, uko rohoni unamkaribia Mungu wakati huo upo mbali na mke/mume wako, hata Mungu anachukia.
Usimpinge mke/mume wako anapokukaribia ili umkaribie Mungu; mwenzako anakutaka, unampinga kisa eti unamkaribia Mungu, wewe ni mpumbavu. Biblia imesema, mkaribieni Mungu, mpingeni Shetani naye atawakimbia na si umkaribie Mungu alafu umpinge mke/mume wako, hii si ya KiMungu, ni ya kishetani inayofanywa kwa Jina la Mungu. Wewe unataka mke/mume wako akukimbie, anapokukaribia unamwona ni kama kikwazo na ni Shetani kumbe wewe umekosea kanuni na utaratibu.
Ukweli ni kwamba, hakikisha unapomkaribia Mungu uwe kwanza umemkaribia mke/mume wako ili utumishi wako usije ukalaumiwa kwa namna yo yote; ili unapoenda kumkaribia Mungu usikute machozi ya mke au mume wako yametangulia mbele za Mungu na utumishi unaoufanya usije kukataliwa.
Biblia inasema, Unawezaje kusema unampenda Mungu usiyemuona wakati unamchukia jirani yako unayemwona siku zote? Hii maana yake ni kwamba, kabla hujaenda kumwonyesha upendo Mungu mwonyeshe kwanza huyo unayeishi naye. Kama mke/mume wako amekosa upendo wako kwa kisingizio cha wewe kubanwa na huduma, hata Mungu upendo wako wa kinafiki hautaki.
Mungu anataka uwiano sahihi na ndio sababu Biblia imeweka mambo haya katika uwiano sahihi; kimoja kiende sambamba na kingine lakini kimoja kisiingilie kingine.
Kama huduma yako na utumishi wako kwa Mungu utamweka mke/mume wako mbali na wewe, kila anapokuhitaji anakukuta upo bize na Mungu, hicho unachokifanya hakina kibali kwa Mungu, yaani kimekataliwa. Rudi kwanza kwa mke/mume wako, mkaribie kwanza yeye ndipo uwe huru kumkaribia Mungu.
Inakuaje mpaka kitandani badala ya kuongea na mwenzi wako unanena kwa lugha, badala ya kumkumbatia mwenzako, umekumbatia Biblia, kila akigeuka anakukuta umezama rohoni, kila akifumbua macho anakukuta upo unasoma Biblia! Ni saa ngapi utakuwa naye? Usifanye amuelewe Mungu (wako) vibaya na Jina lake likatukanwa kwa sababu yako.
4. MARAFIKI ;
Hawa ni watu wazuri lakini unapowapa nafasi kuliko mume/mke wako kuwa na uhakika kabisa watatumia udhaifu wako kukutenga na mume/mke wako.
Marafiki si wa kuamini kwa habari ya ndoa yako, kwa sababu wanaweza kuwa wanatamani hicho ulicho nacho na kwa sababu wamejaa wivu na unafiki, wakatumia ukaribu wako na wao kukuharibia ndoa yako.
Unayekuwa karibu naye zaidi ndiye unayemwamini, na hasa yule anayejionyesha kuwa ni mwema kwako na anakutakia mazuri.
Sasa basi, na huyo unayemwamini ndiye utakayemsikiliza zaidi na kuamini kila anachokuambia, na wewe kukifanyia kazi hata bila kufikiri, hapo sasa ndipo unapomalizwa.
Usiwaamini marafiki zaidi ya unavyomwamini mke/mume wako. Na ili iwe hivyo, kuwa karibu na mume/mke wako na uwe mbali na rafiki zako kwa habari ya ndoa yako.
Daima, usione kampani ya marafiki zako ni bora zaidi kuliko kampani ya mume/mke wako; ukishaona hivyo tu, utatumia muda wa kuwa na mke/mume wako pamoja na rafiki zako na wakati mwenzako yupo peke yako.
Kuhusu wewe na mwenzi wako, marafiki hawana nafasi, ukiwapa nafasi tu, watakutenga na mwenzi wako! Watakupa sababu za kufurahia maisha pamoja nao kwenye mitoko (outing) wakati mume/mke wako yupo nyumbani peke yake anaugua moyo.
Marafiki hawa wanaweza kutoa fedha zao ili utoke nao kuponda maisha na raha za dunia hii na umuache mke/mume wako nyumbani akiwa ameshinda njaa, amelala njaa, na hana mtu wa karibu wa kuwa naye kushiriki maumivu yake pamoja.
Rafiki wana tabia moja, ya kukusonga ili kukutenganisha na mke/mume wako na hasa wakiona wewe na mwenzako mnaishi vizuri kwa raha.
Wawekee mpaka kwa wewe kuwa na mipaka na ujiwekee nidhamu kubwa ya kuwa karibu na mwenzi wako bila kuingiliwa na wao! Inapofikia ndoa yako, usiwe na rafiki isipokuwa mke/mume wako tu, urafiki ni kazini, kwenye biashara, kanisani, lakini wakiwa mbali sana na ndoa yako! Waonyeshe kuwa mke/mume wako ni wa kwanza na unaweza kuvunja ratiba yo yote ya muhimu sana kwa ajili yake.
Usichelewe nyumbani kwa sababu ya marafiki zako, usishindwe kupokea simu ya mwenzi wako kwa sababu yao! Yeye ni namba moja wako anayeishi ndani ya nafsi yako kwa kuwa wewe na yeye ni mwili mmoja.
5. MPANGO WA KANDO :
Hakuna mtu mtamu zaidi ya mume/mke wako, utamu wake ukutoshe na uridhike nao, usitafute utamu wa kando kwa maana ni mtamu kinywani lakini ukiishanoga tumboni ni mchungu.
Mithali anasema,
Mithali 5:15-19
Na maji yenye kububujika katika kisima chako.
[16]Je! Chemchemi zako zitawanyike mbali,
Na mito ya maji katika njia kuu?
[17]Yawe yako mwenyewe peke yako,
Wala si ya wageni pamoja nawe.
[18]Chemchemi yako ibarikiwe;
Nawe umfurahie mke wa ujana wako.
[19]Ni ayala apendaye na paa apendezaye;
Maziwa yake yakutoshe sikuzote;
Na kwa upendo wake ushangilie daima.
Kwa nini amesema hivi? Kwa sababu mpango wa kando huwa unakuweka mbali na mpango wa Mungu ambao ni mke/mume wako. Hii huleta madhara ndani ya ndoa yanayopelekea mwisho wa siku ndoa kufa.
Mpango wa kando unaua ndoa yako, lakini pia unakuua na wewe mwenyewe, kuuepuka ni hekima zaidi. Na ili uuepuke ni muhimu ukadumu kuwa karibu na mke/mume wako.
6. WAZAZI, NA NDUGU ZAKO:
Ndugu na wazazi ni wa muhimu sana kwako na mke au mume wako, lakini wanapokuwa na nafasi kubwa kwako kuliko mke/mume wako na wasiwe na mipaka kwenye ndoa yako, watakuwa karibu na wewe na wewe utajikuta umemweka mke/mume wako mbali na wewe; utawasikiliza zaidi ndugu na wazazi wako kuliko mke/mume wako.
Ukweli, ndoa ni tendo la kuacha ili kuambatana; mwanaume anawaacha baba na mama yake anaambatana na mkewe, na mwanamke anawasahau watu wa nyumbani mwa baba yake na kuambatana na mume wake ili wawe mwili mmoja.
Mwanzo 2:24
Hii ni kwa upande wa mwanaume; inapofikia kwenye swala la ndoa anawaacha baba yake na mama yake na ndugu wote wa damu ili aambatane na mke wake, wakati wote amfukuzie mke wake kwa upendo akiacha watu wengine wote ikiwa ni pamoja na wazazi wake.
Zaburi 45:10-11
Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.
[11]Naye mfalme atautamani uzuri wako,
Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.
Binti naye ili mfalme autamani uzuri wake, yaani aridhike na kutosheka na hali ya yeye kuwa mke wake, ni lazima awasahau watu wake na nyumba ya baba yake (yaani, mahali alipozaliwa; inajumuisha wazazi wake na ndugu zake wa damu).
Tatizo linaanza pale mwanaume anapogoma kuacha baba na mama yake na mwanamke anapogoma kusahau watu wake na nyumba ya baba yake, ndoa huwa ni genge la wahuni wa kifamilia; hakuna kusikilizana, hakuna kuelewana, kila siku ni mivutano na mashindano. Wewe usikubali kufika huko!
Wawekee mipaka ndugu zako, na wewe jiwekee mipaka, ongea nao mambo ya familia yenu, kuhusu ndoa yako jiwekee miiko, na wao wakija kwako, wazungumze ya familia na si ya ndoa yako; Wawekee miiko. Mambo ya ndoa yako, zungumza na mke/mume wako.
Hakikisha wako mbali na ndoa yako, wako mbali na chumba chenu, kiwe fumbo la Siri kwao, wasijue lililo la wawili chumbani na wasiingilie maisha yenu.
- BIBLICAL FINANCIAL EDUCATION
- SPIRITUAL EDUCATION
- MASWALI & MAJIBU
- WORLD'S EDUCATION
- MAHUSIANO KIBIBLIA
- Injili Ya Yesu Kristo
- OTHERS